Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 19 Aprili 2018

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII MHE. UMMY MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019










MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

A: UTANGULIZI
1.          Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ndani ya Bunge lako Tukufu, ambayo imechambua Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba kutoa hoja sasa Bunge lako likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2017/18 na Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2018/19. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2018/19.

2.    Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuwasilisha hotuba yangu siku ya leo. Aidha, ninapenda kutumia fursa hii kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake imara kwa nchi yetu na maelekezo yake ambayo yamekuwa dira sahihi katika utendaji wangu na katika kuimarisha huduma za Afya na Maendeleo ya Jamii nchini.  Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Afya kwa kutoa msukumo mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi hapa nchini. Msukumo huo utaboresha huduma za afya kwa Watanzania kama nyenzo muhimu ili kufikia Uchumi wa Kati.

3.          Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuboresha huduma za afya kwa Watanzania hasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Afya ya Mama na Mtoto, Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza pamoja na Afya ya Vijana. Wizara yangu itaendelea kutumia ushauri, nasaha, ushawishi na uzoefu wake ili kuhakikisha Watanzania wanaweza kujikinga na maradhi na kujenga jamii ya Watanzania wenye Afya Bora.

4.          Mheshimiwa Spika, ninaomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri unaosaidia kuleta tija na ufanisi katika utendaji na kuimarisha huduma zinazotolewa katika Sekta ya Afya. Aidha, ninampongeza kwa hotuba yake aliyoiwasilisha kwenye Bunge lako tukufu ambayo imetoa dira ya jinsi Serikali itakavyotekeleza majukumu yake katika mwaka 2018/19.

5.          Mheshimiwa Spika, ninapenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuendelea kutekeleza majukumu yako kwa weledi katika kuliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb) katika utekelezaji wa majukumu yake. Vilevile, nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge kwa kusimamia vyema mijadala ndani ya Bunge.


6.          Mheshimiwa Spika, kipekee ninapenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Serukamba (Mb), na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Juma Nkamia (Mb) kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa wakati wa maandalizi ya Bajeti hii. Aidha ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia ikiwemo kutoa ushauri na maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma za afya na maendeleo ya jamii nchini. Ninawaahidi kwamba, Wizara yangu itazingatia ushauri wao na kuendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu na kazi zetu za kuwatumikia wananchi ndani na nje ya Bunge.

7.          Mheshimiwa Spika, ninatoa pole kwa Watanzania wote, waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa, ajali na majanga. Aidha, ninatoa pole kwa wagonjwa na majeruhi wa ajali waliopo hospitalini na majumbani pamoja na wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Ninamuomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka ili waweze kuendelea na ujenzi wa Tanzania ya Viwanda.

8.          Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo, ninapenda sasa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa mwaka 2017/18, Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2018/19 pamoja na maombi ya fedha ambazo zitaiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake.




B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18
9.          Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara imeendelea kuzingatia Sera, Mipango Mikakati pamoja na makubaliano ya Kitaifa na Kimataifa yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini. Maeneo haya ya vipaumbele yameainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati 2016/17 – 2020/21, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020, na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030). Aidha, Wizara imezingatia vipaumbele vilivyoainishwa katika Sera ya Afya (2007) na Mpango Mkakati wa IV wa Sekta ya Afya (2015 – 2020); Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996); Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2001); Sera ya Wazee (2003); na Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008).

10.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18, kupitia Fungu 52, Wizara yangu ilipanga kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utoaji huduma za Afya katika maeneo yafuatayo;
a)   Kuimarisha Huduma za Kinga, Tiba, na kuongeza usawa katika kutoa huduma za afya,
b)   Kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto,
c)   Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya,
d)   Kuimarisha miundombinu kwenye vyuo vya mafunzo ya afya kwa lengo la kuongeza udahili na upatikanaji wa rasilimali watu,
e)   Kuimarisha matibabu ya kibingwa nchini kwa kuendeleza ujenzi, upanuzi, ukarabati wa miundombinu na kufunga mitambo ya kisasa ya kutolea huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali Maalum za Mirembe na Kibong’oto; pia Hospitali za Rufaa za Kanda; Kanda ya ziwa (Bugando), Kanda ya Kaskazini (KCMC), Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Kanda ya Kusini (Mtwara),
f)    Kuimarisha mazingira ya ubia na ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za afya,
g)   Kuimarisha huduma za lishe na upatikanaji wake katika jamii na vituo vya kutolea Huduma za Afya,
h)  Uimarishaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha huduma za afya,
i)     Kuhamasisha wananchi kujiunga na Mifuko ya Bima za Afya kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya zenye uhakika.

11.      Mheshimiwa Spika, kupitia Fungu 53, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ilipanga kutekeleza kazi zifuatazo:
a)   Kuratibu utekelezaji na ufuatiliaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22;
b)   Kuimarisha upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi watoto ikiwemo kwa watoto walio katika mkinzano wa Sheria;
c)   Kuwezesha wazee wasiojiweza na watoto walio katika mazingira hatarishi kupata huduma za msingi;
d)   Kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo kwa kuzingatia rasilimali walizonazo;
e)   Kuelimisha jamii hususan wanawake na katika ngazi ya Halmashauri kujiunga na VICOBA na SACCOS kwa ajili ya kuwawesha kiuchumi;
f)    Kuwezesha utoaji wa huduma za ustawi wa jamii katika makazi ya wazee, Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini, mahabusu za watoto na Shule ya Maadilisho; na
g)   Kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo na Taasisi za Maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Mapato na Matumizi ya Fedha – Fungu 52
12.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Fungu 52 (Afya), hukusanya mapato yake kupitia huduma za tiba zitolewazo na hospitali zilizo chini yake, tozo za huduma katika Taasisi mbalimbali, Bodi na Mabaraza, ada za uchangiaji wa gharama za mafunzo, marejesho ya masurufu, malipo ya ununuzi wa vitabu vya maombi ya zabuni, pamoja na makusanyo yatokanayo na utoaji wa huduma katika Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara. Hadi kufikia mwezi Machi 2018, Wizara pamoja na Taasisi zake imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 162,891,572,942 sawa na asilimia 72 ya lengo la mwaka la kukusanya kiasi cha Shilingi 227,041,160,573 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato. Mafanikio haya yametokana na utaratibu wa kulipia huduma kupitia benki, uhamasishaji kuhusu kulipa maduhuli ya serikali, udhibiti wa makusanyo, kuongezeka kwa ari ya utendaji kazi, uboreshwaji wa Huduma za Bima na Kuimarishwa kwa mfumo wa malipo kwa njia ya Ki-elektroniki.

13.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara iliidhinishiwa na Bunge lako Tukufu kupokea na kutumia jumla ya Shilingi 1,077,701,892,000. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi 291,895,940,000 sawa na asilimia 27 ya bajeti yote ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, na Shilingi ni Shilingi 785, 805, 952,000 sawa na asilimia 72.9 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

14.      Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi 2018, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 617,507,623,167 sawa na asilimia 57 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi 1,077,701,892,000 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, fedha zilizopokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida katika kipindi cha Julai hadi Machi, 2018 ni Shilingi 216,736,325,825,824 sawa na asilimia 74 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa mwaka. Kati ya fedha hizo, Shilingi 68,814,900,939 zilitumika katika Matumizi Mengineyo (OC) ikiwa ni sawa na asilimia 73.3 ya kiasi kilichotengwa na Shilingi 147,921,424,885 zilitumika kulipia mishahara (Fungu 52) sawa na asilimia 65 ya kiasi cha fedha kilichotengwa.

Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, hadi kufikia Machi, 2018 kiasi cha Shilingi 400,771,297,343 kilipokelewa, sawa na asilimia 51 ya fedha zilizoidhinishwa kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 79,756,079,206 ni fedha za ndani sawa asilimia 24 ya fedha iliyoidhinishwa. Fedha za nje zilizopokelewa ni Shilingi 321,015,218,137.12 sawa na asilimia 71 ya fedha zilizoidhinishwa. Aidha Wizara ilipokea kiasi cha Shilingi 82,515,009,463.82 na kuzipeleka OR–TAMISEMI kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya ili viweze kutoa huduma za dharura ikiwa ni pamoja na upasuaji wa akinamama wajawazito (CEmONC) ili kumtoa mtoto tumboni pindi wanapokabiliwa na uzazi pingamizi. Kati ya fedha hizo Shilingi 63,015,009,462.82 ni kutoka Benki ya Dunia na Shilingi 19,500,000,000.00 kutoka Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund).

Mapato na Matumizi - Fungu 53

15.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Fungu 53 (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), ilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 2,101,874,000 kutokana na ada za wanafunzi kutoka katika Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Uyole, Rungemba, Mlale, Misungwi, Ruaha, Mabughai na Monduli; uuzaji nyaraka za zabuni na ada mbalimbali za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2018 jumla ya Shilingi 1,775,466,155 sawa na asilimia 84 zilikusanywa.

16.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/18, Wizara kupitia Fungu 53 ilitengewa jumla ya Shilingi 37,909,880,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 19,142,252,240 ni bajeti ya Mishahara, Shilingi 16,161,349,760 ni Matumizi Mengineyo na Shilingi 2,606,278,000 ni kwa Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2018, jumla ya Shilingi 18,352,527,400 sawa na asilimia 48 zilipokelewa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 8,848,331,727 sawa na asilimia 55 ni Matumizi Mengineyo; Shilingi 8,470,927,127 sawa na asilimia 44 ni Mishahara ya Idara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara; na Shilingi 1,033,268,546 sawa na asilimia 40 fedha za Miradi ya Maendeleo.

17.      Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 ulikuwa kama ifuatavyo:

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA AFYA

HUDUMA ZA KINGA

Chanjo
18.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Mwaka 2017/2018, Wizara ilisimamia shughuli za utoaji wa chanjo kwa   watoto ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa. Takwimu za Januari hadi Desemba 2017 zinaonyesha kuwa asilimia 101.2 ya Watoto waliolengwa nchini walipatiwa chanjo zote muhimu ili kuwakinga na magonjwa.  Mnamo mwezi Desemba 2017, Serikali ya Tanzania ilipongezwa Shirika la Afya Duniani na wadau wa Kimataifa wa Chanjo kwa kufikia kiwango cha juu cha chanjo kwa asilimia 97 ya uchanjaji watoto kwa chanjo ya pentavalent kwa takwimu za mwaka 2016. Lengo la Mkakati wa Dunia kupitia Shirika la Afya Duniani ni nchi kufikia kiwango cha uchanjaji wa asilimia 90. Mikakati ya Wizara imewezesha nchi yetu kufikia kiwango hicho ambapo inakuwa nchi ya Tatu barani Afrika ikitanguliwa na Zambia yenye kiwango cha asilimia 99 ikifuatiwa na Rwanda yenye asilimia 98.

19.      Mheshimiwa Spika, Saratani ya mlango wa kizazi ndio inayoongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na pia kusababisha vifo vya wanawake wengi.  Kwa mujibu wa Takwimu za Taasisi ya Saratani Ocean Road za mwaka 2016/17 Asimilia 32.8 ya wagonjwa wa saratani nchini ni wa saratani ya mlango wa kizazi ikifuatiwa na saratani ya  matiti yenye asilimia 12.9. kwa bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi inazuilika kwa kuwapatia chanjo wasichana kuanzia miaka 9 hadi 14. Katika kukabiliana na saratani hiyo, mwaka 2017/18 Serikali imeanza kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vacacine). Kutokana na upatikanaji wa dozi kutoka kwa wazalishaji, kwa mwaka 2018 chanjo hiyo imeanza kutolewa kwa wasichana wenye miaka 14, ambapo, hadi Desemba 2018, Wizara imelenga kuwafikia wasichana 616,734 wa umri huo. Chanjo hiyo ni salama na inatumika katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Rwanda, Uganda, Afrika ya Kusini, Zambia na Lesotho. Kupitia Bunge lako Tukufu, nawasihi wazazi na walezi wenye watoto kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo hiyo muhimu ili kuwakinga dhini ya saratani ya mlango wa kizazi.

