Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 7 Oktoba 2018

WATANZANIA WAASWA KUPIMA MACHO MARA KWA MARA.

- Hakuna maoni

Washiriki kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi wakiwa katika maandamano kuadhimisha wiki ya afya ya macho yaliyofanyika jijini Dodoma mapema leo
Kaimu Mganga Mkuu Wa Serikali Dkt. Eliud Eliakim akipata maelezo kutoka Titus Nyange jinsi mashine ya Perkins inavyochapa nukta nundu zinazosomwa na watu wenye ulemavu wa macho wakati wa maadhimisho ya wiki ya afya ya macho duniani yanayofanyika jijini Dodoma. 

Mganga Mkuu Wa Mkoa wa Dodoma  Dkt. Charles Kiologwe akisisitiza jambo katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya afya ya macho uliofanyika katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma mapema leo.

Kaimu mganga mkuu wa serikali Dkt. Eliud Eliakim (Kushoto) akimkabidhi Kaimu Meneja wa Mpango  wa Taifa wa huduma za macho Dkt. Bernadetha Chilio kitabu cha muongozo wa utoaji huduma za macho katika maadhimisho ya wiki ya afya ya macho yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma.

Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Dodoma wakiwa wamejipanga katika mstari ili kupata huduma za macho katika maadhimisho ya wiki ya afya ya macho duniani yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere mkoani humo.

NA WAMJW-DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imewaasa Watanzania kujijengea tabia ya kupima macho mara kwa mara ili kuweza kuepuka aina mbalimbali za magonjwa ya macho ikiwemo vikope.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakimu wakati wa kufungua hafla ya kuelekea siku ya Afya ya Macho Duniani ambayo huadhimishwa kila alhamisi ya Pili ya mwezi Octoba.
“Asilimia kubwa ya magonjwa ya macho yanatibika ikiwemo upeo mdogo wa macho kuona  ambao yanazuilika kwa miwani  endapo mtu akiwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya na akigundulika ana tatizo la macho basi atapata matibabu mapema”alisema Dkt. Eliakimu.
Aidha, Dkt. Eliakimu alisema kuwa kwa Tanzania watu wasioona kabisa ni asilimia moja sawa na watu laki 5.7 huku watu wenye matatizo mbalimbali ya macho wanakadiriwa kuwa mara tatu ya wasioona kabisa sawasawa na mil.7.
Kwa mujibu wa Dkt. Eliudi amesema kuwa takwimu zinaonesha kwamba ugonjwa wa macho umepungua kutoka asilimia 4.6 mwaka 1990 na kufikia asilimia 3.4 mwaka 2015 kutokana na hamasa ya juu ya upimaji toka kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Huduma za Macho Nchini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Benadertha Chilio amesema kuwa tatizo la macho linaloongoza nchini ni mtoto wa jicho ambapo wagonjwa wanafikia kwa asilimia 50 na wengi wao ni wanawake.
“Watanzania wanatakiwa kuacha matumizi ya mitishamba na badala yake wanatikwa kuhudhuria hospitali pindi wanapohisi wanamatatizo ya macho kwani matumizi ya mitishamba kunaweza kusababisha makovu katika kioo cha jicho hivyo kunaweza kusababisha jicho kutofanya kazi kabisa” alisema Dkt. Chilio.
Aidha,Dkt. Chilio amewataka wanaohitaji tiba ya kuvaa miwani kwa ajili ya kuona vizuri waende hospitali zilizosajiliwa wapate vipimo stahiki na kupewa miwani kutokana na uwezo wao wa kuona na sio kupata huduma hizo kwenye vituo visivyosajiliwa.
Naye Mkanga Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Charles Kiologwe amewataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kupata huduma za macho ili kutokomeza ugonjwa huo  mkoani humo ili kuendelea katika shughuli za  kujenga uchumi wa viwanda.
“Nawaomba wakazi wenzangu wa Dodoma tujutokeze kwa wingi kupata huduma za macho ili kulinda afya zetu pamoja na kuondoa ule usemi uliopo vichwani kwa watu wengi kwamba kila mgonjwa wa macho anatokea Dodoma” alisema Dkt. Kiologwe.

Jumamosi, 6 Oktoba 2018

WATOA HUDUMA ZA AFYA WATAKIWA KUTOWASAHAU WATOTO KATIKA KUWAKINGA NA MAAMBUKIZI YA VVU.

- Hakuna maoni
Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikata utepe   kuashiria uzinduzi wa muongozo wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe .

Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi waliojitokeza kupima VVU katika viwanja vya Turbo mkoani Njombe mapema leo wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe .

Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisikiliza maelezo kutoka kwa mtoa huduma wakati alipotembelea mabanda ya kupima VVU na kutoa ushauri nasaha katika viwanja Turbo mkoani Njombe wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe.

Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi  Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka kitabu cha muongozo wa utoaji huduma kwa wauguzi na wakunga nchini wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe

NA WAMJW-NJOMBE


Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto imewataka watoa huduma za afya nchini kutokuwasahau watoto na vijana   katika kuwakinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri nasaha, kupima VVU na kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa uliofanyika mapema leo mkoani Njombe.

“Bado tuna changamoto kwa watoa huduma wetu wa afya kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kutokuwapima watoto  hali ya maambukizi, kutoa dawa kwa watoto na kuwapa elimu vijana hivyo natoa rai kwa wahudumu wa afya tuweze kuweka mkakati wa kufikia makundi hayo” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amewasisitiza Wauguzi na Wakunga kutoa huduma kwa kuzingatia miiko na maadili hususan katika kutoa huduma za VVU kwa jamii inayowazunguka ikiwemo kutumia lugha nzuri na kuwa wanyenyekevu kwa wananchi.

Sambamba na hilo Dkt. Ndugulile amewaasa wanaume nchini kuacha uoga na kujitokeza kupima VVU ili kutambua afya zao na kuanza matibabu mara moja iwapo watakutwa na maambukizi.

“Tutawafuata wanaume popote walipo hususan waliopo  kwenye mikusanyiko yao ikiwemo kwenye sehemu za starehe, viwanja vya mipira , Migodini na sehemu za uvuvi ili kutoa elimu na kuwashauri wapime ili kujua afya zao” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kusudio la kufanya hivyo ni kuhakikisha kufikia malengo ya 90 90 90 ya kutokuwa na maambukizi mapya ifikapo mwaka 2030. Ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wawe wanajua hali zao za maambukizi.

Ili kutimiza malengo ya serikali katika kupambana na maambukizi, Dkt Ndugulile amesema Serikali imekuja na utaratibu wa dawa kinga ambapo dawa hizo zitatumika kwa makundi maalumu ambayo yako hatarini kupata maambukizi.

“Lakini vile vile tumekuja na utaratibu unaoitwa dawa-kinga ambazo kuna makundi ambayo tumebaini, ambayo yako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya UKIMWI. Makundi haya kuna dawa ambayo tunataka tuwape zisaidiane na kinga nyingine ili kusaidia watu wasipate maambukizi ya virusi vya UKIMWI lakini hatusemi kwamba tumeshapata kinga”. Dkt Ndugulile.

Sambamba na hayo Dkt. Ndugulile amewataka watoa huduma waende wakatoe msisitizo na kuelimisha jamii katika maeneo ambayo dawa-kinga zimeanza kufanyiwa majaribio ili kuleta matokeo chanya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amesema ukanda wa nyanda za juu kusini ni ukanda ambao una maambukizi makubwa ya VVU na serikali ya mkoa ilianza kampeni ya tohara kwa wanaume, na sasa inaelekea kwa watoto wa sekondari na shule ya msingi ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na maambukizi mapya.

“Takwimu zinaonesha sisi tuna kiwango kikubwa cha maambukizi kuliko katika ukanda ule ambao tohara kwa wanaume inaanzia katika umri mdogo kiwango cha maambukizi kiko chini lakini pia kuna mahusiano kati aya tohara ya wanaume na maambukizi ya VVU kwahiyo kama mkoa kampeni hii tumeivalia njuga chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na TAMISEMI”. Alisema Ole Sendeka.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waganga Wakuu wa mikoa na Wafawidhi wa mikoa mbalimbali pamoja na wauguzi na wakunga waliopata muongozo wa kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri nasaha, kupima VVU na kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa.

Ijumaa, 5 Oktoba 2018

WAZIRI UMMY AUAGIZA UONGOZI WA HOSPITALI YA ST. FRANCIS KUSHUSHA BEI ZA MATIBABU MARA MOJA.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy amwalimu akikagua vifaa vya moja ya kati ya wagonjwa waliopata Rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya St. Francis pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliefika na mama yake kupata huduma katika kituo cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya viongozi wa Mkoa wa Morogoro walioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ifakara James Lihunyo (hayupo kwenye picha)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikagua cheti cha mgonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma kisha kuelekea Hospitali ya Rufaa  ya St. Francis.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliefika na mama yake kupata huduma katika kituo cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jisnsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akieleza umuhimu wa Bima ya Afya kwa watoto kwa mmoja kati ya wamama waliofika kupata huduma za Afya katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa maelekezo kwa Baba Askofu wa jimbo la Ifakara Salutaris Libenaambae baada ya kikao cha kuboresha hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo.

