Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 11 Januari 2018

DKT NDUGULILE AWAASA WANANCHI KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwaonesha nembo ya MSD GOT inayotambulisha kuwa Dawa hiyo inatolewa na Serikali kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua moja kati ya Friji ya kuhifadhia  chanjo.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwa ndani ya duka la Dawa la MSD kufanya ukaguzi juu ya upatikanaji wa Dawa zote, Kulia ni Mfamasia wa duka hilo Bahati Kazimili

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua mashine ya  Utla Sound wakati akiwa katika ziara yake Mkoani Katavi ya kukagua shughuli za utoaji wa huduma za Afya na kutathimini shughuli za maendeleo zinazofanywa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na Serikali.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na mgonjwa katika wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Manispaa Mpanda wakati akiwa katika ziara yake Mkoani Katavi ya kukagua shughuli za utoaji wa huduma za Afya, Kulia ni Mganga Mkuu Manispaa ya Mpanda Dkt. Mahenge

WAMJW-KATAVI

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsioa,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile amewataka wananchi kutumia nguvu  kazi yao katika ujenzi na uboreshaji wa Zahanati katika Wilaya zao kuliko kupeleka pesa nyingi kwa wakandarasi.
Dkt.Ndugulile ameyasema hao wilayani hapa wakati wa ziara ya kikazi ya  kukagua shughuli za utoaji huduma za afya na kutathimini  shughuli za maendeleo ikiwemo ya upanuzi wa miundombinu zikiwemo ya Zahanati
Alisema kutumia nguvu kazi zao itasaidia  kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama ambazo zingeweza kujitokeza kama wangetoa tenda hiyo kwa wakandarasi.”Nyinyi ndio wasimamizi wakuu wa shughuli hizi na mkiharibu tutakuja kuwalaumu nyinyi
Aidha,alisema Serikali imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha miundombinu  ya huduma za afya  nchini  kwa upande wa uzazi wa dharura ikiwemo upasuaji, wodi ya wazazi,maabara ,wodi ya watoto pamoja na nyumba ya mtumishi kwenye vituo vya afya ambapo ujenzi huo unaanza mara moja
Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile ameendele kuwatoa hofu wananchi juu ya hali ya upatikanaji wa dawa, huku akiwasisitiza wananchi wasiuziwe dawa zozote muhimu kwani hali ya upatikanaji wa Dawa ni nzuri maeneo yote na sasa ni wastani wa asilimia 80.

“Katika kituo cha Afya Kanoge, bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Milioni 300 mpaka Bilioni 2.5, kwahiyo dawa tunazo za kutosha, hivyo hatutarajii kuona mtu aje hapa aambiwe akanunue dawa sehemu nyingine, wamenithibitishia waganga wangu asilimia 90 ya dawa muhimu zipo” aliendelea Dkt. Ndugulile

Wakati huo huo Dkt. Ndugulile amesisitiza watumishi wa afya juu ya utunzaji wa kumbukumbu za dawa katika stoo ya madawa ikiwemo kuweka za kujua idadi za dawa zilizoingia na kutoka pamoja na utunzaji wa takwimu za mahudhurio ya wagonjwa wa kila siku, jambo linalopunguza ufanisi katika kazi.

Hata hivyo Dkt. Ndugulile amemtaka Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda Dkt. Mahenge kuanzisha ofisi ya kushughulikia malalamiko ya watu pindi wanapokutana na changamoto wakati wakipata huduma katika Kituo hicho cha Afya.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Yahaya Hussein wakati akiwasilisha taarifa ya Mkoa alisema kuwa Mkoa wa Katavi unakabiriwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya Afya hali inayopelekea changamoto kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Hadi kufikia Septemba 2017 Mkoa wa Katavi una jumla ya watumishi 693 sawa na asilimia 28 kati ya watumishi 2,437 wanaohitajika, kati ya hao 19 ni watumishi ngazi ya Mkoa na 674 ngazi ya Serikali za mitaa, kwa ujumla Mkoa wa Katavi una jumla ya upungufu wa watumishi 1,744” Alisema Dkt.  Hussein.
Dkt. Yahaya Hussein aliongeza kuwa Mkoa unaendelea kuzisimamia Halmashauri kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwakatia kadi za Afya ya Jamii (CHF) wazee ili kuendelea kupata Huduma za Afya kwa urahisi katika maeneo yao.
Mpaka kufikia Mwezi Septemba 2017 jumla ya wazee 19,248 wametambuliwa, na kati ya hao jumla ya wazee 1,807 sawa na asilimia 9.4 wameshapatiwa kadi za CHF katika Halmashauri zote za Mkoa wa Katavi.

