Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 7 Septemba 2020

TANZANIA YATOKOMEZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU MWAKA MMOJA SASA

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 
Dkt. Leonard Subi

Na Gerard Chami - WAMJW, Arusha. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kutokomeza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu (Cholera) hapa nchini.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi wakati akizindua kikao kazi cha kufanya tathmini, maboresho na kuandaa mpango kazi wa miaka mitano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini. 


“Tangu mwezi Julai mwaka 2019 hatuna kesi yoyote iliyotolewa taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa Cholera hapa nchini. Kwa miaka kadhaa tumekua na takribani asilimia 11 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanyika katika maeneo tofauti ikiwemo kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, kaya karibu zote nchini kuwa na vyoo safi na bora, kuimarishwa kwa usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama nchini kipindupindu kilipungua mpaka asilimia 1.7 na kwa kipindi cha mwaka jana hadi sasa hatuna mgonjwa aliyetolewa taarifa kabisa kuwa na maambukizi hayo.” Amesema Dkt.Subi 


Amesema, kazi iliyopo hivi sasa na inayopewa kipaumbele na Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuchambua kwa umakini mkubwa mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa ugonjwa huu, kufanya ufuatiliaji, tathmini na uperembaji wa afua mbalimbali za afya hapa nchini na kuja na mpango kazi wa utekelezaji kimkakati katika kudumisha hali hii hapa nchini kwani hivi sasa nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo ni vema kudumisha hali ya afya ya wananchi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo, kukuza kipato na kuboresha hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja. 


Aidha Dkt.Subi amesisitiza kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono muda wote kwa maji safi yanayotiririka na sabuni kwani unasaidia kukabiliana na maradhi mengine zaidi ya Corona ikiwa ni pamoja na kudumishwa kwa utoaji elimu ya afya kwa umma ili twende pamoja kama taifa linaloendelea kwa kasi. 


Akiongezea Dkt.Subi amesema ni vema kwa pamoja tukaendelea kuongeza nguvu na ushirikiano katika kulinda vyanzo na mikondo ya maji safi na salama kwani maji ni uhai na uhai ni afya hivyo itatusaidia kama Taifa kupambana na maradhi mbalimbali mijini na vijijini. 


Vilevile Dkt.Subi amesema suala la chanjo ya kuzuia kipindupindu kwasasa sio kipaumbele na badala yake nguvu kubwa inazidi kuwekwa katika kuimarisha miundombinu stahiki ya huduma za afya, usafi zaidi wa mazingira na upatikanaji zaidi wa maji safi kwa wananchi katika maeneo yote. 


Nae Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa eneo la Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa Dkt.Janeth Mghamba akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ameahidi kwa niaba ya timu za wataalamu wa afya kuendelea kuwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa katika jamii wanazotoka (kata, mitaa na vijiji), kusukuma uimarishaji wa maabara katika ngazi zote; mkoa, wilaya, zahanati na halmashauri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu. 


Pamoja nae, Dkt.Faraja Msemwa kwa niaba ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umoja na mshikamano uliopo kwa kuwaweka wadau wa maendeleo karibu katika kukabiliana na majanga ya maradhi mbalimbali hapa nchini na yale yanayoikumba dunia kwa ujumla wake kwani afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote. 


Mwisho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg.Gerard Chami, amewataka wanahabari kuendelea kutumia vyombo vyao ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuelimisha umma juu ya utunzaji wa mazingira, matumizi sahihi na utunzaji wa vyoo bora, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kudumisha utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka na sabuni. 

Mwisho

0 on: " TANZANIA YATOKOMEZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU MWAKA MMOJA SASA"