Afya na Usafi wa Mazingira
20.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira inayotekelezwa katika Halmashauri zote nchini pamoja na kudhibiti magonjwa ya mlipuko hususan kipindupindu. Shughuli zilizotekelezwa zimeainishwa katika aya 22 mpaka 24 ya Hotuba

21.      Mheshimiwa Spika, Hali ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini inaendelea kudhibitiwa. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 jumla ya wagonjwa wa kipindupindu 4,508 na vifo 92 viliripotiwa katika Mikoa ya Songwe, Dodoma, Ruvuma na Mbeya. Nitoe rai kwa viongozi katika mikoa yote nchini kulifanya suala la kupambana na ugonjwa wa kipindupindu kuwa ni agenda ya kudumu katika vipaumbele vyao.

Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto

22.      Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto nchini, Wizara imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, mama, watoto na vijana pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020. Katika kutekeleza mkakati huo, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni: huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua.

23.      Mheshimiwa Spika, huduma za uzazi wa mpango ni muhimu katika kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara imenunua na kusambaza dawa za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma za afya nchini. Aidha, jumla ya wateja 519,817 walifikiwa na huduma ya uzazi wa Mpango kupitia utaratibu wa mkoba (out reach services) na 424,595 walipata huduma kutoka katika vituo vya kutolea huduma za afya.

24.      Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya afya wakati wa ujauzito ni afua muhimu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kwani matatizo mengi yanaweza kuzuilika, kugundulika na kutibiwa kama wanawake wajawazito watahudhuria kliniki ya wajawazito na kupimwa na wahudumu wenye ujuzi ndani ya wiki 12 tangu wanapokuwa wamejigundua kuwa wanaujauzito. Katika kipindi cha 2017/18, Wizara iliendelea kuhakikisha kwamba huduma kwa wanawake wajawazito zinapatikana sambamba na kuelimisha wajawazito kuhudhuria kliniki. Aidha, kulingana na taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma ya afya, hadi kufikia mwezi Februari 2018 asilimia 81.7 walihudhuria angalau mara moja, lengo likiwa ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara 4 katika kipindi cha ujauzito ifikapo mwaka 2020. Nitumie fursa hii kuwahimiza wajawazito wote kuhudhuria kliniki kama inavyoshauriwa.

25.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhamasisha na kuhimiza wanawake wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma. Mwelekeo ni kwamba Idadi ya akinamama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma inaendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 68.5 mwezi Machi 2018 katoka asilimia 64 mwaka 2015/16. Napenda kutoa wito kwa wanawake wajawazito wote nchini, wajifungulie kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupunguza vifo na changamoto za uzazi kwa mama na mtoto.

26.      Mheshimiwa Spika, kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano ni moja ya kipaumbele cha Wizara. Kulingana na Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa 2016-2020, Serikali imedhamiria kuwa ifikapo 2020 vifo vya watoto wa chini ya mwezi mmoja vipungue kutoka 21 hadi 16 katika kila vizazi hai 1,000; vifo vya watoto wa chini ya umri wa mwaka mmoja kutoka 45 hadi 25 katika kila vizazi hai 1,000 na vifo vya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutoka 54 hadi 40 katika kila vizazi hai.

27.      Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi ya Vituo vya Afya ili viweze kutoa huduma za dharura za upasuaji ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kutoa mtoto tumboni (CEmONC) pindi mama mjamzito anapohitajika. Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI inaboresha vituo vya afya takribani 208 (kama ilivyoainishwa katika hotuba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI) ili kuviwezesha kutoa huduma za CEmONC. Hadi Machi 2018, maboresho ya vituo hivyo yalikuwa yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji. Maboresho haya yanahusu ujenzi wa vyumba vya upasuaji (Theatres), wodi ya wakinamama wajawazito (Martenity/Labour wards), vyumba vya maabara na nyumba za watumishi. Kukamilika kwa maboresho haya kutaongeza idadi ya vituo vinavyomilikiwa na Serikali vyenye uwezo wa kutoa huduma hiyo ya CEmONC kufikia 283 kati ya Vituo vya Afya 527. Hii itakuwa sawa na asilimia 53.7 ya vituo vya afya vya umma vitakavyoweza kutoa huduma za upasuaji wa dharura kutoka asilimia 21 mwezi Juni 2016.

28.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea na juhudi za kudhibiti saratani za via vya uzazi (Reproductive cancers) ikiwemo saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti na saratani ya Tezidume. Aidha, katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kupima na matibabu ya Mabadiliko ya awali ya Saratani ya Mlango wa kizazi na saratani ya matiti ambazo ndizo zinazoongoza nchini, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeanzisha vituo vipya 100 vya uchunguzi na tiba ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Songwe, Geita, Dodoma, Singida, Manyara, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Simiyu, Mara na Ruvuma.


Udhibiti wa UKIMWI
29.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Desemba 2017, jumla ya watu wapatao 5,164,297 walipimwa VVU na kupewa majibu ya hali zao za afya, ambapo watu 145,104 (sawa na asilimia 2.8) kati yao waligundulika kuwa na maambukizi na kuanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI. Aidha, takwimu za hadi Desemba, 2017 zinaonesha kuwa jumla ya watu wanaoishi na VVU wapatao 965,081 walikuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU, ikiwa ni sawa na asilimia 69 ya watu 1,400,000 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI nchini na kati yao watoto walikuwa 55,304 ambao ni sawa na asilimia 5.7. Kutokana na takwimu hizo Tanzania tumebakiza asilimia 21 kufikia lengo la dunia la asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuanzishiwa dawa za kufubaza VVU ifikapo mwaka 2020. Wizara imeweka mikakati mbalimbali ili kufikia lengo hilo.

30.      Mheshimiwa Spika, Huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), zimeendelea kutolewa, ambapo, jumla ya akina mama wajawazito 1,967,260 sawa na asilimia 98.7% ya akina mama 1,993,639 walipatiwa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU. Kati yao akina mama 79,242 sawa na asilimia 4 waligundulika kuwa wanaishi na VVU. Akina mama 79,240 sawa na asilimia 99.9 ya akina mama wenye maambukizi ya VVU walipatiwa dawa (ARV) kwa ajili ya kufubaza virusi vya UKIMWI. Hivi sasa, maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni asilimia 4.9 kutoka asilimia 12 mwaka 2011.

Huduma za Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma

31.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mkakati wake wa Udhibiti wa ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma ambapo katika kipindi cha Julai hadi Machi 2017, Serikali ilinunua na kusambaza dawa za Kifua Kikuu na Ukoma. Katika kuhakikisha Serikali inaboresha matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa watoto, mwezi Machi 2018, Wizara yangu ilizindua matumizi ya dawa mpya za kifua kikuu kwa watoto. Dawa hizi mpya ni za mseto (RHZ/RH) ulioboreshwa, zina ladha nzuri ya matunda, zinayeyuka kwa urahisi zikiwekwa kwenye maji na hivyo hazihitaji kukatwakatwa ili kupata dozi sahihi. 

32.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za ugunduzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia vipimo vya vinasaba (gene-xpert) katika wilaya zote nchini ili kuongeza kazi ya kuwagundua wagonjwa wengi wa TB na kuwatibu. Kwa mwaka 2017/18, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ilinunua na kusambaza mashine za “genexpert” 189 ikilinganishwa na mashine 66 zilizokuwepo mwaka 2015. Mashine hizi zimesambazwa kwenye hospitali zote za rufaa za kanda, mikoa, wilaya na baadhi ya vituo vikubwa vya afya. Teknolojia ya mashine hizi inatuwezesha kupata majibu ndani ya masaa 2 badala ya kusubiri kwa zaidi ya masaa 24 kama ilivyo kwa njia za kawaida za hadubini (Microscopes). Aidha, mashine hizi zina uwezo wa kupima usugu wa dawa za kifua kikuu wakati huo huo wa upimaji wa makohozi, na hivyo kugundua kifua kikuu sugu kwa urahisi zaidi.

33.      Mheshimiwa Spika, Katika kudhihirisha nia ya serikali ya kushirikiana na Sekta binafsi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu hasa kuongeza idadi ya wagonjwa wa TB wanaogunduliwa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 70 mwaka 2020, Wizara yangu imekabidhi mashine za gene-xpert tano (5) kwa hospitali binafsi za jijini Dar es Salaam. Hospitali zilizopokea mashine hizi ambayo kila moja ina thamani ya Shilingi milioni 38 ni Aga Khan, Hubert Kairuki, Regency Medical Center, TMJ na Hindul Mandal. Tumeanza na hospitali hizi zenye viwango vikubwa vya wagonjwa wanaohudumiwa na pia kwa kuzingatia utayari wa hospitali hizi katika kutoa huduma za kifua kikuu sanjari na malengo ya Serikali yetu ya awamu ya tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote. Kadhalika, ushirikishwaji huu wa Sekta Binafsi katika kutambua wagonjwa wa kifua kikuu umeonesha ongezeko la wagonjwa wa TB wanaoibuliwa na sekta binafsi kutoka wagonjwa 3,476 mnamo mwaka 2014 hadi wagonjwa 7,281 katika mwaka 2017 ambao ni sawa na 10.4% ya wagonjwa wa TB waligunduliwa na sekta binafsi. Nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sekta binafsi kwa ushiriki wao katika kutokomeza TB nchini.

34.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya wagonjwa wa kifua kikuu sugu nchini. Katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Machi 2018 Wizara iliongeza vituo 41 na kufanya jumla ya vitu vinavyotoa huduma hiyo kufikia vituo 63 ikilingalishwa na kituo kimoja cha hospitali Maalum ya Kibong’oto mwaka 2015. Mikoa yenye vituo hivyo vilivyoweza kuanzisha matibabu ya wagonjwa chini ya ugatuzi ni Dar es salaam, Kagera, Geita, Mtwara, Lindi, Mbeya, Pwani, Morogoro, Tanga, Unguja, Tabora, Kigoma, Mwanza, Arusha, Rukwa na Simiyu. Vile vile, Wizara imeanzisha matibabu ya muda mfupi kwa wagonjwa wa kifua kikuu sugu kufupisha tiba hiyo kutoka miezi ishirini ya hapo awali mpaka miezi tisa kwa wagonjwa wanoakidhi vigezo.

35.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma, Wizara ilifanya uchunguzi wa vimelea vya Ukoma katika ngazi ya jamii kwenye Wilaya 6 zenye maambukizi makubwa katika mikoa ya Geita (Chato), Lindi (Liwale), Mtwara (Nanyumbu), Morogoro (Kilombero) na Tanga (Mkinga na Muheza). Katika zoezi hilo takriban watu 500 wamefanyiwa uchunguzi, ambapo watu 54 sawa na asilimia 10.8 waligundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa ukoma na kuanzishiwa matibabu, takriban watu 300 wamepatiwa tiba kinga.

Udhibiti wa Malaria

36.      Mheshimiwa Spika, Malaria imeendelea kuwa sababu ya vifo vya wananchi wengi ambapo kwa takwimu za Januari – Desemba 2017, jumla ya watu 5,592,844 wameugua ugonjwa huu, kati yao wagonjwa 4,421 walifariki kutokana na ugonjwa wa Malaria. Katika kuendeleza juhudi za kupunguza maambukizi ya malaria nchini; Wizara yangu imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za udhibiti wa malaria ikiwa ni pamoja na kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kusambaza katika vituo vya huduma za afya nchini. Ili kuendelea kuwakinga wananchi dhidi ya malaria, na hasa kulenga makundi maalum; wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja, Serikali imesambaza jumla ya vyandarua 4,726,763 kwa jamii bila malipo kupitia wanafunzi shuleni na kupitia kliniki za wajawazito na watoto (Chandarua Kliniki).

37.      Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu Afua ya kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia (larviciding), Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeratibu zoezi la usambazaji wa viuadudu vya kibailojia (biolarviciding) jumla ya lita 236,420 katika Halmashauri zote nchini, na Halmashauri zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa afua katika maeneo yao.

Udhibiti wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele

38.      Mheshimiwa Spika, Kutokana na utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele zikiwemo zilizoainishwa katika aya 48 na 49 ya Hotuba, jumla ya Halmashauri 93 zimefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha na hivyo kuondolewa kwenye orodha ya Halmashauri  zenye maambukizi makubwa zinazoshiriki katika zoezi la Kingatiba kulingana na vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO). Haya ni mafanikio makubwa kwani Watanzania wapatao 20,446,532 wanaoishi katika halmashauri hizi hawapo tena katika hatari ya maambukizi ya magonjwa haya.

Huduma za Lishe

39.      Mheshimiwa Spika, Katika kupambana na utapiamlo nchini, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wa Lishe imetoa matone ya nyongeza ya vitamin A kwa watoto wa kati ya miezi sita na miaka mitano sambamba na dawa za minyoo kwa watoto wa umri kati ya mwaka mmoja na miaka mitano. Aidha, Wizara yangu imeendelea kutoa huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto kupitia; kuongeza idadi yaHospitali zinazotoa matibabu ya utapiamlo, kuboresha miundombinu ya hospitali kwenye wodi za kulaza watoto, kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa chakula dawa na vifaa vya kupimia hali ya Lishe pamoja na kujengea uwezo wa watoa huduma.

Elimu ya Afya kwa Umma
40.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kutunza afya zao dhidi ya magonjwa, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kujenga tabia inayozingatia kanuni za afya. Wizara kupitia mpango wa Elimu ya Afya kwa Umma imeandaa mkakati wa mawasiliano utakaowezesha namna ya kuwasiliana kwa haraka wakati wa majanga na milipuko ya magonjwa, tayari timu za mikoa ya mipakani zimeelimishwa juu ya mkakati huo. Aidha, Wizara imekamilisha ujenzi wa studio ya radio na televisheni ambavyo vimeanza kurekodi vipindi vitakavyorushwa nchi nzima kwa ajili ya kuelimisha jamii ya Watanzania kuhusu masuala mbalimbali ya afya.

HUDUMA ZA TIBA

Usajili na Usimamizi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya


41.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia upatikanaji wa huduma za afya kupitia vituo vya kutolea huduma nchini vikiwemo vya Serikali, binafsi na mashirika ya dini. Hadi kufika Machi 2018, huduma za afya zimeendelea kutolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya 7,437 ikilinganishwa na vituo 7,284 mwezi Juni 2017. Aidha, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya Vituo binafsi 153 vya kutolea huduma za Afya vilisajiliwa.

 

Uimarishaji wa Huduma za Matibabu ya Kibingwa


42.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, moja ya jukumu la kipaumbele kwa Wizara ilikuwa ni kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa yatolewayo nchini. Maboresho hayo, yanalenga katika kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya matibabu nje ya nchi ili kupunguza gharama kubwa kwa Serikali katika kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Hadi kufikia mwezi Machi 2018, idadi ya Wagonjwa waliopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ilipungua na kufikia Wagonjwa 103 ikilinganishwa na wagonjwa 304 mwaka 2016/17. Mafanikio haya ni kutokana na maboresho yaliyofanyika katika Hospitali zilizo chini ya Wizara ambapo kwa hivi sasa zimeongezewa uwezo wa kutoa huduma za Kibingwa ambazo awali hazikuwa zikitolewa hapa nchini na hivyo kulazimu wagonjwa kupatiwa rufaa nje ya nchi. Jumla ya wagonjwa 1,090,863 walihudumiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani Ocean Road, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Magonjwa ya Akili Mirembe, Hospitali ya Magonjwa ya Kifua Kikuu Kibon’goto na Hospitali za Rufaa za Kanda za Mbeya, KCKM na Bugando.  Mchanganuo wa idadi ya wagonjwa kwa kila Hospitali umeoneshwa katika Kiambatisho Namba 2 cha Hotuba yangu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

43.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Hospitali ilifanya ukarabati wa jengo la kutolea huduma za upandikizaji wa Figo na ununuzi wa vifaa Tiba kwa ajili huduma za upandikizaji wa figo iliyoanza kutolewa Mwezi Novemba 2017 ambapo Mgonjwa mmoja (1) alipatiwa huduma hiyo na kwa sasa wagonjwa watano (5) wamepangwa kupatiwa huduma hii mwishoni mwa Mwezi Aprili 2018. Hatua hii imepunguza gharama za kupandikiza figo kwa mgonjwa mmoja nje ya nchi kutoka wastani wa Shilingi milioni mia 100 hadi milioni 20.

44.      Mheshimiwa Spika, Hospitali imeanzisha huduma za upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (Cochlea implant), hadi kufikia mwezi Machi 2018, wagonjwa sita (6) walipata huduma ya kuwekewa vifaa vya usikivu. Huduma ya kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia inatolewa kwa wastani wa Shilingi milioni 36 kulinganisha na Shilingi milioni 80 hadi 100 ambazo zingetumika endapo mgonjwa angepelekwa nje ya nchi.

45.      Mheshimiwa Spika, ukusanyaji wa mapato ya Hospitali kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi, 2018 umeongezeka na kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 46.51 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 31.91 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho 2016/17. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 45.7. Mafanikio haya yamewezesha hospitali kukamilisha miradi yake mbalimbali iliyoainishwa katika aya 59 ya Hotuba.


Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)

46.      Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Februari 2018, Taasisi kwa mara ya kwanza imeweza kufanya upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu (Laparascopy) kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya BLK ya India. Upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa, lengo mahsusi ikiwa ni kuwapatia weledi madaktari wa MOI ili waweze kufanya upasuaji huo. Aidha,katika mwaka 2017/18, Taasisi ilikamilisha jengo la MOI awamu ya III pamoja na ununuzi wa Vifaa tiba mbalimbali kutokana na fedha Shilingi Bilioni 16.5 zilizopokelewa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zilizofanyika zimeainishwa katika aya 64 ya Hotuba. Makusanyo katika Hospitali hadi mwezi Februari, 2018 yamefikia kiasi cha Shilingi 10,807,695,141.93 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi 6,707,172,559.43 zilizokusanywa kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwezi Februari, 2017.

 

Taasisi ya Moyo - Jakaya Kikwete (JKCI)


47.      Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilihudumia jumla ya wagonkwa wenye matatizo ya moyo 42,029. Kati ya hao, wagonjwa 111 walifanyiwa upasuaji ambao watu wazima walikuwa 52 na watoto walikuwa 59. Aidha wagonjwa 157 walipatiwa matibabu kwa njia ya upasuaji  wa moyo kupitia mishipa ya damy (cardiac catheterization). Hivi sasa Taasisi ina uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za ubingwa wa hali ya juu kwa asilimia 85 kwa huduma za awali ambazo awali zilikuwa zikipatikana nje ya nchi. Hali hii imesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa wa moyo nje ya nchi na kuipunguzia Serikali gharama ambapo hadi kufikia March 2018 wagonjwa wa mouo waliopeleela India ni 12 kutoka wagonjwa 43 kwa mwaka 2016/17. Taasisi kwa kushirikiana na Madaktari rafiki wa nchi za Marekani, India, Italy, Israel na Australia walifanya kambi maalum za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa watoto na watu wazima nchini kwa mafanikio makubwa kama ilivyoainishwa katika aya 66 mpaka 68 ya Hotuba. Aidha, Taasisi imeweza kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 8,462,092,000 Katika kipindi cha hadi Machi 2018 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi 4,105,000,000.00 kilichokusanywa katika kipindi hicho mwaka 2016. 

Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI)

48.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa wa Saratani ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2018, Taasisi imeboresha tiba za mionzi ya nje kwa kufunga kifaa kiitwacho 'multi-leaf collimator' katika mashine ya EQ80 ambacho kimenunuliwa kwa kushirikiana na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA). Aidha, Taasisi imenunua vyanzo vipya vya mionzi kupitia Bohari ya Dawa kwa gharama ya Shilingi 473,363,437.50. Hatua hii imeboresha utoaji wa tiba ya mionzi ya ndani kwa kutibu wagonjwa 70 kutoka wagonjwa 30 kwa siku. Vile vile, Taasisi inaendelea kufunga mashine za tiba mpya na za kisasa za mionzi aina ya “Linear Accelerator”, (LINAC) 2 na ‘CT Simulator’ (1) ambazo zimenunuliwa kwa gharama ya Shilingi 9,500,000,000. Mashine hizo zitaiwezesha Taasisi kutoa huduma ya matibabu ya mionzi na kupunguza muda wa wagonjwa kusubiria tiba kutoka wiki 6 sasa kufikia wiki 2 na kuongeza ufanisi katika tiba inayotolewa. Vilevile, Taasisi tayari imewapeleka mafunzoni nje ya nchi watumishi 7 kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa kutumia mashine hizo ambao ni Madaktari bingwa 2, Wataalamu wa tiba ya mionzi 2, Medical physicist 2 na Bio-engineer 1.  

49.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Taasisi imeanzisha huduma za wodi za binafsi ambayo ina vitanda 4 vya VIP na vitanda 20 vya binafsi. Hatua hii imesaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa wenye uhitaji huo na pia kuongeza mapato. Lengo la huduma hizi ni kuhakikisha kuwa wananchi wenye uwezo wa kuchangia gharama wanakaa katika wodi binafsi. Kukamilika kwa wadi binafsi kumechangia kuongezeka kwa makusanyo ya Taasisi, ambapo katika kipindi Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya Shilingi 86,622,300 zilikusanywa ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi 40,320,000 kilichokusanywa kwa kipindi cha mwaka 2016/17.  Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 53.

Hospitali ya Benjamin Mkapa –Dodoma


50.      Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa, mnamo tarehe 22/3/2018, Hospitali kwa kushirikiana na TOKUSHIKAI Medical group kutoka nchini Japan, ilifanikiwa kufanya upandikizaji figo kwa mara ya kwanza kwa mgonjwa mmoja mwenye umri wa miaka 51. Hali ya mgonjwa inaendelea vizuri na amepewa ruhusa kwenda nyumbani. Aidha, Matayarisho ya kuanzisha huduma za upasuaji wa moyo yapo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji. Vile vile, Hospitali iko katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo kwa kutumia mashine maalum (Hemodialysis). Pia, hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma za chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Upatikanaji wa dawa katika hospitali ilikuwa kwa asilimia 95.2 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018. Uwezo wa hospitali kukusanya mapato umeendelea kuimarika ambapo jumla ya Shilingi 1,892,978,585 kimekusanywa hadi Machi 2018 ukilinganisha na Shilingi 794,162,415 zilizokusanywa katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari 2017 kwa mwaka  2016/17.

Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe

51.      Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Mirembe na Tasisi ya Isanga imeendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili ambapo hali ya upatikanaji wa dawa imeendelea kuimarika na kufikia zaidi ya asilimia 90 kwa dawa muhimu za magonjwa ya akili. Aidha, hospitali imeendelea kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wa akili wa kawaida na wagonjwa wa akili walio na tuhuma za uvunjaji wa sheria kwa kuwafanyia uchunguzi, kutoa ushauri kwa mahakama, Tiba kwa umeme, Tiba kwa vikundi, Tiba kwa familia, Tiba kwa maongezi na Tiba kwa kazi (Occupational Therapy) kwa wataalamu wa kada mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa wa afya ya Akili (Psychiatrist), Saikolojia (Clinical Psychologist), Mishipa ya fahamu (Clinical Neurologist) na wengine. Vile vile, katika mwaka 2017/18, hospitali imeendelea na ujenzi wa Jengo la kuhudumia waathirika wa Dawa za kulevya lililopo chini ya Hospitali ya Mirembe katika eneo la Itega ambapo mkandarasi yupo katika eneo husika anaendelea na kukamilisha ujenzi ili huduma zianze kutolewa mapema.

Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu- Kibong'oto

52.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Hospitali iliendelea kutoa huduma za utambuzi na matibabu ya Kifua kikuu, Kifua kikuu sugu, VVU na magonjwa mengine ya kuambukiza.  Aidha, Hospitali imeweza kutoa elimu kwa wataalamu 239 (Madaktari, wauguzi, wataalam wa maabara pamoja na wafamasia) kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuanzisha matibabu ya kifua kikuu sugu (Multi-Drug Resistant TB, MDR TB). Pia Hospitali imeweza kuanzisha jengo la kutolea huduma kwa waathirika mahala pa kazi (Occupational Health Services). Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Southern African Development Community (SADC) imeanzisha huduma za afya kwa wachimbaji Madini na familia za Wachimbaji Madini katika Hospitali hii.

