Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 24 Septemba 2020

MIUNDOMBINU YASAIDIA HUDUMA YA DAMU SALAMA KANDA YA MAGHARIBI





 



Na. Catherine Sungura,WAMJW-Tabora

Imeelezwa kuwa kuboreshwa kwa miundombinu imesaidia kwa kiasi kikubwa huduma ya damu salama kwenye Kanda ya Magharibi ambayo inahudumia mikoa ya Tabora,Katavi,Singida na Kigoma.

Kaimu Meneja wa kanda hiyo Bi. Zaitun Abdalah ameyasema hayo wakati wa kampeni ya kukusanya damu kwenye shule ya sekondari Mabama iliyoko Manispaa ya Tabora.

“Kwa kiasi kikubwa uboreshwaji wa barabara umesaidia sana kurahisisha upatikanaji wa mahitaji wa damu salama kwenye mikoa hii tunayoihudumia ambayo inayo eneo kubwa kijiografia hivyo inapohitajika damu kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma tunawapatia kwa wakati”Alisema.

Kwa upande wa wiki hii ya kampeni ya kukusanya damu iliyoanza tarehe 21 mwezi huu na kumalizika tarehe 25 ,Kaimu Meneja huyo amesema Kanda yake imeweza kukusanya chupa 186 kwa siku mbili ikiwa imekaribia lengo lililoweka la kukusanya chupa 100 kwa siku na chupa 500 zinazotarajiwa kukusanywa kwa wiki.

Aliongeza kuwa kwa mkoa wa tabora timu yake imejipanga katika ukusanyaji wa damu katika wilaya ya Igunga na timu nyingine katika manispaa pamoja na halmashauri ya wilaya ya Uyui na wamelenga kuwafikia wanafunzi wa sekondari kwani upatikanaji wa kundi hilo ni rahisi katika kipindi hiki.

“kama kanda hatujachoka kuhamasisha wananchi licha ya changamoto ya uelewa kwa jamii kuhusu uchangiaji damu,hivyo tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwenye makundi yote ili tuweze kuwa na damu za kutosha kwenye hospitali zetu”.

Hata hivyo alisema kama Kauli mbiu ya kampeni hii  inavyosema “changia damu,ili kuokoa maisha ya akina mama wanaoleta uhai duniani “hivyo jamii inapaswa kuelewa uchangiaji wa damu mara kwa mara ni muhimu ili kuokoa vifo vya akina mama wajawazito  wanapoteza uhai wakati wanapotimiza haki yao ya kuleta watoto duniani. 

Naye Afisa Mhamasishaji wa kanda hiyo Constantine Chiba alisema wamejiwekea utaratibu kutoa elimu ya kuchangia damu kwa kutembelea vijiji mbalimbali kwenye mkoa huu,nyumba za ibada pamoja na makundio mengine katika jamii ili kuweza kuwa na akiba ya damu na pindi inapohitajika waweze kuokoa maisha ikiwemo ya akina mama wanaojifungua.

Chiba alisema yapo makundi matano ya wahitaji wa damu yakiwemo akina mama akina mama wajawazito na watoto wachanga,wahanga wa ajali,wanaohitaji tiba ya upasuaji,wenye matatizo ya kuishiwa damu (sikoseli) na kundi la mwisho ni watu wote ambao wanaweza kuugua na kuhitajika kuongezewa damu“kumbe sisi sote ni wahitaji wa damu kwani hatuyawezi kuyakwepa makundi haya yote kama binadamu kwani ugonjwa au ajali haiwezi kukwepa jinsia au umri wa mtu”.

Jumatano, 23 Septemba 2020

WAUGUZI NCHINI WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU







Na. WAMJW-Singida


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewakumbusha wauguzi wote nchini kuhakikisha wanajiendeleza kielimu, ili baadae wawe na maarifa zaidi ambayo yatawaongezea ubunifu na utendaji wao wa kazi. 

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ziada Sellah, kwenye mkutano baina yake na wauguzi na wakunga wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida.

Mkurugenzi huyo licha ya kusisitiza umuhimu wa kujiendeleza kielimu, pia amewapongeza watumishi wa kada ya uuguzi mkoani Singida, kwa kutekeleza vema majukumu yao, licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wakiwa kazini.

"Niwapongeze wauguzi wote kwa jitihada zenu mnazofanya kila siku za kuwahudumia wananchi,mmekua  muda mwingi mko na wagonjwa na hamchoki kutoa huduma kwa rika zote"Alisema Bi. Sellah

Alisema Wizara ya Afya inatoa udhamini kwa masomo ya ngazi za juu kwa watumishi wa sekta ya afya kila mwaka,hivyo wanapaswa kuomba nafasi hizo bila kusita.

Naye Muuguzi mkuu wa mkoa wa SINGIDA Hyasinta Alute, amesema kuwa hospitali na vituo vingi vya afya mkoani humo havina magari ya kubebea wagonjwa, hali inayohatarisha maisha ya wajawazito wanaopata rufaa, huku muuguzi mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Theresia Ntui, akiwaasa wauguzi kufanya kazi kwa weledi ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaofika Hospitalini hapo kupata huduma.

