Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumanne, 31 Oktoba 2017

- Hakuna maoni


Naibu Waziri Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile akiwasilisha taarifa ya utendaji wa shughuli za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania(TFNC) mbele ya  Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamiii inayoongozwa na Mwenyekiti wake Peter Serukamba(wa kwanza kulia) leo mjini Dodoma,ambapo imeonekana tatizo la ulaji wa chakula bora kwa Watanzania bado ni tatizo kubwa.




Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt.Vicent Assey akijibu maswali ya wajumbe wa kamati hiyo ambapo ilionekana licha ya uzalishaji chumvi kwa wingi bado kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto bado ipo chini kwa asilimia 30 kwenye Mikoa ya Simiyu,Mtwara na Lindi.wakati kiwango cha mahitaji ya mwili ni asilimia 61 kwa takwimu za mwaka 2015/2016 hivyo kiwango hicho kimepanda kutoka asilimia 47 cha mwaka 2010.


Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamiii wakifuatilia kwa umakini uwasilishaji wa taarifa kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Faustine Ndugulile(Hayupo kwenye picha) leo jijini Dodoma.




















LISHE BORA KWA WATANZANIA BADO NI TATIZO, ASEMA MH. PETER SERUKAMBA

- Hakuna maoni


Na.WAMJW.Dodoma

Taasisi ya Chakula na lishe nchini imetakiwa kujikita katika kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kujua faida ya kula chakula bora na kuepukana na utapiamlo na udumavu
Hayo yamesemwa na Mwenyeketi wa kamati ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii  Mhe. Peter Serukamba wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji wa shughuli za taasisi hiyo mjini Dodoma leo.
Mhe.Serukamba alisema bila elimu kwa umma wananchi watakuwa wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu kwa kuwa hali ya udumavu ni mkubwa ,”watu wakiwa na chakula na lishe bora unakuwa na uhakika hutougua hovyo na kupoteza fedha nyingi kwa ajili ya matibabu,lakini wakijua wale mlo gani ambao ni sahihi hii itasaidia kutokomeza kabisa tatizo hili”
Aidha, alisema Tanzania haina tatizo la chakula ila hawafahamu ni mlo gani sahihi wanapaswa kula hivyo kwa kutoa zaidi elimu itakua ni kinga na itasaidia wananchi wasiugue
“Taasisi hii iboreshwe na mkishirikiana na Tamisemi,wakulima na wasafirishaji wa mazao kupitia maofisa maendeleo ya jamii mtawafikia wananchi wengi na hakutokuwa na vizazi vyenye udumavu na matatizo ya akili.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto dkt.Faustine Ndugulile alisema zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini vinachangiwa na matatizo ya lishe duni na  katika kipindi cha mwaka 199 hadi 2015/2016 vifo vya watoto vimepungua  kutoka 147 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1000.
“Serikali inafanya jitihada kubwa  katika kumjenga mtoto ili akue vizuri kimwili na kiakili kuanzia siku elfu moja za mwanzo za mtoto ambazo ni muhimu kwa makuzi ya mtoto”.
Hata hivyo dkt.Ndugulile alisema hali ya lishe nchini inaendelea kuimarika kutokana na kupungua kwa viwango vya utapiamlo nchini kati ya mwaka 1992 na 2015.
Alisema udumavu (urefu wa umri) umepungua kutoka asilimia 49.7 hadi 34.4 na mikoa inayoongoza ni Rukwa (56%) na Ruvuma (44%) ,kwa upande wa ukondefu (uzito kwa urefu) kutoka asilimia 7.8 hadi 4.5 na mikoa inayoongoza ni Zanzibar-Kusini Pemba na Kaskazini Pemba(9%),Manyara (6.4%),Geita (6.2%),Kigoma (6%) na Morogoro (6.0%)
Kwa upande wa uzito pungufu alisema (uzito kwa umri) kutoka asilimia 25.1 hadi 13.7 na mikoa inayoongoza ni Rukwa (23%),Arusha (20%) pamoja na Kigoma (20%).
Vilevile,mwanamke mmoja kati ya kila wanawake 10 walio katika umri wa kuzaa ana uzito pungufu (underweight) wakati asilimia 18 wana uzito mkubwa (over weight) na asilimia 10 wana kiribatumbo(obesity).Mikoa inayoongoza kwa kiribatumbo ni Zanzibar mjini Magharibi kwa 22%,Unguja Kusini 19%,Dar es Salaam 21%,Kilimanjaro 19% na Tanga 17%.
Naibu Waziri huyo aliahidi kuwa watajipanga katika kutoa elimu ya afya kwa umma na kuwafikia wananchi wengi zaidi “bado Watanzania hawajui kula lishe iliyokamilika na matumizi bora ya chakula.

Jumatatu, 30 Oktoba 2017

TANZANIA HATUNA UHABA WA DAWA, ASEMA DKT. FAUSTINE NDUGULILE

- Hakuna maoni

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa mkutano wan ne wa chama cha wataalamu wa figo nchini uliofanyika leo mjini Dodoma.

UTAALAMU WA KUPANDIKIZA FIGO UPEWE KIPAUMBELE NCHINI, ASEMA DKT. NDUGULILE

- Hakuna maoni




Na WAMJW-DODOMA
UTAALAMU wa huduma ya kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye magonjwa hayo upewe kipaumbele hapa nchini ili kuweza kuokoa watanzania wengi wenye matatizo hayo kwa muda mfupi na kupunguza gharama kubwa ya rufaa za kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa mkutano wan ne wa chama cha wataalamu wa figo nchini uliofanyika leo mjini Dodoma.
“Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa wagonjwa 35  kwa mwaka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na India kwa ajili ya kupandikiza figo ambapo inagharimu takribani shilingi milioni 75 hadi 77 kwa mtu mmoja ikiwa ni gharama za malazi na kupandikiza figo” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa ikiwa  Tanzania itazalisha wataalamu wengi wa kupandikiza na kusafisha figo itafanikiwa kupunguza gharama hizo na kufanya huduma hiyo ipatikane kwa shilingi milioni 20.3 ikiwa huduma hiyo itapatikana hapa nchini.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuwekeza huduma ya kupandikiza figo Serikali imefunga mashine katika maeneo yafuatayo, UDOM 10, 5Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  42, Hospitali ya Rufaa Mbeya 5, Hospitali ya Rufaa Bugando 10, KCMC 10, Hospitali ya Misheni Serian  10, Hospitali ya NSK Arusha 5, TMK 10,Regency 15, Hurbert Kairuki 5, Aga Khan 10 na Access 10 ambapo takwimu zinaonyesha mashine hizi zina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 783 kupitia huduma ya NHIF na 391 kwa huduma malipo ya papo kwa papo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa chama cha Wataalam wa Figo Tanzania Dkt. Paschal Rugajjo amesema kuwa wamepiga hatua kubwa katika kuongeza madaktari wa figo hapa nchini kwani mpaka sasa wapo madaktari 12 kutoka daktari mmoja miaka kumi iliyopita.
Mbali na hayo Dkt. Rugajjo amesema kuwa ushirikiano unahitajika kati ya chama hicho pamoja na Serikali kutoa kipaumbele kwenye elimu juu ya ugonjwa huo ili kuweza kupambana na tatizo hilo kuanzia ngazi ya wananchi mpaka kwenye taasisi za afya nchini.

DKT. FAUSTINE NDUGULILE AFUNGUA MKUTANO WA NNE WA CHAMA CHA WATAALAMU WA FIGO.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto dkt.Faustine Ndugulile akiongea kwenye mkutano huo wa wataalamu wa magonjwa ya figo nchini.Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kwenye Hotel ya Morena Mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka Hospitali nchini,Wadau wa Maendeleo pamoja na wataalamu wengine kutoka nchi za Kenya,Sudan,India pamoja na Norway.







Makamu wa Rais wa Chama cha wataalamu wa magonjwa ya Figo Tanzania (NESOT), Dkt.Paschal Ruggajjo akiongea dhima kubwa ya mkutano huo  ni teknolojia ya upandikizaji wa viungo nchini ili kuweza kuhudumia wagonjwa takribani milioni 23.












