Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 5 Julai 2019

DKT. NDUGULILE ATAKA UONGOZI BORA NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI.

- Hakuna maoni

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wakati akifunga Kikao kazi kilichofanyika kwa siku tano na kupitisha maazimio ya kuimarisha huduma Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa tiba toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Maghembe akiongea wakati wa kilele cha kikao kazi cha Waganga Wafawidhi kilichofanyika Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi cheti cha pongezi kwa uongozi bora na usimamizi kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi Dkt. Yustina Tizeba wakati akifunga kikao cha waganga wafawidhi kilichofanyika Jijini Dodoma.


Picha mbalimbali zikimuonesha Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikabidhi vyeti kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana Dkt. Meshack Shimwela wakati akifunga kikao cha waganga wafawidhi kilichofanyika Jijini Dodoma. Hospitali ya Rufaa ya Amana imeongoza na kupata vyeti vitatu ikiwa ni pamoja na kuongoza kupunguza vifo vya mama na mtoto, uongozi bora na mikakati endelevu ya kukusanya mapato.


Picha za pamoja za Viongozi wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile, Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na Wakurugenzi wa Idara Mbalimbali wakati wa kufunga kikao cha Waganga Wafawidhi kilichofanyika katika ukumbu wa Mwalimu Nyerere Chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Na WAJMW-DOM

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka Waganga wafawidhi kutekeleza maazimio waliyopitisha katika kikao kazi kilichofanyika kwa siku tano Jijini Dodoma.

Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati akifunga kikao hicho kilichohusisha Waganga Wafawidhi, Makatibu Tawala wa Halmashauri na Manispaa pamoja na wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya nchini waliohudhuria kikao hicho.

“Ninatambua kuwa katika kikao hiki tumepitia mwongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na kuweka mipango na mikakati endelevu kwa timu za uendeshaji wa Hospitali hizi, ninaomba sana muende mkatekeleze ili kuimarisha Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa. Amesema Dkt. Ndugulile.

Katika kikao hicho Waganga Wafawidhi wameweka maazimio ambayo yataratibiwa katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato na kuondoa mianya ya upotevu wa mapato, kuimarisha na kuendelea kuzijengea uwezo timu za uendeshaji za Hospitali za rufaa za Mikoa katika kusimamia rasilimali watu, fedha, miundombinu n.k. Kuweka mikakati endelevu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, kila Hospitali kuandaa mkakati wa kununua vifaa na vifaa tiba vitakavyowezesha huduma za kibingwa kutolewa wakati wote, pamoja na kila Hospitali kuja na ubunifu/mikakati ya kukabiliana na upungufu wa watumishi katika maeneo yao kwa kushirikiana na wadau wa mikoa yao.

Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa maagizo kwa Waganga Wafawidhi kutekeleza mambo muhimu katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo wa uongozi na utawala, upatikanaji wa watumishi wenye sifa stahiki katika kada zote, uimarishaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma zilizokusudiwa, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba na vitendanishi pamoja na uimarishaji wa matumizi ya teknolojia, taarifa za afya na mawasiliano.

Pamoja na hayo Naibu Waziri amewapongeza Waganga Wafawidhi kwa kushiriki kikao hicho na kuwataka kwenda kutekeleza maazimio waliyopitisha ili kuboresha Hospitali za Rufaa za Mikoa katika maeneo tofauti yaliyokusudiwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kabla ya kufunga kikao Dkt. Ndugulile alitoa vyeti vya ubora wa huduma na pongezi, ambapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Katavi Dkt. Yustina Tizeba alipata cheti cha pongezi kwa muongozo wa maono, uongozi bora na usimamizi huku Hospitali ya Rufaa ya Amana ikipata vyeti vitatu vya ubora ikiwa ni pamoja na kuongoza katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, uongozi bora na mikakati endelevu ya kukusanya mapato na kuwepo kwa vifaa na vifaa tiba vinavyotumika katika huduma za kibingwa.

