Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Habari. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Habari. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 14 Juni 2020

WAZIRI UMMY AZITAKA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUACHA KUWADAI DAMU WAGONJWA KABLA YA HUDUMA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma mapema leo.
Meneja wa Mpango wa Damu Salama nchini Dkt. Magdalena Lyimo akifafanua jambo kwa Waziri Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kituo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.





Picha mbalimbali zikionesha Waziri Ummy Mwalimu akiwajulia hali wananchi waliojitokeza kutoa damu katika Kituo cha Damu Salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.


NA WAJMW-DODOMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali zote nchini za Serikali na binafsi, Zahanati na Vituo vya Afya kuacha kuwadai damu wagonjwa kabla ya kuwapa huduma.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wachangia damu duniani yenye kauli mbiu “Damu Salama inaokoa maisha” ambayo kitaifa yamefanyika katika kituo cha kidogo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

“Nazitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi kuacha tabia ya kuwadai damu wagonjwa na ndugu kabla ya kumpatia mgonjwa huduma, mnatakiwa kutoa huduma kwanza na masuala ya wanandugu kuambiwa walete watu wa kuchangia damu kabla ya huduma ni kinyume na taratibu na kanuni za utoaji wa huduma za afya”. Amesisitiza Waziri Ummy.

Waziri Ummy amezitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi na vituo vya Afya nchini kushirikiana na Mpango wa taifa wa damu salama katika kukusanya damu na wasibaki wao kuwa watumiaji wa damu bila kuweka fedha au jitihada zozote za ukusanyaji.

Waziri Ummy amesema  takwimu zinaonyesha kuwa, wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani mwaka 2015 jumla ya chupa za damu 104,632 zilikusanywa, kupimwa na kusambazwa. Idadi hii imeongezeka hadi kufikia chupa 309,376 ziizokusanywa mwaka 2019 ambayo ni ongezeko la chupa 204,744 ambayo ni sawa na asilimia 195 ikilinganishwa na chupa za damu zilizokusanywa mwaka 2015.

“Tumeboresha huduma kwenye Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa kuwapitia mashine za kisasa za kupimia damu ambapo uwekezaji huo umegharimu karibu Bilioni 13. Kwa kutumia mashine hizi Mpango una uwezo wa kufanya vipimo 4000 kwa masaa 6 kutoka vipimo 1404 kwa mashine zilizokuwepo awali kabla Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuchangia damu ni tendo la huruma, utu na upendo hivyo amewashukuru wachangia damu wote nchini hususani wale wanaochangia mara kwa mara. Pia amewahamasisha wananchi ambao hawajawahi kuchangia waweze kuchangia damu angalau mara moja kwa mwaka.

Waziri Ummy ametaka Mpango wa damu salama nchini kuweka utaratibu wa kufikia kaya zote nchini na kuhamasisha angalau awepo mtu mmoja kwa kila kaya ambae atakua anachangia damu mara kwa mara ili kuweza kukidhi mahitaji ya kitaifa ya damu salama.

Mwisho Waziri Ummy ameipongeza mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kuweka mikakati mizuri ya uchangiaji damu ambapo mgonjwa mwenye uhitaji wa damu anahudumiwa kwanza kabla ya kutafuta ndugu wa kuchangia damu.

MWISHO

Ijumaa, 5 Juni 2020

EWURA NA MOUNT MERU ZATOA MSAADA KWA AJILI YA UDHIBITI WA CORONA NCHINI

- Hakuna maoni




Na Emmanuel Malegi-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo amepokea msaada wa hundi ya kiasi cha Tsh. Milioni 100 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)uliokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi Bw. Godfrey Chibulunje akiwa na Meneja Mawasiliano na uhusiano wa mamlaka hiyo Bw. Titus Kaguo.

