Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 5 Septemba 2018

TAARIFA KWA UMMA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO






TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU KAMPENI YA UMEZESHAJI WA DAWA ZA KINGATIBA DHIDI YA KICHOCHO NA MINYOO TUMBO NCHINI

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwataarifu kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na OR -TAMISEMI imekuwa ikitekeleza zoezi la umezeshaji wa dawa za kingatiba dhidi ya magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo kwa watoto walio na umri wa kwenda shule. Zoezi hili lilianza tangu mwaka 2005 kwa baadhi ya Halmashauri zenye maambukizi mengi na makubwa Zaidi ya magonjwa haya na baadae mwaka 2015, Serikali iliweza kuzifikia Halmashauri zote 184 nchini baada ya tafiti kuonyesha kuwa maambukizi yapo kila Halmashauri.

Ni vyema tukakumbuka kwamba nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikiwa ni mojawapo zimeridhia azimio Namba 66.12 la mwaka 2013 ambalo utekelezaji wake ni pamoja na udhibiti wa magonjwa ya kichocho na minyoo.



Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Waathirika wakuu wa ugonjwa wa Kichocho na Minyoo ya tumbo ni watoto wenye umri wa kwenda shule, yaani watoto wenye umri kati ya miaka 5 na 14, ambao wanakuwa katika shule za msingi.
Hivyo, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Afya, inayohimiza kinga dhidi ya magonjwa mbali mbali, Serikali hutoa dawa hizi za kingatiba ya kichocho na minyoo ya tumbo (Vidonge) walau mara moja kwa kila mwaka katika Halmashauri zote zilizoathirika. Kwa vile magonjwa haya yapo katika jamii na mazingira yetu, zoezi hili limekuwa ni endelevu kwa takribani miaka 13 sasa. Kwa mwaka 2018, Halmashauri zote nchini zimetekeleza zoezi hili kwa mafanikio makubwa, na kwa Mkoa wa Dar es salaam ndio unahitimisha zoezi hili kwa mwaka huu. (Jedwali la zoezi la ugawaji dawa shuleni 2018)

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazosambaa kupitia vyombo vya habari kama magazeti na mitandao ya kijamii inayozungumzia zoezi hilo la umezeshaji wa dawa hizi za kingatiba shuleni. Napenda kutoa ufafanuzi kwamba tunachotoa ni KINGATIBA na sio  CHANJO. Aidha dawa hizi  za kingatiba ni salama na zimethibitishwa ubora wake na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania( TFDA) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO). Aidha, dawa hizi (Praziquantel na Albendazole) pia zimesajiliwa kulingana na taratibu za nchi na mamlaka husika. Vile vile, dawa hizi zinazotumika katika zoezi hili zinatumika katika Hospitali na vituo mbali mbali nchini na hupatikana katika maduka ya dawa nchi nzima kwa maelekezo ya Madaktari.



Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kutoa maelezo kuhusu magojwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo kama ifuatavyo:
Minyoo ya Tumbo: Ipo ya aina tatu (3); Minyoo Mviringo (Round worms), Minyoo Mjeledi (Flat worms) na Minyoo safura (Hookworms). Maambukizi ya minyoo hii hutokea pale mtu anapokula mayai ya minyoo hiyo kutoka katika udongo (kupitia mbogamboga, matunda, au vyakula vingine vibichi ambavyo havijaandiliwa vizuri kwa kufuata kanuni za afya) au kwa mtu kuambukizwa minyoo hii kwa kupenya kwenye ngozi. Dalili za ugonjwa wa minyoo ya tumbo ni pamoja na tumbo kuuma, upungufu wa damu, udumavu, utumbo kujifunga, kukosa hamu ya kula, mwili kuchoka na hivyo kupelekea mahudhurio hafifu shuleni na mtoto kuwa na uelewa mdogo wa masomo.
Ugonjwa wa Kichocho: Husababishwa na minyoo jamii ya Schistosoma. Kuna aina mbili (2) za kichocho; kichocho cha kibofu cha mkojo (husababishwa na minyoo ya Schistosoma haematobium) na kichocho cha tumbo (husababishwa na minyoo ya Schistosoma mansoni). Maambukizi ya vimelea hivi hutokana na mtu kugusa maji yaliyotuama yenye vimelea hivyo. Vimelea hivi hujificha na kukua katika mwili wa konokono waishio katika maji yaliyotuama. Baadhi ya dalili za ugonjwa huu ni damu kutoka kwenye mkojo na choo, kuvimba tumbo, na baadae inaweza kusababisha saratani ya kibofu cha mkojo, shinikizo la damu kwenye ini, kutapika damu, n.k.