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya


53.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2017/18, Hospitali imeendelea kuboresha huduma za kibingwa kwa kuongeza miundombinu ya kutolea huduma kama ilivyoainishwa katika aya 82 ya Hotuba. Upatikanaji wa dawa katika hospitali umekuwa katika kiwango cha asilimia 95 hivyo wananchi wameondolewa usumbufu wa kufuata dawa nje ya hospitali. Ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 ulikuwa Shilingi 9,931,439,974.57 ukilinganisha na Shilingi 5,607,223,511.78 kwa mwaka 2016/17.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando

54.      Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando imeendelea kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka mikoa 8 ya Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu, Kigoma, Shinyanga na Tabora. Kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, hospitali ilifanya upasuaji kwa wagonjwa 72 wenye matatizo ya Saratani ya Utumbo mpana, saratani za tumbo, magonjwa ya pua na koo pia uti wa mgongo. Upasuaji huu ulifanywa na Madaktari wazalendo kwa kushirikiana na madaktari kutoka Marekani (Mending Kids). Pia, Hospitali imenunua Mashine ya kutibu mionzi ya ndani (Brachytherapy) kwa kushirikiana na Shirika la nguvu la Atomiki Duniani (IAEA). Kuhusu Huduma ya tiba ya saratani, jumla ya wagonjwa 131 wa saratani ya mlango wa kizazi walipatiwa huduma ya tiba ya saratani kwa njia ya mionzi (Radiotherapy). Vilevile, Hospitali imenunua mashine 2 za vipimo vya moyo na 1 ya ultrasound, pamoja na mashine ya CT Scan (128 slice) kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.7 kutokana na mapato ya ndani.

 

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kaskazini (KCMC)


55.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Hospitali imeendelea kuboresha na kutoa huduma kwa wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga ambapo Hospitali imeweza kuhudumia wagonjwa 1,123 wa saratani ambapo wagonjwa 47 walipatiwa huduma shufaa (Palliative care). Aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu kwa jamii juu ya maradhi ya saratani, Hospitali kwa kushirikiana na Taasisi ya “Mission Eine Welt” ya nchini Ujerumani, imeanzisha kampeni maalum mwezi Oktoba 2017 ijulikanayo kama PrevACamp yaani Prevention and Awareness Campaign yenye lengo la kutoa elimu juu ya saratani, kuainisha mila na imani potofu na kufanya uchunguzi wa viashiria vya awali vya saratani.

Hospitali za Rufaa za Mikoa
56.      Mheshimiwa Spika, Uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ulikuwa unasimamiwa na kuratibiwa na OR-TAMISEMI. Hata hivyo, baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa tarehe 25 Novemba 2017, usimamizi na uendeshaji wa Hospitali hizi sasa upo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizopo ni 28. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi 2018, jumla ya wagonjwa 1,637,835 walihudumiwa katika Hospitali ya Rufaa za Mikoa ya Mount Meru (Arusha), Dodoma General (Dodoma), Kitete (Tabora), Shinyanga, Geita, Singida, Mpanda (Katavi), Mawenzi (Kilimanjaro), Bombo (Tanga), Morogoro, Ligula (Mtwara), Sokoine (Lindi), Maweni (Kigoma), Sekou Toure (Mwanza), Mwananyamala, Amana, Temeke (Dar es Salaam), Songwe, Kibena (Njombe), Iringa, Tumbi (Pwani), Sumbawanga ( Rukwa), Bariadi (Simiyu), Musoma (Mara), Songea (Ruvuma), Mbeya, Babati (Manyara) na Bukoba (Kagera).
57.      Mheshimiwa Spika,  Wizara imeweka mikakati ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ili kuhakikisha kwamba huduma muhimu za kibingwa za Upasuaji (General Surgery), Magonjwa ya Wanawake na Uzazi (Obstetrics & Gynaecology), Magonjwa ya Watoto (Paediatrics & Child Health), Magonjwa ya ndani (Internal Medicine), Magonjwa ya Kinywa na Meno (Dentistry) na Radiolojia (Radiology) zinazotolewa katika Hospitali hizo zinaboreshwa. Mikakati hiyo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kutoa huduma, kuongeza idadi ya madaktari bingwa, kuboresha upatikanaji wa dawa, kupanga kwa uwiano watumishi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kwa kuzingatia huduma na uzito wa kazi zinazotolewa na hospitali hizo, kuanzisha na kuboresha huduma za afya kwa njia ya masafa (telemedicine) kwa kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kufanya huduma hiyo kutumika kama kiunganishi kati ya Hospitali hizo na Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa, kuboresha utoaji wa huduma za uchunguzi wa maabara na radiolojia kwa kupanua na kuimarisha miundombinu ya huduma za uchunguzi ikiwa ni pamoja na kununua na kuweka vifaa vya kisasa vya maabara na radiolojia.

Udhibiti wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCDs)

58.      Mheshimiwa Spika, Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba kumekuwa na ongezeko la Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza hapa nchini. Utafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012, ulionesha kuwa kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Utafiti huo ulionesha kuwa asilimia 15.9 ya wananchi wanavuta sigara, asilimia 29.3 wanakunywa pombe, asilimia 97.2 wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa wiki. Aidha, utafiti ulionesha kuwa, asilimia 26 ya wananchi ni wanene kupita kiasi, asilimia 26 wana lehemu nyingi mwilini, asilimia 33.8 wana mafuta mengi mwilini, asilimia 9.1 wana kisukari na asilimia 25.9 wana shinikizo kubwa la damu. Utafiti pia ulionesha kwamba, asilimia 25 ya wananchi waliohojiwa hawajishughulishi na kazi zinazotumia nguvu na hawafanyi mazoezi yeyote.

59.      Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiendelea ndani ya Wizara yangu na yamejikita zaidi katika masuala ya Kinga, kama tunavyofahamu kuwa Kinga ni bora kuliko Tiba. Tangu kuanzishwa kwa kampeni ya “Afya Yangu Mtaji Wangu” iliyozinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara imeendelea kuhimiza jamii kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara sambamba na kujiepusha na visababishi vingine vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo ulevi kupita kiasi na uvutaji wa sigara na tumbaku. Aidha, Wizara imeendelea kushirikiana na Wadau kufanya Kampeni za uchunguzi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika Mikoa yote. Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge lako tukufu kwa kuanzisha Jukwaa la Waheshimiwa Wabunge la Kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ili waweze kupata elimu juu ya namna ya kujikinga na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza na kuwaelimisha wananchi juu ya magonjwa hayo.

Upatikanaji wa Damu Salama

60.      Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa damu salama, Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeendelea kukusanya, kuhifadhi na kusambaza damu salama katika vituo vya kutolea huduma za afya. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018 Mpango ulifanikiwa kukusanya idadi ya chupa za damu 233,953 ambazo ni sawa na asilimia 101 ya lengo la makusanyo kwa mwaka ambalo lilikuwa ni kukusanya chupa za damu 230,000.  Nitumie Bunge lako Tukufu kuwashukuru wananchi wote wanaojitolea kuchanga damu. Aidha, nitoe rai kwa watanzania kuchangia damu mara kwa mara ili kuokoa maisha ya wagonjwa hasa wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka 5.

Upatikanaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi

61.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara yangu imeendelea kuhakikisha kwamba hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma inaendelea kuimarika.  Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuimarika hadi kufikia wastani wa asilimia 81 kwa Dawa muhimu 135. Aidha, katika kipindi hicho, hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo ilifikia asilimia 92 kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vilevile, kutokana na kuendelea kuwasili kwa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na chanjo nchini, na kwa mujibu wa mikataba iliyopo kati ya wazalishaji na Bohari ya Dawa, hali ya upatikanaji wa dawa kwenye hospitali inatarajiwa kuimarika na kufikia asilimia 89 ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili 2018.

62.      Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuanzisha viwanda vya dawa Nchini ili kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliweza kuandaa mkutano mkubwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika viwanda vya dawa na vifaa tiba. Jumla ya wadau mia nne thelathini (430) walihudhuria mkutano huo na wawekezaji thelathini na nane (38) walijitokeza kwa nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa dripu (infusion), uzalishaji wa bomba za sindano, uzalishaji wa vifungashio vya dawa, uzalishaji wa bidhaa za pamba zinazotumika hospitalini na uzalishaji wa dawa za kuhifadhi maiti. Uwepo wa Viwanda hivyo utawezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza dawa toka nje ya nchi. Jitihada hizi zitasaidia kuongeza uzalishaji wa ndani ambao kwa sasa hivi ni asilimia 6 hivyo na kupunguza kiwango cha uagizaji wa dawa nje ya nchi ambao kwa sasa ni asilimia 94.

UHAKIKI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

63.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanya Uhakiki na Ukaguzi kwa vituo vya kutolea huduma za Afya. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilifanya  zoezi la tathmini ya mara ya pili (re-assessment) ya kutoa nyota kulingana na ubora kwa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ya Msingi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika Halmashauri/Wilaya) katika mikoa 14 ya Dar es Salaam, Iringa, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Mara, Mwanza, Pwani, Tanga, Tabora, Singida, Simiyu na Shinyanga. Matokeo yanaonesha vituo 180 sawa na asilimia 4.7 tu ndivyo vimepata nyota sifuri na Vituo 749 sawa na asilimia 19.4 vilipata nyota 3 na zaidi ukilinganisha na matokeo ya tathmini ya awali ya mwaka 2016 ambapo jumla ya vituo 1,244 sawa na asilimia 33 ya vituo vyote 3,713 vilivyofanyiwa tathmini ya ubora katika mikoa vilipata nyota sifuri na vituo 62 sawa na asilimia 2 vilipata nyota 3 au zaidi. Matokea haya yanaonyesha kuimarika kwa ubora wa huduma za afya katika vituo hivyo ambako ndiko wananchi wengi wanapata huduma za afya.

RASILIMALI WATU KATIKA SEKTA YA AFYA

64.            Mheshimiwa Spika, Katika kuongeza idadi ya wataalamu wa Afya nchini, Wizara imeendelea kushirikiana na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE katika kusimamia ubora wa mafunzo ya kada za Afya zisizo katika kiwango cha shahada.Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya wanafunzi 16,214 walichaguliwa kujiunga na vyuo vya Afya. Kati ya hao wanafunzi 6,564 walichaguliwa kwenye vyuo vya Serikali na 9,650 kwenye vyuo binafsi katika programu za Uuguzi na Ukunga, Sayansi Shirikishi za Afya na wahudumu Afya ya Jamii. Aidha, Jumla ya wanafunzi 23,098 walifanya mitihani ya kuhitimu katika kipindi hiki, kati yao 10,669 ni wa Sayansi Shirikishi za Afya, 7,300 wa Uuguzi na Ukunga na wa Wahudumu Afya ya Jamii 5,129.

65.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Maendeleo katika kutoa ufadhili wa mafunzo ya kibingwa ya muda mfupi na muda mrefu yanayolenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa sekta ya Afya. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 jumla ya Watumishi 376 wameendelea kulipiwa gharama za masomo yao ndani na nje ya nchi katika ngazi ya shahada ya Uzamili hususan Madaktari Bingwa katika fani za kipaumbele za upasuaji, magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani na radiolojia.

66.            Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2017/18 ,Wizara yangu, ilipokea kibali cha ajira ya watumishi 3,152 wa kada za afya kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kibali hicho kilikuwa na nafasi za Madaktari Daraja la II 45, Madaktari Bingwa (Medical Specialist) 24, Madaktari Washauri (Medical Consultant) – 2, Wauguzi Daraja la II 137 na kada nyingine za Afya 3,081 ambapo mchakato mzima wa kujaza nafasi za ajira ambazo Wizara ilipewa ulikamilika na Watumishi wote walipatikana isipokuwa Madaktari Washauri. Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishawapangia Vituo vya kazi Watumishi hao. Aidha Katika kipindi hiki jumla ya Wataalam wa kigeni 35 walipata ajira katika taasisi mbalimbali za Serikali.