Aidha, Waziri Ummy amepokea msaada wa ndoo 480 sawa na Lita 9600 za vitakasa mikono (Hand Sanitizer) zenye thamani ya Tsh. Milioni 11 zilizotolewa na kampuni ya Mafuta ya Mount Meru ambazo zitatumika katika kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini. Vitakasa mikono hivyo vimekabidhiwa na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Prabhat Yadau.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Ummy kwa niaba ya Waziri Mkuu ameshukuru kupata misaada hiyo ambayo itasaidia katika kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini na pia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari licha ya maambukizi ya ugonjwa huo kupungua nchini.

Alhamisi, 4 Juni 2020

UVUTAJI WA TUMBAKU UNA ATHARI UCHUMI WA MTU MMOJA MMOJA ANAYETUMIA

- Hakuna maoni






Na Emmanuel Malegi-Dodoma

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania kama nchi nyingine za Kiafrika wavutaji wa tumbaku wako hatarini kuyumba kiuchumi na kupata magonjwa yasiyoambukizwa kama tahadhari hazitachukuliwa mapema.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa matumizi ya tumbaku kwa watu wazima wa mwaka 2018 nchini uliofanyika mapema leo katika Ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema utafiti huo umeonesha kuwa kwa wastani matumizi ya tumbaku kwa mtu mmoja kwa mwezi inagharimu Shilingi za Kitanzania 28,840/= fedha ambayo ingetosha kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa asilimia 58 na umaskini wa kupindukia (mahitaji ya chakula) kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa asilimia 85.

Kwa kutumia taarifa za Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa Mwaka 2017-18, fedha za kujikimu kwa ajili ya mahitaji ya msingi kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Shilingi za Kitanzania 49,320/= na mahitaji ya chakula kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Shilingi za Kitanzania 33,748/=”. Amesema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Matokeo yameonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10 (8.7%), wenye umri wa miaka 15 au zaidi nchini Tanzania wanatumia tumbaku ya aina yeyote na hivyo kuwa na watu milioni 2.6 kati ya watu zaidi ya  milioni 55. Wanaume ni asilimia 14.6 na wanawake ni asilimia 3.2.

Aidha, Waziri Ummy amesema watu 4 kati ya 10 (40.3%) nchini wamewahi kuona onyo la matumizi ya tumbaku kupitia redio au runinga. Pia matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, watu 9 kati ya 10 (92.3%) wenye umri wa miaka 15 au zaidi wanaamini uvutaji wa sigara husababisha magonjwa, wakati watu 8 kati ya 10 (84.4%) wanaamini kuvuta hewa ya mtu anaevuta sigara kunaweza kuwasababishia magonjwa hata kama wao hawavuti sigara.

katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.  Taarifa inaonesha kuwa watu 4 kati ya 10 (32.9%) wameathiriwa na moshi wa tumbaku sehemu za kazi ikiongozwa na sehemu za mabaa na kumbi za starehe kwa asilimia 77 (watu milioni 3), maeneo ya huduma za biashara za vyakula asilimia 31.1(watu milioni 3.5) na majumbani asilimia 13.8 (watu milioni 4.1).

Waziri Ummy amesema utafiti huo una umuhimu wa kipekee katika Wizara, kwani matokeo yake yatasaidia katika kutathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na magonjwa makuu manne yasiyoambukiza ambayo ni Saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mfumo wa hewa na kisukari.

katika kuhakikisha elimu dhidi ya athari ya tumbaku inaifikia jamii ipasavyo. Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa  Watendaji wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wadau wengine, kutengeneza au kupitia upya Sheria ya kudhibiti matumizi ya Tumbaku ili iendane na Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya Tumbaku na kuendelea kutoa Elimu kwa jamii kuhusu madhara yake; Wizara ya Elimu kuendelea kuimarisha juhudi za kuwakinga wanafunzi dhidi ya tumbaku na bidhaa zake; Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha wale wanaokiuka miongozo kama vile kuendelea kuvuta sigara kwenye maeneo ya wazi wanachukuliwa hatua stahiki; Watengenezaji na wauzaji wa sigara, kufuata miongozo iliyowekwa na Serikali ikiwemo kutokuweka mabango au kutangaza na kuhamasisha matumizi ya sigara, kupitia bidhaa kama miamvuli, T-Shirts, kofia, na kutowauzia watoto wenye umri chini ya miaka 18; jamii kuacha kutumia tumbaku na bidhaa zake na Taasisi za Utafiti kufanya Tafiti za kuangalia vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku ilikuwe na takwimu za nchi na siyo kutegemea za kutoka nje.