Baadhi ya Wataalamu wa magonjwa ya figo waliohudhuria mkutano huo.Mkutano huo ni wa siku mbili ambapo watajadili dhana mbalimbali ya ugonjwa wa figo ikiwemo kutoa elimu kwa umma ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya figo pamoja na upandikizaji.Tanzania imekua ikipeleka wastani wa wagonjwa thelathini na tano(35) kwa mwaka nje ya nchi kwa ajili ya kupandikiza figo na gharama ya kupandikiza nje ya nchi ikiwemo India ni shilingi milioni 75 hadi 77 kwa mtu mmoja ikiwemo kupandikiza,nauli pamoja na malazi
 
Makamu wa Rais wa Chama hicho akimpa zawadi mmoja wa wataalamu wa figo ambaye amefanya tafiti na kuwasilisha mada ya katika mkutano huo Profesa Ainory Gesase ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Sayansi ya Tiba.











Picha ya pamoja ya Mgeni Rasmi wa mkutano huo Dkt.Ndugulile akiwa na wataalamu wa figo nchini pamoja na wadau wengine wa ndani ya nchi na nje ya nchi.
 
 
 
 
 
 
 
 
Naibu Waziri akisalimiana na washiriki wa Mkutano huo mara baada ya ufunguzi.Dkt.Ndugulile alisema Serikali mgonjwa mmoja anahitaji wastani wa shilingi za kitanzania 37,620,504 kwa mwaka kwa ajili ya kulipia gharama za kusafisha damu nchini.
 
 
 
 
 
 
Mashine za kusafisha figo (Dialysis Machine) ambazo zimefungwa kwenye hospitali nchini.Serikali imefunga mashine katika hospitali nchini ikiwemo UDOM (10),Hospitali ya Muhimbili (42), Hospitali ya Rufaa Mbeya(5), Hospitali ya Rufaa Bugando (10), KCMC(10),Hospitali ya Misheni Serian(10),Hospitali ya NSK Arusha(5),TMK(10),Regency(15),
Hurbert Kairuki(5), Aga Khan(10) na Access(10).Mashine hizo  zina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 783 kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) na 391 kwa huduma ya malipo ya papo kwa papo(Picha zote na Wizara ya Afya).
 

TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG

- Hakuna maoni

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

 

TAARIFA KWA UMMA

TAHADHARI YA UGONJWA WA MARBURG
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), mnamo tarehe 19 Oktoba 2017 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika nchi jirani ya Uganda tangu tarehe 17 Octoba, 2017. Maeneo yaliyoathirika  na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kween, Kanda ya Mashariki ya nchi, ambayo  inapakana n nchi ya  Kenya. Hadi kufikia  tarehe 19 Oktoba 2017, watu 4 walikwishapata maambukizo ya ugonjwa huo, ambapo wawili kati yao   wamepoteza maisha.

Wizara  inatoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi  katika mikoa yote ya Tanzania, hususan kwa wale wanaoishi  katika mikoa ambayo inapakana na na nchi  ya Uganda (Mikoa ya Mara, Mwanza na Kagera).

Ugonjwa wa Marburg  unafanana sana na ugonjwa wa Ebola. Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Marburg vinajulikana kama  “Marburg Virus”, navyo vipo katika jamii moja na virusi vinavyosababisha Ebola (Ebola virus). Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.

Dalili kuu za ugonjwa huu ambazo huanza ghafla ni pamoja na Homa kali, maumivu makali ya kichwa pamoja na mwili kuishiwa nguvu ambapo baadaye huambatana na kuharisha sana (majimaji), maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kutapika na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na ha­raka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili, ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Marburg. Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya mgonjwa wa Marburg.

Wizara ya Afya , imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

o   Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kupitia OR-TAMISEMI.  Taarifa hiyo imejumuisha namna  Ukweli kuhusu ugonjwa (Fact sheet),

o   Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka ya nchi kavu na maji. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema na kushughulikiwa.

o   Vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya na vipima joto maalum (thermoscan) tayari vipo katika maeneo husika ya mikoa.


Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani hadi  sasa hakuna mgonjwa yeyote wa Marburg aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.



Kitengo cha mawasiliano Serikalini,
30/10/2017.

