Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 24 Aprili 2019

WAZIRI UMMY ALIPONGEZA JIJI LA DODOMA KWA JITIHADA ZA KUTOKOMEZA MALARIA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamoi, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akimuangalia mtoto aliyeletwa kliniki ya kituo cha Afya cha Makole kilichopo Jijini Dodoma kwa ajili ya kupata chanjo wakati alipotembelea kituo hicho kwa ajili ya kugawa vyandarua vyenye dawa.

Waziri Ummy Mwalimu akimpongeza baba aliyeleta mtoto kliniki kwa ajili ya kupata chanjo wakati alipofika katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma kwa ajili ya zoezi la kutoa vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito na watoto walio chini ya mwaka mmoja.

Waziri Ummy Mwalimu akimpongeza baba aliyeleta mtoto kliniki kwa ajili ya kupata chanjo wakati alipofika katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma kwa ajili ya zoezi la kutoa vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito na watoto walio chini ya mwaka mmoja.Picha mbalimbali zikimuonesha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akigawa vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito, wakina baba na wakina mama walioleta watoto kliniki na katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma.

Waziri Ummy akiwa na baadhi ya akinamama waliopewa vyandarua baada ya kufika kliniki katika kituo cha afya cha Makole Jijini Dodoma wakati Waziri alipofika na kugawa vyandarua hivyo.


Na WAMJW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amelipongeza Jiji la Dodoma kwa jitihada kubwa zilizofanyika kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Waziri Ummy ametoa pongezi hizo wakati alipokua anagawa vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito na wenye watoto wadogo katika Kituo cha Afya cha Makole Jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema Jiji la Dodoma limetokomeza Malaria kutoka Asilimia 1 mpaka asilimia 0.6 ikiwa mafanikio makubwa, ambapo amesema katika kipindi cha miaka mitatu nchi nzima ugonjwa wa Malaria umeweza kupungua kutoka asilimia 14 mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018.

“Toka Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli iingie madarakani tumeweza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza Malaria nchini, katika kipindi kifupi cha miaka mitatu tumeweza kupunguza Malaria zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 14 mwaka mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018”. Amesema Waziri Ummy.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy amewataka wananchi kwa ujumla kutimiza wajibu wao ili kutokomeza Malaria kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema “Ziro Malaria inaanza na mimi”, hivyo amewataka wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao na kufanyiwa vipimo vyote kikiwemo kipimo cha Malaria.

Waziri Ummy amebainisha kuwa Tanzania bado haijafanya vizuri katika takwimu za akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ambapo katika akinamama wajawazito 100 ni akinamama 29 ndiyo wanaohudhuria kiliniki mara nne katika kipindi cha ujauzito.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mratibu wa Malaria wa mkoa, Dkt. Francis Bujiku amesema mafanikio ya kutokomeza Malaria katika jiji la Dodoma yamekuja baada ya utekelezaji wa afua mbalimbali za Malaria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tiba sahihi za Malaria zinatolewa katika vituo vyote vya afya, elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, pamoja na mkoa kufanikiwa kuangamiza viluilui wa mbu kwa kunyunyizia dawa kwenye mazalia yao.

Dkt. Bujiku amesema mwaka 2015 mkoa uliendesha zoezi la ugawaji vyandarua vyenye dawa kwenye ngazi ya kaya, takribani vyandarua milioni moja na laki tano viligawiwa kwa wananchi, vile vile akina mama wajawazito waliofika kliniki kwenye hudhurio la kwanza la ujauzito na watoto chini ya mwaka mmoja waliofika kupata chanjo ya surua walipewa vyandarua hivyo.

MWISHOJumanne, 23 Aprili 2019

SERIKALI YA CHINA YAAHIDI KUCHANGIA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

- Hakuna maoni

Mratibu wa ushirikiano wa Tanzania na China kwenye eneo la sekta ya afya Dkt. Ligile Vumilia akiongea mbele ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya wizara ya afya mapema leo.

Wajumbe wa kikao cha menejimenti ya wizara ya afya na wageni kutoka jimbo la Shadong nchini China wakiwa katika majadiliano ya mkakati wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizo.

