Alhamisi, 15 Novemba 2018
SERIKALI YAJIPANGA KUTOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VVU KWA WATOTO WACHANGA.
Alhamisi, Novemba 15, 2018
-
Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali ina mpango madhubuti wa
kuhakikisha wamama wajawazito hawawaambukizi watoto walio tumboni Virusi vya
Ukimwi na kipindi wanapozaliwa.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa
machapisho ya uchambuzi wa bajeti katika sekta ya maendeleo ya jamii ikiwa ni
pamoja na masuala ya lishe, uliofanyika katika ukumbi wa Hazini, Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema hadi hivi sasa asilimia 99 ya
wajawazito wenye maambukizi ya VVU wanapewa huduma za kumkinga mtoto asipate
maambukizi hayo huku la serikali ifikapo mwaka 2020 ni kuhakikisha hakuna mtoto atakayezaliwa na maambukizi ya VVU.
“Sasa hivi asilimia 99 ya wanawake wajawazito wote
wenye maambukizi ya VVU tumewaingiza
katika mpango wa dawa, na hiyo asilimia moja bado hatujawafikia ila kwa nguvu
na msukumo tuliouweka juzi wa kuwasainisha Wakuu wa Mikoa kwenda kufuatilia
masuala ya afya ya mama na mtoto, tunaamini hakuna mtoto yeyote Tanzania
atakayezaliwa na maambukizi ya UKIMWI”. Amesema Waziri Ummy.
Katika Uzinduzi huo, Waziri Ummy ameipongeza
Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kwa Waziri wake Mhe. Dkt. Philipo
Mpango inavyojikita katika mipango ya
kuendeleza wanawake na watoto kwa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na
masuala ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na
Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) imefanya uchambuzi wa bajeti katika sekta
mtambuka ya jamii, hususani katika elimu, afya, Virusi vya Ukimwi, maji, usafi
wa mazingira na lishe kwa lengo la kuboresha upangaji na utekelezwaji wa
masuala ya mama na mtoto.
Pamoja na hayo, uzinduzi wa machapisho hayo
umelenga kupunguza tatizo la lishe linalosababisha udumavu kwa watoto walio
katika umri mdogo. Ambapo katika ripoti iliyotolewa katika mkutano wa IMF na
Benki ya dunia uliofanyika nchini Indonesia mwezi Oktoba mwaka 2018, inaonesha
Tanzania inashika nafasi ya 128 kati ya nchi 157 duniani katika kipimo cha
ubora wa nguvukazi katika uwekezaji wa
rasilimali watu hususani katika sekta ya afya na elimu ya lishe.
Kufuatia hali hiyo, Tanzania inaonekana kuwa na
matatizo ya udumavu, elimu ya lishe na afya kwa watoto wenye umri mdogo ambapo
serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wazazi na
jamii kwa ujumla ili kupambana na tatizo la udumavu. Na kufikia mwaka 2015
tatizo la udumavu limeshuka kutoka asilimia 34 kutoka asilimia 42 mwaka 2010.
Alisema Waziri huyo.
Tatizo la lishe limeonekana kupungua nchini huku
viashiria vya tatizo hilo vikipungua ambavyo ni uzito pungufu umeshuka kutoka
asilimia 16 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 14 mwaka 2015/16, pamoja na
ukondefu wa mwili kuendelea kubakia chini ya asilimia 5 kwa mwaka 2015/16.
Jumatano, 14 Novemba 2018
TANZANIA INATOA HUDUMA ZA CHANJO KWA ASILIMIA 98.
Jumatano, Novemba 14, 2018
-
Hakuna maoni
NA WAMJW- DODOMA
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kutoa huduma za chanjo kwa magonjwa yanayohitaji huduma hiyo kwa asilimia 98 Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati wa ufunguzi wa Mkutano mkuu wa mwaka wa kujadili masuala mbalimbali ya afya uliofanyika jijini Dodoma.
"Tanzania tumepiga hatua katika kutoa huduma za chanjo kwa asilimia 98 ambapo tumetanguliwa na wenzetu wa Rwanda kwa asilimia 99 ila tunaamini mpaka kufikia mwakani tutakua mbele zaidi" alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha, Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka hivi sasa Tanzania inatoa chanjo ya Surua na Rubella kwa asilimia 78 ambapo bado lengo halijatimia.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa mpaka sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kutibu wagonjwa wa Kifua Kikuu kwa asilimia 99 kwa wote waliogundulika wana vimelea vya ugonjwa huo.
Dkt. Ulisubisya amesema kuwa pia katika mkutano huo wanajadili na kutoka na mikakati mbalimbali ya kuibua maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi nchini ili kuweza kufikia lengo la 90 90 90 .
Mbali na hayo Dkt. Ulisubisya amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo katika jamii kutekeleza afua za kupambana na ugonjwa wa Malaria katika mkutano huo watahakikisha wanatoka na afua za kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa mpaka hivi sasa Serikali imepata fedha ya kukarabati vituo 350 na kuweka vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya kibingwa ya huduma za mama na mtoto.
Naye Mwakilishi wa watoa huduma za Afya binafsi Dkt. Josephine Balati amesema kuwa mpaka sasa zaidi ya vituo vya afya binafsi 190 vimeweza kuingia mkataba na Serikali katika kutoa huduma za afya nchini .
"Katika vituo binafsi vya afya 190 vilivyoingia mkataba na Serikali vituo 84 ni vya mashirika ya dini na 106 ni vya watu binafsi" alisema Dkt. Balati .
Mkutano huo wa kila mwaka unaokutanisha wataalam na wadau mbalimbali wa afya una lengo la kupitia changamoto na mafanikio sera ya afya inayotumika katika kuboresha afya za Watanzania.
Jumanne, 13 Novemba 2018

DKT. MPOKI AELEZA UCHOVU NI SABABU ZA AJALI ZA BARABARANI
Jumanne, Novemba 13, 2018
-
Hakuna maoni
![]() |
| Mkurugenzi wa idara ya dharura hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt.Juma Mfinanga akipokea kitabu hicho cha mafunzo kutoka kwa Katibu Mkuu Dkt.Mpoki Mara baada ya kukizindua |
![]() |
| Picha ya Pamoja ya watumishi toka wizara ya Afya, hospitali, Shirika la msalaba Mwekundu, Chuo kikuu MUHAS Pamoja na majeshi ambao kwa Pamoja watatekeleza mpango huo nchini. |
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa moja ya sababu za ajali barabarani, ni uchovu wa madereva.
Dkt. Mpoki ameyasema leo Novemba 13,2018 wakati wa kufungua mafunzo ya watoa huduma za tiba, uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali na wagonjwa wenye dharura mbalimbali nje ya Hospitali nchini.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Mpoki amelitaka jeshi la Polisi nchini kuangalia namna ya kuweka utaratibu wa madereva kubadilishana kwani suala la uchovu linachangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.
Aidha,akitolea mfano suala la uchovu, dereva kutoka Mwanza au Bukoba kwenda Dar es Salaam, basi ashuke Singida ili aingie dereva mwingine kumalizia safari na hiyo itasaidia kuepusha ajali.
“Tumemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi atusaidie kama mchango wa Polisi katika kupunguza ajali kwa kuhakikisha kwamba wanaweka utaratibu wa madereva wanaendesha kwa muda maalum. Kuliko ilivyo sasa madereva wanaweza kuendesha siku nzima, Hivyo wanakuwa wachovu na kuchangia kwa kiasi kikubwa sana ajali mbalimbali barabarani” amesema Dkt. Mpoki.
Hata hivyo ameeleza kuwa, mpango huo ni hatua ya kwanza ambayo Serikali imewekeza kuingilia kati pale watu wanapokuwa wameumia, ambapo huko nyuma maisha ya watu wengi yalikuwa yakipotea kwa sababu vifaa vilikuwa vinachelewa sana kufika mahali tukio na hivyo kushirikiana na Benki ya dunia kwa kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya uwekezaji na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za wataalam.
“Katika fani ya tiba, Tunazungumzia saa ya kwanza ni saa muhimu sana kusaidia mtu aliyepata changamoto ya ajali. Hawa watakuwa chachu ya kusaidia kati ya wale waliopata mafunzo.” Amesema Dkt. Mpoki
Dkt. Mpoki ameongeza kuwa katika afua hiyo,itakuwa na vituo maalum vyenye miundombinu ya kutoa huduma hizo ambapo awamu ya kwanza itaanzia Dar e Salaam hadi Ruaha Mbuyuni na kwa kila kituo kutakuwa na gari la kubebea wagonjwa, vifaa vya zima moto na kuweka utaratibu wa kusafirisha majeruhi kwa kushirikiana majeshi yakiwemo la Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Zimamoto pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD).
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma (MUHAS), Profesa Appolenary Kamuhabwa amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwani kutakuwa na mfumo thabiti wa kuwahudumia wagonjwa wa dharura watokanao na ajali na ni hatua muhimu kwani bila afya bora, wananchi hawawezi kutumikia nchi hususani ajenda ya Serikali ya viwanda.
Profesa Kamuhabwa amesema katika mpanguo huo, utakuwa na vituo mbalimbali vya Afya vitakavyokuwa vikitoa huduma za dharura ikiwemo: Vituo vya Afya vya Kimara (Dar es Salaam), Tumbi, Chalinze (Pwani), Mikese, St, Kizito, Doma-Mikumi (Morogoro) na Ruaha Mbuyuni (Iringa).
Jumanne, 6 Novemba 2018

Jumanne, Novemba 06, 2018
-
Hakuna maoni
![]() |
| Baadhi ya Wakuu wa Mikoa wakifurahia Mambo wakati wa uzinduzi wa Kampeni hiyo |
![]() |
| Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ahadi ya makubaliano ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga. |
MAMA SAMIA AWASAINISHA WAKUU WA MIKOA AHADI YA MAKUBALIANO YA UWAJIBIKAJI WAKUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI.
NA WAMJ-DODOMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasainisha Wakuu wa mikoa yote nchini AHADI ya makubaliano ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo cha Watoto wachanga nchini.
Hayo yamefanyika leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa inayolenga kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi nchini inayojulikana kwa jina la "JIONGEZE TUWAVUSHW SALAMA " jijini Dodoma.
"Leo nawasainisha makubaliano haya wakuu wa mikoa mkaifanyie kazi na kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga ntahitaji taarifa ya viashiria vya afya ya uzazi kila baada ya miezi 6 katika ofisi yangu", alisema Mhe. Samia.
Aidha,Mhe. Samia amesema kuwa mbali na wakuu wa mikoa kuwasilisha taarifa hizo kwake pia kila baada ya miezi 3 wawasilishe Wizara ya Afya ili kuzifanyia kazi taarifa hizo na kutatua changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi.
Kwa mujibu wa Mhe. Samia amesema kuwa mbali na vikwazo vingine vinavyosababisha vifo vitokanavyo na uzazi tunatakiwa kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.
Mbali na hayo Mhe. Samia Suluhu amesema kuwa mapambano haya zidi ya vifo vitokanavyo na uzazi ni la kila mtu kuanzia, Viongozi wa Serikali, Jamii nzima inaotuzunguka, watumishi wa sekta ya afya, wanahabari pamoja na viongozi wa dini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa takwimu ya mwaka 2017 za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa wanawake milioni 2. 2 kila mwaka wanapata ujauzito na asilimia 85 hujifungua bila ya shida na asilimia 15 sawa na laki 3. 3 hupata matatizo mbalimbali yatokanayo na uzazi.
"Kuna sababu mbalimbali zinazochangia vifo vitokanavyo na uzazi ikiwa kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, asilimia 28, kifafa cha mimba asilimia 17, uchungu pingamizi asilimia 11, uambukizo asilimia 11 na mengineyo asilimia 11" alisema Waziri Ummy.
Aidha,Waziri Ummy amesema kuwa wajawazito wanatakiwa kuhudhuria kliniki kwani ni asilimia 60 ndio wanaohudhuria kliniki angalau mara nne .
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binirith Mahenge amesema kuwa mkoa wake umepiga hatua katika ujenzi wa vituo vya afya mpaka kufikia 21 ndani ya miaka 3.
"Licha ya ujenzi huo pia Serikali imeongeza bajeti ya dawa kwa upande wa mkoa wa Dodoma kutoka milioni 900 mpaka kufikia bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2018" alisema Dkt. Mahenge.
Jumapili, 4 Novemba 2018

WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI
Jumapili, Novemba 04, 2018
-
Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifafanua jambo mbele ya
waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati alipotembelea Hospitali ya
Rufaa ya Manyara kuona huduma zinazotolewa hapo. Kulia ni Mganga
Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Catherine Magali.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akimkabidhi Mwenyekiti wa kamati ya mkoa wa Manyara
ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto wa kike Bw. Anza Amen Ndosa
miongozo ya utendaji wa kamati hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akisalimiana na wazee wanaolelewa katika kituo cha
kulelea wazee cha Sarame kilichopo wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akimulekeza mbunge wa Babati vijijini, Jitu Son alama
ambazo zimewekwa katika dawa za serikali ili kuzilinda kuuzwa katika
maduka ya watu binafsi. Kulia ni mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth
Kitundu.
WANANCHI SASA KUANZA KUJICHAGULIA VIFURUSHI VYA HUDUMA YA BIMA YA AFYA NCHINI
Na.WAMJW-BABATI
Serikali
imesema ina mpango wa kuanzisha huduma ya bima ya afya ambayo
itamwezesha mwananchi kujichagulia “Kifurushi” kulingana na uwezo wake.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokua akiongea na
wafanyakazi wa kituo cha afya cha Magugu pamoja na wananchi wa kata ya
Magugu iliyopo wilayani Babati katika mkoa wa Manyara, wakati
alipotembelea kituo hicho cha afya.
Dkt.
Ndugulile amesema, kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi,
serikali sasa chini ya Wizara ya Afya, imeamua kutengeneza mkakati
mpya wa huduma za bima za afya zitakazokidhi mahitaji ya wananchi
kulingana na kipato chao.
“Serikali
imeanza mchakato wa mkakati mpya wa bima za afya utakaokua na vifurushi
viwili, kimoja kinaitwa Jipimie na kingine Dunduliza ambavyo vitaanza
hivi karibuni ambapo Vifurushi hivi vimelenga wananchi wa vipato
tofauti, ambapo katika kifurushi cha Jipimie mwananchi ana uwezo wa
kuchagua aina ya gharama za huduma za bima ya afya kulingana na kipato
chake. Lakini katika kifurushi cha Dunduliza mwananchi atakua na wigo
mpana wa kulipa kidogo kidogo kifurushi chake atakachoona kinafaa lakini
akiwa anapewa huduma za bima ya afya kama kawaida”. Amesema Dkt.
Ndugulile.
Katika
kuboresha huduma za afya nchini, Dkt. Ndugulile amesema serikali ina
mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya ifikapo
mwaka 2020. Na itakua ni lazima na siyo jambo la hiyari kwa sababu
magonjwa huwa hayana hodi yanapompata mtu, hivyo kupelekea wananchi
wengi kushindwa kugharamia matibabu kwa sababu wanakua hawajajiandaa
kukabili changamoto za kugharamia matibabu.
Pamoja
na hayo Naibu waziri huyo alionekana kutoridhishwa na hali ya utoaji
huduma kituo cha afya cha Magugu huku ujenzi wa wodi, maabara na nyumba
za watumishi ukichelewa pamoja na kwamba serikali ilipeleka Shilingi
Milioni 400 za ukarabati na ujenzi wa majengo mapya.
Aidha,
Dkt. Ndugulile alionekana kuchukizwa na baadhi ya watoa huduma za afya
kituoni hapo kuwaandikia wagonjwa kununua dawa katika maduka binafsi
wakati dawa hizo zikiwepo katika stoo ya kuhifadhia dawa.
Kufuatia
hali hiyo, Dkt. Ndugulile alimuagiza mganga mfawidhi wa kituo hicho
Dkt. Eliaremisa Palangyo kumrudishia mgonjwa aliyenunua dawa katika duka
binafsi Bw. Onesphory Mfugale kurudishiwa hela yake kiasi cha Shilingi
27,000.
.
Naibu waziri huyo
yupo katika ziara ya siku tatu katika mkoa wa Manyara ambapo atatembelea
Hospitali ya Hydom iliyopo wilaya ya Hanang kisha kuelekea Simanjiro
ambapo atakagua kazi mbadala za wasichana wa kimasai za ujasiriamali pia
atatembelea kituo cha afya cha Orkesumet.
Jumatano, 31 Oktoba 2018
SERIKALI YARAHISISHA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA VIFO VINAVYOTOKEA KATIKA NGAZI YA JAMII NCHINI.
Jumatano, Oktoba 31, 2018
-
Hakuna maoni
SERIKALI kupitia Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto imerahisisha ukusanyaji wa takwimu za vifo vinavyotokea kwenye ngazi
ya jamii nchini kwa kugawa vifaa maalumu vya kukusanyia takwimu hizo kwa
Maafisa afya katika kata za mkoa wa Iringa.
Hayo yamezungumzwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendelo ya
jamii,Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya
wakati akikabidhi Kompyuta Kibao ( Tablets) zanye mfumo maalum wa kukusanyia
takwimu hizo kwa Maafisa Afya leo Mkoani Iringa.
“Takwimu zitakazokusanywa kuhusu vifo na Maafisa hawa wa
afya kutokana na Mifumo hii zitawasaidia madaktari kujadili changamoto
pamoja na sababu za vifo hivyo ili kupata ufumbuzi wa matatizo hayo na kuweza
kupunguza idadi ya vifo nchini” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha,Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa takwimu hizo
zikikusanywa kikamilifu zitasaidia kutoa elimu kwa jamii na kupunguza imani za
kishirikina kwa wananchi kwani zitaleta picha sahihi ya kugundua vyanzo
vya vifo hivyo kwenye jamii husika.
Hata hivyo Dkt. Ulisubisya amewataka maafisa hao kutumia
vifaa hivyo kwa matumizi ya kazi ya kukusanyia takwimu na sio matumizi binafsi
na kama itatokea afisa afya yeyote atakayehama kituo cha kazi basi
arudishe ofisini kwa ajili ya mtumishi mwingine atakayekuja.
Kawa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa iringa Bw. Fikira
Kissimba amesema kuwa mfumo huo wa ukusanyaji taarifa zitasaidia pia
uandikishwaji wa mirathi ya marehemu wakati ndugu husika anapokwenda kufungua
mirathi yake mahakamani.
Naye Mratibu wa usajili wa Takwimu wa Masuala muhimu ya Binadamu
nchini kutoka wizara ya afya Dkt.
Gregory Kabadi amesema kuwa jumla ya Kompyuta kibao (Tablets) zilizogawiwa ni
106 kwa kila kata ya mkoani Iringa na thamani yake ni takribani shilingi
Milioni 61.5.
Aidha , Dkt Kabadi amesema kuwa zoezi hilo limeanza kwa
majaribio katika halmashauri tano kwenye mikoa mitatu ikiwemo Pwani,Tanga na
Morogoro na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mifumo hiyo katika mkoa wa
Iringa kabla ya kutumika nchi nzima.
Kwa upande wake Afisa afya wa kata ya Kitwilu Bw. Wilson
Ntagondwa amesema kuwa kupitia mfumo huo waliokabidhiwa itawasaidia kukusanya
takwimu kwa urahisi hivyo kupelekea kujua sababu zinazosababisha vifo na
kusaidia kupanga maendeleo.

WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA
Jumatano, Oktoba 31, 2018
-
Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akinawa mikono baada ya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji wenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo Elfu 30 kutoka kijiji cha Rurumakilichopo kata ya Kiomboi wilaya ya Ilamba, ikiwa ni muendelezo wa zaiara yake Mkoani Singida.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akiangalia chanjo zilizohifadhiwa katika boksi maalum
wakati alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi iliyopo wilayani
Iramba katika Mkoa wa Singida. Kushoto ni muhudumu wa chanjo Christowelo
Palangyo na Dkt. Abbas Sepoko (kulia).
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akiionesha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya
Iramba (hawapo pichani) dawa za serikali zilizo na alama maalumu ili
zisiuzwe katika maduka binafsi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba,
Emmanuel Gwaula.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akipokea zawadi ya mbuzi kutoka kwa Diwani wa
Kinyambuli Rubeni Charles wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho
ili kujionea hali ya ujenzi wa kituo pamoja na utoaji huduma za afya
kijijini hapo.
WANANCHI WAMETAKIWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA NA KUZINGATIA LISHE BORA
Na WAMJW-MKALAMA- SINGIDA
Watanzania
kote nchini wametakiwa kufuata kanuni na taratibu bora za maisha
ikiwemo kubadili mfumo wa maisha ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya
kuambukiza pamoja na udumavu kwa watoto wachanga.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida wakati alipotembelea kituo
cha afya na kuongea na wananchi.
"Serikali
chini ya uongozi wa Rais Magufuli inataka kila mtanzania awe na afya
bora, ndo maana tunajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusiana na kutunza
afya zenu ikiwemo kufanya mazoezi na kuepuka vyakula ambavyo si salama
kwa afya zetu pamoja na kubadili mfumo mzima wa maisha". Alisema Dkt.
Ndugulile.
Aidha,Naibu
waziri huyo ameendelea kusisitiza kwa upande wa akina mama walio na
watoto wadogo chini ya miaka miwili kuendelea kuwanyonyesha na kuwapa
vyakula vyenye lishe bora watoto wao ikiwa ni sehemu ya kumsaidia mtoto
kukua kiakili na kuwa na afya bora huku akisisitiza siku 1000 za mwanzo
kwa mtoto ndizo siku muhimu katika kumuwezesha kuwa na afya bora na
kukua vizuri.
"Siku 1000
za mwanzo tunaanza kuzihesabu toka mimba inapotungwa, anapozaliwa na
kufikisha miaka miwili, hiki ni kipindi muhimu sana cha mama
kumnyonyesha mtoto ikiwa ni pamoja na kumpa vyakula vyenye lishe ili
mtoto aweze kuwa na afya bora na ubongo unaofanya kazi sawa sawa".
Alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Pamoja
na hayo, Dkt. Ndugulile amekipongeza kituo cha afya cha Kinyambuli kwa
kuzitendea haki fedha zilizotolewa na Serikali Shilingi milioni 400 ili
kusaidia kupanua kituo hicho kwa kujenga majengo mapya ya kuhudumia
wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi.
"Nawapongeza
sana wananchi wa Kinyambuli kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo
hiki, ninachokiona hapa kipo mara 300 nchi nzima, kwa kweli mnastahili
pongezi na fedha za serikali tulizoleta milioni 400 mmezitendea haki".
Alisema Dkt. Ndugulile.
Hata
hivyo Dkt.Ndugulile amesema serikali bado ina nia kubwa ya kuboresha
hali ya utoaji huduma za afya nchini, huku ujenzi wa Hospitali kubwa ya
wilaya ya Mkalama ukitarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Dkt.
Ndugulile amesema mkoa wa Singida umetengewa bajeti ya Bilioni 1.5 kwa
ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya wilaya ya Mkalama pamoja na Singida
DC.
Kwa upande wake
diwani wa Kinyambuli, Rubeni Charles ameishukuru serikali ya awamu ya
tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa kuwakumbuka wananchi wa
kijiji hicho kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo kikubwa cha afya.
"Kwakweli
naishukuru sana serikali kwa kutukumbuka, wananchi wa kijiji hiki
walikua wanapata shida sana kupata huduma za afya hasa wakinamama
wajawazito ambao tulipoteza wengi kutokana na kukosa huduma hii muhimu".
Alisema Rubeni.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)













