Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Kilimanjaro. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Kilimanjaro. Onyesha machapisho yote

Ijumaa, 21 Agosti 2020

TUSHIRIKIANE KUPAMBANA DHIDI YA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA - MGANGA MKUU WA SERIKALI.

- Hakuna maoni

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (watatu kutoka kushoto) akikagua taarifa za mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (watatu kutoka kushoto) akipokea taarifa za hali ya mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo.

Kiwanda cha uzalishaji mitungi ya oksijeni kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC. 

Baadhi ya mashine za uzalishaji wa gesi ya oksijeni inazotumika katika matibabu  ya wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC.


TUSHIRIKIANE KUPAMBANA DHIDI YA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA - MGANGA MKUU WA SERIKALI.

Na WAMJW- KILIMANJARO

MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa watoa huduma za Afya kushirikiana kwa pamoja kwa kutoa elimu, katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ambukiza yanayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwemo ulaji usiofaa, matumizi ya vileo na kutofanya mazoezi.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Makubi ametoa rai hiyo wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa wananchi.

Prof. Makubi amesema kuwa, ni muhimu watoa huduma za afya kuungana kwa pamoja kushirikiana kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyo ambukiza (NCD), kwa njia ya kuwafuata wagonjwa katika maeneo yao, jambo ambalo litasaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa katika hospitali za Rufaa nchini.

"Mshirikiane kwa pamoja kutoa Elimu ya ufahamu, na kupima angalau mara 2 kwa mwaka juu ya  magonjwa yasiyo ambukiza  kupitia njia ya kuwafuata wateja katika maeneo yao na kuwafanyia upimaji (outreach program)" alisema Prof. Makubi.

Hata hivyo, Prof. Makubi ametoa rai kwa watoa huduma za afya kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati kwa wagonjwa ili kuepusha msongamano unaoweza sababisha mlipuko wa magonjwa mengine katika hospitali na kupunguza usumbufu kwa wagonjwa.

Aidha, Prof. Makubi ameridhishwa kwa kiasi kikubwa hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo, huku akiwataka kuongeza jitihada ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kupunguza malalamiko yanayoweza kuepukika kwa urahisi.

"Mimi kwa KCMC, sipati malalamiko mengi sana, simamìeni katika ubora huo, na mhakikishe mnaongeza Juhudi zaidi, na kwa hilo nawapongèza sana sana" alisema Prof. Abel Makubi.

Hata hivyo, Prof. Makubi amewapongeza watumishi wa Hospitali ya KCMC wakiongozwa na Mkurugenzi wao Prof. Gileard Masenga kwa kuanzisha mradi wa uzalishaji wa gesi ya oksijeni, jambo linalosaidia kuongeza mapato na kuokoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kingetumika kununua mitungi ya gesi, na pesa hizo kuelekezwa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Naye, Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Maghembe amewataka watumishi kutobweteka, katika kuwahudumia wananchi, licha ya kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa na uongozi kwa kushirikiana na Mkoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uhakika ubora huduma Wizara ya Afya Dkt. Eliakim Eliud amewataka watoa huduma kuhakikisha wanafuata miongozo ya kujikinga ya utoaji huduma (IPC guidelines) wakati wa kuhudumia wagonjwa ili kujikinga wao na wagonjwa wanaowahudumia.

Mwisho.

Ijumaa, 14 Februari 2020

HOSPITALI YA WILAYA MWANGA YAPEWA WIKI MBILI KUJA NA MKAKATI WA UPATIKANAJI WA VIPIMO MUHIMU VYA AFYA

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson (kulia) mara baada ya kuwasili katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mwanga.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kulia) akifafanua jambo kwa watumishi wa Wilaya ya Mwanga (hawapo pichani) kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson.

Mbunge wa Jimbo la Mwanga Prof. Jumanne Maghembe akisema jambo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati wa Ziara ya Dkt. Ndugulile Wilayani Mwanga.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akionyesha alama ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika dawa zote ambazo zinatolewa Serikali kwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Prof. Jummane Maghembe.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua uwekaji wa kumbukumbu za taarifa za jotoridi la jokofu la dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua kadi ya bima ya afya ngazi ya jamii iliyoboreshwa kutoka kwa mgonjwa aliyefika hospitali ya Wilaya ya Mwanga kupata huduma za afya.

