Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Ijumaa, 17 Julai 2020

PROF. MCHEMBE AWATAKA WAFAMASIA KUSIMAMIA MAADILI

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiongea na wafamasia na wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya (hawapo pichani) wakati akifungua kikao kinachoendelea mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe akiwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa ununuzi Serikalini Prof. Geraldine wakifuatilia moja ya mada zilizokua zinawasilishwa katika kikao cha wadau wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.
Mfamasia Mkuu Ndg. Daud Msasi akitolea ufafanuzi moja ya hoja wakati akiwasilisha mada katika kikao cha wafamasia na wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kinachoendelea Mkoani Morogoro.

Picha za Wafamasia na Wadau mbalimbali waliohudhuria kikao cha Wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kutoka Sekta mbalimbali za Serikali na Binafsi waliokutana Mkoani Morogoro.


Na WAJMW-MOROGORO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewataka Wafamasia nchini kote kuzingatia maadili na kutumia taaluma waliyonayo ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Prof. Mchembe amesema hayo wakati akifungua semina inayojumuisha Wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kutoka Sekta mbalimbali za Serikali na Binafsi waliokutana Mkoani Morogoro.

“Ninawataka Wafamasia wote mbadilike kulingana na mazingira yaliyopo, hivi sasa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati, hii inamaana mboreshe utaalamu wenu ili kukidhi mahitaji ya nchi. Corona imekuja na faida kubwa, imetufanya sasa tunaweza kutengeneza Vitakasa mikono vyetu (Hand Sanitizer) na barakoa jambo ambalo hapo awali halikuwepo”. Amesema Katibu Mkuu Prof. Mchembe.

Prof. Mchembe amesisitiza kuboreshwa kwa huduma za dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya zikiwemo Zahanati na vituo vya afya vya umma kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana ili mwananchi anapofika kupata huduma asikose dawa na kulazimika kwenda kununua kwenye maduka ya watu binafsi.

Aidha, Prof. Mchembe amewataka wataalamu hao kutochagua vituo vya kazi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa wanadidimiza taaluma yao kwa kufanya kazi maeneo ambayo hayana vifaa.
“Rais wetu ana nia njema katika kuboresha huduma za afya nchini, utakuta Hospitali fulani ina vifaa vizuri sana vya kufanyia kazi lakini haina wataalam wa kuvitumia”. Amesema Katibu Mkuu huyo.

Katika kutatua changamoto hizo Katibu Mkuu Mchembe amemuagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg. Daud Msasi kuweka muongozo mzuri katika kuwapangia vituo vya kazi Wafamasia na wataalam wengine ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya popote walipo.

Pia Prof. Mchembe amesisitiza matumizi ya data katika kutoa huduma na kutunza kumbukumbu kupitia mifumo ya GOTHOMIS na mingineyo ili kurahisisha utoaji wa huduma na kutunza rekodi za wagonjwa na pia kuweka mnyororo wa huduma zote za Hospitali kuwa katika hali nzuri.

Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg. Daud Msasi amewataka wadau waliohudhuria katika kikao hicho kuhakikisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia mambo ya msingi ambayo ni Pamoja na uzuiaji wa kukua kwa madeni yasiyolipika, nyaraka za mali za serikali zitunzwe vizuri, matumizi ya miongozo ili kuepika gharama zisizo za lazima, uwepo wa maduka ya dawa yanayojiendesha bila kuathiri huduma nyingine Pamoja na kuweka taarifa zilizo sahihi.

MWISHO



Ijumaa, 10 Julai 2020

SERIKALI YAAGIZA KUBORESHWA KWA VIWANGO VYA HUDUMA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA DODOMA

- Hakuna maoni


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akikagua wodi ya wanaume iliyoko hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma.Kushoto ni Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo Stanley Mahumbo.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akikagua duka la dawa la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali akitazama moja ya faili la   mgonjwa aliolazwa kwenye wodi hiyo ambapo alibaini mapungufu.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiangalia moja ya mashine zilizopo kwenye maabara ya hospitali hiyo.

Na. WAMJW-Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameuagiza Uongozi wa  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuboresha huduma za tiba kwa wananchi wanaofika kupata huduma za afya katika hospitali hiyo.

Prof. Makubi ametoa maagizo hayo kufuatia ziara ya kushtukiza aliyoifanya kwenye Hospitali hiyo na kushuhudia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wagonjwa kuchelewa kupewa huduma, Madaktari bingwa kutowaona wagonjwa kwa wakati na huduma za vipimo kuchelewa.

“Yapo mazuri tumeona mnayofanya kwa wananchi na tunawapongeza, ila lazima kuangalia upande wa pili ambao wananchi wanayataka, kwa yale mapungufu tuliyoyaona tungependa kuona yanaboreshwa haraka ili hospitali hii iwe ya mfano kwa hospitali zote za rufaa za mikoa kwa kutoa huduma zilizo bora”.

Prof. Makubi amesema hospitali hiyo inatakiwa kuonesha mfano kuanzia utoaji wa huduma bora kwa mteja pamoja, kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri huduma, upatikanaji wa wauguzi na mabingwa wanapohitajika na usafi wa wodi kwani ndiyo chachu ya wananchi wengi kufika hapo na kupata huduma kabla hawajapewa rufaa ya kwenda Hospitali kubwa kama Benjamin Mkapa.

Aidha, Mganga Mkuu huyo ameutaka uongozi na watumishi wa hospitali hiyo kutambua majukumu yao  kwa kuonesha kuwajali wananchi  wote na kuwataka kuweka utaratibu usio na usumbufu kwa wagonjwa na kupatiwa huduma kwa wakati.

Prof. Makubi alionyesha kusikitishwa alipokuta wodini  baadhi ya wagonjwa wamelazwa na hawajaonwa na Mabingwa kwa zaidi ya siku tatu, wauguzi wakiwa hawajaambatana na madaktari katika kuzungukia wagonjwa huku madaktari wa vitendo (interns)  wakifanya “procedures” peke yao bila uangalizi na baadhi ya  wagonjwa wengine wakiwa wamelazwa chini wakati vitanda viko wazi pamoja na mazingira ya wodi hayakuwa ya kuridhisha na kukosekana kwa mpangilio wa vifaa (5S)

 “Lazima watumishi mjitambue mko wapi kwani awamu hii ni ya kuwajali wanyonge na kufanya kazi  kwa bidii ndio kanuni ya awamu hii hapa kazi tu”. Alisisitiza Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameelekeza madaktari wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na wauguzi katika kuwahudumia wagonjwa katika wodi, kuleta mabadiliko kwa kutengeneza miongozo mbalimbali ya kusimamia huduma na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kila mwananchi anayefika hospitalini hapo ahudumiwe kwa wakati na huduma inayostahili.

Kwa upande mwingine Mganga Mkuu huyo wa Serikali ameitaka hospitali hiyo kuboresha idara ya huduma kwa wateja (Customer Care) kwani hakuna mgonjwa anayependa kuchelewa kupata huduma hivyo lazima kutoa huduma bora na zinazohitajika kwa wananchi wote.

Prof. Makubi ameelekeza Uongozi wa Hospitali kuhakikisha mashine za maabara ambazo zimeishiwa vitendanishi, zinaanza kufanya kazi haraka.

"Ni vizuri mkapunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo vya damu, X-ray, ultrasound, na Moyo na vipimo vingine".Alielekeza Prof. Abel Makubi.

Prof. Makubi aliagiza Hospitali zote nchini zifanyie kazi changamoto alizoziona hapo Dodoma, na akaagiza Idara ya ukaguzi wa huduma bora kutoka wizarani wafanye ufuatiliaji wa utoaji wa huduma mikoani,  wilayani na Vituo vya afya kila mwezi na kutoa taarifa kwake.

