Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 22 Agosti 2018

TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akionesha bango lenye ujumbe kuhusu Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akijibu maswali ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati waTamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Waandishi wa Habari waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akitoa Tamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.


TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Ndugu Wanahabari, 
Manamo tarehe 10/08/2018 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) uliotangazwa na shirika la Afya Duniani mnamo tarehe 1/08/2018. Katika taarifa hiyo ilielezwa kwamba jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 (CFR = 38.5%) vilitokea katika Nchi ya DRC. 
 
Hata hivyo tangu tulivyotoa tamko hadi tarehe 18/08/2018, hali ya ugonjwa imeendelea kwa kasi sana na kufikia wagonjwa 91 na vifo 50 (CFR = 54.9%). Aidha wagonjwa hawa wanatokea maeneo matano ya afya (Health zones) katika jimbo la Kivu Kaskazini na eneo jingine moja la Ituri. Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola kutokea nchini DRC, na umetokea wiki moja tu baada ya nchi hiyo kutangaza kumalizika kwa mlipuko mwingine uliotokea mwezi Mei 2018.

Ndugu Wanahabari
Sambamba na takwimu za hizi zilizotolewa na WHO, Wafanyakazi tisa (9) wa Afya wamethibitishwa kuugua ugonjwa huu, huku ikifanya jumla yao kufikia 10 (9 wamethibitika na 1 anafuatiliwa); na hadi sasa mfanyakazi mmoja amepoteza maisha. Wafanyakazi hawa wa Afya inaaminika kwamba wamepata ugonjwa huu wakati wakiwahudumia wagonjwa katika Kliniki zao za kawaida na sio zile za kutibia wagonjwa wa Ebola (Ebola Treatment Centres (ETCs), na wengi wao wameambukizwa kabla ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutangaza mlipuko huu. 

Ndugu Wanahabari
Tumeona ipo haja ya kuongea nanyi leo kutokana na ukweli kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limefanya tena tathmini ya hatari ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola nchini DRC na katika nchi zinazopakana  na DRC na kubaini kuwa hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huu kwa nchi zilizo jirani na DRC, ikiwemo Tanzania, imeongezeka maradufu na ni “kubwa” (yaani High risk) kutokana na kwamba; eneo lililoathirika la Kivu Kaskazini linapakana na nchi jirani ya Uganda, uwepo wa uhusiano wa wasafiri na wakimbizi wa DRC wanaoingia nchi jiarani za Uganda na Rwanda, na pia machafuko ya kijamii ambayo yameendelea kuchukua muda mrefukwenye  majimbo ya Kivu kaskazini na Ituri na hivyo kutatiza kwa kiwango kikubwa makabiliano dhidi ya ugonjwa huu. 
 
Aidha, eneo hili la sasa ni la karibu na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na ukaribu na mwingiliano  wa watu, hasa wasafiri wanaotoka na kuingia DRC kuja hapa nchini. 

Ndugu Wanahabari
HADI SASA HAKUNA MGONJWA YEYOTE ALIYEHISIWA AU KUTHIBITISHWA KUWA NA VIRUSI VYA EBOLA HAPA NCHINI. Hata hivyo kutokana na ukweli kwamba  kuna mwingiliano mkubwa wa wananchi kati ya nchi hizi mbili na ugonjwa huu kugunduliwa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini ambalo linapakana na nchi ya Uganda ni ukweli unaotuweka kwenye hali ya wasiwasi mkubwa. 
 
Hivyo tunasistiza kwamba wanajamii wote ikiwemo wafanyakazi wa sekta ya Afya kuelewa vyema dalili za ugonjwa huu pamoja na kuongeza nguvu katika kufuata kanuni za kuzuia maambukizi katika vituo vya Afya yaani Infection Prevention and Control (IPC) measures. 
 
Wizara inapenda kutoa tahadhari kubwa ya ugonjwa huu kwa Wananchi wote, na katika mikoa yote hasa ile inayopakana na nchi jirani ya DRC ambayo ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha, hii haiondoi ukweli kwamba, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA) cha Dar es Salaam, Kilimajaro (KIA) na Songwe cha Mbeya kuwa vipo katika hatari ya kuweza kuingiza mgonjwa wakati wowote ule. 
 
Kutokana na hali hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Washirika mbali mbali, ikiwemo WHO, wanafanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaopita katika mipaka yetu yote ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa huu hapa nchini.  

Ndugu Wanahabari
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola na mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Ebola hutokea pale binadamu anapogusana na mnyama aliyeathirika na ugonjwa huu kama vile Nyani, Sokwe au Popo. Aidha ugonjwa huu huenezwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa binadamu mwingine kwa njia zifuatazo;
Kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa Virusi vya Ebola
Kugusa vitu vya mgonjwa wa Ebola, kama vile nguo, shuka au godoro
Kugusa au kutumia vifaa vilivotumika kwa mgonjwa wa Homa ya Ebola kama sindano
Kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa Ebola
Kugusa wanyama (mizoga au wanyama hai) walioambukizwa kama vile sokwe na nyani wa msituni
Kukutana kimwili na binadamu mwenye maambukizi ya virusi vya Ebola.

Aidha tunasisitiza kwamba ugonjwa wa Homa ya Ebola hauenezwi kwa njia ya hewa, maji au chakula.
Dalili za Ugonjwa
Dalili za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa kutoka siku 2 hadi 21 tangu kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Dalili hizo ni pamoja na;
Homa kali ya ghafla, 
Kulegea kwa mwili,
Maumivu ya misuli, 
Kuumwa kichwa na vidonda kooni. 
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi. 
Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu nyingi ndani na nje ya mwili. 


Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola:
Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:-
Epuka kugusa damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa  wa Ebola
Epuka kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki kwa dalili za ugonjwa wa Ebola; Aidha unatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za Afya kwa ushauri.
Epuka mila na desturi zinazoweza kuchelewesha mgonjwa kupatiwa huduma muhimu za Afya na kupelekea kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kuzingatia  kanuni za Afya na usafi wa mwili
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na kwa wahudumu wa Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.

Ndugu Wanahabari
Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha uwezo wetu wa utayari katika kukabiliana na ugonjwa huu kwa kuzuia usiingie, na hatua za kuchkua iwapo utaingia hapa nchini. 
Hadi sasa Wizara imefanya yafuatayo; 

Kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Ebola hapa nchini (Operational readiness assessment). Tayari tathmini hiyo imefanyika kwa kushirikiana na WHO kwenye mikoa minane ambayo ni Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya, Kigoma, Kagera, Arusha na Kilimanjaro na kuanisha uwezo uliopo na mapungufu ambayo yanafanyiwa kazi. 
Aidha, WAMJW imeajiri wataalamu wapya 33 ili kuongeza nguvu katika mipaka yetu na tayari wamesambazwa kwenye vituo vya mipakani.  
Tunaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (Travellers entry screening) kwa kutumia vifaa vya kupima joto (thermo scaners) na fomu maalum za wasafiri wanaoingia nchini, ambapo tayari kupitia MSD imepokea vifaa vyenye thamani ya Bilioni 5 kutoka WHO na vimeshapelekwa  kwenye maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa kinga kwa watumishi wa afya (Personal Protective Equipment, PPE’s) kwenye maeneo yote nchini.  
WAMJW kwa kushirikiana na Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani (Centres for Diseases Control, CDC) na Water Reed imenunua “kits” nne za kupima Ebola zenye uwezo wa kupima wagonjwa zaidi ya 400 na hivyo kuiwezesha Maabara ya Taifa na hile ya kanda ya Mbeya kuwa na uwezo mzuri. 
Hadi sasa WAMJW ina uwezo wa kupima ugonjwa huu Nchini kwa kutumia maabara ya Taifa Dar es Salaam, Hospitali ya kanda ya MBEYA na KCRI katika Hospitali ya KCMC, Kilimanjaro
Mafunzo ya usimamizi wa sampuli yamefanyika kwa Mikoa ya Mwanza, Arusha, Ruvuma, Kilimanjaro, Kigoma na Kagera kwa wiki iliyopita na kupatiwa jumla ya Triple packaging materials 18.
Uelimishaji wa umma unaendelea kufanyika kupitia matamko pamoja na matumizi ya vyombo vya habari ikiwemo vile vya kitaifa, vya binafsi, mitandao ya kijamii, vipeperushi na mabango. 
WAMJW tayari imeshatoa tahadhari kwa wadau na sekta muhimu wakiwemo TAMISEMI pamoja na mamlaka ya viwanja vya ndege ili kuongeza utayari wa maeneo husika
Vilevile Wizara yangu imepanga kufanya yafuatayo
Kuendelea kutoa mafunzo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwemo kuwaongezea wataalamu wapatao 80 wa mipakani uwezo wa ufuatliaji na utambuzi wa ugonjwa huu. Mafunzo haya yanaendelea mjini Morogoro 
Kutoa mafunzo kwa Timu za dharura na maafa (Rapid Respond Teams) ambayo yanategemewa kuanza mnamo tarehe 27 Agosti 2018 jijini Mwanza. Lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuratibu na kukabiliana na ugonjwa huu endapo utatokea hapa Nchini. Idadi ya wataalam watakao pata mafunzo hayo ni kama ifuatavyo; Mkoa wa Mwanza (15), Kagera (15) na Kigoma (15) ili kujaza nafasi ya mapungufu katika wilaya ambazo ziko katika hatari na bado hazijapata mafunzo haya. 
Timu ya Wakurugenzi wa Wizara ikiongozwa na Mganga Mkuu wa serikali itatembelea mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza. Lengo la ziara hii ni kufuatilia kwa ukaribu utayari wa mikoa hii katika kukabiliana na ugonjwa huu endapo utatokea
Kituo chetu cha uratibu wa milipuko ya magonjwa na majanga yaani Public Health Emergency Operation Center (PHEOC) kipo katika utahadhari wa juu (level 1 - High Alert) ili kufuatilia kwa ukaribu ugonjwa huu nchini DRC pamoja na kuratibu utayari wetu Kitaifa na katika ngazi ya Mikoa 

Hitimisho
Wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa huu, pamoja na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa  kuugua ugonjwa huu hapa nchini. 


Hivyo naelekeza yafuatayo:-
Wakuu wa Mikoa yote, waitishe kikao cha Afya ya msingi (PHC) na kujadili jinsi mikoa yao ilivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia kwenye maeneo yao
Wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika ofisi za serikali za mitaa au kijiji au kituo cha kutolea huduma za Afya endapo kutatokea mtu  yeyote mwenye dalilil za ugonjwa wa Ebola
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, na hasa wale walioko katika mikoa iliyo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi, wawe macho na makini zaidi katika kusimamia jitihada hizi za Wizara. 
Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali, zikiwemo taasisi za kimataifa katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti iugonjwa huu ili usiingie hapa nchini. 
.
Ahsanteni kwa kunisikiliza

0 on: " TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO"