Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu akiongea na Wadau wa masuala ya Afya katika kikao cha tathimini
yakuokoa maisha ya mama na mtoto iliyofanywa mapema leo jijini Dar es
salaam na shirika la Thamini Uhai.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Mstaafu Emmanuel Maganga
akisisitiza jambo wakati wa kikao cha tathimini yakuokoa maisha ya mama
na mtoto iliyofanywa mapema leo jijini Dar es salaam na shirika la
Thamini Uhai.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkurugenzi wa Kinga kutoka
Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati wa kikao cha tathimini yakuokoa
maisha ya mama na mtoto iliyofanywa mapema leo jijini Dar es salaam na
shirika la Thamini Uhai.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu baada ya kikao cha
tathimini yakuokoa maisha ya mama na mtoto iliyofanywa mapema leo
jijini Dar es salaam na shirika la Thamini Uhai.
WAZIRI UMMY AWAAGIZA WAGANGA WAKUU WA MIKOA KUTIMIZA WAJIBU WAO KATIKA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI.
Na WAMJW-DSM
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa yote nchini kuhakikisha wanatimiza
wajibu wao kikamilifu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Amesema
hayo mapema leo jijini Dar es salaam katika kikao cha tathmini ya miaka
kumi (10) ya kuokoa maisha ya mama na mtoto katika maeneo ambayo ni
magumu kufikika, iliyofanywa na Shirika la Thamini Uhai katika Mkoa wa
Kigoma.
“Nawataka Waganga
Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutimiza wajibu wao katika kuondokana na
tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi, kwa kuhakikisha vipaumbele vyao
viwe na lengo moja kwa moja la kupunguza vifo vya watoto wachanga na
mama wajawazito” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri
Ummy alisema kuwa kama kila mtu atatimiza wajibu wake, inawezekana
kabisa ifikapo 2020 vifo vitokanavyo na uzazi vikapungua kwa zaidi ya
Asilimia 50%, hivyo kuwaagiza Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya
kuhakikisha vifaa muhimu vya huduma za uzazi vinakuwepo ili kumsaidia
mama mjamzito .
Aidha,Waziri
Ummy amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kufanyia uchunguzi juu ya Vifo
vyote vya akina mama wajawazito vinavyotokea katika vituo vya kutolea
huduma za Afya jambo litaloweza saidia kubaini tatizo lilipo.
“Tumetoa
maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha vifo vyote vya akina
mama wajawazito vinavyotokea katika vituo vya kutolea huduma na katika
jamii, vitolewe taarifa” alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Sambamba
na hayo Waziri Ummy alisema kuwa Serikali katika kuhakikisha inapunguza
vifo vya uzazi kwa kuboresha vituo vya Afya ili kuviwezesha kutoa
huduma za wa Dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni,
Aliendelea
kusema kuwa Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kati
ya vituo vya Afya vya Serikali takribani 473, ni vituo vya Afya 117 sawa
na Asilimia 21% vilikuwa na uwezo wa kutoa Huduma za upasuaji wa
Dharura, hivyo kuwashukuru Wadau kwa kushirikiana na Serikali kuboresha
vituo vya Afya 208.
Hata
hivyo, Waziri Ummy alisema kuwa katika kuimarisha Afya ya Mama, Uzazi na
Mtoto, Serikali imeweka malengo kuwa ifikapo mwaka 2020 angalau
Asilimia 50% ya Vituo vya Afya nchini viweze kutoa huduma hizi kwa ubora
unaotakiwa.
“Tunataka
itapofika mwaka 2020, tunataka angalau Asilimia 50 ya Vituo vya Afya
nchini viweze kutoa huduma hizi, hivyo nikiwa kama msimamizi wa Sera za
Afya mpango wangu wa sasa ni kutaka kuhakikisha Ubora wa huduma hizi”
alisema Mhe. Ummy Mwalimu
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Emmanuel Maganga alisema kuwa Mkoa wa Kigoma
umepiga hatua kubwa katika kusogeza huduma za dharura kwa wananchi na
kufikia Asilimia 53 ya vituo vya Afya vyote vilivyopo huku wakitarajia
kufikia Asilimia 83 ifikapo Desemba mwaka huu baada ya uboreshaji wa
vituo vya Afya vingine 10 unaoendelea sasa.
“Hadi
sasa idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za Dharura za upasuaji
ni Asilimia 53 ya vituo vya Afya vyote vilivyopo huku matarajio ni
kufikia asilimia 83 ifikapo Desemba mwaka huu (2018) baada ya uboreshaji
wa vituo vya Afya vingine 10 unaoendelea sasa” alisema Mhe. Maganga.
Aliendelea
kusema kuwa Idadi ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya
kutolea Huduma za Afya imeendelea kuongezeka kwa kasi sana , mwaka 2015
wakina mama waliojifungua katika vituo vya kutolea huduma za Afya
ilikuwa Asilimia 58 ya matarajio, Mwaka 2016 ilikuwa Asilimia 65 na
Mwaka 2017 ni Asilimia 78, huku Idadi ya wanaohudhuria kliniki
iliongezeka na kufikia Asilimia 113 ya matarajio.
0 on: "WAZIRI UMMY AWAAGIZA WAGANGA WAKUU WA MIKOA KUTIMIZA WAJIBU WAO KATIKA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI."