Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 30 Oktoba 2017

UONGOZI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA DODOMA WAPOKEA KWA MASIKITIKO JUU YA TAARIFA YA RUSHWA ILIYORIPOTIWA KWENYE MTANDAO WA JAMII FORUM

 
 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

                                                                                      
                                                                                                                 
TAARIFA KWA UMMA JUU YA TUHUMA YA UWEPO WA VITENDO VYA RUSHWA KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA, DODOMA KAMA ILIVYORIPOTIWA KWENYE MTANDAO WA KIJAMII WA JAMII FORUM TAREHE 28/10/2017
Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma umepokea kwa masikitiko taarifa iliyotolewa kwenye mtandao tajwa hapo juu kwamba, “Serikali na Takukuru muimulike Hospitali ya Mkapa Dodoma” kwamba, “imekuwa kawaida kabisa kwa mgonjwa kutopata huduma ya aina yoyote bila kutoa chochote na kuna mgonjwa ana wiki matokeo ya vipimo hayajatoka na hajapewa huduma yoyote zaidi ya dawa za kuondoa maumivu”.
Uongozi wa Hospitali unapenda kuwahakikishia watumiaji wa huduma za hospitali hii kwamba, madai husika hayana ukweli wowote. Mara baada ya kupokea malalamiko na tuhuma tajwa hapo juu, siku hiyo hiyo ya tarehe 28/10/2017 uongozi wa hospitali ulichukua hatua ya kufanya ufuatiliaji kwa kuwatembelea wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa wodini na kuzungumza nao pamoja na ndugu zao ili kubaini kero walizonazo kuhusu huduma za Hospitali.
Ufuatiliaji huu ulizingatia kubaini tarehe ya kulazwa, ugonjwa alio nao, vipimo alivyoandikiwa, vipimo ambavyo havijafanyika na sababu za kutofanyika.  Aidha, kila mgonjwa/ndugu aliridhia na kutoa ushirikiano mkubwa ili kubaini ukweli na pia wote walitoa mawasiliano yao ya simu ya mkononi iwapo ufuatiliaji zaidi ungehitajika.
Yatokanayo na ufuatiliaji huo ni;
Jumla ya wagonjwa 34 ndio walikuwemo wodini siku ya tarehe 28/10/2017. Tarehe za kulazwa kwao zilikuwa kati ya 20/9/2017 na 28/10/2017. Kati ya hao, wanawake watu wazima walikuwa 20 na wanaume 14 ambapo kati yao 2 walikuwa watoto wachanga.
Wagonjwa 24 tu ndiyo matibabu yao yalikuwa yanahitaji vipimo mbalimbali na wengine hawakuhitaji kutokana na asili ya magonjwa waliyokuwa wanaugua.
Wagonjwa waliombwa kutoa maoni yao kuhusu hali ya huduma kwa ujumla pia kuhusu upatikanaji wa vipimo vya uchunguzi wa maabara na mionzi na kama kuna ucheleweshaji wa vipimo husika na dalili za kuombwa rushwa. Jumla ya wagonjwa 18 kati ya 24 waliohitaji vipimo, walikuwa wamepimwa na kupewa majibu. Wagonjwa sita (6) waliobakia; wawili (2) kati yao walikuwa wamelazwa tarehe 27/10/2017 na tayari walikuwa wameshaanzishiwa matibabu na kupangiwa kupimwa ECHO na ECG tarehe 30/10/2017. Aidha, wagonjwa wengine wawili (2) walikuwa wamepimwa tarehe 27/10/2017 na walikuwa wanasubiri majibu na waliobakia 2 ndiyo kwanza walikuwa wamelazwa siku hiyo ya tarehe 28/10/2017.
Hakukuwa na mgonjwa yeyote aliyelalamikia kusumbuliwa kuhusu vipimo wala kuona dalili za rushwa na badala yake, wote walishukuru kwa juhudi zinazofanywa na watumishi wa hospitali katika kuwapatia huduma.


Hata hivyo, tangu awali hospitali hii imeweka mifumo mbalimbali ya kuhakikisha inabaini vitendo vinavyo athiri utoaji wa huduma bora na salama vikiwemo vitendo vya rushwa. Mifumo hii ni pamoja na:-
1.       Utoaji wa elimu kwa wateja maeneo ya  mapokezi, maabara na kliniki.
2.       Uwepo wa Sanduku la Maoni
3.       Uwepo wa namba za simu za kutolea malalamiko ya wateja.
4.       Viongozi wa hospitali kutembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma na kuongea na wateja.
5.       Wateja kujaza dodoso la kutoa maoni baada ya huduma (client exit interview).
Elimu inayotolewa huelekeza juu ya haki za wateja, huduma zinazopatikana, mfumo wa malipo, kujiepusha na kutoa au kupokea rushwa, na jinsi ya kutoa maoni na malalamiko juu ya huduma wanazopata kwa kutumia sanduku la maoni, kupiga namba za simu zilizobandikwa sehemu mbalimbali na kuwaelekeza mahala palipo na dawati la malalamiko na jinsi ya ujazaji wa dodoso la mteja baada ya huduma (Client Exit Interview). Elimu hii hutolewa na Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopo hapa hospitalini.
Aidha, tangu awali, hospitali iliweka Sanduku la Maoni maeneo ya mapokezi ili  wateja waweze  kuweka maoni yao wakati wowote wanapohitaji. Tangu sanduku la maoni lianze kufunguliwa, hakuna aliyelalamikia uwepo wa vitendo vya rushwa au viashiria vyake.
Vilevile, hospitali imebandika namba Nne (4) tofauti za Simu mkononi za Viongozi katika sehemu mbalimbali za kutolea huduma ili kuwarahisishia wananchi/wateja kuwasilisha maoni yao kuhusu huduma. Namba ya kwanza kwenye orodha ni ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, ikifuatiwa na ya Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Katibu wa Hospitali. Tangu Wananchi waanze kutumia namba hizi hakuna aliyewahi kulalamikia uwepo wa rushwa ndani ya hospitali hii.
Uongozi wa Hospitali umejiwekea utaratibu wa kutoka ofisini na kupita sehemu mbalimbali za kutolea huduma na kuongea na wagonjwa ili kubaini kama kuna changamoto wanazozikabili wakati wa kupokea huduma. Maeneo hayo ni pamoja na mapokezi, eneo la wagonjwa wa nje (OPD), Kliniki mbalimbali, maabara, eneo la kutolea huduma za mionzi, na mawodini. Zoezi hili huongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali na hufanyika angalau mara tatu kwa wiki zikiwemo siku za mapunziko za Jumamosi na Jumapili. Tangu zoezi hili lianze, hakuna mwananchi/mteja aliyewahi kulalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Hospitali pia ilianzisha Dodoso Maalumu la Mteja (Client Exit Interview) linalojazwa na mteja baada ya kupewa huduma ili kubaini sehemu zenye changamoto. Tangu madodoso haya yaanze kujazwa, hakuna mteja/mgonjwa aliyelalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Uongozi wa Hospitali unatoa Shukrani za pekee kwa watumiaji wa huduma za hospitali hii na wote wanaotoa maoni kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma. Tunapenda kuwahakikishia kuwa, tutaendelea kusimamia maadili ya tiba na kuhakikisha wateja wote wanafurahia huduma zetu. Hata hivyo, hatutasita kuchukua hatua stahiki za kisheria endapo tutabaini kwamba taarifa iliyotolewa ni ya upotoshaji na / au imetolewa kwa lengo la kuichafua hospitali, wizara au Serikali.
Uongozi wa hospitali unatoa wito kama kuna ambaye hajatendewa haki ajitokeze na kutumia fursa za mawasiliano zilizoainishwa hapo juu ili kero yake iweze kufanyiwa kazi au afuate utaratibu rasmi wa kuripoti tukio husika la vitendo vya rushwa kwenye vyombo husika vya kisheria ili taratibu za kisheria zichukuliwe.
Aidha, milango ya hospitali iko wazi wakati wowote kwa ajili ya kupokea kero na maoni toka kwa wateja wake ili kuboresha zaidi huduma.

AHSANTENI SANA.

30/10/2017.

0 on: "UONGOZI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA DODOMA WAPOKEA KWA MASIKITIKO JUU YA TAARIFA YA RUSHWA ILIYORIPOTIWA KWENYE MTANDAO WA JAMII FORUM"