Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 4 Julai 2019

TANZANIA BILA DENGUE INAWEZEKANA

- Hakuna maoni
Timu ya Wahamasishaji wa masuala ya Afya, kutoka Manispaa ya Kinondoni wakichanganya dawa, ikiwa ni moja kati ya maandalizi ya kuanza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika maeneo yenye mazalia ya mbu wa Dengue.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiongoza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika Manispaa ya Kinondoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akieleza jambo mbele ya viongozi wa Manispaa wakati wa zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika Manispaa ya Kinondoni. Wakatikati ni Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Maulid Mtulia.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) wakielekea katika eneo lenye mazalia ya  mbu wanaosababisha homa ya Dengue, zoezi limefanyika katika eneo la Msisili Manispaa ya Kinondoni.

Moja kati ya eneo la mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa homa ya Dengue, ililopo eneo la Msisili Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.


TANZANIA BILA DENGUE INAWEZEKANA

Na WAMJW-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. @ummymwalimu leo ametembelea katika Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa Mikoa/Halmashauri ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Dengue.

Katika ziara hiyo Waziri @ummymwalimu ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zinazochukuliwa na Manispaa ya Kinondoni za kupambana na Ugonjwa wa Homa ya Dengue hali iliyochangia kupungua kwa Idadi ya Wagonjwa kutoka Wagonjwa 604 Mwezi Mei hadi kufikia Wagonjwa 450 Mwezi Juni. 

“ Nafurahi kuona kwamba idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue katika Wilaya ya Kinondoni, Mwezi Mei kulikuwa na Wagonjwa ambao wamepima na kuthibitishwa 604, lakini mwezi wa tano Wagonjwa wamepungua hadi 450” Alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, takwimu za Kitaifa za Wizara ya Afya, mwezi Mei tulikuwa na idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue 3170, na wamepungua Mwezi wa Sita hadi kufikia Wagonjwa 1446, hali inayotoa matumaini katika kuimaliza vita hii ya homa ya Dengue.

Aidha, Waziri Ummy amewapongeza Watendaji wa Sekta ya Afya katika Manispaa ya Kinondoni kwa hatua wanazoendelea kuchukua, ikiwemo kununua Viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu na kununua mashine mpya za kupuliza dawa (motorised sprayers), katika maeneo yenye mazalia ya mbu.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesisitiza juu ya ushiriki wa Wananchi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa homa ya Dengue, huku akieleza kuwa mapambano dhidi ya mbu wa Dengue yatasaidia kupunguza magonjwa mengine kama Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano.

“Ushiriki wa Wananchi ni muhimu sana katika kupambana na ugonjwa wa Dengue, tukipambana na Dengue, kwa upande mwingine tunakuwa tunapambana na ugonjwa wa Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano, kwhiyo ni lazima tuhakikishe kila mtu anashiriki katika kupambana dhidi ya mbu.” Alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Maulid Mtulia amekazia kwa kuwahasa Wananchi juu ya ushiriki katika vita hii dhidi ya ugonjwa wa Dengue na kusisitiza kuwa Serikali haiwezi kushinda vita hii bila ushirikiano wa Wananchi.

Nae, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamin Sitta amesema kuwa Jumla ya shilingi Milion 132 kwaajili ya zoezi lakutokomeza homa ya Dengue, 90 zimetumika kwaajili ya zoezi zima la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, huku 42 kwaajili ya kununua Mashine za kubwa ya upuliziaji wa dawa hizo.

“Tumetumia gharama ya takribani Milion 90 kwaajili ya upuliziaji katika kila kata na tupo mbioni kuongeza Milioni 42 kwajili ya mashine kubwa yenye uwezo wa kusambaza mara moja kwa kata 10, kwahiyo kwa ujumla tutakuwa tumetumia takribani Milion 132 kwaajili ya zoezi la kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa wa Dengue.” Alisema Mhe. Benjami Sitta.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt.  Festo amesisitiza kuwa Huduma za vipimo vya homa ya Dengu zinapatikana katika vituo vya Serikali vya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo na vituo binafsi bei elekezi isizidi shilingi 50,000/

“Huduma hizi za vipimo zinapatikana kwenye vituo vyetu, na katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo, lakini katika vituo binafsi, bei elekezi isizidi 50,000/ kwa kipimo cha Dengue” alisema Dkt. Festo

Pia, amewaasa Wananchi kuwahi katika vituo vya Afya, pindi waonapo dalili za ugonjwa wa homa ya Dengue na kuachana na mawazo potofu ya matibabu ya Dengue kama majani ya mpapai kwani yanawezapelekea kupata matatizo mengine yakiafya.

Mwisho.

Jumatano, 3 Julai 2019

DKT. NDUGULILE AISIFU HALMASHAURI YA WILAYA YA BAHI KWA KUFANIKISHA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akitoa maelekeozo kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakati alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Mpya ya Wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Bi. Mwanahamisi Mkunda, Mkurugenzi wa Halmashauri Dkt. Fatuma Mganga na kulia ni Mbunge viti maalum wa Dodoma Bi. Felista Bula, mbunge wa jimbo la Bahi Omary Badwel na Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Philipina Philipo.

Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile akimuangalia fundi mwana mama aliyekua anapaka rangi katika majengo ya Hospitali Mpya ya Wilaya ya Bahi wakati alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo mapema leo.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulie akielekeza jambo kwa viongozi wa wilaya wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Hospitali mpya ya wilaya ya Bahi mapema leo. 



Baadhi ya majengo ya Hospitali mpya ya Wilaya ya BAHI.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile akihesabu mabati ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi wakati alipofanya ziara ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa zahanati hiyo leo.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi wa kijiji cha Chonde waliofika katika mkutano ambao ulitanguliwa na ziara ya ukaguzi wa zahanati ya kijiji hicho.

NA WAMJW-BAHI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameusifu uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kutekeleza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo ukiwa umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90.

Dkt. Ndugulile amesema hayo mapema leo baada ya kutembelea ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia hatua za mwisho na kuridhishwa na hatua iliyofikia hadi sasa huku akiusifu uongozi wa Halmashauri chini ya Mkuu wa Wilaya Bi. Mwanahamisi Mkunda kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.

“Napenda kuwapongeza sana kwa kazi nzuri na ushirikiano mnaoonesha katika kutekeleza mradi huu, ninaamini majengo haya yakikamilika tutaanza kutoa huduma kwa sababu OPD tunayo, jengo la upasuaji, Maabara, jengo la Radiolojia na pia huduma ya Mama na Mtoto tunaweza kuanza nazo”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Baada ya kutembelea majengo mbalimbali ya Hospitali hiyo Dkt. Ndugulile ameonesha kuridhishwa na ujenzi huo na kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa haraka iwezekanavyo ili kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi wa eneo hilo.

Aidha, Dkt. Ndugulile ametembelea ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi na kushangazwa na kasi ndogo ya ujenzi ambao ulianza toka mwaka 2007 lakini haujakamilika mpaka leo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa fedha.

Dkt. Ndugulile ameonyesha kutoridhishwa na gharama za ujenzi ambao unagharimu Shilingi Milioni 90 mpaka kukamilika. Kufuatia hatua hiyo ameagiza ujenzi wa zahanati hiyo kutumia utaratibu wa Force Account na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Dkt. Fatuma Mganga kuleta wataalamu kwa ajili ya kuhakiki gharama za vifaa vinavyohitajika.

Pamoja na hayo Naibu Waziri huyo ameahidi kutoa mifuko 50 ya Saruji ili kuchangia gharama za ujenzi huku akitoa miezi mitatu ya ukamilishaji wa ujenzi huo. Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. Mwanahamisi Mkunda amemuahidi Naibu Waziri kukamilika kwa ujenzi wa zahanati ndani ya muda uliowekwa na amechangia mifuko 10 ya saruji huku Mbunge wa Viti Maalum wa Dodoma Bi. Felista Bula akichangia Mifuko 20 ili kuchochea kasi ya ujenzi na huduma zianze kutolewa ifikapo Septemba mwaka 2019.

MWISHO

SERIKALI YAJIIMARISHA KUIMALIZA DENGUE

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiambatana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakiwa katika  zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiongozana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakielekea katika  zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Iliyobebwa ni moja kati ya mashine mpya 14 za kupuliza dawa (motorised sprayers) zilizonunuliwa na Manispaa ya Ilala ikiwa ni moja ya jitihada yakupambana dhidi ya ugonjwa wa homa ya Dengue katika Manispaa hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongoza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, katika eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiambatana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakinyunyiza dawa katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Baadhi ya mtaro katika eneo la Ilala Mchikichini Jijini Dar es salaam, ambao ni moja ya sababu ya mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa homa ya Dengue


Na WAMJW- DSM 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. @ummymwalimu leo amefanya ziara katika eneo la Mchikichini Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa Mikoa/Halmashauri ya kupambana dhidi ya ugonjwa  wa Dengue.

Kwa kiasi kikubwa Waziri @ummymwalimu ameridhishwa na hatua walizochukua na Manispaa ya Ilala ikiwemo kununua mashine mpya 14 za kupuliza dawa (motorised sprayers), kununua Viuadudu kutoka kiwandani Kibaha lita 3,980 (shs 53m) na kununua lita 210 za kuua mbu wapevu. Huku upuliziaji ukiendelea ktk kata 25.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa, Matokeo ya jitihada hizi yanaoneka, huku Idadi ya wagonjwa wa Dengue Wilaya ya Ilala ikipungua kutoka wagonjwa 527 mwezi Mei 2019  hadi wagonjwa 207 mwezi June 2019. 

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, katika Jiji zima la Dar es Salaam wagonjwa wa homa  ya Dengue wamepungua kutoka 2,759 mwezi Mei 2019 hadi wagonjwa 790 mwezi June.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amewataka wananchi kushiriki kikamilifu ktk kutokomeza mazalia  ya mbu, kwa kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka, kupulizia dawa maeneo yote yenye mazalia ya mbu,  pia kutumia chandarua chenye dawa wakati wote.

Mwisho.

Jumatatu, 1 Julai 2019

HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA ZATAKIWA KUWA NA VIFAA MUHIMU VYA KUTOLEA HUDUMA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu akihutubia Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa waliofika katika Mkutano unaoanza leo jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (katikati) akizndua muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za mikoa wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Mikoa unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace Maghembe na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Muhammad Kambi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alifurahia muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa aliouzindua mapema leo, kulia ni Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace Maghembe, akipokea muongozo huo kutoka kwa katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na katikati ni Naibu waziri Dkt. Faustine Ndugulile akishuhudia.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza alilozindua wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile na Kulia ni Katibu wa Afya Dkt. Zainab Chaula
Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Afya na TAMISEMI wakiongozwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza lililozinduliwa leo na Waziri Ummy.

NA WAMJW-DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kuhakikisha wanakua na vifaa vya muhimu vya kutolea huduma za afya kwa wagonjwa wanaofika Hospitalini kupata matibabu.

Waziri Ummy amesema hayo wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Waziri Ummy amewataka Waganga Wafawidhi hao kubainisha aina ya vifaa vya matibabu vinavyotakiwa kupelekwa katika Hospitali  zao ili kuhakikisha mgonjwa anapofika Hospitalini hakosi huduma wakati anapoenda kupata matibabu.

“Mganga Mfawidhi unatakiwa useme vifaa gani ukivipata utaboresha huduma, hatutaki mgonjwa afike Hospitali halafu akose huduma, boresha kwanza kupata vifaa vya msingi kabla ya vile vikubwa kama CT-Scan”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya chini ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa ili mwananchi akifika katika Hospitali za Rufaa aseme kweli huduma zimeboreshwa.

“Lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kila Hospitali ya Rufaa inakua na huduma za kipaumbele 13 zikiwepo huduma za mama na mtoto ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na magonjwa mengine ambayo yanaweza kutibiwa bila kumpa rufaa mgonjwa”. Ameongeza Waziri Ummy.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za mikoa kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato kwa kufunga mfumo utakaotumika kukusanya mapato na kuachana na makaratasi.

“Tuendelee kuboresha huduma za afya na kusimamia ubora wa huduma tunazozitoa na kuboresha upatikanaji wa vifaa na kuwa wabunifu japokuwa tuna changamoto za rasilimali watu ila huduma za kibingwa ziboreshwe ili kupunguza rufaa za nje”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula amewataka Waganga Wafawidhi hao kuhakikisha wanaripoti taarifa za maendeleo ya Hospitali na atakayeshindwa kufanya hivyo hataendelea na uongozi. Pia amewataka Waganga Wafawidhi hao kuwa na ushirikiano ili kufanya sekta ya afya kuwa ya mfano.

“Tuhakikishe tunaweka mifumo vizuri ya kutoa huduma kwa wahitaji kuanzia ngazi ya chini kwa kufuata miongozo na mikataba iliyotolewa, na tufanye kazi kwa ushirikiano bila kujali cheo au nafasi ya mtu”. Amesema Dkt. Chaula.

Pamoja na hayo katika Mkutano huo Waziri Ummy alizindua muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na jarida la afya ya jamii toleo la kwanza.

MWISHO

Jumamosi, 29 Juni 2019

HUDUMA ZA DHARURA KWA WAJAWAZITO ZAENDELEA KUSAMBAA NCHINI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza  jambo mbele ya wananchi (hawapo kwenye picha) wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Watatu kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama,  Kulia kwa Waziri Ummy ni Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakinyoosha viungo muda mfupi baada ya kumaliza matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu akiwasilisha taarifa ya mradi wa  SUAM mbele ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wenye lengo la kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakatikati) pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakimkabidhi zawadi ya cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Charles Itembe kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha matembezi hayo ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa wakunga kwa uzazi salama nchini.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.


Na WAMJW- DSM 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, yaendelea kuboresha huduma za Afya za dharura nchini kwa kuviwezesha vituo vya Afya kuweza kutoa huduma za uzazi wa dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ili kuokoa vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi pingamizi. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu leo wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuchangia Juhudi za kupunguza na kuepusha vifo vya wajawazito na Watoto wachanga vitokanavyo na uzazi, katika viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam. 

Waziri Ummy amesema kuwa wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani ilikuwa vituo vya Afya takribani 109 sawa na asilimia 19 ya vituo vya Afya ambavyo vilikuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura pamoja na kumtoa mtoto tumboni, huku sasa kuongezeka hadi kufikia takribani vituo 460.

Aidha, Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa kila mwaka Wanawake 11,000 hufariki nchini, sawa na wanawake 900 kila mwezi, ikiwa ni sawa na wanawake 30 kila siku hufariki wakiwa wanatimiza wajibu wao wa msingi wakuleta kiumbe Duniani, hivyo ni lazima Juhudi za ziada ziendelee kuchukuliwa. 

Kulingana na takwimu zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba vifo katika kila vizazi hai 100,000 wanawake 556 hufariki, huku wanawake wajawazito nchini wakiwa Milioni 2 kwa mwaka

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa hadi kufikia takribani Bilioni 260, ikilinganishwa na bajeti ya Bilioni 30 iliyokuwepo kabla ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, huku dawa kama ’magnesium sulfate' kwa ajili ya kifafa cha mimba zikipatikana bila malipo.

"Tumeweza kuongeza bajeti ya dawa, wakati tunaingia madarakani ilikuwa takribani Bilioni 30, sasa hivi tunazungumzia bajeti ya dawa ya Bilioni 260, huku dawa kama magnesium sulfate kwa ajili ya kifafa cha mimba zinapatikana bure bila malipo yoyote katika vituo vyetu vya kutoa huduma za Afya " alisema Waziri Ummy. 

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa licha ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa bado kuna changamoto ya Watoa huduma za Afya, hivyo amelipongeza Shirika la Amref kwa jitihada za kuajiri baadhi ya Watoa huduma jambo linalosaidia kupunguza changamoto katika Sekta ya Afya. 

"Tunauhitaji wa watumishi wa Afya takribani 200,008 katika vituo vya Afya vya Serikali kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka ngazi ya Hospitali za rufaa za mikoa, huku watumishi waliopo ni takribani 98,000, hivyo pengo likiwa ni Asilimia 52, huku Zahanati zikiwa ndio waathirika wakubwa" alisema Waziri Ummy

Nae Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed amewataka wakina mama kuwai katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi waonapo dalili za ujauzito, ili kuokoa vifo ambavyo vinaweza zuilika wakati wa kujifungua.

"Katika zile siku 12 za mwanzo wajitahidi kufika katika vituo vya Afya kupata uangalizi, na vifo vingi ndio huanza kutokea hapa, kwahiyo ningeomba sana wakinamama kuwahi katika vituo vya Afya, kuonana na wakunga waliopata elimu ili wapate huduma kwa wakati " alisema Hamad Rashid.

Mwisho

Jumatano, 26 Juni 2019

BODI ZA HOSPITALI ZA RUFAA ZATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya akisema jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (hawako pichani) katika Kikao kazi kilichofanyika jana Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wakiwa katika kikao kazi.


Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wakiwa katika kikao kazi.

Na.WAMJW,Dodoma

Wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa nchini wametakiwa kutatua changamoto zilizopo kwenye hospitali zao ili wananchi wapate huduma zilizo bora

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu,Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Zainabu Chaula wakati akifungua kikao kazi cha uhamasishaji wa wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa za mikoa kinachofanyika jijini hapa

Dkt.Chaula alisema wizara inawategemea na kuwathamini wajumbe hao  katika kuleta mabadiliko ya uimarishaji wa huduma za afya katika hospitali za mikoa zilipo katika maeneo yao hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu.

“Nyie ndio macho yetu kule,tumewapa wajibu hivyo tunawategemea mtushauri na kuleta mafanikio katika maeneo yenu".Alisisitiza Dkt.Chaula

Aidha,aliwataka wabuni katika kuongeza vyanzo vya mapato ili hospitali hizo ziweze kuwahudumia wananchi ipasavyo na si kwenda hospitali za ngazi za juu“madaktari bingwa wanatengenezwa wananchi hawapaswi kwenda hospitali kubwa bali hospitali za rufaa"alisema Dkt.Chaula

Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Mohhamad Bakari Kambi alisema wanatarajia mabadiliko makubwa katika rasiliamali watu hususan kwenye sekta ya afya  kwa kuwa wabunifu.

"Tutawapima kwa utendaji  na mafanikio yenu na hivyo tutapenda baadae muwe bodi tendaji ili muwe na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi na si ushauri kama ilivyo sasa.Alisema Prof.Kambi

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Dkt.Grace Maghembe alisema wanatambua mchango wa bodi hizo kwani ndio walezi kwenye hospitali za rufaa za mikoa hivyo watasaidiana panapotokea mapungufu ili kuweza kurekebisha kwa haraka.

