WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA
WAZEE NA WATOTO
TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU USAMBAZAJI WA KONDOM KWA UMMA.
Kumekuwa
na taarifa mbalimbali, hamaki na kejeli zinazoenea katika mitandao ya kijamii
kuhusiana na taarifa iliyotolewa tarehe 27 Novemba 2017, Mnazi Mmoja kwenye uzinduzi
wa Mkakati wa Taifa wa Kondom kuhusu mpango wa Serikali kununua na kusambaza
kondom 500,000,000 katika kipindi cha miaka mitatu 2018 hadi 2020.
Tunapenda
kuukumbusha umma wa Watanzania kwamba maambukizi ya VVU na UKIMWI bado ni
tatizo katika nchi yetu. Takriban watu 1,400,000 wanakadiriwa kuwa na VVU. Hivyo
katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI Serikali inaendeleza afua mbalimbali ili kuzuia
maambukizi mapya. Asilimia 40% ya maambukizi mapya yanatokea miongoni mwa vijana
wenye umiri wa miaka 15-24. Aidha makundi maalum kama vile wanaojidunga madawa
ya kulevya, wanaofanya biashara ya ngono na wale wanaoamiiana wa jinsia moja
wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi. Makundi mengine ya walio katika hatari ni
waendesha magari ya masafa marefu, wavuvi na wananchi wa kwenye migodi.
Wizara
inatekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushauri nasaha na kupima uwepo
wa VVU, na kisha kuanza tiba na matunzo, pamoja na kutoa dawa za kufubaza kwa
watakao kuwa na maambuzi ya VVU. Kuna afua pia za kuzuia maambukizi ya mama
kwenda kwa mtoto, kutoa elimu ya VVU/UKIMWI na afya uzazi kwa vijana, elimu
kuhusu VVU/UKIMWI kwa jamii na tohara kwa wanaume. Matumizi ya kondom ni moja
wapo ya afua katika kuzuia maambukizi mapya. Hata hivyo utafiti wa viashiria vya Malaria na UKIMWI wa mwaka 2011/12 umebaini
kuwa kuna matumizi duni ya kondom, kwani ni asilimia 27 tu ya watu wenye wenza
zaidi ya mmoja waliokiri kutumia kondom mara ya mwisho walipofanya ngono. Hivyo
Serikali
itaendelea kununua na kusambaza kondom kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU,
magonjwa ya ngono na mimba zisizo tarajiwa ikiwa ni mojawapo ya afua hizo za
kudhibiti maambukizi ya VVU.
Tunasisitiza kuwa Wizara na wadau wake
inaendelea kutoa elimu ya kondom sambamba na elimu ya kusubiri kufanya ngono
kwa wale ambao hawajaanza na wale ambao wameanza lakini wanapaswa kusubiri (Abstinence) na elimu ya kuwa waaminifu
kwa mwenza mmoja aliye mwaminifu na anaejua hali yake ya maambukizi ya VVU (Be faithfull). .
Hivi
sasa nchini kuna vyanzo vya upatikanaji wa kondom vya aina tatu. Kwanza ni
kondom zinazopatikana kupitia sekta ya umma
ambazo husambazwa na Serikali kwa wananchi bila malipo. Pili, kuna
kondom zinazosambazwa na wadau ambazo zinauzwa kwa bei ya chini kwa kuwa wadau wamechangia.
Mfano kondom za Salama na Dume, na chanzo cha tatu ni kondom za kibiashara
ambazo zinauzwa kwa bei ya kati na ya juu.
Kondom
za sekta ya umma husambazwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na huduma
za mkoba ngazi ya jamii, Kondom za wadau na zile za biashara husambazwa katika
maduka ya dawa, maduka ya bidhaa mbambali, baa na nyumba za wageni.
Kwa
mwaka 2016/17 Serikali iliboresha kondom zinazopatikana kupitia ya sekta ya umma
kwa kuipa kifungashio kipya na jina la ZANA, ambapo kondom 36,916,911 zilisambazwa. Kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2018 hadi 2020 Serikali
kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa kudhibiti malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu
inatarajia kununua kondom za kiume
takribani 500,000,000. Kondom hizi zitasambazwa kupitia vituo vya kutolea
huduma za afya na katika maeneo hatarishi yanayoaminika kuwa na watumiaji
wengi. Aidha, kwa vile imebainika kuwa watu ambao hawaumwi hawaendi vituo vya
afya kwa ajili ya kuchukua kondom tu na hivyo kupelekea kutofikia
walengwa, usambazaji na ugawaji huu utalenga maeneo ambayo
Kunamatukio ambayo yanaendana na
ngono na yana walengwa wa afua za kondom. Maeneo haya ni kama baa, nyumba za
kulala wageni, maeneo yenye mikusanyiko ya magari ya masafa marefu, maeneo ya
uvuvi na migodini.
Aidha ikumbukwe kwamba nchi yetu
ina sera sheria, mila, desturi na maadili yetu kama watanzania, Hivyo kondom zote haziruhusiwi kusambazwa bila kufuata miongozo ya Wizara, ili
kulinda zisifike kwa wasiolengwa.
Hivyo basi, iwapo tunataka kuzuia na kumaliza maambukizi
ya VVU na UKIMWI ifikapo 2030 tunapaswa kama nchi kuwekeza katika kuzuia
maambukizi mapya. Matumizi ya kondom, ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi, dawa
za ARV na za magonjwa nyemelezi ni afua muhimu. Tunaomba wanahabari na wananchi
waunge mkono juhudi hizi kwa kuwa tunahitaji watanzania wenye afya bora na
uwezo wa kuzalisha ili kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Imetolewa
na:
KATIBU MKUU
- AFYA
30 Novemba, 2017
0 on: "UFAFANUZI KUHUSU USAMBAZAJI WA KONDOM KWA UMMA"