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Zipo njia mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya minyoo ya tumbo na kichocho ikiwemo utoaji wa elimu ya afya, utoaji wa dawa za kukinga na kutibu magonjwa haya, utumiaji sahihi wa vyoo, kuweka maeneo katika hali ya usafi na kula vyakula vilivyopikwa na kuiva vizuri.
Dawa za vidonge za Praziquantel ambayo ni kingatiba ya ugonjwa wa kichocho, na dawa ya Albendazole hutolewa ili kudhibiti ugonjwa wa Minyoo ya Tumbo. Dawa hizi hutolewa kwa watoto kwa kufuata kipimo cha urefu. Kipimo hiki kimehakikiwa na kinashabihiana na uzito wa mtoto husika na hutoa makadirio sahihi ya dozi inayohitajika. Zipo tafiti nyingi zilizohakiki kipimo hicho na kuonyesha kuwa ni kipimo sahihi kinachofaa kwa zoezi la kingatiba kwa watu wengi (Mass Drug Administration - MDA).
Zipo faida nyingi wanazopata watoto wetu kwa kumeza dawa hizi na baadhi ya faida hizo ni:
·        Kuua kabisa minyoo ya kichocho na minyoo ya tumbo
·        Kuboresha ukuaji wa mtoto
·        Kuongeza uelewa wa mtoto awapo shuleni
·        Kupunguza upungufu wa damu na unyemelezi wa magonjwa kama Malaria
·        Kuepusha athari zote za Minyoo na Kichocho mfano Kansa ya kibofu, presha ya ini n.k

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwafahamisha kwamba, kabla ya kuanza zoezi hili kuanza kutekelezwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Halmashauri husika walitoa mafunzo kwa waratibu wa afya na wa elimu wa Halmashauri zote. Aidha, uraghabishi (advocacy) kwa kupitia Kamati za Afya za Mkoa na Wilaya (PHC) pia ulifanyika.
Aidha, Halmashauri zote pia ziliandaa mafunzo rasmi kwa walimu wa shule za msingi na wataalamu wa afya wanaohusika na undeshaji wa zoezi hili.
Wanajamii pia wameendelea kuhamasishwa kushiriki kwa wingi katika zoezi hili kwa kupitia njia mbalimbali zinazofaa kwa sehemu husika. Masuala makuu ya hamasa yanahusisha kuandaa chakula ili watoto wapewe mlo kabla ya kumeza dawa na kushiba na kumeza dawa hizo ndani ya masaa 2 baada ya kupata chakula.

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Kama ilivyo kawaida kwa dawa nyingine yapo maudhi madogo madogo yanayoweza kujitokeza pale mtoto atakapomeza dawa hizo, hasa iwapo atameza bila ya kuwa na kitu chochote tumboni. Maudhi hayo ni kama yafuatayo:
·        kutapika,
·        kupata kizunguzungu,
·        kuharisha,
·        mwili kukosa nguvu.
Maudhi haya yatokanayo na dawa hizi yanaisha kwa muda mfupi na yanakabiliwa kwa kumpumzisha mtu sehemu tulivu na kumpatia maji. Maudhi haya yakiendelea baada ya masaa 24 tunashauri mtoto apelekwe kituo cha afya cha karibu yake.

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Napenda kuwathibitishia Watanzania kwamba tangu afua hii ianze kutumika hapa nchini kuanzia mwaka 2005 tumekuwa na mafanikio makubwa, ambayo ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha maambukizi (Prevalence) ya ugonjwa wa kichocho na minyoo tumbo kutoka wastani wa asilimia 80 % (2005) hadi 30% (2018) katika maeneo mengi nchini, pia wingi wa maambukizi ya minyoo kwa mtoto mmoja mmoja umepungua sana ambapo hivi sasa ni chini ya asilimia 10 ya watoto walio na umri wa kwenda shule nchini ndio wanamaambuki makubwa ya kichocho na minyoo ya tumbo (High intensity).
Aidha, nia yetu ni kuendelea na afua hii ili hatimaye tuweze kuyatokemeza kabisa magonjwa haya nchini kwetu.

