Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 31 Desemba 2017

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA DKT. NDUGULILE ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO DKT. FAUSTINE NDUGULILE ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu  ametujaalia  kwani kuna wengi walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.  Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa  Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa.  Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya  watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
i.            Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia,  kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa  katika  misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba  kuaminiwa  huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika  utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za nchi,  Kanuni, Sera, pamoja na  Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko  ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha, nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.

ii.            Mabaraza ya Taaluma
Natumia fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa  mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na ujuzi  unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.

iii.            Wanajamii
Napenda kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia heshima na utu wa binadamu.  Pia, mnayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za Nchi.  Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi, dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.

Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
a)     Wanataaluma na Watoa Huduma,
        i.            Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili  wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
      ii.            Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
   iii.            Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.

    iv.            Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
      v.            Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).

b)    Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe (e-mails).

c)     Wanajamii kwa ujumla:
        i.            Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
     ii.            Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
a.     Uongozi wa kituo husika,
b.     Mganga Mkuu wa Wilaya,
c.      Mganga Mkuu wa Mkoa,
d.     Ofisa wa TAKUKURU,
e.     Baraza la Taaluma Husika,
f.       Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
g.     Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
h.     Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
 Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.

Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.

Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
31/12/2017.

TANGAZO KWA UMMAJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anawatangazia wanafunzi wote walioko vyuoni wanaosoma masomo ya Shahada za Uzamili (Masters Degree) katika fani za Afya kwamba Wizara imepata fedha zitakazowezesha ufadhili (Sponsorship) kwa baadhi ya Wanafunzi, na kwa baadhi ya maeneo, kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Hivyo, kwa Tangazo hili, wale wote wenye nia ya kuomba ufadhili wanatakiwa kuwasilisha maombi yao.
Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo (Tuition fee), pamoja na posho ya utafiti pindi mwanafunzi anapokuwa kwenye kipindi cha kufanya utafiti kama sehemu ya mafunzo yake (Dissertation allowance).
Vigezo vitakavyotumika kuchagua watakaowasilisha maombi yao ni hivi vifuatavyo :

1. Kuwasilishwa kwa maombi rasmi ya ufadhili
2. Mwombaji kuwa Raia wa Tanzania.
3. Awe amedahiliwa Chuoni kuanza masomo kwa mwaka wa kwanza 2017/2018
4. Kipau mbele kitatolewa kwa:
a. Watumishi wa Serikali waliomo kwenye sekta ya Afya wanaofanya kazi katika vituo vilivyoko Wilayani/Mikoani ambao baada ya mafunzo watarudi kuendelea kufanya kazi katika vituo vyao vya awali, au watapangiwa vituo vya kazi sehemu nyingine yeyote nchini
b. Waombaji waliodahiliwa katika fani ambazo ni za msingi katika utoaji wa huduma za rufaa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Nyanja hizo ni Anaesthisiology, Surgery, Neurosurgery, Obstetrics and Gynaecology, Orthopaedics Surgery, Emergency Medicine, Paediatrics, Internal Medicine, Critical Care in Nursing na Midwifery and Womens Health
c. Waombaji waliodahiliwa katika nyanja za Ubingwa/Ubingwa wa Juu (Specialities na Super-specialities) zenye umuhimu mkubwa katika Hospitali za Kitaifa (kama Cardiology, Nephrology, na Oncology) ili kujenga uwezo wa ndani ya nchi katika jitihada za kupunguza wagonjwa wa rufaa wanaotibiwa nje ya nchi.
5. Aidha, mwombaji atatakiwa awe:
a. na barua ya ruhusa ya masomo kutoka kwa mwajiri wake (iambatanishwe)
b. Tayari kuingia mkataba wa kuitumikia Serikali kwa muda usiopungua miaka 5 baada ya kuhitimu mafunzo.
c. Hana ufadhili mwingine wa masomo yake

Tangazo hili linafuta ufadhili uliokuwa umetolewa awali kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya Shahada za Uzamili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu Dodoma (UDOM). Hivyo wanafunzi waliokuwa wamechaguliwa watapaswa kuomba upya kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kwenye tangazo hili.
Aidha kwa kuwa wanafunzi wamekwisha ripoti vyuoni wahakikishe barua za maombi zinapitishwa kwa Wakuu wa Vyuo ili kuthibitisha kuwa mwanafunzi yuko chuoni.
Tangazo hili linahusu wale walioko vyuoni kwa mwaka wao wa kwanza wa masomo wa 2017/2018 tu.
Mwisho wa kupokea maombi haya ni tarehe 12/01/2018.
Maombi yote yaelekezwe kwenye anuani ifuatayo;

Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Chuo Kikuu Dodoma,
Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Maendeleo ya Jamii
S.L.P 743
DODOMA

Jumamosi, 23 Desemba 2017

SERIKALI YATARAJIA KUANZISHA BIMA YA AFYA KWA WATU WOTE

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya baadhi ya Watumishi(hawapo kwenye picha) wa Taasisi ya Kiuma inayomiliki chuo cha Uuguzi, Kituo cha Afya na Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma.

