Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 10 Oktoba 2018

VIJANA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA ILI KUEPUKA ATHARI ZA AFYA YA AKILI

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Serikali  Prof. Mohamed Bakari Kambi  akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati akitoa tamko la kuadhimisha siku ya afya ya akili ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 10.

Mtaalamu wa magonjwa ya akili kutoka hospitali ya Milembe Dodoma Dkt. Mwombeki akifafanua jambo juu ya magonjwa ya afya akili mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa tamko la kuadhimisha siku ya afya ya akili ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 10.

Na WAMJW-DODOMA
Vijana wametakiwa kujiepusha na matumizi  ya madawa ya kulevya , makosa ya kimtandao, kucheza kamali na kukaa katika magenge ambayo yanaweza kupelekea kupata fikra mbaya zinazoweza kusababisha kuathirika kwa afya ya akili.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali  Prof. Mohamed Bakari Kambi  Jijini Dodoma wakati akitoa tamko la kuadhimisha siku ya afya ya akili ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 10.
“Utumiaji wa mihadarati kuwa ni changamoto kubwa inayowakabili vijana katika mataifa yote pia utumiaji wa madawa ya kulevya na pombe vimehusishwa kwa kiasi kikubwa na tabia hatarishi ya ngono zembe na ajali za barabarani” alisema Prof. Kambi.
Prof Kambi amesema kuwa  sambamba na elimu kwa Umma  Wizara itaendelea kutoa matibabu ya afya ya akili katika hospitali zote za Umma nchini pamoja na kuendelea kutoa dawa za Methadone kwa watumiaji wa madawa ya kulevya katika mikoa ya Dar es salaam,Mbeya,Mwanza na Dodoma  hivi karibuni.
Aidha Prof. Kambi amesema kutokana na tafiti za shirika la afya duniani (WHO) zinaonesha vijana wanaoathirika na kupata matatizo ya akili ni wale walio katika umri wa kuanzia miaka 14, lakini wengi wao hawapati nafasi ya kutambulika na kupata matibabu katika wakati muafaka.
“Tafiti za shirika la afya duniani (WHO) zinaonesha takribani nusu ya magonjwa yote ya akili huanzia katika umri wa miaka 14 ambapo magonjwa ya akili na matumizi ya vilevi ni miongoni mwa changamoto kubwa sana za kiafya na kiusalama zinazoathiri rika hili la binadamu”. Amesema Prof. Kambi.
Prof. Kambi amesema kuwa  kujiua kunaaminika kuwa ni chanzo kikuu cha pili cha vifo vyote vinavyowakabili vijana wengi duniani ambapo Ugonjwa wa Sonona (Depression) umetajwa kushika nafasi ya tatu duniani katika magonjwa yote yanayoathiri vijana duniani.
Kwa mujibu wa Prof. Kambi amesema kuwa Takwimu za mwaka 2015 hapa nchini zinaonesha  vijana kuanzia miaka  13 hadi 17 walioko katika shule za misingi na sekondari zinaonesha kuwepo na dalili za Sonona, ambapo vijana zaidi ya asilimia 7 walionyesha kuwa na dalili hizo
Kwa upande wake mtaalamu wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Milembe Dkt. Damas Andrew  kuwa  matatizo ya unywaji pombe na uvutaji wa sigara yalitaarifiwa kwa kiwango sawa cha asilimia 5, huku asilimia 3.1 wakiripotiwa  kuvuta bangi katika maisha yao huku utafiti huo ulionesha kuwa robo ya vijana wote waliohojiwa waliripoti kufanyiwa uonevu na wenzao.
“Vijana wote waliohojiwa waliripoti kufanyiwa uonevu na wenzao ama kwa kupigwa, kusukumwa au kufungiwa madarasani kunakopelekea kupata athari ya akili”. Amesema Dkt. Damas
Dkt. Damas amesema utafiti umeripoti kuwepo kwa matukio mbalimbali ya ukatili kwa vijana kutoka kwa wazazi na walezi yanayosababisha kuzorotesha ya akili kwa watoto na vijana wanaowalea. Vilevile kiwango kikubwa cha unyanyasaji kimeripotiwa kufanyika katika mitandao ya kijamii dhidi ya watoto na vijana na kufanya changamoto hizi kuathiri kwa kiasi kikubwa afya ya akili.

DKT. NDUGULILE AAGIZA KUBORESHWA KWA MFUMO WA UKUSANYAJI TAKWIMU NCHINI

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya baada ya kufungua mkutano wa masuala mbali mbali ya Afya uliofanyika jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifungua Mkutano wa Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya uliofanyika jijini Dar es salaam.

Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Afya TAMISEMI Dkt. Zainabu Chaula akiongea na Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya katika mkutano uliofanyika jijini Dar es salaam.

Kiongozi Mkuu wa Mkutano wa Masuala ya Afya, hususani katika mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi Bw. Mavelle Tukai akiwakaribisha Wadau wa masuala ya Afya waliofika katika Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea jambo na Mkurugenzi wa Bohari kuu ya Dawa nchini Bw. Laurean Bwanakunu, katikati ni Afisa mfamasia kutoka Wizara ya Afya Siana Mapunjo.

Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya wakifuatilia kwa makini mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile (hayupo kwenye picha)


DKT. NDUGULILE AAGIZA KUBORESHWA KWA MFUMO WA UKUSANYAJI TAKWIMU NCHINI.

Na WAMJW - Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameagiza kuboreshwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa Takwimu nchini utaosaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na zinazifanana katika taasisi zote.

Ameyasema hayo mapema wakati akifungua Mkutano wa masuala ya Afya, hususani katika mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi leo jijini Dar es salaam.

Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali inataka kuona mifumo yote ya ukisanyaji Takwimu inaboreshwa mara moja huku akisisitiza kuwa mifumo hiyo ni lazima iweze kuwasiliana jambo litalosaidia kupata Takwimu sahihi na zinazofanana kwa mifumo yote.

"Tunataka kuona mnaboresha mfumo wa ukusanyaji Takwimu, Takwimu bado ni changamoto kubwa sana katika utoaji wa huduma za Afya na katika mfumo mzima wa usambazaji, na ni lazima kuhakikisha kuwa mifumo hii inawasiliana na inakuwa endelevu" Alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile amewaonya watumishi wa Serikali hususani kutoka Wizara ya Afya wanaokwamisha mawazo endelevu yanayopelekea kupiga hatua kwa Sekta ya Afya, na kuahidi kuwachukulia hatua endapo yeyote atabainika kufanya hivo.

" Muda wowote, mtu yeyote mwenye Mawazo mazuri na Endelevu kwaajili ya Maendeleo ya Sekta yetu ya Afya, njoo unione Mimi au Waziri wangu, milango yetu ipo wazi, wengine sisi hatuna urasimu, Serikali hii ya awamu ya tano haitaki ubabaishaji" Alisema Dkt Ndugulile.

Aidha, amewaagiza Waganga Wafawidhi wote nchini kuhakikisha wanaandaa orodha ya Dawa zilizopo kila mwanzo wa wiki ili kusaidia kufahamu orodha ya Dawa zilizopo na zinazohitajika kwa kipindi hicho, huku akisisitiza kumchukulia hatua yeyote ataebainika.

"Tumepata taarifa baadhi ya makampuni ya Dawa yanapita katika Hospitali zetu, hususani Hospitali kubwa na wanawarubuni Madaktari wetu kuandika kwa MSD orodha ya Dawa ambazo hazipo katika mwongozo wetu wa Serikali, tutachukua hatua Kali" Alisema Dkt Ndugulile.

Mbali na hayo Dkt Ndugulile amepiga marufuku Madaktari wote nchini kuandika Dawa kwa kutumia majina ya bishara na kuwataka kutumia majina ya asili ya Dawa hizo.

"Jukumu la Serikali sio kufanya Bishara ya kumtangazia mtu, mfano Panaldo sio jina lake kitaalamu, ukienda baadhi ya nchi unaweza usikute Panaldo jina lake halisi ni Parasetamo na ndio linatakiwa litumike" Alisema Dkt Ndugulile.