ALIYOYASEMA NAIBU WAZIRI DKT. NDUGULILE KATAVI

Jumatano, 10 Januari 2018

WAZIRI UMMY MWALIMU ATEMBELEA HOSPITALI YA TAALUMA NA TIBA MLOGANZILA

Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kushoto akimjulia hali mgonjwa aliyelazwa kwenye hospitali ya taaluma na Tiba Mloganzila wakati alipotyembelera hospitali hiyo ili kuangalia hali ya utoaji huduma leo jijini Dar es salaam.

Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya wananchi waliokuwa wanasuburi huduma kwenye hospitali ya taaluma na Tiba Mloganzila wakati alipotyembelera hospitali hiyo ili kuangalia hali ya utoaji huduma leo jijini Dar es salaam.. wa kwanza kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Huduma za Hospitali hiyo Prof. Aboud Said.

Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akiongea na waandishi wa habari alipotyembelea hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila ili kuangalia hali ya utoaji huduma leo jijini Dar es salaam,wa kwanza kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Huduma za Hospitali hiyo prof. Aboud Said.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Huduma za Hospitali Mloganzila wa kwanza kulia Prof. Aboud Said. Akizungumza na waandishi wa habari wakati Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati alipotyembelea hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila ili kuangalia hali ya utoaji huduma leo jijini Dar es salaam.

Waziri wa afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikatiakitembelea maeneo ya Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila alipotyembelera hospitali hiyo ili kuangalia hali ya utoaji huduma leo jijini Dar es salaam.. wa kwanza kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Huduma za Hospitali hiyo Prof. Aboud Said.

PICHA NA ALLY DAUD.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo Januari 10 ,2018 ametembelea Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Cha Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila iliyofunguliwa rasmi  na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 25 ,2017  .
Lengo la kutembelea hospitali hiyo ni kuangalia utoaji wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Baada ya kutembelea hospitali hiyo Waziri Ummy ameagiza Idara yote ya magonjwa ya ndani (Internal Medicine) iliyopo hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhamia mara moja katika hospitali hiyo wakiwemo Madaktari,Madaktari Bingwa,Wauguzi pamoja na wataalmu wengine wa idara hiyo.
Wakati huo huo Waziri Ummy ameagiza kuhamisha wagonjwa waliopo wodi namba 3,4,5,6,7 na 8 zilizopo kwenye jengo la Mwaisela Muhimbili na kupelekwa hospital ya Mloganzila isipokuwa wagonjwa walio mahututi na wenye sababu maalumu na baada ya kuondoka wagonjwa hao wodi hizo zifanyiwe ukarabati mara moja. .”Nawaagiza waganga wafawidhi wa hospitali za Rufaa za Temeke,Mwananyamala na Amana kuanzia sasa rufaa zote za wagonjwa wa magonjwa ya ndani zije Mlongazila”, Alisema Mhe.Ummy.

Aidha, Waziri Ummy alisema Wizara imeshapokea Hospitali za Rufaa za Mikoa kutoka TAMISEMI hivyo amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo kukamilisha kuwapangia baadhi ya Madaktari Bingwa waliopo hospitali hiyo ya Taifa na kuwapeleka hospitali za Rufaa za Mkoa na Kanda mapema Februari mwaka huu.
“Tumeomba kibali Utumishi wa Umma ili kuwahamisha Madaktari Bingwa zaidi ya ishirini (20) waliopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na mishahara yao,”Madaktari wetu ni Wazalendo wapo tayari kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwenye hospitali zetu za Mikoa na Kanda”.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuwahudumia wananchi wote ikiwemo kupata huduma za matibabu ya kibingwa bila kubagua hivyo Wizara yake imejipanga kununua vifaa na vifaa tiba na kuvisambaza kwenye hospitali hizo za rufaa za Mikoa. Alitaja Madaktari bingwa watakaohamishiwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa na kanda miongoni mwao ni wa Magonjwa ya akina Mama na  Uzazi, Watoto,Upasuaji wa jumla,Radiolojia,Usingizi Macho pamoja na Magonjwa ya ndani.
Mloganzila ni Hospitali ya Taaluma na Tiba ambayo imewekwa vifaa tiba vya kisasa na teknolojia ya hali ya juu na ina vitanda 571 vya kulaza wagonjwa  na vyumaba 13 vya upasuaji na inatoa huduma masaa ishirini na nne.
Imetolewa na

Catherine Sungura
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Afya
10/1/2018



HAYA NDIYO ALIYOYASEMA WAZIRI UMMY ALIPOTEMBELEA MLOGANZILA

Jumanne, 9 Januari 2018

DKT. FAUSTINE NDUGULILE MKOANI KIGOMA

- Hakuna maoni

DKT. FAUSTINE AVIAGIZA VYOMBO VYA USALAMA MKOANI KIGOMA KUIMARISHA MIFUMO YA UDHIBITI WA UPOTEVU WA DAWA.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akihesabu harambee ndogo aliyoiongoza pindi alipofanya ziara yake katika kata ya Kazuramimba, harambee hiyo itasaidia katika jitihada za kuendeleza ujenzi wa madarasa hayo, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua Mlindoko

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wazazi juu ya umuhimu wa virutubisho vilivyo kwa mama pindi ananyonyesha katika eneo la kupokea chanjo kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5


Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua nembo ya MSD GOT katika dawa inayoonesha kuwa dawa hiyo imetolewa na Serikali na haipaswi kuuzwa

Kundi la wanakijiji wa kata ya Kazuramimba waliojitokeza kumsikiliza Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile pindi alipofanya ziara katika Kata ya Kazuramimba kujionea ujenzi wa Madarasa ya shule.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Kasulu Mkoani Kigoma




Na.WAMJWW. KIGOMA

Serikali imeviagiza vyombo vya usalama na kamati za Afya za vijiji kuimarisha mifumo yote ya udhibiti wa upotevu wa Dawa nchini, kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, ili kuondoa ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) katika ziara yake katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ya kukagua utoaji huduma za Afya na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya jamii ambao unasisitiza ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi,

“Niwaombe sana ndugu zangu wananchi tuwe walinzi, hiyo dawa ingeweza kukusaidia wewe, au ndugu yako, hivyo kushiriki katika ubadhilifu huo ni kujiumiza mwenyewe” alisema Dkt. Ndugulile.

Katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto Dkt. Faustine amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewekeza kiasi cha shilingi Milioni 400 katika Halmashauri 175, kikiwemo kituo cha Afya cha Uvinza , fedha zitakazotumika kuboresha na kujenga vyumba vya kutolea huduma ya dharura wakati wa kujifungua, nyumba za watumishi pamoja na maabara.

Dkt. Faustine aliendelea kusema kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa  wote wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.

Dkt. Ndugulile aliongeza kuwa anatambua uhaba wa watumishi unaovikabili vituo vingi vya Afya katika Wilaya ya Uvinza ambao umefikia asilimia 66 na kuahidi kulifanyia kazi ombi hilo ili kupunguza  changamoto katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile ameendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza Bajeti ya dawa , kutoka Bilioni 30 mpaka Bilioni 270 wa mwaka huu wa fedha hali iliyosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali.

Aidha, Dkt. Ndugulile aliwapongeza wananchi wa kata ya Kazuramimba kwa kuonesha kwa vitendo utayari wao wa kusukuma guruduma la maendeleo ya elimu katika Kijiji hicho kwa kuamua kujenga madarasa ya shule katika Kijiji cha Nyanganga kilicha kata ya Kazuramimba ili kuweza kuwakomboa watoto wao na janga la ujinga na umasikini.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi Mwanamvua Mlindoko ameeleza faida ya mradi wa ujenzi wa madarasa ikiwemo ongezeko la ufaulu kutoka wanafunzi 4115  mwaka 2017 huku waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni wanafunzi 1641 ambao ni sawa na asilimia 36 tu, hivyo kutokana na ujenzi wa madarasa haya utasaidia wanafunzi 2482 sawa na asilimia 64 kuendelea na elimu.

Jumatano, 3 Januari 2018

MAGONJWA YASIYO YAKUAMBUKIZA YACHANGIA ASILIMIA 27 YA VIFO VYOTE NCHINI

Kaimu Mkurugenzi magonjwa yasiyo yakuambukiza Dkt. Sarah Maongezi akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) katika kikao kilichofanyika mapema leo katika ukumbi wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kikihusu tuzo ya Elimu kwa jamii waliopata kutoka Shirikisho la kimataifa la magonjwa yasiyo yakuambukiza mwishoni mwa mwaka katika mkutano wa kimataifa uliofanyika katika falme zakiarabu.

Kaimu Mkurugenzi magonjwa yasiyo yakuambukiza Dkt. Sarah Maongezi akipokea tuzo ya Elimu kwa jamii kutoka kwa Mwenyekiti wa TANCDA Dkt. Tatizo Waane mapema leo katika ukumbi wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Wapili kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa TANCDA Andrew Swai.

Kaimu Mkurugenzi magonjwa yasiyo yakuambukiza Dkt. Sarah Maongezi akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) katika kikao kilichofanyika mapema leo katika ukumbi wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road kikihusu tuzo ya Elimu kwa jamii waliopata kutoka Shirikisho la kimataifa la magonjwa yasiyo yakuambukiza mwishoni mwa mwaka katika mkutano wa kimataifa uliofanyika katika falme zakiarabu, pembeni yake ni Mwenyekiti wa TANCDA Dkt. Tatizo Waane.


Na WAMJWW, Dsm

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yasema kuwa magonjwa yasiyo yakuambukiza yanachangia kiasi kikubwa katika vifo vyote vinavyotokea hapa nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa magonjwa yasiyokuwa yakuambukiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Sarah Maongezi wakati akipokea tuzo kutoka kwa TANCDA waliopata mwishoni mwa mwaka huu kutoka katika Shirikisho la Kimataifa la Magonjwa yasiyo yakuambukiza.

“Muongeze juhudi katika kupambana na magonjwa hayo ambayo yanachangia asilimia27 ya vifo vyote hapa Tanzania” Alisema Dkt Maongezi.

Dkt Maongezi aliendelea kusema kwamba Serikali imedhamiria kwa nia kabisa katika kupambana na magonjwa haya kwa kuamua kushirikiana na Asasi mbali mbali nchini ili kutimiza azma hiyo ya kupambana na magonjwa haya.

“Serikali pekee yetu hatuwezi na ndio maana tukashirikiana na Asasi kama TANCDA  inayojumuisha vyama vingine kama vile, Taasisi ya Saratani, Taasisi ya Magonjwa ya Moyo, Taasisi ya Mfumo wa Hewa na Taasisi ya Kisukari ambazo kwa ujumla zimejenga ushirikiano katika kupambana na magonjwa haya” Aliongeza Dkt. Maongezi.

Aidha Dkt. Maongezi amewahasa TANCDA kuongeza juhudi na kasi zaidi katika kupambana na magonjwa haya ili kuisaidia jamii kubwa ya Watanzania inayoangamia kutokana na kukosa elimu juu ya magonjwa hayo.

