Jumatatu, 12 Machi 2018
WATANZANIA WATAKIWA KUPIMA UGONJWA WA MACHO ANGALAU MARA MOJA KWA MWAKA.
Jumatatu, Machi 12, 2018
-
Hakuna maoni
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akielezea jambo mbele ya Waandishi wa Habari na Watumishi wa uma wakati akitoa tamko katika wiki ya maadhimisho ya ugonjwa wa
Shinikizo la Macho Jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Waandishi wa Habari wakati akitoa tamko katika wiki ya maadhimisho ya ugonjwa wa
Shinikizo la Macho Jijini Dar es salaam.
Na WAMJW-Dar Es salaam.
WATANZANIA wametakiwa kujua afya zao
hususan magonjwa yanayohusu macho angalau mara moja katika mwaka ili kuweza
kutambua juu ya mustakabali wa macho yao.
Hayo yamezengumzwa na Naibu Waziri
wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile
wakati wa kutoa tamko katika wiki ya maadhimisho ya ugonjwa wa
Shinikizo la Macho Jijini Dar es salaam.
"Wanaohathirika zaidi na Ugonjwa
huu ni Barani Afrika na watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea hivyo
watanzania tujijengee mazoea ya kwenda kuangalia afya zetu hususani ugonjwa huu
angalau mara moja kwa mwaka" alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa
ugonjwa huo wa shinikizo la macho huambatana na kushindwa kuona mbali na dalili
zake za mwanzo si rahisi kuziona kwa wakati huo.
Kwa mujibu wa Dkt. Ndugulile amesema
kuwa takribani watu milioni1. 74 wana changamoto ya kutoona vizuri nchini
Tanzania na bado haijakadiriwa ni mikoa gani hasa ina athari kubwa kwani
ukusanyaji wa takwimu bado unaendelea.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa
matibabu ya ugonjwa wa presha ya macho yanapatikana katika
hospitali zote za serikali nchini ikiwemo dawa pamoja na upasuaji kama utawahi
mapema.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile
alisistiza kuacha utumiaji ovyo wa vilevi, uvutaji sigara na badala yake
kujikita kwenye ufanyaji wa mazoezi na kuzingatia lishe bora ili kuepuka
magonjwa yasioambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo na
mengineyo.
Siku ya Ugonjwa wa presha ya macho
itahadhimishwa kwa vituo vya afya kutoa huduma ya upimaji macho kuanzia tarehe
11 mpaka itapofikia kilele 17 machi 2018 na imebeba kauli mbiu
"OKOA UONI WA MACHO YAKO".
Jumapili, 11 Machi 2018
SERIKALI YAONGEZA HUDUMA ZA MATIBABU YA UGONJWA WA FIGO.
Jumapili, Machi 11, 2018
-
Hakuna maoni
Naibu
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile
katika matembezi ya Siku ya figo duniani ambayo yamefanyika katika viwanja vya
Farasi Oysterbay jijini Dar es salaam, kulia kwake ni Mwenyekiti wa Madaktari
Bingwa wa Figo Dkt. Onesmo Kisanga.
Naibu
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile
akikata utepe kuashiria ufunguzi wa matembezi ya Siku ya figo duniani ambayo
huazimishwa kila machi 8, ambayo yamefanyika katika viwanja vya Farasi
Oysterbay jijini Dar es salaam
Kiongozi wa Lions
International Club Sayed Rizwan Qadri akikabidhi hundi ya shilingi Milioni 1.4
kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile ikiwa moja ya juhudi za
kuunga mkono kupambana dhidi ya magonjwa ya Figo. Wakwanza kulia ni Mwenyekiti
wa Madaktari Bingwa wa Figo Dkt. Onesmo Kisanga.
Naibu
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile
akifanya mazoezi ya viungo wakati wa kujiandaa kuanza kwa matembezi ya Siku ya
figo duniani ambayo yamefanyika katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar
es salaam.
Na WAMJW. Dar Es salaam.
SERIKALI kupitia Wizara wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeongeza wigo wa kutoa huduma za matibabu ya
ugonjwa wa figo nchini kwa kuongeza vituo vya usafishaji damu hadi kufikia
vituo zaidi ya 17, na kufanya mafunzo
kwa madaktari bingwa ili kuongezea nguvu madaktari bingwa 13 waliopo.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto
Dkt.Faustine Ndugulile wakati wa matembezi ya Siku ya figo duniani ambayo
yamefanyika mapema leo katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es
salaam.
