Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 18 Desemba 2019

NIMR MKOANI MBEYA YAFANIKIWA KUTAFITI KIPIMO CHA VVU KWA WATOTO WACHANGA

Mkurugenzi wa NIMR Mkoani Mbeya, Dkt. Nyanda Ntinginya akiongea na maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Afya na Taasisi zake ambao wametembelea nyanda za juu kusini katika kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta ya Afya”.

Dkt. Nyanda akitoa maelezo kwa  Maafisa wa Wizara na Taasisi zake kuhusiana na moja za mashine za maabara zinazopatikana katika Maabara ya NIMR - Mbeya.

Mtaalam wa Maabara akiwa anatimiza majukumu yake katika Maabara ya NIMR mkoani Mbeya

Mtaalamu wa Maabara Abisai Kisinda akionesha mtungi wa Liquid Nitrogen Tank wa kuvuna Nitrogen kwa ajili ya kuhifadhia sampuli za utafiti ulioko kwenye maabara ya NIMR mkoani Mbeya.

Mtaalamu wa Maabara Bariki Mtafya akionesha mashine za Gene Xpert zinazotumika kupima sampuli za Kifua Kikuu zilizoko katika Maabara ya NIMR Mkoani Mbeya.


Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Afya na Taasisi zake  wakiwa pamoja na Waandishi wa Habari walipotembelea Maabara ya NIMR Mkoani Mbeya.



Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu kanda ya nyanda za juu kusini (NIMR) imepiga hatua kubwa katika shughuli za utafiti inazofanya ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na watalaamu waliobobea.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa NIMR wa kanda hiyo Dkt. Nyanda Ntinginya wakati akiongea na maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara ya Afya na Taasisi zake ambao wametembelea nyanda za juu kusini katika kutekeleza kampeni ya “Tumeboresha Sekta ya Afya” ili kuona mafanikio ya  sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano ya Rais John Magufuli akiwa madarakani.

Dkt. Nyanda amesema moja ya mafanikio makubwa ya NIMR ya kanda hiyo ni Utafiti wa vipimo vya awali vya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye maambukizi.

Utafiti huo ujulikanao kwa jina la 'BABY' uliofanywa na Taasisi  hiyo unatumia kipimo cha “Early Infant Diagnosis (EID)” ambacho ufanyika kwa kutumia mashine za Gene Xpert.

Kwa mujibu wa Dkt. Nyanda amesema awali, upimaji wa kawaida ulikuwa unafanywa kwa watoto wachanga wenye wiki 4 hadi 6 na majibu yake yalikuwa yakichukua wiki mbili.

Dkt. Nyanda amesema utafiti huo uliofanyika Julai 2015 hadi Novemba 2016 kituo cha NIMR Mbeya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Munich cha nchini Ujerumani ulilenga kutathimini vipimo vya awali vya VVU kwa watoto wachanga ambao wazazi wao wameathirika.

"Huu utafiti ulilenga kufanya tathmini ya vipimo vya awali vya VVU katika kituo cha kutolea huduma na vipimo vilifanywa na wauguzi tofauti na upimaji wa sasa ambao huhitaji wataalamu wa maabara na hivyo kuhitaji usafirishaji wa sampuli za damu kwenda maabara ya kanda au ya mkoa”. Amesema Dkt. Nyanda.

Matokeo ya utafiti yameonesha vipimo hivyo vilifanya vizuri kwa asilimia 100 na vinatoa majibu ndani ya masaa mawili tu na hivyo mgonjwa kupewa majibu yake siku hiyo hiyo ukilinganisha na upimaji wa kawaida ambapo huchukua wiki mbili au zaidi kupata majibu.

“Upimaji wa VVU wa awali kwa watoto wachanga umejumuishwa katika muongozo wa sasa wa utoaji wa huduma za VVU nchini,”alisema.

Hata hivyo, matokeo ya utafiti huo uliofanywa nchini Tanzania, Afrika ya kusini na Msumbiji yamepelekwa Shirika la Afya Duniani(WHO) kutoa miongozo ya upimaji wa VVU kwa watoto hao katika muongozo wa utoaji wa huduma za VVU wa mwaka 2016.