*MWISHO*








Jumamosi, 30 Mei 2020

HONGERENI WATUMISHI WOTE WA AFYA KWA JINSI MLIVYO PAMBANA KATIKA JANGA LA CORONA.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akisisitiza jambo wakati akiongea na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (hawapo kwenye picha).

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiteta jambo na Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe akiteta jambo na Mkururugenzi msaidizi anaesimamia hospitali za Rufaa Dkt. Caroline, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Baadhi ya Watumishi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakifuatilia neno kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel pindi alipofanya ziara katika Hospitali hiyo. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mtoto aliefika na mzazi wake kupata matibabu katika wodi ya watoto, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiwa na baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Afya, katika chumba cha Watoto njiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mama aliyempeleka mtoto kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. 

 Picha ya pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiwa na viongozi kutoka Wizara ya Afya na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma pindi alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi hao.

Jengo la Idara ya magonjwa ya wanawake na uzazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.



HONGERENI WATUMISHI WOTE WA AFYA KWA JINSI MLIVYO PAMBANA KATIKA JANGA LA CORONA.

Na WAMJW- DOM

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewashukuru Watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kwa namna walivyojitoa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

"Jinsi ambavyo nyie mmepambana dhidi ya virusi vya Corona na bado mkamuunga mkono Mhe. Rais na ushauri alioutoa yeye na Wataalamu wengine wa Wizara kupitia Waziri wa Afya, nyie mmekuwa mashujaa na jeshi la uzalendo wa hali ya juu, nawashukuru sana" alisema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel aliendelea kwa kukemea tabia za wanasiasa wachache kupotosha Watanzania na Dunia kwa ujumla juu ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa Watumishi wa Sekta ya Afya nchini jambo ambalo sio kweli.

"Kuna wanasiasa wanapiga kelele kuhusu Corona kuliko sisi, nawaomba watu tuache kupiga siasa, sisi watumishi wa afya ndio watu wakwanza kukutana na wagonjwa wa Corona laikini leo watumishi mpo 504 je niambieni kuna yoyote amelazwa, watumishi walijibu hapana, kama kweli kuna Watumishi wanakufa basi nyie mngekuwa wa kwanza kuugua na kupoteza maisha" alisema.

Aidha, Dkt Mollel alitoa wito kwa Watumishi wa Sekta ya Afya nchini kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi ili kutoa huduma bora, huku akiweka wazi kuwa kazi ya kuwahudumia wananchi ni ya wito na ya uzalendo.

Pia, Mhe Mollel alielezea kuwa Rais alikuwa na maono ya kusitisha matibabu ya nje ya nchi kwa kuboresha huduma za kibingwa nchi na hii imejizihirisha baada ya dunia kupata janga la corona nchi yetu imeendelea kutoa huduma za kibingwa pasipo kutegemea matibabu ya nje kwa wananchi ambao walikuwa na sifa za kutibiwa nje .

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest ameweka wazi kuwa Hospitali hiyo imeendelea kutoa huduma za Afya bila kutetereka na kutoa elimu kwa umma licha ya kupitia katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona ulioikumba nchi.

"Tumeendelea kutoa huduma bora kwa wananchi bila kutetereka hata katika wakati huu wa janga la mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona ulioikumba nchi, Watumishi wetu wamesimama imara huku wakiendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya Corona "alisema.

