Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Taarifa kwa Vyombo vya Habari. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Taarifa kwa Vyombo vya Habari. Onyesha machapisho yote

Jumatano, 20 Mei 2020

MSIBWETEKE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA CORONA

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akipokea msaada wa barakoa 17,500 na vipukusi lita 700 kutoka kwa Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace Tanzania Bi. Sukyung Kim leo Jijini Dar es Salaam.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akiwa ameshika box la barakoa 17,500 na vipukusi lita 700, kulia ni, Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace Tanzania Bi. Sukyung Kim.



MSIBWETEKE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA CORONA.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DSM

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ametoa wito kwa wananchi, hususan Jijini Dar es Salaam kutobwete na kuwataka kuendelea kuchukua hatua za tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika kipindi hiki.

Dkt. Rashid Mfaume ametoa wito huo leo, wakati akipokea msaada wa barakoa 17,500 sawa na maboksi 350, na vipukusi (sanitizers) lita 700 ambayo ni sawa na madumu 140 yenye ujazo wa lita 5 kutoka kwa Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace linalohusika na mradi wa mama na mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Licha ya elimu tunayoendelea kutoa juu ya namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, tunawahamasisha wananchi wasibweteke katika kipindi hiki, ili kuumaliza kabisa ugonjwa huu katika nchi yetu, na hili linawezekana kabisa" alisema

Dkt. Rashid Mfaume aliendelea kusema kuwa, Msaada huo utaelekezwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya vya Sinza Hospitali, Vijibweni Hospitali, Rangi Tatu Hospitali, Kituo cha afya Kimara, Kituo cha afya Tandale, Kituo cha afya Mbezi, Kituo cha afya Round table, Kituo cha afya Kimbiji, Kituo cha afya Buguruni, Tegeta Dispensari, Bunju Dispensari.

Aidha, amefafanua kuwa, kumekuwa na ongezeko la wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, hususan katika Jiji la Dar es Salaam baada ya Serikali kuziteua baadhi ya Hospitali kuwa vituo vya kutolea huduma za Corona, hivyo kuelekezwa msaada huo katika vituo vya Afya kutasaidia mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya Corona.

"Sasa hivi tumeona wagonjwa wameongezeka sana katika vituo vya kutolea huduma za Afya, mfano katika Mkoa wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuitangaza Hospitali ya Amana kuwa kituo cha kuhudumia wagonjwa wa COVID-19, wagonjwa wengi wamekuwa wakienda katika vituo vingine, hivo msaada huu utasaidia sana kupambana dhidi ya maambukizi mapya" alisema.

Mbali na hayo, Dkt. Mfaume amewataka Wadau wengine kutoka Mashirika mbali mbali nchini kuendelea kuisaidia Serikali vifaa kinga vya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona ili kuvisaidia vituo vya kutolea huduma za Afya vyiweze kujitosheleza mahitaji hayo, hasa kutokana na vituo vya Afya kuwa sehemu inayopokea watu tofauti kwa wingi.

Hata hivyo, Dkt. Mfaume amewatoa wasi wasi Wananchi kuwa, hali ya Afya katika Mkoa wa Dar es Salaam ni shwari, huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua tahadhari za karibu dhidi ya maambukizi hayo ili kuumaliza kabisa ugonjwa huo nchini.

Nae, Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Medipeace Tanzania Bi. Sukyung Kim amesema kuwa, Medipeace inayofadhiliwa na KOICA imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Dar-es-salaam.

Aliendelea kusema kuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona, Shirika hilo linaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo kwa kutoa vifaa kinga ambavyo vitasaidia kwa Watoa huduma za Afya na wagonjwa wataofika kupata matibabu katika vituo hivyo.

Mwisho.

Jumatano, 13 Mei 2020

WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akionesha moja ya kifaa kinga dhidi ya maambukizi ya Corona wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini kwenye mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiteta jambo na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini.

Baadhi ya Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini wakitizama vazi la kujikinga dhidi ya Corona wakati wa mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini ulioongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa.

Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini wakiendelea na mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini ulioongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa.


WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUZALISHA VIFAA KINGA KUKABILIANA NA CORONA

Na.WAMJW- Dar es Salaam

Wamiliki wa viwanda vya Dawa, Vifaa na vifaa tiba nchini wametakiwa kuanza kuzalisha vifaa kinga kuweza kukabiliana na janga la Corona nchini ili kuondokana na changamoto ya ucheleweshaji wa kupata vifaa kinga toka nje ya nchi pamoja na kupunguza gharama.

Wito huo umetolewa leo jijini hapa  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na Umoja wa Wazalishaji Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba (TPMA) nchini kwenye mkutano wa kuangalia jinsi gani wanaweza kuzalisha vifaa kinga kutoka wazalishaji wa ndani hapa nchini.

“Tukizalisha hapa nchini tutaokoa rasiliamali fedha nyingi, muda pia tutazalisha ajira na kuwa na uhakika wa   ubora na usalama unaohitajika kupitia mamlaka zetu za ndani kwa urahisi”. Alisema Waziri Ummy.

Waziri amesema kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa kinga , hivyo wale wote wanaozalisha vifaa kinga wanatakiwa kuongeza uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya soko nchini na hata kuweza kuuza nchi za jirani.

Aidha, amesema  Wizara inahitaji kuipa nguvu  huduma salama kwenye vituo vya kutolea huduma za afya  vya serikali na visivyo vya Serikali kwa watumishi wa afya kuzingatia miongozo ya kukinga na kudhibiti maambukizi angalau kuvaa barakoa,glove na eproni hivyo amewasisitiza kuzalishaji vifaa vyenye  viwango vyenye  ubora ili kukidhi soko la ndani nan chi za jirani.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amewapongeza wamiliki wa viwanda hivyo kwa kubuni na kugundua teknolojia na uzalishaji wa  vifaa kinga kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

“Kuanzisha viwanda ni sehemu ya ulinzi wa nchi,hivyo kuwa na viwanda vyetu nchini hususani wakati wa shida imesaidia upatikanaji wa baadhi za vifaa kinga kwa bei nafuu”.Alisema Waziri Bashungwa.

Amesema katika kikao hicho wamekubalia kujipanga vizuri katika uzalishaji wa vifaa kinga na hivyo wamewataka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kujikita katika kuzalisha barakoa aina ya N95 na glove kutokana na kwamba viwanda vya namna hii havipo nchini.

Pia Waziri Bashungwa ameitaka TMDA kushirikia na wizara ya viwanda kuisaidia NDC kuweza  kufanya kiwanda hicho kuanza kuzalisha kwa wakati na hivyo kusaidia watumishi wa afya walio mstari wa mbele kutoa huduma bila hofu.

Kwa upande wa MSD, Waziri Bashungwa ameitaka  kununua vifaa kinga vinavyozalishwa na viwanda vya ndani ambavyo vimekidhi viwango na vimesajiliwa na TMDA badala ya kutumia fedha iliyotengwa na Serikali kununua vifaa hivyo nje ya nchi.

Waziri Bashungwa ameahidi kukitembelea kiwanda cha Msagala Investment kilichopo Bagamoyo ambacho kinatarajia kuanza kuzalisha malighafi za utengenezaji wa barakoa kutokana na pamba zinazolimwa nchini.

 -Mwisho-

Jumanne, 12 Mei 2020

SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

- Hakuna maoni
Mfanyabiashara wa duka la dawa baridi, eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam akisafisha kitasa na kioo cha duka lake ikiwa ni sehemu ya maeneo hatarishi kupata virusi vya Corona kutoka na kushikwa mara kwa mara na wateja.

 Dereva boda boda eneo la Bagamoyo mjini. Bw. Octavian Leonard Nyoni akisafisha mikono yake kwa maji safi yanayotiririka na sabuni ikiwa ni sehemu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

 Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji kwa wananchi wa eneo la kituo cha mabasi cha Bagamoyo Mkoa wa Pwani, jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akitoa maelekezo namna ya kukaa mita moja au zaidi baina ya mtu mmoja na mwingine katika eneo la kituo cha mabasi ya Bagamoyo, ikiwa ni moja ya njia ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Abiria katika kituo cha mabasi cha Kisarawe Mkoa wa Pwani wakisafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka na wengine kwa kutumia sanitizer kabla ya kupanda basi na kuanza safari, wamefanya hivo ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), akimkabidhi vipeperushi vya elimu juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa Afisa Afya wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima.

Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.


SAFISHA VITASA KATIKA MAENEO YA BIASHARA NA MAKAZI YETU

Na WAMJW- PWANI

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kusafisha vitasa na maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara katika maeneo ya shughuli za kila siku na makazi yetu.

Ndg. Anyitike ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Kisarawe na Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo ya biashara na makazi.

"Tuhakikishe tunasafisha maeneo yote tunayoyashika mara kwa mara kwa maji yenye sabuni, sanitizer au spirit, futa maeneo yote yanayoshikwa mara kwa mara, lakini kumbuka kufuta sehemu za vitasa vya mlango na meza " alisema

Pia, alisisitiza kuwa, ni muhimu kujenga tabia ya kufuta katika maeneo yote ambayo watu wanapendelea kukaa kama vile maeneo ya viti, meza na vioo katika maeneo ya biashara bila kusahau milango.

Aidha, Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa rai kwa wananchi hususan vinyozi katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanavaa Barakoa (mask) pindi wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi, ili kuvunja mnyororo wa maambukizi Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine endapo utakuwepo.

"Unapoenda saluni usikubali kinyozi yoyote akunyoe nywele kama hajavaa Barakoa hali itayosaidia kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona katika maeneo ya kazi na kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi hivyo" alisema.

Nae, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, ameendelea kuwakumbusha wazazi na walezi, kuhakikisha wanawalinda Watoto dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwapa elimu, na kuhakikisha hawazululi hovyo mtaani, hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa ili kuepusha misongamano inayoweza sababisha kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.

"Tuhakikishe Watoto wanakaa nyumbani, Watoto wasiende kuzulula hovyo, ni rahisi Watoto kupata maambukizi ya Corona kwasababu ya ufahamu na uelewa wao juu ya madhara ya ugonjwa huu wa Corona " alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amewaasa wafanyabiashara wa Barakoa kutoruhusu wateja kujaribu barakoa na kuzirudisha, hali inaweka wanunuzi wengine katika hatari yakupata maambukizi ya virusi vya Corona.

" kwa wauzaji wa Barakoa, chonde chonde usiruhusu mtu ajaribu Barakoa alafu akaiacha, hii itasaidia kuvunja mnyororo wa maambukizi ya virusi vya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine endapo atatokea mtu mwenye maambukizi" alisema.

Timu ya Wizara ya Afya na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR kupitia kampeni ya Mikono Safi, Tanzania Salama imeendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona katika, Wilaya ya Bagamoyo, Wilaya ya Kisarawe na Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Mwisho.

Jumatatu, 4 Mei 2020

WAFANYA KAZI WA SALUNI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA MAAMBUKIZI YA CORONA.

- Hakuna maoni
Kinyozi katika eneo la Mgeninani Kijichi Jijini Dar es Salaam akiwa amevaa Barakoa kama sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkazi wa eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam akisafisha mikono yake kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mfanyabiashara katika Soko la Shangwe Kigamboni Jijini Dar es Salaam akiendelea kumhudumia mteja wake huku akiwa amevaa Barakoa ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona

Dereva boda boda katika eneo la Geza ulole Kigamboni wakipata elimu ya maambukizi ya virusi vya Corona kutoka katika timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya.

Eneo la Mbagala Jijini Dar es salaam ambapo timu kutoka Wizara ya Afya ilipita kutoa elimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.



WAFANYA KAZI WA SALUNI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA MAAMBUKIZI YA CORONA.