Jumanne, 9 Oktoba 2018

MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE YANALETA ULEMAVU

- Hakuna maoni
 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila akifungua semina ya uraghibishaji na uhamasishaji wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa Jijini Mbeya.Kulia ni Ofisa mpango toka Wizara ya Afya Osca Kaitaba na mwisho ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela Bi.Claudia Kitta.
 Ofisa Mpango toka Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Osca Kaitaba akifafanua jambo kwenye semina hiyo.
Wataalam mbalimbali kutoka Sekratariet ya Mkoa wa Mbeya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa semina ya  uraghibishaji na uhamasishaji wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa viongozi na wataalam wa Sekretariet na Mamlaka za Serikali wa Mkoa wa Mbeya.

Na WAMJW - Mbeya

Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yamekuwa yakusumbua na kuleta athari kwa wananchi wa Mkoa wa mbeya hadi kusababisha ulemavu.

Hayo yamesemwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila katika ufunguzi wa semina ya uraghibishaji na uhamasishaji wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa  iliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa Oktoba 9, 2018.

Alisema Magonjwa hayo yamekuwa yakiathiri zaidi wananchi kwa kiasi kikubwa na kupunguza uwezo wa wananchi katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa taifa.

"Magonjwa haya, pamoja na kusababisha usumbufu mkubwa kwa waathirika pia yanaongeza matumizi ya rasilimali chache tulizonazo katika kuyakabili "alisema Mkuu huyo mkoa.

Aidha Chalamila alisema kwamba uwepo wa magonjwa hayo umefanya watoto kutokuwa na mahudhurio mazuri mashuleni kutokana na muda mwingi kutumika kwenye matibabu.

Hata hivyo alisema kuwa jambo la kutia moyo ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wamekuwa wakitoa kingatiba za kukinga magonjwa hayo katika mkoa wa Mbeya.

"Hii ni kutokana na lengo la Serikali ya awamu ya tano ambalo ni kudhibiti magonjwa haya na hivyo kupunguza gharama kwa wananchi kwa kugawa kingatiba hizo"Alisisitiza Chalamila

Akielezea zaidi Chalamila alisema Mkoa wa Mbeya walikuwa wanakabiliwa na magonjwa yote matano ambayo ni minyoo ya tumbo, kichocho, matende na mabusha katika Wilaya zote ila kutokana na usimamizi na uhamasishaji nzuri Mkoa wake hivi sasa wamepunguza magonjwa hayo na hivyo kuwataka viongozi wa mkoa na Wilaya zake kuzidi kuhamasisha na kuelimisha zaidi wananchi kujitokeza kumeze kingatiba ili kutokomeza magonjwa hayo.

Aliyataja magonjwa yanayoendelea kuwa changamoto kwa Wilaya za Mkoa wa Mbeya ukiwemo ugonjwa wa Trakoma kwa Wilaya za Kyela, Chunya na Mbarali pamoja na ugonjwa wa usubi kwa Wilaya za Rungwe, Kyela na Busokelo.

Kwa upande wake Ofisa Mipango kutoka Mpango wa Kudhibiti  Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana. Oscar Kaitaba alisema semina hiyo imejumuisha wajumbe kutoka Halmashauri tatu za Mkoa wa Mbeya ambazo ni Rungwe, Kyela, Busokelo.

Aidha Bw. Kaitaba alitaja wajumbe hao kuwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Waweka Hazina za Wilaya, Waganga Wakuu  Waratibu  pamoja na Maafisa Usalama wa Wilaya.



Mwisho.

Jumatatu, 8 Oktoba 2018

TANGAZO LA KUITWA KAZINI

- Hakuna maoni

Jumapili, 7 Oktoba 2018

WATANZANIA WAASWA KUPIMA MACHO MARA KWA MARA.

- Hakuna maoni

Washiriki kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi wakiwa katika maandamano kuadhimisha wiki ya afya ya macho yaliyofanyika jijini Dodoma mapema leo
Kaimu Mganga Mkuu Wa Serikali Dkt. Eliud Eliakim akipata maelezo kutoka Titus Nyange jinsi mashine ya Perkins inavyochapa nukta nundu zinazosomwa na watu wenye ulemavu wa macho wakati wa maadhimisho ya wiki ya afya ya macho duniani yanayofanyika jijini Dodoma. 

Mganga Mkuu Wa Mkoa wa Dodoma  Dkt. Charles Kiologwe akisisitiza jambo katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya afya ya macho uliofanyika katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma mapema leo.

Kaimu mganga mkuu wa serikali Dkt. Eliud Eliakim (Kushoto) akimkabidhi Kaimu Meneja wa Mpango  wa Taifa wa huduma za macho Dkt. Bernadetha Chilio kitabu cha muongozo wa utoaji huduma za macho katika maadhimisho ya wiki ya afya ya macho yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma.

Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Dodoma wakiwa wamejipanga katika mstari ili kupata huduma za macho katika maadhimisho ya wiki ya afya ya macho duniani yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere mkoani humo.

NA WAMJW-DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imewaasa Watanzania kujijengea tabia ya kupima macho mara kwa mara ili kuweza kuepuka aina mbalimbali za magonjwa ya macho ikiwemo vikope.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakimu wakati wa kufungua hafla ya kuelekea siku ya Afya ya Macho Duniani ambayo huadhimishwa kila alhamisi ya Pili ya mwezi Octoba.
“Asilimia kubwa ya magonjwa ya macho yanatibika ikiwemo upeo mdogo wa macho kuona  ambao yanazuilika kwa miwani  endapo mtu akiwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya na akigundulika ana tatizo la macho basi atapata matibabu mapema”alisema Dkt. Eliakimu.
Aidha, Dkt. Eliakimu alisema kuwa kwa Tanzania watu wasioona kabisa ni asilimia moja sawa na watu laki 5.7 huku watu wenye matatizo mbalimbali ya macho wanakadiriwa kuwa mara tatu ya wasioona kabisa sawasawa na mil.7.
Kwa mujibu wa Dkt. Eliudi amesema kuwa takwimu zinaonesha kwamba ugonjwa wa macho umepungua kutoka asilimia 4.6 mwaka 1990 na kufikia asilimia 3.4 mwaka 2015 kutokana na hamasa ya juu ya upimaji toka kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Huduma za Macho Nchini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Benadertha Chilio amesema kuwa tatizo la macho linaloongoza nchini ni mtoto wa jicho ambapo wagonjwa wanafikia kwa asilimia 50 na wengi wao ni wanawake.
“Watanzania wanatakiwa kuacha matumizi ya mitishamba na badala yake wanatikwa kuhudhuria hospitali pindi wanapohisi wanamatatizo ya macho kwani matumizi ya mitishamba kunaweza kusababisha makovu katika kioo cha jicho hivyo kunaweza kusababisha jicho kutofanya kazi kabisa” alisema Dkt. Chilio.
Aidha,Dkt. Chilio amewataka wanaohitaji tiba ya kuvaa miwani kwa ajili ya kuona vizuri waende hospitali zilizosajiliwa wapate vipimo stahiki na kupewa miwani kutokana na uwezo wao wa kuona na sio kupata huduma hizo kwenye vituo visivyosajiliwa.
Naye Mkanga Mkuu wa Mkoa Dodoma Dkt. Charles Kiologwe amewataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kupata huduma za macho ili kutokomeza ugonjwa huo  mkoani humo ili kuendelea katika shughuli za  kujenga uchumi wa viwanda.
“Nawaomba wakazi wenzangu wa Dodoma tujutokeze kwa wingi kupata huduma za macho ili kulinda afya zetu pamoja na kuondoa ule usemi uliopo vichwani kwa watu wengi kwamba kila mgonjwa wa macho anatokea Dodoma” alisema Dkt. Kiologwe.

Jumamosi, 6 Oktoba 2018

WATOA HUDUMA ZA AFYA WATAKIWA KUTOWASAHAU WATOTO KATIKA KUWAKINGA NA MAAMBUKIZI YA VVU.

- Hakuna maoni
Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikata utepe   kuashiria uzinduzi wa muongozo wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe .

Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi waliojitokeza kupima VVU katika viwanja vya Turbo mkoani Njombe mapema leo wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe .

Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisikiliza maelezo kutoka kwa mtoa huduma wakati alipotembelea mabanda ya kupima VVU na kutoa ushauri nasaha katika viwanja Turbo mkoani Njombe wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe.

Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi  Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka kitabu cha muongozo wa utoaji huduma kwa wauguzi na wakunga nchini wakati wa uzinduzi wa  Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii uliofanyika Kitaifa  Mkoani Njombe

NA WAMJW-NJOMBE


Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto imewataka watoa huduma za afya nchini kutokuwasahau watoto na vijana   katika kuwakinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa Mkakati  wa wauguzi na wakunga kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri nasaha, kupima VVU na kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa uliofanyika mapema leo mkoani Njombe.

“Bado tuna changamoto kwa watoa huduma wetu wa afya kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kutokuwapima watoto  hali ya maambukizi, kutoa dawa kwa watoto na kuwapa elimu vijana hivyo natoa rai kwa wahudumu wa afya tuweze kuweka mkakati wa kufikia makundi hayo” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amewasisitiza Wauguzi na Wakunga kutoa huduma kwa kuzingatia miiko na maadili hususan katika kutoa huduma za VVU kwa jamii inayowazunguka ikiwemo kutumia lugha nzuri na kuwa wanyenyekevu kwa wananchi.

Sambamba na hilo Dkt. Ndugulile amewaasa wanaume nchini kuacha uoga na kujitokeza kupima VVU ili kutambua afya zao na kuanza matibabu mara moja iwapo watakutwa na maambukizi.

“Tutawafuata wanaume popote walipo hususan waliopo  kwenye mikusanyiko yao ikiwemo kwenye sehemu za starehe, viwanja vya mipira , Migodini na sehemu za uvuvi ili kutoa elimu na kuwashauri wapime ili kujua afya zao” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kusudio la kufanya hivyo ni kuhakikisha kufikia malengo ya 90 90 90 ya kutokuwa na maambukizi mapya ifikapo mwaka 2030. Ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wawe wanajua hali zao za maambukizi.

Ili kutimiza malengo ya serikali katika kupambana na maambukizi, Dkt Ndugulile amesema Serikali imekuja na utaratibu wa dawa kinga ambapo dawa hizo zitatumika kwa makundi maalumu ambayo yako hatarini kupata maambukizi.

“Lakini vile vile tumekuja na utaratibu unaoitwa dawa-kinga ambazo kuna makundi ambayo tumebaini, ambayo yako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya UKIMWI. Makundi haya kuna dawa ambayo tunataka tuwape zisaidiane na kinga nyingine ili kusaidia watu wasipate maambukizi ya virusi vya UKIMWI lakini hatusemi kwamba tumeshapata kinga”. Dkt Ndugulile.

Sambamba na hayo Dkt. Ndugulile amewataka watoa huduma waende wakatoe msisitizo na kuelimisha jamii katika maeneo ambayo dawa-kinga zimeanza kufanyiwa majaribio ili kuleta matokeo chanya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amesema ukanda wa nyanda za juu kusini ni ukanda ambao una maambukizi makubwa ya VVU na serikali ya mkoa ilianza kampeni ya tohara kwa wanaume, na sasa inaelekea kwa watoto wa sekondari na shule ya msingi ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na maambukizi mapya.

“Takwimu zinaonesha sisi tuna kiwango kikubwa cha maambukizi kuliko katika ukanda ule ambao tohara kwa wanaume inaanzia katika umri mdogo kiwango cha maambukizi kiko chini lakini pia kuna mahusiano kati aya tohara ya wanaume na maambukizi ya VVU kwahiyo kama mkoa kampeni hii tumeivalia njuga chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na TAMISEMI”. Alisema Ole Sendeka.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waganga Wakuu wa mikoa na Wafawidhi wa mikoa mbalimbali pamoja na wauguzi na wakunga waliopata muongozo wa kusogeza huduma za VVU na UKIMWI karibu na jamii ikiwemo ushauri nasaha, kupima VVU na kufuatilia maendeleo ya afya za walengwa.

Ijumaa, 5 Oktoba 2018

WAZIRI UMMY AUAGIZA UONGOZI WA HOSPITALI YA ST. FRANCIS KUSHUSHA BEI ZA MATIBABU MARA MOJA.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy amwalimu akikagua vifaa vya moja ya kati ya wagonjwa waliopata Rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya St. Francis pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliefika na mama yake kupata huduma katika kituo cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya viongozi wa Mkoa wa Morogoro walioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ifakara James Lihunyo (hayupo kwenye picha)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikagua cheti cha mgonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma kisha kuelekea Hospitali ya Rufaa  ya St. Francis.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliefika na mama yake kupata huduma katika kituo cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jisnsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akieleza umuhimu wa Bima ya Afya kwa watoto kwa mmoja kati ya wamama waliofika kupata huduma za Afya katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa maelekezo kwa Baba Askofu wa jimbo la Ifakara Salutaris Libenaambae baada ya kikao cha kuboresha hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo.

Upande wa mbele wa Hospitali ya Rufaa ya St. Francis.



WAZIRI UMMY AUAGIZA UONGOZI WA HOSPITALI YA ST FRANCIS KUSHUSHA BEI ZA MATIBABU MARA MOJA.

Na WAMJW - IFAKARA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Dini ya St.Francis kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi ndani ya mwezi mmoja kabla hajarudi kufanya ukaguzi wa mara ya pili.

Ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya St Francis iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara Mkoa wa Morogoro kufuatia taarifa isiyoridhisha juu ya gharama za matibabu iyoripotiwa siku ya Octoba 3 na Televisheni ya Taifa (TBC).

Waziri Ummy alisema kwamba, Serikali inatoa Jumla ya Watumishi 243 sawa na Asilimia 68% katika Hospitali hiyo, lengo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma za  bora za afya na zenye unafuu ikiwa ni moja kati ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati anaingia madarakani.

"Kati ya Watumishi 352, watumishi 219 wanalipwa mshahara na Serikali Kuu, ambapo kila mwezi tunalipa shilingi milioni 153.7, bila kuhesabu gharama za watumishi 12 walioshikizwa kutoka Wizara ya Afya, Watumishi 12 kutoka Halmashauri ya Kilombero, Katibu tawala Morogoro ameleta watumishi 2, jumla watumishi 243, ambao ni sawa na  Asilimia 68% wanalipwa mshahara kutoka Serikali kwa Asilimia 100%". Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa mwaka wa bajeti 2015/2016 Serikali ilipeleka dawa zenye thamani ya shilingi Millioni 119.5, bajeti ya mwaka  2016/2017 shilingi milioni 177.9 huku kwa mwaka 2017/2018 dawa zenye thamani ya shilingi milioni 118.7 zilinunuliwa hospitalini hapo.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema kuwa mwongozo wa Wizara ya Afya, unazitaka Hospitali zote kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito, wazee wasio na uwezo na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupata huduma za matibabu bila malipo.

Mbali na hayo Waziri Ummy alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya bila kuwasahau watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao hupata bima ya afya kwa shilingi 50,400/=
"Wakati umefika  wa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua, na uhakika huo ni wa kupitia Bima ya Afya", alihimiza Waziri Ummy kwa msisitizo.

Waziri Ummy, aliendelea kusema kuwa, Serikali inaelekea kutunga sheria ambayo itamlazimu kila Mtanzania kupata Bima ya Afya, ili aweze kupata huduma za matibabu ya Afya bila kikwazo chochote cha fedha.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mhe. Peter Ambrose Lijualikali amemuomba Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kuikumbuka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa kujenga Hospitali ya Wilaya, jambo litaloimarisha hali ya utoaji huduma za Afya kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya St. Fransis, Baba Askofu Salutaris Libena ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kufika hospitali hapo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote ambayo yametolewa na Serikali.

" Tunaahidi kwamba tumeelewa na tutatekeleza maelekezo yote, katika lengo la kuboresha huduma za Afya kwa wananchi ", alisema Baba Askofu Libena.