67.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu, imeendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi ambao wanafanya kazi katika maeneo yenye mazingira magumu ili kuwapatia motisha ili kuendelea kutoa huduma za afya katika maeneo hayo. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2018 jumla ya nyumba 30 zimejengwa na kukamilika katika Halmashauri tatu (3) za mkoa wa Manyara, ambazo ni ; Halmashauri za Kiteto 10, Simanjiro 10 na Hanang nyumba 10.  Kukamilika kwa nyumba hizo kumeongeza idadi ya nyumba za watumishi zilizojengwa kupitia mradi huu wa ‘Global Fund’ na kufika nyumba 480 katika maeneo yenye mazingira magumu.

UGHARAMIAJI WA HUDUMA ZA AFYA

68.              Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inaendelea na utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Hadi kufikia Machi 2018, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na jumla ya kaya 2,096,692 zilizojiunga ukilinganisha na kaya 2,030,666 zilizokuwa zimejiunga mwaka 2016/17. Aidha, wanufaika wameongezeka kutoka 12,183,996 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanufaika 12,580,149 Machi 2018 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote. Vilevile, katika kuchangia juhudi za wananchi wanaochangia CHF na kuboresha huduma zitolewazo, Serikali hutoa malipo ya tele kwa tele kwenye Halmashauri kulingana na kiwango cha makusanyo ya CHF. Malipo yaliyofanyika kwa Halmashauri kwa kipindi cha kuanzia Julai 2017 hadi Machi 2018 ni Shilingi bilioni 1.4.  na hivyo kuwezesha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kulipa malipo ya Tele kwa Tele yenye jumla ya Shilingi bilioni 15.8 kwa Halmashauri mbalimbali nchini tangu Mfuko ulipokabidhiwa jukumu hili mwezi Julai 2009.

69.                Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za kuhakikisha inafikia malengo ya afya kwa wote (Universal Health Coverage) ambapo kila mwananchi atakuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma bora za afya bila kuwa na kikwazo cha kifedha. Lengo ni kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 70 ya wananchi wawe wamejiunga na mifuko ya Bima ya Afya. Hali iliyopo sasa kuwa ni takribani asilimia 32 ya watu wote ndiyo waliopo katika mfumo wa Bima za Afya nchini. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, kwa nafasi zao na ushawishi mkubwa walionao katika jamii tunayoishi, kuendelea kuwaelimisha wananchi wote umuhimu wa kujiunga na kuchangia katika mfuko huo wa bima ya afya ili waweze kupata huduma za tiba bila kikwazo cha fedha.

70.              Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeanza utekelezaji wa azimio la kupeleka fedha moja kwa moja katika Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini (Direct Health Facility Financing (DHFF) badala ya kuzipeleka kwenye Halmashauri zao. Hatua hii imelenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za afya na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Utekelezaji wa azimio hili umeanza katika kipindi cha 2017/2018 ambapo fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya vituo vya kutolea huduma za Afya zilipelekwa moja kwa moja kutoka Hazina kwenda katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati. Jumla ya Shilingi 45,751,004,800 zimetolewa na kupelekwa katika vituo 5,170. Hatua hii imechangia kuboresha upatikanaji wa fedha katika vituo kwa wakati na kusaidia vituo kupanga mikakati ya kuboresha huduma na kuleta ufanisi.




TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO

71.            Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa eHealth strategy 2013-2018. Katika mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI na Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation kupitia mdau wa maendeleo PATH ilizindua Mpango wa Uwekezaji (Digital Health Investment Recommendation Roadmap). Mpango huu umeainisha vipaumbele vinavyohitajika vya matumizi ya mifumo ya kielektroniki ili kuboresha huduma za afya katika ngazi zote, pamoja na umuhimu wa kukusanya taarifa na matumizi sahihi ya takwimu za sekta ya Afya kwa ujumla. Aidha, Wizara imefunga mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji wa taarifa za chanjo katika vituo vya Afya. Hadi kufikia Machi 2018, jumla ya vituo 1,303 vya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro Tanga, Manyara na Dodoma vilifungiwa mfumo na kupewa vifaa vya komputa. Vilevile jumla ya watumishi 3,258 walipewa mafunzo ya jinsi ya kutumia mfumo huu.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO INAYOPATA RUZUKU TOKA SERIKALI KUU KWA MWAKA 2017/18

72.            Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, Wizara ilitenga kiasi cha Shilingi 785,805,952,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizi, Shilingi, 336,300,000,000 ni fedha kutoka vyanzo vya ndani na Shilingi 449,505,952,000 ni fedha kutoka vyanzo vya nje.

Miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Ndani

73.            Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea Shilingi 74,756,079,206.00 (Fedha za Ndani) ambazo zilitumika kutekeleza miradi iliyoainishwa kwenye aya 128 ya Hotuba yangu.

Miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Nje

74.          Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea fedha, dawa, vifaa na vitendanishi vyenye thamani ya Shilingi 403,530,227,600.94kutoka katika Vyanzo vya Nje kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kuboresha huduma za afya nchini kwa mchanganuo ufuatao:

Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund)
Kazi zilizotekelezwa kupitia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja zimeainishwa katika aya 129 ya Hotuba.

Mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF)

75.            Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2018, Wizara yangu kwa kushirikiana na OR– TAMISEMI ilikarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Vituo 1,325 vya Serikali vya kutolea huduma za afya katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Pwani, Tabora, Simiyu, Kigoma, Kagera na Geita. Aidha, jumla ya Shilingi 3,425,162,919 zilipelekwa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kulipwa kama motisha kwa Timu za Uendeshaji wa shughuli za Afya za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Uimarishaji wa huduma za dharura za mama na mtoto (CEmONC)

76.            Mheshimiwa Spika, moja ya vipaumbele vya Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 ni kupunguza vifo vya akina mama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza azma hiyo serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeanza kufanya ukarabati/ ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ikiwemo chumba cha upasuaji, maabara, wodi ya wazazi na wodi ya watoto utakaowezesha upatikanaji wa huduma kamili za uzazi ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, ili kupunguza vifo vya mama na watoto. Kupitia mpango huo, jumla ya vituo vya Afya 208 vinaboreshwa. Katika kutekeleza mradi huu, jumla ya Shilingi 40,000,000,000 kutoka Banki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha Vituo vya Afya 100 na Shilingi 19,500,000,000.00 kutoka Denmark kwa ajili ya vituo vya Afya zimepelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini kukamilisha kazi ya ukarabati na ujenzi ambao upo katika hatua mbalimbali chini ya uangalizi wa OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI inakamilisha mchanganuo wa vituo vya afya 21 vitakavyoboreshwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja.

Mfuko wa Dunia (Global Fund):

77.             Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara ilipokea fedha, dawa, vifaa tiba na vitendanishi vyenye thamani ya Shilingi 303,238,541,795.37 kwa ajili ya kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu, na Malaria.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI CHINI YA IDARA KUU YA AFYA

 

Bohari Kuu ya Dawa (MSD)


78.            Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2017/18, Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa kuingia makubaliano ya muda mrefu (Framework Agreement) na viwanda vya uzalishaji dawa. Jumla ya wazalishaji 110 tayari wana mikataba na MSD na kati ya hao wazalishaji 10 ni viwanda vya ndani. Mpango huu umewezesha MSD kufanikiwa kupunguza bei ya dawa 109 kwa  wastani wa asilimia 40. Hali hiyo imesaidia vituo vya afya kuweza kununua dawa kwa bei nafuu na hivyo kuongeza kiasi cha dawa. Aidha, Bohari  Kuu ya Dawa inaendelea kuimarisha mfumo wake wa usambazaji wa dawa ili kuhahikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma  unafikia asilimia 100. Katika kufanikisha hili jumla ya magari 181 yamenunuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Global Fund, Magari hayo yalizinduliwa na Mhe. Rais tarehe 26 Machi, 2018. Hali hiyo imewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na dawa muhimu kwa asilimia 89.6. Vilevile, upatikanaji wa dawa za  ARVs umeimarika na kuwa  kati ya asilimia 92 hadi 100

MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)

79.            Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuongeza wigo wa wanufaika wa bima ya afya.kufuatia utekelezaji wa mikakati hiyo, katika kipindi cha Julai 2017 hadi kufikia Machi 2018, Mfuko umeweza kusajili idadi ya wanachama wapya wapatao 167,791 kutoka katika Sekta ya Umma na Binafsi sawa na asilimia 97 ya lengo. Hivyo idadi ya wanachama wachangiaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeongezeka kutoka wanachama 753,992 waliokuwa wameandikishwa mwaka 2016/17 hadi kufikia wanachama 763,068 mwezi Machi 2018. Aidha, idadi ya wanufaika nayo iliongezeka kutoka 3,491,400 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanufaika 3,619,697 mwezi Machi 2018 sawa na asilimia 7 ya Watanzania wote. Hii inaonyesha kuwa wanachama wa Mfuko wameongezeka kwa wastani wa asilimia 10 na wanufaika asilimia 7 katika kipindi cha miaka mitano.

80.                Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inaendelea na  utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018 kaya mpya zilizoandikishwa kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) zilikuwa 66,026 na kufanya jumla ya kaya 2,096,692 zilizojiunga ukilinganisha na kaya 2,030,666 zilizokuwa zimejiunga mwaka 2016/17. Aidha, wanufaika wameongezeka kutoka 12,183,996 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanufaika 12,580,149 Machi 2018 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote. Aidha, mafanikio hayo yametokana na  juhudi zinazofanywa na Mfuko za kuelimisha wananchi pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza wigo wa wanachama, kama kuanzishwa kwa mpango wa KIKOA (unaojumuisha kundi la wajasiriamali, vikundi vya vikoba, saccos na wavuvi), TOTO AFYA KADI (unaojumuisha watoto chini ya miaka 18), Wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya Juu, Wastaafu na wanachama binafsi.

81.                  Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia NHIF na kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) Ilianza kutekeleza  Mpango wa NHIF/CHF kwa Wanawake Wajawazito na Watoto ujulikanao kama Tumaini la Mama mwaka 2012 ambapo kina mama wajawazito hulipiwa kadi za NHIF/CHF na kuwa na uhakika  wa kupata matibabu katika kipindi chote cha ujauzito na miezi sita baada ya kujifungua kwa mama na mtoto. Mpango huu una lengo la kupunguza vifo vya kina mama na watoto ili kwenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu (SDGs). Katika kipindi cha kuanzia Julai 2017 mpaka Machi 2018, akina mama 199,954 na watoto 20,998 walikuwa wamesajiliwa na kunufaika na mpango huu. Tangu kuanzishwa kwa mpango, tayari wanawake wapatao 875,375 wamenufaika katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Lindi, Mtwara na Songwe. Aidha, shughuli nyingine zinazofanywa na NHIF katika kuboresha huduma za afya zimeainishwa katika aya 141 mpaka 144 ya Hotuba.


82.                Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa, inatekeleza Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (5) wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (2017/18 - 2021/22). Mamlaka ilifanya tathmini ya maombi ya usajili wa vyakula na kukagua viwanda vya dawa na viwanda vya vyakula nje ya nchi ambapo matokeo yalikuwa kama ilivyoainishwa kwenye aya 146 na 147 ya Hotuba. Aidha, Mamlaka imeendelea na utoaji wa elimu kwa umma kwa makundi mbalimbali ya wananchi kuhusu  madhara ya dawa, vipodozi hatarishi na usalama wa chakula pamoja na jumbe fupi zilirushwa kupitia redio, runinga, magazeti na mitandao mbalimbali ya kijamii.