Maabara ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ya Mkoani Mbeya imepata ithibati ya ubora wa kimataifa Maabara za utafiti ya nchini Marekani "College of American Pathologists" (CAP) kutokana na ubora wake wa kufanya tafiti ambapo ithibati hiyo imetolewa kwa nchi mbili tu katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa ni Tanzania na Uganda.

WARATIBU WA MTUHA WATAKIWA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA TAKWIMU SAHIHI

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Saitore Laizer akiongea na waratibu wa  mfumo wa taarifa,na ufuatiliaji wa huduma za afya kutoka mikoa na halmashauri nchini.

Kaimu mkurugenzi msaidizi ufuatiliaji na tathimini kutoka wizara ya afya Tumainiel Macha  akiongea kwenye kikao kazi hicho.

Mwenyekiti wa waratibu hao Dkt. Ally Msoke akitoa neno la shukrani wakati wa ifunguzi wa mkutano huo.

 Waratibu hao wakimsikiliza mgeni rasmi(hayupo pichani)  wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho.kinachofanyika chuo cha mipango Dodoma.

Picha ya pamoja ya watumishi kutoka wizara ya afya na OR-TAMISEMI na mgeni rasmi.


WARATIBU WA MTUHA WATAKIWA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA TAKWIMU SAHIHI

Na. Catherine Sungura, Dodoma

Waratibu wa Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya (MTUHA) nchi wametakiwa kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi za sekta ya afya  katika maeneo yao ya kazi.

Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mkurugenzi wa mafunzo na rasiliamali watu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Saitore Laizer wakati akifungua  kikao kazi cha waratibu MTUHA wa mikoa na halmashauri Tanzania kinachofanyika jijina hapa.

Dkt. Saitore amesema kuwa Wizara imeboresha mfumo wa takwimu kulingana na mahitaji  ya sasa na zinaingizwa na kuchanganuliwa kwa kutumia program maalum ya kompyuta katika ngazi ya wilaya ijulikanayo  kama ‘District health information software-DHIS 2’, hivyo ana imani  watasimamia na kuratibu kwa umakini.

“Matarajio ya wizara ni kuwa takwimu  zinazopatikana kutoka katika program hii zitakuwa sahihi  na mtatengeneza  orodha ya kielekroniki ya vituo vya kutolea huduma  za afya  ili kusaidia  katika mipango na kutoa maamuzi katika Sekta ya Afya”.

Vile vile Dkt. Saitore aliwataka waratibu hao kuweka mipango kabambe ili kuhakikisha mrejesho wa zoezi la uhakiki  wa ubora wa takwimu za afya  uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja  na kutoa mafunzo ya mrejesho katika meza maalum zitakazoandaliwa ili kutoa msaada wa watumishi ambao wanahitaji kujifunza,kupata ufafanuzi au kuuliza na kupata majibu ya masuala ya MTUHA yanayowasumbua  katika maeneo ya kazi .

Hata hivyo aliwataka waratibu hao kuhakikisha  halmashauri zinatenga fedha kwa ajili ya  MTUHA katika mpango kabambe wa  halmashauri(CCHP) na timu za  za afya za mikoa na halmashauri na Wadau wa Maendeleo wanashiriki kikamilifu katika kuimarisha  upatikanaji wa takwimu sahihi za Sekta ya Afya.

Mfumo wa taarifa za utoaji wa huduma za afya nchini umesaidia kuwezesha sekta ya afya kupata takwimu sahihi na kwa wakati zinazowezesha kufanya maamuzi sahihi katika kupanga na kutekeleza malengo yake ili hatimaye kufikisha huduma bora kwa wananchi kutoka asilimia 43 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2019.

Jumanne, 17 Desemba 2019

KAYA ZENYE VYOO BORA ZIMEONGEZEKA KUFIKIA ASILIMIA 62.4 NCHINI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza jambo katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Mhe. Musa Sima akitoa maelekezo kwa maafisa Afya katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akiwasalimia Maafisa Afya, katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Ntuli Kapologwe akitoa salamu za Waziri wa OR TAMISEMI katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi akieleza jambo katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Afya waliohudhuria katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini Dodoma. 

