Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 25 Novemba 2020

PROF. MCHEMBE AWAAGIZA WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA KUFIKIRIA HUDUMA BORA NA NAFUU KWA WANANCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa saba wa Afya uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Afya ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Ntuli Kapologwe akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa saba wa afya, uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa afya nchini, Jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akipita katika banda la NIMR kujionea shughuli zinazoendelea, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Afya uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya waliohudhuria Mkutano wa saba wa masuala ya Afya unaoendelea Jijini Dodoma kujadili namna bora ya kuboresha huduma za Afya nchini.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akiwa na Wadau mbali mbali wa Afya wakati wa  Mkutano wa saba wa Afya unaoendelea Jijini Dodoma.PROF. MCHEMBE AWAAGIZA WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA KUFIKIRIA HUDUMA BORA NA NAFUU KWA WANANCHI

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW - DOM 

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa Sekta ya Afya nchini kuhakikisha wanafikiria namna ya utoaji huduma bora na kwa gharama nafuu ili wananchi wenye hali zote waweze kuzimudu.

Wito huo ameutoa leo, wakati akifungua Mkutano wa saba wa Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Watumishi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau mbali mbali wanaojihusisha na masuala ya Afya nchini.

"Ni wajibu wetu sisi, tukiwa kwenye Mkutano huu wa wa Afya kuwaza vyema tunamsaidiaje mwananchi wa hali ya chini kupata huduma bora, zenye unafuu na zinazofikika kila sehemu bila kumuumiza mwananchi" alisema Prof. Mchembe.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amesema kuwa, Wizara ya Afya itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wadau wote ili kufanikisha utoaji huduma bora na nafuu kwa wananchi, huku akiweka wazi kuwa kama Serikali itatendea kazi mapendekezo na ushauri utakaotokana na Mkutano huo. 

Aidha, Prof. Mchembe amesisitiza kuwa, ni muhimu mijadala itayoendelea katika Mkutano huo kuhakikisha inapita kwenye malengo ya Wizara yakiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupunguza maambukizi ya VVU, TB, Ukoma, 

Mbali na hayo, Prof. Mabula Mchembe amewataka Wataalamu hao kujadili masuala ya kupunguza magonjwa yasiyo yakuambukiza ambayo yanaongeza mzigo kwa Serikali kutokana na gharama za kuyatibu magonjwa hayo, yanayotokana na mtindo wa maisha ikiwemo matumizi ya pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi. 

Naye, Mkurugenzi Idara ya Afya ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa, Serikali imefanya maboresho mengi sana katika miaka saba iliyopita, huku akiweka wazi kuwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho yataendana na mpango mkakati wa Sekta afya unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya. 

Pia, Dkt.Kapologwe amesema kuwa, kama wasimamizi wa Sera watahakikisha maazimio yatakayotoka kwenye kikao hicho yanaingizwa kwenye mipango ya utekelezaji kwenye Hospitali zote ngazi ya Wilaya, Halmashauri na zahanati kwa utekelezaji zaidi. 

"Katika kikao hiki, pamoja na maelekezo ambayo utayatoa, sisi tukiwa kama wasaidizi wako tutahakikisha, maelekezo yako pamoja na maazimio utakayotoa katika kikao hiki, tunaenda kuyaingiza katika mipango yetu katika Hospitali za Mikoa, Halmashauri na Zahanati" amesema Dkt. Ntuli Kapologwe. 

Mwisho

Jumanne, 24 Novemba 2020

KUELEKEA MPANGO MKAKATI WA TANO WA SEKTA YA AFYA, SERIKALI YAJIDHATITI KUSOGEZA ZAIDI HUDUMA KWA WANANCHI.

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa Tathmini ya Utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anaeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima akieleza jambo wakati wa ufunguzi  wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa Tathmini ya Utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akimkaribisha mgeni  rasmi Katibu Mkuu Wizara  ya Afya Prof. Mabula Mchembe (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya wakiteta jambo wakati  wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi wasaidizi kutoka Wizara ya Afya  walioshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wadau waliohudhuria ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya na Wadau wa Sekta ya Afya nchini walio hudhuria  ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe, akiwa na Sekretarieti ya mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya.Na, Rayson Mwaisemba WAMJW- DOM 

SERIKALI, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kujidhatiti katika kuboresha utoaji huduma za Afya kwa wananchi ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, uboreshaji wa huduma za chanjo, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba. 

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe wakati akifungua Mkutano wa 21 wa kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya ulioandaliwa kwa pamoja na Wizara yake na Ofisi ya Rais TAMISEMI ukishirikisha Wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya nchini unaoendelea Jijini Dodoma.

Prof. Mchembe amesema kuwa, kikao hicho kina umuhimu mkubwa sana katika Wizara na Sekta ya Afya kwa ujumla kwa sababu ndio kinachoweza kuweka mikakati ya nini kifanyike miaka mitano ijayo, baada ya kupitia mikakati ya miaka mitano iliyopita na kuona mafanikio na changamoto zake.

"Kama Serikali tumefanikiwa kuboresha katika kupunguza vifo vya mama na mtoto,  huduma za chanjo, vifaa na vifaa tiba pamoja na uboreshaji wa utoaji huduma zinazotolewa na Watumishi wa Afya" amesema Prof. Mchembe. 

Aidha,  Prof. Mchembe amesema mpango mkakati wa tano unaoenda kuanza ni matokeo ya ule wa nne ambapo unaangazia mafanikio, na kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha Sekta ya Afya. 

Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, kama wasimamiaji wa utekelezaji wa Sera katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za mitaa wapo tayari kutekeleza maagizo na miongozo itayotolewa kupitia kikao hicho cha tathmini ya Sera kilichohudhuriwa na Wadau wote wa Sekta ya Afya nchini. 

"Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameeleza mambo mengi, sisi tupo kama Wadau ambao tunasimamia utekelezaji kwenye ngazi ya Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa tunasubiri maelekezo  na miongozo ya Kisera ili kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo tuweze kutekeleza kwa kasi ile ile" alisema Dkt. Gwajima. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga amesema kuwa, kikao hicho cha Sera hupokea mambo yote katika Sekta ya Afya yaliyofanyiwa tathmini na yaliyokubalika kuwa ndio yatakuwa malengo na muelekeo wa Sekta ya Afya nchini. 

Mwisho.

Jumatatu, 23 Novemba 2020

MGANGA MKUU WA SERIKALI “TUMEONGEZA UWEZO WA KUGUNDUA WAGONJWA WAPYA WA KIFUA KIKUU”

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akisema jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Jijini Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akigawa cheti cha pongezi kwa Uongozi wa Afya wa Mkoa wa Manyara kupitia Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Damas Kayera mara baada ya kushika nafasi ya kwanza ngazi ya mikoa kwa kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa afua za kupambana na kifua kikuu na ukoma.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Zuweina Kondo akisema jambo kwa wadau wa mkutano wa mwaka wa mpango huo (hawapo pichani)
Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini

Na Englibert Kayombo WAMJW - Dodoma

Serikali ya Tanzania imeazimia kutokomeza kabisa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kuongeza uwezo wa ugunduzi wa wagonjwa wapya wa kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu an Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.

“Uwezo wa nchi kugundua wagonjwa wapya na kuwaweka kwenye matibabu umeongezeka kutoka wagonjwa 62,908 (33%) mwaka 2015 na kwa sasa kufikia wagonjwa 82,166 (59%)” amesema Prof. Makubi

Kufuatia hatua hiyo Prof. Makubi amesema kuwa maisha ya wananchi takribani 300,000 ikiwemo ya watoto 45,000 yameponywa kwa kupatiwa dawa kwa wakati na kufuatiliwa kwa usahihi kuanzia mwaka 2015 hadi sasa.

Juhudi hizo pia zimeweka kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na kifua kikuu kwa 33%. “Mwaka 2015 kulikuwa na vifo 30,000 hivi sasa vimepungua hadi kufikia vifo 20,000” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema kuwa mafanikio hayo ya ongezeko la kasi ya ugunduzi wa wagonjwa wapya yametokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma ikiwemo kuboresha huduma za ugunduzi wa TB na kutoa kipaumbele kwa makundi yaliyoathirika zaidi kama vile kaya zenye wagonjwa, wanaoishi kwenye kaya duni, gerezani, wachimbaji wadogo wadogo na kwa waathirika wa madawa ya kulevya.