“Wataalamu
tunao 13 kwa upande wa madaktari, tumeiona hiyo changamoto kama Serikali,
tumeongeza wigo wakufanya mafunzo kwa madaktari bingwa, na hivi karibuni
tutatangaza ufadhili kupitia Serikali, vile vile tumetenga fedha kwaajili ya
kuwafundisha madaktari ili kuweza kufanya matibabu ya figo” alisema Dkt.
Ndugulile.
Dkt.
Ndugulile aliendelea kusema kwamba Serikali imeongeza wigo wa usafishaji damu
kwa kuongeza vituo Zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu kwa
wagonjwa wa Figo katika hospitali binafsi na Hospitali za Serikali.
“Tumeongeza
wigo wa usafishaji damu hadi tunavyoongea, tunavituo Zaidi ya 17 ambavyo
vinatoa huduma ya kusafisha damu katika hospitali binafsi pamoja na hospitali
zetu za Serikali , Muhimbili kuna vitanda 42, Mloganzira kuna vitanda 12,
Bugando vitanda 6, KCMC vitanda 6, Mbeya vitanda 6, bila kusahau Regency, TMJ,
Agakhan, Hindumandal, na tunaendelea
kuimarisha huduma”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Vile
vile Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali imeanza upandikizaji wa Figo na
imeshafanikisha kwa mgonjwa mmoja mpaka sasa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na matarajio ni kufanya
upasuaji kwa mgonjwa mmoja kila mwezi mmoja.
Aliendelea kusema mgonjwa
mmoja anahitaji wastani wa shilingi milioni 37 kwa mwaka kwa ajili ya kulipia
gharama ya kusafisha damu. Aidha, anahitaji kusafiri na kufika kwenye huduma
kwa wastani wa safari 126 kwa mwaka sawa na wastani wa safari 3 hadi 4 kwa
wiki.
Kwa
upande mwingine Dkt. Ndugulile aliendelea kuwa kukumbusha kuwa Serikali ya
awamu ya tano imeongeza Bajeti ya Dawa kutoka Bilioni 30 ilipokuwa ikiingia
madarakani hadi sasa ni Bilioni 270 kwaajili ya Dawa, vifaa na vifaa tiba
kwaajili ya magonjwa yakiwemo magonjwa ya Figo.
“Tumeongeza
bajeti kwaajili ya Vifaa, Dawa na Vifaa Tiba kutoka Bilioni 30 wakati Serikali
hii inaingia madarakani mbaka Bilioni 270, yaani mara tisa Zaidi, kwahiyo Dawa
na Vifaa Tiba kwaajili ya matibabu ya Figo tunazo” alisema Dkt. Ndugulile.
Mwisho
Dkt.Ndugulile alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula
nyumbani, mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha
mafuta kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu
(hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha familia
kufanya mazoezi.
“Watanzania
hatujui kula, tunakula bora chakula kuliko chakula bora, Matumizi ya vyakula
vya mafuta, matumizi ya chumvi nyingi, matumizi ya vilevi, matumizi ya sigara
kama hayana ulazima basi tupunguze, tutumie vyakula vilivyochemshwa na
vilivyochomwa, bila kusahau kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi angalau mara 3
kwa wiki kwa lisaa limoja inatosha” alisema Dkt. Ndugulile.
Ijumaa, 9 Machi 2018
MAGONJWA YA FIGO YANAATHIRI ZAIDI WANAWAKE.
Ijumaa, Machi 09, 2018
-
Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akitoa
maelekezo mbele ya Watumishi wa Umma na Waandishi wa Habari wakati akitoa
taarifa ya Siku ya Figo Duniani tukio lililofanyika mapema leo katika ofisi ndogo
za Wizara ya Afya Jijini Dar es salaam.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Dkt. Kisanga
akifafanua moja ya swali lililoulizwa na mwandishi wa Habari kutoka East Afrika
Tv Oliver Nyerige (hayupo kwenye picha) wakati
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Ndugulile akitoa tamko la siku ya Figo duniani ambapo
huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Watumishi wa Umma na Wataalamu wa magonjwa ya
Figo wakifuatilia kwa umakini taarifa ya siku
ya Figo duniani iliyosomwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ambapo siku hiyo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Na WAMJW. Dar es salaam.
Magonjwa
ya figo yanakadiriwa kuwaathiri takribani wanawake milioni 195 duniani
kote na yanashika nafasi ya 8 kama chanzo cha vifo vya wanawake duniani
na inakadiriwa kuwa wanawake 600,000 hupoteza maisha kutokana na
matatizo ya figo duniani kote kila mwaka
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na
Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati akitoa tamko la siku ya Figo
duniani ambapo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Dkt.Ndugulile
alisema tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO),
zinaonyesha wanawake wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya figo
ukilinganisha na wanaume. Kwa wastani asilimia 14% ya wanawake
wanaathiriwa na matatizo ya figo ukilinganisha na asilimia 12% kwa
wanaume
Kwa upande wa
Tanzania Naibu Waziri huyo alisema ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka na
tafiti zilizofanya Kanda ya Kaskazini mwaka 2014, ulionyesha kuwa kati
ya 7% – 15% ya Watanzania wana matatizo sugu ya figo na kwa asilimia
kubwa yamekuwa yakichangiwa na magonjwa ya Shinikizo la Damu na Kisukari
Hata
hivyo aliongeza kuwa kwa utafiti uliofanywa na Hospitali ya Kanda
Bugando, umeonesha kuwa 83% ya Wagonjwa wa Kisukari wana matatizo sugu
ya figo na kati ya hawa, 25% walikuwa wanahitaji huduma za usafishaji
damu.
“Wagonjwa waliokuwa
wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kutokana na figo kushindwa kufanya
kazi, ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
walikuwa 178. Kwa sasa idadi ya Wagonjwa hawa imeongezeka na kufikia
783.
Aidha,
alisema mgonjwa mmoja anahitaji wastani wa shilingi milioni 37 kwa
mwaka kwa ajili ya kulipia gharama ya kusafisha damu. Aidha, anahitaji
kusafiri na kufika kwenye huduma kwa wastani wa safari 126 kwa mwaka
sawa na wastani wa safari 3 hadi 4 kwa wiki.
Alisema
Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa wagonjwa thelathini na tano(35)
kwa mwaka nje ya nchi kwa ajili ya kupandikiza figo na idadi ya
waliokwishapandikizwa figo na ambao wanafuatiliwa matibabu yao katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni takribani 204.“Gharama za
kupandikiza figo nje ya nchi ni wastani wa fedha za Kitanzania milioni
75 hadi 77 kwa mtu mmoja,ikijumuisha upandikizaji,nauli na
malazi”Alisema Dkt.Ndugulile
Dkt.Ndugulile
alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula nyumbani,
mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha mafuta
kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu
(hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha
familia kufanya mazoezi.Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya figo ya
mwaka huu wa 2018 ni “FIGO NA AFYA YA WANAWAKE: WASHIRIKISHWE,
WATHAMINIWE NA WAWEZESHWE”.
Jumatano, 7 Machi 2018

WAZIRI UMMY AWAAHIDI AMBULANCE WAKAZI WA LUBANDA- ILEJE,
Jumatano, Machi 07, 2018
-
Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy
Mwalimu akitoa udongo wakati wa uchimbaji wa msingi katika ziara yake
ya ufunguzi wa kituo cha Afya cha Mtura kata ya Lubanda wilaya ya Ileje.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy
Mwalimu akiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa kituo cha Afya Mtura kilicho
katika kata ya Lubanda Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akielekea eneo la gari lililokwama kutokana na
changamoto ya Barabara, wakati akiwa katika ziara yake ya ufunguzi wa
kituo cha Afya cha Mtura kata ya Lubanda wilaya ya Ileje. Kulia ni
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje Haji Mnasi, Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kheri Kagya.
.
Wananchi wa kata ya Lubanda katika kijiji cha Mtura wilaya ya Ileje
wakimsalimia Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe.Ummy Mwalimu.
Na WAMJW. Songwe
WAZIRI
wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
amewaahidi wananchi wa kata ya Lubanda Wilayani Ileje kuwapatia gari ya
kubebea wagonjwa mapema mwaka huu.
