Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 13 Desemba 2018

SERIKALI YATOA RAI KWA WANANCHI KUJITOKEZA KUPATA DAWAKINGA YA MATENDE NA MABUSHA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini, pembeni yake ni mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo Mungila

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile akitoa tamko kuhusu kampeni ya kumeza dawa kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya Tumbo, Usubi, Trakoma na Matende na Mabusha katika mikoa saba hapa nchini, pembeni yake ni mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. Upendo Mungila


TAMKO LA MHE. DKT. FAUSTINE NDUGULILE (MB.) NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU KAMPENI YA KUMEZESHA DAWA  KINGATIBA YA MAGONJWA YA MINYOO YA TUMBO, USUBI, TRAKOMA, MATENDE NA MABUSHA KATIKA MIKOA SABA (7) HAPA NCHINI. 

Ndugu Wananchi
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikishirikiana na wadau itafanya kampeni ya kugawa dawa za Kingatiba ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, usubi, trakoma, matende na mabusha katika mikoa saba (7) hapa nchini, ambayo ni Dar es Salaam katika Manispaa zote, Iringa wilaya ya Mufindi DC, Mtwara wilaya ya Masasi, Pwani wilaya ya Kibaha na Mafia, Rukwa wilaya ya Kalambo, Songwe wilaya ya Songwe na Tanga wilaya ya Mkinga na Korogwe. 
Lengo kuu la kufanya kampeni ni kutibu na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya minyoo ya tumbo, Usubi, Trakoma, Matende na mabusha au Ngirimaji. Aidha, dawa hizi au kingatiba hii, zitasaidia kupungua kwa ulemavu na adha za magonjwa haya. Kuna faida kubwa kwa wananchi wakishiriki katika zoezi hili la umezaji kinga tiba hii. Faida hizo ni:
Kukinga upungufu wa damu.
Kumuepusha mtu kupata upofu.
Kupunguza maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Kuua vimelea vya Magonjwa haya.
Kukinga na kupunguza maumivu na madhara yanayosababishwa na Magonjwa haya.
Kupungua kwa Magonjwa ya ngozi.
Kuongeza virutubisho bora mwilini.
Kuboresha nguvukazi katika jamii.
Kuwezesha watoto kukua vizuri.
Kuongeza uelewa wa watoto wawapo shuleni.

Ugonjwa wa Minyoo ya tumbo huathiri zaidi jamii maskini na husababishwa na mtu kula mayai ya minyoo kutoka katika udongo au minyoo hii kupenya kwenye ngozi. Aidha, Kuna minyoo ya aina tatu ambayo husababisha ugonjwa huu,minyoo mviringo,minyoo mijeledi  na minyoo ya safura. Pamoja na kutoa dawa za kutibu ugonjwa huu lakini pia jambo la msingi ni vyema wananchi mkaweka maeneo yanu katika hali ya usafi na kula vyakula vilivyopikwa vizuri na kuiva. 
Ugonjwa wa Usubi husababishwa na minyoo inayoitwa Onchocerca volvulus, huenezwa na inzi weusi wadogo wanaokaa kandokando ya mito yenye maji yaendayo kasi. Athali za ugonjwa huu ni ngozi kuwasha,  ngozi kuwa na mabakamabaka kama ya chui, ngozi kuwa na muonekano wa kenge, pia uono hafifu na upofu. 

Trakoma au vikope ni ugonjwa sugu unaoshambulia macho na kusababisha kope kupinda na kugusa kioo cha jicho ambapo husababisha makovu juu ya kioo cha jicho na hupunguza uwezo wa kuona na kusababisha upofu usiotibika. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aina ya Chlamydia trachomatis. 
Juhudi kubwa za kutokomeza ugonjwa wa Trakoma au Vikope zimefanyika na kuweza kupunguza kiwango cha maambukizi. Kati ya Wilaya 71 zilizokuwa na uambukizo, Wilaya 63 sawa na Asilimia Themanini na Tisa (89%) zimeweza kufikia kiwango cha chini  ya asilimia 5% ambayo inaruhusu kusimamisha zoezi la kingatiba ya Trakoma  katika ngazi ya Jamii. Katika mwaka huu wa 2018 ni Wilaya 8 tu ndio zinaendelea na zoezi la  Kingatiba ya  ugonjwa wa Trakoma kwa kutumia dawa aina ya Zithromax. 
Ugonjwa wa Matende na Mabusha husababishwa  na minyoo midogo midogo ambayo huenezwa na mbu wa aina zote kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. 
Dalili za ugonjwa huu ni homa kali ambayo huchukua siku 3 – na huambatana na baridi kali, Kichefuchefu, kutapika, kuvimba kwa mitoki, kubabuka ngozi, kuvimba kwa miguu, mikono, matiti au sehemu za siri kwa jinsia zote.
Mafanikio katika kutokomeza ugonjwa wa Matende na mabusha yameanza kuonekana, kati ya Wilaya 120 ambazo zilikuwa na uambukizo, Wilaya 98 ambazo ni sawa na asilimia sabini na Saba (77) zimeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo na hivyo kufikia kiwango cha kusimamisha ugawaji wa kingatiba kwa jamii katika Wilaya hizo. 

Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu 2018 ni wilaya 28 tu ndizo zitakuwa na zoezi la umezeji kingatiba kwa ajili ya kukinga na kutibu ugonjwa wa Matende na mabusha katika ngazi ya jamii. Magonjwa haya yasipopatiwa tiba haraka mtu anaweza kupata madhara kama:-
Maumivu ya muda mrefu na wakati mwingine ulemavu mkubwa.
Umaskini na kudumaza uchumi wa kaya na hatimaye Taifa.
Kudhoofisha ukuaji hasa kwa watoto wenye umri mdogo kimwili na kiakili.
Utapia mlo kwa watoto
Utumbo kujisokota 
Hatimae kifo kama mgonjwa hakutibiwa.

Ndugu Wananchi
Pamoja na kwamba ugawaji wa dawa utafanyika katika mikoa saba (7) hapa nchini, napenda nijikite sana katika kuelezea umezaji wa dawa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka huu wa 2018. Hii siyo mara ya kwanza kwa mkoa huu kufanya zoezi la umezaji wa dawa Kingatiba ya minyoo ya tumbo, matende na mabusha. Zoezi hili kwa mkoa wa Dar es Salaam lilianza mwaka 2013 na limekuwa likitekezwa kila mwaka. Katika mwaka wa kwanza watu wapatao 3,028,828 walijitokeza na kupatiwa kingatiba hii. Idadi hii imekuwa ikiongezeka kila mwaka zoezi linapotekelezwa na kwa mwaka jana 2017, watu waliojitokeza kupatiwa kingatiba walikuwa 4,914,351 ambayo ni sawa na asilimia 86 (86%) ya lengo lililotarajiwa.  
Ingawa kiwango cha umezaji wa dawa hizi kwa jamii kimeendelea kuwa juu, lakini idadi ya watu wanaojitokeza kwenye zoezi hili bado haijaridhisha sana kutuwezesha kutangaza kwamba tutatokomeza magonjwa haya katika mkoa wa Dar es Salaam, bado maambukizi yapo juu ya kiwango cha asilimia mbili (2%). Lengo la mwaka huu ni kugawa dawa watu wapatao 5,376,207 katika Manispaa zote tano (5) za Mkoa wa Dar es Salaam. 

Kama wizara tumeweza kuwezesha rasilimali za dawa na fedha za utekekelezaji wa kampeni hi muhimu. Aidha tumeweza kusaidiana na wenzetu wa TAMISEMI kufanya uhamasishaji kwa ngazi mbalimbali kwa viongozi wa jamii, kata na mitaa. Kampeni hii itawapa fursa wanajamii kupunguza uambukizo wa magonjwa haya na hatimaye kuwa jamii kuwa huru na vimelea vya magonjwa haya kwa vizazi vijavyo. 
Kampeni hii kwa mwaka huu, itahusisha wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na wageni waliopo katika Jiji hili wenye umri wa kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea. Dawa zitakazotolewa ni aina Albendazole kidonge kimoja (kitatafunwa) na Ivermectin (Mectizan)  ambayo itatolewa kulingana kimo chake . 
Ndugu Wananchi
Napenda kuwataarifu kuwa kampeni hii itaendeshwa kuanzia tarehe 15  hadi 20 mwezi Disemba, 2018 kwa watu wenye umri uliotajwa hapo juu. Napenda kusisitiza kuwa viongozi wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na ngazi ya jamii wanawajibika kutoa taarifa hii na kuhamasisha wananchi wote washiriki kikamilifu katika kampeni. Aidha, katika kufanikisha zoezi hili nawasishi wananchi na viongoziu wote kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kama vile vyombo vya habari, kuhamasisha wananchi makanisani na misikitini  kujitokeza kushiriki zoezi hili.
Aidha, wanachi mtambue kuwa vituo vya kutolea huduma hizi vimesogezwa karibu jamii ili kurahisisha upatikanaji wa huduma. Ambapo Jumla ya vituo mia tisa kumi na tano (915) ambavyo ni pamoja na Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali, stendi za mabasi, masoko, ofisi za serikali za mitaa, ofisi za taasisi mbalimbali pamoja na kambi za Majeshi yetu na Magereza vitatoa huduma hiin a takribani wagawa dawa Elfu moja mia nane thelathini (1,830) waliopatiwa mafunzo watahusika katika kutoa huduma hiyo kwenye vituo Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na wa mikoa mingine ambayo zoezi hili litafanyika  kushiriki kikamilifu katika umezaji dawa hizi. Zoezi hili ni muhimu kwani magonjwa haya yanaathiri sana jamii yetu. Kwa viongozi wenzangu na wanahabari tunaomba muendelee kuelimisha umma kuhusu magonjwa haya na umuhimu wa umezaji wa kingatiba hii. 

LINDA, OKOA MAISHA, ZUIA ULEMAVU JITOKEZE KUMEZA DAWA-KINGATIBA’


0 on: "SERIKALI YATOA RAI KWA WANANCHI KUJITOKEZA KUPATA DAWAKINGA YA MATENDE NA MABUSHA"