"vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati, ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki” amesema Prof. Makubi.
Ijumaa, 4 Desemba 2020

"VIFO VYA MAMA WAJAWAZITO HAVIVUMILIKI TENA" – MGANGA MKUU WA SERIKALI
"vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati, ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki” amesema Prof. Makubi.
Alhamisi, 3 Desemba 2020

MABARAZA YA KITAALUMA YAPEWA SIKU 14 KWENDA MKOA WA MWANZA KUZUNGUMZA NA WATUMISHI
NA Englibert Kayombo WAMJW - Mwanza
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa muda wa siku 14 kwa baraza la madaktari pamoja na baraza la wauguzi kwenda Mkoa wa Mwanza kuzungumza na watumishi wa kada wanazosimamia ili kurekebisha na kuwajengea uelewa zaidi wa maadili ya taaluma zao.
Prof. Makubi ametoa agizo hilo akiwa Wilayani Kwimba alipokuwa ziara ya kikazi kukagua hali ya utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa kada ya afya.
“Mabaraza mengi yamekuwa yanabaki huko makao makuu kuhukumu watu, wamejiondoa kabisa kwenye kazi ya kuwajenga watumishi, badala ya kupita huku na kuwaelekeza watumishi, wao wanasubiri kupokea malalamiko” amesema Prof. Makubi
Amesema ni lazima mabaraza yahakikishe watumishi hawafanyi makosa kwa kuwaweka katika maadili mema bila kufanya hivyo tutakuwa na watumishi wasio na sifa.
Prof. Makubi amesisitiza kuwa mabaraza yote 10 yanatakiwa kutelekeza majukumu yao ipasavyo na yote wajiwekee utaratibu wa kuzunguka na kuzungumza na watumishi kuanzia ngazi ya Mikoa hadi Wilayani
Mwisho.
Jumatano, 2 Desemba 2020

WATUMISHI KADA YA AFYA WAASWA KUDHIBITI VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NA WATOTO WACHANGA.
Na Englibert Kayombo, WAMJW - MWANZA
Watumishi wa kada ya afya nchini wameaswa kuhakikisha wanadhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kuwajibika ipasavyo wakiwa kazini na kuepukana na tabia za uzembe.
Kauli hiyo imetolewa na na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapologwe alipokuwa akizungumza na timu ya afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa mkoa huo.
“Suala la vifo, pasipokuwepo na uwajibikaji na umoja ni vigumu sana kuweza kulifanikisha, kuchukua hatua imekuwa changamoto kwa timu nyingi hivyo kupelea kuongezeka kwa vifo” amesema Dkt. Ntuli.
Ameendelea kusema kuwa wataalam wa afya hawatakiwi kuoneana aibu endapo mjumbe wa timu hatofanya kazi yake ipasavyo kwa uzembe wake mwenyewe achukuliwe hatua za kinidhamu ili kuweza kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.
Amesema kuwa wataalam wa afya wanapaswa kuwa wamoja na kushirikiana kikamilifu wakiwa kazini na kuacha kusubiri wataalam kutoka ngazi ya juu kuja kutoa maamuzi ya vitu ambavyo vingewezwa kufanywa na viongozi katika eneo husika.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel Tutuba amesema vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vimekuwa viongezeka mkoani humo na kuwataka watumishi wa kada ya afya kuhakikisha wanapunguza kiwango cha vifo hivyo kwa mkoa huo ambao ni kinara wa huduma bora za afya katika Kanda ya Ziwa.
Akitaja takwimu za vifo hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Tutuba amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 vifo vilikuwa 145, mwaka 2016 vifo 151, mwaka 2017 vifo 193, mwaka 2018 vifo 151, mwaka 2019 vifo 171 na kwa mwaka huu mpaka kufikia mwezi Septemba vimetokea vifo 142.
“Lazima tukae tutafakari, licha ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya lakini vifo vinaongezeka, tunapokutana hivi tusiishie tuu kupashiana, ni lazima tutimize wajibu wetu” amesisitiza Bw. Tutuba.
Hata hivyo Bw. Tutuba amepongeza watumishi wa kada ya afya mkoani humo kwa juhudi zao wanazofanya kuhakikisha wanaokoa maisha ya watanzania pamoja na raia wa kigeni wanaokuja mkoani humo kwa ajili ya huduma za matibabu.
“Tumejitahidi kufanya mazuri mengi, lakini badi hatujatekeleza kwa asilimia 100, tumefanya vizuri lakini bado tungeweza kufanya vizuri zaidi endapo kila mmoja angetimiza wajibu wake” amesema Bw. Tutuba.
Mwisho
Jumanne, 1 Desemba 2020
WANAOFANYA MAPENZI NA WASICHANA WENYE UMRI MDOGO WAONYWA
Ijumaa, 27 Novemba 2020

HAKIKISHENI UKOMA UNATOKOMEA NCHINI TANZANIA.
Jumatano, 25 Novemba 2020
PROF. MCHEMBE AWAAGIZA WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA KUFIKIRIA HUDUMA BORA NA NAFUU KWA WANANCHI
Jumanne, 24 Novemba 2020
KUELEKEA MPANGO MKAKATI WA TANO WA SEKTA YA AFYA, SERIKALI YAJIDHATITI KUSOGEZA ZAIDI HUDUMA KWA WANANCHI.
Jumatatu, 23 Novemba 2020
MGANGA MKUU WA SERIKALI “TUMEONGEZA UWEZO WA KUGUNDUA WAGONJWA WAPYA WA KIFUA KIKUU”
Na Englibert Kayombo WAMJW - Dodoma
Serikali ya Tanzania imeazimia
kutokomeza kabisa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuongeza uwezo wa ugunduzi wa
wagonjwa wapya wa kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu
wa Serikali Prof. Abel Makubi alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Mpango wa
Taifa wa Kifua Kikuu an Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.
“Uwezo wa nchi kugundua wagonjwa
wapya na kuwaweka kwenye matibabu umeongezeka kutoka wagonjwa 62,908 (33%) mwaka
2015 na kwa sasa kufikia wagonjwa 82,166 (59%)” amesema Prof. Makubi
Kufuatia hatua hiyo Prof. Makubi
amesema kuwa maisha ya wananchi takribani 300,000 ikiwemo ya watoto 45,000 yameponywa
kwa kupatiwa dawa kwa wakati na kufuatiliwa kwa usahihi kuanzia mwaka 2015 hadi
sasa.
Juhudi hizo pia zimeweka kupunguza
idadi ya vifo vinavyosababishwa na kifua kikuu kwa 33%. “Mwaka 2015 kulikuwa na
vifo 30,000 hivi sasa vimepungua hadi kufikia vifo 20,000” amesema Prof.
Makubi.
Prof. Makubi amesema kuwa mafanikio
hayo ya ongezeko la kasi ya ugunduzi wa wagonjwa wapya yametokana na mikakati
mbalimbali iliyowekwa na Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu
na Ukoma ikiwemo kuboresha huduma za ugunduzi wa TB na kutoa kipaumbele kwa
makundi yaliyoathirika zaidi kama vile kaya zenye wagonjwa, wanaoishi kwenye
kaya duni, gerezani, wachimbaji wadogo wadogo na kwa waathirika wa madawa ya
kulevya.
“Aidha tumewekeza katika afua bunifu
mbalimbali za matumizi ya teknolojia mpya za molekyula za kubaini TB kwa
usahihi na kwa haraka” amesisitiza Prof. Makubi.
Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Huduma
za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema Wizara imefanya vizuri
kwenye kwa kufikia malengo waliyoyaweka kwenye Mpango mkakati ambao unamalizika
mwaka huu 2020.
“Malengo ambayo tulijiwekea ya
kupunguza vifo vitokanavyo na kifua kikuu tumeweza kuyafikia pamoja na
kupunguza madhaa yanayotokana na ugonjwa huo” amesema Dkt. Subi
Amesema kuwa Serikali imefanikiwa
kuongeza vituo vya upimaji wa kifua kikuu sugu kutoka kituo 1 mwaka 2015 hadi
kufika vituo 145 hivyo kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya ugonjwa huo
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi
wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa
Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana Wizara ya Afya
katika kipindi cha miaka 5 ijayo imejiwekea mikakati ya kuwawezesha watumishi
katika vituo vya kutolea huduma za afya ili wawe na ujuzi na uwezo wa kutambua
na kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu.
Jumamosi, 17 Oktoba 2020

WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUNZA TAARIFA ZA UTENDAJI WAO WA KAZI KILA SIKU
Na WAMJW – Dar Es Salaam
Wauguzi na wakunga nchini wamekumbushwa kuhakikisha wanatunza vizuri taarifa za kazi kwenye
majarada ya kazini kwa kuandika yale yote ambayo wanafanya tangu wanapoingia kazini hadi kutoka.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga katika
Hosptali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala – Dar Es Salaam.
“Kila unachofanya kazini aidha umemhudumia mgonjwa au ukiwa na majukumu mengine hakikisheni
mnatunza taarifa za kazi kwa kuandika kwenye majadara yenu ya kazi” amesema Bi. Ziada
Bi. Ziada amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia pia madaktari, wauguzi na wakunga wengine
wanaoingia zamu tofauti kutambua kwa haraka nini ambacho kimefanyika na kuweza kuendelea na kazi
ambayo wengine wameacha.
Amesema kuwa wauguzi na wakunga wamekuwa wakilaumiwa kwa kutotunza vizuri taarifa za utendaji
kazi jambo ambali hupelekea changamtoto kwa wagonjwa kutopata huduma sahihi wakiwa hospitalini.
“Tumekuwa tukilaumiwa hatutunzi kumbukumbu zetu vizuri, andikeni kila mnachofanya, kama umemwita
daktari saa 1, hadi saa 3 hajafika andikeni, tufanye ‘documentation’ kadiri inavyowezekana” amesisitiza
Bi. Ziada.
Hata hivyo Bi. Ziada Sellah hakusita kuwakumbusha wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa malengo ili
waweze kujipima ufanisi wa kazi zao na kujua eneo wanapofanya vizuri na kwenye changamoto.
“Tufanye kazi kwa malengo ili mwisho wa siku tuweze kujipima kwa kufanya tathimini ya malengo
tuliyojiwekea kubaini kama tumeweza kuyatimiza” amesema Bi. Ziada.
Amesema kuwa malengo yanaweza kuwa ya siku moja hadi mwaka mmoja kulingana shabaha
ulizojiwekea muuguzi au mkunga na yatawaongoza kujua ni wapi walikwama na wapi walifanikiwa.
Mwisho
Ijumaa, 16 Oktoba 2020

WANANCHI WAKUMBUSHWA KUCHUKUA TAHADHARI KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO
Watanzania wamekumbushwa kuzingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Prof. Abel Makubi Mganga Mkuu wa Serikali , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Wizara jijini Dodoma.
“Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema” Alisema Prof. Makubi.
Prof. Makubi amesema kufuatia kujitokeza kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka hali hiyo ina hatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.
Aidha, Mganga Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuzingatia kanuniz za afya kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa au kutatibu kwa dawa maalumu na kuhakikisha maji ya kunywa nay ale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi.
“Tunawapongeza wananchi na ninyi wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwa sababu wananchi wamekuwa wasikivu na kutii masharti ya usafi na jinsi ya kujikinga,ni zaidi ya mwaka na nusu sasa Tanzania tumeweza kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini”.
Aidha, amesema jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama na ushirikiano mzuri wa wananchi na hivyo kusababisha baadhi ya magonjwa yanayotokana na uchafu yamepungua.
Hata hivyo Prof. Makubi amesisitiza kutumia ipasavyo vyoo na hasa kipindi hiki cha mvua kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa,kabla ya kula kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.
“Tuongeze usimamizi wa usafi wa nyumba na hasa usafi wa mikono wananchi wamekua wakihamasika usafi wa mikono katika vipindi mbalimbali,hivyo tungeomba kasi ya kunawa mikono iwe endelevu katika mikusanyiko, mashule, madukani, hospitalini,vituo vya mabasi,na taasisi pamoja na masoko,sehemu za kunawia mikono iwe ndelevu kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafi wa kunawa mikono wa hali ya juu.
Pia,aliwata Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaelekezwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikaili za mitaa, Wananchi na wadau mbali mbali ili kuhakisha kila eneo lilio chini yao, haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko kwa kutotapisha vyoo au vyovyote vinavyotoka kwenye vyoo kwenda kwenye mazingira ya wananchi.
Kwa upande wa kujikinga dhidi ya kuumwa na Mbu Prof. Makubi aliwataka wananchi kutumia ipasavyo vyandarua kabla ya kwenda kulala au wenye uwezo wa kununua dawa za kujipaka wapake ili ziwasaidie.
Prof. Makubi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini na shime kuimarisha afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na tabia za usafi katika familia na jamii kwa ujumla ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu.
-Mwisho-