MWISHO

MAKATIBU TAWALA WAOMBWA KUENDELEA KUZISIMAMIA HOSPITSLI ZA RUFAA.

- Hakuna maoni

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula akisema jambo kwa wajumbe wa kikao cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika jana Jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Makatibu Tawala Mikoa Bi. Zena Said, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga akisema jambo katika kikao kazi cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichoandaliwa na Wizara ya Afya na kufanyika katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Mipango Dodoma.

Makatibu Tawala Mikoa nchini Tanzania wakisikiliza mada zinazowasilishwa katika Kikao Kazi na Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa.


Na WAMJW - Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewataka Makatibu Tawala nchini kuendelea kuzisimamia Hospitali za rufaa za mikoa ambazo kwa sasa zinasimamiwa na Wizara ya Afya.

Dkt. Chaula amesema hayo alipokutana na Makatibu Tawala kutoka Mikoa ya Tanzania Bara katika Kikao Kazi cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kinachoendela kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha mipango Jijini Dodoma.

“Licha ya Hospitali hizi kuhamishiwa usimamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  lakini bado zipo kwenye maeneo yenu, tunawategemea nyie Makatibu Tawala kuzisimamia hospitali hizi.” Amesema Dkt Chaula.

Dkt. Chaula amesema kuwa ni dhahiri lengo lilikuwa ni jema tuu kutoka kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwamba Hospitali zisimamiwe na Wizara ya Afya ili ziweze kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na Wizara ya Afya ambayo ndiyo Wizara mama inayotunga Sera na Miongozo pamoja na kusimamia Wadau.

Naye Mwakilishi wa Makatibu Tawala wa Mikoa katika kikao hicho Bi. Zena Said amempongeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao hicho cha kihistoria ambacho hakijawahi kufanyika kabla.

“Hili ni jambo la busara, pamoja na kwamba hizi Hospitali zimeondolewa kwenye mamlaka za Tawala za Mikoa lakini bado kuna mambo mengi ambayo bado tunayafanya kwa niaba ya Wizara” amesema Bi. Zena na kuendelea “Sisi kama viongozi tupo mikoani hatuwezi kukaa kuangalia mambo yakiharibika tukisema hizi Hospitali sio za kwetu”

Bi. Zena Said amesema kuwa Bado wanawajibika kwa njia moja au nyingine kuzisimamia kwa ajili ya kuleta ustawi kwa wananchi.

Kikao hicho cha kihistoria kinafanyika kwa mara ya kwanza tangu kuhamishiwa kwa usimamizi wa  Hospitali za Rufaa za Mikoa tarehe 25, Novemba 2017 ambacho kitakuwa endelevu kila mwaka huku kikiwakutanisha viongozi wa hospitali, Waganga wakuu wa Mikoa pamoja na watendaji na wadau wa Sekta ya Afya nchini.

Mwisho

Alhamisi, 4 Julai 2019

TANZANIA BILA DENGUE INAWEZEKANA

- Hakuna maoni
Timu ya Wahamasishaji wa masuala ya Afya, kutoka Manispaa ya Kinondoni wakichanganya dawa, ikiwa ni moja kati ya maandalizi ya kuanza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika maeneo yenye mazalia ya mbu wa Dengue.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiongoza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika Manispaa ya Kinondoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akieleza jambo mbele ya viongozi wa Manispaa wakati wa zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika Manispaa ya Kinondoni. Wakatikati ni Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Maulid Mtulia.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) wakielekea katika eneo lenye mazalia ya  mbu wanaosababisha homa ya Dengue, zoezi limefanyika katika eneo la Msisili Manispaa ya Kinondoni.

Moja kati ya eneo la mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa homa ya Dengue, ililopo eneo la Msisili Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.


TANZANIA BILA DENGUE INAWEZEKANA

Na WAMJW-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. @ummymwalimu leo ametembelea katika Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa Mikoa/Halmashauri ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Dengue.