83.              Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2017/18, mfumo wa kupokea taarifa za usajili wa vitendanishi kwa njia ya mtandao umetengenezwa na kuanza kutumika na hivyo kupungua kwa muda wa kushughulikia maombi yanayowasilishwa na wateja. Mamlaka imeweza kuweka taarifa za bidhaa zote zilizosajiliwa nchini kwenye mtandao ambao umeunganishwa na mfumo wa kielektroniki wa ndani (www.tfda.go.tz/portal/registered-products). Taarifa hizi zinasaidia wananchi na wateja kwa ujumla kuona bidhaa zilizosajiliwa na tarehe za kuisha muda wa usajili.

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

84.                Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2017/18, Taasisi iliyokuwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilibadilishwa rasmi na kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sheria Na. 8 ya mwaka 2016. Katika kuhakikisha kwamba Mamlaka inafanya kazi kwa ufanisi, mamlaka imesaini mikataba mitatu (3) ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4, vifaa hivyo vinatarajiwa kupokelewa kabla ya mwezi Juni, 2018. Aidha, ukarabati wa Maabara ya DNA Makao Makuu Dar es Salaam umeanza na unategemewa kumalizika mwezi Juni 2018.

 

TAASISI YA CHAKULA NA LISHE (TFNC)


85.                 Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Chakula na Lishe imeendelea kutekeleza majukumu mbalimbali katika kuimarisha utoaji wa huduma za Lishe nchini. Katika kutekeleza azma ya Serikali  ya kupunguza vifo vya watoto wadogo na wachanga nchini, Taasisi imeendelea kuratibu zoezi la kitaifa la utoaji wa vitamini A ya nyongeza kwa watoto wenye umri kati ya miezi 6 hadi 59 na dawa za kutibu minyoo kwa watoto wenye umri wa miezi 12 hadi 59. Msisitizo katik kipindi hiki ulikuwa ni kufuatilia  na kutoa usaidizi katika mikoa na Halmshauri  ambao zilibainika  kutofikia asilimia 90 inayopendendwawa na Shirika la Afya Dunia.


TAASISI YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU (NIMR)

86.                Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeendelea kutekeleza majukumu yake ya Utafiti. Taasisi imefanya tafiti mbalimbali ikiwemo tafiti za Majaribio ya Chanjo ya UKIMWI, Tiba Mbadala, Afya ya mama na mtoto, Malaria na TB. Matokeo ya tafiti hizi yamesaidia kuandaa afua mbalimbali za kuboresha huduma kwa waathirika wa magonjwa hayo. Aidha, tafiti kwenye afya ya mama na mtoto zinalenga kuboresha mfumo wa afya hasa upatikanaji wa huduma ikiwemo chanjo, elimu ya lishe na hatua za kupunguza vifo vya mama na watoto chini ya miaka 5. Taasisi kwa kushirikiana na Wizara na wadau wa Afya imefanya tathmini ya uwepo wa maji salama na usafi wa mazingira (WASH) katika vituo vya afya mbalimbali vinavyotoa huduma za kujifungua. Taarifa zilizopatikana kutokana na utafiti huo ni kwamba, pamoja na Serikali kupitia Sekta ya Afya kusisitiza wananchi kwenda kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya, bado yapo mapungufu makubwa ikiwa ni pamoja na yafuatayo; Asilimia 19 ya vituo hutumia maji toka vyanzo visivyoboreshwa vikiwemo vyanzo wazi kama mito na mabwawa na visima visivyoboreshwa; Asilimia 46.5 ya sampuli za maji zilizopimwa zilionekana kuwa na vimelea vya maambukizi ya magonjwa mbalimbali; Asilimia 42 ya vyumba vya kuzalia havikuwa na sehemu za kunawia mikono; Asilimia 10 ya vituo hasa zahanati vilikuwa na vyoo duni visivyoboreshwa na kuleta hatari ya maambukizi.

87.                Mheshimiwa Spika, Wizara imejipanga kufanyia kazi matokeo yaliyobainishwa na utafiti huo kwa kuelekeza msukumo mkubwa katika eneo la afya Kinga ikiwa ni pamoja na kushirikiana na OR-TAMISEMI kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuondoa changamoto zilizobainishwa na utafiti huo.

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII

88.                Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea  kutekeleza afua kwa kushirikiana wadau mbalimbali katika maeneo muhimu yafuatayo:

Uwezeshaji Wanawake

89.                Mheshimiwa Spika,  katika kuwawezesha wanawake kiuchumi,  Wizara yangu iliendelea kuratibu na kusimamia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF). Katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2017, Halmashauri 130 kati ya 185 zilichangia Shilingi bilioni 7.3 katika Mfuko ikilinganishwa na Shilingi bilioni 8.9 zilizochangiwa na Halmashauri kwa mwaka 2016/17. Fedha zilizochangiwa ni sawa na asilimia 26 ya Shilingi bilioni 28.3 zilizopaswa kuchangiwa kwa mwaka 2017/18. Fedha hizo zilitolewa kama mikopo kwa vikundi 4,365 vyenye wanawake wajasiriamali 39,449.

90.                Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo SIDO, Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote(EOTF) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliendelea kuwezesha ushiriki wa wanawake katika Maonesho ya Biashara ya Kitaifa na Kimataifa. Katika mwaka 2017/18, wanawake wajasiriamali 1,183 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara waliwezeshwa kushiriki katika Maonesho ya Sabasaba, Juakali, Nanenane na VICOBA.

91.                Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, wajasiriamali 6,237 (Ke 5,097 na Me 1,140) walipatiwa mikopo na Benki ya Wanawake Tanzania ikilinganishwa na wajasiriamali 6,267 (Ke 4,596 na Me 1,671) mwaka 2016/17. Juhudi hizi zimewesha wajasiriamali 87,063 (Ke 71,744 na Me 15,319) kupata mikopo tangu mwaka 2010. Kwa upande wa thamani ya mikopo iliyotolewa mwaka 2017/18, benki ilitoa mikopo ya Shilingi bilioni 10.1 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 13.3 mwaka 2016. Tthamani ya mikopo iliyotolewa tangu mwaka 2010 mpaka Machi, 2018 ni Shilingi bilioni 131.9.

92.                Mheshimiwa Spika, Benki ya Wanawake Tanzania imefungua vituo 244 vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wanawake wajasiriamali katika mikoa ya Dar es Salaam (115), Mwanza (46), Dodoma (27), Mbeya (5), Iringa (9), Ruvuma (24) na Njombe (18) katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na vituo 88 mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 177.

93.                Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/18, jumla ya akaunti 10,415 (Ke 7,811 na Me 2,604) zilifunguliwa hadi kufikia akaunti 88,397 Machi, 2018 katika matawi mawili ya Benki ya Wanawake Tanzania (tawi la Mkwepu na Mjasiriamali) kutoka mwaka 2009. Kati ya akaunti hizo, akaunti 65,419 ni za wateja wanawake sawa na asilimia 74, akaunti 20,961 za wanaume na akaunti 2,017 za makampuni.

   Maendeleo ya Jamiii

94.                Mheshimiwa Spika, Wizara, inaendelea kuamsha ari ya Wananchi kushiriki katika Miradi ya Maendeleo. Katika kipindi cha Julai hadi Machi 2018, Wizara imefanya uhamasishaji katika Mikoa 11 ya Iringa, Dodoma, Mwanza, Pwani, Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Kagera na Shinyanga. Uhamasishaji huu umewezesha ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Mondo, Wilaya ya Misungwi (Mwanza); ujenzi wa bwawa la maji Maghangu Mpwapwa (Dodoma); ujenzi wa Zahanati Ufyambe (Iringa); ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Uvinza (Kigoma); ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Mpanda (Katavi); ujenzi wa kituo cha afya –  Sumbawanga (Rukwa); ujenzi wa kituo cha afya – Mbozi (Songwe); ujenzi wa shule ya sekondari – Manispaa ya Mbeya (Mbeya); kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa Makazi ya wazee (Kagera); kuzindua Kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) cha wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto Wilaya ya Kahama (Shinyanga) na ujenzi wa madarasa mawili katika Kijiji cha Chambasi, Kisarawe (Pwani).

95.                Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu uzalishaji wa wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutoka katika vyuo 8 vya maendeleo ya jamii vya Buhare, Mlale, Misungwi, Rungemba, Mabughai, Ruaha, Uyole na Monduli. Vyuo hivyo hutoa mafunzo ya Maendeleo ya jamii katika ngazi ya Cheti na Stashahada. Katika mwaka 2017/18, jumla ya wanafunzi 1,588 (Ke 984 na Me 604) walidahiliwa ikilinganishwa na 3,248 (Ke 1,987 na Me 1,261) mwaka 2016/17. Aidha, katika mwaka 2017/18, jumla ya wanafunzi 3,320 (Ke 1,947 na Me 1,373) walihitimu katika Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii ikilinganishwa na wahitimu 3,694 (Ke 2,228 na Me 1,466) mwaka, 2016/17.

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                    

96.                Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa. Kwa kipindi cha Julai hadi Machi, 2018, jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 192 yalisajiliwa. Kati ya mashirika yaliyosajiliwa, mashirika 21 yalisajiliwa katika ngazi ya Kimataifa,162 katika ngazi ya Kitaifa na Mashirika 9 ngazi ya Wilaya. Usajili huu umewezesha jumla ya mashirika 8,211 kusajiliwa nchini kuanzia mwaka 2005 hadi Machi, 2018 (Kiambatisho Na.5).

97.                Mheshimiwa Spika, Wizara ilihakiki mashirika na hadi kufikia Machi, 2018, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 4,868 yalikuwa yamehakikiwa. Aidha, katika uhakiki huo, wizara imebaini jumla ya mashirika 513 yenye sifa za mashirika ambayo yaliyokuwa yamesajiliwa chini ya Sheria nyingine na kuyajumuisha chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002. Hatua hii imesaidia kuimarisha uratibu na usimamizi mzuri wa mashirika haya katika misingi ya uwazi, utoaji taarifa na uwajibikaji kwa jamii.

Haki na Maendeleo ya Mtoto

98.                Mheshimiwa Spika, ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2017, matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalikuwa 13,457 ikilinganishwa na matukio 10,551 mwaka 2016. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22). Katika mwaka 2017/18, Kazi zilizofanyika chini ya mpango huu ni kutoa elimu kuhusu athari za mila na desturi zenye madhara kwa jamii ikiwemo ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kwa makundi mbalimbali katika jamii. Jumla ya wananchi 13,020 walipatiwa elimu wakiwemo wanafunzi 8,546, walimu 476, wazee wa mila 56, viongozi wa dini 64, ngariba 38, waendesha bodaboda 168, wazazi/walezi 3,600 na watendaji 72 kutoka mikoa ya Shinyanga, Mara, Tabora, Lindi, Dodoma, Tanga, Dar es Salaam na Katavi.

99.                Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuwapatia huduma watoto waliofanyiwa ukatili kupitia Huduma ya Simu kwa Watoto (Child Help Line). Katika mwaka 2017/18, simu 18,464 zilipokelewa kuhusu ukatili dhidi ya watoto. Kati ya simu hizo, simu za watoto 1,072 (Ke 621 na Me 451) ziliwezeshwa kupata huduma (chakula, vifaa vya shule na huduma za sheria na afya) ikilinganishwa na simu za watoto 441 (Ke 325 na Me 96) waliopata huduma mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 143.

100.             Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha watoto wanashiriki katika maendeleo yao na kujitambua, kwa mwaka 2017/18 Wizara imeendelea kuwezesha ushiriki wa watoto katika mabaraza na klabu za wasichana za Kujikinga na mimba za utotoni. Jumla ya mabaraza ya watoto 13 na klabu 600 katika shule za msingi na sekondari zimeanzishwa kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018 na kufikia idadi ya mabaraza 1,669 na Klabu 2,000.

Huduma ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Watoto

101.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia utoaji wa huduma ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto walio chini ya miaka mitano walio katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Day Care Centres) vya Serikali na Binafsi.  Kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, vituo 139 vilipatiwa usajili ikilinganishwa na vituo 270 vilivyopatiwa usajili mwaka 2016/17 na hivyo kufikia vituo 1,046 vilivyosajiliwa nchi nzima. Aidha, watoto 6,075 (Ke 4,018 na Me 2,057) waliandikishwa katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 2016/17 ikilinganishwa na watoto 4,450 (Ke 3,097, Me 1,353) mwaka 2015/16.