Ujumbe kutoka jimbo la Shadong nchini China wakiwa katika kikao cha Menejimenti ya Wizara ya Afya chini ya Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula (hayupo pichani) wakati walipotembelea ofisi za wizara Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula akipokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa wajumbe kutoka jimbo la Shadong nchini China. Kulia ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bi. Deodatha Makani na kulia mwisho ni Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Grace Maghembe.

Katinu Mkuu wa Wizara ya Afya, ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakurugenzi na wajumbe kutoka jimbo la Shadong nchini China.

Na WAJMW-Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula leo amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe kutoka jimbo la Shadong la nchini China katika ofisi za Wizara zilizoko Mtumba nje kidogo ya jiji la Dodoma.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mbele ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti yalilenga kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China, Dkt. Chaula amesema wamekubaliana kushirikiana katika kubadilishana uzoefu na kuzalisha wataalamu wa afya waliobobea katika sekta mbalimbali.

“Kimsingi tumekubaliana na wajumbe hawa toka jimbo la Shadong lililopo China kuendelea kushirikiana katika kuboresha sekta ya afya nchini na kwa kuanza tumesaini makubaliano ya kusomesha Watanzania madaktari bingwa kwenda kusoma kozi mbalimbali kwa muda mrefu na muda mfupi”. Amesema Dkt. Chaula.

Dkt. Chaula amesema lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha Tanzania inapata wataalamu wa afya wabobezi watakaosaidia katika kuboresha huduma za kibingwa nchini mara baada ya kusoma kozi mbalimbali za kada ya afya chini China.

Nae Dkt. Ligile Vumilia ambaye ni mratibu wa ushirikiano wa Tanzania na China kwenye eneo la Sekta afya ambayo chini ya idara ya tiba amesema jimbo la Shadong limekua likileta wataalamu chini katika sekta ya afya kuanzia miaka ya 1960 na wamekua wakihudumu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za mikoa ya Tabora, Dodoma na Mara.

Dkt. Vumilia amesema timu iliyokuja ni ya viongozi ambayo itasaidia kuendeleza uhusiano kwa kuleta vifaa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya JKCI, kuleta madaktari wanaotoka China kwa ajili ya kutoa huduma nchini na pia kutoa fursa kwa madaktari bingwa 50 nchini kwenda kusoma China na kuongeza ujuzi zaidi.

Aidha, Dkt. Vumulia amesema ujumbe huo utasaidia kuleta vifaa tiba ambavyo vitasaidia katika kutibu magonjwa ya moyo nchini, pia ugeni huo utasaidia kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano katika Mji wa Serikali eneo la Wizara ya Afya  utakaoitwa Shadong ambao utatumika katika masuala mbalimbali ya elimu ya afya (tiba mtandao) ambapo Katibu Mkuu na uongozi watakua na uwezo wa kuwasiliana na madaktari kutoka Hospitali mbalimbali za Rufaa za mikoa na Kanda pasipo wao kufunga safari.

MWISHOAlhamisi, 18 Aprili 2019

WAZIRI UMMY ATEMBELEWA NA BALOZI WA NORWAY JIJINI DODOMA

- Hakuna maoniNa WAJMW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Bi. Elisabeth Jacobsen katika ofisi za Wizara zilizopo jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo yaliyolenga uboreshaji wa sekta ya afya nchini, Balozi Elisabeth amesema Serikali ya Norway itaendelea kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya afya hasa katika kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI na ukosefu wa lishe bora.

Bi. Elisabeth amesema Serikali ya Norway itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya kupitia Shirika la GAVI ambalo linajihusisha na ununuaji na usambazaji wa chanjo kwa nchi wanachama wa shirika hilo.

Aidha, Balozi huyo amesema kupitia mfuko wa Global Fund utawezesha Serikali  kukabiliana na magonjwa ya Malaria, TB na UKIMWI na hivyo kuwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazofikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyoanzishwa na Umoja Mataifa.

Kwa upande wake Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Norway kupitia Balozi huyo na Mifuko wa GAV, GF na GFF ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kwa watoto kupata chanjo hadi kufikia asilimia 98 nchini. Pia Waziri huyo ameushukuru mfuko wa Global Fund kwa kusaidia kusambaza dawa za kufumbaza Virusi kwa UKIMWI(ARV) na kuwafikia watumiaji Milioni 1.1 mwaka 2018 kutoka watumiaji 965,000 mwaka 2017.

Lakini pia Waziri Ummy ameishukuru Global Fund kwa kuwezesha kuboresha huduma za upatikanaji wa huduma za mama na mtoto nchini na kuepusha vifo vinavyoweza kutokea kwa sababu ya uzazi .

Pamoja na hayo, Waziri Ummy amemuomba Balozi huyo kuisadia Serikali katika harakati za kuwawezesha wanawake kupambana na umasikini kwa kutoa mikopo kwenye vikundi vyao ili waweze kujihushisha na shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wa lishe, Waziri Ummy amesema Serikali imeshaanza uhamasishaji wa Lishe Bora kupitia taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwa kutoa elimu ya lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano ili kukabiliana na udumavu ambao kwa kiasi kikubwa umeathiri ukuaji wa watoto katika baadhi ya mikoa nchini.

Jumatatu, 15 Aprili 2019

VIONGOZI WA DINI NA WAGANGA WA TIBA ASILI NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUTOKOMEZA TB NCHINI

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Wadau wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi akieleza jambo kuhusu mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini baada yakupewa fursa ya Kumkaribisha mgeni rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha) katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya UKIMWI na Madwa ya Kulevya, Mhe. Oscar Mukasa akisisitiza jambo mbele ya Wadau wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu nchini (Hawapo kwenye picha) katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini.

Meneja Mpango wa Taifa wa kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma Beatrice Mutayoba akielezea jambo mbele ya Mgeni rasmi Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha) katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akibadilishana mawazo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambipamoja na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa Wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Baadhi ya Wadau wa masuala ya Kifua Kikuu wakifuatilia neno kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo kwenye picha) katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa Wadau wenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa huo nchini.
Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Wadau wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu katika ufunguzi wa Mkutano wakwanza wa Wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa huo nchini.


VIONGOZI WA DINI NA WAGANGA WA TIBA ASILI NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUTOKOMEZA TB NCHINI

Na WAMJW – DSM

Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu  amesema kuwa viongozi wa madhehebu ya dini na Waganga wa tiba asili ni nguzo muhimu sana katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu(TB) nchini.

Ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wenye lengo la ushirikiano katika kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini uliofanyika Jijini Dar es salaam

Waziri Ummy amesema kuwa Waganga wa Jadi na Viongozi wa Dini ni Wadau muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB, huku akidai kutokana na utafiti uliofanywa 2018 na Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma unaonesha kuwa waganga wa jadi wamekuwa wahanga wakubwa wa  ugonjwa wa kifua kikuu.

Aliendelea kusema kuwa, viongozi wa dini ni kundi lingine muhimu  katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini, hii ni kutokana na idadi kubwa ya waumini wanaowaamini katika kufikisha ujumbe.

“Waganga wa jadi, ni wadau muhimu sana katika mapambano ya kifua kikuu, utafiti wa 2018 uliofanywa na mpango wa taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma unaonesha kuwa Waganga wa jadi na wenyewe wamekuwa wahanga wa ugonjwa wa kifua kikuu, na viongozi wa dini tunawahitaji wanaposimama katika makanisa na katika misikiti yetu ili wawe wanawakumbusha waumini juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu” alisema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa 2017, Tanzania iligundua na kuwapatia matibabu takribani wagonjwa 75,000 ikiwa ni sawa na 44% tu ya wagonjwa wanaokadiriwa kuugua TB, hii ina maana  ya kuwa wagojwa 85,000 (56%) hawagunduliwi na hivyo kukosa matibabu kila mwaka nchini.

Pia, Waziri Ummy amesema kuwa TB huathiri takriban watu milioni 10.4 duniani kila mwaka na 25% ya wagonjwa wanatoka barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi 13 barani Afrika zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa TB na inakadiriwa kuwa na  wagonjwa wapya wa TB 154,000 kila mwaka.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imeendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo katika vituo vya kutolea huduma vya serikali na binafsi, hali iliyoleta mafanikio ikiwamo kuvuka malengo ya mwaka 2018 ambapo tuliwafikia wagonjwa 75,845 ikiwa ni sawa ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka 2015.

Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammad Bakari Kambi amesema kuwa Tanzania ina wastani wa jumla ya Wagonjwa 154,000 ambao wanatakiwa  kuibuliwa na kuanzishiwa matibabu, licha ya changamoto ya kutowafikia wote ametoa wito juu ya umuhimu wa ushirikishwaji wa watu na taasisi mbali mbali ili kurahisisha mapambano haya dhidi ya ugonjwa wa TB.

Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt.Beatrice Mutayoba amesema kuwa kila mwaka watoto 1,000,000 wanaugua kifua kikuu Duniani, huku watoto 250,000 wanafariki.

“Kwa bahati mbaya Kifua kikuu hakijaacha watoto, kila mwaka watoto 1,000,000 wanaugua kifua kikuu Duniani, huku watoto 250,000 wanafariki, huku nchini Tanzania 10% ya watu 68,000 wanaogundukila kuwa na Kifua  kikuu huwa ni watoto” alisema Beatrice Mutayoba

MWISHO

Jumamosi, 13 Aprili 2019

RAIS MAGUFULI AZINDUA MJI WA SERIKALI JIJINI DODOMA

- Hakuna maoni


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifungua jiwe la msingi ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa ofisi za wizara mbalimbali ambazo zimejengwa katika kata ya Ntumba nje kidogo ya Jiji la Dodoma.

Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (Kushoto) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (Kulia) wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la wizara ya Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kama kiashirio cha uzinduzi wa Mji wa Serikali ambapo Majengo ya Wizara zote yamejengwa huko.

Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (Kushoto) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (Kulia) na viongzi wengine waliokaa, wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri na Manaibu Waziri (Waliosimama) wakati wa uzinduzi wa Mji Mpya wa Serikali uliopo kata ya Ntumba Jijini Dodoma.

Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (Kushoto) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (Kulia) na viongozi wengine waliokaa, wakiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Mji Mpya wa Seriakali Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akiongea na Watumishi wa Wizara hiyo wakati walipotembelea jengo jipya la Wizara lililopo kata ya Ntumba Jijini Dodoma mara baada ya Rais Magufuli kuzindua mji wa Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali za Afya, Wakurugenzi wa Vitengo mbalimbali pamoja Watumishi wa Wizara ya Afya wakati walipotembelea Jengo la ofisi za Wizara hiyo.

Alhamisi, 11 Aprili 2019

SERIKALI YATOA TAHADHARI KUHUSU UGONJWA WA DENGUE NCHINI

- Hakuna maoni
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akitoa tahadhari kuhusu kuzuka kwa ugonjwa wa Dengue nchini. Kushoto ni Mganga mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Kambi
Na WAJMW-DODOMA

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini ambao umebainika katika mikoa ya Dar Es Salaam na Tanga.

Akitoa tahadhari hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema hadi kufikia April 2 2019 kati ya watu 470 waliopimwa, wagonjwa 307 wamethibitishhwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Dengue, na kati ya hao 252 ni kutoka Dar Es Salaam na 55 ni kutoka Tanga.

Dkt. Ndugulile amesema ugonjwa wa homa ya Dengue unasababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya “Aedes” ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung’aa.

Aidha, Dkt. Ndugulile  ametaja dalili za ugonjwa huu kuwa ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambikizwa  virusi vya ugonjwa huu.

Naibu Waziri huyo amewataka wananchi kuwa makini pindi wapatapo homa na wahakikishe wanakwenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kupimwa na kupatiwa tiba sahihi.

Dkt. Ndugulile amewataka wananchi kusafisha mazingira na kufukia madimbwi ambayo mbu aina ya Aedes hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba, kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalia ya mbu kama vile vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari. Pia wanatakiwa kufyeka vichaka na kusafisha gata za mapaa ya nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.

Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile amesema mbu hawa huwa na tabia ya kuuma Zaidi wakati wa mchana hasa wakati wa asubuhi jua linapochomoza na jioni jua linapozama na hivyo wananchi wanatakiwa kujihadhari.

Jumatano, 10 Aprili 2019

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA NJOMBE KUANZA KUTOA HUDUMA MWEZI JULAI, 2019.

- Hakuna maoni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akikagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akikagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wengine mara baada ya ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Njombe.


Picha ya Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe. 

NA WAMJW - NJOMBE

Huduma za matibabu katika Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe zinatarajiwa kuanza rasmi Mwezi Julai, 2019 huku kwa sasa ujenzi wa hospitali hiyo ukiwa umefikia asilimia 96.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba Mkoani Njombe kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali hiyo.

“Mheshimiwa Rais Tumejipanga katika kipindi hiki cha miezi miwili tuweke vifaa na vifaa tiba, kukamilisha usajili wa hospitali pamoja na kusimika mifumo ya kutolea taarifa”, amesema Waziri Ummy na kuendelea  kwa kusema kuwa Wizara yake tayari inao watumishi 119 ambao watapelekwa katika hospitali hiyo ili kutoa huduma kwa wananchi.

Waziri Ummy  amemshukuru Mhe. Rais kwa kuipatia Wizara yake Shilingi Bilioni 3.5 ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za wodi za kulaza wagonjwa wa ndani, upasuaji na mifupa katika hospitali hiyo ujenzi ambao utafanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Wizara inao mpango wa kuhakikisha Hospitali za Wilaya zinakuwa na madaktari bingwa wa kada muhimu za kipaumbele zikiwemo Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, watoto, mama na uzazi, upasuaji wa jumla, upasuaji wa mifupa na huduma za dharura kama ajali pamoja na daktari bingwa wa mionzi.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu umetuwezesha sasa tunasomesha madaktari 311 katika vyuo mbalimbali na unatupatia Shilingi Bilioni 2.5 kila mwaka kwa ajili ya ufadhili.” Amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa madaktari wanaosoma kwa ufadhili wamepewa mikataba pindi wakimaliza masomo warudi kufanya kazi katika vituo na hospitali za Serikali angalau kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu kabla ya kwenda sehemu nyingine.

Baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali hiyo, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli  amekagua jengo hilo ambapo ameonyeshwa kuridhika na ujenzi na kuipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.

Mwisho

Jumanne, 9 Aprili 2019

DAWA MUHIMU ZAIDI YA 300 ZINAPATIKA KATIKA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akikagua dawa zilizopo katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.


 Ukaguzi wa hali ya utoaji huduma ukiendelea katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe, Kutoka upande wa kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula na mwisho ni Mganga Mfawidhi Hospitali hiyo Dkt Winfred Kyambile.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula mapema jana walipotembelea Hospitali Teule ya Mkoa wa Njombe kujionea hali ya utoaji wa huduma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa amemebeba mtoto mchanga kwa furaha kwenye wodi ya mama na mtoto katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Picha ya pamoja Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (aliye katikati mstari wa chini), Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula (wa pili kushoto mstari wa chini) na watendaji kutoka Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.


Na WAMJW - NJOMBE

Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuvuka kiwango cha upatikanaji wa dawa muhimu kwa binadamu kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ngazi ya Hospitali ya Wilaya kwa kuwa na idadi kubwa ya dawa muhimu zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kujioinea hali ya utoaji wa huduma.

Waziri Ummy Mwalimu aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula pamoja na watendaji walio chini ya Wizara yake, amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa wananchi huku ikipitiliza kiwango kilichowekwa na WHO kwa kuwa na dawa muhimu 312 huku kigezo kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kikiwa ni dawa 30.

“Tuna mfumo wa ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya mpaka hospitali unaotuwezesha Serikali kutambua mahitaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma” amesema Waziri Ummy wakati akifafanua namna ya Serikali ilivyojipanga kupata takwimu sahihi za dawa.

Waziri Ummy amesema kuwa zipo propaganda zinazoendeshwa na watu wenye ushawishi ambao wamekuwa wakiwahadaa wananchi kwa kusema kuwa dawa hakuna ili hali dawa zipo na zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma.

“Ni lazima tumtendee haki Rais wetu DKt. John Pombe Magufuli, amefanya makubwa kwenye Sekta ya Afya kwa kuboresha upatikanaji wa Dawa, tunaposema tumeongeza upatikanaji wa dawa maana yake dawa zinapatikana kwa urahisi hata kwenye vituo binafsi” amesema Waziri Ummy,

Waziri Ummy amezitaja dawa zenye kipaumbele kikubwa zikiwemo Dawa za kudhibiti maambukizi ya bakteria (Antibiotics), Dawa za kudhibiti Malaria, Dawa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dawa za uzazi salama pamoja na Dawa za maumivu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Ofisi yake kupitia Waziri wa Afya wako mbioni kuwasilisha muswada wa Bima ya Afya ambao utawawezesha wananchi wote sasa kuwa na bima ya afya.

Aidha, Dkt. Chaula amewataka watumishi katika Hospitali hiyo kuwahamasisha zaidi wagonjwa kujiunga na huduma za bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapougua.

“Niwaombe watendaji wote hapa kuwasisiza wagonjwa wanaofika hapa kupata matibabu kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya” Alisema Dkt. Chaula.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Winfred Kyambile amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma imeimarika kutokana na mapato kuongezeka hivyo kuiwezesha Hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dkt. Kyambile amesema kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa  imesaidia kuongezeka kwa mapato hospitalini hapo, amesema kuwa hapo awali mapato ya hospitali hiyo kwa mwezi yalikuwa Shilingi Milioni 12 huku sasa mapato hufikia Shilingi milioni 90 mpaka 100, fedha ambazo amesema wanazitumia kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.

Mwisho

Jumatatu, 8 Aprili 2019

WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI WATAKIWA KUTOJIHUSISHA NA IMANI ZA KISHIRIKINA KATIKA HUDUMA ZAO

- Hakuna maoni

Picha mbalimbali zikionesha Maafisa kutoka Baraza la  Tiba Asili na Tiba Mbadala wakiongozwa na Msajili Dkt. Ruth Suza wakitoa elimu kwa Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.


WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI WATAKIWA KUTOJIHUSISHA NA IMANI ZA KISHIRIKINA KATIKA HUDUMA ZAO

Na WAMJW-MWANZA

Watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala wametakiwa kutojihusisha na imani za kishirikina ikiwa ni pamoja na uchawi katika kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo.

Hayo yamesemwa na Msajili kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Ruth Suza wakati akiongea na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wa mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita waliojitokeza katika kikao kazi kilichohusisha wataalam kutoka Baraza hilo lililo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Dkt. Ruth amesema kuna baadhi ya Watoa huduma wa tiba za asili wanaojihusisha na mambo ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kupiga ramli chonganishi, kuhitaji viungo vya binadamu kwa ajili ya kutengeneza dawa na kuwa na nyara za serikali ambazo kiuhalisia hazitakiwi katika matibabu hayo.

“Ninawataka waganga wote kutojihusisha na tiba za kishirikina zinazoenda sambamba na uchawi, kupiga ramli chonganishi na kutumia nyara ambazo hazina vibali kama mikia na ngozi za wanyama wa porini. Endapo mganga yeyote akikutwa na kasoro hizi baraza halitasita kumfutia usajili mhusika na atashitakiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na Serikali”. Amesema Dkt. Ruth.

Aidha, Dkt. Ruth amewataka waganga hao kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kupata vibali vya vitendea kazi vyao hasa nyara za Serikali zinazotokana na wanyama, nyoka, ndege na wadudu wa porini, ambapo vibali hivyo vinatolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dkt. Ruth pia amewataka waganga hao kutunza siri za wagonjwa wanaowatibu ikiwa ni haki ya msingi ya mgonjwa kama hospitali zinavyofanya. Vile vile Dkt. Ruth amewataka waganga wa jadi kuwapeleka Hospitalini haraka wagonjwa walioshindwa kupata ahueni kwa dawa za jadi ili kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.

Kwa upande wao Waganga wa mkoa hiyo wametoa kero zao ikiwa ni pamoja na  kukamatwa mara kwa mara na vyombo vya usalama wanapokua katika kazi zao, dawa zao kutosajiliwa kwa wakati na kupata leseni kutoka Baraza. Hivyo kulitaka baraza hilo kuhakikisha Serikali inawatambua kwa kuwapa vibali na kusajili dawa zao ambazo kwa kiasi kikubwa zimekua tegemeo kwa wananchi wengi wenye matatizo mbalimbali.

Baraza la tiba asili na tiba mbadala limeendelea kufanya zoezi la ukaguzi nchi nzima kwa ajili ya kuangalia usajili na vibali kwa waganga wanaotoa huduma. Ambapo zoezi hili limeanzia mkoa wa Dar Es Salaam, Kagera, Geita na Mwanza na kufuatiwa na mikoa mingine.