UONGOZI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA DODOMA WAPOKEA KWA MASIKITIKO JUU YA TAARIFA YA RUSHWA ILIYORIPOTIWA KWENYE MTANDAO WA JAMII FORUM

- Hakuna maoni
 
 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

                                                                                      
                                                                                                                 
TAARIFA KWA UMMA JUU YA TUHUMA YA UWEPO WA VITENDO VYA RUSHWA KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA, DODOMA KAMA ILIVYORIPOTIWA KWENYE MTANDAO WA KIJAMII WA JAMII FORUM TAREHE 28/10/2017
Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma umepokea kwa masikitiko taarifa iliyotolewa kwenye mtandao tajwa hapo juu kwamba, “Serikali na Takukuru muimulike Hospitali ya Mkapa Dodoma” kwamba, “imekuwa kawaida kabisa kwa mgonjwa kutopata huduma ya aina yoyote bila kutoa chochote na kuna mgonjwa ana wiki matokeo ya vipimo hayajatoka na hajapewa huduma yoyote zaidi ya dawa za kuondoa maumivu”.
Uongozi wa Hospitali unapenda kuwahakikishia watumiaji wa huduma za hospitali hii kwamba, madai husika hayana ukweli wowote. Mara baada ya kupokea malalamiko na tuhuma tajwa hapo juu, siku hiyo hiyo ya tarehe 28/10/2017 uongozi wa hospitali ulichukua hatua ya kufanya ufuatiliaji kwa kuwatembelea wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa wodini na kuzungumza nao pamoja na ndugu zao ili kubaini kero walizonazo kuhusu huduma za Hospitali.
Ufuatiliaji huu ulizingatia kubaini tarehe ya kulazwa, ugonjwa alio nao, vipimo alivyoandikiwa, vipimo ambavyo havijafanyika na sababu za kutofanyika.  Aidha, kila mgonjwa/ndugu aliridhia na kutoa ushirikiano mkubwa ili kubaini ukweli na pia wote walitoa mawasiliano yao ya simu ya mkononi iwapo ufuatiliaji zaidi ungehitajika.
Yatokanayo na ufuatiliaji huo ni;
Jumla ya wagonjwa 34 ndio walikuwemo wodini siku ya tarehe 28/10/2017. Tarehe za kulazwa kwao zilikuwa kati ya 20/9/2017 na 28/10/2017. Kati ya hao, wanawake watu wazima walikuwa 20 na wanaume 14 ambapo kati yao 2 walikuwa watoto wachanga.
Wagonjwa 24 tu ndiyo matibabu yao yalikuwa yanahitaji vipimo mbalimbali na wengine hawakuhitaji kutokana na asili ya magonjwa waliyokuwa wanaugua.
Wagonjwa waliombwa kutoa maoni yao kuhusu hali ya huduma kwa ujumla pia kuhusu upatikanaji wa vipimo vya uchunguzi wa maabara na mionzi na kama kuna ucheleweshaji wa vipimo husika na dalili za kuombwa rushwa. Jumla ya wagonjwa 18 kati ya 24 waliohitaji vipimo, walikuwa wamepimwa na kupewa majibu. Wagonjwa sita (6) waliobakia; wawili (2) kati yao walikuwa wamelazwa tarehe 27/10/2017 na tayari walikuwa wameshaanzishiwa matibabu na kupangiwa kupimwa ECHO na ECG tarehe 30/10/2017. Aidha, wagonjwa wengine wawili (2) walikuwa wamepimwa tarehe 27/10/2017 na walikuwa wanasubiri majibu na waliobakia 2 ndiyo kwanza walikuwa wamelazwa siku hiyo ya tarehe 28/10/2017.
Hakukuwa na mgonjwa yeyote aliyelalamikia kusumbuliwa kuhusu vipimo wala kuona dalili za rushwa na badala yake, wote walishukuru kwa juhudi zinazofanywa na watumishi wa hospitali katika kuwapatia huduma.