Na WAMJW – Mwanga, Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameutaka uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kuandaa mkakati madhubuti utakaowawezesha kuwa na vipimo muhimu vya afya.
Dkt Ndugulile ametoa agizo hilo alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kujionea hali ya utoaji huduma na kubaini kuwa hospitali hiyo haina vipimo vya damu, vipimo vya kemia pamoja vipimo vya CD4.
”Kwa miaka miwili sasa hakuna vipimo vya msingi katika hospitali hii, tunawakosesha huduma wananchi” amesema Dkt. Ndugulile
”Haiwezekani Hospitali kubwa ndani ya Wilaya kukosa vipimo vya msingi, haiwezekani mtu hapa sasa hivi anahitaji kipimo cha damu atoke hapa aende Hospitali ya Mawenzi Moshi kwa ajili ya vipimo” amesema Naibu Waziri Ndugulile.
Katika hatua za kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, Waziri Ndugulile ameushauri uongozi wa afya ndani ya Wilaya kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kununua vifaatiba hivyo ili wananchi waweze kupata huduma za vipimo ndani ya Wilaya ya Mwanga.
Aliendelea kushauri kuwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wao wanatoa mkopo wa majengo na vifaa kwa taasisi za umma na binafsi, mnaweza kuwafikia NHIF na kujadili kuhusu suala hili.
”Huko kwingine wanazitumia hizo fursa, kaeni na watu wa NHIF, Meneja wa NHIF kaa na viongozi wa Hospitali hii ikiwezekana mkubaliane hivyo vitu vipatikane kwa haraka” ameshauri Dkt. Ndugulile.
”Naamini mna wadau wa maendeleo ambao mnashirikiana nao katika mambo mbalimbali, timu ya afya ndani ya mkoa, wilaya pamoja na hospitali nawaombeni sana tuwe tunaomba vitu ambavyo vina manufaa kwa wananchi” amesisitiza Dkt. Ndugulile.
Awali akitoa salamu za wananchi wa Wilaya ya Mwanga, Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe amesema kuwa changamoto ya kijiografia ndani ya Wilaya hiyo inachangia wananchi kukimbilia hospitali za Wilaya jirani ili kuweza kupata huduma.
”Wilaya yetu hii ina upande wa mlimani na huku tambarare, wananchi wengi walio huku tambarare wanaona ni bora kwenda Moshi kwa ajili ya matibabu kuliko kwenda juu mlimani iliko Hospitali” amesema Prof. Maghembe.
Hata hivyo Prof. Maghembe amesema kuwa tayari ndani ya Wilaya wameshaanza taratibu za kujenga Hospitali nyingine eneo la chini (tambarare) ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waweze kupata huduma za afya ndani ya Wilaya ya Mwanga.

Jumapili, 26 Januari 2020

KINU CHA KUFUA OKSIJENI KCMC KUWA MSAADA KWA WENYE MATATIZO YA UZAZI

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Dkt. Sarah Urasa akizungumza katika Mkutano wa Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake katika kampeni ya "TumeboreshaAfya".

Bibi Catherine Mushi akiendesha  kinu cha kuzalisha hewa safi (Oxygen plant) katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.

 Mtaalam wa kutengeneza baskeli za magurudumu matatu(wheelchair) Bw. Samson Shirima akiwa katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa hizo katika hospitali ya rufaa ya KCMC.

Madaktari pamoja na wauguzi wakiwahudumia watoto  njiti katika wodi maalum ya watoto hao   KCMC.

Mtaalam kutoka Idara ya ngozi Bw. Maghembe Juma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kilimanjaro KCMC akitengeneza dawa na mafuta maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika Hospitali hiyo.

Grace Manyika akiweka alama za ukomo wa matumizi ya mafuta maalum kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) katika kiwanda hicho  kilichopo hospitali ya KCMC, Kilimanjaro.

Mtambo wa kinu cha kisasa cha kuzalisha hewa safi (oxygen plant)wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku ambao upo katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC.

KCMC



KINU CHA KUFUA OKSIJENI KCMC KUWA MSAADA KWA WENYE MATATIZO YA UZAZI

Na Mwandishi wetu, KILIMANJARO.

IMEELEZWA kuwa uwepo wa kinu kipya na cha kisasa chenye uwezo wa kufua hewa ikiwemo hewa safi ya Oxygen na ile ya  Naitrojeni kitakuwa msaada kwa wenye tatizo la uzazi nchini.

Akizungumzia hospitalini hapo ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya Tumeboresha sekta ya Afya yenye lengo la kuonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uwamu ya tano ndani ya Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Kaimu Mkurugenzi wa KCMC Dkt. Sarah Urasa alisema:

"Uhifadhi wa mbegu za kiume  na kike upo mbioni kuanza hapo baadae. Hatua hiyo kwani tayari tumeanzisha klininiki maalumu kwa ajili ya watu wenye matatizo ya uzazi ambayo tunaonana na wagonjwa kwa wiki mara moja  ambapo huwahudumia watu 10 mpaka 12." Alisema.

Mbali na kazi hiyo  kinu hicho kinauwezo wa kufua hewa ya Oksijeni ambayo kwa kiwango kikubwa hutumika kuwasaidia watu wenye matatizo ya kupumua ambapo kwa siku mitungi 400 hufuliwa katika kinu hicho.

Dkt. Sarah Urasa aliongeza kuwa: "Hii ni hospitali ya kwanza kuwa na kinu ya kufua hewa ya oksijeni na Nitrogen  hapa nchini.

Hewa ya Oksijeni pia inatumika kwa wale wagonjwa wanaopewa dawa za usingizi kwaajili ya upasuaji, hewa ya nitrogen inatumika kuhifadhi sampuli kutoka kwa wagonjwa,tiba kwa magonjwa ya ngozi vile vile hutumika kukata matokeo kwenye ngozi au kwenye viungo vya uzazi" alisema.
 
Huduma hiyo ambayo imeanza mwaka huu Dkt. Sarah alisema ununuzi wa mitungi ya gesi ya oksijeni pekee ulikuwa ukiwagharimu takribani milioni tatu kwa wiki huku gharama za usafirishaji ikiwa haijajumuishwa hatua ambayo imeokoa gaharama za uendeshaji hospitalini hapo.

Dkt.Sarah alieleza kuwa kwa kadiri uzalishaji unavyoongezeka katika kinu hicho wataanza kutumia mfumo wa kuunganisha gesi moja kwa moja hadi katika kitanda cha mgonjwa.

"Tumeona uharibifu mkubwa unaotokana namitungi hii ya gesi sakafu yetu imekuwa ikiharibika kutokana na uzito wa mitungi yenyewe kwahiyo mfumo tutakapkuja kuutumia utakuwa bora zaidi tofauti na sasa "alisema.

Mafanikio mengine aliyoyataja Dk.Sarah alisema katika utawala wa Rais Dk.John Magufuli wamefanikiwa kuanza kutengeneza maji tiba 'dripu' kwaajili ya kuwasaidia wagonjwa ndani na nje ya hospitali.

"Hii inetusaidia kwa kiwango kikubwa hata hospitali zingine zimekuwa zikifika hapa kwaajili ua kujifunza namna ya kutengeneza maji tiba "alisema.

Pia alisema KCMC ndio kituo pekee inayotambulika kimaitafa kutoa mafunzo ya magonjwa ya ngozi na zinaa kwa nchi zote za Afrika Mashariki.

"Kituo hiki ndio kinachozalisha mafuta ya ngozi kwaajili ya watu wenye ualbino na tayari tumeingia makubaliano na Bohari kuu ya Dawa MSD kwaajili ya kusambaza dawa na tayari tumefikia mikoa 25 kwa kutumia mfumo wetu wa usambazaji na sasa MSD watatuongezea nguvu ili kusambazwa nchi mzima "alisema

Kwa upabde wake,  Mhandisi KCMC Dustan Kanza alisema mgonjwa mmoja hutumia mtungi mmoja lengo kuepukana na maambukizi.

Alisema katika kinu hicho kwa saa 24 inauwezo wa kuzalisha mitungi 400 na mpaka sasa tayari zaidi ya mitungi 600 imezalishwa tangu kuanza kufanya kazi kwa kinu hicho januari mwaka huu.

Mwisho.




Ijumaa, 23 Novemba 2018

DKT. NDUGULILE – “SEKTA YA AFYA NCHINI INAKUWA KWA KASI”

- Hakuna maoni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akisoma nyaraka za matibabu za Bi. Mary Nyange (kulia) anayepatiwa huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akihojiana na Bw. Longini Mtalo, Mteknolojia kutoka kituo cha utengenezaji wa viungo bandia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC  huku akiwa ameshika sampuli ya kiungo bandia kilichotengenezwa na kituo hicho.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akikagua benki ya damu zilizopo katika jokofu Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akionyesha mafuta maalum kwa ajili ya kuwakinga wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya miale ya jua yanayotengenezwa na  kitengo cha Kilimanjaro Sunscreen Production kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akihojiana na  Bw. Prosper Kaaya, Mteknolojia kutoka kituo cha utengenezaji wa viungo bandia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC  huku akiwa ameshika kiungo bandia kilichotengenezwa na kituo hicho.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (aliyesimama) akisema jambo wakati wa kikao na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC (hawapo pichani) aliye upande kulia ni Mganga Mkuu Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Best Magoma upande wa kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskasini KCMC Dkt. Gileard Masenga.

Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC wakisiliza jambo wakati wa kikao kazi na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) aliyetembelea hospitali hiyo Novemba 22, 2018.


NA WAMJW- KILIMANJARO

“Sekta ya afya inakua kwa kasi huku huduma muhimu za afya kwa sasa zikiwa zinapatikana hapa hapa nchini”

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile alipokua akizungumza na watumishi wa Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro jana Novemba 22, 2018.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Sekta ya Afya imepewa kipaumbele cha hali ya juu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu mageuzi makubwa ndani ya sekta ya afya yameanza kuonekana huku huduma za matibabu ya kibingwa yakiwa zikipatikana hapa hapa nchini.

“Tunasimama hapa kifua mbele tukiona mabadiliko katika hali ya upatikanaji wa dawa kuimarika zaidi, bajeti ya dawa imeongezeka toka Shilingi Bilioni 30 mpaka Shilingi Bilioni 270 yaani mara tisa zaidi ndani ya miaka mitatu” alisema Mhe.Naibu Waziri na kuendelea “Tumeboresha vituo vya afya takribani 300, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa na Vituo 8 vilivyoboreshwa vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 na kwa mwaka huu 2018 Serikali imeanza kujenga Hospitali za Wilaya 67 nchini”

Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali imetenga Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya Hospitali mpya za Rufaa za Mikoa ili  ziweze kutoa huduma za kibingwa, kupunguza msongamano wa wagonjwa na ucheleweshwaji wa huduma katika Hospitali za rufaa za kanda.

Naibu Waziri huyo Aliendelea kusema  kuwa fedha hizo Shilingi Bilioni 30 zitaelekezwa katika maeneo makuu matano ambayo aliyataja kuwa ni kuhakikisha kila Hospitali ya Mkoa ina Kitengo cha dharura, chumba cha upasuaji, kitengo cha uangalizi wa wagonjwa mahututi pamoja na kitengo cha mama na mtoto.

"Hospitali hii inatakiwa kuhudumia wagonjwa waliopata rufaa toka hospitali za mikoa ya jirani waje huku kupatiwa huduma za matibabu na sio wagonjwa wa malaria na mafua alisema Dkt. Ndugulile.

Katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwenye hospitali za rufaa za mikoa, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeweka maeneo muhimu katika mafunzo kwa watumishi wa kada ya afya huku akitaja watumishi wenye kuhitajika zaidi kwa sasa kuwa ni madaktari wa magonjwa ya ndani, watoto, wakina mama, upasuaji, mifupa pamoja na madaktari wa usingizi.

Kuhusu upatikanaji wa huduma za kibingwa, Dkt.Ndugulile alisema  mafanikio  kuona huduma hizo zikiwa zinapatikana hapa nchini tofauti na zamani  “Tunafanya upandikizaji wa figo pamoja na upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa wa watoto huduma ambazo zilikuwa ni za kufikirika ndani ya miaka mitatu sasa zinapatikana hapa nchini” alisema Dkt. Ndugulile.

Awali akitoa taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Dkt. Gileard Masenga aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Hospitali hiyo "Licha ya kumilikiwa na Taasisi ya kidini lakini Serikali imeendelea kutupatia wataalam, misamaha ya kodi za malighali zinazoingizwa nchini ambazo hutumika kutengeneza mafuta ya kuwakinga wenye ulemavu wa ngozi dhidi ya jua.

Aidha, Dkt.Masenga alisema hospitali yake imetengewa  Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya dawa za Saratani huku fedha kiasi cha Shilingi Milioni 250 tayari  zimeshapelekwa Bohari ya dawa kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.

 Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani hapa kwa ziara  ya kikazi  inayolenga kukagua shughuli za huduma ya Afya,Maendeleo ya Jamii pamoja na kuongea na watumishi wa sekta  hizo.

MWISHO.