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Kwa kuhitimisha napenda kutoa wito kwa Wazazi na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika mazoezi haya ya utoaji wa dawa za kingatiba. Mazoezi haya ni muhimu na endelelevu kwani magonjwa haya yanaathiri sana jamii yetu.
Nanyi wanahabari tunaomba muendelee kuelimisha umma kuhusu magonjwa haya na umuhimu wa kingatiba. Dawa hizi huimarisha afya ya mtoto na hivyo kujenga taifa lenye afya bora na lenye nguvu ya kutosha ili kuleta maendeleo.

Aidha Ratiba ya Ugawaji dawa shuleni Mwaka 2018 ilikuwa kama ifuatavyo
Namba
Tarehe
Mikoa husika
1
APRIL, 2018
Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Geita, Rukwa, Katavi, Manyara, Singida, Pwani, Lindi, Mtwara, Tabora, Njombe, Iringa (14)
2
JULAI, 2018
Tanga, Ruvuma, Morogoro, Mbeya, Songwe (5)
3
AGOSTI 2018
Shinyanga, Mwanza, Mara, Kigoma, Simiyu, Kagera na Dar Es Salaam (7)

Ndugu Wananchi na Wanahabari,
Aidha, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inawataka wananchi kuzipuuza taarifa za upotoshaji zinazolenga kuharibu huduma za chanjo zilizotolewa hivi karibuni kwa njia ya Mitandao ya Kijamii kuwa chanjo zinazotolewa zina lengo la kuleta ugumba na kutozaa, na kwamba ni mpango mahususi wa nchi za Ulaya katika kupunguza idadi ya Waafrika duniani. Tunapenda kueleza kuwa taarifa kama hizi zilishawahi kutolewa tena huko nyuma na watu wasio na utaalamu wa masuala ya chanjo na wenye lengo chafu dhidi ya mafanikio ya chanjo nchini na duniani. Aidha ufafanuzi umekuwa ukitolewa mara kwa mara kuhusu upotofu wa dhana hii mbaya.
Wizara inawahakikishia wananchi kuwa Chanjo zinazotolewa nchini ni salama na zinathibitishwa na mamlaka zetu hapa nchini na Shirika la Afya Duniani na zina lengo la kuwakinga binadamu dhidi ya magonjwa hatari ya kuambukiza na si kuzuia mimba au kuleta ugumba.

Ndugu Wanahabari na Wananchi,
Faida za chanjo zinafahamika na mafanikio yake sote tumeyaona. Tunayo mifano mingi sana. Mmojawapo ni kwamba kwa kupitia afua ya utoaji chanjo Tanzania imefanikiwa kutokomeza na kuondoa magonjwa kama vile ndui, ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua, na Ugonjwa wa pepopunda wa watoto wachanga. Sote tumeshuhudia kufungwa kwa wodi za wagonjwa wa Surua katika Hospitali zote; kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ugonjwa wa Kuhara kwa watoto n.k. Lengo la kutoa chanjo ni kuundaa mwili kupambana na magonjwa kwa kuuamushia kinga na ni mojawapo ya kinga mahususi dhidi ya magonjwa husika inayoaminika Duniani kote. Aidha, wote tumeshuhudia kupungua sana kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi kufikia vifo 54 kwa kila vizazi hai 1000 na hivyo kufikia lengo la Maendeleo ya Milenia Namba 4 mwaka 2015.



Ndugu Wanahabari na Ndugu Wananchi,
Wizara inawataka wananchi kupata Taarifa sahihi kutoka Wizara ya Afya, na kuacha mara moja kutumia mitandao ya kijamii vibaya na kupotosha jamii. Aidha, niwaombe Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kote nchini kuendelea kuelimisha wananchi juu ya faida za chanjo.  Pia Wizara inaviomba vyombo vinavyohusika kuchukua hatua dhidi ya watu wanaopotosha jamii na kuhatarisha usalama na afya za watanzania.

Imetolewa na:

Ummy A. Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
04/09/2018


0 on: "TAARIFA KWA UMMA"