Hata hivyo, tangu awali hospitali hii imeweka mifumo mbalimbali ya kuhakikisha inabaini vitendo vinavyo athiri utoaji wa huduma bora na salama vikiwemo vitendo vya rushwa. Mifumo hii ni pamoja na:-
1.       Utoaji wa elimu kwa wateja maeneo ya  mapokezi, maabara na kliniki.
2.       Uwepo wa Sanduku la Maoni
3.       Uwepo wa namba za simu za kutolea malalamiko ya wateja.
4.       Viongozi wa hospitali kutembelea sehemu mbalimbali za kutolea huduma na kuongea na wateja.
5.       Wateja kujaza dodoso la kutoa maoni baada ya huduma (client exit interview).
Elimu inayotolewa huelekeza juu ya haki za wateja, huduma zinazopatikana, mfumo wa malipo, kujiepusha na kutoa au kupokea rushwa, na jinsi ya kutoa maoni na malalamiko juu ya huduma wanazopata kwa kutumia sanduku la maoni, kupiga namba za simu zilizobandikwa sehemu mbalimbali na kuwaelekeza mahala palipo na dawati la malalamiko na jinsi ya ujazaji wa dodoso la mteja baada ya huduma (Client Exit Interview). Elimu hii hutolewa na Idara ya Ustawi wa Jamii iliyopo hapa hospitalini.
Aidha, tangu awali, hospitali iliweka Sanduku la Maoni maeneo ya mapokezi ili  wateja waweze  kuweka maoni yao wakati wowote wanapohitaji. Tangu sanduku la maoni lianze kufunguliwa, hakuna aliyelalamikia uwepo wa vitendo vya rushwa au viashiria vyake.
Vilevile, hospitali imebandika namba Nne (4) tofauti za Simu mkononi za Viongozi katika sehemu mbalimbali za kutolea huduma ili kuwarahisishia wananchi/wateja kuwasilisha maoni yao kuhusu huduma. Namba ya kwanza kwenye orodha ni ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, ikifuatiwa na ya Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Katibu wa Hospitali. Tangu Wananchi waanze kutumia namba hizi hakuna aliyewahi kulalamikia uwepo wa rushwa ndani ya hospitali hii.
Uongozi wa Hospitali umejiwekea utaratibu wa kutoka ofisini na kupita sehemu mbalimbali za kutolea huduma na kuongea na wagonjwa ili kubaini kama kuna changamoto wanazozikabili wakati wa kupokea huduma. Maeneo hayo ni pamoja na mapokezi, eneo la wagonjwa wa nje (OPD), Kliniki mbalimbali, maabara, eneo la kutolea huduma za mionzi, na mawodini. Zoezi hili huongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali na hufanyika angalau mara tatu kwa wiki zikiwemo siku za mapunziko za Jumamosi na Jumapili. Tangu zoezi hili lianze, hakuna mwananchi/mteja aliyewahi kulalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Hospitali pia ilianzisha Dodoso Maalumu la Mteja (Client Exit Interview) linalojazwa na mteja baada ya kupewa huduma ili kubaini sehemu zenye changamoto. Tangu madodoso haya yaanze kujazwa, hakuna mteja/mgonjwa aliyelalamikia uwepo au viashiria vya rushwa.
Uongozi wa Hospitali unatoa Shukrani za pekee kwa watumiaji wa huduma za hospitali hii na wote wanaotoa maoni kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma. Tunapenda kuwahakikishia kuwa, tutaendelea kusimamia maadili ya tiba na kuhakikisha wateja wote wanafurahia huduma zetu. Hata hivyo, hatutasita kuchukua hatua stahiki za kisheria endapo tutabaini kwamba taarifa iliyotolewa ni ya upotoshaji na / au imetolewa kwa lengo la kuichafua hospitali, wizara au Serikali.
Uongozi wa hospitali unatoa wito kama kuna ambaye hajatendewa haki ajitokeze na kutumia fursa za mawasiliano zilizoainishwa hapo juu ili kero yake iweze kufanyiwa kazi au afuate utaratibu rasmi wa kuripoti tukio husika la vitendo vya rushwa kwenye vyombo husika vya kisheria ili taratibu za kisheria zichukuliwe.
Aidha, milango ya hospitali iko wazi wakati wowote kwa ajili ya kupokea kero na maoni toka kwa wateja wake ili kuboresha zaidi huduma.

AHSANTENI SANA.

30/10/2017.

UGONJWA WA KIHARUSI UNAZUILIKA NA KUTIBIKA

- Hakuna maoni


Ukiona mojawapo ya dalili hizi nenda haraka kwenye kituo cha huduma za Afya kwa matibabu.
Hakikisha unafanya uchunguzi wa Afya yako mara kwa mara.


Pitia :https://www.facebook.com/afyatz/?ref=bookmarks

Jumamosi, 28 Oktoba 2017

MH. UMMY AAGIZA HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA VYOTE VYA SERIKALI KUTOA HUDUMA YA UCHUNGUZI WA SARATANI.