Katika ziara hiyo Waziri @ummymwalimu ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zinazochukuliwa na Manispaa ya Kinondoni za kupambana na Ugonjwa wa Homa ya Dengue hali iliyochangia kupungua kwa Idadi ya Wagonjwa kutoka Wagonjwa 604 Mwezi Mei hadi kufikia Wagonjwa 450 Mwezi Juni. 

“ Nafurahi kuona kwamba idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue katika Wilaya ya Kinondoni, Mwezi Mei kulikuwa na Wagonjwa ambao wamepima na kuthibitishwa 604, lakini mwezi wa tano Wagonjwa wamepungua hadi 450” Alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, takwimu za Kitaifa za Wizara ya Afya, mwezi Mei tulikuwa na idadi ya Wagonjwa wa homa ya Dengue 3170, na wamepungua Mwezi wa Sita hadi kufikia Wagonjwa 1446, hali inayotoa matumaini katika kuimaliza vita hii ya homa ya Dengue.

Aidha, Waziri Ummy amewapongeza Watendaji wa Sekta ya Afya katika Manispaa ya Kinondoni kwa hatua wanazoendelea kuchukua, ikiwemo kununua Viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu na kununua mashine mpya za kupuliza dawa (motorised sprayers), katika maeneo yenye mazalia ya mbu.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesisitiza juu ya ushiriki wa Wananchi katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa homa ya Dengue, huku akieleza kuwa mapambano dhidi ya mbu wa Dengue yatasaidia kupunguza magonjwa mengine kama Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano.

“Ushiriki wa Wananchi ni muhimu sana katika kupambana na ugonjwa wa Dengue, tukipambana na Dengue, kwa upande mwingine tunakuwa tunapambana na ugonjwa wa Malaria, Matende, Chikungunya, Zika, Homa ya Manjano, kwhiyo ni lazima tuhakikishe kila mtu anashiriki katika kupambana dhidi ya mbu.” Alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Maulid Mtulia amekazia kwa kuwahasa Wananchi juu ya ushiriki katika vita hii dhidi ya ugonjwa wa Dengue na kusisitiza kuwa Serikali haiwezi kushinda vita hii bila ushirikiano wa Wananchi.

Nae, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamin Sitta amesema kuwa Jumla ya shilingi Milion 132 kwaajili ya zoezi lakutokomeza homa ya Dengue, 90 zimetumika kwaajili ya zoezi zima la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, huku 42 kwaajili ya kununua Mashine za kubwa ya upuliziaji wa dawa hizo.

“Tumetumia gharama ya takribani Milion 90 kwaajili ya upuliziaji katika kila kata na tupo mbioni kuongeza Milioni 42 kwajili ya mashine kubwa yenye uwezo wa kusambaza mara moja kwa kata 10, kwahiyo kwa ujumla tutakuwa tumetumia takribani Milion 132 kwaajili ya zoezi la kuhakikisha tunatokomeza ugonjwa wa Dengue.” Alisema Mhe. Benjami Sitta.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt.  Festo amesisitiza kuwa Huduma za vipimo vya homa ya Dengu zinapatikana katika vituo vya Serikali vya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo na vituo binafsi bei elekezi isizidi shilingi 50,000/

“Huduma hizi za vipimo zinapatikana kwenye vituo vyetu, na katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Hospitali ya Lugalo bila malipo, lakini katika vituo binafsi, bei elekezi isizidi 50,000/ kwa kipimo cha Dengue” alisema Dkt. Festo

Pia, amewaasa Wananchi kuwahi katika vituo vya Afya, pindi waonapo dalili za ugonjwa wa homa ya Dengue na kuachana na mawazo potofu ya matibabu ya Dengue kama majani ya mpapai kwani yanawezapelekea kupata matatizo mengine yakiafya.

Mwisho.