Na WAMJW - DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa wito kwa Wafanya kazi katika maeneo ya saluni kuchukua tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Kwa wale ambao wanasafisha nywele, kucha, wanafanya masaji, wanaosuka nywele, mchukue tahadhari kwasababu mpo katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa lakini vile vile kuambukiza watu wengine maambukizi ya virusi vya Corona" alisema

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuwakumbusha wafanya kazi wote katika maeneo ya saluni kuhakikisha wanaepuka msongamano pindi wanapokuwa katika majukumu yao, huku akisisitiza ni muhimu kwa kinyozi kuvaa Barakoa pindi ananyoa.

"Tunawakumbusha tena, kwa upendo kabisa, Tunawakumbusha muepuke msongamano ndani, awepo mtu anaenyoa na anaenyolewa na yule ambae ananyoa ahakikishe muda wote amevaa Barakoa, tunawaambia hivi kwasababu tunawapenda" alisema.

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.

Nae, Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza kuwa ili kupambana na ugonjwa huu watu wasichoke kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya Corona.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho

Alhamisi, 30 Aprili 2020

SAFARI ZA KWENDA KUWATEMBELEA NDUGU VIJIJINI ZISUBIRI CORONA IISHE - DKT. SUBI

- Hakuna maoni
Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akieleza jambo wakati akiongea na Waandishi wa habari katika juu ya mwenendo wa kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkurugenzi msaidizi wa Afya mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khalid Massa akimkaribisha Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi.

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akieleza jambo, mbele ya Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha) wakati akiongea na Waandishi wa habari katika juu ya mwenendo wa kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akifuatilia taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha).

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) akifuatilia mjadala kutoka kwa Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha).

Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akinawa  mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akiwa na timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya na taasisi isiyo yakiserikali ya Project CLEAR juu ya elimu ya kujikinga  dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.



SAFARI ZA KWENDA KUWATEMBELEA NDUGU VIJIJINI ZISUBIRI CORONA IISHE - DKT. SUBI

Na WAMJW- DSM

Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi ametoa wito kwa wananchi kutosafiri kwenda vijijini kwa lengo la kuwasalimia ndugu katika kipindi hiki ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona kusambaa zaidi nchini.

Wito huo ameutoa leo, wakati akiongea na Waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam juu ya mwenendo wa kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Kwa wanaotaka kwenda kuwatembelea Wazee kijijini, wasubiri Corona iishe, kwasababu tunaona watu watatoka kwenye miji ambayo inamaambukizi wanaenda vijijini kuwatembelea wazazi ambao umri wao umeenda, inawezekana wana magonjwa ya uzeeni, kunauwezekano mkubwa wakuwaambukiza huko" alisema.

Aliendelea kusisitiza kuwa, katika maeneo yote yenye msongamano hususan maeneo  ya biashara na huduma za Afya, waweke utaratibu mzuri, utaosaidia wateja kukaa umbali wa mita moja au zaidi pindi wanaposubiri kupata huduma, hali itayosaidia kukata mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

"Maeneo ya kutoa huduma mbali mbali, ikiwemo Hospitali na vituo vya Afya, waweke utaratibu mzuri, watu wanaokuja kupata huduma wakae katika utaratibu wa mita moja au zaidi ili watu hawa wasiweze kuambukizana maradhi, lengo likiwa kukata mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine " alisema

Aliendelea kusema, ni muhimu uvaaji wa Barakoa uzingatiwe katika ngazi zote, hasa katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kuzichoma moto Barakoa zilizotumika ili kuepusha usambaaji wa magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza.