Mkurugenzi Mkuu wa chuo cha Uuguzi na Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo mbele ya Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile (Hayupo kwenye picha) wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua daftari la baadhi ya Vifaa vya Maabala wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua baadhi ya vifaa katika chumba cha Kompyuta wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa kike(Matroni) wa Kituo cha Afya cha Kiuma Maria Ntazama,  kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kiuma na Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua moja ya darasa katika chuo cha Uuguzi Kiuma wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Kituo cha Afya cha Kiuma.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua vitabu katika maktaba ya chuo cha Uuguzi na ukunga Kiuma wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) wakiwa katika ziara yake Wilayani  Tunduru, wakwanza ni Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara Ya Afya Dkt. Otilia Gowele na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Kiuma ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Dkt. Matomola.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Kiuma ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Upendo wa Kristo Dkt. Matomola, wakati akikagua  mabweni ya chuo cha Uuguzi na ukunga Kiuma kilichopo Wilaya ya Tunduru.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha uuguzi na ukunga Kiuma kilichopo Wilaya ya Tunduru wakifuatilia hotuba kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Dkt Faustine (hayupo kwenye picha),  wakati alipofanya ziara katika taasisi hiyo ya Kiuma Wilayani Tunduru.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua kwa umakini Daftari la opokeaji Dawa pembeni yake ni Afisa wa Kliniki Hassan Miengende.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Kadi za dawa wakati alipofanya ziara katika kituo cha Afya Mkasale Wilayani Tunduru.

Wanchi wa Kijiji cha Mkasale wakifuatilia kwa makini agizo kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile juu ya usimamiaji wa rasilimali fedha katika kituo chao cha Afya.


Na WAMJWW, TUNDURU
Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuanzisha mfuko wa Bima ya Afya kwa watu wote nchini jambo litalosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma katika Taasisi ya Kiuma inayomiliki Hospitali, Chuo cha Uuguzi na Kanisa la Upendo wa Kristo.

“Tunatambua kwamba si kila mtu anamudu gharama hizo, kwa bahati mbaya ugonjwa unakuja wakati hatuja jiandaa, serikali imeliona hilo, pamoja na mikakati tunayoendelea nayo ya Bima ya Afya ya NHIF na CHF, tunatarajia kuja na utaratibu wa bima ya afya kwa wote, suala la matibabu lisiwe la kuwaza” alisema Dkt. Faustine Ndugulile.

Dkt. Faustine aliendelea kusema kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa  wote wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.

“Tumefkia hatua kubwa sana ya walengwa wote wanaohitaji kupata chanjo, jambo linaloifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi chache sana zilizofikia malengo hayo” alisema Dkt. Faustine

Aidha Serikali imetoa fedha kwa Vituo vya Afya 172 kwa lengo la kujenga thieta, Chumba cha Kujifungulia, Wodi ya Wazazi, nyumba ya Watumishi na Maabara, Huku Wilaya ya Tunduru ikifanikiwa kupata fedha hizo kwa vituo viwili, kikiwepo kituo cha Afya cha Mkasale.

Kwa upande mwingine  Dkt. Faustine ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Kiuma kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ikiwemo kutoa huduma za afya kwa wananchi, kutoa ajira, jambo linalotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Taasisi hiyo hivyo kuipunguzia mzigo Serikali katika Nyanja hizo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Uuguzi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanisa la Kanisa Upendo wa Kristo Kiuma Dkt. Matomola ameiomba Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile itambue huduma inayotolewa chuoni hapo na kuwaongezea Watumishi, pia Serikali iwasaidie kuchangia mahitaji madogo madogo kama vitabu, maabara na vifaa.

Katika ziara hiyo Dkt. Ndugulile alifanikiwa kutembelea Kituo cha Afya Mkasale katika Wilaya hiyo ya Tunduru na kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa huku akiwasisitiza wananchi wasiuziwe dawa zote muhimu kwani hali ya upatikanaji wa Dawa ni nzuri maeneo yote na sasa ni wastani wa asilimia 80.

Aidha Dkt. Ndugulile amewahakikishia wanakijiji wa Mkasale kuwa kituo chao cha Afya kipo katika Vituo 172 vilivyopata mgao wa fedha za ujenzi wa maabara, chumba cha kujifungulia, Wodi ya wazazi, thieta, na kuwataka kusimamia vizuri fedha hizo ili kuweza kuboresha Zaidi huduma katika kituo hicho.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Wilaya ya Tunduru Mhe. Chiza Marando wakati akiwasilisha taarifa ya Wilaya alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 65 zikiwemo Hospitali 3 Vittuo vya Afya 5 na Zahanati 57 kati ya hizo 52 ni za serikali, 3 ni za mashirika ya dini na 2 zinamilikiwa na watu binafsi.

