Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 26 Mei 2021

WIZARA YA AFYA KUJA NA MFUMO WA UFUAUTILIAJI WA WAJAWAZITO NCHI NZIMA






Na Englibert Kayombo – WAMJW, Dodoma


Wizara ya Afya inatarajia kuja na mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito wote toka wanapofika kliniki kwa mara ya kwanza hadi baada ya siku 42 za kujifungua.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo alipokutana na wataalam wa afya katika kikaokazi cha maandalizi ya utengenezaji wa mfumo huo.


“Nataka muwe mnafuatilia taarifa za wajawazito na kujua maendeleo yao toka wanapofika kituoni siku ya kwanza mpaka baada ya kujifungua kwa data za kila siku na kujua kwa namna gani wajawazito au mama baada ya kujifungua ameweza kupata huduma zetu na muweze kuchukua hatua pale mnapoona changamoto” amesema Dkt. Dorothy Gwajima.


Waziri Gwajima amesema kuwa ili kuweza kuwa na mfumo wenye ufanisi ni lazima tusisitize matumizi sahihi ya takwimu na kuwataka wataalam wa afya katika kazi zao kuhakikisha wanachukua takwimu zote zinazohitajika kwa ajili ya matuzimu katika mfumo huo.


Waziri Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali katika kupambana na vifo vya wajawazito imefanya mambo mengi ikiwemo kuanzisha Kampeni maalum ya Jiongenze Tuwavushe Salama iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kupunguza na kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi. 


“Serikali imejenga vituo vingi vya huduma ngazi zote na mwamko wa wajawazito wanaojitokeza kuhudhuria kliniki umekuwa mkubwa” amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongezea kuwa bado elimu inahitajika kutolewa kwa ili wajawazito wafike katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuanza kliniki mapema.


“Sasa hivi mwitikio umeongezeka, wajawazito wanajitokeza na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma kati yao wengine wanafariki, lakini tukijadili kujua kwanini amefariki na tukifuatilia wakati alipokuwa kliniki tunagundua hatukumfuatilia vizuri, hiki ndio kitu tunachoimarisha ili ufuatiliaji uwe imara” amefafanua Dkt. Dorothy Gwajima.


Waziri Gwajima amesema kuwa katika kuimarisha mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito, wanatarajia kuimarisha ufuatiliaji wa mteja mmoja mmoja toka anapopata ujauzito, muda wa kuanza kliniki, kujifungua mpaka baada ya siku 42. 


Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale amesema kuwa kwa kupitia kanzidata wanazochukua kutoka kwenye taarifa za wajawazito zinawasadia kujua bidhaa gani za dawa zinazihitajika kumhudumia mjamzito, miundombinu ipi wanahitaji, inaonyesha uwajibikaji wa watumishi wa afya kwa ujumla wao na mmoja mmoja, pamoja na kutuonyesha kama miongozi iliyopo inatija katika kusaidia kutoa huduma bora kwa wajawazito. 


“Hakuna njia nyingine ambayo tutaitumia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi zaidi ya kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mama mmoja mmoja kama kanzidata hii inavyotaka” Amesema Dkt. Sichwale


-Mwisho-

Jumatatu, 24 Mei 2021

HEDHI SIO UGONJWA WALA LAANA – Waziri Gwajima



Na WAMJW - Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hedhi wanayopata wanawake sio ugonjwa wala laana bali ni uumbaji wa Mungu katika kumkamilisha mwanamke.


Waziri Gwajima amesema hayo leo katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu siku ya hedhi ambayo inaadhimishwa kila mwaka duniani kote kila ifikapo tarehe 28 mwezi Mei ambayo mwaka huu ina kaulimbiu inayosema “Ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa msichana/mwanamke”.


“Siku ya hedhi duniani inaadhimishwa kila mwaka, licha ya mwaka jana kutofanyika kutokana na changamoto ya Covid 19 lakini jumuiya ya Kimataifa imeendelea kufahamishana, kuelimishana na kukumbushana juu ya jambo hili muhimu kwa njia ya mtandao. Lengo kuu ni kueleza Dunia na Umma wa Tanzania kuwa hedhi sio ugonjwa wala laana bali ni hali ya kawaida na Baraka ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu inayomtokea msichana mara baada ya kuvunja ungo kama ishara ya mabadiliko kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi”. Amesema Waziri Gwajima.


Waziri huyo ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kila siku wanawake zaidi ya milioni 12 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wanakuwa kwenye Hedhi duniani.


Aidha, Waziri Gwajima amesisitiza Hedhi Salama akimaanisha kwamba msichana au mwanamke anapokuwa katika siku zake anatakiwa kuzingatia mazingira salama na anapata huduma zote muhimu ikiwemo miundombinu ya vyoo vyenye usiri, maji safi, taulo za kike au vifaa salama vya kujisitiri na utupaji salama wa vifaa/taulo za kike zilizotumika.


Hata hivyo, Waziri amesema kuna baadhi ya wasichana au wanawake wanakua katika mazingira ya kutokua na hedhi salama ambayo inachangiwa na miundombinu duni ya vyoo, kukosekana kwa maji safi na salama, matumizi ya vifaa vya hedhi visivyo salama na utupaji ovyo wa vifaa vilivyotumika.


“Matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na OR -TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Hedhi Salama mwaka 2019, yanaonesha Nchi yetu imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya ajenda ya afya ya hedhi. Hata hivyo, changamoto ni nyingi katika ngazi ya jamii hususan kuwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya hedhi salama. Kwa mfano ni asilimia 28 tu ya wasichana ndiyo wenye uelewa thabiti juu ya hedhi salama”. Ameongeza Waziri Gwajima.


Takwimu zinaonesha kuwa maeneo mengi hapa Nchini jamii inakosa uelewa wa umuhimu wa hedhi salama. Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuonesha ukosefu wa uelewa wa hedhi salama ni pamoja na Halmashauri za Namtumbo, Muleba, Mbeya, Igunga, Temeke, Karatu, Tandahimba, Rorya, Kusini Unguja na Kaskazini Pemba ambayo jamii yake ilionekana inauelewa mdogo juu ya suala la hedhi salama. Huku utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ukionesha kuwa asilimia 60 ya wasichana walionekana kutomudu gharama za taulo za kike.


Hata hivyo, Waziri Gwajima amewashukuru wadau kupitia mtandao wa hedhi salama kuendelea kuhamasisha upatikanaji wa vifaa vya hedhi salama ndani ya nchi kwa unafuu na ubora unaotakiwa ili kila mhitaji kwa makundi yote aweze kutumia.

Jumapili, 23 Mei 2021

WIZARA YA AFYA YAANZA UTEKELEZAJI WA MABORESHO YA HUDUMA ZA MATIBABU KWA WAZEE


Waziri wa Afya Dkt.Gwajima akiwa Kwenye chumba Cha kuwahudumia Wazee kilichopo Kwenye jengo la wagonjwa wa nje,mbele yake ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt.Ernest Ibenzi

Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima akiangalia Bango linaloelezea huduma za wazee wakati wa ziara ya kuona utekelezaji wa maboresho ya Huduma ya Wazee Kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akipima afya Kwenye jengo wa wagonjwa wa nje kwa kutumia  'patient monitor' ambayo unapima Presha,mapigo ya Moyo na wingi wa hewa ya Oksjeni.

Waziri Dkt.Gwajima akiangalia mfumo wa kuwahudumia wagonjwa uliopo Kwenye hospitali hiyo.

Mmoja wa mzee aliyefika kupata matibabu kweenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma

Waziri Dkt.Gwajima akiwa amevalia vazi maalumu la kumtambulisha mtoa huduma ambaye anawahudumia Wazee kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.Mkakati huo itatekelezwa nchi nzima Kwenye vituo vya kutolea huduma.


Na.WAMJW-Dodoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya ufuatiliaji  wa maelekezo yake  katika kuboresha huduma za matibabu kwa wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kujionea jinsi walivyoweza kutekeleza maagizo ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee wanaofika kupata matibabu hospitalini hapo.

Dkt. Gwajima amesema mahitaji ya maboresho ni mengi  hivyo wizara yake imeona ianze na vitu  vile vya msingi  ambavyo wazee wamekuwa wakiyalalamikia   kila siku wanapofika kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya.

Ametaja malalamiko yanayokuwa yakilalamikiwa na wazee  wanapofika kwenye vituo vya afya ni pamoja na mapokezi yasiyoeleweka na kutokupata huduma iliyokusudiwa na kuongeza kuwa   wazee nguvu zimekwisha hivyo wanahitaji kuongozwa kwahiyo wizara yake wamefanya maboresho kwa kuwa na watu maalumu wa kuwapokea wazee hao pale wanapoifika hadi kuondoka na kuwatambulisha kwa kuvaa sare maalumu.

“Kila kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare ambayo itamtambulisha na imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’  pamoja na kuweka mabango yanayomuelekeza au kumuongoza mzee wapi atapata huduma anazozihitaji na ambayo yameandikwa "Mpishe Mzee apate huduma kwanza".

Dkt. Gwajima amesema maelekezo hayo wameyatoa katika hospitali na vituo vya afya vyote na kwa hatua hiyo sasa wizara inaenda kutengeneza muongozo ambao utakua wa uwiano kwa hospitali zote.  Hata hivyo ameipongeza hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma kwa kuanza utekelezaji huo na kuwa itakuwa ya mfano wengine kujifunza utaratibu unaotumika na kuboresha kulingana na mazingira yao.

Aidha, Dkt. Gwajima amewataka hospitali zingine kutokusubiri miongozo katika kutekeleza  maelekezo yanayolewa na kusiwe na visingizio vingi kwamba haiwezekani kwani maagizo yanayotolewa yanawezekana na utekelezaji wake ni wa mara moja hususan katika hospitali za kuanzia halmashauri hadi ngazi ya Taifa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vivian Wonanji  amesema idara yake imeandaa mkakati wa huduma wa wazee wa  miaka kumi na ifikapo mwezi Juni mwaka huu wataanza kuandaa mpango wa utekelezaji wake.

Dkt. Wonanji amesema mpango mkakati huo utakuwa na mambo makuu yakiwemo kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za wazee,"kama tunavyofahamu wazee wanahitaji mambo mengi ikiwemo masuala ya lishe na utengamao hivyo mkakati huo utakua na maono muhimu ambayo yatasaidia kuboresha huduma za wazee nchini”.

Wakati huo huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema hospitali yake imejipanga kuwahudumia wazee wa rika tofauti wakiwemo wenye uoni hafifu na hivyo waratibu wa wazee huwafuata wazee mara wafikapo hospitalini  hivyo wanashukuru mapokeo ya wazee pamoja na wagonjwa wanaofika kupata huduma. 

Mnamo tarehe 7 Mei, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dar es salaam aliahidi kuboresha tiba kwa wazee  kwani tiba ni haki yao ya msingi  katika daraja lolote lile watakalokua wanaugua kuanzia vituo vya afya, zahanati hata hospitali za Taifa.

-Mwisho-

Jumatano, 19 Mei 2021

FAHAMU ZAIDI KUHUSU KIPIMO CHA RT-PCR KWA WASAFIRI

 


Jumatatu, 3 Mei 2021

TRAVEL ADVISORY NO.6 OF 3RD MAY 2021