Jumatano, 3 Julai 2019

DKT. NDUGULILE AISIFU HALMASHAURI YA WILAYA YA BAHI KWA KUFANIKISHA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akitoa maelekeozo kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma wakati alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Mpya ya Wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Bi. Mwanahamisi Mkunda, Mkurugenzi wa Halmashauri Dkt. Fatuma Mganga na kulia ni Mbunge viti maalum wa Dodoma Bi. Felista Bula, mbunge wa jimbo la Bahi Omary Badwel na Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Philipina Philipo.

Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile akimuangalia fundi mwana mama aliyekua anapaka rangi katika majengo ya Hospitali Mpya ya Wilaya ya Bahi wakati alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo mapema leo.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulie akielekeza jambo kwa viongozi wa wilaya wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Hospitali mpya ya wilaya ya Bahi mapema leo. 



Baadhi ya majengo ya Hospitali mpya ya Wilaya ya BAHI.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile akihesabu mabati ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi wakati alipofanya ziara ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa zahanati hiyo leo.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wananchi wa kijiji cha Chonde waliofika katika mkutano ambao ulitanguliwa na ziara ya ukaguzi wa zahanati ya kijiji hicho.

NA WAMJW-BAHI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameusifu uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kutekeleza ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo ukiwa umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90.

Dkt. Ndugulile amesema hayo mapema leo baada ya kutembelea ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia hatua za mwisho na kuridhishwa na hatua iliyofikia hadi sasa huku akiusifu uongozi wa Halmashauri chini ya Mkuu wa Wilaya Bi. Mwanahamisi Mkunda kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao.

“Napenda kuwapongeza sana kwa kazi nzuri na ushirikiano mnaoonesha katika kutekeleza mradi huu, ninaamini majengo haya yakikamilika tutaanza kutoa huduma kwa sababu OPD tunayo, jengo la upasuaji, Maabara, jengo la Radiolojia na pia huduma ya Mama na Mtoto tunaweza kuanza nazo”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Baada ya kutembelea majengo mbalimbali ya Hospitali hiyo Dkt. Ndugulile ameonesha kuridhishwa na ujenzi huo na kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya kuhakikisha huduma zinaanza kutolewa haraka iwezekanavyo ili kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi wa eneo hilo.

Aidha, Dkt. Ndugulile ametembelea ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Chonde Wilayani Bahi na kushangazwa na kasi ndogo ya ujenzi ambao ulianza toka mwaka 2007 lakini haujakamilika mpaka leo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa fedha.

Dkt. Ndugulile ameonyesha kutoridhishwa na gharama za ujenzi ambao unagharimu Shilingi Milioni 90 mpaka kukamilika. Kufuatia hatua hiyo ameagiza ujenzi wa zahanati hiyo kutumia utaratibu wa Force Account na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Dkt. Fatuma Mganga kuleta wataalamu kwa ajili ya kuhakiki gharama za vifaa vinavyohitajika.

Pamoja na hayo Naibu Waziri huyo ameahidi kutoa mifuko 50 ya Saruji ili kuchangia gharama za ujenzi huku akitoa miezi mitatu ya ukamilishaji wa ujenzi huo. Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. Mwanahamisi Mkunda amemuahidi Naibu Waziri kukamilika kwa ujenzi wa zahanati ndani ya muda uliowekwa na amechangia mifuko 10 ya saruji huku Mbunge wa Viti Maalum wa Dodoma Bi. Felista Bula akichangia Mifuko 20 ili kuchochea kasi ya ujenzi na huduma zianze kutolewa ifikapo Septemba mwaka 2019.

MWISHO

SERIKALI YAJIIMARISHA KUIMALIZA DENGUE

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiambatana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakiwa katika  zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiongozana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakielekea katika  zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Iliyobebwa ni moja kati ya mashine mpya 14 za kupuliza dawa (motorised sprayers) zilizonunuliwa na Manispaa ya Ilala ikiwa ni moja ya jitihada yakupambana dhidi ya ugonjwa wa homa ya Dengue katika Manispaa hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongoza zoezi la upuliziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu, katika eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliyevaa buti) akiambatana na Mkuu  wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia  Mjema pamoja na Mbunge wa Ilala Mhe. Mussa Azzan Zungu, wakinyunyiza dawa katika mazalia ya mbu, eneo la Mchikichini Manispaa ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.

Baadhi ya mtaro katika eneo la Ilala Mchikichini Jijini Dar es salaam, ambao ni moja ya sababu ya mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa homa ya Dengue


Na WAMJW- DSM 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. @ummymwalimu leo amefanya ziara katika eneo la Mchikichini Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa Mikoa/Halmashauri ya kupambana dhidi ya ugonjwa  wa Dengue.

Kwa kiasi kikubwa Waziri @ummymwalimu ameridhishwa na hatua walizochukua na Manispaa ya Ilala ikiwemo kununua mashine mpya 14 za kupuliza dawa (motorised sprayers), kununua Viuadudu kutoka kiwandani Kibaha lita 3,980 (shs 53m) na kununua lita 210 za kuua mbu wapevu. Huku upuliziaji ukiendelea ktk kata 25.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa, Matokeo ya jitihada hizi yanaoneka, huku Idadi ya wagonjwa wa Dengue Wilaya ya Ilala ikipungua kutoka wagonjwa 527 mwezi Mei 2019  hadi wagonjwa 207 mwezi June 2019. 

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa, katika Jiji zima la Dar es Salaam wagonjwa wa homa  ya Dengue wamepungua kutoka 2,759 mwezi Mei 2019 hadi wagonjwa 790 mwezi June.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amewataka wananchi kushiriki kikamilifu ktk kutokomeza mazalia  ya mbu, kwa kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka, kupulizia dawa maeneo yote yenye mazalia ya mbu,  pia kutumia chandarua chenye dawa wakati wote.

Mwisho.

Jumatatu, 1 Julai 2019

HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA ZATAKIWA KUWA NA VIFAA MUHIMU VYA KUTOLEA HUDUMA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu akihutubia Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa waliofika katika Mkutano unaoanza leo jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (katikati) akizndua muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za mikoa wakati wa uzinduzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Mikoa unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace Maghembe na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Muhammad Kambi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alifurahia muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa aliouzindua mapema leo, kulia ni Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace Maghembe, akipokea muongozo huo kutoka kwa katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na katikati ni Naibu waziri Dkt. Faustine Ndugulile akishuhudia.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza alilozindua wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa unaoendelea jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile na Kulia ni Katibu wa Afya Dkt. Zainab Chaula
Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Afya na TAMISEMI wakiongozwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakionesha jarida la afya ya jamii toleo la kwanza lililozinduliwa leo na Waziri Ummy.

NA WAMJW-DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kuhakikisha wanakua na vifaa vya muhimu vya kutolea huduma za afya kwa wagonjwa wanaofika Hospitalini kupata matibabu.

Waziri Ummy amesema hayo wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Waziri Ummy amewataka Waganga Wafawidhi hao kubainisha aina ya vifaa vya matibabu vinavyotakiwa kupelekwa katika Hospitali  zao ili kuhakikisha mgonjwa anapofika Hospitalini hakosi huduma wakati anapoenda kupata matibabu.

“Mganga Mfawidhi unatakiwa useme vifaa gani ukivipata utaboresha huduma, hatutaki mgonjwa afike Hospitali halafu akose huduma, boresha kwanza kupata vifaa vya msingi kabla ya vile vikubwa kama CT-Scan”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya chini ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa ili mwananchi akifika katika Hospitali za Rufaa aseme kweli huduma zimeboreshwa.

“Lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kila Hospitali ya Rufaa inakua na huduma za kipaumbele 13 zikiwepo huduma za mama na mtoto ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na magonjwa mengine ambayo yanaweza kutibiwa bila kumpa rufaa mgonjwa”. Ameongeza Waziri Ummy.