Dkt.Maghembe aliwataka wajumbe hao kusaidia kwa utashi katika kuimarisha  na kusimamia vyanzo vyanzo vya mapato yanayokusanywa pamoja na matumizi yake na kuzifanya hospitali za rufaa za mikoa kupunguza rufaa za hospitali kubwa na kuzifanya ziwe sehemu za kwanza za rufaa na kupunguza gharama za matibabu.

Kikao kazi hicho kinakutanisha wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa za mikoa kutoka mikoa kumi  kutoka Tanzania bara

Jumanne, 25 Juni 2019

WAZIRI WA AFYA ASISITIZA UBORA WA BIDHAA KATIKA KIWANDA KIPYA CHA DAWA NA VIFAATIBA SIMIYU.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba kwa Profesa Olipa David Ngassapa (kulia)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati akizindua bodi hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Picha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Watendaji Wakuu ndani ya Wizara ya Afya na Taasisi za Afya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu.

Na.WAMJW.Dodoma

Bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba cha Simiyu(SIMIYU MEDICAL PRODUCTS) wametakiwa  kuzalisha bidhaa zenye viwango na kukidhi mahitaji ya ndani nan je ya nchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho uliofanyika leo jijini hapa.

Waziri Ummy amesema kuwa bidhaa zenye viwango itasaidia kuuza nje ya nchi na watanzania kuzitumia kwani lengo la serikali ya awamu ya tano ni ya kukuza uchumi wa viwanda 

“Lakini mhakikishe maamuzi yeyote mtakayofanya mjiridhishe je ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa na je yatatufikisha kule tunapotaka kufika,jiridhisheni katika kuhakikisha mnatumia fedha hizi chache tulizonazo katika kuleta matokeo ya haraka haya ndiyo ya kuyazingatia”.Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy aliitaka bodi hiyo kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao ya nchi kwa kuzalisha bidhaa nchini na kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi,kuongeza ajira na hata kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo aliwataka wasiangalie bidhaa zinazotakana na pamba hivyo kwa baadae  ni bora wakaangalia bidhaa zingine zinazohitajika ambazo zinanunuliwa kwa haraka sana kutoka MSD kwani bohari ya Dawa hivi sasa imepata mkataba wa kununua bidhaa za hospitali kwa niaba ya nchi kumi na sita za nchi ya SADC hivyo wahakikishe bidhaa zinazozalishwa zina viwango na ubora na uzalishaji unakidhi soko la ndani nan je ya Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amempongeza Mtanzania Dkt. Aswar Hilonga kwa kutunukiwa tunzo na Shirika la Afya Duniani kutokana na Ubunifu wake wa kutengeneza mtambo wa kuchuja na kusafisha maji.

Mtambo huo unaotumia nanotechnology una uwezo wa kuchuja maji na kuyafanya yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu na kuondoa bakteria, kemikali na taka katika maji.

"Asilimia 60 ya wagonjwa wa nje wanaokwenda Hospitalini  wanatokana na kiwango duni cha hali ya usafi  ikiwenyo unywaji wa maji yasiyo safi na salama. Hivyo kupitia teknolojia hii tunaweza kuokoa fedha za Serikali kwa ajili ya kutibu wagonjwa" amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Dkt. Hilonga ameiomba Serikali kuweza kuunganisha mtambo huo wa maji ambao unauzwa kwa bei nafuu katika Taasisi za Umma ambao unachuja maji kwa kuondoa batkeria na kemikali na taka katika maji ndani ya muda mfupi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimpongeza Dkt. Askwar Hilonga (kulia) kwa kutunukiwa tuzo kutoka Shirika la Afya Duniani kwa  ubunifu wa mtambo wa kuchuja na kusafisha maji unaotumia nanotechnology kuondoa bakteria, kemikali na taka kwenye maji.

Mwisho.



DKT. CHAULA AWAFUNDA WAKUU WA VYUO VYA AFYA VYA SERIKALI

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Zainab Chaula akieleza jambo wakati akifungua Mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali uliofanyika Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Laizer akifuatilia maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainab Chaula (hayupo kwenye picha) pindi alipofungua Mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali uliofanyika Jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali akisoma Risala mbele ya mgeni rasmi ambae ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali, uliofanyika jijini Dodoma.

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula akiteta jambo na Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara ya Afya Dkt Laizer wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali, uliofanyika jijini Dodoma.

Baadhi Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakati alipofungua Mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali uliofanyika Jijini Dodoma.

Jopo la Wakuu wa Vyuo na Makaimu Wakuu wa vyuo vya Afya vya Serikali wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt Zainab Chaula wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu  wa vyuo vya Serikali uliofanyika Jijini Dodoma.


Na WAMJW- DOM

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Zainab Chaula amefungua Mkutano wa Wakuu wa Vyuo vya Afya vya Serikali uliofanyika Jijini Dodoma. 