Baadhi ya Maafisa Afya kutoka Mikoa,halmashauri  wakifuatilia kwa makini maagizo kutoka kwa mgeni rasmi, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha).

Washindi wa Makala Televisheni ya Usafi wa Mazingira wanaotoka ITVwakipokea tuzo na zawadi kutokana na kuibuka namba moja.

Waandishi waliofanikiwa kushinda tuzo mbali mbali na zawadi kwa kuandaa makala na vipindi (Radio na Televisheni) kuhusu usafi wa mazingira wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Afya na Wadau wa Mazingira.



KAYA ZENYE VYOO BORA ZIMEONGEZEKA KUFIKIA ASILIMIA 62.4 NCHINI

Na. Catherine Sungura,Dodoma

Kaya zenye vyoo bora nchini zimeongezeka hadi kufikia asilimia 62.4 mwaka 2019 kutoka asilimia 34 mwaka 2015 kupitia kampeni ya usichukulie poa, nyumba ni choo iliyoendeshwa kipindi cha miaka miwili na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira  kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa,halmashauri  na wadau uliofanyika jijini hapa .

“Katika kipindi cha miaka miwili ya kampeni hii  kaya zenye vyoo bora zimeongezeka ,vile vile  kaya zisizokuwa na vyoo kabisa imepungua kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 1.9 katika kipindi hiki”Amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema  kwa upande wa wa vijiji ambavyo kaya zake zote zina vyoo imeongezeka kutoka 743 hadi 4,311 na kwa upande wa taasisi wameweza kuboresha  huduma ya maji na usafi wa mazingira katika vituo vya tiba  1,267 kati ya lengo  la vituo 1,000.

“Haya si mafanikio  ya kubeza na kimsingi ninapenda kuwashukuru wadau  kwa kushirikiana  na serikali kufanikisha kapeni hii,lengo letu ni kufuta kabisa  kaya zisizokuwa  na vyoo  na kuongeza kaya zenye vyoo boras hadi asilimia 75 ifikapo Juni,2021”.

Kwa upande wa maeneo ya kutupia taka ngumu,Waziri huyo amesema kuwa  Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuboresha maeneo ya kutupia taka  hususan madampo yaliyopo kwenye miji ili yawe ya kisasa.

Hata hivyo amesema kuwa uchakuzi wa mazingira utokanao na taka ngumu umeendele kuwa changamoto  katika maeneo ya mijini,hivyo serikali imejipanga kuongeza nguvu kwenye mamlaka za serikali za mitaa ili kuboresha miundombinu iliyopo katika mitaa hapa nchini.

“Serikali pia imeandaa mwongozo wa uwekezaji  katika taka ngumu ili kuhamasisha  uwekezaji na kuongeza jitihada  za kuboresha usimamizi wa taka hapa nchini”.

Tafiti zinaonesha kwamba nchi inapoteza takribani  asilimia moja ya pato ghafi la taifa(GDP) kutokana na hali duni ya usafi na utafiti uliofanywa na benki ya dunia mwaka 2012 ulionesha kwamba kila mwaka shilingi bilioni 450 zinapotea kutokana na madhara ya uchafu.

#TunaboreshaAfya

SAMPULI 2589 ZAFANYIWA UCHUNGUZI KATIKA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

- Hakuna maoni



Meneja wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya nyanda za juu kusini, Gaspar Gerald akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Maofisa habari wa Wizara na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya katika kampeni ya 'Tunaboresha sekta ya afya".


Baadhi ya Wakemia wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya Nyanda za juu kusini wakionesha namna vifaa vya maabara vinavyofanya kazi na baadhi ya sampuli wanazopata kwa ajili ya kufanyia uchunguzi.

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA) kanda ya nyanda za juu kusini, imekusanya sampuli mbalimbali 2589 na kuzifanyia uchunguzi na kutoka ushahidi mahakamani katika kesi 68.

Aidha, kati ya sampuli hizo 221 zilikuwa za Vinasaba(DNA) ambazo zililenga masuala kibinadamu ya utambuzi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa kanda hiyo, Gaspar Gerald alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walioambatana na Maofisa habari wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya katika kampeni ya 'Tunaboresha sekta ya afya' inayolenga kuangalia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.