“Aidha tumewekeza katika afua bunifu mbalimbali za matumizi ya teknolojia mpya za molekyula za kubaini TB kwa usahihi na kwa haraka” amesisitiza Prof. Makubi.

Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema Wizara imefanya vizuri kwenye kwa kufikia malengo waliyoyaweka kwenye Mpango mkakati ambao unamalizika mwaka huu 2020.

“Malengo ambayo tulijiwekea ya kupunguza vifo vitokanavyo na kifua kikuu tumeweza kuyafikia pamoja na kupunguza madhaa yanayotokana na ugonjwa huo” amesema Dkt. Subi

Amesema kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza vituo vya upimaji wa kifua kikuu sugu kutoka kituo 1 mwaka 2015 hadi kufika vituo 145 hivyo kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya ugonjwa huo

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana Wizara ya Afya katika kipindi cha miaka 5 ijayo imejiwekea mikakati ya kuwawezesha watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili wawe na ujuzi na uwezo wa kutambua na kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu.

Jumamosi, 17 Oktoba 2020

WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUNZA TAARIFA ZA UTENDAJI WAO WA KAZI KILA SIKU

- Hakuna maoni

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah akisema jambo kww wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dar es Salaam (hawapo pichani)


Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah (kulia) akikagua nyaraka za wauguzi kuona jinsi wanavyotunza taarifa za utendaji kazi.

 
Picha ya Pamoja Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah pamoja na Wauguzi na Wakunga Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala, Dar es Salaam.Na WAMJW – Dar Es Salaam

Wauguzi na wakunga nchini wamekumbushwa kuhakikisha wanatunza vizuri taarifa za kazi kwenye
majarada ya kazini kwa kuandika yale yote ambayo wanafanya tangu wanapoingia kazini hadi kutoka.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga katika
Hosptali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala – Dar Es Salaam.

“Kila unachofanya kazini aidha umemhudumia mgonjwa au ukiwa na majukumu mengine hakikisheni
mnatunza taarifa za kazi kwa kuandika kwenye majadara yenu ya kazi” amesema Bi. Ziada

Bi. Ziada amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia pia madaktari, wauguzi na wakunga wengine
wanaoingia zamu tofauti kutambua kwa haraka nini ambacho kimefanyika na kuweza kuendelea na kazi
ambayo wengine wameacha.

Amesema kuwa wauguzi na wakunga wamekuwa wakilaumiwa kwa kutotunza vizuri taarifa za utendaji
kazi jambo ambali hupelekea changamtoto kwa wagonjwa kutopata huduma sahihi wakiwa hospitalini.

“Tumekuwa tukilaumiwa hatutunzi kumbukumbu zetu vizuri, andikeni kila mnachofanya, kama umemwita
daktari saa 1, hadi saa 3 hajafika andikeni, tufanye ‘documentation’ kadiri inavyowezekana” amesisitiza
Bi. Ziada.

Hata hivyo Bi. Ziada Sellah hakusita kuwakumbusha wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa malengo ili
waweze kujipima ufanisi wa kazi zao na kujua eneo wanapofanya vizuri na kwenye changamoto.

“Tufanye kazi kwa malengo ili mwisho wa siku tuweze kujipima kwa kufanya tathimini ya malengo
tuliyojiwekea kubaini kama tumeweza kuyatimiza” amesema Bi. Ziada.

Amesema kuwa malengo yanaweza kuwa ya siku moja hadi mwaka mmoja kulingana shabaha
ulizojiwekea muuguzi au mkunga na yatawaongoza kujua ni wapi walikwama na wapi walifanikiwa.

Mwisho

Ijumaa, 16 Oktoba 2020

WANANCHI WAKUMBUSHWA KUCHUKUA TAHADHARI KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

- Hakuna maoni

 


Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma.

Watanzania wamekumbushwa kuzingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko  kufuatia kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.

Tahadhari hiyo imetolewa leo na Prof. Abel Makubi  Mganga Mkuu wa Serikali , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Wizara jijini Dodoma.