Dkt. Maongezi amewashukuru Waandishi wa Habari wote kwa mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa katika kuisaidia jamii ya Tanzania hususani katika kupambana na Magonjwa yasiyo yakuambukiza kwa kuandika Makala za magazetini na vipindi vya Redioni na Tv, na kuwahasa kuendelea kufanya kazi hivyo ya kuelimisha jamii kwa juhudi.

Nae Makamu Mwenyekiti wa TANCDA Pro Andrew Swai ametoa wito kwa Asasi hizo kufanya tafiti zaidi katika maeneo mbali mbali bila kusahau vijijini, ili kuweza kufahamu idadi kamili ya watu waliohathirika na maradhi hayo na kurahisisha kufikisha ujumbe katika maeneo hayo.

“TANCDA inatakiwa kujitanua ili waweze kuwafikia watu wote, pia ule ujumbe unaopelekwa uweze kuwafanya watu ili aweze kubadilika”. Alisema Prof. Andrew Swai.

Jumapili, 31 Desemba 2017

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA DKT. NDUGULILE ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO DKT. FAUSTINE NDUGULILE ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu  ametujaalia  kwani kuna wengi walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.  Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa  Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa.  Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya  watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
i.            Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia,  kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa  katika  misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba  kuaminiwa  huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika  utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za nchi,  Kanuni, Sera, pamoja na  Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko  ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha, nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.

ii.            Mabaraza ya Taaluma
Natumia fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa  mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na ujuzi  unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.

iii.            Wanajamii
Napenda kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia heshima na utu wa binadamu.  Pia, mnayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za Nchi.  Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi, dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.

Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
a)     Wanataaluma na Watoa Huduma,
        i.            Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili  wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
      ii.            Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
   iii.            Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.

    iv.            Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
      v.            Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).

b)    Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe (e-mails).

c)     Wanajamii kwa ujumla:
        i.            Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
     ii.            Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
a.     Uongozi wa kituo husika,
b.     Mganga Mkuu wa Wilaya,
c.      Mganga Mkuu wa Mkoa,
d.     Ofisa wa TAKUKURU,
e.     Baraza la Taaluma Husika,
f.       Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
g.     Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
h.     Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
 Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.

Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.

Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
31/12/2017.

TANGAZO KWA UMMA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anawatangazia wanafunzi wote walioko vyuoni wanaosoma masomo ya Shahada za Uzamili (Masters Degree) katika fani za Afya kwamba Wizara imepata fedha zitakazowezesha ufadhili (Sponsorship) kwa baadhi ya Wanafunzi, na kwa baadhi ya maeneo, kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Hivyo, kwa Tangazo hili, wale wote wenye nia ya kuomba ufadhili wanatakiwa kuwasilisha maombi yao.
Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo (Tuition fee), pamoja na posho ya utafiti pindi mwanafunzi anapokuwa kwenye kipindi cha kufanya utafiti kama sehemu ya mafunzo yake (Dissertation allowance).
Vigezo vitakavyotumika kuchagua watakaowasilisha maombi yao ni hivi vifuatavyo :

1. Kuwasilishwa kwa maombi rasmi ya ufadhili
2. Mwombaji kuwa Raia wa Tanzania.
3. Awe amedahiliwa Chuoni kuanza masomo kwa mwaka wa kwanza 2017/2018
4. Kipau mbele kitatolewa kwa:
a. Watumishi wa Serikali waliomo kwenye sekta ya Afya wanaofanya kazi katika vituo vilivyoko Wilayani/Mikoani ambao baada ya mafunzo watarudi kuendelea kufanya kazi katika vituo vyao vya awali, au watapangiwa vituo vya kazi sehemu nyingine yeyote nchini
b. Waombaji waliodahiliwa katika fani ambazo ni za msingi katika utoaji wa huduma za rufaa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Nyanja hizo ni Anaesthisiology, Surgery, Neurosurgery, Obstetrics and Gynaecology, Orthopaedics Surgery, Emergency Medicine, Paediatrics, Internal Medicine, Critical Care in Nursing na Midwifery and Womens Health
c. Waombaji waliodahiliwa katika nyanja za Ubingwa/Ubingwa wa Juu (Specialities na Super-specialities) zenye umuhimu mkubwa katika Hospitali za Kitaifa (kama Cardiology, Nephrology, na Oncology) ili kujenga uwezo wa ndani ya nchi katika jitihada za kupunguza wagonjwa wa rufaa wanaotibiwa nje ya nchi.
5. Aidha, mwombaji atatakiwa awe:
a. na barua ya ruhusa ya masomo kutoka kwa mwajiri wake (iambatanishwe)
b. Tayari kuingia mkataba wa kuitumikia Serikali kwa muda usiopungua miaka 5 baada ya kuhitimu mafunzo.
c. Hana ufadhili mwingine wa masomo yake

Tangazo hili linafuta ufadhili uliokuwa umetolewa awali kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya Shahada za Uzamili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu Dodoma (UDOM). Hivyo wanafunzi waliokuwa wamechaguliwa watapaswa kuomba upya kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwenye tangazo hili.
Aidha kwa kuwa wanafunzi wamekwisha ripoti vyuoni wahakikishe barua za maombi zinapitishwa kwa Wakuu wa Vyuo ili kuthibitisha kuwa mwanafunzi yuko chuoni.
Tangazo hili linahusu wale walioko vyuoni kwa mwaka wao wa kwanza wa masomo wa 2017/2018 tu.
Mwisho wa kupokea maombi haya ni tarehe 12/01/2018.
Maombi yote yaelekezwe kwenye anuani ifuatayo;

Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Chuo Kikuu Dodoma,
Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Maendeleo ya Jamii
S.L.P 743
DODOMA

Jumamosi, 23 Desemba 2017

SERIKALI YATARAJIA KUANZISHA BIMA YA AFYA KWA WATU WOTE

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya baadhi ya Watumishi(hawapo kwenye picha) wa Taasisi ya Kiuma inayomiliki chuo cha Uuguzi, Kituo cha Afya na Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma.

Mkurugenzi Mkuu wa chuo cha Uuguzi na Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile (Hayupo kwenye picha) wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua daftari la baadhi ya Vifaa vya Maabala wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua baadhi ya vifaa katika chumba cha Kompyuta wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa kike(Matroni) wa Kituo cha Afya cha Kiuma Maria Ntazama,  kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kiuma na Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua moja ya darasa katika chuo cha Uuguzi Kiuma wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua vitabu katika maktaba ya chuo cha Uuguzi na ukunga Kiuma wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) wakiwa katika ziara yake Wilayani  Tunduru, wakwanza ni Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara Ya Afya Dkt. Otilia Gowele na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Kiuma ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Dkt. Matomola.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Kiuma ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Dkt. Matomola, wakati akikagua  mabweni ya chuo cha Uuguzi na ukunga Kiuma kilichopo Wilaya ya Tunduru.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha uuguzi na ukunga Kiuma kilichopo Wilaya ya Tunduru wakifuatilia hotuba kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Dkt Faustine (hayupo kwenye picha),  wakati alipofanya ziara katika taasisi hiyo ya Kiuma Wilayani Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua kwa umakini Daftari la opokeaji Dawa pembeni yake ni Afisa wa Kliniki Hassan Miengende.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Kadi za dawa wakati alipofanya ziara katika kituo cha Afya Mkasale Wilayani Tunduru.

Wanchi wa Kijiji cha Mkasale wakifuatilia kwa makini agizo kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile juu ya usimamiaji wa rasilimali fedha katika kituo chao cha Afya.


Na WAMJWW, TUNDURU
Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuanzisha mfuko wa Bima ya Afya kwa watu wote nchini jambo litalosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma katika Taasisi ya Kiuma inayomiliki Hospitali, Chuo cha Uuguzi na Kanisa la Upendo wa Kristo.

“Tunatambua kwamba si kila mtu anamudu gharama hizo, kwa bahati mbaya ugonjwa unakuja wakati hatuja jiandaa, serikali imeliona hilo, pamoja na mikakati tunayoendelea nayo ya Bima ya Afya ya NHIF na CHF, tunatarajia kuja na utaratibu wa bima ya afya kwa wote, suala la matibabu lisiwe la kuwaza” alisema Dkt. Faustine Ndugulile.

Dkt. Faustine aliendelea kusema kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa  wote wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.

“Tumefkia hatua kubwa sana ya walengwa wote wanaohitaji kupata chanjo, jambo linaloifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi chache sana zilizofikia malengo hayo” alisema Dkt. Faustine

Aidha Serikali imetoa fedha kwa Vituo vya Afya 172 kwa lengo la kujenga thieta, Chumba cha Kujifungulia, Wodi ya Wazazi, nyumba ya Watumishi na Maabara, Huku Wilaya ya Tunduru ikifanikiwa kupata fedha hizo kwa vituo viwili, kikiwepo kituo cha Afya cha Mkasale.

Kwa upande mwingine  Dkt. Faustine ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Kiuma kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ikiwemo kutoa huduma za afya kwa wananchi, kutoa ajira, jambo linalotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Taasisi hiyo hivyo kuipunguzia mzigo Serikali katika Nyanja hizo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Uuguzi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Kanisa Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola ameiomba Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile itambue huduma inayotolewa chuoni hapo na kuwaongezea Watumishi, pia Serikali iwasaidie kuchangia mahitaji madogo madogo kama vitabu, maabara na vifaa.

Katika ziara hiyo Dkt. Ndugulile alifanikiwa kutembelea Kituo cha Afya Mkasale katika Wilaya hiyo ya Tunduru na kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa huku akiwasisitiza wananchi wasiuziwe dawa zote muhimu kwani hali ya upatikanaji wa Dawa ni nzuri maeneo yote na sasa ni wastani wa asilimia 80.

Aidha Dkt. Ndugulile amewahakikishia wanakijiji wa Mkasale kuwa kituo chao cha Afya kipo katika Vituo 172 vilivyopata mgao wa fedha za ujenzi wa maabara, chumba cha kujifungulia, Wodi ya wazazi, thieta, na kuwataka kusimamia vizuri fedha hizo ili kuweza kuboresha Zaidi huduma katika kituo hicho.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Wilaya ya Tunduru Mhe. Chiza Marando wakati akiwasilisha taarifa ya Wilaya alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 65 zikiwemo Hospitali 3 Vittuo vya Afya 5 na Zahanati 57 kati ya hizo 52 ni za serikali, 3 ni za mashirika ya dini na 2 zinamilikiwa na watu binafsi.

Mhe. Chiza Marando aliongeza kuwa Halmashauri ya Tunduru inakabiriwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya Afya hali inayopelekea changamoto kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika halmashauri hiyo.
“Tunduru ina jumla ya watumishi 339 wa Serikali sawa na asilimia 26.3 kati yawatumishi 1286 wanaohitajika na kufanya upungufu wa watumishi 974 sawa na asilimia 73.6, huku upungufu mkubwa ukiwa  katika kada ya madaktari, waganga, maafisa Afya na wauguzi.” Alisema Mhe. Chiza Marando

Kwa upande mwingine Mhe. Marando aliongeza kwa kusema hali ya utoaji huduma imeongezeka ikiwemo Huduma ya Chanjo kutoka 94 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 95 mwaka 2016 na kwa mwaka 2017 kiwango kimefikia asilimia 92.

Aidha Mhe. Chiza Marando alisema kuwa Wilaya hiyo inatoa huduma kwa makundi maalumu kwa kuzingatia Sera ya Wizara ya Afya kwa kutoa vitambulisho vya matibabu ya Wazee kwa baadhi ya kata zilizofanyiwa utambuzi, tayari vitambulisho 1234 vimetolewa kwa Wazee.