Katika Mkutano huo Dkt. Zainab Chaula amewataka Wakuu wa vyuo kuongeza ubunifu katika utoaji huduma kwenye taasisi zao na kuboresha miundombinu jambo litakalosaidia kuinua kiwango cha elimu katika maeneo yao.

Kwa upande mwingine, Dkt. Chaula amewataka Wakuu hao wa vyuo vya Afya kuondoa dhana ya kuitegemea Serikali katika kila jambo ili kuwaletea Maendeleo, huku akisisitiza uanzishwaji wa vitega uchumi katika vyuo hivo jambo litalosaidia kupambana dhidi ya ukata wa fedha.

Aidha, Dkt Zainab Chaula amekemea vitendo vya uvunjaji wa maadili vinavyofanywa na baadhi ya Wakuu wa vyuo ikiwemo suala ya Rushwa, kufelisha wanafunzi, mambo yanayopelekea kutia doa Maendeleo ya taasisi hizo. 

"Mkuu wa Chuo ni kama mzazi, kuna baadhi ya maeneo unakuta Mkuu wa chuo anatongoza wanafunzi, wengine wanafukuzisha wanafunzi, mnaharibu Watoto wa wenzenu, kwa hali hii tutazipata wapi baraka za Mwenyezi Mungu " alisema Dkt Chaula 

Mbali na hayo, Dkt Zainab amewapongeza Wakuu hao wa Vyuo kwa Juhudi wanazoendelea kuchukua katika kuboresha vyuo hivo licha ya changamoto lukuki wanazoendelea kukumbana nazo.

Dkt. Chaula aliendelea kusema kuwa, Serikali inatambua Juhudi kubwa zinazofanywa na Wakuu wa vyuo vya Afya nchini na kuahidi kupokea changamoto zote na kuendelea kutafutia ufumbuzi kadiri inavyowezekana.

Ijumaa, 21 Juni 2019

KAULI YA SERIKALI KUHUSU MLIPUKO WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE NCHIN

- Hakuna maoni




KAULI YA SERIKALI KUHUSU MLIPUKO WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE NCHINI

1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni Na. 49 Ibara ya (1), (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la Mwaka 2016, naomba kutoa Kauli ya Serikali kuhusu mlipuko wa Homa ya Dengue nchini.

Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa Dengue sio ugonjwa mpya. Ugonjwa huu ulianza kutolewa taarifa hapa nchini tangu mwaka 2010, na kutolewa tena mwaka 2013, 2014, 2018 na mwaka huu (2019). Kidunia inakadiriwa watu milioni 390 huugua ugonjwa wa homa ya Dengue kila mwaka huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikiwa 40,000 kwa mwaka ikilinganishwa na ugonjwa wa Malaria ambapo watu 216 Million huugua ugonjwa huo kwa mwaka huku vifo vikiwa 450,000. Kama ilivyo katika nchi  nyingi duniani zinazoathirika na mlipuko wa ugonjwa huu, mara nyingi hutokea nyakati za mvua hasa katika maeneo ya mijini ambayo kuna mazalia mengi ya mbu kutokana na kutuwama kwa maji. Ugonjwa huu huenezwa na mbu aina ya Aedes ambae ni mbu mweusi mwenye madoadoa meupe ya kung’aa na ambaye hupendelea kuuma hasa wakati wa asubuhi, mchana na jioni.

Mheshimiwa Spika, dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa na kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati siku ya 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa Malaria. Aidha, mara chache hutokea mgonjwa wa homa ya Dengue, anapata vipele vidogovidogo, anavilia damu kwenye ngozi na wengine kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo. 

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019, ugonjwa huu umeanza kutolewa taarifa katika vituo vya kutolea huduma za Afya hapa nchini kuanzia mwezi Januari hadi tarehe 19 Juni 2019  jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo 4 vilivyotokana na  homa ya Dengue vimetolewa taarifa huku Mkoa wa Dar es salaam ndio unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi. Ifuatayo ni idadi ya wagonjwa na vifo kwa mikoa: Dar es salaam 4,029 na vifo 3, Dodoma 3 na kifo 1, Tanga 207 na vifo 0, Pwani 57 na vifo 0, Morogoro 16 na vifo 0, Arusha 3 na vifo 0, Singida 2 na vifo 0, na Kagera 2  na vifo 0. Aidha vifo vilivyotolewa taarifa  ni kutoka  katika hospitali za;   Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma -1, Hindu-Mandal -1 na Hospitali ya  Regency-2.