Kwa upande wake, Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za mikoa kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato kwa kufunga mfumo utakaotumika kukusanya mapato na kuachana na makaratasi.

“Tuendelee kuboresha huduma za afya na kusimamia ubora wa huduma tunazozitoa na kuboresha upatikanaji wa vifaa na kuwa wabunifu japokuwa tuna changamoto za rasilimali watu ila huduma za kibingwa ziboreshwe ili kupunguza rufaa za nje”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula amewataka Waganga Wafawidhi hao kuhakikisha wanaripoti taarifa za maendeleo ya Hospitali na atakayeshindwa kufanya hivyo hataendelea na uongozi. Pia amewataka Waganga Wafawidhi hao kuwa na ushirikiano ili kufanya sekta ya afya kuwa ya mfano.

“Tuhakikishe tunaweka mifumo vizuri ya kutoa huduma kwa wahitaji kuanzia ngazi ya chini kwa kufuata miongozo na mikataba iliyotolewa, na tufanye kazi kwa ushirikiano bila kujali cheo au nafasi ya mtu”. Amesema Dkt. Chaula.

Pamoja na hayo katika Mkutano huo Waziri Ummy alizindua muongozo wa uendeshaji wa Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na jarida la afya ya jamii toleo la kwanza.

MWISHO

Jumamosi, 29 Juni 2019

HUDUMA ZA DHARURA KWA WAJAWAZITO ZAENDELEA KUSAMBAA NCHINI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza  jambo mbele ya wananchi (hawapo kwenye picha) wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Watatu kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama,  Kulia kwa Waziri Ummy ni Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakinyoosha viungo muda mfupi baada ya kumaliza matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi wa Amref Health Africa nchini Bi. Florence Temu akiwasilisha taarifa ya mradi wa  SUAM mbele ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) wenye lengo la kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wakatikati) pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakimkabidhi zawadi ya cheti Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Charles Itembe kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha matembezi hayo ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa wakunga kwa uzazi salama nchini.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuwezesha uwepo wa Wakunga kwa uzazi salama, yaliyofanyika katikati viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam.


Na WAMJW- DSM 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, yaendelea kuboresha huduma za Afya za dharura nchini kwa kuviwezesha vituo vya Afya kuweza kutoa huduma za uzazi wa dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ili kuokoa vifo vitokanavyo na matatizo ya uzazi pingamizi. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu leo wakati wa matembezi ya hisani yanayolenga kuchangia Juhudi za kupunguza na kuepusha vifo vya wajawazito na Watoto wachanga vitokanavyo na uzazi, katika viwanja vya farasi Jijini Dar es Salaam. 

Waziri Ummy amesema kuwa wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani ilikuwa vituo vya Afya takribani 109 sawa na asilimia 19 ya vituo vya Afya ambavyo vilikuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura pamoja na kumtoa mtoto tumboni, huku sasa kuongezeka hadi kufikia takribani vituo 460.

Aidha, Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa kila mwaka Wanawake 11,000 hufariki nchini, sawa na wanawake 900 kila mwezi, ikiwa ni sawa na wanawake 30 kila siku hufariki wakiwa wanatimiza wajibu wao wa msingi wakuleta kiumbe Duniani, hivyo ni lazima Juhudi za ziada ziendelee kuchukuliwa. 

Kulingana na takwimu zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba vifo katika kila vizazi hai 100,000 wanawake 556 hufariki, huku wanawake wajawazito nchini wakiwa Milioni 2 kwa mwaka

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa hadi kufikia takribani Bilioni 260, ikilinganishwa na bajeti ya Bilioni 30 iliyokuwepo kabla ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, huku dawa kama ’magnesium sulfate' kwa ajili ya kifafa cha mimba zikipatikana bila malipo.