102.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuzalisha wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara. Jumla ya wanafunzi 83 (Ke 58 na Me 25) walidahiliwa kwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wanafunzi 56 (Ke 39 na Me 17) waliodahiliwa mwaka 2016/17. Aidha, wanafunzi 52 (Ke 35 na Me 17) wahitimu katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wahitimu 8 wote wanawake mwaka 2016/17.

103.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuzalisha wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara. Jumla ya wanafunzi 83 (Ke 58 na Me 25) walidahiliwa kwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wanafunzi 56 (Ke 39 na Me 17) waliodahiliwa mwaka 2016/17. Aidha, wanafunzi 52 (Ke 35 na Me 17) wahitimu katika mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wahitimu 8 wote wanawake mwaka 2016/17.

Huduma za Ustawi kwa Watoto

104.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na Asasi Zisizo za Kiserikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msingi za malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi nchini. Jumla ya watoto 6,132 (Ke 2,972 na Me 3,160) walio katika mazingira hatarishi walipatiwa huduma za msingi katika makao ya watoto 157 yanayoendeshwa na Taasisi za dini, Mashirika ya watu binafsi na Serikali ikilinganishwa na watoto 4,515 (Ke 2519 na Me 1,996) mwaka 2016/17. Kati ya watoto hao, watoto 78 (Ke 43 na Me 35) wanaishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini ambayo yanamilikiwa na Serikali.

105.             Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, jumla ya leseni 14 za usajili wa Makao ya watoto zimetolewa ikilinganishwa na leseni 50 kwa mwaka 2016/17 na kufikia idadi ya makao 157 nchi nzima. Kati ya makao hayo, moja ni la Serikali na 156 yanamilikiwa na kuendeshwa na watu binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya kijamii au Taasisi za kidini. Nitumie fursa hii kuwataka watu/Taasisi zote zinazotoa huduma za malezi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kujisajili katika Halmashauri zao mara moja.

106.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa watoto walio katika mkinzano na Sheria wanapata haki za msingi ikiwa ni pamoja na huduma za sheria na elimu katika mahabusu tano za watoto za Mbeya, Moshi, Tanga, Arusha na Dar es Salaam. Katika mwaka 2017/18, jumla ya watoto 291 (Ke 13 na Me 278) walio katika mkinzano na sheria waliwezeshwa kupata huduma za msingi (chakula, malazi, mavazi, huduma za matibabu na elimu) ikiwa ni pamoja na huduma za msaada wa kisheria ikilinganishwa na watoto 255 (Ke 18 na Me 237) mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 14.

107.             Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria imewachepusha watoto 126 (Ke 24 na Me 102) kutoka katika mfumo rasmi wa haki jinai kwa kuwarekebisha tabia na kuwaunganisha na familia zao ikilinganishwa na watoto 72 (Ke 8 na Me 64) waliochepushwa mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 67. Aidha, katika mwaka 2017/18, Wizara imeendelea kuwezesha huduma za msingi (chakula, malazi, mavazi na huduma za matibabu) ikiwa ni pamoja na marekebisho ya tabia, elimu na mafunzo kwa watoto wa kiume 35 waliobainika na makosa ya jinai waliopo katika Shule ya Maadilisho Irambo Mbeya ikilinganishwa na watoto 72 mwaka 2016/17.

108.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kwa kushirikiana na OR - TAMISEMI imeendelea na juhudi ya kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika ngazi ya familia kulingana na Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009 kwa kutoa huduma za malezi ya kambo na uasili. Wizara imewezesha watoto 44 (Ke 24 na Me 20) kuwekwa chini ya malezi ya kambo ikilinganishwa na watoto 54 (Ke 21 na Me 33) mwaka 2016/17. Aidha, watoto 17 (Me 8 na Ke 9) waliasiliwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na watoto 21 (Ke 11 na Me 10) mwaka 2016/17.

109.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwatambua Watu wa Kuaminika (Fit Persons) ili kulea watoto walio katika mazingira hatarishi. Juhudi hii imewezesha Watu wa Kuaminika 187 kutambuliwa katika Halmashauri 19 mwaka 2017/18. Hadi kufikia Machi, 2018, jumla ya watoto 243 wamepitia kwenye familia za watu wa kuaminika katika Halmashauri 19 za Magu DC, Kasulu DC, Kasulu TC, Musoma Dc, Iringa MC, Iringa DC, Mufindi DC,  Njombe DC, Makete DC, Mbeya Jiji, Mbeya DC, Mbarali DC, Hai DC, Temeke DC, Arusha DC, Kakonko DC, Kibondo DC, Misenyi DC na Chunya DC.

Huduma za Ustawi kwa Wazee

110.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu upatikanaji wa huduma za msingi kwa wazee wasiojiweza. Katika mwaka 2017/18,  jumla ya wazee wasiojiweza 517 (Ke 250 na Me 267) wanaoishi katika makazi 17 ya Serikali walipatiwa huduma za msingi - chakula, malazi, mavazi na matibab ikilinganishwa na wazee 465 (Ke 221 na Me 244) mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la asilimia 11.

111.             Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana OR - TAMISEMI iliwezesha wazee 506,943 (Ke 220,312 na Me 286,631) kupata vitambulisho vya matibabu bure katika kipindi cha Julai hadi Machi, 2018 ikilinganishwa na wazee 74,590 waliopata vitambulisho vya matibabu bure mwaka 2016/17. Juhudi hizi zimewezesha kufikia idadi ya wazee 581,533 (Ke 254,793 na Me 326,740) waliopata vitambulisho ikiwa ni asilimia 35 ya wazee 1,657,206 waliotambuliwa katika Halmashauri zote.

Huduma za Usuluhisho wa Migogoro ya Ndoa na mashauri ya matunzo kwa watoto

112.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa lililopo chini ya usimamizi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii na Ofisi za Ustawi wa Jamii za Halmashauri zimeendelea kutoa huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa kwa familia. Kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2018, jumla ya mashauri ya migogoro ya ndoa 13,382 yalipokelewa na kufanyiwa usuluhishi ikilinganishwa na mashauri ya migogoro ya ndoa 8,454 mwaka 2016/17. Kati ya mashauri hayo, mashauri 11,326 sawa na asilimia 85 yamesuluhishwa na yamekamilika, mashauri 1,397 sawa na asilimia 10 yamepelekwa mahakamani na mashauri 659 sawa na asilimia 5 yanaendelea na usuluhishi.

113.             Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa, watoto wanapata matunzo kutoka kwa wazazi, Wizara imeendelea kufanyia kazi mashauri ya matunzo ya watoto nchini.  Kwa kipindi cha mwezi Julai, 2017 hadi Machi, 2018 jumla ya mashauri ya matunzo ya watoto 11,815 yalipokelewa. Kati ya mashauri hayo, 4,965 yalihusu matunzo ya watoto walio ndani ya migogoro ya ndoa na 5,708 watoto waliozaliwa nje ya ndoa  Kati ya mashauri yaliyopokelewa, 10,673 yalikamilika kuwezesha huduma kwa watoto na mashauri 1,142 yaliyopewa rufaa kwenda mahakamani ikilinganishwa mashauri ya matunzo ya watoto 12,406 yaliyokamilika mwaka 2016/17 (matunzo ya watoto walio kwenye migogoro ya ndoa 6,557, matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa 4,133 na mashauri 1,716 yaliyopewa rufaa kwenda  mahakamani).

UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI CHINI YA IDARA KUU YA MAENDELEO YA JAMII

 Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru

114.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ilidahili jumla ya wanafunzi 1,169 katika fani ya Maendeleo ya Jamii ikiwa ni ongezeko la asilimia 86 ya udahili wa wanafunzi 628 mwaka 2016/17. Kati ya wanafunzi waliodahiliwa, wanafunzi 486 walidahiliwa katika ngazi ya cheti, wanafunzi 83 Stashahada na wanafunzi 600 ngazi ya Shahada. Aidha, wanafunzi 684 walihitimu mwaka 2017/18 ikilinganishwa na wahitimu 609 mwaka 2016/17 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.

115.             Mheshimiwa Spika, Taasisi pia imefanya tafiti tatu ambazo ni Tathmini ya mahitaji ya Ushiriki wa Jamii katika kijiji cha Kikwe wilaya ya Arumeru, tafiti kuhusu watoto walio katika mazingira hatarishi katika sekta isiyo rasmi katika Wilaya ya Arumeru (utafiti kuhusu watoto katika masoko ya jamii) na Tathmini ya changamoto inayowakabili Maafisa Maendeleo ya Jamii Tanzania katika Halmashauri.  Matokeo ya tafiti hizi yatawezesha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Wizara kuboresha utoaji wa mafunzo na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jamii.

 Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kijitonyama

116.             Mheshimiwa Spika, Taasisi ya Ustawi wa Jamii - Kijitonyama imeendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili. Katika mwaka 2017/18, Taasisi ilidahili wanafunzi 1,185 (Ke 811 na Me 374) katika fani zitolewazo katika ngazi mbalimbali ikiwa upungufu wa asilimia 6.91 ya wanafunzi 1,273 waliodahiliwa mwaka 2016/17. Aidha, wanafunzi 1,122 (Ke 722 na Me 400) walihitimu mwaka 2016/17 katika fani na ngazi mbalimbali ikilinganishwa na wanafunzi 1,172 (Ke 789, Me 383) waliohitimu mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 4.

C: VIPAUMBELE VYA WIZARA KWA MWAKA 2018/19

117.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara kupitia fungu 52 (Idara kuu ya Afya) imejiwekea vipaumbele vifuatavyo ili kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini;
i)             Kuimarisha huduma za chanjo kwa watoto ili kuendelea kubaki katika viwango vya juu vya utoaji wa huduma za chanjo ili kuwaepusha watoto na magonjwa yanayoweze kuepukika kwa chanjo.
ii)           Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa yanayotokana na kutozingatia kanuni za usafi na usafi wa mazingira kama magonjwa ya kuhara, kuhara damu na kipindupindu kwa kuongeza uhamasishaji na usimamizi wa usafi na usafi wa mazingira
iii)          Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari na saratani kwa kuhamasisha jamii kuepukana na tabia hatarishi na kujijengea tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa ili kujiepusha na hatari ya kupata magonjwa hayo.
iv)         Kuimarisha huduma za afya ya uzazi na mtoto nchini ili kupunguza idadi ya vifo vya wanawake na watoto vinavyotokana na Uzazi kwa kukarabati na kujenga Wodi Maalum kwa ajili ya Watoto wachanga (Neonatal Care Units) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 na Wodi za Wazazi na kujenga vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) wanaotokana na uzazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa (5) mitano yenye viwango vikubwa vya vifo vitokanavyo na uzazi.
v)           Kupunguza maambukizi ya Malaria, TB na VVU/UKIMWI;
vi)         Kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kukusanyia Damu Salama (Satellite Blood Banks)
vii)        Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za za afya nckiahini
viii)        Kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa nchini katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maaluma na za Kitaifa ili kusogeza huduma hizi karibu zaidi na wananchi na kupunguza rufaa za nje ya nchi zisizo na ulazima
ix)         Kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na Serikali
x)           Kuboresha vyuo vya mafunzo ya afya ili kuendelea kuzalisha wataalam wenye ubora kwa kufanya upanuzi na ujenzi wa majengo na ukarabati kwenye Vyuo vya Mafunzo ya Afya vya Uuguzi vya Nachingwea, Kibondo, Kagemu, Kondoa, Same na Kiomboi; Vyuo vya Mafunzo ya Maafisa Afya vya Bombo Tanga, Mpwapwa na Ngudu Mwanza; vyuo vya Maafisa Tabibu vya Kibaha, Tanga na katika Chuo cha Maabara cha Singida
xi)         Kuimarisha Mifumo ya Habari, Takwimu na Teknolojia ili kurahisisha upatikanaji wa Takwimu katika sekta ya Afya.
xii)        Kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa huduma za afya nchini kwa kuongeza wigo wa huduma za bima ya afya kwa wananchi ili kufikia malengo ya kuwa na bima kwa wananchi wote na kufikia lengo la afya kwa wote (Universal Health Coverage – UHC)