"KUTOA HUDUMA ZA AFYA ZA UHAKIKA NI JUKUMU LETU"-PROF. MAKUBI

- Hakuna maoni

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiongea na wataalam kutoka Wizara ya Afya na TAMISEMI wakati wa kujadili utoaji wa huduma bora za afya kwenye vituo vya afya,hospitali za halmashauri na rufaa zilizojengwa kukarabatiwa na Serikali
Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akiongea wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akiwasilisha mada wakati wa kikao baina ya Wizara ya Afya na TAMISEMI














Na. WAMJW-Dodoma

Serikali imefanikiwa kutimiza dhamira ya kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na uwiano wa kutosha katika utoaji huduma za afya pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya za uhakika na wakati.

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akifungua kikao kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI cha kujadili utoaji huduma bora za afya kwenye vituo vya afya, Hospitali za Halmashauri na Rufaa zilizojengwa na kukarabatiwa na serikali ya awamu ya tano.

“Sisi kama wataalam tunawajibu wa kuendeleza chachu ya maendeleo  yaliyofikiwa na kuhakikisha vituo hivi vinafunguliwa kwa kuzingatia utaratibu unaotakiwa na kuendelea kutoa huduma vikiwa na vifaa vyote muhimu na wataalam wenye weledi na stadi katika kupambana na magonjwa na kupunguza vifo vinavyozuilika”.Amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kufuatia sekta ya afya kuchukua jukumu la kufanya ukarabati wa ujenzi katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo iliweka kipaumbele kwenye vituo vya afya vya msingi ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga.

“Tumejenga hospitali mpya za wilaya 99, kutoka hospitali 70 za awamu ya kwanza zimekamilika na nyingi zimeanza kutoa huduma hata hivyo serikali imeongeza kujenga hospitali nyingine 29 na fedha zake zimetengwa tayari”. Ameongeza Prof. Makubi.

Awali akiongea kwa niaba ya Naibu katibu Mkuu wa Afya TAMISEMI, Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na ustawi wa jamii Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kuwa na muelekeo mzuri wa sekta ya afya hivyo ushirikiano wa pamoja kati ya Wizara hizo mbili ni muhimu katika kufanikisha na kusukuma mbele sekta hiyo nchini.

Naye Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema kuwa vituo vya afya 570 vilivyojengwa na kukarabatiwa na Serikali vimeweza kuboresha huduma za afya na kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga huku vikiwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kama upasuaji.

MWISHO

Alhamisi, 2 Julai 2020

WAZIRI UMMY ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA HOSPITALI YA KANDA MTWARA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa wakikagua ujenzi wa Hospitali mpya ya kanda ya kusini inayojengwa Mkoani Mtwara.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo kutoka kwa msanifu majengo anayesimamia mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini wakati alipotembelea Hospitali hiyo kuona hali ya ujenzi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Mbunge wa Mtwara vijijini Mhe. Hawa Ghasia wakitembelea ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini iliyopo Mtwara.


Sehemu ya jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mikoa ya kusini inayoendelea na ujenzi.

Na. WAJMW-Mtwara

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mikoa ya kusini iliyopo mkoani Mtwara na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

Waziri Ummy ameonekana kuridhidhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia asilimia 80 na inagharimu Shilingi Bilioni 15.8 mpaka kukamilika kwake.

"Kukamilika kwa Hospitali hii kutasaidia kupunguza rufaa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwenda kutafuta huduma za kibingwa Muhimbili, MOI au JKCI, huduma zote zitakua zinapatikana hapa". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuona huduma zinaanza kutolewa katika Hospitali hiyo kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwani ilikua ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipopita mwaka 2015 kuomba kura na Hospitali hiyo ipo kwenye utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

"Hatutaki watu wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla muende Dar Es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za CT-Scan, huduma za madaktari bingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, mishipa ya fahamu, Madaktari wa watoto na uzazi. Huduma zote hizi zitapatikana hapa mara baada ya ujenzi wa Hospitali hii kukamilika". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya sekta ya Afya mkoani Mtwara ni nzuri ambapo katika kipindi cha miaka mitano Hospitali mpya za Wilaya tatu zimejengwa ambazo ni Nanguluwe, Nanyamba pamoja na Masasi. Aidha, vituo vya Afya vinane vimejengwa katika Mkoa huo katika kipindi hicho na kufanya idadi kufikia vituo 23 kutoka 15 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani.