Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 12 Juni 2020

DKT. MOLLEL ATETA NA MADEREVA WA MALORI, NAMANGA

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiongea na madereva malori mpaka wa Tanzania na Kenya Namanga Jijini Arusha, lengo kuwasikiliza changamoto zao.





Baadhi ya madereva wa malori waliokwama katika mpaka wa Tanzania na Kenya Namanga Jijini Arusha wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel.




DKT. MOLLEL ATETA NA MADEREVA WA MALORI, NAMANGA 

Na WAMJW- Arusha. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amefanya ziara katika mpaka wa Tanzania na Kenya Namanga Jijini Arusha na kuzungumza na madereva wa malori yanayokwenda Kenya ili kusikiliza changamoto zinazowakumba. 

Dkt. Mollel amefanya ziara hiyo leo, ikiwa ni sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakumba madereva hao, katika kipindi hiki ambacho Dunia imekumbwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona. 


Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali imeliona tatizo hilo na kuweka wazi kuwa itaongeza kasi katika kuhakikisha inapata suluhu ya changamoto wanazokumbana nazo madereva hao katika eneo la mpaka wa Namanga. 

"Nimekuja kuwaambia poleni, lakini Serikali yetu itaenda kwa kasi ya ajabu kuhakikisha kwamba hili tatizo lenu katika mpaka huu linatatuliwa " alisema. 

Aidha, Dkt. Mollel amewataka madereva hao kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho, Serikali inatafuta utatuzi wa changamoto yao, huku akiwapa salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli na kusema anawapenda sana.

Mbali na hayo Dkt. Mollel alisema kuwa changamoto hii iliyojitokeza katika mpaka wa Namanga ni suala mtambuka ambalo linahusisha Wizara zaidi ya moja, huku akiweka wazi kuwa suala hili lina uhusiano wa kibiashara na uchumi baina ya nchi hizo.

Nae, dereva wa malori yanayokwenda nchini Kenya Bw. Abdullah Hassan amesema kuwa, kama madereva hawakubaliani na majibu ya vipimo wanavyopewa kutoka Kenya kutokana na vipimo hivyo kuonesha idadi kubwa ya madereva kuwa na ugonjwa wa Corona jambo ambalo sio kweli.

"Tunaishi maisha magumu sana kutokana na hali iliyojitokeza, na kunachosikitisha zaidi, sisi hatukubaliani na vipimo ambavyo tunapimwa upande wa pili. 

Kwa upande wake, Japhet Jeremiah alisema kuwa, wamekuwa wakiombwa kiasi cha shilingi 2000 za Kenya ili kuandikiwa kuwa hawana Corona, hali aliyeweka wazi kuwa ni uonevu kwa madereva kutoka Tanzania. 

"Sisi kero yetu, tumekuwa tukipima Kenya tumeambiwa tuna Corona, na mimi wiki mbili nilipima nikapewa cheti nina Corona lakini ukweli ni kwamba sina Corona na sijawai tumia dawa yoyote mpaka sasahivi" alisema 

Mwisho.

Alhamisi, 11 Juni 2020

WAZIRI UMMY AZINDUA BARAZA JIPYA LA MADAKTARI TANGANYIKA

- Hakuna maoni








Na WAJMW-DODOMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu jana amezindua Baraza jipya la Madaktari Tanganyika katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa LAPF jijini Dodoma.

Katika uzinduzi huo Waziri Ummy amelipongeza Baraza jipya linaloongozwa na Mwenyekiti  Prof. David Ngassapa na wajumbe wake wanane walioteuliwa lakini pia hakusita kulishukuru na kutaja baadhi ya mafanikio ya baraza lililopita ambalo lilikua linaongozwa na Prof. Muhammad Kambi ambaye alikua Mwenyekiti.

