Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 15 Novemba 2018

SERIKALI YAJIPANGA KUTOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VVU KWA WATOTO WACHANGA.

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta ya afya hawapo pichani wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii pamoja na masuala ya lishe leo jijini Dodoma.

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akikata utepe kuashiria kuzindua chapisho la uchambuzi  wa masuala ya lishe wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii pamoja na masuala ya lishe leo jijini Dodoma, wa pili kushoto ni Naibu Waziri OFisi ya Waziri TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kulia akionesha moja ya chapisho la uchambuzi  wa masuala ya lishe wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii pamoja na masuala ya lishe leo jijini Dodoma, wa pili kushoto ni Naibu Waziri OFisi ya Waziri TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .

Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akifuatilia mada iliyokuwa inawasilishwa na moja ya wawasilishaji hayupo pichani  wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii pamoja na masuala ya lishe leo jijini Dodoma, wa pili kulia ni Naibu Waziri OFisi ya Waziri TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .

Baadhi ya  wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta ya afya wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu  wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya jamii pamoja na masuala ya lishe leo jijini Dodoma.


NA WAMJW-DODOMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali ina mpango madhubuti wa kuhakikisha wamama wajawazito hawawaambukizi watoto walio tumboni Virusi vya Ukimwi na kipindi wanapozaliwa.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na masuala ya lishe, uliofanyika katika ukumbi wa Hazini, Jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema hadi hivi sasa asilimia 99 ya wajawazito wenye maambukizi ya VVU wanapewa huduma za kumkinga mtoto asipate maambukizi hayo huku la serikali ifikapo mwaka 2020 ni kuhakikisha  hakuna mtoto atakayezaliwa na maambukizi ya VVU.

“Sasa hivi asilimia 99 ya wanawake wajawazito wote wenye maambukizi  ya VVU tumewaingiza katika mpango wa dawa, na hiyo asilimia moja bado hatujawafikia ila kwa nguvu na msukumo tuliouweka juzi wa kuwasainisha Wakuu wa Mikoa kwenda kufuatilia masuala ya afya ya mama na mtoto, tunaamini hakuna mtoto yeyote Tanzania atakayezaliwa na maambukizi ya UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy.

Katika Uzinduzi huo, Waziri Ummy ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Philipo Mpango  inavyojikita katika mipango ya kuendeleza wanawake na watoto kwa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na masuala ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) imefanya uchambuzi wa bajeti katika sekta mtambuka ya jamii, hususani katika elimu, afya, Virusi vya Ukimwi, maji, usafi wa mazingira na lishe kwa lengo la kuboresha upangaji na utekelezwaji wa masuala ya mama na mtoto.

Pamoja na hayo, uzinduzi wa machapisho hayo umelenga kupunguza tatizo la lishe linalosababisha udumavu kwa watoto walio katika umri mdogo. Ambapo katika ripoti iliyotolewa katika mkutano wa IMF na Benki ya dunia uliofanyika nchini Indonesia mwezi Oktoba mwaka 2018, inaonesha Tanzania inashika nafasi ya 128 kati ya nchi 157 duniani katika kipimo cha ubora wa nguvukazi  katika uwekezaji wa rasilimali watu hususani katika sekta ya afya na elimu ya lishe.

Kufuatia hali hiyo, Tanzania inaonekana kuwa na matatizo ya udumavu, elimu ya lishe na afya kwa watoto wenye umri mdogo ambapo serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wazazi na jamii kwa ujumla ili kupambana na tatizo la udumavu. Na kufikia mwaka 2015 tatizo la udumavu limeshuka kutoka asilimia 34 kutoka asilimia 42 mwaka 2010. Alisema Waziri huyo.

Tatizo la lishe limeonekana kupungua nchini huku viashiria vya tatizo hilo vikipungua ambavyo ni uzito pungufu umeshuka kutoka asilimia 16 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 14 mwaka 2015/16, pamoja na ukondefu wa mwili kuendelea kubakia chini ya asilimia 5 kwa mwaka 2015/16.


TANGAZO LA KUITWA KAZINI

ORODHA YA MAJINA IMEAMBATANISHWA HAPA CHINI





Jumatano, 14 Novemba 2018

TANZANIA INATOA HUDUMA ZA CHANJO KWA ASILIMIA 98.

