Na WAMJW- DOM
KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewaagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili.
Prof. Mchembe ameyasema hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu ya "Miongo miwili ya Tiba Asili Afrika 2001 mpaka 2020 Nchi zina mafanikio gani".
"Kwa maana hiyo basi nawaagiza Baraza la Tiba Asili na tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili" alisema Prof. Mabula Mchembe.
Aliendelea kusisitiza kuwa, ni vyema Baraza la tiba asili na Mamlaka zote nchini, kushirikiana na taasisi zote zinazohusiana na tiba asili hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutokana na kuwepo kwa kitengo kinachohusiana na mimea.
Prof. Mchembe amesema kuwa, katika kuadhimisha miaka 18 ya siku ya tiba asili ya Mwafrika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mambo mengi ikiwemo, kuitambua huduma ya tiba asili katika Sera ya Afya kuanzia, kutungwa kwa Sheria ya tiba asili na tiba mbadala Namba 23 ya mwaka, kutengenezwa kwa kanuni na miongozo mbalimbali ya Tiba Asili na Tiba Mbadala mwaka, kuanza kutoa mafunzo kwa Waratibu na watoa huduma wa tiba asili nchini.
Aidha Prof. Mchembe, ameliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili.
Mbali na hayo Prof. Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini kutumia fursa kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake.
"Nitoe wito kwa Waganga na wadau wa Tiba Asili kutumia fursa iliyopo ya Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake" alisema Prof. Mchembe
Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe amesema kuwa, kupitia maadhimisho ya tiba asili kama nchi tumepata mafanikio mengi sana ikiwemo kuongezeka idadi kubwa ya wananchi wanaotumia dawa za asili hususan katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona.
"Kupitia maadhimisho ya tiba asili, tangu tumeanza kama nchi, Luna mafanikio mengi sana yameweza kupatikana, lakini kubwa naloweza kulisemea, ni kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaotumia dawa zetu za asili pamoja na tiba mbadala, na mfano mzuri ni katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, kama nchi tunaweza kusimama kifua mbele na kusema tiba zetu za asili zimetutoa kwa kiwango kikubwa, " alisema.
Aliendelea kusema kuwa, pamoja na kuendelea na utafiti wa dawa mbali mbali za asili ambazo zilitumika katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, takribani zaidi ya watu 100,018 walitumia dawa za asili, ikiwemo njia ya kujifukiza (nyungu), na kuonesha mafanikio kwa kiasi kikubwa.
Nae Kaimu Msajili Baraza la tiba asili na tiba mbadala Wizara ya Afya Ndg. Patrick Seme amesema kuwa, hadi sasa Baraza la tiba asili na tiba mbadala limeshasajili dawa 30, huku akiweka wazi kuwa kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa ni kidogo ukilinganisha na uhalisia, huku akiweka wazi kuwa Baraza linaendelea kuhakikisha linasajili dawa nyingi zaidi kwa kufuata kanuni na taratibu.
"Kama mnavyofahamu kuwa mwaka 2017 tulianza kusajili dawa za asili kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kuwa hadi sasa dawa 30 zimesajiliwa. Kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa nichache sana ukilinganisha na uhalisia." Alisema.
Akiwawawakilisha Waganga wa tiba asili Mkoa wa Dodoma Mzee Issa Mdoe amesema kuwa, Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kushirikiana na Waganga wa tiba asili limekuwa na mafanikio mengi yakiwemo kutoa elimu mara kwa mara kwa Waganga kujua dhana ya tiba asili ikiwemo kujiepusha na mauaji ya vikongwe na mauaji ya albono na mauaji ya watoto wadogo.
Mbali na hayo Mzee Issa Mdoe ameweka wazi kuwa, baadhi ya changamoto zinazowakumba, zikiwemo gharama za usajili wa dawa kuwa juu, hivyo kuwafanya Waganga wengi kushindwa kisajili dawa zao, elimu ndogo ya malipo ya njia ya elektroniki inayopelekea baadhi ya Waganga katapeliwa na watu wasio waaminifu.
Mwisho.
0 on: "SIMAMIENI USAJILI WA DAWA ZA ASILI KWA KUTOA ELIMU YAKUTOSHA KWA WATENGENEZAJI - PROF. MCHEMBE."