Picha mbalimbali zikimuonesha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela pamoja viongozi mbalimbali wakipita katika mabanda yaliyopo kwenye maonesho ya Nanenane kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro kuona bidhaa na huduma katika mabanda hayo.
NA EMMANUEL MALEGI-MOROGORO
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto amepiga marufuku shule zote nchini kuwapa wasichana dawa aina
ya Folic Acid na badala yake shule zimetakiwa kulima kuwajengea uwezo wa kulima
maboga na mbogamboga katika bustani za shule.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati alipokua
akihitimisha kilele cha Maonesho ya Nanenane kanda ya Mashariki inayojumuisha
Mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro ambayo yamefanyika mkoani Morogoro.
Waziri Ummy amesema
kuwa ni marufuku kuwapa wanafunzi na wasichana balehe vidonge vya Folic Acid, badala yake fedha hizo
zinazotolewa kwa ajili ya dawa hizo zitumike kuanzisha bustani shuleni ili
kuzalisha vyakula vinavyotoa madini hayo.
“Mbali na kuanzishwa kwa
bustani shuleni lakini pia fedha hizo zinaweza kupelekwa kwa vijana ili
waanzishe miradi ya bustani za mboga kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha
asidi hiyo yakiwemo maboga, matunda na hata karoti badala ya kutoa vidonge kwa
wanafunzi”. Amesema Ummy.
Kuhusu unywaji wa maziwa mashuleni, Waziri Ummy amesema kuwa atamwandikia
barua ya pendekezo Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako ili kuanzia
Septemba mosi mwaka huu kila shule iwe na kibanda cha maziwa kwa ajili ya
wanafunzi kununua.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa utafiti wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) unaonesha kwamba kila mtu anatakiwa kunywa nusu lita ya maziwa
sawa na lita 180 kwa mwaka, lakini kwa sasa kila mtu anakunywa lita 40 kwa
mwaka sawa na vijiko 10 vya chai kwa siku.
Pia Waziri amesema udumavu kwa watoto wa chini ya miaka
mitano umepungua nchini kutoka
asilimia 34.4 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018 licha ya kuwa jitihada zinatakiwa kuendelea
kuchukuliwa.
Pamoja na hayo Waziri Ummy ameupongeza mkoa wa Morogoro kwa kuwa mwenyeji
wa maonesho hayo ambayo yamekua chachu ya ukuaji wa kilimo, uvuvi, ufugaji na ujasiriamali
nchini na amewataka waratibu wake kutoishia hapo na badala yake ujuzi huo
upelekwe vijijini kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo muhimu ambayo kwa kiasi
kikubwa inachangia pato la taifa.
0 on: "WAZIRI UMMY APIGA MARUFUKU WANAFUNZI KUPEWA VIDONGE VYA FOLIC ACID MASHULENI"