Meneja huyo  sampuli hizo 2580 ni za kimazingira,makosa ya jinai,  vinasaba na chakula na dawa ndio zinazopokelewa.

Aidha alisema  kanda hiyo kwa kipindi cha miaka minne wametoa ushahidi kwenye kesi 68 na kwamba sio kila sampuli zinazopimwa zinatolewa ushahidi bali ni zile zinazohitajika kutolewa ushahidi mahakamani.

"Huu ushahidi ni pale mahakama inapohitaji ushahidi ndo tunaenda kutoa na ushahidi tunaotoa ni kile tulichokiona kwenye sampuli iliyoletwa kama vile dawa za kulevya hivyo mkemia anatoa ripoti yake,"alisema

Akizungumzia kuhusu mafanikio mengine, Gerald alisema wamefanikiwa kujenga ofisi yao kwa gharama ya Sh.Milioni 300, kukagua na kudhibiti kemikali, kuongezeka wafanyakazi kutoka watatu hadi 18 na kufanikiwa kupima  sampuli 2580.

"Mwaka 2017 wafanyakazi waliongezeka kwa asilimia 80 na inatokana na juhudi za Rais Magufuli kuhakikisha anatekeleza sera ya serikali ya kufikisha huduma kwa wananchi, kanda hii kijiografia ina mikoa sita lakini kiutawala kwa mujibu wa mkemia wa serikali ni mikoa mitano Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Rukwa,"alisema

Alisema huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa kimaabara, utekelezaji wa sheria za mamlaka ikiwemo ya kemikali za majumbani na viwandani, Vinasaba vya binadamu na sheria ya Mkemia Mkuu.

Alieleza ofisi hiyo imefanikiwa kusimamia kemikali na kudhibiti zinazoingia mipakani kwenye  mpaka wa Tunduma na Kasumulu na kutoa elimu kwa watu zaidi ya 150 wanaojihusisha na kemikali na watu 140 wanaotoka jeshi la polisi kwa ajili ya usimamizi wa sampuli za jinai.

Kadhalika, Gerald alisema udhibiti wa kemikali awali hakuwa mzuri lakini baada ya mamlaka hiyo kuanzishwa udhibiti umekuwa mkubwa na wasafirishaji wamepewa elimu ili kufuata taratibu za kulinda mazingira na afya za watu.

Kuhusu DNA, Meneja huyo alisema vinasaba vinapimwa kwa maana mbili ya utambuzi na masuala ya jamii au ya ndoa.

"Kwenye sheria ya DNA imeanisha mamlaka inayoomba kupimiwa DNA, ile mamlaka ndio zinazoleta maombi kwa mkemia kuomba kupimiwa DNA, hakuna uoga watu wanafuata taratibu, kwenye suala la utambuzi kwa mfano tukio la moto Morogoro pale mkemia aliingia kujua huyu ni nani,"alisema.

Alisema mpaka sasa sampuli 221 za DNA kwa kipindi cha miaka minne na mamlaka zingine zilizowasilisha maombi ya kupimiwa kwa Mkemia ndio zenye majibu ya vinasaba hivyo.

Mwisho.

Jumatatu, 16 Desemba 2019

MAOFISA AFYA WATAKIWA KUWAKINGA WANANCHI DHIDI YA MAGONJWA-DKT. SUBI

Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akieleza jambo mbele ya Maafisa Afya wa Mikoa na Halmashauri, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya usafi wa mazingira.

Afisa kutoka Idara ya Mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee naWatoto Bw. Anyitike Mwakitalima akieleza mafanikio mbali mbali yaliyopatikana kutokana na afua mbali mbali za usafi wa mazingira zinazotekelezwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau.

Maafisa Afya kutoka Mikoa, Halmashauri na Wadau wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi.