"Tumeweza kuongeza bajeti ya dawa, wakati tunaingia madarakani ilikuwa takribani Bilioni 30, sasa hivi tunazungumzia bajeti ya dawa ya Bilioni 260, huku dawa kama magnesium sulfate kwa ajili ya kifafa cha mimba zinapatikana bure bila malipo yoyote katika vituo vyetu vya kutoa huduma za Afya " alisema Waziri Ummy. 

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa licha ya maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa bado kuna changamoto ya Watoa huduma za Afya, hivyo amelipongeza Shirika la Amref kwa jitihada za kuajiri baadhi ya Watoa huduma jambo linalosaidia kupunguza changamoto katika Sekta ya Afya. 

"Tunauhitaji wa watumishi wa Afya takribani 200,008 katika vituo vya Afya vya Serikali kuanzia ngazi ya Zahanati mpaka ngazi ya Hospitali za rufaa za mikoa, huku watumishi waliopo ni takribani 98,000, hivyo pengo likiwa ni Asilimia 52, huku Zahanati zikiwa ndio waathirika wakubwa" alisema Waziri Ummy

Nae Waziri wa Afya wa Serikali ya watu wa Zanzibar Bw. Hamad Rashid Mohamed amewataka wakina mama kuwai katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi waonapo dalili za ujauzito, ili kuokoa vifo ambavyo vinaweza zuilika wakati wa kujifungua.

"Katika zile siku 12 za mwanzo wajitahidi kufika katika vituo vya Afya kupata uangalizi, na vifo vingi ndio huanza kutokea hapa, kwahiyo ningeomba sana wakinamama kuwahi katika vituo vya Afya, kuonana na wakunga waliopata elimu ili wapate huduma kwa wakati " alisema Hamad Rashid.

Mwisho

Jumatano, 26 Juni 2019

BODI ZA HOSPITALI ZA RUFAA ZATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya akisema jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa (hawako pichani) katika Kikao kazi kilichofanyika jana Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wakiwa katika kikao kazi.


Wajumbe wa Bodi ya Ushauri wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wakiwa katika kikao kazi.

Na.WAMJW,Dodoma

Wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa nchini wametakiwa kutatua changamoto zilizopo kwenye hospitali zao ili wananchi wapate huduma zilizo bora

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu,Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Zainabu Chaula wakati akifungua kikao kazi cha uhamasishaji wa wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa za mikoa kinachofanyika jijini hapa

Dkt.Chaula alisema wizara inawategemea na kuwathamini wajumbe hao  katika kuleta mabadiliko ya uimarishaji wa huduma za afya katika hospitali za mikoa zilipo katika maeneo yao hivyo wanatakiwa kuwa wabunifu.

“Nyie ndio macho yetu kule,tumewapa wajibu hivyo tunawategemea mtushauri na kuleta mafanikio katika maeneo yenu".Alisisitiza Dkt.Chaula

Aidha,aliwataka wabuni katika kuongeza vyanzo vya mapato ili hospitali hizo ziweze kuwahudumia wananchi ipasavyo na si kwenda hospitali za ngazi za juu“madaktari bingwa wanatengenezwa wananchi hawapaswi kwenda hospitali kubwa bali hospitali za rufaa"alisema Dkt.Chaula

Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Mohhamad Bakari Kambi alisema wanatarajia mabadiliko makubwa katika rasiliamali watu hususan kwenye sekta ya afya  kwa kuwa wabunifu.

"Tutawapima kwa utendaji  na mafanikio yenu na hivyo tutapenda baadae muwe bodi tendaji ili muwe na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi na si ushauri kama ilivyo sasa.Alisema Prof.Kambi

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Dkt.Grace Maghembe alisema wanatambua mchango wa bodi hizo kwani ndio walezi kwenye hospitali za rufaa za mikoa hivyo watasaidiana panapotokea mapungufu ili kuweza kurekebisha kwa haraka.

Dkt.Maghembe aliwataka wajumbe hao kusaidia kwa utashi katika kuimarisha  na kusimamia vyanzo vyanzo vya mapato yanayokusanywa pamoja na matumizi yake na kuzifanya hospitali za rufaa za mikoa kupunguza rufaa za hospitali kubwa na kuzifanya ziwe sehemu za kwanza za rufaa na kupunguza gharama za matibabu.

Kikao kazi hicho kinakutanisha wajumbe wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa za mikoa kutoka mikoa kumi  kutoka Tanzania bara

Jumanne, 25 Juni 2019

WAZIRI WA AFYA ASISITIZA UBORA WA BIDHAA KATIKA KIWANDA KIPYA CHA DAWA NA VIFAATIBA SIMIYU.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba kwa Profesa Olipa David Ngassapa (kulia)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati akizindua bodi hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisema jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu leo Jijini Dodoma.

Picha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Watendaji Wakuu ndani ya Wizara ya Afya na Taasisi za Afya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Dawa na Vifaatiba cha Simiyu.

Na.WAMJW.Dodoma

Bodi ya wakurugenzi wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba cha Simiyu(SIMIYU MEDICAL PRODUCTS) wametakiwa  kuzalisha bidhaa zenye viwango na kukidhi mahitaji ya ndani nan je ya nchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa bodi ya wakurugenzi wa kiwanda hicho uliofanyika leo jijini hapa.

Waziri Ummy amesema kuwa bidhaa zenye viwango itasaidia kuuza nje ya nchi na watanzania kuzitumia kwani lengo la serikali ya awamu ya tano ni ya kukuza uchumi wa viwanda 

“Lakini mhakikishe maamuzi yeyote mtakayofanya mjiridhishe je ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa na je yatatufikisha kule tunapotaka kufika,jiridhisheni katika kuhakikisha mnatumia fedha hizi chache tulizonazo katika kuleta matokeo ya haraka haya ndiyo ya kuyazingatia”.Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy aliitaka bodi hiyo kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao ya nchi kwa kuzalisha bidhaa nchini na kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi,kuongeza ajira na hata kuondokana na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo aliwataka wasiangalie bidhaa zinazotakana na pamba hivyo kwa baadae  ni bora wakaangalia bidhaa zingine zinazohitajika ambazo zinanunuliwa kwa haraka sana kutoka MSD kwani bohari ya Dawa hivi sasa imepata mkataba wa kununua bidhaa za hospitali kwa niaba ya nchi kumi na sita za nchi ya SADC hivyo wahakikishe bidhaa zinazozalishwa zina viwango na ubora na uzalishaji unakidhi soko la ndani nan je ya Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amempongeza Mtanzania Dkt. Aswar Hilonga kwa kutunukiwa tunzo na Shirika la Afya Duniani kutokana na Ubunifu wake wa kutengeneza mtambo wa kuchuja na kusafisha maji.

Mtambo huo unaotumia nanotechnology una uwezo wa kuchuja maji na kuyafanya yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu na kuondoa bakteria, kemikali na taka katika maji.

"Asilimia 60 ya wagonjwa wa nje wanaokwenda Hospitalini  wanatokana na kiwango duni cha hali ya usafi  ikiwenyo unywaji wa maji yasiyo safi na salama. Hivyo kupitia teknolojia hii tunaweza kuokoa fedha za Serikali kwa ajili ya kutibu wagonjwa" amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Dkt. Hilonga ameiomba Serikali kuweza kuunganisha mtambo huo wa maji ambao unauzwa kwa bei nafuu katika Taasisi za Umma ambao unachuja maji kwa kuondoa batkeria na kemikali na taka katika maji ndani ya muda mfupi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akimpongeza Dkt. Askwar Hilonga (kulia) kwa kutunukiwa tuzo kutoka Shirika la Afya Duniani kwa  ubunifu wa mtambo wa kuchuja na kusafisha maji unaotumia nanotechnology kuondoa bakteria, kemikali na taka kwenye maji.

Mwisho.