Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumanne, 10 Mei 2022

HATUWEZI KUWA NA WATUMISHI BORA WA AFYA KWA KUVUMILIA VYUO VINAVYOFANYA UDANGANYIFU - PROF. MAKUBI

Wakuu wa vyuo vya Afya wakifuatilia neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya akieleza jambo wakati akifungua Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya, Jijini Dodoma

Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer akieleza jambo mbele ya mgeni rasmi (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa NACTVET Bw. Twaha Twaha akitoa salamu kutoka taasisi yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya Afya wakifuatilia neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya Afya wakifuatilia neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya uliofanyika Jijini Dodoma.


Na WAF - DOM 

KATIBU MKUU Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kuwa, Serikali haitaendelea kuvumilia tabia ya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya vyuo vya afya nchini, kwani tabia hizo hupelekea kupata Watumishi wasio na ubora na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi. 

Prof. Makubi amesema hayo leo Mei 10, 2022 wakati akifungua Mkutano wa Wakuu wa vyuo vya afya wenye kauli mbiu ya  "Huduma bora za Afya ni matokeo ya uwepo wa vyuo bora nchini," uliofanyika Jijini Dodoma. 

"Hatuwezi kuwa na Watumishi bora wa Afya kwa kuvumilia baadhi ya vyuo vinavyoendekeza tabia ya udanganyifu kwenye uendeshaji wa mafunzo, hali hii inarudisha nyuma juhudi za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi." Amesema Prof. Makubi. 

Amesema, hali ya udanganyifu ni kinyume cha Sheria, maadili, utaratibu na mbaya zaidi udanganyifu huu umeendelea hadi kwenye mazoezi ya mitihani ya ndani na ile ya Kitaifa kwa kuwahusisha baadhi  ya wanafunzi na walimu katika maeneo yao, hii haikubaliki. 

Sambamba na hilo, Prof. Makubi amewaelekeza Wasajili wa Mabaraza ya kitaaluma kuchukua hatua hatua stahiki kwa wakufunzi wanaoshiriki kwenye udanganyifu kwa kuwafutia leseni na hatua nyingine kwa mujibu wa Sheria za nchi. 

Aliendelea kusisitiza kuwa, Wizara haitasita kuchukua hatua kali kwa chuo chochote kitachoenda kinyume na utaratibu wa uendeshaji wa mafunzo na upimaji wa wanafunzi, ikiwa na sehemu ya uboreshaji wa utoaji huduma. 

Katika kulinda ubora wa Wahitimu, Prof. Makubi ameelekeza kusitisha usajili kwa vyuo ambavyo havijakidhi utaratibu kama vile kutokuwa na miundombinu ya kufundishia ikiwemo hospitali na maabara za mafunzo kwa vitendo,  msongamano wa vyuo vingi katika eneo moja hali inayopelekea wanafunzi kukosa eneo la kufanyia mafunzo kwa vitendo. 

Aidha, amewapongeza Wakuu wa vyuo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya licha mazingira magumu yanayokutana nayo katika maeneo yao ya utendaji, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika utatuzi wa changamoto hizo ili kuboresha huduma kwa wananchi. 

Mbali na hayo, amewataka Wakuu wa vyuo kuwa Wazalendo na kuzingatia misingi ya uongozi bora kwa kushirikisha viongozi wengine katika ngazi ya maamuzi, ikiwemo katika matumizi ya fedha ili kuondoa misuguano inayoweza kuepukika. 

Hata hivyo,  ametoa wito kwa Wakuu wa vyuo kuwa wabunifu katika utendaji wao, ikiwemo kushirikiana na Wadau mbalimbali wanaopatikana katika maeneo yao jambo litakalosaidia kupunguza changamoto katika vyuo vyao. 

Naye,Mkurugenzi wa Mafunzo na rasilimali watu Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer amemshukuru Katibu Mkuu kwa kuendelea kusaidia vyuo vya mafunzo, na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyotoa ili kufikia lengo la Serikali la kuboresha huduma kwa wananchi. 

Mwisho.


Ijumaa, 6 Mei 2022

WARATIBU WA TIBA ASILI WAELEKEZWA KUKEMEA RAMLI CHONGANISHI.

 

KAIMU Mkuregenzi Msaidizi anayeshughulikia Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya Bi. Lucy Mziray akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Waratibu wa tiba asili wa baadhi ya Halmashauri nchini, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza.

Kaimu Msajili wa Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala Bw. Ndehani Msigwa akieleza majukumu ya Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala katika ufunguzi wa mafunzo ya Waratibu wa tiba asili wa baadhi ya Halmashauri nchini yaliyofanyika Jijini Mwanza.

Baadhi ya Waratibu wa Tiba asili walioshiriki mafunzo ya huduma za tiba asili yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo juu ya shughuli mbalimbali za tiba asili nchini, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza.

Baadhi ya Waratibu wa Tiba asili walioshiriki mafunzo ya huduma za tiba asili yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo juu ya shughuli mbalimbali za tiba asili nchini, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza.

Baadhi ya Waratibu wa Tiba asili wakiendelea na mafunzo ya huduma za tiba asili yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo juu ya shughuli mbalimbali za tiba asili nchini, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza.

Picha ya pamoja ya Waratibu wa tiba asili ngazi ya Halmashauri wakiwa pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Afya na Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala baada ya mafunzo ya huduma za tiba asili  yaliyofanyika Jijini Mwanza.



WARATIBU WA TIBA ASILI WAELEKEZWA KUKEMEA RAMLI CHONGANISHI. 

Na WAF - MWANZA. 

KAIMU Mkuregenzi Msaidizi anayeshughulikia Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya Bi. Lucy Mziray ametoa wito kwa Waratibu wa Tiba asili na Tiba mbadala ngazi ya Halmashauri kukemea ramli chonganishi zinazofanywa na baadhi ya Waganga wa tiba asili wasio waaminifu. 

Bi. Lucy ametoa wito huo leo Mei 6 katika ufunguzi wa mafunzo ya Waratibu wa tiba asili wa baadhi ya Halmashauri nchini, mafunzo yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo juu ya shughuli mbalimbali za tiba asili nchini, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza. 

Amesema, wapo baadhi ya Waganga wa tiba asili wanafanya ramli chonganishi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu, Sheria na miongozo ya Serikali, hali inayopelekea uminywaji wa haki na uvunjifu wa amani katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla. 

"Nitoe wito kwa Waratibu wote wa tiba asili na tiba mbadala nchini, kuhakikisha wanakemea ramli chonganishi zinazofanywa na baadhi ya Waganga, na hali hii hupelekea kutotenda haki na inaweza kupelekea uvunjifu wa amani katika ngazi zote ikiwemo ngazi ya familia na jamii." Amesema. 

Sambamba na hilo, amesema kuwa, kuanzia mwaka 2018 Kitengo cha Tiba Asili kwa kushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na baadhi ya vyuo vya kitaaluma imefanikiwa kuwapa mafunzo Waganga wa tiba asili 200 kuhusu miiko ,maadili na usafi katika kuandaa dawa za  asili. 

Aidha, ametoa rai kwa Waratibu wa Tiba asili wote waliohudhuria kupeleka ujuzi kwa kuwafundisha na kuwahamasisha waganga wa tiba asili na tiba mbadala juu ya ya sheria, miiko na maadili ya kazi wanazofanya katika jamii na uzingatiaji wa usafi na usalama katika utoaji wa huduma zao, ikiwa pamoja na uandaaji salama wa dawa za asili. 

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala Bw. Ndehani Msigwa amewapongeza Waratibu wa Tiba asili na Tiba mbadala kwa kuhudhuria mafunzo yenye lengo la kuchochea utoaji wa huduma bora na salama ili kuilinda Afya ya Watanzania. 

Aliendelea kwa kutoa wito kwa Waratibu wa Tiba asili kuhakikisha wanasajili Waganga wote katika maeneo yao na kusajili vituo vyao wanavyotolea huduma ili Watambulike na Wizara pamoja na Baraza linalowasimamia kwa mujibu wa Sheria na taratibu. 

"Bado tunao Wataalamu wengi kwenye maeneo yetu ambao hawajasajiliwa na kwa waliosajiliwa bado vituo vyao havijasajiliwa, hii ni changamoto kubwa ambayo naamini baada ya kutoka kwenye mafunzo haya tutakwenda kuitatua." Amesema Bw. Msigwa. 

Nae, Katibu wa Afya kutoka Balaza la Tiba asili na Tiba mbadala Bw. Patrick Seme amewataka Waratibu wa Tiba asili na Tiba mbadala ngazi ya Halmashauri kuratibu matangazo ya tiba asili kwenye vyombo vya habari, na kuchukua hatua kwa wanaotoa na wanaorusha matangazo hayo ambayo hayajapewa kibali na Wizara kupitia Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala kwani matangazo mengi hupotosha umma juu ya uwezo wa kutibu. 

"Mkakemee vitendo vibaya vinavyofanywa na baadhi ya Waganga wa Tiba Asili  ambavyo vinakiuka sheria ya Tiba Asili ya 2002 ikiwa ni pamoja na utoaji wa matangazo ya huduma za tiba asili ambayo hayajapekuliwa na kupewa kibali na Baraza la Tiba Asili na utoaji wa huduma za tiba asili bila kusajiliwa." Amesema. 

Mwisho.