Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 29 Agosti 2018

VIONGOZI WA DINI WAWE SEHEMU MUHIMU KATIKA MIKAKATI YA KUJIKINGA NA EBOLA.

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi wa kwanza kulia akikagua kituo cha muda mfupi cha kuhifadhia wagonjwa watakaopatikana  au kusadikika kuwa na ugonjwa wa  Ebola katika Bandari ya kigoma  kabla ya kuwapeleka katika Kituo husika wakati wa ukaguzi na mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo leo Mkoani Kigoma, katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Ally  Mohammed.

 Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Ally Mohammed akitoka kukagua ndani ya  kituo cha muda mfupi cha kuhifadhia wagonjwa watakaopatikana  au kusadikika kuwa na ugonjwa wa  Ebola katika Bandari ya kigoma  kabla ya kuwapeleka katika Kituo husika wakati wa ukaguzi na mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo leo Mkoani Kigoma.

 Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi wa kwanza kulia akikagua maeneo mbalimbali ya Bandari  ya Kigoma wakati wa ukaguzi na mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo leo Mkoani Kigoma  katikati ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chawote na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Ally  Mohammed.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chawote aliyesimama akisoma taarifa ya ugonjwa wa Ebola na hatua wanazochukua kujikinga na ugonjwa huo pindi utakapoingia nchini  kwani kwa sasa ugonjwa huo umetaarifiwa upo  nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo  wakati wa ukaguzi na mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo leo Mkoani humo. 

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi katikati akiongea na baadhi ya watumishi wa afya pamoja waandishi wa habari wa Mkoa Kigoma hawapo Pichani wakati wa  mafunzo ya kujiandaa kujikinga na Ugonjwa wa Ebola ambao umetaarifiwa kuwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo mkoani humo. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya Wizara ya Afya Dkt. Mohammed Ally  Mohammed na wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua Mulindoko.


VIONGOZI WA DINI WAWE SEHEMU MUHIMU KATIKA MIKAKATI YA KUJIKINGA NA EBOLA. 


NA WAMJW-KIGOMA

VIONGOZI wa dini zote wametakiwa kushirikishwa kwenye maandalizi ya  mapambano ya ugonjwa wa ebola ambao umetaatifiwa upo nchi jirani ya Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  endapo itatokea utaingia nchini Tanzania ili kuweza kuutokomeza kabisa. 

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi wakati alipotembelea Mkoa wa Kigoma akiongozana na timu yake ya wataalam kwa ajili ya ukaguzi wa nyenzo na afua mbalimbali  zilizowekwa ili kupambana na ugonjwa wa ebola leo Mkoani humo. 

"Afua muhimu ya mkoa wowote  katika kupambana na ugonjwa huu ni kuwashirikisha vizuri viongozi wa dini zetu pamoja na viongozi wa kimila na jamii kwani ndio wanaokutana na wanajamii kwa muda mwingi zaidi hivyo kuwashirikisha kwao elimu juu ya kujikinga na  Ebola itakuwa kubwa zaidi na hatimae tutafanikiwa kujikinga na ugonjwa huu" alisema Prof. Bakari. 

Aidha Prof. Bakari Kambi amesema kuwa Mkoa wa Kigoma upo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa Ebola kwa kuwa kuna mipaka mingi iliyo wazi ambayo inaingiza wageni kutoka Burundi na Congo ambapo ugonjwa huo umetaarifa upo maeneo ya nchi ya Congo. 

Mbali na hayo Prof. Bakari Kambi ameuoingeza  uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa jitihada na mikakati waliyoiweka na kuifanyia kazi ili kuweza kudhibiti ugonjwa wa Ebola endapo utaingia Mkoani humo. 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chaote amesema kuwa Kigoma amesema kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola katika maeneo yote ya Mkoa huo. 

"Utambuzi wa joto la Mwili kwa wageni kutoka nchi jirani ya Congo wanaoingia kupitia bandari ya Kigoma, Manyovu, Kibirizi, Mabamba , Uwanja wa Ndege , Kituo cha Gari Moshi bado unaendea kufanyika kwa uhakika kwa kutumia Thermo scanner ili kudhibiti ugonjwa huo" alisema Dkt. Chaote. 

Aidha Dkt. Chaote amesema kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwa jamii, watumishi wa Afya, madereva wa magari ya kubebea wagonjwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kujikinga na ugonjwa huo endapo utaingia nchini. 

"Tumetoa mafunzo kwa timu za kitaalam  mbalimbali za Mkoa  pamoja na kuhakikisha madawa, vifaa tiba na PPE vipo vya kutosha wakati wote katika vituo vyote vilivyoanishwa kupokea na kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola" alisema Dkt. Chaote. 

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Kambi ameambatana na jopo la wataalam ikiwemo idara ya uhakiki ubora wa huduma za afya , Kitengo cha Dharura na Maafa,Elimu ya Afya kwa Umma , Kitengo Cha mawasiliano Wizara ya Afya zote kutoka Wizara ya Afya pamoja na  Wawakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kukagua na kujiridhisha mikakati ya kujikinga na Ebola endapo itaingia nchini.SERIKALI YASOGEZA HUDUMA ZA KIFUA KIKUU SUGU KARIBU NA WANANCHI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.

Wajumbe wakifuatilia mjadala uliokua unaendelea katika kikao cha mawasilisho ya taarifa za uendeshaji wa Hospitali za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto katika kamati ya kudumu ya Huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma
SERIKALI YASOGEZA HUDUMA ZA KIFUA KIKUU SUGU KARIBU NA WANANCHI 

Na.WAMJW,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya afya imefanya ugatuaji kwa kusogeza karibu na wananchi huduma ya kifua kikuu sugu (TB) ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kwa wananchi  katika ngazi ya vituo vya afya  sabini na nane nchini.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa fya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  ummy mwalimu wakati akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji wa hospitali ya magonjwa ambukizi Kibong’oto kwa kamati ya huduma za jamii ya Bunge jijini hapa.

Waziri Ummy alisema wamefanya ugatuaji  wa vituo hivyo vya afya ili kuwezesha wagonjwa kupata tiba jirani na jamii inayowazunguka na hivyo  kujenga uelewa wa wananchi juu ya ugonjwa  na kushiriki kikamilifu katika kumhudumia mgonjwa hasa katika chakula,masuala ya kijamii na kisaikolojia.

Alitaja mikoa ambayo vituo hivyo vipo ni pamoja na Kagera, Mtwara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma, Geita,  Mbeya, Pwani,Mrorgoro,Njombe,Iringa, Tanga, Mwanza , Lindi na Pemba na kuongeza kuwa hadi sasa wagonjwa wapatao 112 wamepata huduma  za tiba ya TB sugu.

“Takwimu zinaonesha kuwa kati ya watu laki moja, watu 287 wana TB na kati ya watu 100 kati yao 40 tunawagundua wana  TB hapa nchini”alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo mnamo  mwaka 2017 Serikali ilizindua kituo bora katika hospitali hiyo kwa kutoa huduma za afya kwa wachimbaji wa migodi wanaougua magonjwa ya TB, Mapafu na usikivu unaosababishwa na ulipuaji wa baruti migodini kwa kushirikiana na mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF).

Tangu kuanzishwa kwa kituohicho  jumla ya wagonjwa 863 wamepata huduma,wagonjwa 614 walipima makohozi na 116(19%) waligundulika kuwana TB na 123(15%) walikuwa na magonjwa ya mapafu yanayosababishwa na vumbi na 125(15.3%) walikuwa na upotevu wa usikivu.Jumanne, 28 Agosti 2018

SERIKALI IMETENGA BILIONI 30 KUJENGA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.

Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwasilisha ripoti ya uendeshaji wa Hospitali za rufaa za mikoa mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe. Peter Selukamba akitoa neno wakati wa kuwasilisha kwa taarifa za uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto jijini Dodoma.

Wajumbe wakifuatilia mjadala uliokua unaendelea katika kikao cha mawasilisho ya taarifa za uendeshaji wa Hospitali za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto katika kamati ya kudumu ya Huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma


SERIKALI IMETENGA BILIONI 30 KUJENGA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA
Na.WAMJW-Dodoma
Serikali imetenga shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kujenga  na kukarabati miundombinu ya hospitali zaRufaa za Mikoa  kila mkoa  ili kuweza kuwawezesha wananchi kupata huduma za rufaa za kibingwa karibu na wanapoishi na hivyo kupunguza adha ya kusafiri  umbali mrefu  kufuata huduma hizo
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati akiwasilisha  taarifa za uendeshaji wa hospitali za rufaa za Mkoa kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa  fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha hospitali za Rufaa za Mikoa ya Geita, Katavi, Simiyu, Njombe na Songwe ambapo zipo katika hatua za ujenzi wa  hospitali hizo hivyo itafanya idadi ya hospitali hizo kuwa 28 pindi zitakapokamilika.
“Serikali ilifanya mabadiliko ya kuzihamishia hospitali za Rufaa za Mikoa  Wizarani ili kuboresha huduma za kibingwa  ikiwemo kutoa fursa nzuri  ya udhibiti ,usimamizi na mgawanyo wenye tija zaidi wa rasilimali chache zilizopo”alisema Dkt.Ndugulile.
Alisema kuwa baada ya Wizara kukabidhiwa hospitali hizo ilifanya tathimini  ya awali ya hali halisi na kubaini  changamoto  mbalimbali zilizoathiri utoaji wa huduma za afya katika maeneo yote ambayo ni nguzo ya msingi  katika kuwezesha upatikanaji wa huduma bora.
“Hospitali za Rufaa za Mikoa zinapaswa kutoa huduma za kibingwa ambazo hazitolewi   katika hospitali ngazi ya Halmashauri,Huduma za kibingwa ambazo ni lazima kupatikana katika  hospitali za Rufaa”.Alisema Naibu Waziri Dkt. Ndugulile
Alitaja huduma za kibingwa ambazo zinatakiwa kutolewa katika hospitali hizo za Rufaa za Mikoa ni pamoja na upasuaji wa jumla,magonjwa ya uzazi na yanayoathiri wanawake, magonjwa ya watoto,magonjwa ya ndani ,magonjwa ya kinywa na meno na Radilojia.
Kwa upande wa ubora wa huduma zinazotolewa Naibu Waziri huyo alisema Wizara ilifanya kaguzi za kuzitambua hali halisi ya ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hizo  na jumla ya hospitali  za rufaa ishirini na moja zilifanyiwa tathimini na kupewa nyota kutokana na vigezo vilivyowekwa na kupewa  mpango kazi wa kuboresha huduma .
“Ni hospitali 9 zilipata nyota mbili, hospitali kumi na moja zilipata nyota moja na hospitali moja ilipata nyota sifuri,hivyo hakuna hospitali yeyote iliyopata nyota 3 hapa nchini.Alimalizia Dkt.Ndugulile

Jumatatu, 27 Agosti 2018

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI THABITI ILI KUDHIBITI UGONJWA WA EBOLA USIINGIE NCHINI.

- Hakuna maoni
Waziri wa Áfya Mhe Ummy Mwalimu akisisitiza jambo juu ya mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini wakati alipofanya ziara katika Mpaka wa Lusumo Wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera.

Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu  akimwelekeza jambo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt Marco Mbata mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini, wakati alipofanya ziara katika Mpaka wa Lusumo Wilaya ya Ngara.
Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara Luten Kanali Michael M.

Afisa Afya wa kituo cha uhamiaji Mpaka wa Lusumo Stanley S. Chipasula akipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Áfya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara ya kuangalia utayari wa Kagera kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie nchini kupitia Mpaka wa Lusumo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt Marco Mbata (aliyevaa suti ya bluu) akimwelekeza jambo Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu (wakatikati) leo wakati alipofanya ziara katika Mpaka wa Lusumo Wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera.