“Kufuatia mvua hizi, ni wazi kuwa uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu, na yale yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue, endapo wananchi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema” Alisema Prof. Makubi.

Prof. Makubi amesema kufuatia kujitokeza  kwa uharibifu wa miundo mbinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka hali hiyo ina hatarisha afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko.

Aidha, Mganga Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kuzingatia kanuniz za afya kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa au kutatibu kwa dawa maalumu na kuhakikisha maji ya kunywa nay ale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi.

“Tunawapongeza wananchi na ninyi wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu  kwa sababu wananchi wamekuwa wasikivu na kutii masharti ya usafi na jinsi ya kujikinga,ni zaidi ya mwaka na nusu sasa Tanzania tumeweza kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini”.

Aidha, amesema  jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama na ushirikiano mzuri wa wananchi na hivyo kusababisha baadhi ya magonjwa yanayotokana na uchafu yamepungua.

Hata hivyo Prof. Makubi amesisitiza kutumia ipasavyo vyoo na hasa kipindi hiki cha mvua kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara hasa,kabla ya kula kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.

“Tuongeze usimamizi wa usafi wa nyumba na hasa usafi wa mikono wananchi wamekua wakihamasika usafi wa mikono katika vipindi mbalimbali,hivyo tungeomba kasi ya kunawa mikono iwe endelevu katika mikusanyiko,  mashule, madukani, hospitalini,vituo vya mabasi,na taasisi pamoja na masoko,sehemu za kunawia mikono iwe ndelevu kuhakikisha wananchi wanakuwa na usafi wa kunawa mikono wa hali ya juu.

Pia,aliwata Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wanaelekezwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikaili za mitaa, Wananchi na wadau mbali mbali ili kuhakisha kila eneo lilio chini yao, haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko kwa kutotapisha vyoo au vyovyote vinavyotoka kwenye vyoo kwenda kwenye mazingira ya wananchi.

Kwa upande wa kujikinga dhidi ya kuumwa na Mbu Prof. Makubi aliwataka wananchi kutumia ipasavyo vyandarua kabla ya kwenda kulala au wenye uwezo wa kununua dawa za kujipaka wapake ili ziwasaidie.

Prof. Makubi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini na shime kuimarisha afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na tabia za usafi katika familia na jamii  kwa ujumla ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu.

-Mwisho-

Jumatatu, 12 Oktoba 2020

WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUJIENDELEZA KITAALUMA

- Hakuna maoni

`
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah akisema jambo kwa wauguzi na wakunga wa Mkoa wa Mtwara (hawapo pichani) katika kikao kazi 

Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara BW. Ahmed Chibwana akisema jambo kwa wauguzi na wakunga wa Mkoa wa Mtwara

Afusa Muuguzi kutoka Idara ya Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Jamila Hamudu akisema jambo

Afisa Muuguzi kutoka Idara ya Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Aziza Machenje akisema jambo

Na WAMJW – Mtwara.

Wauguzi na Wakunga nchini wamekumbushwa kujiendeleza kitaaluma ili kuweza kuongeza ujuzi zaidi katika utendaji kazi na kutoa huduma zilizo bora zaidi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah alipokuwa akizungumza na wauguzi na wakunga wa Mkoa wa Mtwara katika kikao kazi kilichofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula)

“Tujitahidi twende na kasi wanayokwenda wauguzi na wakunga katika nchi nyingine nasi tujiendeleze kimasomo, hapo zamani tulikuwa tunaishia diploma sasa hivi tuna hadi ‘phd’ hii ina maana tunakuwa" Amesema Bi. Ziada Sellah

Amesema kuwa wauguzi na wakunga wachangamkie fursa za kujiendeleza kimasomo zinazotolewa na Wizara ya Afya pindi tu zinapotangazwa na wasiridhike ngazi za elimu walizonazo ikiwa wana nafasi ya kujiendeleza zaidi.

Bi. Ziada amesema kuwa kujiendeleza kielimu kuna faida nyingi ikiwemo, kuongeza ujuzi zaidi katika kazi, kuwa na uhakika na kile unachokifanya ukiwa kazini na kupelekea utendaji kazi mzuri pamoja na kuwa kwenye nafasi ya kupanda madaraja ya mshahara kwa haraka.