2.   HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI KUDHIBITI UGONJWA HUU
Mheshimiwa Spika, toka kuripotiwa kwa mlipuko wa Dengue, Wizara imeendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu, kwanza kwa kuandaa mpango wa dharura wa miezi sita (Mei-Oktoba, 2019) wa kukabiliana na ugonjwa wa Denguenchini. Katika mpango huu yafuatayo yanatekelezwa;
(i)           Kuangamiza mazalia ya mbu wapevu (Adults mosquitoes ) na viluwiluwi nchini ambapo Wizara imeshanunua kiasi cha lita 60,000 za Viuavidudu (biolarvicides) kutoka kwenye kiwanda cha uzalishaji kilichopo Kibaha kwa ajili ya kuangamiza viluwiluwi katika mazalia ya mbu. Kati ya hizi Lita 11,400 zimesambazwa kwenye Halmashauri 5 za mkoa wa Dar es Salaam. Lita 48,600 zinasambazwa kwenye Halmashauri za Mikoa ya Geita (lita 8,092), Kagera (Lita 12,308), Kigoma (7,616), Lindi (9,048) na Mtwara (Lita 11,536). Pia lita zingine 36,000 zimeagizwa ambapo zitasambazwa kwenye Mikoa yenye Mlipuko wa Ugonjwa huu ikwemo Pwani, Morogoro Tanga na Singida. Aidha Wizara imeagiza pia mashine kubwa 6 kwa ajili ya kupulizia mbu wapevu (aina ya Fogging machine) na mashine hizi zinatarajiwa kufika kabla ya mwisho wa mwezi Julai, 2019. Dawa za kunyunyizia nje (aina ya Acteric) lita 2,000 kwa ajili ya kuua mbu wapevu pia zimeagizwa ambazo zitasambazwa katika Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Tanga.
(ii)         Kuunda kikosi kazi cha watalaam cha kushughulikia udhibiti  wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa Dengue na Malaria nchini na inategemewa kuwa kikosi kazi hiki kitaimarisha jitihada za udhibiti mbu ndani  ya Mikoa na Halmashauri zote nchini hususan zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Dengue na Malaria yaani Dar es salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita na Kagera.
(iii)       Katika kuimarisha uchunguzi na matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Dengue, Bohari ya Dawa imeshanunua  vipimo 30,000 vya kupima Homa ya Dengue na awali Wizara ilielekeza Vituo vya umma vya kutolea huduma kutoa huduma ya vipimo vya Dengue kwa utaratibu wa kawaida wa uchangiaji wa gharama za matibabu.

(iv)       Kutengeneza na Kusambaza Mwongozo wa matibabu ya ugonjwa huu kwa ajili ya watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma
(v)         Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na magonjwa mengine.
(vi)       Kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari pamoja na ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, kupitia hatua hizi, takwimu za hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Dengue zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yameanza kupungua kutoka wagonjwa 2494 wa mwezi Mei 2019 hadi wagonjwa 813 kufikia tarehe 19 Juni, 2019.


3.   CHANGAMOTO YA UDHIBITI WA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto mbalimbali katika kudhibiti mlipuko wa Homa ya Dengue nchini. Changamoto hizi  ni pamoja na:
1.   Gharama za kupima Ugonjwa Homa ya Dengue
Ingawa Serikali kupitia Bohari ya Dawa imenunua vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na hivyo kuviuza kwa bei nafuu ukilinganisha na gharama inayotozwa kutoka kwenye baadhi ya Hospitali binafsi, bado Wananchi wanashindwa kumudu gharama za uchangiaji matibabu ya ugonjwa wa Homa Dengue

2.   Ushirikishwaji wa Jamii
Jamii bado haijaweza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni ya usafi wa mazingira ambayo ni njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mbu
3.   Matibabu ya Ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma
Watoa huduma za Afya kutokufuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa Homa ya Dengue

4.HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa Wizara imepitia  Miongozo na Kanuni za Kimataifa, ambayo pia ipo katika Sheria  ya Afya ya Jamii  namba 1. ya mwaka 2009 kuweza kupata mwongozo wa namna bora ya utoaji wa matibabu kwa mlipuko wa ugonjwa wa Dengue ambao upo sasa nchini. Kupitia sheria hii, vipo vipengele mbalimbali ambavyo vimeanisha jinsi gani matibabu ya magonjwa ya milipuko mikubwa kama ya Homa ya Dengue inapaswa kutolewa na hii ikiwemo utoaji wa matibabu bure ili  kurahisisha udhibiti wa magonjwa ya milipuko  yasisambae kwa haraka katika jamii.

Mheshimiwa Spika,  kwa kuzingatia sheria hii, Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mhe Rais, Dkt John Pombe Magufuli, inayojali wananchi wake, sasa imeamua kuwa vipimo kwa ajili ya Homa ya Dengue vitatolewa  BURE kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya vya umma wakati huu wa mlipuko.Aidha, Serikali itaboresha matibabu kwa wagonjwa kwa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa dawa za kutosha na pia itaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa  Afya sambamba na kuboresha mifumo ya ukusanyaji takwimu.

Mheshimiwa Spika,  ili kuhakikisha kuwa tunadhibiti  ugonjwa huu nchini, ninaitaka Mikoa na Halmashauri zote nchini hasa zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Dengue na Malaria kusimamia kikamilifu kampeni za usafi wa mazingira na kuangamiza mbu kwa kunyunyizia dawa kwa ajili ya kuuwa mbu wapevu na kutokomeza mazalia ya mbu. Aidha natoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kuchukuwa hatua stahiki za kujikinga na ugonjwa huu na kuimarisha usafi wa mazingira na kuangamiza mazalia ya mbu.



UMMY A. MWALIMU
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
 JINSIA, WAZEE NA WATOTO

21/06/2019

SERIKALI YAAGIZA KILA KIFO KINACHOTOKEA KUFANYIWA UFUATILIAJI

- Hakuna maoni
Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akisisitiza jambo mbele ya 
Wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam (RHMT) wakati alipokutana na  kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan magonjwa ya Dengue na Kipindupindu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Yudas Ndungile akiyoa maelezo kuhusu hali ya Afya na jitihada za mkoa katika kukabiliana na changamoto za magonjwa ya mlipuko wakati wa kikao cha Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya (Wakulia) na wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam.

Baadhi ya Wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam, wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipokutana na  kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan magonjwa ya Dengue na Kipindupindu.

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (aliyevaa suti) akieleza jambo mbele ya Wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam (RHMT) wakati alipokutana na  kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan magonjwa ya Dengue na Kipindupindu.


SERIKALI YAAGIZA KILA KIFO KINACHOTOKEA KUFANYIWA UFUATILIAJI

Na WAMJW- DSM 

Serikali imeagiza Waganga Wakuu wote kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa kila kifo kitakachotokea katika Hospitali zote nchini ili kubaini chanzo cha vifo hivo jambo litalosaidia kuimarisha mikakati katika kupambana na magonjwa, hususan magonjwa ya milipuko. 

hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi leo wakati alipokutana na wasimamizi wa huduma za Afya katika jiji la Dar es Salaam (RHMT) kujadiliana mbinu mbali mbali ili kuweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan katika kipindi hichi cha milipuko ya magonjwa ya Dengue na Kipindupindu. 

Dkt. Subi amesema kuwa katika vita dhidi ya magonjwa ya mlipuko ni lazima kushirikiana na taasisi nyingine kama vile DAWASA ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kurekebisha na kuimarisha miundombinu ya maji ambayo yanaweza kuwa moja ya chanzo cha mlipuko wa magonjwa hayo. 

Pia, Dkt Subi amesema kuwa moja ya makubaliano ya kikao hicho ni kuhakikisha inapofika Juni 30, ugonjwa wa Dengue uwe umekwisha katika jiji la Dar es Salaam.

"Wamenihakikishia kwamba inapofika tarehe 30, wamesema mbinu zote inatumika kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Dengue unaisha jijini Dar es Salaam au unapungua kwa kiwango ambacho hautoonekana" alisema Dkt Leonard Subi. 

Aidha, Dkt Subi amemwagiza Mganga Mkuu kuhakikisha wanatumia taarifa zote za wagonjwa ambao wanafariki kutoka na magonjwa ya Kipindupindu pamoja na ugonjwa wa homa ya Dengue ili kupata takwimu sahihi ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Aliendelea kusema kuwa Serikali imefanikiwa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu, huku ikifanikiwa kupunguza maambukizi ya homa ya Dengue kutoka wagonjwa 1000 kwa mpaka kufikia wagonjwa 200 kwa wiki, na jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huu.

Mbali na hayo Dkt. Subi alisisitiza kuwa katika mapambano dhidi ya mbu anaesababisha homa ya ugonjwa wa Dengue ni lazima kushirikisha wananchi katika ngazi ya Jamii ili kutoa elimu ya kutosha juu ya namna yakuzuia ugonjwa huu.

Kwa upande mwingine, Dkt. Subi amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha anashirikiana na Wakurugenzi ili kutimiza ahadi za kununua mashine za kunyunyizia maazalia ya mbu ambao wanasababisha ugonjwa wa Dengue. 

Hata hivyo, Dkt Subi ameagiza watu wote wanaobainika kutapisha maji machafu katika mazingira kuchukuliwa hatua kali kupitia sheria ya Afya ya jamii ya mwaka 2009.

Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Yudas Ndungile amemshukuru Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt Leonard Subi kwa muda aliotenga ili kufahamu kiundani hali ya utendaji kazi katika Sekta ya Afya katika ngazi ya mkoa na ameahidi kutekeleza maagizo yote ili kuendelea kuimarisha Sekta ya Afya.

Mwisho.