“Katika kipindi chao cha uongozi, Baraza limepata mafanikio mengi ikiwemo Sheria za Madaktari, Madaktari wa meno wa wataalamu wa Afya shirikishi ya Mwaka 2017, na kuitengenezea kanuni zake tano ambazo ni ya Watarajali, Usajili wa mitihani, Ada na Tozo, pamoja na Uchunguzi wa mashauri ya mafunzo endelevu”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema mabadiliko hayo yameboresha sana muundo wa Baraza na hivyo usimamizi wa taaaluma ya udaktari na udaktari wa meno umeongeza wigo wa usimamizi wa taaluma kwa kuongeza kada za Afya shirikishi ambazo mwanzo zilikua hazina usimamizi.

Waziri Ummy amesema majukumu ya Baraza hilo ni pamoja na kuwatambua wanataaluma inaowasimamia kwa njia ya kuwasajili na kuwapa leseni zinazowaruhusu kufanya kazi hizo na kuwakagua mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa wako hai kitaaluma.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo ofisi ya Msajili wa Baraza la Madaktari inaonyesha kuwa jumla ya madaktari wa kada mbalimbali 13,973 wamesajiliwa nchi nzima, hata hivyo madaktari walipo kwenye ajira ni 5568.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy amelitaka Baraza jipya chini Mwenyekiti Prof. David Ngassapa kuhakikisha kuwa: Wananchi wanahudumiwa na wanataaluma kwa namna ambayo ni salama, Kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya mgonjwa na Daktari yanakuwa ya kuaminiana, Wanataaluma wanapata mafunzo na elimu ya kujiendeleza (CPD) ili waendane sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani pamoja na Baraza kuhakikisha lina kumbukumbu na taarifa sahihi za wanataaluma linaowasajili na ambazo zinaweza kupatikana kirahisi ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi ya wanataaluma wanaoruhusiwa kutoa huduma.

Mwisho, Waziri Ummy amelitaka Baraza hilo kuwa na wajibu wa kutangaza majina ya wanataaluma wenye usajili halali na unaoendana na wakati.

MWISHO

Jumanne, 9 Juni 2020

UGONJWA WA CORONA UNAELEKEA KUISHA NCHINI-WAZIRI UMMY

- Hakuna maoni








Na WAJMW-DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa Corona unaelekea kuisha nchini ambapo mikoa zaidi ya 15 haijaripoti mgonjwa yeyote wa Corona kwa zaidi ya wiki.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati alipotembelea kituo cha afya cha Mkonze kilichotengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona jijini Dodoma na kukuta vitanda vikiwa tupu bila kuwa na mgonjwa yeyote kwa zaidi ya wiki.

Waziri Ummy amesema kupitia Waganga wakuu wa Mikoa 15 nchini wamethibitisha kutokua na mgonjwa wa Corona na Mikoa mingine yenye wagonjwa imeripoti kuwa wagonjwa hao wanaendelea vizuri.

Aidha, Waziri Ummy amewashukuru watoa huduma za afya wa kituo cha Mkonze kwa kazi nzuri walioifanya ya kuwahudumia wagonjwa na kuchukua tahadhari zilizosaidia wahudumu hao kutopata maambukizi ya Corona.

Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema licha ya ugonjwa wa Corona kuelekea kumalizika nchini, amewataka wananchi kutobweteka na kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kuvaa barakoa za vitambaa wanapokua kwenye mikusanyiko.

Ijumaa, 5 Juni 2020

EWURA NA MOUNT MERU ZATOA MSAADA KWA AJILI YA UDHIBITI WA CORONA NCHINI

- Hakuna maoni




Na Emmanuel Malegi-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo amepokea msaada wa hundi ya kiasi cha Tsh. Milioni 100 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)uliokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi Bw. Godfrey Chibulunje akiwa na Meneja Mawasiliano na uhusiano wa mamlaka hiyo Bw. Titus Kaguo.

Aidha, Waziri Ummy amepokea msaada wa ndoo 480 sawa na Lita 9600 za vitakasa mikono (Hand Sanitizer) zenye thamani ya Tsh. Milioni 11 zilizotolewa na kampuni ya Mafuta ya Mount Meru ambazo zitatumika katika kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini. Vitakasa mikono hivyo vimekabidhiwa na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Prabhat Yadau.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Ummy kwa niaba ya Waziri Mkuu ameshukuru kupata misaada hiyo ambayo itasaidia katika kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini na pia amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari licha ya maambukizi ya ugonjwa huo kupungua nchini.

Alhamisi, 4 Juni 2020

UVUTAJI WA TUMBAKU UNA ATHARI UCHUMI WA MTU MMOJA MMOJA ANAYETUMIA

- Hakuna maoni






Na Emmanuel Malegi-Dodoma

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania kama nchi nyingine za Kiafrika wavutaji wa tumbaku wako hatarini kuyumba kiuchumi na kupata magonjwa yasiyoambukizwa kama tahadhari hazitachukuliwa mapema.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa matumizi ya tumbaku kwa watu wazima wa mwaka 2018 nchini uliofanyika mapema leo katika Ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema utafiti huo umeonesha kuwa kwa wastani matumizi ya tumbaku kwa mtu mmoja kwa mwezi inagharimu Shilingi za Kitanzania 28,840/= fedha ambayo ingetosha kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa asilimia 58 na umaskini wa kupindukia (mahitaji ya chakula) kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa asilimia 85.

Kwa kutumia taarifa za Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa Mwaka 2017-18, fedha za kujikimu kwa ajili ya mahitaji ya msingi kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Shilingi za Kitanzania 49,320/= na mahitaji ya chakula kwa mwezi kwa mtu mmoja ni Shilingi za Kitanzania 33,748/=”. Amesema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa utafiti huo, Matokeo yameonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10 (8.7%), wenye umri wa miaka 15 au zaidi nchini Tanzania wanatumia tumbaku ya aina yeyote na hivyo kuwa na watu milioni 2.6 kati ya watu zaidi ya  milioni 55. Wanaume ni asilimia 14.6 na wanawake ni asilimia 3.2.

Aidha, Waziri Ummy amesema watu 4 kati ya 10 (40.3%) nchini wamewahi kuona onyo la matumizi ya tumbaku kupitia redio au runinga. Pia matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, watu 9 kati ya 10 (92.3%) wenye umri wa miaka 15 au zaidi wanaamini uvutaji wa sigara husababisha magonjwa, wakati watu 8 kati ya 10 (84.4%) wanaamini kuvuta hewa ya mtu anaevuta sigara kunaweza kuwasababishia magonjwa hata kama wao hawavuti sigara.

katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.  Taarifa inaonesha kuwa watu 4 kati ya 10 (32.9%) wameathiriwa na moshi wa tumbaku sehemu za kazi ikiongozwa na sehemu za mabaa na kumbi za starehe kwa asilimia 77 (watu milioni 3), maeneo ya huduma za biashara za vyakula asilimia 31.1(watu milioni 3.5) na majumbani asilimia 13.8 (watu milioni 4.1).

Waziri Ummy amesema utafiti huo una umuhimu wa kipekee katika Wizara, kwani matokeo yake yatasaidia katika kutathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na magonjwa makuu manne yasiyoambukiza ambayo ni Saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mfumo wa hewa na kisukari.

katika kuhakikisha elimu dhidi ya athari ya tumbaku inaifikia jamii ipasavyo. Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa  Watendaji wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wadau wengine, kutengeneza au kupitia upya Sheria ya kudhibiti matumizi ya Tumbaku ili iendane na Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya Tumbaku na kuendelea kutoa Elimu kwa jamii kuhusu madhara yake; Wizara ya Elimu kuendelea kuimarisha juhudi za kuwakinga wanafunzi dhidi ya tumbaku na bidhaa zake; Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha wale wanaokiuka miongozo kama vile kuendelea kuvuta sigara kwenye maeneo ya wazi wanachukuliwa hatua stahiki; Watengenezaji na wauzaji wa sigara, kufuata miongozo iliyowekwa na Serikali ikiwemo kutokuweka mabango au kutangaza na kuhamasisha matumizi ya sigara, kupitia bidhaa kama miamvuli, T-Shirts, kofia, na kutowauzia watoto wenye umri chini ya miaka 18; jamii kuacha kutumia tumbaku na bidhaa zake na Taasisi za Utafiti kufanya Tafiti za kuangalia vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku ilikuwe na takwimu za nchi na siyo kutegemea za kutoka nje.

*MWISHO*








Jumapili, 31 Mei 2020

TANZANIA IPO TAYARI KUPOKEA WATALII - DKT. KIGWANGALLA

- Hakuna maoni
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel pindi walipofanya ziara ya kukagua utayari katika uwanja wa KIA.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akieleza jambo katika sehemu ya kukagua mizigo pindi aliooongozana na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla katika uwanja wa ndege wa KIA.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel pindi walipofanya ziara ya kukagua utayari katika uwanja wa KIA.

Magari manne yakubeba wagonjwa yaliyotolewa na yametolewa na wakala wa huduma za utalii kama sehemu ya tahadhari katika kuhakikisha usalama wa Watalii wataoingia nchini kwaajili ya utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakisikiliza jambo kutoka  kwa Mtaalamu kutoka wakala wa huduma  za utalii nchini wakati wa makabidhiano wa magari hayo manne.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakikagua maendeleo ya utengenezaji wa gari linalotumia umeme.


TANZANIA IPO TAYARI KUPOKEA WATALII - DKT. KIGWANGALLA

Na WAMJW- Kilimanjaro

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ameweka wazi kuwa, Tanzania ipo tayari kupokea wageni kutoka sehemu yoyote Dunia kwa ajili ya utalii, kufuatia kuimarisha mifumo ya tahadhari zote za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo leo katika ziara iliyomjumuisha Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ikiwa na lengo la kukagua utayari wa nchi katika kudhibiti ugonjwa wa Corona katika uwanja wa ndege wa KIA na kupokea magari manne ya kubeba wagonjwa endapo watatokea pindi wawapo nchini kwenye utalii.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kuweka miongozo wakati wa kuingia na kutoka uwanja wa ndege, muongozo wa namna ya kusafirisha watalii pamoja na muongozo wa namna ya kuandaa chumba cha wageni

"Katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona Duniani, tumeweka miongozo kwa pale uwanja wa ndege, tumeweka muongozo wakati wa kuingia na kutoka tumeweka muongozo namna ya kusafisha Watalii kutoka uwanja wa ndege mpaka hotelini, tumeweka muongozo namna ya kuandaa chumba cha mgeni, namna ya kuandaa chakula, kila kitu tumeweka muongozo " alisema

Aliendelea kusema kuwa, Serikali imechagua baadhi ya vituo vya Afya mahususi kwa ajili ya watalii Mkoani Arusha, Serengeti na Ngorongoro lengo ni kuthibitisha usalama wa afya ya Watalii waingiapo nchini.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, Serikali imepokea magari manne ya kubeba wagonjwa(ambulance) yaliyokidhi miongozo ambayo yametolewa na wakala wa huduma za utalii nchini ikiwa ni sehemu ya tahadhari katika kuhakikisha usalama wa Watalii wataoingia nchini.

"Tumeona magari ambayo yamezingatia zile taratibu  na miongozo yote ambayo inatakiwa kuhakikisha Watalii wetu wapo salama na endapo kutakuwa na tatizo litaweza fanyiwa utatuzi mara moja " alisema Dkt. Mollel.

Aidha, alisema kuwa, katika kuboresha tahadhari zaidi magari yaliyotolewa yanalenga kuwakinga madereva na Watalii kwa kutenganishwa kwa kioo ili kudhibiti mnyororo wa maambukizi ya virusi vya Corona endapo atatokea.

"Magari yenyewe yatakuwa Dereva anaingia ndani, lakini kunakuwa na kinga inayowatenganisha Watalii na madereva wetu jambo litalosaidia kudhibiti maambukizi endapo yatatokea " alisema.

Mwisho.

Jumamosi, 30 Mei 2020

HONGERENI WATUMISHI WOTE WA AFYA KWA JINSI MLIVYO PAMBANA KATIKA JANGA LA CORONA.

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akisisitiza jambo wakati akiongea na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (hawapo kwenye picha).

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiteta jambo na Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe akiteta jambo na Mkururugenzi msaidizi anaesimamia hospitali za Rufaa Dkt. Caroline, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Baadhi ya Watumishi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakifuatilia neno kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel pindi alipofanya ziara katika Hospitali hiyo. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mtoto aliefika na mzazi wake kupata matibabu katika wodi ya watoto, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiwa na baadhi ya Watumishi kutoka Wizara ya Afya, katika chumba cha Watoto njiti, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akimjulia hali mama aliyempeleka mtoto kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. 

 Picha ya pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akiwa na viongozi kutoka Wizara ya Afya na Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma pindi alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi hao.

Jengo la Idara ya magonjwa ya wanawake na uzazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.



HONGERENI WATUMISHI WOTE WA AFYA KWA JINSI MLIVYO PAMBANA KATIKA JANGA LA CORONA.

Na WAMJW- DOM

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amewashukuru Watumishi wote wa Sekta ya Afya nchini kwa namna walivyojitoa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Dkt. Mollel ameyasema hayo leo, wakati alipofanya ziara ya kuongea na Watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

"Jinsi ambavyo nyie mmepambana dhidi ya virusi vya Corona na bado mkamuunga mkono Mhe. Rais na ushauri alioutoa yeye na Wataalamu wengine wa Wizara kupitia Waziri wa Afya, nyie mmekuwa mashujaa na jeshi la uzalendo wa hali ya juu, nawashukuru sana" alisema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel aliendelea kwa kukemea tabia za wanasiasa wachache kupotosha Watanzania na Dunia kwa ujumla juu ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona kwa Watumishi wa Sekta ya Afya nchini jambo ambalo sio kweli.

"Kuna wanasiasa wanapiga kelele kuhusu Corona kuliko sisi, nawaomba watu tuache kupiga siasa, sisi watumishi wa afya ndio watu wakwanza kukutana na wagonjwa wa Corona laikini leo watumishi mpo 504 je niambieni kuna yoyote amelazwa, watumishi walijibu hapana, kama kweli kuna Watumishi wanakufa basi nyie mngekuwa wa kwanza kuugua na kupoteza maisha" alisema.

Aidha, Dkt Mollel alitoa wito kwa Watumishi wa Sekta ya Afya nchini kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi ili kutoa huduma bora, huku akiweka wazi kuwa kazi ya kuwahudumia wananchi ni ya wito na ya uzalendo.

Pia, Mhe Mollel alielezea kuwa Rais alikuwa na maono ya kusitisha matibabu ya nje ya nchi kwa kuboresha huduma za kibingwa nchi na hii imejizihirisha baada ya dunia kupata janga la corona nchi yetu imeendelea kutoa huduma za kibingwa pasipo kutegemea matibabu ya nje kwa wananchi ambao walikuwa na sifa za kutibiwa nje .

Nae Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest ameweka wazi kuwa Hospitali hiyo imeendelea kutoa huduma za Afya bila kutetereka na kutoa elimu kwa umma licha ya kupitia katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona ulioikumba nchi.

"Tumeendelea kutoa huduma bora kwa wananchi bila kutetereka hata katika wakati huu wa janga la mlipuko wa maambukizi ya virusi vya Corona ulioikumba nchi, Watumishi wetu wamesimama imara huku wakiendelea kutoa elimu ya kujikinga dhidi ya Corona "alisema.