Jumatano, 20 Mei 2020

WAZIRI UMMY AMESEMA UGONJWA WA KIFUA KIKUU UNAENDELEA KUPUNGUA NCHINI

- Hakuna maoni




Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Hadubini 7 za kuchunguza kifua kikuu zilizotolewa na Wizara kwa Wilaya ya Chamwino.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongea jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Bilinith Mahenge wakati wa hafla ya makabidhiano ya Hadubini 57 zilizotolewa na Wizara ya Afya katika Mkoa wa Dodoma. Hafla hiyo ilifanyika Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi moja ya Hadubini za kuchungua ugonjwa wa kifua kikuu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Bilinith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Vumilia Nyamaga, Mbunge wa Chilonwa Mhe. Joel Mwaka huku Mkurugenzi wa huduma za kinga Dkt. Leonard Subi akishuhudia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Bilinith Mahenge na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Vumilia Nyamaga wakibeba moja ya Hadubini zilizotolewa na Wizara ya Afya kwa Wilaya ya Chamwino.
Baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa kituo cha afya cha Buigiri waliojitokeza kushuhudia makabidhiano ya Hadubini mpya za kupima kifua kikuu zilizotolewa na Wizara ya Afya.


Na WAJMW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema maambukizi ya Kifua Kikuu (TB) yamepungua nchini kutoka wagonjwa  164,000 mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa 142,000 mwaka 2018.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akikabidhi Hadubini 57 katika Mkoa wa Dodoma zitakazotumika kufanya vipimo vya ugonjwa wa Kifua Kikuu ambazo zitasambazwa katika Hospitali na Vituo vya Afya mbalimbali mkoani humo.

“Leo nimeanza zoezi la kukabidhi Hadubini 941 zilizonunuliwa na Serikali kwa ufadhili ya Global Fund zenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.3 ambapo leo nitamkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binilith Mahenge Hadubini 7 za Wilaya ya Chamwino zitakazosambazwa katika vituo vya Afya mbalimbali”. Amesema Waziri Ummy.

Pamoja na hayo Waziri Ummy ametumia muda huo kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma ikiwa ni pamoja na kupungua maambukizi mapya kwa asilimia 18 lengo likiwa ni asilimia 20 na vifo vimepungua kwa asilimia 27 lengo likiwa ni asilimia 35.

Aidha, Waziri Ummy amesema ugunduzi wa Kifua Kikuu unaendelea kuimarika ambapo idadi ya wagonjwa waliogundulika na kuwekwa kwenye matibabu imeongezeka kutoka wagonjwa 62,180 mwaka 2015 hadi kufikia 82,,140 mwaka 2019.

Kwa upande wa vituo vya ugunduzi wa tiba, Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu vituo vimeongezeka kutoka 662 mwaka 2016 hadi kufikia vituo 1201 mwaka 2019.

Katika kipindi cha miaka idadi ya wagonjwa waliogundulika kuwa na Kifua Kikuu imepungua kutoka wagonjwa 164,000 mwaka 2015 hadi 142,000 mwaka 2018.

Waziri Ummy amesema vifo vinavyotokana na TB vimepungua  kutoka makadirio ya vifo 30,000 mwaka 2015 hadi vifo 22,000 mwaka 2018.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Hadubini hizo zitapelekwa katika vituo vipya vya kutolea Huduma za afya 487 ambavyo vimejengwa, Hospitali za Mikoa 3, Hospitali za Wilaya 69 pamoja na vituo vya afya vya zamani 315 pia kubadilisha hadubini zilizoharibika katika vile vituo vyenye uhitaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutambua ulazima wa kuwepo Hadubini hizo katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya lengo likiwa ni kuondoa usumbufu kwa wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.

MWISHO

Jumanne, 12 Mei 2020

SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

- Hakuna maoni
Mfanyabiashara wa duka la dawa baridi, eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam akisafisha kitasa na kioo cha duka lake ikiwa ni sehemu ya maeneo hatarishi kupata virusi vya Corona kutoka na kushikwa mara kwa mara na wateja.

 Dereva boda boda eneo la Bagamoyo mjini. Bw. Octavian Leonard Nyoni akisafisha mikono yake kwa maji safi yanayotiririka na sabuni ikiwa ni sehemu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

 Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji kwa wananchi wa eneo la kituo cha mabasi cha Bagamoyo Mkoa wa Pwani, jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akitoa maelekezo namna ya kukaa mita moja au zaidi baina ya mtu mmoja na mwingine katika eneo la kituo cha mabasi ya Bagamoyo, ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Abiria katika kituo cha mabasi cha Kisarawe Mkoa wa Pwani wakisafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka na wengine kwa kutumia sanitizer kabla ya kupanda basi na kuanza safari, wamefanya hivo ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), akimkabidhi vipeperushi vya elimu juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa Afisa Afya wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima.

Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.


SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

Na WAMJW- PWANI

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kusafisha vitasa na maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara katika maeneo ya shughuli za kila siku na makazi yetu.

Ndg. Anyitike ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Kisarawe na Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo ya biashara na makazi.

"Tuhakikishe tunasafisha maeneo yote tunayoyashika mara kwa mara kwa maji yenye sabuni, sanitizer au spirit, futa maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara, lakini kumbuka kufuta sehemu za vitasa vya mlango na meza " alisema

Pia, alisisitiza kuwa, ni muhimu kujenga tabia ya kufuta katika maeneo yote ambayo watu wanapendelea kukaa kama vile maeneo ya viti, meza na vioo katika maeneo ya biashara bila kusahau milango.

Aidha, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa rai kwa wananchi hususan vinyozi katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanavaa Barakoa (mask) pindi wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi, ili kuvunja mnyororo wa maambukizi Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine endapo utakuwepo.

"Unapoenda saluni usikubali kinyozi yoyote akunyoe nywele kama hajavaa Barakoa hali itayosaidia kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona katika maeneo ya kazi na kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi hivyo" alisema.

Nae, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, ameendelea kuwakumbusha wazazi na walezi, kuhakikisha wanawalinda Watoto dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwapa elimu, na kuhakikisha hawazululi hovyo mtaani, hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa ili kuepusha misongamano inayoweza sababisha kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.

"Tuhakikishe Watoto wanakaa nyumbani, Watoto wasiende kuzulula hovyo, ni rahisi Watoto kupata maambukizi ya Corona kwasababu ya ufahamu na uelewa wao juu ya madhara ya ugonjwa huu wa Corona " alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amewaasa wafanyabiashara wa Barakoa kutoruhusu wateja kujaribu barakoa na kuzirudisha, hali inaweka wanunuzi wengine katika hatari yakupata maambukizi ya virusi vya Corona.

" kwa wauzaji wa Barakoa, chonde chonde usiruhusu mtu ajaribu Barakoa alafu akaiacha, hii itasaidia kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi vya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine endapo atatokea mtu mwenye maambukizi" alisema.

Timu ya Wizara ya Afya na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR kupitia kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama imeendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika, Wilaya ya Bagamoyo, Wilaya ya Kisarawe na Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Mwisho.

Ijumaa, 8 Mei 2020

SERIKALI ITAENDELEA KUTOA TAKWIMU ZA MWENENDO WA UGONJWA WA CORONA

- Hakuna maoni



Picha mbalimbali zikimuonesha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiangalia namna watoa huduma wanavyopokea simu kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Corona

Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mwananchi  kupitia kituo cha afya cha huduma kwa wateja mara baada ya kukizindua
Picha ya pamoja ikionesha Waziri Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na viongozi na wafanyakazi wa kituo cha afya cha huduma kwa wateja.

Na. WAMJW,Dar es Salaam.

Serikali itaendelea kutoa takwimu za mwenendo kuhusu Ugonjwa wa Corona mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya kiufundi ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizindua kituo cha Afya cha huduma kwa wateja (Afya call center) kilichopo eneo la Chuo cha Afya ya Sayansi ya Jamii Muhimbili (MUHAS), upanga Dar es Salaam.

“Takribani siku Saba sasa hatukuweza kutoa taarifa za takwimu za maabara  kuhusu mwenendo wa Corona nchini kwa sababu sasa hivi tunafanya maboresho  ya  maabara ya taifa ya afya ya jamii,hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba ndani ya siku chache zoezi litakamilika na tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara”, alisema.