Katibu Mkuu Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  (Idara Kuu ya afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na baadhi ya wataalam na wadau wa afya hawapo pichani wakati wa mkutano wa mwaka wa kujadili mafanikio na chanagamoto za sera ya afya uliofanyika leo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  (Idara Kuu ya afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya wa kwanza kulia akifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikiwasilishwa na mmoja wa wawasilishaji mada hayupo pichani mkutano wa mwaka wa kujadili mafanikio na chanagamoto za sera ya afya uliofanyika leo jijini Dodoma.

Mkurugenzi  Msaidizi wa Tathimini na Ufuatiliaji  Wizara ya Afya Tumainieli Macha akiwasilisha mada kwa wataalam na wadau wa afya  wakati wa mkutano wa mwaka wa kujadili mafanikio na chanagamoto za sera ya afya uliofanyika leo jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Sarah Maongezi  akiongea na baadhi ya wataalam na wadau wa afya hawapo pichani wakati wa mkutano wa mwaka wa kujadili mafanikio na chanagamoto za sera ya afya uliofanyika leo jijini Dodoma.

Baadhi ya wadau na wataalam wa afya nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  (Idara Kuu ya afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya hayupo pichani wakati wa mkutano wa mwaka wa kujadili mafanikio na chanagamoto za sera ya afya uliofanyika leo jijini Dodoma.


NA WAMJW- DODOMA 

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kutoa huduma za chanjo kwa magonjwa yanayohitaji huduma hiyo kwa asilimia 98 Afrika Mashariki. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa Mkutano mkuu wa mwaka wa kujadili masuala mbalimbali ya afya uliofanyika jijini Dodoma. 

"Tanzania tumepiga hatua katika kutoa huduma za chanjo kwa asilimia 98 ambapo tumetanguliwa na wenzetu wa Rwanda kwa asilimia 99 ila tunaamini mpaka kufikia mwakani tutakua mbele zaidi" alisema Dkt. Ulisubisya. 

Aidha, Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka hivi sasa Tanzania inatoa chanjo  ya Surua na Rubella kwa asilimia 78 ambapo bado lengo halijatimia. 

Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kutibu wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 99 kwa wote waliogundulika wana vimelea vya ugonjwa huo. 

Dkt. Ulisubisya amesema kuwa pia katika mkutano huo wanajadili na kutoka na mikakati mbalimbali ya kuibua  maambukizi mapya ya  Virusi vya Ukimwi nchini ili kuweza kufikia lengo la 90 90 90 . 

Mbali na hayo Dkt. Ulisubisya amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo katika jamii kutekeleza afua za kupambana na ugonjwa wa Malaria katika mkutano huo watahakikisha wanatoka na afua za kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo nchini. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI  Dkt.  Zainabu Chaula amesema kuwa mpaka hivi sasa Serikali imepata fedha ya kukarabati vituo 350 na kuweka vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya huduma za mama na mtoto. 

Naye Mwakilishi wa watoa huduma za Afya binafsi Dkt.  Josephine Balati amesema kuwa mpaka sasa zaidi ya vituo vya afya binafsi 190 vimeweza kuingia mkataba na Serikali katika kutoa huduma za afya nchini . 

"Katika vituo binafsi vya afya 190 vilivyoingia mkataba na Serikali vituo 84 ni vya mashirika ya dini na 106 ni vya watu binafsi" alisema Dkt. Balati . 

Mkutano huo wa kila mwaka  unaokutanisha wataalam na wadau mbalimbali wa afya una lengo la kupitia changamoto na mafanikio  sera ya afya inayotumika katika kuboresha afya za Watanzania. 


TAARIFA KWA UMMA - TAMKO LA WIZARA KUHUSU SIKU YA KISUKARI DUNIANI TAREHE 14 NOVEMBA, 2018.






Jumanne, 13 Novemba 2018

DKT. MPOKI AELEZA UCHOVU NI SABABU ZA AJALI ZA BARABARANI

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Dkt. Mpoki Ulisubisya akizindua kitabu cha mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi  Wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje  ya hospitali nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa idara ya dharura hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt.Juma Mfinanga akipokea  kitabu hicho  cha mafunzo  kutoka kwa Katibu Mkuu  Dkt.Mpoki  Mara baada ya kukizindua

Picha ya Pamoja ya watumishi toka wizara ya Afya, hospitali, Shirika la msalaba Mwekundu, Chuo kikuu MUHAS  Pamoja na majeshi ambao kwa Pamoja watatekeleza mpango huo  nchini.


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa moja ya sababu za ajali barabarani, ni uchovu wa madereva.

Dkt. Mpoki ameyasema leo Novemba 13,2018 wakati wa kufungua mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje ya Hospitali nchini.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Mpoki amelitaka jeshi la Polisi nchini kuangalia namna ya kuweka utaratibu wa madereva kubadilishana kwani suala la uchovu linachangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.

Aidha,akitolea mfano suala la uchovu, dereva kutoka Mwanza au Bukoba kwenda Dar es Salaam, basi ashuke Singida ili aingie dereva mwingine kumalizia safari na hiyo itasaidia kuepusha ajali.

“Tumemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi atusaidie kama mchango wa Polisi katika kupunguza ajali kwa kuhakikisha kwamba wanaweka utaratibu wa madereva wanaendesha kwa muda maalum. Kuliko ilivyo sasa madereva wanaweza kuendesha siku nzima, Hivyo wanakuwa wachovu na kuchangia kwa kiasi kikubwa sana ajali mbalimbali barabarani” amesema Dkt. Mpoki.

Hata hivyo ameeleza kuwa, mpango huo ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imewekeza kuingilia kati pale watu wanapokuwa wameumia, ambapo huko nyuma maisha ya watu wengi yalikuwa yakipotea kwa sababu vifaa vilikuwa vinachelewa sana kufika mahali tukio na hivyo kushirikiana na Benki ya dunia kwa kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya uwekezaji na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za wataalam.

“Katika fani ya tiba, Tunazungumzia saa ya kwanza ni saa muhimu sana kusaidia mtu aliyepata changamoto ya ajali. Hawa watakuwa chachu ya kusaidia kati ya wale waliopata mafunzo.” Amesema Dkt. Mpoki

Dkt. Mpoki ameongeza kuwa katika afua hiyo,itakuwa na vituo maalum   vyenye miundombinu ya kutoa huduma hizo ambapo awamu ya kwanza itaanzia Dar e Salaam hadi Ruaha Mbuyuni na kwa kila kituo kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, vifaa vya zima moto na kuweka utaratibu wa kusafirisha majeruhi kwa kushirikiana  majeshi yakiwemo la Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Zimamoto pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD).

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (MUHAS), Profesa Appolenary Kamuhabwa  amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwani  kutakuwa na mfumo thabiti wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura watokanao na ajali na  ni hatua muhimu  kwani bila afya bora, wananchi hawawezi kutumikia nchi hususani  ajenda ya Serikali ya  viwanda.

Profesa Kamuhabwa amesema katika mpanguo huo, utakuwa na vituo mbalimbali vya Afya vitakavyokuwa vikitoa huduma za dharura ikiwemo: Vituo vya Afya vya Kimara (Dar es Salaam), Tumbi,  Chalinze (Pwani), Mikese, St, Kizito, Doma-Mikumi (Morogoro) na Ruaha Mbuyuni (Iringa).

Jumanne, 6 Novemba 2018

- Hakuna maoni
Makamu wa Rais Mama  Samia Suluhu  Hassan wakibadilishana mawazo  na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee  na Watoto  Mhe.Ummy Mwalimu tayari kwa UzinduZi wa Kampeni ya Tuwajushe  Salama kwenye  ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo

Makamu wa Rais akipitia  Ratiba  ya uzinduzi  wa Kampeni hiyo na MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.Kampeni hiyo ina  lengo la kuhamasisha viongozi wa Serikali,Dini,Mashirika  yasiyo  ya kiserikali,wadau wa  Maendeleo na datos huduma za afya kuchangia katika juhudi za  kitaifa za kupunguza  vifo vitokanavyo  na uzazi  na watoto  wachanga


Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakifurahia Mambo wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimuelezea Makamu wa Rais vinavyoonesha ubora na mapungufu ya utoaji wa huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Jiongeze, Tuwavushe Salama.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizindua rasmi kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama yenye lengo la kuhamasisha viongozi wa Serikali, Dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Wadau wa Maendeleo, Watoa huduma za afya, Familia na jamii kwa ujumla ili kuchangia katika juhudi za taifa za kupunguza vifo vinyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ahadi ya makubaliano ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe wa kitabu cha muongozo wa pili wa kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati uzinduzi huo.



MAMA SAMIA  AWASAINISHA WAKUU WA MIKOA AHADI YA MAKUBALIANO YA UWAJIBIKAJI WAKUPUNGUZA  VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI. 

NA WAMJ-DODOMA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasainisha Wakuu wa mikoa yote nchini AHADI ya makubaliano ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo cha Watoto wachanga nchini. 

Hayo yamefanyika leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa inayolenga kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi nchini inayojulikana kwa jina la "JIONGEZE TUWAVUSHW SALAMA "  jijini Dodoma. 

"Leo nawasainisha makubaliano haya wakuu wa mikoa mkaifanyie kazi na kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga ntahitaji taarifa ya viashiria vya afya ya uzazi kila baada ya miezi 6 katika ofisi yangu", alisema Mhe. Samia. 

Aidha,Mhe. Samia amesema kuwa mbali na wakuu wa mikoa kuwasilisha taarifa hizo  kwake pia  kila baada ya miezi 3 wawasilishe Wizara ya Afya ili kuzifanyia kazi taarifa hizo na kutatua changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi. 

Kwa mujibu wa Mhe. Samia amesema kuwa mbali na vikwazo vingine vinavyosababisha vifo vitokanavyo na uzazi tunatakiwa kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua. 

Mbali na hayo Mhe. Samia Suluhu amesema kuwa mapambano haya zidi ya vifo vitokanavyo na uzazi ni la kila mtu kuanzia, Viongozi wa Serikali,  Jamii nzima inaotuzunguka, watumishi wa sekta ya afya, wanahabari pamoja na viongozi wa dini. 

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa takwimu ya mwaka  2017 za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa wanawake milioni 2. 2 kila mwaka wanapata ujauzito na asilimia 85 hujifungua bila ya shida na asilimia 15 sawa na laki 3. 3 hupata matatizo mbalimbali yatokanayo na uzazi. 

"Kuna sababu mbalimbali zinazochangia vifo vitokanavyo na uzazi ikiwa kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, asilimia 28, kifafa cha mimba asilimia 17, uchungu pingamizi asilimia 11, uambukizo asilimia 11 na mengineyo asilimia 11" alisema Waziri Ummy. 

Aidha,Waziri Ummy amesema kuwa wajawazito wanatakiwa kuhudhuria kliniki kwani ni asilimia 60 ndio wanaohudhuria kliniki angalau mara nne . 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binirith Mahenge amesema kuwa mkoa wake umepiga hatua katika ujenzi wa vituo vya afya mpaka kufikia 21 ndani ya miaka 3. 

"Licha ya ujenzi huo pia Serikali imeongeza bajeti ya dawa kwa upande wa mkoa wa Dodoma kutoka milioni 900 mpaka kufikia bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2018" alisema Dkt. Mahenge.

Jumapili, 4 Novemba 2018

WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI





Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Manyara kuona huduma zinazotolewa hapo. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Catherine Magali.
 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi Mwenyekiti wa kamati ya mkoa wa Manyara ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wa kike Bw. Anza Amen Ndosa miongozo ya utendaji wa kamati hiyo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na wazee wanaolelewa katika kituo cha kulelea wazee cha Sarame kilichopo wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimulekeza mbunge wa Babati vijijini, Jitu Son alama ambazo zimewekwa katika dawa za serikali ili kuzilinda kuuzwa katika maduka ya watu binafsi. Kulia ni mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu.

WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI 

Na.WAMJW-BABATI
 
Serikali imesema ina mpango wa kuanzisha huduma ya bima ya afya ambayo itamwezesha mwananchi kujichagulia “Kifurushi” kulingana na uwezo wake.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokua akiongea na wafanyakazi wa kituo cha afya cha Magugu pamoja na wananchi wa kata ya Magugu iliyopo wilayani Babati katika mkoa wa Manyara, wakati alipotembelea kituo hicho cha afya.

Dkt. Ndugulile amesema, kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, serikali sasa chini  ya Wizara ya Afya,  imeamua kutengeneza mkakati mpya wa huduma za bima za afya zitakazokidhi mahitaji ya wananchi kulingana na kipato chao.

“Serikali imeanza mchakato wa mkakati mpya wa bima za afya utakaokua na vifurushi viwili, kimoja kinaitwa Jipimie na kingine Dunduliza ambavyo vitaanza hivi karibuni ambapo Vifurushi hivi vimelenga wananchi wa vipato tofauti, ambapo katika kifurushi cha Jipimie mwananchi ana uwezo wa kuchagua aina ya gharama za huduma za bima ya afya kulingana na kipato chake. Lakini katika kifurushi cha Dunduliza mwananchi atakua na wigo mpana wa kulipa kidogo kidogo kifurushi chake atakachoona kinafaa lakini akiwa anapewa huduma za bima ya afya kama kawaida”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Katika kuboresha huduma za afya nchini, Dkt. Ndugulile amesema serikali ina mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2020. Na itakua ni lazima na siyo jambo la hiyari kwa sababu magonjwa huwa hayana hodi yanapompata mtu, hivyo kupelekea wananchi wengi kushindwa kugharamia matibabu kwa sababu wanakua hawajajiandaa kukabili changamoto za kugharamia matibabu.

Pamoja na hayo Naibu waziri huyo alionekana kutoridhishwa na hali ya utoaji huduma  kituo cha afya cha Magugu huku ujenzi wa wodi, maabara na nyumba za watumishi ukichelewa pamoja na kwamba serikali ilipeleka Shilingi Milioni 400 za ukarabati na ujenzi wa majengo mapya.

Aidha, Dkt. Ndugulile alionekana kuchukizwa na baadhi ya watoa huduma za afya kituoni hapo kuwaandikia wagonjwa kununua dawa katika maduka binafsi wakati dawa hizo zikiwepo katika stoo ya kuhifadhia dawa.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Ndugulile alimuagiza mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Eliaremisa Palangyo kumrudishia mgonjwa aliyenunua dawa katika duka binafsi Bw. Onesphory Mfugale kurudishiwa hela yake kiasi cha Shilingi 27,000.
.
Naibu waziri huyo yupo katika ziara ya siku tatu katika mkoa wa Manyara ambapo atatembelea Hospitali ya Hydom iliyopo wilaya ya Hanang kisha kuelekea Simanjiro ambapo atakagua kazi mbadala za wasichana wa kimasai za ujasiriamali pia atatembelea kituo cha afya cha Orkesumet.

Jumatano, 31 Oktoba 2018

SERIKALI YARAHISISHA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA VIFO VINAVYOTOKEA KATIKA NGAZI YA JAMII NCHINI.

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki  Ulisubisya akiongea na baadhi ya Wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali na Maafisa Afya mkoani Iringa wakati wa kukabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo ngazi ya jamii kwa Maafisa Afya mkoani humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki  Ulisubisya katikati akionesha Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo ngazi ya jamii pamoja na Maafisa afya wa kata mbalimbali Mkoani Iringa

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa iringa Bw. Fikira Kissimba akiongea nna na baadhi ya Wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali na Maafisa Afya mkoani Iringa wakati wa kukabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo ngazi ya jamii kwa Maafisa Afya mkoani humo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki  Ulisubisyakushoto akimkabidhi Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafinga Mji bw. Fredrick Kayombo kulia wakati wa kukabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo ngazi ya jamii kwa Maafisa Afya mkoani humo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Tathimini kutoa Wizara ya Afya Bw. Tumainieli Macha wa kwanza kulia akifuatilia kwa makini maelekezo ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki  Ulisubisya hayupo pichani wakati wa kukabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu za vifo ngazi ya jamii kwa Maafisa Afya mkoani Iringa.