Awali akizungumza Bi. Jamila Hamudu kutoka Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na mamlaka husika wanapitia upya muundo wa kada hizo na endapo utakidhi vigezo husika itapindishwa na kuwa muundo rasmi wa kada za uuguzi na ukunga.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wauguzi na wakunga kujiendeleza kimasomo zaidi ili kunufaika  na muundo huo ambao umeongeza majumuku ya kada hizo pamoja na stahiki zao.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Ahmed Chibwana amesema kuwa Mkoa huo una jumla ya wauguzi 780 ambao wanatoa huduma mbali mbali katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, Bw. Chibwana amesema kuwa majumuku ya wauguzi yamekuwa yakiongezeka kuliko na ilivyokuwa awali na wamekuwa na mwamko wa kazi huku akiomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi na wakunga ili stahiki zao ziendane na kazi wanazofanya.

“Niwapongeze wauguzi hawa, kwa moyo wa kujitoa, licha ya kuongezeka kwa kazi wanazofanya lakini wamekuwa na moyo wa kujituma kuhakikisha wanatoa huduma bora, tunaziomba mamlaka husika kuwaangalia upya wauguzi hawa” amesema Bw. Chibwana.

Naye, Bi. Albertina Mlowala Afisa Muuguzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara (Ligula) ameomba Wizara kuongeza watumishi wa kada za afya mkoani humo ili kupunguza wingi wa kazi kwa wauguzi na kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi.

Mwisho.

Jumatano, 7 Oktoba 2020

SERIKALI IMEFANIKIWA KUWEKEZA KWENYE UTOAJI HUDUMA ZA AFYA NCHINI

- Hakuna maoniNa. Catherine Sungura.WAMJW-DSM

erikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kuwekeza kwenye utoaji huduma za afya kwa wananchi wote nchini kwa kuboresha majengo,dawa,vifaa na vifaa tiba.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Bernad Konga mwanzoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa mpango wa dunduliza utakaomuwezesha mwananchi kudunduliza fedha kidogokidogo za mchango wa bima ya afya kupitia bank ya NMB.

Konga alisema kuwa ili wananchi kuwa na uhakika wa matibabu,Serikali iliona kutafuta namna nyepesi ya mwananchi wa hali ya chini aweze kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa kuweka kidogo kidogo kwa muda atakaochagua na atakapokamilisha kiwango husika atapatiwa kadi ya matibabu na kuanza kunufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF.

"Serikali imejipanga kumfikia kila mwananchi bila kujali hali yake kikazi na hata makazi,lengo ni kila mwananchi kuwa na uhakika wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa kuwa na bima ya afya ya NHIF".Alibainisha

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema Serikali inaendelea na utoaji elimu yenye lengo la kuwajengea wananchi utamaduni wa kuwa na bima kabla ya kuugua na sasa imekuja na mpango wa kujiwekea fedha kwa njia ya benki kwa ajili yake na familia yake.

"Menejimenti ya mfuko iliona uwezo wa wananchi kulipa fedha zote kwa awamu moja itakua ni changamoto,hivyo tumefungua milango wananchi wadundulize kidogo kidogo ili wawe na uhakika wa matibabu wakati wowote ".

Mwananchi anayehitaji kujiunga na huduma za NHIF ambaye atahitaji kuweka fedha kidogo kidogo  kwa muda atakaochagua ni yule,anayejiunga kupitia mpango wa vifurushi ambavyo vinajulikana kwa majina ya Najali Afya,Wekeza Afya na Timiza Afya ambavyo pia vinampa fursa  mwananchi anayehiraji kuchangia kuchagua huduma kulingana na mahitaji yake,umri na wanufaika anaohitaji kuwajumuisha.

Mpango huu unamwezesha mwananchi kujiwekea fedha kwa ajili yake mwenyewe ama kwa ajili yake na mwenza wake ama kwa ajili yake na mtoto ama watoto alionao.

Mfumo huo pia ni rahisi kuutumia kwa kuwa unahitaji mtumiaji kuwa na,simu ya mkononi ya aina yoyote na kuzingatia hatua zilizoweka na endapo atakwama hatua za kujisajili anaweza kupiga simu bila malipo kwa namba 0800110063 kupatiwa maelezo namna ya kufanya.