Waziri Ummy amesema kuwa Corona ipo na itaendelea kuwepo kwa  miezi kadhaa,pia kumekuwepo na vifo kutokana na ugonjwa huu, hivyo wananchi wanapaswa kujua namna ya kuishi na ugonjwa huo kwa kujikinga na maambukizi.

 “Ninawasihi wananchi muondoe hofu na muendelee kuchukua tahadhari  ya kujikinga kwani ugonjwa wa Corona bado upo Tanzania, wagonjwa wapo na vifo vinavyotakana na COVID-19  vipo, ni muhimu kutambua kuwa ugonjwa huu utaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa hivyo lazima mchukue tahadhari ya kujikinga kama magonjwa mengine”Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wananchi kuendelea na  shughuli zao za ujenzi wa Taifa za kila siku pamoja na kuchukua tahadhari kwa  kuepuka  mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu mwingine.

Kuhusu Uvaaji wa barakoa, Waziri huyo amewataka wananchi kuendelea kuvaa   barakoa za vitambaa ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwa barakoa za viwandani ziachwe zitumike kwa ajili ya watoa huduma za afya.

Amewashauri wananchi kufua na kupiga pasi barakoa za vitambaa kabla ya kuzitumia na kusisitiza kuwa zinapaswa kuwa safi kabla ya kuvaliwa.

MWISHO

Alhamisi, 7 Mei 2020

DKT. NDUGULILE AIAGIZA NIMR KUFANYA UTAFITI KUHUSU UGONJWA WA CORONA

- Hakuna maoni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika mkutano na watafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Waziri wa Afya, Dkt. Ndugulile akifafanua jambo baada ya kumalizika kwa mkutano kujadili jinsi ya kupambana na Covid-19 nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya.






Dkt. Ndugulile akijadiliana jambo pamoja na watafiti wa taasisi hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

WAMJW- Dar es Salaam                                                                           

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya utafiti kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) kwa kuwa kuna tofauti kubwa ya dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa hapa nchini ukilinganisha na wagonjwa waliopo nje ya  nchi.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokutana na watafiti wa taasisi hiyo wakati  wakijadili maambukizi ya ugonjwa wa Corona na aina ya matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa hasa baada ya kubainika kuwa dalili za ugonjwa huo zinatofautiana na dalili za wagonjwa wa mataifa mengine.

“Kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti wa kisanyansi, moja ni uelewa wa jamii, tunataka kujua wagonjwa wanaougua Corona ni wagonjwa wa namna gani, wana magonjwa ya aina gani, dalili zinazowapata wagonjwa ni za aina gani.  Hapa tunataka tupate uwelewa,” amesema Dkt. Ndugulile.

Pia, amesema kupitia utafiti huo wanataka kujua aina za matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa ili kuhakikisha ugonjwa wa Covid-19 unadhibitiwa hapa nchini.

“Kutokana na muitikio mkubwa wa tiba asili na tiba mbadala, kupitia kikao hiki nawaelekeza wataalamu wetu wajipange kufanya utafiti na kutoa majibu ya tiba ya maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Dkt. Ndugulile.

Amesema wamekubaliana na watafiti hao kufanyia kazi maagizo hayo ndani ya muda mfupi na kutoa majibu sahihi ambayo yatasaidia katika mapambano ya ugonjwa wa Corona.

Naye Mkurugenzi Mkuu  wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya amesema mapambano dhidi ya ugonjwa Covid-19  ni vita ambayo inapaswa kufanyiwa utafiti ambao utasaidia kupatikana kwa njia sahihi za kukabiliana na maambukizi ya ugponjwa huo.

“Tunafahamu kwamba jamii za kiafrika zina utaalamu katika miti shamba. Katika hili kuna tafiti mbalimbali zinaendelea ili kuchunguza uwezo wa miti shamba kwa lengo la kupunguza makali ya Covid-19.

Mwisho