SERIKALI YAWEKA MIKAKATI THABITI ILI KUDHIBITI UGONJWA WA EBOLA USIINGIE NCHINI.


Na WAMJW - KAGERA, NGARA 

Serikali kupitia Wizara ya Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yaendelea kuweka mikakati thabiti katika maeneo yote hatarishi ikiwemo mipakan na njia za panya ili kudhibiti ugonjwa wa Ebola kuingia nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Áfya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu leo wakati alipofanya ziara katika Mpaka wa Rusumo kati ya nchi ya Tanzania na Rwanda  ili kuangalia ni jinsi gani Mkoa wa Kagera umejipanga katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kuingia nchini. 

Waziri Ummy amesema kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umetokea eneo la Kivu katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo unaiweka Tanzania katika hatari zaidi ya kuweza kupata wagonjwa wa Ebola kutokana na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizo.

"Mlipuko huo wa Ugonjwa wa Ebola ambao umetokea katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo sasa hivi inatuweka Tanzania katika hatari kubwa zaidi kupata wagonjwa kutokana na mlipuko huo kutokea eneo la Kivu Kaskazini ambalo ni karibu na Tanzania na muingiliano wa wananchi baina ya nchi hizi mbili ni mkubwa " Alisema Waziri Ummy Mwalimu. 

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu wa Sekta ya Áfya ili kufahamu jinsi ya kuwahudumia wanaohisiwa kuwa na Virusi vya ugonjwa wa Ebola sambamba na hilo Serikali imeleta vifaa kinga watakavyovaa wakati wakitoa huduma kwa mgonjwa au mhisiwa wa ugonjwa wa Ebola. 

"Kama Serikali, kubwa ambalo tumelifanya ni kuhakikisha tunatoa mafunzo kwa watoa hudumu wa sekta ya Áfya nchini.kwa mujibu wa taarifa ya WHO nchini Kongo watoa huduma wa Áfya 9 wamepata ugonjwa wa Ebola huku mmoja amefariki" Alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatenga Zahanati moja katika maeneo ya mipaka ambayo itakuwa inapokea wahisiwa au wagonjwa wa Ebola, vivyo hivyo kwa  ngazi ya Wilaya kutenga hospitali kwa ajili ya wahisiwa pindi utapoingia nchini.

Hata hivyo h Waziri Ummy amewataka wananchi wanaokaa katika vijiji vya mipakani ambavyo vinapokea watu kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Burundi wamuonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola wamwelekeze kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyo jirani.

" Wananchi ambao wanakaa mipakani hasa katika vijiji ambavyo vinapokea watu kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Burundi mnaowajibu wa kuhakikisha mnafuata taratibu za uhamiaji, lakini pale ambapo mtu ameingia na ana dalili za ugonjwa wa Ebola muelekezeni aende kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya" alisema Waziri Ummy

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Áfya imeajiri Watumishi wapya wa Sekta ya Áfya 33 ambao wamesambazwa kwenye maeneo ya mipakani ili kusaidia kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.

"Zuli ambalo tumelifanya, tumeajiri watumishi wapya wa Áfya 33 kwa ajili ya kuwasambaza katika maeneo haya ya mipakani ili kudhibiti ugonjwa huu wa Ebola usiingie nchini kwetu" alisema Waziri Ummy. 

Mbali na hayo Waziri Ummy amekiagiza kitengo cha Elimu ya Áfya kwa umma kutoka Wizara ya Áfya kutoa Elimu juu ya ugonjwa wa Ebola kwenye Serikali za vijijini kupitia Redio, vipeperushi, video jambo litalosaidia kuweka msukumo kwa wananchi ili kujua athari za ugonjwa huo kwa maendeleo ya Taifa.

Mwisho Waziri Ummy aliendelea kuwatoa hofu wananchi wa Tanzania kuwa ugonjwa wa Ebola bado haujaingia nchini. 

Ijumaa, 24 Agosti 2018

ZIARA KATIKA HOSPITALI TEULE YA RUFAA YA MKOA WA PWANI - TUMBI.