"Tunasisitiza uvaaji wa Barakoa, hasa unapokuwa kwenye mkusanyiko wa watu, lakini barakoa sio kitu salama baada ya kumaliza kukitumia, kinakuwa kichafu na maambukizi, kwa mantiki hiyo, hakikisha unaitupa sehemu salama na unachoma moto ili mtu mwingine asiweze kuikokota na kuitumia tena " alisema

Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, bado elimu ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka haijaeleleweka vizuri, hivyo kuitaka timu ya hamasa kuongeza nguvu katika hatua zote tano za unawaji mikono ili elimu hiyo isaidie katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Tunaposema kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni tunamaana kwamba, unapokwenda kunawa hakikisha sabuni imekolea vizuri kwenye kiganja cha mikono, hakikisha umesugua vizuri, povu la sabuni limeshika vizuri, na hakikisha umenawa vizuri mbele, nyuma, kwenye vidole na kila eneo la mikono vizuri kwa sekunde zisizopungua 20"alisema

Akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi wa kampeni ya "mikono safi, Tanzania salama," Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ameweka wazi kuwa, mpaka sasa timu hiyo ya uhamasishaji imeshatembelea jumla ya maeneo 145 kati ya 213 yaliopangwa yametembelewa ikiwa ni sawa na asilimia 68.

Mbali na hayo amesema kuwa, licha ya kutoa elimu ya tahadhari, kikosi cha uhamasishaji kimekuwa kikitoa zawadi kwa taasisi na watu ambao wanazingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara, vikiwemo vitakasa mikono (Sanitizer), viang'azi (Reflectors) na khanga za Kampeni.


Mwisho.

Jumanne, 28 Aprili 2020

TEKETEZA/HARIBU BARAKOA YAKO VIZURI KABLA YAKUITUPA/ BAADA YA KUMALIZA KUTUMIA.

- Hakuna maoni
Barakoa (mask) iliyotupwa baada ya matumizi, katika maeneo ambayo sio rasmi, hali inayoweza sababisha kusambaa kwa maambukizi.

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, akitoa elimu kwa wafanyabiashara katika kituo cha daladala cha feli Jijini Dar es Salaam.

Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji jinsi  ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika eneo la soko la Mabibo Jijini Dar es Salaam.

Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na utoaji  elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika kituo  cha daladala cha feli Jijini Dar es Salaam.


TEKETEZA/HARIBU BARAKOA YAKO VIZURI KABLA YAKUITUPA/ BAADA YA KUMALIZA KUTUMIA.

Na WAMJW- DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa wito kwa wananchi kuteketeza Barakoa zao vizuri baada ya kumaliza matumizi yake kisha kuitupa sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Wito huo, ameutoa Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Wale ambao mmevaa Barakoa (mask) zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika (disposable mask) , ukumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiweze kuiokota na kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko jambo litalosaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa Corona" alisema.

Alisema, katika baadhi ya nchi imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa Corona anaweza kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya watu, hivyo kutoa wito juu ya kuchukua tahadhari kwa hali ya juu.

"Kwa baadhi ya nchi zilizopata maambukizi, inasemekana kuwa, mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivi anauwezo wa kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja" alisema.

Aidha, alisema kuwa, kwa wale ambao wanatumia Barakoa za kitambaa, kuhakikisha wanabadirisha mask hizo kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kabla ya kuivaa zifuliwe kwa maji na sabuni kisha ipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.

"Kwa wale ambao mnavaa Barakoa (mask) za kitambaa basi mkumbuke kuwa, mask hiyo inatakiwa ivuliwe kila baada ya masaa manne mpaka sita, na hakikisha kuwa, unaifua kwa maji na sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa, usivae barakoa (mask) ambazo ni chafu" alisema

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, alisisitiza kuwa, wazazi watoe elimu kwa watoto kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuhakikisha wananawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, huku akisisitiza waepuke kuzulula mtaani kuepusha kuokota Barakoa zilizotupwa hovyo bila utaratibu.

Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), amewakumbusha Watanzania kuepuka msongamano katika maeneo yote, huku akisisitiza kuwa, kama hakuna sababu yakutoka nje ni vema watulie majumbani.

Mwisho.

Jumapili, 26 Aprili 2020

TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA - ASP SWEBE

- Hakuna maoni
Mrakibu mwandamizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ASP Edith Swebe akieleza jambo mbele ya timu ya uhamasishaji wa elimu juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona katika kituo cha polisi Pangani Ilala.

Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji jinsi  ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa abilia na bodaboda katika kituo cha daladala cha Mbezi kwa Msuguli.

Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi akiongea na madereva boda boda wa kituo cha Mbezi mwisho Jijini Dar es Salaam juu ya tahadhari za kuchukua ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Flavour) Banana Zolo akinawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, ishara ya kuunga mkono kampeni ya kusafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka kama moja ya nyenzo ya kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkazi wa Mbezi Mwisho Jijini dar es salaam aliyeweka uzio wa kamba kwenye duka lake kujitenganisha na mteja, inayosaidia kumzuia mteja kuingia dukani kabla ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka na kuzuia mteja asikae karibu nae wakati anamhudumia, ikiwa ni muitikio chanya kutoka Wizara ya Afya wa kukaa mita moja au zaidi baina ya mtu mmoja na mwingine na kusafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka kabla ya kupata huduma yoyote ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), pamoja na askari polisi kituo cha polisi Pangani Ilala wakinyoosha mikono, ishara ya kuunga mkono kampeni ya mikono safi, Tanzania salama inayohamasisha kunawa mikono kwa sabuni  na maji safi yanayotiririka.



TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA - ASP SWEBE

Na WAMJW- DSM

Mrakibu mwandamizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ASP Edith Swebe ametoa wito kwa wananchi, hususan Wana Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Ameyasema hayo wakati akiwa katika majukumu yake ya ukaguzi wa namna gani kituo cha Polisi Pangani kilichopo Ilala Jijini Dar es Salaam kimechukua hatua ya kukabiliana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

"Tunaendelea kukumbusha Wananchi wa hususan Wanaotoka Jijini Dar es Salaam kunawa mikono na kuchukua hatua zote za tahadhari zinazotakiwa, tunaendelea kusisitiza kila mmoja katika familia yake aendelee kuchukua hatua ambazo Wizara ya Afya inapendekeza" alisema

Kwa upande mwingine, ASP Swebe ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuja na kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" inayohamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, hali inayoonesha jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi.

"Kwanza nitoe shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa Kampeni inayoendelea ya "Mikono safi, Tanzania salama", hii inaonesha ni jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi" alisema.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kulisaidia Jeshi la polisi vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ikiwemo vitakasa mikono na Barakoa (mask).

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho

Jumapili, 19 Aprili 2020

TUACHE MZAHA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA CORONA

- Hakuna maoni
Wafanya biashara ndogo ndogo katika kituo cha mabasi Makumbusho wakipata mafunzo juu ya namna yakunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka wakati,   elimu ya kujikinga dhidi ya Corona ilipokuwa ikitolewa kituoni hapo.

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akiwaelekeza madereva bajaji namna ya kunawa  kwa kufuata taratibu za unawaji mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka kwa usahihi kulingana na miongozo ya Wizara.

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akielekeza  jambo wakati wa kampeni ya uhamasishaji kwa Jamii juu ya namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), akisisitiza jambo kwa wafanyabiashara katika eneo la Coco Beach Dar es salaam juu ya umuhimu wa kuchukua tahadhari wakati wote ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) akisisitiza kukaa umbali wa mita moja au zaidi ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona pindi watu wanapoongea au mtu anapopiga chafya au kukohoa.


TUACHE MZAHA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA CORONA

Na WAMJW- DSM

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg. Anyitike Mwakitalima ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kuacha mzaha na kufuata taratibu kutoka kwa Wataalamu wa Afya ili kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

Ameyasema hayo leo, wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona

"Watanzania tusifanye mzaha, huu ugonjwa sio wakufanyiwa mzaha, wenzetu wa nchi zilizoendelea pamoja na uchumi wao kuwa mkubwa na sayansi yao kubwa, lakini wamefika mahali wameshindwa, hizi tahadhari za msingi ambazo tunaelekeza ni muhimu kuzizingatia " alisema.

Alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya, inaendelea kutoa elimu ya Corona kwa jamii kupitia vyombo vya habari, lakini pia kuwafuata wananchi walipo ili kuwapa elimu hiyo na kujibu maswali yanayowatatiza, hali itayosaidia watu kufahamu njia zote za kujikinga na kuepuka kupata maambukizi ya virusi hivyo.