NA WAMJW-IRINGA


SERIKALI kupitia Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imerahisisha ukusanyaji wa takwimu za vifo vinavyotokea kwenye ngazi ya jamii nchini kwa kugawa vifaa maalumu vya kukusanyia takwimu hizo kwa Maafisa afya katika kata za mkoa wa Iringa.

Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki  Ulisubisya wakati akikabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia takwimu hizo  kwa Maafisa Afya leo  Mkoani Iringa.

“Takwimu zitakazokusanywa kuhusu vifo na  Maafisa hawa wa afya  kutokana na Mifumo hii zitawasaidia madaktari kujadili changamoto pamoja na sababu za vifo hivyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo hayo na kuweza kupunguza idadi ya vifo nchini” alisema Dkt. Ulisubisya.

Aidha,Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa takwimu hizo zikikusanywa kikamilifu zitasaidia kutoa elimu kwa jamii na kupunguza imani za kishirikina kwa wananchi kwani zitaleta picha sahihi ya kugundua vyanzo vya  vifo hivyo kwenye jamii husika.

Hata hivyo Dkt. Ulisubisya amewataka maafisa hao kutumia vifaa hivyo kwa matumizi ya kazi ya kukusanyia takwimu na sio matumizi binafsi na kama itatokea afisa afya yeyote atakayehama kituo cha kazi  basi arudishe  ofisini kwa ajili ya mtumishi mwingine atakayekuja.

Kawa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa iringa Bw. Fikira Kissimba amesema kuwa mfumo huo wa ukusanyaji taarifa zitasaidia pia uandikishwaji wa mirathi ya marehemu wakati ndugu husika anapokwenda kufungua mirathi yake mahakamani.

Naye Mratibu wa usajili wa Takwimu wa Masuala muhimu ya Binadamu nchini kutoka wizara ya afya  Dkt. Gregory Kabadi amesema kuwa jumla ya Kompyuta kibao (Tablets) zilizogawiwa ni 106 kwa kila kata ya mkoani Iringa na thamani yake ni takribani shilingi Milioni 61.5.

Aidha , Dkt Kabadi amesema kuwa zoezi hilo limeanza kwa majaribio katika halmashauri tano kwenye mikoa mitatu ikiwemo Pwani,Tanga na Morogoro na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mifumo hiyo katika mkoa wa Iringa kabla ya kutumika nchi nzima.

Kwa upande  wake Afisa afya wa kata ya Kitwilu Bw. Wilson Ntagondwa amesema kuwa kupitia mfumo huo waliokabidhiwa itawasaidia kukusanya takwimu kwa urahisi hivyo kupelekea kujua sababu zinazosababisha vifo na kusaidia kupanga maendeleo.

WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA

- Hakuna maoni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akinawa mikono baada ya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji  wenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo  Elfu 30 kutoka kijiji cha  Rurumakilichopo kata ya Kiomboi wilaya ya Ilamba, ikiwa ni muendelezo wa zaiara yake Mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia chanjo zilizohifadhiwa katika boksi maalum wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi iliyopo wilayani Iramba katika Mkoa wa Singida. Kushoto ni muhudumu wa chanjo Christowelo Palangyo na Dkt. Abbas Sepoko (kulia).

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiionesha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iramba (hawapo pichani) dawa za serikali zilizo na alama maalumu ili zisiuzwe katika maduka binafsi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Gwaula.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa Diwani wa Kinyambuli Rubeni Charles wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho ili kujionea hali ya ujenzi wa kituo pamoja na utoaji huduma za afya kijijini hapo.


WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA

Na WAMJW-MKALAMA- SINGIDA

Watanzania kote nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za maisha ikiwemo kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na udumavu kwa watoto wachanga.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kituo cha afya na kuongea na wananchi.

"Serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na afya bora, ndo maana tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza afya zenu ikiwemo kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama kwa afya zetu pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha". Alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha,Naibu waziri huyo ameendelea kusisitiza kwa upande wa  akina mama walio na watoto wadogo chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na kuwapa vyakula vyenye lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto kukua kiakili na kuwa  na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo kwa mtoto ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na kukua vizuri.

"Siku 1000 za mwanzo tunaanza kuzihesabu toka mimba inapotungwa, anapozaliwa na kufikisha miaka miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama kumnyonyesha mtoto ikiwa ni pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili mtoto aweze kuwa na afya bora na ubongo unaofanya kazi sawa sawa". Alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli kwa kuzitendea haki fedha zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili kusaidia kupanua kituo hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi.

"Nawapongeza sana wananchi wa Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo hiki, ninachokiona hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili pongezi na fedha za serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki". Alisema Dkt. Ndugulile.

Hata hivyo Dkt.Ndugulile  amesema serikali bado ina nia kubwa ya kuboresha hali ya utoaji huduma za afya nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama ukitarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu. 

Dkt. Ndugulile amesema mkoa wa Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida DC.

Kwa upande wake diwani wa Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.

"Kwakweli naishukuru sana serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji hiki walikua wanapata shida sana kupata huduma za afya hasa wakinamama wajawazito ambao tulipoteza wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu". Alisema Rubeni.

Jumanne, 30 Oktoba 2018

SERIKALI YAAHIDI KUPELEKA GARI YA WAGONJWA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA MANYONI

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile  akikagua cheti cha mgonjwa katika wodi ya akina mama wakati alipotembelea Hospitali ya wilaya ya Manyoni kuona hali ya utoaji huduma za afya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akikagua madaftari ya wagonjwa waliolazwa katika wodi ya akina mama wakati alipotembelea Hospitali ya wilaya ya Manyoni kuona hali ya utoaji huduma za afya. kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo Bi. Rahabu Solomon.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (Kulia) akifafanua jambo wakati alipotembelea kitengo cha kuzalisha chakula cha lishe kwa mama wajawazito na watoto katika Hospitali ya Mtakatifu Gasper. Kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali hiyo Fr. Seraphine Lesiriam.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi waliokuwa wakisubiri huduma Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida wakati alipofanya ziara hospitalini hapo kuona hali ya utoaji wa huduma za afya.


SERIKALI YAAHIDI KUPELEKA GARI YA WAGONJWA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA MANYONI

NA WAMJW-SINGIDA

Serikali imetangaza neema ya kupeleka gari ya  wagonjwa (Ambulance)  katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni ili kutatua tatizo linaloikabidi Wilaya hiyo hususan ya vifo vitokanavyo na uzazi.

Ahadi hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipoitembelea hospitali hiyo kwa lengo la kutazama utoaji wa huduma za afya ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu katika mkoa wa Singida.

Dkt. Ndugulile amefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza kero kutoka kwa wananchi wanaotumia hospitali hiyo ambapo wengi walisema kungekuwepo na gari ya wagonjwa kungeepusha vifo vya akina mama wajawazito na watoto pamoja na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

"Naomba niwaahidi wananchi wa Manyoni, Serikali imeagiza magari ya kubebea wagonjwa ambayk yanaweza kufika mwezi Disemba mwaka huu,hivyo nitahakikisha katika mgao wa magari hayo basi na hospitali hii ya Wilaya  inapata gari moja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa hapa. Alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt.Ndugulile aliahidi kuwatafutia wataalam wa Afya watakaoweza kwenda  kupunguza uhaba wa watumishi wanaokabiliana nayo hospitali hiyo

Naye Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Atupele Mohamed alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa majengo ikiwemo chumba cha huduma za uzazi ambapo uwezo wake kwa mwezi ni  kuzalisha akina mama 90 lakini kwa sasa huzalisha  wastani wa akina mama 400.

Aidha, Dkt. Atupele alisema Hospitali hiyo ina upungufu mkubwa wa watumishi wenye sifa, ambapo ina jumla ya watumishi 107 sawa na asilimia 53 ya watumishi wanaohitajika.

Dkt. Atupele alitaja   uhaba mkubwa wa watumishi hao  ni Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa mionzi na wataalamu wa kutoa huduma za usingizi.

Katika Wilaya hiyo Naibu Waziri huyo aliweza kutembelea  kutembelea kituo cha kulea wazee na wasiojiweza cha Sukamahela pamoja na Hospitali ya rufaa ya Mtakatifu Gasper iliyopo  Itigi na  kuridhika na hali ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali hiyo.