- Hakuna maoni
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi (Wa nne kutoka Kushoto) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha uzalishaji Dripu pindi walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi

Kushoto ni Mkurugenzi wa Ubora wa Uduma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Mohamed Mohamed akikagua Ubora wa chupa ya Maji ya Dripu pindi walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi, Wapili kutoka kushoto ni Mganga Mkuu wa Hospitali Dkt. Edward Wayi na watatu ni kiongozi wa Msafara Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Kambi.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi (Wapili kushoto) akipitia Mbao ya matangazo katika jengo la mionzi pindi walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi, wakwanza kushoto ni Daktari Msaidizi Mionzi Dkt. Patricia Petro, Watatu kushoto ni Mganga Mkuu wa Hospitali Dkt. Edward Wayi na wa mwisho ni Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima.

Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi (Wapili kutoka kushoto) wakati walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi

Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad Bakari Kambi wakiendelea na ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi

Na WAMJW-PWANI
Picha mbali mbali za matukio zikionesha Wakurugenzi mbali mbali kutoka Wizara ya Áfya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bakari Kambi walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika hospitali teule ya Mkoa wa Pwani -Tumbi leo.

Jumatano, 22 Agosti 2018

TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akionesha bango lenye ujumbe kuhusu Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akijibu maswali ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati waTamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Waandishi wa Habari waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akitoa Tamko kuhusu Tahadhari ya Ugonjwa wa homa ya Ebola uliojitokeza katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.


TAMKO KUHUSU TAHADHARI YA UGONJWA WA HOMA YA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Ndugu Wanahabari, 
Manamo tarehe 10/08/2018 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) uliotangazwa na shirika la Afya Duniani mnamo tarehe 1/08/2018. Katika taarifa hiyo ilielezwa kwamba jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 (CFR = 38.5%) vilitokea katika Nchi ya DRC. 
 
Hata hivyo tangu tulivyotoa tamko hadi tarehe 18/08/2018, hali ya ugonjwa imeendelea kwa kasi sana na kufikia wagonjwa 91 na vifo 50 (CFR = 54.9%). Aidha wagonjwa hawa wanatokea maeneo matano ya afya (Health zones) katika jimbo la Kivu Kaskazini na eneo jingine moja la Ituri. Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola kutokea nchini DRC, na umetokea wiki moja tu baada ya nchi hiyo kutangaza kumalizika kwa mlipuko mwingine uliotokea mwezi Mei 2018.

Ndugu Wanahabari
Sambamba na takwimu za hizi zilizotolewa na WHO, Wafanyakazi tisa (9) wa Afya wamethibitishwa kuugua ugonjwa huu, huku ikifanya jumla yao kufikia 10 (9 wamethibitika na 1 anafuatiliwa); na hadi sasa mfanyakazi mmoja amepoteza maisha. Wafanyakazi hawa wa Afya inaaminika kwamba wamepata ugonjwa huu wakati wakiwahudumia wagonjwa katika Kliniki zao za kawaida na sio zile za kutibia wagonjwa wa Ebola (Ebola Treatment Centres (ETCs), na wengi wao wameambukizwa kabla ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutangaza mlipuko huu. 

Ndugu Wanahabari
Tumeona ipo haja ya kuongea nanyi leo kutokana na ukweli kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limefanya tena tathmini ya hatari ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola nchini DRC na katika nchi zinazopakana  na DRC na kubaini kuwa hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huu kwa nchi zilizo jirani na DRC, ikiwemo Tanzania, imeongezeka maradufu na ni “kubwa” (yaani High risk) kutokana na kwamba; eneo lililoathirika la Kivu Kaskazini linapakana na nchi jirani ya Uganda, uwepo wa uhusiano wa wasafiri na wakimbizi wa DRC wanaoingia nchi jiarani za Uganda na Rwanda, na pia machafuko ya kijamii ambayo yameendelea kuchukua muda mrefukwenye  majimbo ya Kivu kaskazini na Ituri na hivyo kutatiza kwa kiwango kikubwa makabiliano dhidi ya ugonjwa huu. 
 
Aidha, eneo hili la sasa ni la karibu na nchi yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu umeshawahi kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu kutokana na ukaribu na mwingiliano  wa watu, hasa wasafiri wanaotoka na kuingia DRC kuja hapa nchini. 

Ndugu Wanahabari
HADI SASA HAKUNA MGONJWA YEYOTE ALIYEHISIWA AU KUTHIBITISHWA KUWA NA VIRUSI VYA EBOLA HAPA NCHINI. Hata hivyo kutokana na ukweli kwamba  kuna mwingiliano mkubwa wa wananchi kati ya nchi hizi mbili na ugonjwa huu kugunduliwa kwenye jimbo la Kivu Kaskazini ambalo linapakana na nchi ya Uganda ni ukweli unaotuweka kwenye hali ya wasiwasi mkubwa. 
 
Hivyo tunasistiza kwamba wanajamii wote ikiwemo wafanyakazi wa sekta ya Afya kuelewa vyema dalili za ugonjwa huu pamoja na kuongeza nguvu katika kufuata kanuni za kuzuia maambukizi katika vituo vya Afya yaani Infection Prevention and Control (IPC) measures. 
 
Wizara inapenda kutoa tahadhari kubwa ya ugonjwa huu kwa Wananchi wote, na katika mikoa yote hasa ile inayopakana na nchi jirani ya DRC ambayo ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha, hii haiondoi ukweli kwamba, viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA) cha Dar es Salaam, Kilimajaro (KIA) na Songwe cha Mbeya kuwa vipo katika hatari ya kuweza kuingiza mgonjwa wakati wowote ule. 
 
Kutokana na hali hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Washirika mbali mbali, ikiwemo WHO, wanafanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaopita katika mipaka yetu yote ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa huu hapa nchini.  

Ndugu Wanahabari
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola na mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Ebola hutokea pale binadamu anapogusana na mnyama aliyeathirika na ugonjwa huu kama vile Nyani, Sokwe au Popo. Aidha ugonjwa huu huenezwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa binadamu mwingine kwa njia zifuatazo;
Kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa Virusi vya Ebola
Kugusa vitu vya mgonjwa wa Ebola, kama vile nguo, shuka au godoro
Kugusa au kutumia vifaa vilivotumika kwa mgonjwa wa Homa ya Ebola kama sindano
Kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa Ebola
Kugusa wanyama (mizoga au wanyama hai) walioambukizwa kama vile sokwe na nyani wa msituni
Kukutana kimwili na binadamu mwenye maambukizi ya virusi vya Ebola.

Aidha tunasisitiza kwamba ugonjwa wa Homa ya Ebola hauenezwi kwa njia ya hewa, maji au chakula.
Dalili za Ugonjwa
Dalili za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa kutoka siku 2 hadi 21 tangu kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Dalili hizo ni pamoja na;
Homa kali ya ghafla, 
Kulegea kwa mwili,
Maumivu ya misuli, 
Kuumwa kichwa na vidonda kooni. 
Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi. 
Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu nyingi ndani na nje ya mwili. 


Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola:
Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:-
Epuka kugusa damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa  wa Ebola
Epuka kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki kwa dalili za ugonjwa wa Ebola; Aidha unatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutolea huduma za Afya kwa ushauri.
Epuka mila na desturi zinazoweza kuchelewesha mgonjwa kupatiwa huduma muhimu za Afya na kupelekea kueneza ugonjwa wa Ebola.
Kuzingatia  kanuni za Afya na usafi wa mwili
Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na kwa wahudumu wa Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili za ugonjwa huu.