118.             Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Fungu 52 kwa mwaka 2018/19, kazi zitakazotekelezwa zimeainishwa kwenye aya ya 199 mpaka 205 vya hotuba ya bajeti. Hata hivyo ningependa kutaja kazi muhimu na za kipaumbele zifuatazo:-
     i.        Kununua na kusambaza chanjo za watoto na chanjo ya kwa wasichana wenye miaka kati ya 9 – 14 ambapo jumla ya shilingi bilioni 30 zimetengwa.
     i.        Kuongeza wigo na kasi ya uibuaji na tiba kwa wagonjwa wa kifua kikuu katika mikoa yote nchini, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 5 kimetengwa
    ii.        Kukarabati na kujenga Wodi Maalum kwa ajili ya Watoto wachanga (Neonatal Care Units) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 ya Dar es Salaam, Katavi, Geita, Rukwa, Kilimanjaro, Iringa na Kigoma ambapo shilingi milioni 900 zimetengwa.
  iii.        Kupanua Wodi za Wazazi na kutenga vyumba vya wagonjwa mahututi wanaotokana na uzazi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa (5) ya Mbeya, Shinyanga, Morogoro, Pwani na Kigoma  mitano ya ambapo, shilingi bilioni 1 zimetengwa.
  iv.        Kuimarisha upatikanaji wa huduma ya damu salama kwa kujenga vituo vya kukusanyia Damu Salama (Satellite Blood Banks) katika mikoa 12 ya Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Njombe, Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu ambapo kiasi cha shilingi bilioni 4.3 kimetengwa
   v.        Kununua dawa za malaria kwa ajili ya kinamama wajawazito (Sulphadoxine +pyrimethamine), dawa za kuokoa maisha ya mama wajawazito ambapo shilingi bilioni 8.5 zimetengwa.
  vi.        Kununua na kusambaza vitanda, magodoro, mashuka na vitanda vya kuzalia mama wajawazito ambapo kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kimetengwa
vii.        Kuimarisha hali ya upatikanaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi nchini kwa kununua na kuvisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya. Jumla ya shilingi bilioni 270 zimetengwa.
viii.        Kuendelea na huduma za kupandikiza figo (renal transplant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjami Mkapa
ix.        Kuendelea kutoa huduma za upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa kuweka cochlear implants katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
x.        Kununua na kusimika vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ya Saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.5 zimetengwa.
xi.        Kuendelea na ujenzi wa jengo na kusimikia vifaa vya uchunguzi (X-Ray Building), pamoja na kununua vifaa vya tiba ya mionzi, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5 zimetengwa.
xii.        Wizara imepanga kununua na kusambaza Ambulances 27 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa rufaa Nchini
xiii.        Kufanya ukarabati katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 20 zimetengwa
xiv.        Kuendelea na ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa ambayo haina hospitali hizo katika mikoa ya Simiyu, Geita, Katavi, Songwe Mara, Njombe ambapo shilingi bilioni 10 zimetengwa
xv.        Kufanya ukarabati na upanuzi wa vyuo afya ambapo jumla ya shilingi bilioni 8 zimetengwa

119.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/19, Wizara kupitia fungu 53 (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii) imejiwekea vipaumbele vifuatavyo ili kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini;
(i)            Kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi;
(ii)           Kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na watoto;
(iii)          Kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22 ili kupunguza ukatili dhidi yao kwa asilimia 50;
(iv)           Kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Taasisi ya Ustawi wa Jamii – Kijitonyama;
(v)           Kuboresha majengo na miundombinu katika makazi ya wazee, Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini, mahabusu za watoto na Shule ya Maadilisho
(vi)          Kuweka mazingira wezeshi ili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa; na
(vii)         Kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

120.             Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Fungu 53 kwa mwaka 2018/19, kazi zitakazotekelezwa zimeainishwa kwenye aya ya 206 mpaka 213 vya hotuba ya bajeti. Hata hivyo ningependa kutaja kazi muhimu zitakazotekelezwa kwa muhtasari ambazo ni:

(i)        Kukuza usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake ambapo shilingi milioni 413  zimetengwa;
(ii)       Kukarabati majengo katika vyuo vya maendeleo ya jamii vya Uyole, Mlale na Misungwi ambapo kiasi cha shilingi milioni 550 kimetengwa;
(iii)      Kukarabati makazi ya wazee Bukumbi, Mwanzage na Mizufini ambapo shilingi milioni 450 zimetengwa;
(iv)      Kukamilisha ujenzi wa mahabusu ya watoto Mtwara ambapo kiasi cha shilingi milioni 500 kimetengwa;
(v)        Kuimarisha ulinzi wa mtoto  ambapo shilingi bilioni 1.8 zimetengwa; na
(vi)      Kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma za msingi kwa wazee wasiojiweza na watoto walio katika mazingira hatarishi na watoto walio katika mkinzano na sheria ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1 kimetengwa.

   D: SHUKRANI

121.             Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii ya kipekee kuzishukuru nchi wahisani za Denmark, Canada, Ireland, Uswisi na Korea ya Kusini pamoja na Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya UNICEF na Benki ya Dunia kwa kutoa misaada katika Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Afya ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya nchini. Pia shukrani ziende kwa WHO, GAVI na Global Fund kwa mchango wao katika kutekeleza mikakati ya Sekta ya afya. Aidha, napenda kuzishukuru nchi za China, Cuba, Hispania, India, Italia, Japan, Marekani, Misri, Sweden, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na ambazo zimeendelea kuisaidia Sekta ya Afya kwa njia mbalimbali.

122.             Mheshimiwa Spika, vilevile nayashukuru mashirika mengine ya Kimataifa kwa ushirikiano wao waliotoa kwa Wizara pamoja na Wadau wa Maendeleo ambao kwa pamoja wamewezesha wizara yangu kutekeleza mikakati ya kisekta na hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini Wadau wote hawa wameainishwa kwenye Hotuba yangu kuanzia aya ya 214 mpaka ya 216.

123.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha utendaji wangu wa kazi nikiwa Waziri, nimepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mb.), Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, naomba kuwashukuru Dkt. Mpoki M. Ulisubisya Katibu Mkuu (Afya) na Bibi Sihaba Nkinga Katibu Mkuu (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) kwa mchango wao katika kuwezesha utekelezaji wa majukumu yangu. Vilevile, nawashukuru Prof. Muhammad Bakari Kambi, Mganga Mkuu wa Serikali, Makamishna, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Wizara. Nawashukuru pia, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili ( MOI) Dr. Respicious Boniface Rwezimula; Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi; Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI); Dr. Julius Mwaiselage; na Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Dkt. Alphonce Chandika; Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Kibong’oto Dkt. Riziki Kisonga, Mkurugenzi wa Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Erasmus Mndeme, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji; Mkurugenzi wa Hopsitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt Abel Makubi; Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC Dkt Gilead Masenga.  Aidha, nichukue fursa hii pia kuzishukuru  Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na  Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga Wafawidhi wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo vilivyo chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara na Mashirika ya Dini (FBOs), ya kujitolea na Binafsi. Natoa shukrani kwa sekta zote ambazo tunashirikiana nazo katika kutoa huduma za afya, maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii pamoja na wananchi wote kwa ushirikiano wao. Nawaasa waendelee kuzingatia misingi ya huduma bora na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa letu.

124.             Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuishukuru familia yangu, kwa upendo na uvumilivu na kunitia moyo katika kutekeleza majukumu yangu ya Kitaifa. Aidha, Napenda kuwashukuru  wananchi wote wa Mkoa wa Tanga  kwa ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kuendeleza Mkoa wetu. Naahidi kuwa nitaendelea  kuwatumikia kwa akili na nguvu zangu zote ili kuleta Maendeleo katika Mkoa wetu.



E: MAOMBI YA FEDHA KWA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2018/19

   Fungu 52 - Afya

  Mapato

125.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara imekadiria kukusanya mapato ya Shilingi bilioni mia mbili arobaini, milioni arobaini na mbili, mia tano na nane elfu, mia moja hamsini na saba (240,042,508,157.00) Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia mbili ishirini, milioni mia mbili sitini na saba, elfu kumi na hamsini na saba (220,267,010,057.00) zitakusanywa katika mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara na Shilingi bilioni kumi na tisa, milioni mia saba sabini na tano, mia nne tisini na nane elfu, mia moja  (19,775,498,100.00) ni kutoka makao makuu.

Matumizi ya Kawaida

126.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi bilioni mia tatu nne, milioni mia nne sabini na tatu, mia nne sabini na sita elfu (304,473,476,000.00) kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni themanini na nane, milioni mia nne sitini na tano, mia saba hamsini na sita elfu (88,465,756,000.00) zitatumika kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni mia mbili kumi na sita, milioni saba, mia saba ishirini elfu (216,007,720,000.00) zitatumika kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi.

Miradi ya Maendeleo

127.             Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi bilioni mia tano sitini na moja, milioni mia saba hamsini na tisa, mia tisa tisini na tisa elfu (561,759,999,000) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya hizo, fedha za ndani ni Shilingi bilioni mia moja themanini na nne, milioni mia tisa hamsini na tisa, mia tisa tisini na tisa elfu (184,959,999,000) na fedha za nje ni Shilingi bilioni mia tatu sabini na sita, milioni mia nane (376,800,000,000.00.) Jumla ya Makadirio ya Bajeti kwa 2018/19 kwa Fungu 52 ni Shilingi bilioni mia nane themanini na sita, milioni mia mbili thelathini na tatu, mia nne sabini na tano elfu (866,233,475,000.00).

Fungu 53 – Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mapato

128.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara imekadiria kukusanya Shilingi bilioni tatu, milioni tisini, mia saba tisini na sita elfu (3,090,796,000) kutokana na ada za wanafunzi kutoka Vyuo 8 vya Maendeleo ya Jamii na Chuo cha Ustawi wa Jamii Kisangara, ada ya usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na mauzo ya vitabu vya zabuni.

Matumizi Kwa mwaka 2018/19

129.             Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/19 inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni thelathini na mbili, milioni mia moja arobaini, mia sita arobaini na tisa elfu (32,140,649,000). Kati ya makadirio hayo, Matumizi ya Kawaida ni Shilingi bilioni ishirini na saba, milioni mia mbili ishirini na sita, mia nane na nne elfu (27,226,804,000) na Miradi ya Maendeleo ni Shilingi bilioni nne, milioni mia tisa kumi na tatu, mia nane arobaini na tano elfu  (4,913,845,000).

Matumizi ya Kawaida

130.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi bilioni ishirini na saba, milioni mia mbili ishirini na sita, mia nane na nne elfu (27,226,804,000) kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni kumi na tano, milioni mia moja kumi na sita, mia tisa sitini na mbili elfu (15,116,962,000) ni Mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni kumi na mbili, milioni mia moja na tisa, mia nane arobaini na mbili elfu (12,109,842,000) ni Matumizi Mengineyo.

Miradi ya Maendeleo

131.             Mheshimiwa Spika, kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi bilioni nne, milioni mia tisa kumi na tatu, mia nane arobaini na tano elfu (4,913,845,000) kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni moja, milioni mia tano (1,500,000,000) ni fedha za ndani na Shilingi bilioni tatu, milioni mia nne na kumi na tatu, mia nane arobaini na tano elfu (3,413,845,000) ni fedha za nje.

132.             Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha inayoombwa kwa mwaka 2018/19, kwa Fungu 53 ni Shilingi bilioni thelathini na mbili, milioni mia moja arobaini, mia sita arobaini na tisa elfu (32,140,649,000).

133.             Mheshimiwa Spika, Jumla kuu ya fedha inayoombwa kwa mwaka 2018/19, Shilingi bilioni mia nane tisini na nane, milioni mia tatu sabini na nne, mia moja ishirini na nne elfu (898,374,124,000).

134.             Mheshimiwa Spika, Hotuba kamili inapatikana katika tovuti za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto www.moh.go.tz. na www.mcdgc.go.tz.

135.                       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

0 on: "HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII MHE. UMMY MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019"