Ahadi
hiyo ameitoa jana wakati alipotembelea kijij i hicho kujionea ujenzi wa
kituo cha afya cha Lubanda kinachojengwa kupitia mpango wa kuboresha
vituo vya afya nchini kwa kujenga chumba cha upasuaji wa dharura.
Waziri
Ummy alitoa ahadi hiyo baada ya kujionea umbali wa Zahanati ya Lubanda
hadi kufika hospitali ya Isoko, pia hali ya barabara kijijini hapo.
"kwakuwa
nategenea kununua magari ya kubebea wagonjwa yapatayo 60,Tanzania ni
kubwa, nyie mtakuwa namba moja, kwani hali ya barabara nimeiona"alisema
Waziri Ummy.
Aidha,
alisema anataka kushuhudia mwanamke mjamzito wa kijiji hicho anaokolewa
maisha yake kwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya ili
huduma zote za upasuaji ukiwemo wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni kwa
mama mjamzito zinatolewa katika kituo hicho mapema iwezekanavyo
"Serikali
ya awamu ya tano imedhamiria kumuokoa mama mjamzito pale anapopata
uzazi pingamizi, hivyo Serikali kuu imetoa shilingi milioni 500 kwa
ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya vipatavyo 174 nchini.
Hata
hivyo Waziri huyo wa Afya amewataka wananchi hao kujenga utaratibu wa
kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kupata tiba haraka pale
wanapogundulika na matatizo.
"hivi sasa wanawake
wengi wamegundulika na saratani ya shingo ya kizazi na asilimia 80 ya
wanawake wanaofika hospitalini wapo hatua za mwisho hivyo badala ya
kutibiwa wanapunguziwa maumivu" aliendelea Mhe.Ummy
Wilaya
ya Ileje ina vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 33 ikiwemo
hospitali mbili, kituo cha afya kimoja na zahanati 30 zinazomilikiwa na
serikali, dini pamoja na watu binafsi.
Jumatatu, 5 Machi 2018

TAARIFA KWA UMMA
Jumatatu, Machi 05, 2018
-
Hakuna maoni
BARAZA LA
WATAALAMU WA MAABARA LINATANGAZA RASMI KUANZA KWA MITIHANI YA USAJILI YA
BARAZA KUANZIA MWAKA HUU 2018, HII NI KATIKA KUTEKELEZA SHERIA NAMBA 22
YA MWAKA 2007 INAYOSIMAMIA TAALUMA NA HUDUMA ZA MAABARA NCHINI
TANZANIA.
MITIHANI YA BARAZA NI MATAKWA YA KISHERIA
YA KUPIMA UWEZO WA MTAALAMU WA MAABARA KABLA YA KUPEWA USAJILI WA
KUDUMU KATIKA KUTOA HUDUMA ZA MAABARA NCHINI.
MITIHANI HII ITAFANYIKA TAREHE 12 HADI 15 JUNI 2018 KWA NGAZI YA ASTASHAHADA, (NGAZI ZINGINE WATATANGAZIWA TAREHE YA KUANZA).
VITUO
VYA KUFANYIA MITIHANI, MALIPO NA JINSI YA KUJISAJILI VIMEAINISHWA
KATIKA FOMU YA KUJISAJILI NA MAELEKEZO YANAYOPATIKANA KATIKA TOVUTI YA
WIZARA ( www.moh.go.tz)
BARAZA LINASISITIZA KURUDISHA FOMU MAPEMA KUPITIA EMAIL ILIYOANDIKWA KWENYE FOMU YA KUJISAJILI AU OFISI YA MSAJILI(hlpc2018@yahoo.com)
MWISHO
WA KURUDISHA FOMU NI TAREHE 30 APRILI, 2018. TAARIFA YA KITUO
ULICHOCHAGULIWA KUFANYIA MTIHANI UTAJULISHWA KABLA YA TAREHE 30 MEI,
2018
KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NA OFISI YA MSAJILI KWA NAMBA ZIFUATAZO; 076820091 NA 0716020159
Imetolewa na,
OFISI YA MSAJILI;
BARAZA LA WATAALAMU WA MAABARA
03 FEBRUARI, 2018
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)




