Picha za Wafamasia na Wadau mbalimbali waliohudhuria kikao cha Wadau wa mnyororo wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kutoka Sekta
mbalimbali za Serikali na Binafsi waliokutana Mkoani Morogoro.
Na WAJMW-MOROGORO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewataka Wafamasia nchini
kote kuzingatia maadili na kutumia taaluma waliyonayo ili kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Prof. Mchembe amesema hayo wakati akifungua
semina inayojumuisha Wadau wa mnyororo
wa ugavi na usambazaji wa bidhaa za afya kutoka Sekta mbalimbali za
Serikali na Binafsi waliokutana Mkoani Morogoro.
“Ninawataka Wafamasia wote mbadilike kulingana
na mazingira yaliyopo, hivi sasa nchi imeingia kwenye uchumi wa kati, hii
inamaana mboreshe utaalamu wenu ili kukidhi mahitaji ya nchi. Corona imekuja na
faida kubwa, imetufanya sasa tunaweza kutengeneza Vitakasa mikono vyetu (Hand
Sanitizer) na barakoa jambo ambalo hapo awali halikuwepo”. Amesema Katibu Mkuu
Prof. Mchembe.
Prof. Mchembe amesisitiza kuboreshwa kwa huduma
za dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya zikiwemo Zahanati na vituo vya
afya vya umma kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana ili mwananchi anapofika
kupata huduma asikose dawa na kulazimika kwenda kununua kwenye maduka ya watu
binafsi.
Aidha, Prof. Mchembe amewataka wataalamu hao
kutochagua vituo vya kazi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa wanadidimiza
taaluma yao kwa kufanya kazi maeneo ambayo hayana vifaa.
“Rais wetu ana nia njema katika kuboresha
huduma za afya nchini, utakuta Hospitali fulani ina vifaa vizuri sana vya
kufanyia kazi lakini haina wataalam wa kuvitumia”. Amesema Katibu Mkuu huyo.
Katika kutatua changamoto hizo Katibu Mkuu
Mchembe amemuagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg. Daud Msasi kuweka muongozo
mzuri katika kuwapangia vituo vya kazi Wafamasia na wataalam wengine ili
wananchi waweze kupata huduma bora za afya popote walipo.
Pia Prof. Mchembe amesisitiza matumizi ya data
katika kutoa huduma na kutunza kumbukumbu kupitia mifumo ya GOTHOMIS na mingineyo
ili kurahisisha utoaji wa huduma na kutunza rekodi za wagonjwa na pia kuweka mnyororo
wa huduma zote za Hospitali kuwa katika hali nzuri.
Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Ndg.
Daud Msasi amewataka wadau waliohudhuria katika kikao hicho kuhakikisha mnyororo
wa ugavi wa bidhaa za afya unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia mambo ya msingi
ambayo ni Pamoja na uzuiaji wa kukua kwa madeni yasiyolipika, nyaraka za mali
za serikali zitunzwe vizuri, matumizi ya miongozo ili kuepika gharama zisizo za
lazima, uwepo wa maduka ya dawa yanayojiendesha bila kuathiri huduma nyingine Pamoja
na kuweka taarifa zilizo sahihi.
MWISHO
0 on: "PROF. MCHEMBE AWATAKA WAFAMASIA KUSIMAMIA MAADILI"