Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akikagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
akikagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole
Sendeka, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wengine mara
baada ya ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Njombe.
Picha ya Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
NA WAMJW - NJOMBE
Huduma za matibabu katika Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe zinatarajiwa kuanza rasmi Mwezi Julai, 2019 huku kwa sasa ujenzi wa hospitali hiyo ukiwa umefikia asilimia 96.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba Mkoani Njombe kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali hiyo.
“Mheshimiwa Rais Tumejipanga katika kipindi hiki cha miezi miwili tuweke vifaa na vifaa tiba, kukamilisha usajili wa hospitali pamoja na kusimika mifumo ya kutolea taarifa”, amesema Waziri Ummy na kuendelea kwa kusema kuwa Wizara yake tayari inao watumishi 119 ambao watapelekwa katika hospitali hiyo ili kutoa huduma kwa wananchi.
Waziri Ummy amemshukuru Mhe. Rais kwa kuipatia Wizara yake Shilingi Bilioni 3.5 ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za wodi za kulaza wagonjwa wa ndani, upasuaji na mifupa katika hospitali hiyo ujenzi ambao utafanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Wizara inao mpango wa kuhakikisha Hospitali za Wilaya zinakuwa na madaktari bingwa wa kada muhimu za kipaumbele zikiwemo Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, watoto, mama na uzazi, upasuaji wa jumla, upasuaji wa mifupa na huduma za dharura kama ajali pamoja na daktari bingwa wa mionzi.
“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu umetuwezesha sasa tunasomesha madaktari 311 katika vyuo mbalimbali na unatupatia Shilingi Bilioni 2.5 kila mwaka kwa ajili ya ufadhili.” Amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa madaktari wanaosoma kwa ufadhili wamepewa mikataba pindi wakimaliza masomo warudi kufanya kazi katika vituo na hospitali za Serikali angalau kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu kabla ya kwenda sehemu nyingine.
Baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali hiyo, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekagua jengo hilo ambapo ameonyeshwa kuridhika na ujenzi na kuipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Mwisho
0 on: "HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA NJOMBE KUANZA KUTOA HUDUMA MWEZI JULAI, 2019."