"Tunafahamu kwamba , bado suala la elimu halijaweza kufika kwa Jamii vyakutosha, kwahiyo tunatumia njia mbali mbali, tunatumia vyombo vya habari kama tv na redio, lakini tumeona tunakila sababu yakushuka na kwenda ambako Jamii hipo ili tuweze kuzungumza nao, na kujibu maswali ya msingi yanayowatatiza" alisema.

Aidha, alisema kuwa, kwa sehemu kubwa Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanachukua tahadhari, kwa kuweka vifaa vya kunawia mikono na sabuni, na kusafisha mikono ya abiria kabla yakupenda usafiri.

"Kwa sehemu kubwa tumeona wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanachukua tahadhari, ikiwemo kutengeneza jiki kwaajili yakutakasa chombo chake cha usafiri, lakini katika sehemu za biashara watu wameweka vyombo vya kunawia mikono na wanaelekezwa kunawa kabla ya kufanya manunuzi" alisema

Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amewaasa wananchi kunawa mikono mara kwa mara kwa kufuata hatua tano muhimu, kama ifuatavyo moja ni kulowanisha mikono, pili kupakaa sabuni kwenye mikono ili kuua virusi vyote, tatu ni sugua mikono yako kwenye kucha, viganja, vidole na sehemu zote, nne ni kusuuza mikono kwa maji yanayotiririka, na hatua ya tano ni kufuta mikono kwa kitambaa safi.

Aliendelea kusisitiza kuwa, kulingana na miongozo kutoka kwa Wataalamu wa Afya, hairuhusiwi kufuta mikono kwenye nguo baada ya kunawa mikono kwenye hatua tano, kwani kufanya hivyo hupelekea kurudisha maambukizi mikononi endapo vitakuwepo katika nguo hizo.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho

Jumatano, 15 Aprili 2020

TUEPUKE MSONGAMANO KATIKA MAENEO YETU YA KAZI

- Hakuna maoni
 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela akisisitiza jambo wakati akiongea na wahamasishaji kutoka Wizara ya Afya, Shirika lisilo Lakiserikali la Project CLEAR na Mjomba Theatre Gallery katika ofisi zake Vywawa Mkoa wa Songwe. 

Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi, Wizara ya Afya Ndg. Anyitike Mwakitalima akieleza jambo kuhusu ugonjwa wa Corona mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela wakati walipoenda kukabidhi vifaa vya kunawa mikono na vitakasa mikono kwaajili ya Mkoa huo.

Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery akifafanua jambo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela (hayupo kwenye picha).

Waratibu wa kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" kutoka Wizara ya Afya Shirika lisilo Lakiserikali Project CLEAR na Mpoto Gallery wakifuatilia neno kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela juu ya namna Mkoa unavopambana na ugonjwa wa Corona. 

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela akinawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo kutoka Wizara ya Afya na washirika wake, pembeni yake ni Katibu tawala wa Mkoa huo.

Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Songwe akinawa mikono yake kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni moja ya njia ya kupambana dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Mwananchi wa Ichenjezya Vywawa Songwe akinawa mikono yake kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni moja ya njia ya kupambana dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery akikabidhi vitakasa mikono na vifaa vingine vya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi, Wizara ya Afya Ndg. Anyitike Mwakitalima.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwengela katika picha ya pamoja na Waratibu wa kampeni ya "Mikono safi, Tanzania salama" kutoka Wizara ya Afya Shirika lisilo Lakiserikali Project CLEAR na Mpoto Gallery baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo kwaajili ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona Mkoani Songwe.

Afisa kutoka makao makuu jeshi la polisi kitengo cha ushirikishaji Stafu Sajenti Valentino Ngowi akihamasisha wananchi katika kituo cha mabasi Vwawa juu ya umuhimu wa kukaa zaidi ya mita moja kati ya mtu mmoja hadi mwingine ikiwa ni moja ya njia ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona katika Mkoa wa Songwe.

Afisa kutoka makao makuu jeshi la polisi kitengo cha ushirikishaji Stafu Sajenti Valentino Ngowi akikagua moja ya daladala ili kujionea kama wanafuata maelekezo ya Serikali ya kuepuka msongamano ndani ya daladala (level sit) katika kituo cha mabasi Vwawa Mkoa wa Songwe.
 
Wafanyabiashara katika Soko la Ichenjezya Vwawa Songwe wakifuatilia Elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka timu ya uhamasishaji Wizara ya Afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, au kutumia vitakasa mikono (sanitizer) na kuepuka msongamano isiyo na ulazima. 



TUEPUKE MSONGAMANO KATIKA MAENEO YETU YA KAZI.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW-SONGWE

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Breg. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuepuka misongamano katika maeneo yote, ikiwa ni moja ya njia ya kupambana na ugonjwa wa Corona usisambae endapo utaingia Mkoani hapo.

Ameyasema hayo, wakati akipokea vifaa vya kunawia mikono pamoja na vitakasa mikono kutoka Wizara ya Afya na Shirika la Project CLEAR, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya uhamasishaji kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

“Serikali imetoa maagizo mbali mbali, ambayo sisi kama Serikali ya Mkoa tunayasimamia na kuhakikisha yanatekelezwa, ikiwemo kusisitiza kuepuka msongamano na mikutano isiyokuwa yalazima katika maeneo mbali mbali na hili linatekelezwa vizuri kabisa” alisema.

Mbali na hayo, amesema kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Corona yameleta madhara makubwa kwa maisha ya binadamu hasa katika upande wa kiuchumi, huku akisisitiza kuwa nchi nyingi duniani zimeathirika kutokana na janga hili la Corona.

“Ni kweli kabisa huu ugonjwa sasahivi, umeleta madhara makubwa kwa Maisha ya binadamu, lakini pia kiuchumi, nan chi nyingi zenye uwezo mkubwa kiuchumi na kiafya zimeahirika kutokana na janga hili”alisema.

Aidha, Mhe. Alisema kuwa, Serikali inaendelea kutoa elimu na tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa wananchi, hii inafuatia sababu kuwa, Mkoa wa Songwe upo mpakani mwa nchi za Malawi na nchi ya Zambia ambayo inapokea pia watu kutoka nchi ya DR Congo.

“Songwe ipo kwenye mlango, tusipotoa tahadhari ya kutosha kwa wananchi kuna hatari kubwa ya ugonjwa kuingia, Mkoa wa Songwe upo mpakani, tuna KM 135 tunapakana na Zambia, KM 45 tunapakana na Malawi, nchi zote hizo tayari zina maambukizi ya ugonjwa wa Homa kali ya mapafu, huku nchi ya DR Congo ikiongoza kuwa na wagonjwa wengi zaidi” alisema

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima amesema kuwa katika kupambana na ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya inakabidhi vifaa vya kunawa mikono (sanitizer) lita 150 , Dispensa 30 na vifaa maalum vya kunawia mikono Mkoa  wa Songwe na mikoa yote ya mipakani kama sehemu ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu.

Nae, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesema kuwa, vita dhidi ya ugonjwa huu ni vita inayohitaji ushirikiano na umoja baina ya watu wote katika jamii, huku akiweka wazi kuwa baadhi ya silaha za kupambana dhidi ya ugonjwa huu ni kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuepuka msongamano isiyo na ulazima.

“Tupo katika kipindi ambacho tunahitajiana sana, kila mtu kwa nafasi yake anamuhitaji mwingine, kwahiyo tushirikiane kwa pamoja tunaweza kukabiliana na ugonjwa huu, janga hili haliitaji vifaru, janga hili haliitaji jeshi la anga, janga hili linatuhitaji sisi na utayari wet utu, na nguvu pekee tulionayo ni kunawa mikono, na kuepuka misongamano isiyo yalazima, na utamaduni huu uwe endelevu”, alisema

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Mkoa wa Songwe, kisha kuelekea Mkoa wa Rukwa.

MWISHO.