MAOFISA AFYA WATAKIWA KUWAKINGA WANANCHI DHIDI YA MAGONJWA-DKT. SUBI

Na Catherine Sungura, WAMJW - Dodoma

Maofisa afya wa mikoa na halmashauri wametakiwa kusimamia afya ya jamii kwenye maeneo yao ili wananchi wajikinge dhidi ya magonjwa yakuambukiza na yele yasiyoambukiza.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa kinga Dkt. Leonard Subi wakati akiongea na maofisa hao ambao wanakutana jijini hapa  kwa  kikao kazi cha siku tatu wakijadili utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa kwanza mwaka jana  na  Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

“Mkutano huu ni wa pili mwaka huu,ni mkutano muhimu kwa maofisa afya kwani ndio wasimamizi wa shughuli za afya katika ngazi za jamii kwa kuhakikisha wananchi wanajikinga na maradhi, kula chakula bora kuishi makazi bora,usafi wa mazingira pamoja na kuwa vyoo bora”.Amesema Dkt. Subi

Aidha, amesema katika mkutano huu mambo mbali mbali yatajadiliwa ikiwemo  afya mazingira,usafi na uchafuzi wa mazingira na kila kinachotumiwa na kumzunguka  mwananchi ,pia wataangalia mabadiliko ya tabia nchi na kupata taarifa kutoka ngazi za mikoa ni jinsi gani walivyotekeleza majukumu yao.

“Maafisa afya muendelee kuishauri wizara kwa kutumia takwimu kwani tunatarajia mkutano huu mtabadilishana uzoefu  kutoka sehemu zenu za kazi,kama wizara tumekua tukitengeneza sera na miongozo mbali mbali ya kudhibiti maradhi yote yanayoweza kuathiri afya za binadamu hivyo kazi ya wizara ni kukusanya taarifa,kuchakata na kuzitolea miongozo na maelekezo”. Aliongeza Dkt. Subi.

Hata hivyo amesema maofisa hao wana majukumu ya kusimamia na  kulinda afya mipakani ili kusiingie magonjwa ya milipuko kutoka nje hususan  nchi za jirani pamoja na utoaji wa chanjo ambapo Tanzania ipo vizuri.

Mkutano huo ambao utafunguliwa kesho na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu umebeba Kauli mbiu isemayo “Huduma bora za afya mazingira na usafi ni kichocheo muhimu cha uchumi endelevu.


Jumamosi, 14 Desemba 2019

KITUO CHA AFYA KOME CHAFANYA UPASUAJI WA KWANZA

Bango la Kituo cha Afya Kome, linalotoa maelekezo ya Huduma zinazotolewa katika kituo hicho.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea na moja kati ya mama aliyefika kupata huduma katika kituo cha Afya Kome, Halmashauri ya Buchosa, Sengerema Mwanza.


KITUO CHA AFYA KOME CHAFANYA UPASUAJI WA KWANZA

Na.Catherine Sungura

Kituo cha afya Kome kilichopo halmashauri ya buchosa wilayani Sengerema kimefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza  wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni na hivyo kumuokoa mama na mtoto wake.

Akiandika kwenye mtandao wa kijamii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa kwa mara ya kwanza kituo hicho kimeweza kufanya upasuaji huo baada ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  kujenga “theatre” na kuweka vifaa tiba kwenye kituo hicho.

Waziri Ummy ameendelea kuandika kuwa chumba hicho cha upasuaji ambacho kipo kituoni hapo kitawasaidia akina mama wajawazito wa kisiwa cha kome watakaopata uzazi pingamizi na hivyo kutokufuata huduma hizo wilayani sengerema na hivyo kutokuvuka tena maji.

“Hakika tumedhamiria kuokoa maisha  ya akina mama wajawazito na watoto wachanga,tutaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha huduma za uzazi  za dharura ikiwemo ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni(CEmONC) zinapatikana katika vituo vyote vya afya vya umma ,mama na mtoto huyo mwenye uzito wa kilo 3 na nusu wanaendelea vizuri”Amesema waziri Ummy

Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya buchosha Dkt. Ernest Chacha amesema walimpokea mama huyo kituoni hapo siku ya ijumaa ambaye alikua akihudhuria kliniki kwenye zahanati moja huko kisiwani hakuweza kujifungua kawaida kwani alikua akikabiliwa na uchungu pingamizi kwani nyonga zake  hazikuwa zinapanuka hivyo ili kumuokoa ilibidi afanyiwe upasuaji kuweza kumuokoa mama pamoja na mtoto .

Dkt. Chacha ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshaji wa vituo vya afya nchini ikiwemo kituo cha afya cha kome ambacho kipo kisiwani kwa kuboresha miundombinu kwa kujengewa chumba cha upasuaji pamoja na kuwekewa vifaa tiba hivyo kusaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na watoto wachanga hususan visiwani humo.

“Wananchi walikua wanapata adha kubwa sana ya kuvuka maji kutoka kisiwani na kufuata huduma kwenye hospitali ya wilaya iliyopo sengerema,tunamshukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa kuiagiza MSD kutufungia taa kwenye chumba cha upasuaji wakati wa ziara yake hivi karibuni visiwani hapa kwani tumeweza kuokoa maisha ya huyu mama muda mfupi baada ya taa hizo kufungwa”Amesema Dkt. chacha

Hivi karibu waziri wa afya alitembelea kisiwa hicho na kuwaahidi  kuwapatia xray mashine ya kidigitali  kwenye kituo hicho cha afya na kuwataka MSD kufunga taa kwenye chumba hicho cha upasuaji mara moja.

Kisiwa cha kome kimeongeza  idadi ya akina mama wanaojifungulia  kwenye vituo vya afya  kwa  asilimia 80  kwa mwaka ambapo wastani akina mama  50 wanajifungulia kwa mwezi

Ijumaa, 13 Desemba 2019

TAASISI BINAFSI ZAOMBWA KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA AFYA KATIKA KUBORESHA HUDUMA NCHINI

- Hakuna maoni


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vitanda vya wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (PICU) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, vitanda hivyo vimetolewa na Benki ya NMB.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB Bw. Juma Kimoli, Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Afya Bi. Deodatha Makani (Mwisho) wakiwa katika hafla ya upokeaji wa Vitanda vitano vya chumba cha watoto wagonjwa mahututi (PICU) katika Hospitali ya Muhimbili vilivyotolewa na NMB.


 Mwakilishi wa Benki ya NMB Bw. Juma Kimoli akikabidhi rasmi vitanda hivyo kwa Waziri Ummy Mwalimu.
Mwakilishi wa NMB Bw. Juma Kimoli (kushoto) akiwa na Waziri Ummy Mwalimu, Kaimu mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Bi. Zuhura Mawona wakimuangalia mmoja wa watoto aliyelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu Muhimbili.

Waziri Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya wazazi walioleta watoto kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili kitengo cha watoto.

Waziri Ummy Mwalimu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa wodi ya watoto wenye kuhitaji uangalizi maalumu (PICU), pamoja na wawakilishi wa Benki ya NMB.

Na Emmanuel Malegi-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameziomba sekta binafsi ikiwamo benki ya NMB kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za Sekta ya Afya nchini.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akipokea msaada wa vitanda vitano kutoka Benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi Milioni 35 kwa ajili ya wodi ya watoto wanaohitaji huduma ya uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na vitanda 10 pamoja na magodoro 10 kwa Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila vyenye thamani ya shilingi milioni 10. 

Amesema sekta binafsi zina wajibu mkubwa katika kuchangia shughuli za maendeleo ikiwamo huduma za afya kama ilivyofanya Benki ya NMB.

“Nawapongeza NMB kwa jitihada zao kwani msaada wa vitanda vya ICU ni msaada mkubwa kwa watoto na pia benki hii inafanya vizuri kurejesha fedha zake kwa jamii ikiwemo na kutoa gawio Serikalini”. Amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesema kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tano, Muhimbili inaendelea kutoa huduma za kibingwa za hali ya juu zikiwemo huduma ya kupandikiza figo pamoja na huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wenye matatizo ya kusikia.

Naye mwakilishi wa Benki ya NMB, Bw. Juma Kimoli ameipongeza Muhimbili na serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha huduma za afya huku akisisitiza kuwa NMB imeweka utaratibu wa kuisaidia sekta ya afya kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali kwa jamii.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Muhimbili, Bi. Zuhura Mawona ameishukuru NMB kwa msaada huo kwa kuwa umekuja wakati ambapo Hospitali hiyo kwa kushirikiana na wahisani imejenga wodi za uangalizi maalumu kwa watoto wenye umri kati ya siku 1 hadi siku 28 (NICU) na wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14 (PICU), hivyo kuwa na uhitaji wa vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vitanda.

 “Vitanda hivi vya kisasa vinatumia umeme na vinaweza kutumika kwa kupandishwa juu na kushushwa  kulingana na uhitaji,  hivyo vinasaidia mgonjwa kulazwa katika mlalo unaofaa na pia kupunguza maumivu ya mgongo kwa wauguzi na madaktari wakati wa kutoa huduma”. Amesema Bi. Zuhura.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa vitanda hivyo pia vimesaidia wauguzi kutoa huduma kwa urahisi na ufanisi zaidi ikiwamo kumwezesha mgonjwa kupumua (Intubation) kwa urahisi.

Kwa niaba ya Hospitali ya Muhimbili, Bi. Zuhura ameishukuru NMB kwa kutoa msaada huu na pia ameiomba kuongeza vitanda vingine kwani mahitaji ya vitanda ni makubwa kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.

WAZIRI UMMY AITAKA BODI MPYA YA WADHAMINI KUSIMAMIA VYEMA TAASISI YA MOI

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wadhamini wa Taasisi ya MOI mapema leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Dkt. Respicious Boniface akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wadhamini iliyozinduliwa rasmi mapema leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa bodi wadhamini wa Taasisi ya MOI Prof. Charles Mkony sheria pamoja mpango mkakati wa Taasisi hiyo kwa ajili utekelezaji.

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya MOI Prof. Charles Mkony akiongea jambo wakati wa uzinduzi wa bodi ya mpya ya wadhamini ya Taasisi hiyo ambayo imezinduliwa rasmi leo na Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na Bodi mpya ya wadhamini wa Taasisi ya MOI aliyoizindua mapema leo.
Na Emmanuel Malegi-DSM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu Leo amezindua bodi mpya ya wadhamini  ya taasisi ya mifupa (MOI ) na kuitaka bodi hiyo kusimamia vizuri utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Taasisi hiyo ili kuiwezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa viwango vya juu.

Waziri Ummy amesema mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa bodi mpya ya MOI ulikua mgumu kwani majina yalikua mengi lakini  lengo ikiwa ni kupata wajumbe makini watakaoisimamia vyema Taasisi hiyo.

“Ndugu Mwenyekiti, Prof. Mkony pamoja na wajumbe, ni ukweli kwamba wajumbe wa bodi hii wamechelewa kupatikana kutokana na mchujo uliokua unafanyika miongoni mwa majina yaliyokua yamependekezwa, nitumie fursa hii kuwapongeza mliokidhi vigezo na ni matarajio yangu mtaisimamia vyema Taasisi hii ambayo ni tegemeo kubwa hapa nchini”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imefanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi ya MOI jambo ambalo limepelekea huduma za afya kuimarika na kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

“Uboreshwaji wa miundombinu umepelekea kuongezekaa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji hapa MOI, mwaka 2015 idadi ya wagonjwa waliokua wanafanyiwa upasuaji hapa MOI kwa mwezi ilikua kati ya 400 mpaka 500 lakini sasa hivi imeongezeka na kufikia 700 mpaka 900 kwa mwezi.” Waziri Ummy.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali  ya awamu ya Tano katika Taasisi ya MOI, huduma nyingi mpya zimeanzishwa na katika kipindi cha miaka 4 Taasisi imewafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 43,200.

“Mh. Waziri katika kipindi cha Miaka 4 ya Serikali ya awamu ya Tano, kupitia usimamizi wa Wizara yako tumeweza kuanzisha huduma za upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu, upasuaji wa kunyoosha vibiongo kwa watoto, upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo, upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia puani, upasuaji wa mgongo kwa kufungua eneo dogo, hii ni hatua kubwa sana kwetu.” Amesema Dkt. Boniface.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti mpya wa Bodi mpya ya Wadhamini MOI Prof. Charles Mkony ameshukuru kwa kupewa dhamana ya kusimamia Taasisi hiyo muhimu  na kuahidi kendelea kuisimamia MOI ili iendelee kutoa huduma bora na za viwango vya juu kwa wananchi.

-MWISHO-

Alhamisi, 12 Desemba 2019

SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao cha kuzindua Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akiteta  jambo na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure  Prof. Abel Makubi wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akikata  utepe ikiwa kama ishara ya uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Kulia kwake ni Mwenyekiti mpya wa Bodi Prof. Abel Makubi, kushoto kwake ni Kaimu RMO Mkoa Mwanza Dkt. Silas Wambura.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure wakiwa wamebeba kitabu cha mwongozo wa Bodi ya ushauri,  wakati wa kikao cha kuzindua Bodi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akimkabidhi mwongozo mmoja kati  ya wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, katikati ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Silas Wambura.

Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.

Baadhi ya Watumishi wa Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure na Wajumbe wa Bodi ya zamani  ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, waliofika kushuhudia uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali hiyo, uliofanywa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu katika ukumbi wa RMO Mkoa wa Mwanza.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya Mhe.@umwalimu, akiwa na wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo.


SERIKALI YAAGIZA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUANZISHA MFUKO WA FEDHA ZA DAWA.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- MWANZA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza Waganga Wakuu wa Vituo vya Afya na Hospitali zote nchini kuanzisha mfuko wa fedha za Dawa kupitia makusanyo ya fedha za ndani, ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa dawa nchini endapo itatokea.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu katika kikao cha uzinduzi wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza.

"Kuanzia Vituo vya Afya, Hospitali zote za Halmashauri, za Mikoa , kuanzisha mfuko wa fedha za dawa, na vyanzo vikuu vya mifuko hii ni mapato yatokanayo na mauzo ya dawa, huduma za Maabara, huduma za mionzi" alisema Waziri @umwalimu.

Amesema, Bodi hiyo ya ushauri lengo lake kubwa ni kuhakikisha inaboresha huduma za kinga na tiba katika Hospitali, huku ikihakikisha huduma hizo zinaifikia wananchi kwa ubora na gharama nafua.

Aliendelea kusema, Sera ya Afya nchini inawataka Wananchi kuchangia huduma kwa gharama nafuu isipokuwa kwa makundi yote ya msamaha, wakiwemo Wazee, Watoto walio chini ya miaka mitano na mama wajawazito, hivyo kuwataka kuweka mifumo mizuri ili kurahisisha utoaji huduma.

Mbali na hayo, Waziri Ummy ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaboresha huduma za dharura na ajali, ili kuokoa vifo vitokanavyo weza kuepukika kupitia huduma za dharura, keisha kuwashauri kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ili kuboresha huduma kwa wananchi.

"Watu wengi wanakufa wakiwa getini Mwa Hospitali, wakati utaalamu upo, kwamba mkiboresha huduma za dharura na ajari, tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi " alisema Waziri @umwalimu.

Aidha, Waziri Ummy ameeleza majukumu ya Bodi hiyo ni kushauri, kutengeneza, kusimamia na kupitisha miongozo, malengo na mipango mikakati ya Hospitali kulingana na Sera na miongozo ya Serikali.

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou-Toure Dkt. Dkt. Graham Mtui ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa kuleta mashine ya uchunguzi wa figo na ini, mashine ya kusafisha figo ambazo zinatarajia kuanza kutoa huduma Januari 2020.

Kwa upande mwingine amesema, Hospitali inatarajia kupokea mashine sita ikiwemo CT Scan, X- ray yakidigitali, vifaa vya mifupa na mashine zinazosaidia kupumulia kutoka MSD.

Hata hivyo, amesema kuwa, idadi ya Wagonjwa wanaofika kupata huduma, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku kwa mwaka 2015 hadi kufikia wagonjwa kati ya 500 mpaka 700 kwa Mwaka huu 2019, huku akiweka wazi kupunguza Rufaa za kwenda Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando kwa asilimia 50.

"Kutokana na mafanikio hayo, idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali imeongezeka, kutoka wastani wa wagonjwa 350 kwa siku ambayo ilikuwa mwaka 2015, na kufikia wastani wa wagonjwa kati ya 500 hadi 700 kwa mwaka huu 2019", alisema Dkt. Graham Mtui.

Mwisho.