Upande wa mbele wa Hospitali ya Rufaa ya St. Francis.



WAZIRI UMMY AUAGIZA UONGOZI WA HOSPITALI YA ST FRANCIS KUSHUSHA BEI ZA MATIBABU MARA MOJA.

Na WAMJW - IFAKARA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Dini ya St.Francis kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi ndani ya mwezi mmoja kabla hajarudi kufanya ukaguzi wa mara ya pili.

Ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya St Francis iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara Mkoa wa Morogoro kufuatia taarifa isiyoridhisha juu ya gharama za matibabu iyoripotiwa siku ya Octoba 3 na Televisheni ya Taifa (TBC).

Waziri Ummy alisema kwamba, Serikali inatoa Jumla ya Watumishi 243 sawa na Asilimia 68% katika Hospitali hiyo, lengo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma za  bora za afya na zenye unafuu ikiwa ni moja kati ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati anaingia madarakani.

"Kati ya Watumishi 352, watumishi 219 wanalipwa mshahara na Serikali Kuu, ambapo kila mwezi tunalipa shilingi milioni 153.7, bila kuhesabu gharama za watumishi 12 walioshikizwa kutoka Wizara ya Afya, Watumishi 12 kutoka Halmashauri ya Kilombero, Katibu tawala Morogoro ameleta watumishi 2, jumla watumishi 243, ambao ni sawa na  Asilimia 68% wanalipwa mshahara kutoka Serikali kwa Asilimia 100%". Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa mwaka wa bajeti 2015/2016 Serikali ilipeleka dawa zenye thamani ya shilingi Millioni 119.5, bajeti ya mwaka  2016/2017 shilingi milioni 177.9 huku kwa mwaka 2017/2018 dawa zenye thamani ya shilingi milioni 118.7 zilinunuliwa hospitalini hapo.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema kuwa mwongozo wa Wizara ya Afya, unazitaka Hospitali zote kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito, wazee wasio na uwezo na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupata huduma za matibabu bila malipo.

Mbali na hayo Waziri Ummy alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya bila kuwasahau watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao hupata bima ya afya kwa shilingi 50,400/=
"Wakati umefika  wa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua, na uhakika huo ni wa kupitia Bima ya Afya", alihimiza Waziri Ummy kwa msisitizo.

Waziri Ummy, aliendelea kusema kuwa, Serikali inaelekea kutunga sheria ambayo itamlazimu kila Mtanzania kupata Bima ya Afya, ili aweze kupata huduma za matibabu ya Afya bila kikwazo chochote cha fedha.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mhe. Peter Ambrose Lijualikali amemuomba Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kuikumbuka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa kujenga Hospitali ya Wilaya, jambo litaloimarisha hali ya utoaji huduma za Afya kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya St. Fransis, Baba Askofu Salutaris Libena ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kufika hospitali hapo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote ambayo yametolewa na Serikali.

" Tunaahidi kwamba tumeelewa na tutatekeleza maelekezo yote, katika lengo la kuboresha huduma za Afya kwa wananchi ", alisema Baba Askofu Libena.

SERIKALI YANUNUA MA SHINE ZA MIONZI ZENYE THAMANI YA BILIONI 1.7

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu akionesha baadhi ya mashine za mionzi  10 zilizonunuliwa na Serikali zenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 na kusambazwa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Dkt.Mashack Shimwela,akiongea na waandishi wa habari baada ya kupokea mashine hizo(picha zote na Wizara ya Afya

Waziri Ummy akiongea na vyombo vya habari wakati wa kupokea mashine hizo za mionzi (digital X-ray) ambazo zitaboresha huduma za afya nchini hususani za uchunguzi wa mionzi


SERIKALI YANUNUA MA SHINE ZA MIONZI ZENYE  THAMANI YA BILIONI 1.7

Na.WAMJW, Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imenunua mashine za Mionzi (digital X-ray) zipatazo kumi zenye thamani ya shilingi bilioni 1.7.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akipokea mashine hizo kwenye Bohari ya Dawa(MSD)  jijini hapa.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikaki inaendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha huduma za afya nchini ikiwa ni lengo  la kuhakikisha huduma za afya zinawafikia watanzainia wote karibu na maeneo wanayoishi.

"Maendeleo ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa kuzalisha mali,hivyo tunaboresha na kuimarisha huduma za tiba na uchunguzi wa magonjwa katika hospitali zetu kuwa na vifaa vya kisasa zaidi na kuondokana na utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi".Alisema,Waziri Ummy Mwalimu.

