Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 7 Machi 2019

DUP NA MATOKEO BORA YA SEKTA YA AFYA NCHINI

- Hakuna maoni

DUP NA MATOKEO BORA YA SEKTA YA AFYA NCHINI

#Serikali yaTanzania imejiwekea mkakati wa Kitaifa wa kuboresha matumizi ya takwimu za afya, utakaosaidia kuboresha utoaji wa huduma katika Sekta ya Afya,  ambao unaitwa 'Data Use Partnership' #DUP

# Mpango huu unalenga kujenga utamaduni wa ukusanyaji na matumizi ya takwimu katika sekta ya afya.

# Uwepo wa Mifumo mingi iliyopo katika sekta ya afya unapelekea mifumo hiyo kushindwa kuwasiliana (visiwa vya taarifa).

#Mpango huu umeanzishwa ili kuboresha mfumo mzima wa taarifa na takwimu, hali itakayosaidia kuimarisha utoaji huduma katika Sekta ya Afya.
                
# Mpango wa kuboresha matumizi ya takwimu utasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Afya mfano Magonjwa ya Mlipuko, kutambua vituo vyenye utendaji  unaoridhisha na usioridhisha

#Mpango wa kuboresha matumizi ya takwimu za afya Tanzania hauishii kuhamasisha mfumo wa Afya wa kidijitali tu, pia Unajenga uwezo wa kutumia takwimu hizo.

#Sekta ya afya lazima iingize utamaduni wa matumizi ya taarifa ili kuimarisha utawala na sera.

#Matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya takwimu yatapelekea maamuzi sahihi, mifumo kuboreshwa na matokeo mazuri katika sekta

# Takwimu sahihi zinazopatikana kwa wakati zinawawezesha wahudumu wa afya kufanya maamuzi sahihi pale wanapotoa huduma za Afya katika vituo vyao.

# Mpango wa kuboresha matumizi ya takwimu za afya unafanya kazi kuakikisha kila mmoja kuanzia watumishi wa serikali, wahudumu na wateja wa afya wanaweza kufanya maamuzi sahihi ya afya.

Jumatano, 6 Machi 2019

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUTOINGILIANA MAJUKUMU.

- Hakuna maoni
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisema jambo na watendaji wa ofisi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawapo pichani alipotembelea ofisi hizo kuona utendaji kazi wao.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wa (wa tatu kutoka kushoto) akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaj Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) kuelekea maabara za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameshika  dawa ya malaria aina ya DUO -COTECXIN,  halisi kulia na bandia kushoto zilizopimwa na  Maabara ya Mamlaka ya Chakula  na Dawa (TFDA)  wakati alipotembelea ofisi za  TFDA,  wa pili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki na wa tatu kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akionyeshwa sampuli na mtaalam katika maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji kazi wao.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kulia)  wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Jijini Dar Es Salaam.


Na WAMJW - Dar Es Salaam
Serikali imedhamiria kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na  wafanyabiashara kuhusu mkanganyiko wa majukumu baina ya Taasisi za Serikali zinazoingiliana majukumu na kuzitaka kila taasisi kama hizo ziwe na mipaka yake ya kazi na kupunguza urasimu.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji wao wa kazi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Taasisi za Serikali ambazo zimekuwa zikiingiliana majukumu na zimekuwa zikisababisha adha kwa wananchi na kuongeza urasimu na upotevu wa muda mwingi katika kuwahudumia wateja.

“Serikali imedhamiria kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi za Serikali ili kumwondolea usumbufu mwananchi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa na kuendelea kusema kuwa mkanganyiko huo unapelekea watu kutokujua majukumu yao aidha kwa kutokujua sheria au kwa makusudi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya utendaji usiyo sahihi wa mwingiliano wa majukumu hasa kwenye eneo la ukaguzi na uchukaji wa sampuli baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuzitaka taasisi hizo kujiridhisha na kuyafahamu vizuri majukumu yao.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Viongozi wa Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, Mifugo,Wizara ya Viwanda na Uwekezaji kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa “Blueprint” ifikapo Machi 30 mwaka huu.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka TFDA kujiimarisha zaidi kwenye ukaguzi wa vyakula na dawa na kuhakikisha bidhaa zisizokuwa na usajili haziingii sokoni na kuitaka TFDA kuongeza wataalam katika Mikoa na Wilaya ili kudhibiti mapito ya magendo ya bidhaa za chakula na dawa.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika maabara za uchunguzi wa vyakula na dawa na hivi sasa taasisi hiyo imefikia ngazi ya tatu ya ubora wa udhibiti wa dawa kimataifa hivyo kuaminika na mataaifa mbalimbali na kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuingiza bidhaa zao nchini.

Waziri Ummy amesema kuwa TFDA imepewa dhamana ya kulinda afya za watanzania kwa kuhakikisha vyakula na dawa zinazozitumia kila siku ni salama kwa afya za wananchi na kukiri kuwa kweli changamoto zipo na kupitia wizara yake atahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ndani ya muda mfupi.

Naye ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeanzisha huduma ya mahali pamoja iliyopo katika kituo cha uwekezaji (TIC) ambapo mpaka sasa zipo taasisi 16 ikiwemo TFDA huku akiomba Wizara husika kuongeza watumishi katika kitengo hicho ili kuweza kushughulikia kwa uharaka masuala ya uwekezaji katika vyakula na dawa.

Aidha,Waziri Kairuki amekiri kuwepo mkakanganyiko wa majukumu baina ya taasisi za Serikali huku akiitaka TFDA kutowahudumia wawekezaji wanaofika nchini wakiwa na Vyeti vya Usajili wa Vivutio kwani wanatakiwa kuhudumiwa na TIC.

"Naomba kuweka msisitizo, mara anapokuja mwekezaji, swali lenu la kwanza liwe ni kuuliza kama anacho Cheti cha usajili wa vivutio kutoka TIC au la, na endapo anayo basi nyinyi mwelekezeni TIC".Alisisitiza Waziri Kairuki

Mwisho.

KAMATI YA BUNGE MASUALA YA UKIMWI YATAKA MFUKO WA TAIFA WA UKIMWI KUJITEGEMEA.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisema jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya mapema jana.

Mama Salma Kikwete, Mjumbe wa Kamati ya Bunge inajishughulishana Masuala ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya akisoma nyaraka wakati wa ziara ya kamati walipotembelea Shule ya Sekondari Makoka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madwa ya Kulevya, Mhe. Oscar Mukasa akisema jambo kwa wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani) katika ziara ya wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea Mkoa wa Dar Es Salaam kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya kwenye matibau ya Virusi vya Ukimwi.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge inajishughulishana Masuala ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya Mama Salma Kikwete (kulia) akisalimiana na Suzana Paul mwanafunzi katika Shule ya Sekondari Makoka.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya Mhe. Zainab Vullu akichangia mada katika ziara ya wajumbe wa kamati hiyo walipotembea Mkoa wa Dar Es Salaam kujione ahali ya utoaji wa huduma

Wajumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madawa (waliosimama) wakimsikiliza mtoa huduma za afya katika Kituo cha kutolea dawa za kufubaza Virusi vyta Ukimwi (CTC) katika Hospitali ya Sinza





Wajumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madawa wakimsikiliza mtoa huduma za afya katika Kituo cha kutolea dawa za kufubaza Virusi vyta Ukimwi (CTC) katika Hospitali ya Sinza.


KAMATI YA BUNGE  YATAKA MFUKO WA TAIFA WA UKIMWI KUJITEGEMEA

Na WAMJW - Dar Es Salaam.

Serikali imetakiwa kutenga bajeti ya kutosheleza ili kuuwezesha Mfuko wa Taifa wa Ukimwi kujitegemea na kuepukana na utegemezi wa fedha za wafadhili katika mapambano ya Virusi vya Ukimwi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI na Madawa ya kulevya  Oscar Mukasa wakati wa kamati hiyo ilipofanya ziara  katika Kitengo cha kutolea dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (CTC) katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo kujionea hali ya utoaji huduma.

Mhe. Oscar Mukasa (MB) amesema suala la upatikanaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi ni jambo la kitaifa na kamati yake ina mkakati wa kuhakikisha inaongeza nguvu kwenye Mfuko wa Taifa wa Ukimwi (ATF) na nchi kuweza kujitegemea kuhusu masuala ya  UKIMWI.

“Tuna haja ya kujipanga wenyewe kuhakikisha kwamba tunajitegemea, ule utegemezi wa fedha za wadau za mapambano ya Ukimwi unaweza kupungua”. amesema Mhe. Mukasa.

Mhe. Mukasa amesema Serikali imekuwa ikitegemea fedha za wafadhili kutoka nje ya nchi na sasa ni vizuri tukajipanga wenyewe na kuacha utegemezi wa wafadhili hao kutoa fedha muda wote.