Mhe. Chiza Marando aliongeza kuwa Halmashauri ya Tunduru inakabiriwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya Afya hali inayopelekea changamoto kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika halmashauri hiyo.
“Tunduru ina jumla ya watumishi 339 wa Serikali sawa na asilimia 26.3 kati yawatumishi 1286 wanaohitajika na kufanya upungufu wa watumishi 974 sawa na asilimia 73.6, huku upungufu mkubwa ukiwa  katika kada ya madaktari, waganga, maafisa Afya na wauguzi.” Alisema Mhe. Chiza Marando

Kwa upande mwingine Mhe. Marando aliongeza kwa kusema hali ya utoaji huduma imeongezeka ikiwemo Huduma ya Chanjo kutoka 94 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 95 mwaka 2016 na kwa mwaka 2017 kiwango kimefikia asilimia 92.

Aidha Mhe. Chiza Marando alisema kuwa Wilaya hiyo inatoa huduma kwa makundi maalumu kwa kuzingatia Sera ya Wizara ya Afya kwa kutoa vitambulisho vya matibabu ya Wazee kwa baadhi ya kata zilizofanyiwa utambuzi, tayari vitambulisho 1234 vimetolewa kwa Wazee.

Jumatano, 20 Desemba 2017

SHILINGI BILIONI 3.1 ZIMETUMIKA KUJENGA MAJENGO YA CHUO CHA UUGUZI NA UKUNGA MIREMBE

Waziri Ummy Mwalimu akisoma maandishi ya jiwe la ufunguzi wa jengo hilo,kulia ni mwakilishi toka Global Fund Martha Setembo.

Mkandarasi aliyejenga majengo ya Chuo cha Uuguzi Mirembe Nishit Jethwa kutoka kampuni ya V.J. Mistry Co LTD ya Mkoani Kagera.

 Mshauri elekezi wa mradi huo Dkt.Moses Ockony ambae pia ni Mkurugenzi wa Mekon Arch Consult LTD.

Mwakilishi wa Wizara ya Fedha Kamishna Msaidizi Adrian Njau akitoa shukrani mara baada ya ufunguzi wa majengo hayo.

Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Afisa wa mradi huo kutoka Wizara ya Afya Dkt.Catherine Joachim (kulia) na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Mpoki Ulisubisya.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria ufunguzi wa majengo ya chuo cha Uuguzi cha Mirembe ambayo yamegharimu shilingi Bilioni 3.1, majengo yaliyojengwa ni pamoja na bweni moja litakalotumika na wanafunzi 256 ,nyumba mbili za watumishi,jengo la utawala, madarasa,jiko panoja na bwalo la chakula.

 Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Mirembe Athanas Paul akisoma taarifa ya chuo hicho.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa makabidhiano ya majengo hayo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia  wa Kupambana na UKIMWI,KiFUA KIKUU na Malaria(Global Fund), kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya.


Na WAMJW-Dodoma
Shilingi bilioni 3.1 zatumika kujenga majengo ya chuo cha Uuguzi na Ukunga Mirembe mjini hapa ambayo yatasaidia kuongeza idadi ya wahitimu wa kada hiyo nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa makabidhiano ya majengo hayo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia  wa Kupambana na UKIMWI,KIFUA KIKUU na Malaria(Global Fund).

Mhe. Ummy aliwashukuru Global fund kwa kusaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini hasa katika mikoa kumi na saba ya Tanzania bara katika ujenzi wa vyuo, nyumba za watumishi ,maghala ya kuhifadhia dawa pamoja na magari ya kusafirishia dawa kupitia bohari ya dawa(MSD).

"Bila afya hakuna viwanda wala kilimo, hivyo serikali ya awamu ya tano imejikita katika utoaji wa huduma wa afya na rasiliamali watu na hivyo tunatarajia kuona ongezeko la wanafunzi katika vyuo vyetu"
Aidha,Ummy alisema kupitia mfuko huo umesaidia nchi katika kukabiliana na magonjwa ya UKIMWI,Kifua Kikuu na Malaria.

Alisema Watoto 10,000 nchini Tanzania huzaliwa wakiwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa Mwaka huku watu zaidi ya 900,000 wakitumia dawa za kufubaza Makali ya ugonjwa huo (ARVs).

Waziri alisema idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na wajawazito wanaobainika kuwa na VVU hivyo kunahitajika kazi ya ziada ili kukomesha kabisa tatizo hilo na watoto wazaliwe wakiwa wazima.

Ummy alisema serikali imejipanga kuhakikisha tatizo hilo linakwisha kwani inawezekana kabisa mtoto kuzaliwa bila ya maambukizi ya Ukimwi na hilo ndilo lengo lake akiwa Wizara ya afya.

“Hali ya maambukizi bado iko juu, kwa sasa tumeshasajili watu laki tisa ambao wanatumia dawa za kufubaza Makali ya Ukimwi na tatizo kubwa ni idadi ya watoto 10,000 ambao huzaliwa wakiwa na maambukizi, nataka tutoke huko,” alisema Mwalimu.

Waziri alisema wizara kwa sasa bajeti imeongeza kutoka asilimia 9.2 kwa Mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 10 kwa Mwaka 2017/18 na kuifanya sekta ya afya kuwa sekta ya kipaumbele miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mgao wa bajeti hivyo hakuna kisingizio tena.

Kuhusu vyuo vya uuguzi alikiri Wizara kuvisahau kutokana na taarifa ya mkuu wa chuo hicho Athanas Paul kwamba aliomba sh 300 milioni lakini kwa ajili ya shughuli za uendeshaji lakini tangu januari serikali ilipeleka chuoni hapo Sh 150,000 tu.

Alisisitiza Wizara kutupia macho katika eneo hilo ikiwemo kufuta jina la chuo cha Mirembe na badala yake kisomeke Dodoma Mirembe Nursing Collage kwani Mirembe ni hospitali ambayo wengi huamini kuwa walioko huko wanamagonjwa ya akili.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Dk. Mpoki Ulisubisya alisema Chuo hicho kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi bila kusahau majengo kwa ajili ya ofisi na madarasa.

Dkt. Ulisubisya alitaja uhaba wa Watumishi lakini akasema mambo hayo yatashughulikiwa kwa ukaribu zaidi ikiwemo Majengo yaliyojengwa na Global Fund ambayo yanakwenda kupunguza msongamano huo.

Mwakilishi wa Global Fund Martha Setembo alisema ushirikiano wa mfuko huo na serikali ulianza Mwaka 2003 kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya.

Setembo alisema ziko fedha nyingi ambazo zimetengwa kwa ajili ya kusaidia sekta hiyo katika miradi inayotekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo na akaomba Serikali kuendelea kuitumia vema miradi hiyo ikiwemo Majengo wanayokabidhiwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Majengo ya vyuo vya uuguzi.
WAUGUZI NI CHACHU YA HUDUMA BORA NCHINI

Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Gustav Moyo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya maadili kwa wauguzi wakuu wa Mikoa na hospitali za Kitaifa na za Rufaa za kanda unaoendelea chuo cha Uuguzi Mirembe Mkoani Dodoma

Wauguzi wakuu toka mikoa mbalimbali wakifuatilia mada zinazowasilishwa kwenye mafunzo hapo.mafunzo hayo yana lenga kuwakumbusha uadilifu na maadili ya uuguzi wakati wa utoaji huduma za afya nchini.

Baadhi ya wauguzi wa mikoa wakijadili kwenye makundi mikakati ya nini kifanyike katika kutekeleza majukumu yao ili kuondokana na malalamiko ya taaluma yao kutoka kwa wananchi.

 Wauguzi wakuu wakiendelea na kazi kwenye makundi.

Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga Gustav Moyo akiongea na wauguzi wakuu wa mikoa kwenye mafunzo hayo.Na WAMJW-Dodoma

Wauguzi wakuu wa Mikoa na hospitali za Taifa na Rufaa za Kanda wametakiwa kusimamia maadili ili kupunguza malalamiko toka kwa wananchi.

Hayo yamesemwa  jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Mpoki Ulisubisya wakati wa mafunzo juu ya maadili kwa wauguzi wakuu yanayoendelea mjini hapa kwenye chuo cha uuguzi na ukunga Mirembe

Dkt.Mpoki alisema  hivi sasa kumekua na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa hivyo kupitia mafunzo hayo wanapaswa kusimamia ipasavyo maarifa na mikakati watakayojiwekea ili kuleta mabadiliko makubwa na kuondoka malalamiko hayo.

"Jamii na Serikali inawategemea sana katika usimamizi wa huduma bora nchini,naamini kwamba ninyi mna nguvu,nia na maarifa katika kuboresha maadili ya wauguzi wote nchini,hivyo ni muhimu mkasimamie"alisema Dkt.Mpoki

Aidha, alisema wizara yake inatambua umuhimu wa kuboresha maadili hususani kwa wauguzi,hivyo kuwapatia mafunzo kama ni muhimu kwa taaluma yao.

"Kumekuwepo na malalamiko na ongezeko kubwa la vitendo visivyo vya kiadilifu kwa watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na kauli mbovu kwa wagonjwa,naamini kwa mafunzo haya changamoto zote mtazijadili na kusaidia kuondokana na malalamiko toka kwa wananchi"

Naye Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga wizara ya afya Gustav Moyo alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa namna gani ya kuboresha uadilifu na maadili ya sehemu zao za kazi wauguzi nchini

Aidha,ametoa wito kwa wauguzi wote nchi kuzingatia Iadilifu,utu,upendo na maadili yao ya kwa kuipatia thamani stahiki taaluma yao kwani wauguzi ndio wanaokuwepo muda wote mahali pa kazi.
"Serikali ya awamu ya tano inasisitiza suala la uadilifu hivyo wananchi wanahimizwa kuwabaini na kuwasema ili kuwabaini baadhi ya  wanaokiuka maadaili au kufanya vitendo visivyozingatia maadili ili tuwachukulie hatua ama kurekebisha na tuweze kutoa huduma yenye viwango na inayokubalika na salama kwa wananchi".

Jumamosi, 16 Desemba 2017

MPANGO WA MALIPO KWA UFANISIWALETA MABADILIKO SEKTA YA AFYA RUFIJI.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu   akisisitiza jambo mbele ya wakazi wa Kijiji Nyamwage cha wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake ya kuangalia utekelezaji unaofanyika kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika mikoa nane nchini.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akimkabidhi moja yam zee kadi ya Afya ya matibabu bure kwa wazee wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake mapema jana.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongozana na Tabibu mfawidhi wa Zahanati ya Nyamwage Agness Salvatory Kilapilo wakati wa ziara yake ya kuangalia utekelezaji unaofanyika kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika mikoa nane nchini.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Nyamwage (hawapo kwenye picha) wakati alipotembelea duka la dawa katika Zahanati ya Nyamwage.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akifuatilia matangazo katika mbao ya matangazo katika Zahanati ya Nyamwage wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake mapema jana, pembeni yake ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji  Mhe. Juma Njwayo.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akimpa maelekezo Tabibu mfawidhi wa Zahanati ya Nyamwage Agness Salvatory Kilapilo wakati akikagua Usafi wa Choo nkatika Zahanati hiyo.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisalimiwa na  mtendaji kata wa kata ya Umwe baada ya akipokelewa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Juma Njwayo wakati wa ziara yake alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aliyebeba mtoto huku akiwa ametabasamu akiwa na mama wa mtoto huyo Bi. Mwamvua wakati alipotembelea wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya cha Ikwiriri, aliesimama ni Msimamizi wa Wodi ya Wazazi Gidion Stevene.

Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisikiliza jambo kwa umakini kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Mohammed Mchengerwa wakati akijiandaa kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyamwage .

Picha ya pamoja nikiongozwa na Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Wazee wa Kijiji cha Nyamwage wakiwa wameshika kadi za matibabu ya bure kwa wazee.


Na.WAMJW-Rufiji
Utekelezaji wa mpango wa malipo kwa ufanisi(RBF) Wilayani Rufiji umeleta mabadiliko makubwa katika Vituo vya afya na Zahanati kwa uboreshaji wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa dawa muhimu

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake ya kuangalia utekelezaji unaofanyika kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika mikoa nane nchini

Waziri Ummy alisema mabadiliko hayo katika sekta ya afya yamefanyika katika maeneo ya utoaji huduma,Uongozi na Utawala,Rasiliamaliwatu,Mifumo ya usimamizibwa utoaji taarifa za afya,madawa na teknilojia ya afya ambapo mfumo huo umesaidia maboresho, uwajibikaji,ufanisi na usawa kwani dhana hiyo inamfanya mtoa huduma kulipwa kulingana na matokeo ya kazi yake ambayo amehakikiwa na hivyo kucanya vituo hivyo kuweza kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa na kuboresha miundombinu ya vituo hivyo

"Tumeanza mpango huu katika mikoa 8,tumefanya tathimini kwenye vituo vya afya na zahanati zote za Mkoa wa Pwani ikiwemo Wilaya ya Rufiji,tukagundua vituo vya afya na zahanati hazikuwa na viwango vya ubora unaogakiwa tukaona tuwapatie  shilingi milioni 10 kila kituo vilivyokidhi kwa ajili ya kuboresha miundombinu"alisema Waziri ummy.

Hata hivvyo aliipongeza kamati ya afya ya kijiji cha Nyamwage kwa kutumia ipasavyo shilingi milioni 10 kwa kuongeza urefu wa paa na kupaua,kuweka malumaru na kuongeza matundu ya choo pamoja na tundu moja la choo kwa ajili ya walemavu"nikupongeze mganga mfawidhi kwa kuboresha zahanati hii kwakweli unapaswa kupongezwa kwani umefanya vizuri ila badilika lugha chafu kwa wananchi haitakiwi,nakupa mwezi mmoja ila kwa upande huu mwingine umenifurahisa,mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni"

Aidha ,alitoa wito kwa wanawake  kuhudhuria kliniki pale wanapohisi kuwa wajawazito na hasa mahudhurio yote manne ili kuweza kujua hali zao kiafya na kuweza kupata matibabu pale wanapogundulika na matatizo na kujifungua salama"hatutaki kuona mwanamke mjamzito anafariki wakati wa kujifungua,ndiyo maana serikali ya awamu ya tano imeboresha huduma za afya na tumeanza ujenzi wa vyumba vya upasuaji wa dharura kwa mwanamke atakayepata uzazi pingamizi,kujifungua salama ni haki ya kila mwanamke mjamzito

Akisoma taarifa ya  Wilaya,Mkuu wa Wilaya ya Rufiji  Mhe.Juma Njwayo alisema mpango wa malipo kwa ufanisi umeongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye zahanati na kutoka 3,382 mwaka 2016 hadi kufikia 4,086 mwaka 2017 na wanawake wanaohudhuria mahudhurio  manne kliniki wamefikia 3,955 mwaka 2017 kutoka 1,906 mwaka 2016.

"Hali ya upatikanaji dawa muhimu hivi sasa ni asilimia 91 na dawa zingine ni zaidi ya asilimia 50 na hii inachangiwa na mpango huu"alisema Mhe. Njwayo.

Malipo kwa ufanisi (RBF) wilayani Rufiji ulianza kutekelezwa mwaka 2016 kwa kupatiwa shilingi milikni 240 kutoka wizara ya afya na kila kituo cha afya ama zahanati kilipatiwa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na inatekelezwa kwenye vituo kumi na mbili ambavyo vilikidhi vigezo vya mpango huo.

DKT.NDUGULILE AWATAKA TICD KUUNDA BODI MARA MOJA.


Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile aliyevaa shati la vyumbavyumba akikagua na kutoa maelekezo juu ya upatikanaji wa dawa katika baadhi ya vituo vya afya katika Wilaya ya Meru wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katikati akipata maelezo kutoka kwa mmoja ya  mtumishi wa  Chuo Cha Maendeleo ya Jamii cha Tengeru (TICD) wakati alipotembelea chuo hiko katika ziara yake mkoani arusha.

Baadhi ya Watumishi wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru TICD wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile hayupo pichani wakati alipotembelea chuo hiko katika ziara yake mkoani Arusha.

Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katikati akionyeshwa mpaka  wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru TICD wakati alipotembelea chuo hiko katika ziara yake mkoani Arusha.

Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile aliyevaa shati la vyumbavyumba akiwajulia hali baadhi ya wagonjwa  katika vituo vya afya katika Wilaya ya Meru wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wa pili kulia akisikiliza maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Meru Dkt. Cosmas Kilasara wa kwanza kulia kwenye moja ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha.

Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile kulia akiongea na baadhi ya wanakijiji wa kata ya Mbuguni wilayani Meru wakati wa ziara yake mkoani Arusha.

Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru TICD wakitoa chngamoto na maswali kwa Naibu Waziri Wa afya,Maendeleo ya jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile hayupo pichani wakati alipotembelea chuo hiko katika ziara yake mkoani Arusha.


Na WAMJW- ARUSHA.
NAIBU Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amutaka uongozi wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuunda Bodi ya chuo haraka iwezekenavyo ili kuleta maendeleo ya kitaaluma chuoni hapo.

Hayo ameyasema wakati alipotembelea Chuo hiko leo katika ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha kwa ajili ya kuangalia hali ya upatikanaji wa huduma za afya .

"Uongozi wa chuo unatakiwa kuhakikisha unakuwa na bodi ya chuo pamoja na kuwa na Mkuu wa chuo alithibitishwa kwani mpaka sasa hakuna mkuu wa chuo hiyo ni hatari"alisema Dkt. Ndugulile

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa uongozi wa chuo hiko hauna budi kuhakikisha unamaliza tatizo la mipaka na kupata hati miliki ya kiwanja hiko kwani inaweza kusababisha upokwaji wa kiwanja hiko.

Katika ziara hiyo Dkt. Ndugulile alifanikiwa kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Meru na kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa dawa na kuwasisitiza wananchi wasiuziwe dawa zote muhimu.

Aidha Dkt. Ndugulile ametembelea Kituo cha Afya Mbuguni na kuwapongeza kutokana na kupeana elimu juu ya uzazi wa mpango kwa wanakijiji wote wa kata hiyo na kufanya kupata huduma za afya kwa urahisi na kwa ufasaha.

"Ila nataka niwaambie wanakijiji hata kama dawa zipo kwa asilimia 100 na sisi ni lazima tujikinge na magonjwa yasioambukiza kwani yamekuwa tishio kwa watanzania"alisema Dkt. Ndugulile 

Aidha Dkt. Ndugulile amepongeza viongozi wa Hospitali ya Meru na Kituo cha afya Mbuguni Wilayani Meru kwa kupiga hatua katika kutokomeza vifo vya mama na watoto.

Alhamisi, 14 Desemba 2017

HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA HOSPITALI YA RUFAA YA TAALUMA NA TIBA (MAMC) ILIYOKO MLOGANZILAJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA HOSPITALI YA RUFAA YA TAALUMA NA TIBA (MAMC) ILIYOKO MLOGANZILA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayo furaha kuwatangazia wananchi wote na wadau wote wa Sekta ya Afya kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Taaluma na Tiba (MAMC) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyoko Mloganzila, jijini Dar es Salaam, imeanza kupokea wagonjwa waliopewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya ndani (internal medicine).

Hii inafuatia kufunguliwa rasmi kwa Hospitali hiyo na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 25 Novemba, 2017.

Wizara inapenda kutumia fursa hii kuwafahamisha Waganga Wakuu wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda kwamba maelekezo yamekwisha tolewa ya namna ya kuelekeza rufaa za wagonjwa wao katika hospitali ya MAMC.

Aidha, Wizara inapenda kuwataarifu Wananchi na Wadau wa Huduma za Afya kuwa, MAMC ni Hospitali ya kisasa kabisa, na ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kwa kiwango kama kile ambacho kinatolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Vilevile, MAMC inashirikiana na wataalamu mabingwa kutoka MNH katika kuhudumia wagonjwa.

Taarifa hii ni muhimu kwa kuwa, kumekuwa na uvumi kutoka kwa baadhi ya wadau wanaodhani kuwa hospitali hii ni ya mafunzo, na hivyo haiwezi kutoa matibabu sawa na MNH. Wizara inawahakikishia wananchi na wadau wote kuwa, huduma zinazotolewa na MAMC zinajumisha pia huduma za daraja la ubingwa wa ngazi ya juu  (super specialized services) na zenye ubora stahiki.

Wizara inatoa wito kwa wananchi na wadau wote kupokea na kutumia huduma zinazotolewa na MAMC.

Wizara itaendelea kutoa taarifa za huduma mpya za MAMC kwa kadri zitakavyokuwa zinaanzishwa ili rufaa husika zielekezwe huko.Dkt. Mpoki M. Ulisubisya.
KATIBU MKUU (AFYA)
14/12/2017

USIKOSE KUFUATILIA KIPINDI CHA TUNATEKELEZA TBC1 LEO DESEMBA 14, SAA 3:30 USIKU


Jumatano, 13 Desemba 2017

TAARIFA YA MWEZI NOVEMBA KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINIJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


TAARIFA YA MWEZI NOVEMBA KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI ILIYOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 13 DISEMBA 2017

Ndugu wanahabari,
Huu ni mwendelezo wa taarifa za kila mwezi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini ikiwa taarifa hii ni ya mwezi Novemba 2017. Aidha taarifa hii inaendelea kutoa maelekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kudhibiti ugonjwa huu nchini.

Ndugu Wanahabari,
Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 hadi 30 Novemba 2017, jumla ya wagonjwa walioripotiwa walikuwa ni 462 na vifo 15. Jumla ya Mikoa 10 na Halmashauri 17 zimeripoti wagonjwa wa Kipindupindu kwa mwezi Novemba. Mikoa iliyoripoti wagonjwa wa Kipindupindu ni Dar es salaam (14 na kifo 1), Dodoma (20 bila kifo), Tanga (5 bila kifo), Ruvuma (73 na vifo 8), Morogoro (5 bila kifo), Rukwa (7 na kifo 1), Manyara (13 na kifo 1), Songwe (80 bila kifo), Mbeya (119 bila kifo), Kigoma (126 na kifo1). Halmashauri zilizoripoti wagonjwa wa Kipindupindu ni Kinondoni (8 bila kifo), Ubungo (6 na kifo1), Mpwapwa (5 bila kifo), Chamwino (12 bila kifo) na Bahi (3 bila kifo), Mkinga  5 bila kifo), Nyasa (73 na Vifo 8), Kilosa (5 bila kifo), Sumbawanga Vijijini (7 na kifo1), Kiteto (13 na kifo1), Songwe Vijijini (80 bila kifo), Mbeya Vijijini (25 bila kifo), Mbeya Mjini (26 bila kifo), Chunya (10 bila kifo), Kyela (58 bila kifo) na Kigoma vijijini (10 bila kifo), Uvinza (116 na kifo 1)Ndugu Wanahabari,
Takwimu zinatuonesha bado maambukizi mapya ni tishio kwani kuna ongezeko la idadi ya Mikoa na Halmashauri zinazotoa taarifa za wagonjwa ikilinganishwa na mwezi uliopita japokuwa idadi ya wagonjwa imepungua. Mwezi wa Oktoba tulikuwa na jumla ya wagonjwa 570 ikilinganishwa na mwezi huu ambapo tuna jumla ya wagonjwa 462. Jumla ya Mikoa 6 na Halmashauri 11 ziliripoti wagonjwa wa Kipindupindu mwezi uliopita ukilinganisha na jumla ya Mikoa 10 na Halmashauri 17 zilizoripoti wagonjwa mwezi huu.
Pia takwimu za kipindupindu nchini kwa mikoa za tangu mwaka huu uanze zinaonyesha ongezeko za ugonjwa huu, Aidha kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2017, jumla ya mikoa 17 ilitoa taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu, ikiwa na jumla wa wagonjwa 3,839 na vifo 71 (Kama jedwali linalofuata linavyoenesha). Mikoa saba (7) haikuripoti kuwepo kwa ugonjwa huu, mikoa hii ni pamoja na Mwanza, Shinyanga, Arusha, Lindi, Kagera, Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.
Na.
Mkoa
Januari hadi Septemba, 2017
Octoba,2017
Novemba,2017
Jumla(Januari hadi Novemba,2017)
Wagonjwa
Vifo
Wagonjwa
Vifo
Wagonjwa
Vifo
Wagonjwa
Vifo
1
Mbeya
591
7
0
4
119
3
710
14
2
Morogoro
308
11
7
0
5
0
320
11
3
Dar es Salaam
306
4
0
0
14
1
320
5
4
Iringa
274
8
58
1
0
0
332
9
5
Dodoma
216
3
14
1
20
0
250
4
6
Kigoma
188
3
0
0
126
1
314
4
7
Katavi
133
1
0
0
0
0
133
1
8
Tanga
117
2
6
1
5
0
128
3
9
Mara
110
0
0
0
0
0
110
0
10
Pwani
83
1
0
0
0
0
83
1
11
Manyara
0
0
0
0
13
1
13
1
12
Songwe
82
0
376
4
80
0
538
4
13
Singida
58
0
0
0
73
8
131
8
14
Rukwa
46
1
0
0
7
1
53
2
15
Ruvuma
0
0
0
0
0
0
0
0
16
Njombe
10
0
0
0
0
0
10
0
17
Tabora
7
1
0
0
0
0
7
1
Jumla
2816
45
461
11
462
15
3739
71


Ndugu Wanahabari,
Nchi yetu inaelekea katika majira ya mvua ambazo zinaweza kuongeza kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Kipindupindu, hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia ugonjwa huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa.  Aidha, Wizara inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu. Jamii izingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
1.    Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi.
2.    Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo, na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
3.    Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
4.    Kunywa maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au yaliyochemshwa na kupoa.
5.    Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu.
6.    Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
7.    Kutoa huduma ya kwanza katika ngazi ya jamii kwa mgonjwa yeyote mwenye dalili za kipindupindu kwa kumpatia ORS.
8.    Endapo ORS itakuwa haipatikani hasa nyumbani, unaweza kutumia maji yaliyochanganywa na chumvi na sukari. Maji haya huweza kuandaliwa kwa kuchanganya maji safi yaliyochemshwa kiasi cha lita moja na vijiko viwili vya sukari na nusu kijiko ya chumvi.
9.    Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.

Ndugu Wanahabari,
Ni dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi zote hadi katika jamii ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara inasisitiza kuwa wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali ili kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye halmashauri na mikoa. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.

Ndugu Wanahabari,
Changamoto moja wapo katika kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu ni upatikanaji wa maji safi na salama. Wizara inaendelea kusisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye Halmashauri na Mikoa yote nchini.
  1. Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
o   Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
o   Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.
  1. Utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, za ugonjwa wa Kipindupindu kwa kufuata miongozo iliyopo.
  2. Kuongeza uwajibikaji wa viongozi na watendaji (Leadership and accountability): Usimamizi wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu ni muhimu kwa viongozi na wanaowasimawa. Hii ni pamoja na;
o   Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
o   Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
o   Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
  1. Kuihusisha jamii katika ngazi za chini kabisa (serikali ya kijiji/mtaa) kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu katika maeneo yao kwa kusimamiana wenyewe katiaka makundi madogo madogo yenye kaya 10 hadi 20 kufanikisha utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na wataalamu wa afya. Maelekezo hayo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa kaya ambazo hazitibu maji ya kunywa, hazijajenga na hazitumii choo, wanajamii wanaochafua vyanzo vya maji na kaya au wanajamii ambao bado wanaendesha kwa siri biashara za vinywaji au chakuka zilizosimamishwa.

Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Makamu wa Raisi alizindua awamu ya pili ya kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira yenye kaulimbiu, “Usichukulie Poa Nyumba ni Choo”. Napenda kuchukua nafasi hii kuhimiza ujenzi wa vyoo bora kwa kila kaya ili kuweka safi mazingira yetu hasa ikizingatiwa kuwa ni asilimia 40 tu ya kaya hapa nchini zina vyoo bora.
Aidha, Wizara yangu imekuwa karibu na Mikoa na Halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu kwa kufanya yafuatayo:
o   Kutuma timu za wataalamu kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika kushirikiana na Mikoa na Halmashauri katika kudhibiti ugonjwa huu
o   Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa pamoja na kupima usikivu wa dawa inayofaa kutibu wagonjwa katika mlipuko huu
o   Kupeleka Vifaa tiba na dawa katika Mikoa na Halmashauri zilizoathirika kupitia kanda ya bohari ya Dawa (MSD)
o   Kusambaza dawa ya kutibu maji majumbani katika Mikoa na Halmashauri zilizoathirika

HITIMISHO
Ninatambua kuwa zimekuwepo jitihada mbalimbali, na ninawashukuru na kuwapongeza wote wanaoendelea kupambana na ugonjwa huu. Aidha, ninaendelea kuwashukuru wataalam wa sekta husika, mashirika ya kimataifa, watumishi, mikoa, halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.Asanteni sana