Ndugu Wanahabari
Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha uwezo wetu wa utayari katika kukabiliana na ugonjwa huu kwa kuzuia usiingie, na hatua za kuchkua iwapo utaingia hapa nchini. 
Hadi sasa Wizara imefanya yafuatayo; 

Kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Ebola hapa nchini (Operational readiness assessment). Tayari tathmini hiyo imefanyika kwa kushirikiana na WHO kwenye mikoa minane ambayo ni Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya, Kigoma, Kagera, Arusha na Kilimanjaro na kuanisha uwezo uliopo na mapungufu ambayo yanafanyiwa kazi. 
Aidha, WAMJW imeajiri wataalamu wapya 33 ili kuongeza nguvu katika mipaka yetu na tayari wamesambazwa kwenye vituo vya mipakani.  
Tunaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (Travellers entry screening) kwa kutumia vifaa vya kupima joto (thermo scaners) na fomu maalum za wasafiri wanaoingia nchini, ambapo tayari kupitia MSD imepokea vifaa vyenye thamani ya Bilioni 5 kutoka WHO na vimeshapelekwa  kwenye maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa kinga kwa watumishi wa afya (Personal Protective Equipment, PPE’s) kwenye maeneo yote nchini.  
WAMJW kwa kushirikiana na Taasisi ya Udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani (Centres for Diseases Control, CDC) na Water Reed imenunua “kits” nne za kupima Ebola zenye uwezo wa kupima wagonjwa zaidi ya 400 na hivyo kuiwezesha Maabara ya Taifa na hile ya kanda ya Mbeya kuwa na uwezo mzuri. 
Hadi sasa WAMJW ina uwezo wa kupima ugonjwa huu Nchini kwa kutumia maabara ya Taifa Dar es Salaam, Hospitali ya kanda ya MBEYA na KCRI katika Hospitali ya KCMC, Kilimanjaro
Mafunzo ya usimamizi wa sampuli yamefanyika kwa Mikoa ya Mwanza, Arusha, Ruvuma, Kilimanjaro, Kigoma na Kagera kwa wiki iliyopita na kupatiwa jumla ya Triple packaging materials 18.
Uelimishaji wa umma unaendelea kufanyika kupitia matamko pamoja na matumizi ya vyombo vya habari ikiwemo vile vya kitaifa, vya binafsi, mitandao ya kijamii, vipeperushi na mabango. 
WAMJW tayari imeshatoa tahadhari kwa wadau na sekta muhimu wakiwemo TAMISEMI pamoja na mamlaka ya viwanja vya ndege ili kuongeza utayari wa maeneo husika
Vilevile Wizara yangu imepanga kufanya yafuatayo
Kuendelea kutoa mafunzo dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwemo kuwaongezea wataalamu wapatao 80 wa mipakani uwezo wa ufuatliaji na utambuzi wa ugonjwa huu. Mafunzo haya yanaendelea mjini Morogoro 
Kutoa mafunzo kwa Timu za dharura na maafa (Rapid Respond Teams) ambayo yanategemewa kuanza mnamo tarehe 27 Agosti 2018 jijini Mwanza. Lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuratibu na kukabiliana na ugonjwa huu endapo utatokea hapa Nchini. Idadi ya wataalam watakao pata mafunzo hayo ni kama ifuatavyo; Mkoa wa Mwanza (15), Kagera (15) na Kigoma (15) ili kujaza nafasi ya mapungufu katika wilaya ambazo ziko katika hatari na bado hazijapata mafunzo haya. 
Timu ya Wakurugenzi wa Wizara ikiongozwa na Mganga Mkuu wa serikali itatembelea mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza. Lengo la ziara hii ni kufuatilia kwa ukaribu utayari wa mikoa hii katika kukabiliana na ugonjwa huu endapo utatokea
Kituo chetu cha uratibu wa milipuko ya magonjwa na majanga yaani Public Health Emergency Operation Center (PHEOC) kipo katika utahadhari wa juu (level 1 - High Alert) ili kufuatilia kwa ukaribu ugonjwa huu nchini DRC pamoja na kuratibu utayari wetu Kitaifa na katika ngazi ya Mikoa 

Hitimisho
Wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa huu, pamoja na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa  kuugua ugonjwa huu hapa nchini. 


Hivyo naelekeza yafuatayo:-
Wakuu wa Mikoa yote, waitishe kikao cha Afya ya msingi (PHC) na kujadili jinsi mikoa yao ilivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia kwenye maeneo yao
Wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika ofisi za serikali za mitaa au kijiji au kituo cha kutolea huduma za Afya endapo kutatokea mtu  yeyote mwenye dalilil za ugonjwa wa Ebola
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya, na hasa wale walioko katika mikoa iliyo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi, wawe macho na makini zaidi katika kusimamia jitihada hizi za Wizara. 
Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali, zikiwemo taasisi za kimataifa katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti iugonjwa huu ili usiingie hapa nchini. 
.
Ahsanteni kwa kunisikiliza

Jumatatu, 20 Agosti 2018

WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII WANAHITAJIKA NCHINI

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiongea na wadau wa sekta ya afya wakati akifungua kikao cha wahudumu wa afya ngazi ya jamii hii leo jijini Dodoma

Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akifuatilia kwa makini Maelekezo ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya hayupo pichani katika kikao kilichoshirikisha wadau wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kinachofanyika jijini Dodoma.

Wadau wa afya kutoka mikoa mbalimbali nchini wakisikiliza kwa makini mjadala unaoendelea katika kikao kilichoshirikisha wadau wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kinachofanyika jijini Dodoma.

Katibu mkuu wizara ya afya, Maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa afya katika ufunguzi wa kikao kinachoshirikisha wadau wa afya nchini na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.


Wadau wa afya kutoka mikoa mbalimbali nchini wakijadili kwa makundi mada mbalimbali  katika kikao kilichoshirikisha wadau wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kinachofanyika jijini Dodoma.

NA WAMJW-DODOMA 

Wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanahitajika nchini ili waweze kusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza waweze kutafuta huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mahali popote.
Hayo yamesemwa leo na katibu Mkuu Wiraya ya Afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Mpoki Ulisubisya wakati kikao cha wadau cha kujadili taarifa ya uchambuzi yakinifu  kwa ajili ya kuhuisha mtaala wa watoa huduma  ya afya ngazi ya jamii kinachofanyika jijini hapa.
Dkt.Mpoki alisema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya sekta ya afya yenye lengo la kuboresha huduma za afya na kuimarifa afya za wananchi.
Aidha,alisema wahudumu wa afya ngazi ya jamii  wana nguvu  kwani wana mchango mkubwa mkubwa kwani ni makomandoo ambao wanaweza kutoa elimu kwa jamii na hivyo kusaidia kuzuia magonjwa yanayosababisha vifo vitokanavyo na uzazi.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi kati ya akina mama 100,000  ni vifo 556 hutokea  hivyo kuwapo wa hudumu wa afya gazi ya jamii wanaweza kupunguza hali hiyo.
“ Katika kufikia malengo ya Tanzania ya uchumi wa kati na  viwanda, wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanatakiwa kutumika kuwaibua akina mama ambao hawapeleki watoto wao kupata chanjo, na matumizi sahihi ya matumizi ya vyandarua ili kuepuka ugonjwa wa Malaria nah ii imeonekana  pia katika nchi za afrika kam Ethiophia,Rwanda na zingine
Hata hivyo Dkt.Mpoki aliwataka wadau  kuunga mkono  jitihada hizi za serikali na hivyo kubainisha maeneo ambayo watasaidia
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo na Wataalam wa Rasiliamali watu Dkt.Otilia Gowele alisema kwa sasa wanapitia upya  mtaala wa mafunzo kwa wa hudumu wa afya ngazi  ili kuendana na hali halisi ya sasa na mahiaji katika sekta ya afya.
“tuekutana ili kupokea na kujadili maoni ya wadau kwa kuzingatia tathimini ya kina iliyofanywa katika kuuhisha mtaala wa mafunzo ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuangalia changamoto ili kuendana na mahitaji halisi na kukidhi soko la ajira katika hopsitali za umma na binafsi,” alisema.
Alisema tangu kuanza kutumika kwa mataala wa mafunzo ya watoa huduma wa afya ngazi ya jamii mwaka 2015 na kutumika kwenye vyuo 78 hapa nchini, tayari wataoa huduma wapatao 9,000 wamehitimu.
.