Hata hivyo Mhe. Mukasa amesema kamati yake itaendelea kusimamia Serikali hasa Wizara ya fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha  wanapata chanzo mahsusi cha kodi kwa ajili ya ATF.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo na pia Waziri mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ye Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu amefurahishwa kuona Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeanza kutekeleza agizo alilolitoa la kutoa ushauri, kupima pamoja na matibabu ya kufubaza virusi vya ukimwi.

Aidha, Waziri Ummy ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kutekeleza agizo la Serikali kwa kutoa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi kwa muda kwa kipindi cha miezi mitatu kwa wagonjwa ambao wameshachunguzwa na kubainika virusi kufubaa.

“Mpango wetu Serikali kwa wagonjwa ambao watakao kidhi vigezo basi watazipate dawa hizo kwa miezi sita”.  Alisema Waziri Ummy na kuendelea kuwa wanalenga kuwaondolea usumbufu wa kuja mara kwa mara.

Mwisho

Jumatatu, 4 Machi 2019

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI MATUMIZI YA KEMIKALI NCHINI.

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo na wadau wa biashara ya kemikali (hawapo pichani) kwenye mkutano na wafanya biashara za kemikali nchini.
 Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko akisema jambo kwa wadau wa biashara ya kemikali nchini (hawapo pichani) katika mkutano na wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Prof Esther Hellen Jason akisema jambo na wadau wanaojihusiha na biashara ya kemikali (hawapo pichani)

Mdau wa bishara ya kemikalina Katibu Mkuu wa Mawakala wa Forodha Tanzania Mhandisi Anthony Swai akiwa amebeba sampuli ya kemikali mapema leo kwenye kikao cha wadau wanaojihusisha na bishara ya kemikali nchini.

Wadau wanaojihusisha na biashara ya kemikali wakiwa kwenye mkutano.

Na WAMJW -  Dar Es Salaam.

Serikali itaendelea kusimamia na kudhibiti matumizi ya kemikali ili kuhakikisha hazileti madhara kwa afya za wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo alipokuwa kwenye mkutano na wadau wa kemikali kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya kemikali nchini.

“Kemikali zisipodhibitiwa vizuri zinaweza kuleta madhara katika afya, mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa nchini, ipo haja ya kuweka mazingira mazuri ya kusimamia na kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali nchini ili zisilete madhara” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2014 zinaonyesha vifo milioni 12.6 vilitokana na mazingira duni ya kuishi, mojawapo ya kichocheo ni athari za kemikali ambazo zimekuwa zikisababisha magonjwa na vifo.

Waziri Ummy amesema kuwa kemikali zimekuwa na athari kubwa kwa binadamu kwa kusababisha magonjwa zaidi ya 100 huku akiyataja magonjwa ya moyo, saratani, ngozi, athari katika mifumo ya fahamu, upumaji pamoja na chakula kuathiri zaidi wananchi wengi.

“Tukubali kuwa kemikali zina madhara kwa wananchi lakini sasa tuwe na mazingira mazuri ya kuzidhibiti” amesema Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wafanya biashara ya kemikali nchini.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amezitaka Taasisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuangalia upya tozo wanazotoza kwa wafanyabiashara za kemikali nchini pamoja na kupunguza urasimu usiokuwa na ulazima ili kuwawekea mazingira rafiki wafanya biashara za kemikali.

“Msiwe ni kikwazo kwa uwekezaji na biashara, kikwazo cha kushamiri na kukua kwa uwekezaji nchini, nataka muwe mawakala wa kukuza biashara na uchumi nchini” amesema Waziri Ummy.

Awali akisoma taarifa yake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Sheria ya Kemikali ya mwaka 2003 imekuwa na mchango mkubwa katika udhibiti wa matumizi ya kemikali nchini.

“Kabla ya kutungwa kwa sheria hii, kemikali zilikuwa zikiingizwa nchini kiholela na kutumika bila ya kuwa na ufatiliaji au udhibiti wowote” alisema Dkt. Mafumiko.

Dkt. Mafumiko amesema Sheria ya kemikali imewawezesha kudhibiti usafirishaji, utumiaji pamoja uteketezaji wa taka zinazotokana na kemikali.

“Ofisi ya Mkemia inasimamia kwa ukaribu matumizi ya kemikali zote zinazoingizwa nchini kuanzia zinapoingia, mahali zinapokwenda pamoja na matumizi yaliyokusudiwa” alisema Dkt. Mafumiko.

Naye Katibu Mkuu wa Mawakala wa Forodha Tanzania Mhandisi Anthony Swai amesema tozo zimekuwa nyingi kiasi cha kuwaumiza wafanyabiashara wa kemikali huku urasimu pia ukisababisha wafanyabiashara kutumia muda mwingi kufuatilia vibali vya uingiza wa kemikali nchini.

Aidha Mhandisi Swai ameiomba Serikali kuainisha mipaka ya taasisi za umma pamoja na tozo wanatostahili kulipa kwani kumekuwa na mwingiliano wa majumuku baina ya taasisi za Serikali ambazo amezijata kuwa ni GCLA, TDFA na TBS (Shirika la Viwango Tanzania)

Jumapili, 3 Machi 2019

SPIKA ZA MASIKIONI CHANZO CHA MATATIZO YA USIKIVU

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akifanyiwa uchunguzi wa sikio na Daktari bingwa wa masikio Dkt. Godlove Mfuko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akisikiliza maelekezo ya namna bora ya kutunza sikio kutoka kwa Daktari Bingwa wa Masikio Dkt. Godlove Mfuko kutoka Hospitali ya Taifa muhimbili - Mloganzila.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu(kulia) akisalimiana na watoto waliofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya usikivu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyeketi) akiwekewa vifaa vya uchunguzi wa usikivu na mtaalam wa usikivu Bi. Tedi Uiso kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bw. Makwaiya Makani akizungumza jambo katika siku ya Usikivu Duniani ambayo kitaifa imefanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila


Na Englibert Kayombo, WAMJW - Dar Es Salaam

Spika za masikioni maarufu kwa jina la “Headphones” zimetajwa kuwa chanzo kinachopeleka tatizo la usikivu hafifu kwa watu.

Hayo yamesemwa leo na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na wananchi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Jijini Dar Es Salaam katika kuadhimisha siku ya usikivu duniani.

Waziri Ummy amesema kuwa matumizi ya simu za kisasa yameongeza kasi ya watu kutumia spika za masikioni jambo ambalo linahatarisha kuwa na watu wengi wenye matatizo ya usikivu.

“Unakuta kijana kuanzia asubuhi mpaka jioni ameweka spika za masikioni anasikiliza muziki hawajui wanajiweka katika hatari ya kupata tatizo la usikivu” amesema Waziri Ummy na kuendelea kusema kuwa kundi la vijana liko hatariki kupata matatizo ya usikivu.

Waziri Ummy ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kupunguza matumizi ya spika za masikioni ili kuweza kujikinga na matatizo ya usikivu.

“Nitoe rai kwa vijana wapunguze matumizi ya spika za masikioni kwa muda mrefu, tusipo kuwa makini tunaweza kujikuta tuna taifa lenye watu wengi wenye matatizo ya kutosikia vizuri” amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa tatizo la usikivu hutokea pia kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kuzaliwa na tatizo hilo au kulipata ukubwani kutokana na sababu nyinginezo ambazo zinaambata kwa kukaa kwa muda mrefu kwenye sehemu zenye kelele nyingi pamoja matatizo yanayoambata na afya ya sikio.

Waziri Ummy amesema kuwa ni jambo jema kuona sasa matibabu ya matatizo ya usikivu hafifu yanapatikana hapa hapa nchini huku akiwataka wananchi kukata bima za afya ili kuweza kupata matibabu kwa uhakika.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tatizo hili linazuiliwa kabla ya kutokea lakini pia kuhakikisha matibabu yanapatikana yakiwemo kutumia mashine ya mawimbi ya sauti, upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio pamoja na kupandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2018 Hospitali ya Muhimbili imefanikwa kuwapatia wagonjwa 116 vifaa vya mawimbi ya sauti, wagonwja 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa na kuhakikisha matibabu yanapatikana hapa hapa nchini.

Awali akitoa taarifa yake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Bw. Makwaiya Makani amesema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali katika eneo la usikivu ikiwemo kutoa huduma ya upandikizaji vifaa vya usikivu kwa Watoto wenye matatizo ya hayo.

“Tangu mwezi Juni mwaka 2017 tayari watoto 21 wamepandikizwa vifaa vya usikivu kitaalam kwa jina la 'cochlear implants” amesema Bw. Makani

Bw. Makani amesema kuwa wameendesha kliniki ya siku mbili katika Hospitali ya Mloganzila kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya usikuvu ambapo watu 264 wamejitokeza kati yao watu 172 walihitaji uchunguzi zaidi wa usikivu, watu 64 wamekutwa na matatizo ya usikivu na tayari wamepatiwa rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi na watu 31 wamekutwa na nta za masikioni,pia watu 26 wamekutwa na maambukizi kwenye masikio ambao wamepatiwa rufaa ya matibabu zaidi.

Tatizo la usikivu linazidi kuongezeka siku hadi siku. Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 5 ya watu duniani wana tatizo la usikivu. Tatizo hili litaongezeka maradufu kila mwaka. Inatakiwa kila mmoja achukue hatua kujikinga na tatizo hili ikiwemo kuepuka sehemu zenye kelele na pia kusikiliza mziki kwa sauti kubwa na kwa muda mrefu na kwa kutumia spika za masikioni.

Mwisho

Jumamosi, 2 Machi 2019

“BIMA YA AFYA NDIYO SULUHISHO LA UHAKIKA WA MATIBABU”-WAZIRI UMMY MWALIMU

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa kikao na watendaji wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa (hawapo pichani)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (kushoto) akichunguza hali ya utoaji huduma katika duka la dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu ( kulia) akiwasalimia mama na mtoto katika wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akisoma nyaraka za dawa katika chumba cha dawa cha Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (kushoto) akiteta jambo na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Dkt Halima Mangiri.

Na Englibert Kayombo, WAMJW - Kilosa, MOROGORO.

Wananchi wametakiwa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo alipokuwa ziarani Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro akikagua hali ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

“Ni muhimu kwa wananchi kuwa na bima ya afya ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu ikiwemo dawa bila ya kikwazo cha fedha” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa matarajio ya wananchi mara baada ya kujiunga na bima ya afya ni kupata huduma bora za afya bila usumbufu huku wakiwa na uhakika wa kupata dawa kwa makundi yote ikihusishwa wale wa Bima ya Afya pamoja na Mfuko wa Bima ya Afya Ngazi ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa.

“Mwananchi yeyote ambaye amekuja na bima ya afya, CHF iliyoboreshwa wanapaswa kupata huduma zote, kumwona daktari bure, vipimo bure, na dawa bure” amesema Waziri Ummy na kuongezea “Bila ya kufanya hivyo hakuna umuhimu wa kuwaambia wananchi kukata bima za afya.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amewataka watoa huduma za afya nchini kutoa huduma bora kwa kuzingatia Mwogozo wa Taifa wa Matibabu na orodha ya dawa muhimu huku akiwataka kutoa huduma bora za matibabu kwa kutoa dawa kulingana na mwogonzo unavyobainisha.

“Badala ya kumwandikia unayoitaka wewe au mgonjwa, tumeweka utaratibu weka dawa ambayo ipo kwa mujibu wa mwongozo” alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wananchi wanapata dawa katika vituo vya kutolea huduma kwani kumekuwa na malalamiko hapo zamani wagonjwa wakisema madaktari walikuwa waki waambia dawa hakuna huku ili hali dawa zipo.

“Hatutaki kuona wananchi wanalalamika dawa hakuna na kutuona tunadanganya wakati dawa zipo, na mwongozo unasema wazi kama hakuna dawa A mpe dawa B. Alisikika akisema Waziri Ummy.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy ameupongeza Uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa kuhakikisha dawa zinapatikana kwa ufanisi muda wote na kuwataka mafanikio ambayo wameyapata wahakikishe waharudi chini.

“Serikali itaendela kuhakikisha inaboresha Sekta ya afya ili Taifa liweze kuwa na nguvu kazi yenye afya bora kazi yenu nyinyi ni kuhakikisha mnaendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha dawa zinapatikana muda wote” amesema Waziri Ummy.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Dkt. Halima Mangiri ameishukuru Serikali kwa kuuongeza bajeti ya dawa wilayani humo.

Dkt. Mangiri amesema kuwa bajeti ya dawa imekuwa ikiongezeka maradufu mwaka hadi mwaka huku akitolea mfano wa mwaka 2017/18 hali ya upatikanaji wa dawa ilikuwa ni asilimia 86, huku kwa mwaka 2018/19 hali ya upatikanaji dawa ikiongezeka na kufikia asilimia 96.

“Tunaishukuru Serikali, Kwa kweli hali sasa sii kama zamani, tunapata dawa na hali inaridhisha” alisema Dkt Mangiri.

Mwisho