- Hakuna maoni
Na WAMJWW

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu aagiza Hospitali na Vituo vya Afya vyote vya Serikali nchini kuanzia leo October 28 kutoa huduma ya uchunguzi wa Saratani kila siku wakati wa kliniki ya mama na mtoto, sambamba na huduma hizi, kila mwezi vyatakiwa kuwa na siku moja kwaajili ya kuchunguza na kufanya matibabu ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.
Ameyasema hayo wakati alipofungua matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, yalifunguliwa  katika viwanja vya hospitali ya Ocean Road mapema leo jijini Dar es salaam.
Aidha Mh. Ummy ameipongeza kazi nzuri inayofanywa na Uongozi wa Hospitali ya Ocean Road katika kutimiza majukumu yake ikiwemo kuongeza vitanda  40 mpaka vitanda 100  kwa gharama zao kwaajili ya wagonjwa wa saratani pindi wanapopata huduma za matibabu ya Chemotherapy.
“Katika kuwaunga mkono Serikali ya awamu ya tano ya Mh. Magufuli imewapatia Bilioni 5 kwajili yakukamilisha mashine za kisasa za matibabu ya Saratani kwa kutumia mionzi.” Alisema Mh. Ummy Mwalimu
Aidha Mh. Ummy Mwalimu ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Hospitali ya Ocean Road kuwa wanatakiwa kwenda kwenye shule za Msingi na Sekondari ili kuwajengea watoto uelewa kuhusu ugonjwa wa Saratani,  lakini ni vipi wataweza kujikinga na magonjwa yasiyo yakuambulizwa ikiwemo ugonjwa wa Saratani.
Pia Mh. Ummy alitoa rai kwa wananchi wote hususani wanawake kujitokeza kupima ugonjwa huo kwani unatibika endapo itagunduliwa mapema,  
Nae  Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Grace Maghembe ambae pia alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam , ameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto kwa kazi kubwa wanayoifanya ikiwemo kuongeza kwa bajeti ya Dawa , vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu.
Kwa upande mwingine Dkt. Grace Maghembe kwa niaba ya bodi ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa  uaminifu na bidii kubwa katika kuhakikisha kwamba wanakabiliana na ugonjwa huu wa Saratani kwa wananchi hasa wale wa hali ya chini na kuahidi kuendelea kuboresha huduma hii.
“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam kwenda kupima Saratani kwani ni bure, usisubiri mpaka kuugua, ukichelewa grarama zinaongezeka lakini pia uwezekano wa kupona unakuwa ni mdogo”. Alisema Dkt Grace Maghembe
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amemhakikishia Mh. Ummy Mwalimu kwamba upatikanaji wa dawa katika Hospitali hiyo ni 80% na dawa za wagonjwa wengi zinapatikana kwa 100%, ukilinganisha na  2015/2016 upatikanaji wa dawa ilikuwa 4% tu,  jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa na kufanya malalamiko ya dawa kuwa makubwa sana katika hospitali hiyo, hivyo kuishukuru Serikali ya Magufuli kwa niaba ya Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu.
Mwisho Dkt. Julius Mwaiselage amemhakikishia Mh. Waziri kwamba Hospitali ya Ocean Road ipo katika hatua ya Mwisho ya kuweka mashine mpya mbili (Linear accerelators), hivyo zitasaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kusubiri huduma , lakini kubwa kupunguza wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.

MH. UMMY MWALIMU (MB) AFUNGUA MATEMBEZI YA HISANI YAKUHAMASISHA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MATITI.

- Hakuna maoni
Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu watatu kutoka kushoto wakati alipofungua matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, kulia kwa Mh. Waziri ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage na kushoto  ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Grace Maghembe.




Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akimkabidhi cheti moja ya wadau waliofanikisha matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti iliofanyika mapema leo katika viunga vya Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.




Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu wakirusha Maputo juu kuashiria ufunguzi rasmi wa matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, iliofanyika katika viunga vya Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.





Wadau kutoka taasisi mbali mbali walioungana na Mh. Ummy Mwalimu na watumishi wa Hospitali ya Ocean Road katika matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti yaliyofanyika mapema leo jijini Dar es salaam.
 
 
 
 
 
 
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akiambatana na Binti yake katika matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti yaliyofanyika mapema leo jijini Dar es salaam.