Ijumaa, 18 Septemba 2020

HOSPITALI NA TAASISI ZAELEKEZWA KUSIMAMIA VYEMA WANATAALUMA WA AFYA WALIO KATIKA MAFUNZO KWA VITENDO (WATARAJALI-(INTERNS)

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi


Na.WAMJW-Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa taasisi, vyuo vya afya, na waganga wafawidhi kuhakikisha wanawafuatilia kwa karibu wanataaluma wa afya walio katika mafunzo kwa vitendo , yaani watarajali (interns) ili waweze kupata umahiri(competences), utalaamu(skills) na maadili yanayotegemewa. 

Prof. Makubi ameyabainisha hayo wakati akiongea na wasajili wa Mabaraza ya kitaaluma yaliyopo chini ya wizara afya katika ukumbi wa wizara jiji hapa.

Prof. Makubi alisema Serikali imeenza kupata changamoto za baadhi ya Hospitali kushindwa kuwapa mafunzo stahili  wataraji hao na kujikuta wanamaliza mafunzo yao bila umahiri unaotegemewa katika kutoa huduma kwa wananachi.

"Serikali imeanza kuchunguza hizo hospitali na kama hazitasimamia vyema hawa wanataaluma walio mafunzoni, tutazifutia kibali cha kuwapokea"Alisisitiza 

Aidha, Prof. Makubi aliwataka wanafunzi walio kwenye mafunzo kwa vitendo kujituma katika mafunzo yao, kuonyesha nia ya kujifunza na kuweka bidii katika mafunzo yao ya vitendo mahali walipo. 

"Hawa wanataaluma wanapaswa kuonyesha tabia njema wakati wa mafunzo, kuwa watiifu, kulinda viapo vyao kuzingatia maadili ya taaluma zao na kujiheshimu katika lugha zao na hata mavazi wanayovaa mbele ya wateja wao ambao wengi ni wagonjwa na ndugu zao"Aliongeza. 

Hata hivyo Prof. Makubi ameyaagiza mabaraza hayo kuhakikisha utaratibu wa watarajali 'interns' wote kufanya mitihani baada ya mafuzo, uharakishwe ndani ya   mwaka huu ili serikali iweze kupima umahiri wa wanataaluma wote wanaomaliza mafunzo kwa vitendo.

Prof. Makubi aliipongeza Baraza la  Famasi  kwa kuratibu mitihani kwa wafamasia wataraji  na kulitaka  Baraza la Madaktari nalo likamilishe utaratibu wa mitihani kwa madaktari watarajali wote ili kulinda hadhi ya taaluma ya tiba na viwango vya kutoa huduma kwa wananchi.

Alhamisi, 17 Septemba 2020

WANATAALUMA WA SEKTA YA AFYA WAPEWA MIEZI SITA YA KUJISAJILI NA KUHUISHA LESENI ZAO



Mganga Mkuu wa Serikali wa Serikali Prof. Abel Makubi

Na. WAMJW-Dodoma

Wanataaluma wote wa sekta ya afya nchini wametakiwa wawe wamejisajili, na kuhuisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaalam ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Aidha kwa wale ambao wamejiendeleza zaidi kitalaamu wanatakiwa kuwasilisha(update) vyeti vyao vya viwango katika mabaraza ili kutambulika kisheria na kitaaluma. 

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akiongea na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalam ya Wizara ya Afya pamoja na wasajili wa bodi zilizo chini ya wizara hiyo.

“Kila mwanataaluma aliyemaliza mafunzo yake ni vizuri awe amesajiliwa katika mabaraza yao, agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika, na uzuri hivi sasa kuna tovuti hivyo mnaweza kupata kujisali , kulipia na baadae kutumiwa  vyeti vyenu bila kuchelewa.  Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita wawe wamesajiliwa”. Alisisitiza

Pia wanatataaluma wanaojiendelea kwa ngazi mbalimbali ya taalauma ya afya kama uzamili na uzamivu 'PhD’ wanatakiwa kusajili hivi viwango katika mabaraza yao ili watambulike. 

Prof. Makubi amesema utaratibu huo umewekwa na Serikali kupitia mabaraza hayo hivyo kila mwana taaluma anatakiwa kujisajili au kuhuisha leseni ambazo zimeisha muda ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.

Aidha,Prof. Makubi ameongeza kuwa wizara kupitia mabaraza hayo imeweka miundombinu ya mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa kila taaluma kwa kufanya mitihani kwa ngazi zote."Lakini mtu aliyefanya mtihani nje ya utaratibu huu basi anatakiwa kuleta  ili kufanya usajili ili kupata alama na uwekwe kwenye kiwango stahili na ndio utaonekana bado upo kwenye kiwango cha uelewa kwenye taaluma yako na kuwatumikia wananchi”.

Kwa upande wa baadhi ya watu wa sekta ya afya wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma, Prof. Makubi ametoa miezi mitatu kwa wale wanataaluma wenye vyeti vyao wajisajilii ili kutambulika wapo katika kiwango fulani cha taaluma. 

“Kuna baadhi ya wataaluma wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha kitaaluma wakati hawajasajili vyeti vyao  kwenye mabaraza, nitoe mfano kuna wanataaluma wanaojiita mabingwa wa kitu fulani (specialist, consultant …) na wanajitangaza kwa wananchi wakati hatuna ushahidi na kumbukumbu. Kwahiyo tumekubaliana na mabaraza suala hilo sasa lifikie mwisho na wote waliojiendeleza zaidi waje wajisajili haraka kwa kuwasilisha vyeti vyao.” Alisisitiza Prof. Makubi.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Serikali aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa Hsopitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kuzingatia kusimamia utekelezaji wa maagizo haya kwenye sekta zote za afya ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma husika. “Taaluma zote za afya lazima ziendelee kuheshimika na kusimamiwa vizuri ili kulinda afya za wananchi kwa viwango vya juu na bila kuruhusu wanataaluma bubu”, Alisema Prof Makubi.

Pia kwa Waganga wa tiba asili wametakiwa kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala kwani serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano kwa kuwasaidia malengo yao ya utoaji wa tiba asili yanafanikiwa.

-MWISHO-

Jumatatu, 7 Septemba 2020

TANZANIA YATOKOMEZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU MWAKA MMOJA SASA

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 
Dkt. Leonard Subi

Na Gerard Chami - WAMJW, Arusha. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kutokomeza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu (Cholera) hapa nchini.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi wakati akizindua kikao kazi cha kufanya tathmini, maboresho na kuandaa mpango kazi wa miaka mitano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini. 


“Tangu mwezi Julai mwaka 2019 hatuna kesi yoyote iliyotolewa taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa Cholera hapa nchini. Kwa miaka kadhaa tumekua na takribani asilimia 11 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanyika katika maeneo tofauti ikiwemo kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, kaya karibu zote nchini kuwa na vyoo safi na bora, kuimarishwa kwa usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama nchini kipindupindu kilipungua mpaka asilimia 1.7 na kwa kipindi cha mwaka jana hadi sasa hatuna mgonjwa aliyetolewa taarifa kabisa kuwa na maambukizi hayo.” Amesema Dkt.Subi 


Amesema, kazi iliyopo hivi sasa na inayopewa kipaumbele na Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuchambua kwa umakini mkubwa mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa ugonjwa huu, kufanya ufuatiliaji, tathmini na uperembaji wa afua mbalimbali za afya hapa nchini na kuja na mpango kazi wa utekelezaji kimkakati katika kudumisha hali hii hapa nchini kwani hivi sasa nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo ni vema kudumisha hali ya afya ya wananchi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo, kukuza kipato na kuboresha hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja. 


Aidha Dkt.Subi amesisitiza kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono muda wote kwa maji safi yanayotiririka na sabuni kwani unasaidia kukabiliana na maradhi mengine zaidi ya Corona ikiwa ni pamoja na kudumishwa kwa utoaji elimu ya afya kwa umma ili twende pamoja kama taifa linaloendelea kwa kasi. 


Akiongezea Dkt.Subi amesema ni vema kwa pamoja tukaendelea kuongeza nguvu na ushirikiano katika kulinda vyanzo na mikondo ya maji safi na salama kwani maji ni uhai na uhai ni afya hivyo itatusaidia kama Taifa kupambana na maradhi mbalimbali mijini na vijijini. 


Vilevile Dkt.Subi amesema suala la chanjo ya kuzuia kipindupindu kwasasa sio kipaumbele na badala yake nguvu kubwa inazidi kuwekwa katika kuimarisha miundombinu stahiki ya huduma za afya, usafi zaidi wa mazingira na upatikanaji zaidi wa maji safi kwa wananchi katika maeneo yote. 


Nae Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa eneo la Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa Dkt.Janeth Mghamba akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ameahidi kwa niaba ya timu za wataalamu wa afya kuendelea kuwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa katika jamii wanazotoka (kata, mitaa na vijiji), kusukuma uimarishaji wa maabara katika ngazi zote; mkoa, wilaya, zahanati na halmashauri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu. 


Pamoja nae, Dkt.Faraja Msemwa kwa niaba ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umoja na mshikamano uliopo kwa kuwaweka wadau wa maendeleo karibu katika kukabiliana na majanga ya maradhi mbalimbali hapa nchini na yale yanayoikumba dunia kwa ujumla wake kwani afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote. 


Mwisho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg.Gerard Chami, amewataka wanahabari kuendelea kutumia vyombo vyao ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuelimisha umma juu ya utunzaji wa mazingira, matumizi sahihi na utunzaji wa vyoo bora, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kudumisha utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka na sabuni. 

Mwisho