Alisema mashine hizo zitapelekwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa 10 ambazo X-ray za zamani zimekwisha muda wake na zimekua zikiharibika mara kwa mara.

Alizitaja hospitali hizo ni Amana, Bukoba, Katavi,Morogoro,Njombe,Ruvuma,Simiyu na Singida pamoja na hospitali  za Wilaya ya Magu na Nzega.

Aidha,Waziri Ummy alisema katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Wizara yake imepanga kununua mashine za mionzi nyingine zipatazo ishirini na nne(24) zenye thamani ya shilingi bilioni 4.1 ambazo zitapelekwa kwenye hospitali za rufaa za Mikoa na Wilaya ambazo hazina au zina X-ray za kizamani au chakavu.

Akizungumza kwa niaba ya Waganga Wakuu wa hospitali   zinazopelekwa mashine hizo,Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana Dkt.Mashack Shimwela alisema ujio wa mashine hizo za kisasa zitasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa uchunguzi  za mionzi pia utunzaji wa mazingira tofauti na aina zilizokuwa zikitumika mwanzo

Aidha,alisema mashine hizo zina ubora wa picha  pia ina mifumo ya Tehama ambayo ni rahisi kusomwa hata nje ya hospitali husika endapo hakuna msoma picha

DKT. NDUGULILE AHIMIZA USHIRIKIANO WENYE MATOKEO YANAYOONEKANA BAINA SEKTA BINAFSI NA SEKTA ZA SERIKALI

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya, kutoka Sekta Binafsi na Sekta za Serikali wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa mwaka wa Sekta Binafsi na Sekta za Serikali.




Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi akimkaribisha Mgeni rasmi katika Mkutano wa pili wa mwaka wa masuala ya Afya jlioshirikisha Sekta Binafsi na Sekta za Serikali leo jijini Dar es salaam.



Mwakilishi Kutoka Sekta Binafsi Bw. akiongea na Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya, kutoka Sekta Binafsi na Sekta za Serikali wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa mwaka wa Sekta Binafsi na Sekta za Serikali.



Wadau mbali mbali kutoka Sekta Binafsi na Sekta za Serikali walioshiriki katika Mkutano wa pili wa mwaka wa Masuala ya Afya uliofanyika katika ukumbi wa Bank Kuu ya Tanzania (BoT) leo jijini Dar es salaam


Picha ya pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile baada ya kufungua Mkutano wa pili wa mwaka wa masuala ya Afya jlioshirikisha Sekta Binafsi na Sekta za Serikali leo jijini Dar es salaam.



DKT. NDUGULILE AHIMIZA USHIRIKIANO WENYE MATOKEO YANAYOONEKANA BAINA SEKTA BINAFSI NA SEKTA ZA SERIKALI.


Na WAMJW- Dar es salaam

NAIBU WAZIRI Wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amehimiza ushirikiano wa karibu wenye tija na matokeo yanayoonekana baina ya Sekta Binafsi na Sekta za Serikali katika kuleta Maendeleo chanya kwa wananchi.

Amesema hayo mapema leo wakati akifungua  mkutano wa pili wa mwaka wa Sekta binafsi na Sekta ya Serikali uliofanyika katika ukumbi wa Bank kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar ea salaam.

Dkt. Ndugulile alisema kuwa katika kuboresha Sekta ya Afya nchini, Serikali inahitaji ushirikiano wa karibu na Sekta Binafsi ili kurahisisha utoaji wa Huduma za Afya kwa wananchi, huku akisisitiza matokeo yanayoonekana katika ushirikiano wa pande hizo .

"Kusudio la Serikali ni jema kabisa, na ndomana tumeweka Sera na Sheria, sisi kama Serikali hatuwezi kuyafanya yote, tunahitaji Sekta ya Binafsi tushirikiane, Serikali iliyopo saivi madarakani inataka matokeo, hatupo hapa kukutana kila mwaka wakati hatuna mradi ulioshirikisha pande zote" alisema Dkt. ndugulile.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile ameagiza watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kuacha ubabaishaji pindi Sekta Binafsi zinapohitaji ushirikiano katika kuleta Maendeleo kwa wananchi na kuagiza kumchukulia hatua yeyote atakaebainika kutenda kosa hilo.

"Niwaombe sana wafanyakazi wenzangu wa Sekta ya Serikali tuache urasimu, tuangalie jinsi gani yakurahisisha ushirikiano ili mawazo mazuri yalete Maendeleo, tunataka kuwekeza katika viwanda, bado tunahitaji Huduma zakibingwa, watu wapo tayari, nataka tuache vikwazo", alisema Dkt Ndugulile

Pia, Dkt Ndugulile alitoa ushauri kwa Afisa Tabibu juu ya namna yakudhibiti matumizi ya fedha nyingi ambayo yanatumika kununua vifaa vya matibabu na mashine za maabara na thieta kwa kutoa fursa kwa Sekta Binafsi kununua na kuendesha mashine hizo huku Serikali ikijikita katika kutoa Huduma zilizo bora kwa wananchi.

"Sioni sababu ya Serikali kuingia gharama za kununua vifaa vya kutibu, maabara na thieta, kwanini tusiweke utaratibu wa watu wa Sekta Binafsi,  wawekeze kwenye vifaa, sisi kama Serikali tujikite katika kutoa Huduma, itatusaidia sana sisi kutoa Huduma bora" alisema Dkt Ndugulile.

Dkt. Ndugulile aliendelea kusisitiza kwamba , Sekta Binafsi si washindani wala maadui wa Sekta za Serikali hivyo ni lazima kuhakikisha ushirikiano unakuwa katika kutoa Huduma bora kwa wananchi, hivyo kutoa mwanya kwa yoyote mwenye wazo zuri ikiwemo ujenzi wa viwanda vya dawa kuleta wazo hilo ofisini kwake na kuahidi kulitekeleza Mara moja.

Sambamba na hilo Dkt Ndugulile alisema kuwa Serikali imedhamiria kuja na Sera ambayo itamtaka kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya ili aweze kupata Huduma za Afya, hivyo kuwataka Sekta Binafsi kuja na mawazo jinsi gani inaweza kushiriki katika kufanikisha wazo hili.


Jumamosi, 29 Septemba 2018

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI THABITI YA KUPAMBA DHIDI YA UGONJWA WA MOYO

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongoza Matembezi ya Siku ya Moyo Duniani yaliyoanzia viwanja vya Leaders Club na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es sala, matembezi hayo yamebeba kauli mbiu ya "Moyo wangu Moyo Wako". Wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya.

Matembezi ya Siku ya Moyo Duniani yakiendelea, ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya 'Moyo wangu, Moyo wako"

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiambatana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya wakinyoosha viungo baada ya kumaliza matembezi ya Siku ya Moyo Duniani katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akikagua moja kati ya mabanda yaliyokuwepo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani. Kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Robert Mvungi, kulia kwake ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Dkt. Amalberga Kasangala.


SERIKALI YAWEKA MIKAKATI THABITI YA KUPAMBA DHIDI YA UGONJWA WA MOYO

Na WAMJW-Dar es salaam.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kuweka mikakati thabiti ya kupambana dhidi ya maradhi ya Moyo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.

Dkt. Ndugulile alisema kwamba Serikali imeendelea kutoa Elimu kupitia vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii, kuanzisha Mpango wa Taifa wa magonjwa yasiyo yakuambukiza, na kuhakikisha TV zote katika Hospitali na Vituo vya Afya zinaonesha jumbe zinazohusu masuala ya Afya tu. 

“Serikali tumeona kwamba tunahitaji kuongeza msukumo kwemnye magonjwa yasiyo yakuambukiza, matamasha tunayofanya ni moja ya mkakati tunaofanya wa kutoa Elimu kwa jamii, kuoa Elimu kupitia njia mbali mbali ikiwemo TV, magazeti, pamoja na mtandao wa jamii, kuanzisha Mpango wa Taifa wa magonjwa yasiyo yakuambukiza, kuelekeza hospitali zote kuonesha jumbe mbali mbali za masuala ya Afya” Alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile alisema kwamba kuna ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyo yakuambukiza ikiwemo maradhi ya Moyo ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na kutofanya mazoezi, aina ya vyakula tunavyokula, matumizi yaliyopitiliza ya vilevi. 

“Kama taifa tunaona kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo yakuambukiza ikiwemo ugonjwa wa Moyo, na visababishi vikubwa ni aina ya vyakula tunavyokula, watu kutofanya mazoezi, matumizi ya pombe na sigara kupita kiasi”, alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile alisema kuwa Magonjwa ya moyo yanaongoza kwa kusababisha vifo duniani na inakadiriwa kuwa watu 17,500,000 hufa kila mwaka duniani kote kutokana na magonjwa ya moyo na kiharusi. 

Aidha, Dkt Ndugulile alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kwamba asilimia 40% ya vifo vyote vinavyotokea duniani vinasababishwa na magonjwa ya moyo huku nusu ya vifo ambavyo vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vinatokana na magonjwa ya moyo.

Pia, Dkt. Ndugulile alisema kuwa matumizi ya Tumbaku na bidhaa zake yanakadiriwa kusababisha vifo vya watu 6,000,000 duniani kila mwaka na pia huchangia kusababisha asilimia 10% ya wagonjwa wenye magonjwa ya moyo. 

Mbali na Hayo Dkt. Ndugulile alisema kwamba kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la Moyo ifikapo mwaka 2035 litaongezeka na kufikia makadirio ya wagonjwa wapya milioni 131,978,870 (sawa na ongezeko la 45% kutoka hali ilivyo kwa sasa), huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa mojawapo.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile alisema kuwa nia thabiti ya Serikali ya Awamu ya tano ni kuboresha huduma za afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyohitajika katika kutoa huduma za afya nchini kwa kuongeza bajeti ya afya kila mwaka. 

“Sisi sote ni mashahidi wa juhudi hizi za Serikali kwa uwepo wa Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete yenye wataalamu wabobezi katika tiba ya magonjwa ya moyo” Alimaliza Dkt. Ndugulile. 


Ijumaa, 28 Septemba 2018

HUDUMA ZA MRI NA CT SCAN ZAANZA KUTOLEWA MOI.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Mkono wa Bandia uliotengenezwa katika Taasisi hiyo, Kulia ni Mtaalamu wa viungo Bandia Bw. Deus David.

Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimsalimia mtoto, aliyefika na mzazi wake kupata matibabu katika Taasisi ya mifupa ya MOI, alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na kusimikwa kwa Mitambo ya MRI,CT Scan na X-Ray

Mkuu wa Kitengo cha Fiziotherapia Bw. Lucas Machage akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile, alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na kusimikwa kwa Mitambo ya MRI,CT Scan na X-Ray MOI.

Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na mmoja kati ya wanufaika wa Vifaa vya Bandia katika Taasisi ya Mifupa MOI aliowekewa baada ya kukatwa Mkono wake.

Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Cheti cha moja kati ya Wagonjwa waliofika kupata huduma za Afya katika Taasisi ya Mifupa ya MOI.

Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua moja kati ya mtambo wa kisasa uliosimikwa tayari kuanza kufanya kazi, katika Taasisi ya Mifupa ya MOI, Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Respicious Bonface.

Wataalamu mbali mbali kutoka Taasisi ya Mifupa ya MOI wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma na kusimikwa kwa Mitambo ya MRI,CT Scan na X-Ray.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua kitabu cha Kusaini Wataalamu wa Maabara, Kushoto ni Muuguzi wa Kitengo cha Dharura MOI Levlin Masama.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiendelea na Ziara katika Taasisi ya Mifupa ya MOI, Kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Respicious Bonface.


HUDUMA ZA MRI NA CT SCAN ZAANZA KUTOLEWA MOI.

Na WAMJW-Dar es Salaam.

Huduma za kupima magonjwa mbalimbali kwa kutumia Mashine  za kisasa ya CT Scan na MRI sasa zimeanza kutolewa kwa ufanisi baada ya kusimikwa na kuanza kufanya kazi  katika Hospitali ya Mifupa ya MOI.

Hayo yamesemwa leo na  Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii ,JiAnsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea  na kukagua hali ya utoaji wa huduma na usimikaji wa mitambo ya kisasa katika kitengo cha radiolojia yenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 5.6 Hospitalini hapo .

"Lengo la ziara yangu ni kukagua maendeleo ya usimikaji wa mitambo hii ya kisasa  ya MRI, CT SCAN, Xray, Ultra sound, mitambo mingine , nimeona na kujiridhisha imekamilika kwa asilimia 99% " Alisema Dkt.Ndugulile.

Aidha ,  Dkt. Ndugulile ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha unakamilisha  mambo machache yaliyobaki ndani ya wiki hii ili wiki ijayo wagonjwa waanze kupata huduma hapa.

 Mbali na hayo Dkt Ndugulile ameupongeza uongozi wa MOI kwa kuhakikisha usimikaji wa Mitambao unafanyika kwa wakati na hali ya utoaji huduma ni nzuri na ya kuridhisha kwani wagonjwa wamekuwa wakipata changamoto ya kwenda nje ya MOI kufuata vipimo hivi.

Mbali na hayo Dkt.  Ndugulile amesema ni adhma ya Serikali kuhakikisha huduma zote zinapatikana hapa nchini hivyo ni vyema kama kuna kifaa chochote kinachohitajika taarifa ikatolewa Wizarani ili kifaa hicho kiwekwe kwenye mpango na bajeti na kununuliwa kwani utaalamu na weledi upo wakutosha.

Dkt Ndugulule ametembelea vitengo vya mazoezi tiba pamoja na utengenezaji wa viungo bandia ambapo amekagua na kujiaone hali ya utoaji huduma na kujiridhisha kwamba huduma zimeboreka katika kipindi cha miaka 3 tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani  na kwa sasa watanzania wanapata huduma kwa wakati licha ya kuwa  kuna changamoto ya ununuzi wa vifaa tiba nje ya nchi.

Akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma na usimikaji wa mitambo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema kwamba hali ya utoaji wa huduma ni nzuri, wagonjwa wanapata huduma stahiki kwa wakati na idadi ya wagonjwa wanaopata huduma imeongezeka maradufu baada ya eneo la kutolea huduma kuboreshwa na kupanuliwa .

"Mh Naibu Waziri, hali ya utoaji huduma katika taasisi yetu ni nzuri, idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji imeongezeka na kufikia 700-900 kwa mwezi kutoka 500 na ongezeko la vyumba 2 vya upasuaji katika jengo hili, awali tulikua na vyumba 6 sasa vimekuwa 8, hii nikutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali hii ya awamu ya 5 inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli" alisema Dkt Boniface. 

Jumatano, 26 Septemba 2018

OCEAN ROAD YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 7.5 KWA MWAKA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimsikiliza moja kati ya Wataalamu wa Picha za Mionzi kwenye jengo la Mionzi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar Es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwajulia hali Wagonjwa waliofika kupata Huduma za Afya katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road Jijini Dar es salaa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile  akiongea na Mgonjwa aliyetoka nchi ya Jirani ya Kenya kupata matibabu Kansa nchini katika Taasisi ya Ocean Road Jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua vifaa ambavyo vimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilion 9.5, alipofanya Ziara katika Taasisi ya Ocean Road jijini Dar es salaam. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage.
 Baadhi ya Mitambo ya Mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyogharimu jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 9.5.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongoza msafara wa kukagua hali ya utoaji huduma za Afya, na kukagua vifaa ambavyo vimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilion 9.5. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Julius Mwaiselage.
OCEAN ROAD YAOKOA ZAIDI YA BILIONI 7.5 KWA MWAKA.

Na WAMJW-DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kuokoa zaidi ya Bilion 7.5 zilizokuwa zikitumika kwaajili ya matibabu ya Wagonjwa wa Saratani nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Taasisi ya Ocean Road na kukagua vifaa ambavyo vimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilion 9.5.

Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa vifaa hivi (Linac Mashine na CT Similator) vinaifanya nchi ya Tanzania kuwa moja kati ya Nchi chache barani Afrika ambayo inavifaa vya kisasa katika kutibu wagonjwa wa Saratani.

“Mashine hizi ambazo zipo ndani ya majengo haya yamenunuliwa na Serikali ya awamu ya Tano kwa gharama ya Shilingi Bilion 9.5, Vifaa hivi vinaitwa Linac Mashine na CT Similator vinaifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi chache sana Barani Afrika ambazo zinavifaa vya kisasa zaidi kwaajili ya matibabu ya Saratani” Alisema Dkt. Ndugulile

Pia, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Vifaa hivi vyenye ufanisi mkubwa vinasaidia sana katika kuongeza idadi ya Wagonjwa kupata matibabu kutoka wagonjwa 170, mpaka 270 kwa siku, huku ikipunguza muda wa wagonjwa kusubiria matibabu kutoka wiki 6 mpaka chini ya wiki 2.

Aidha, Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali inajipanga kufunga kifaa kikubwa cha Pate Scan ambacho kitasaidia kwa kiasi kikubwa wagonjwa wa Saratani.

Akisoma Risala ya Taasisi hiyo Mkurugenzi wa Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage alisema kuwa gharama za ujenzi wa jengo la vifaa vifaa hivo ni shilingi Bilion 2.3 ambazo zote zilitolewa na Serikali.

“Gharama ya ujenzi huu ni shilingi Bilion 2.33 ambapo zilitolewa zote na Serikali, Jengo hili limekwishakamilika, na liliweza kufanyiwa uhakiki na Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania, pamoja na shilika la kimataifa la nguvu za Atomic walilipitia na kuliangalia vigezo vyake kama vimefikiwa na waliona vinafaa”. Alisema Dkt. Mwaiselage.

Mbali na hayo Dkt. Mwaiselage alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kugharamia Mradi huo uliogharimu jumla ya shilingi Bilion 9.5, zilizojumuhisha gharama za kupeleka Wataalamu kwaajili ya kupata mafunzo nje na ndani ya nchi.

“Mradi ulikuwa na sehemu ya Mafunzo kwa Wataalamu nje na ndani ya nchi, jumla ya gharama ya mradi huu ilikuwa ni Bilion 9.5, na fedha zote hizi, ziligharamiwa na Serikali chini ya Raisi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na tunamshukuru sana kwa kuweza kutoa fedha kwaajili ya mradi huu”. Alisema Dkt. Mwaiselage.

Jumanne, 25 Septemba 2018

KANUSHO KUHUSU AKAUNTI BATILI YA WAZIRI UMMY MWALIMU


Jumamosi, 22 Septemba 2018

WAKUU WA MIKOA NCHINI WATAKIWA KUTENGA VITUO MAALUM VYA KUHUDUMIA WAGONJWA WA EBOLA.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongoza Matembezi ya Hiari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini yalipoanzia katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi (Wakwanza Kulia) akiwa na Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakiwa katika matembezi ya Hiari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini yalipoanzia katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam. 

Kikundi Shupavu cha Vijana wa Skauti kikiwa kimeshika Bango lenye maandishi ya kutoa Elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola wakati wa matembezi ya Hiari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini yalipoanzia katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mwongozo utaosaidia jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika nchi yetu endapo utainia nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa ameshika Mwongozo utaosaidia jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika nchi yetu endapo utaingia nchini.
 
WAKUU WA MIKOA NCHINI WATAKIWA KUTENGA VITUO MAALUM VYA KUHUDUMIA WAGONJWA WA EBOLA. 

Na WAMJW - DSM 

WAZIRI  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wakuu wa mikoa wote kutenga vituo maalumu katika kila halmashauri cha kuhudumia na  kuhifadhi wagonjwa wa Ebola endapo wataingia nchini.

Waziri Ummy Ameyasema hayo mapema leo katika Matembezi ya Hiari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini yalipoanzia katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam. 

"Lazima kila mikoa, Halmashauri kutenga kituo maalumu cha kuhudumia wagonjwa wa Ebola endapo watatokea, katika kila mkoa, kila Wilaya lazima wawe na chumba maalumu kwaajili ya kuhifadhi wagonjwa wa Ebola endapo wataingia "alisema Waziri Ummy Mwalimu. 

Aidha, Waziri Ummy aliwaomba Viongozi wa Dini kutumia majukwaa yao katika Maubiri yao kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu wa Ebola,  huku akiwaomba wasanii na viongozi wa Siasa nchini kutumia majukwaa yao ili kutoa madaraja kufikisha taarifa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Waziri  Ummy  amesema kuwa licha ya ugonjwa wa Ebola kutoingia nchini, bado tupo katika hatari kubwa ya kuupata ugonjwa huu kutokana na muingiliano wa wananchi baina ya nchi ya Tanzania na eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni karibu na nchi ya Tanzania.

"Ebola bado haijaingia nchini Tanzania, lakini ni Kweli Kwamba tupo katika hatari kubwa zaidi kupata Ugonjwa huu wa Ebola, hii inatokana Na mlipuko wa ugonjwa huu kuwepo katika eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni karibu na nchi ya Tanzania na kutokana na muingiliano wa wavuvi baina ya nchi hizi", Alisema Waziri Ummy. 

Aidha Waziri Ummy alisema kuwa Tanzania inaweza   kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini kwa vitengo vinavyihusika  kutoa elimu na uelewa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ebola, itakuwa ni moja ya njia kubwa ya kuzuia ugonjwa huu usiingie. 

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa kwa mujibu wa taarifa kutoka WHO watu 111 wametolewa taarifa kuugua ugonjwa huu wa Ebola na watu 75 sawa na Asilimia 67% wamefariki kutokana na ugonjwa huu, vifo ni zaidi ya Asilimia 50%. Maana yake kukiwa na wagonjwa 100, tunapoteza wagonjwa 50.

"Kwa mujibu wa Takwimu za shirika la Afya Duniani (WHO) Mpaka sasa, watu 111 wametolewa taarifa ya kuugua ugonjwa huu wa Ebola, watu 75 sawa na Asilimia 67% wamefariki, ndiomaana tunaogopa sana kama tutaruhusu ugonjwa huu utaingia nchini, vifo ni zaidi ya Asilimia 50%, maana yake tukiwa na wagonjwa 100 , tunaweza kupoteza wagonjwa 50, kwakweli tusikubali ugonjwa huu kuingia nchini "Alisema Waziri Ummy . 

.