-Mwisho-

Jumatatu, 5 Oktoba 2020

JARIDA LA WIZARA YA AFYA - TOLEO LA 2

- Hakuna maoni


Alhamisi, 24 Septemba 2020

MIUNDOMBINU YASAIDIA HUDUMA YA DAMU SALAMA KANDA YA MAGHARIBI

 Na. Catherine Sungura,WAMJW-Tabora

Imeelezwa kuwa kuboreshwa kwa miundombinu imesaidia kwa kiasi kikubwa huduma ya damu salama kwenye Kanda ya Magharibi ambayo inahudumia mikoa ya Tabora,Katavi,Singida na Kigoma.

Kaimu Meneja wa kanda hiyo Bi. Zaitun Abdalah ameyasema hayo wakati wa kampeni ya kukusanya damu kwenye shule ya sekondari Mabama iliyoko Manispaa ya Tabora.

“Kwa kiasi kikubwa uboreshwaji wa barabara umesaidia sana kurahisisha upatikanaji wa mahitaji wa damu salama kwenye mikoa hii tunayoihudumia ambayo inayo eneo kubwa kijiografia hivyo inapohitajika damu kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma tunawapatia kwa wakati”Alisema.

Kwa upande wa wiki hii ya kampeni ya kukusanya damu iliyoanza tarehe 21 mwezi huu na kumalizika tarehe 25 ,Kaimu Meneja huyo amesema Kanda yake imeweza kukusanya chupa 186 kwa siku mbili ikiwa imekaribia lengo lililoweka la kukusanya chupa 100 kwa siku na chupa 500 zinazotarajiwa kukusanywa kwa wiki.

Aliongeza kuwa kwa mkoa wa tabora timu yake imejipanga katika ukusanyaji wa damu katika wilaya ya Igunga na timu nyingine katika manispaa pamoja na halmashauri ya wilaya ya Uyui na wamelenga kuwafikia wanafunzi wa sekondari kwani upatikanaji wa kundi hilo ni rahisi katika kipindi hiki.

“kama kanda hatujachoka kuhamasisha wananchi licha ya changamoto ya uelewa kwa jamii kuhusu uchangiaji damu,hivyo tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwenye makundi yote ili tuweze kuwa na damu za kutosha kwenye hospitali zetu”.

Hata hivyo alisema kama Kauli mbiu ya kampeni hii  inavyosema “changia damu,ili kuokoa maisha ya akina mama wanaoleta uhai duniani “hivyo jamii inapaswa kuelewa uchangiaji wa damu mara kwa mara ni muhimu ili kuokoa vifo vya akina mama wajawazito  wanapoteza uhai wakati wanapotimiza haki yao ya kuleta watoto duniani. 

Naye Afisa Mhamasishaji wa kanda hiyo Constantine Chiba alisema wamejiwekea utaratibu kutoa elimu ya kuchangia damu kwa kutembelea vijiji mbalimbali kwenye mkoa huu,nyumba za ibada pamoja na makundio mengine katika jamii ili kuweza kuwa na akiba ya damu na pindi inapohitajika waweze kuokoa maisha ikiwemo ya akina mama wanaojifungua.

Chiba alisema yapo makundi matano ya wahitaji wa damu yakiwemo akina mama akina mama wajawazito na watoto wachanga,wahanga wa ajali,wanaohitaji tiba ya upasuaji,wenye matatizo ya kuishiwa damu (sikoseli) na kundi la mwisho ni watu wote ambao wanaweza kuugua na kuhitajika kuongezewa damu“kumbe sisi sote ni wahitaji wa damu kwani hatuyawezi kuyakwepa makundi haya yote kama binadamu kwani ugonjwa au ajali haiwezi kukwepa jinsia au umri wa mtu”.

Jumatano, 23 Septemba 2020

WAUGUZI NCHINI WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMUNa. WAMJW-Singida


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewakumbusha wauguzi wote nchini kuhakikisha wanajiendeleza kielimu, ili baadae wawe na maarifa zaidi ambayo yatawaongezea ubunifu na utendaji wao wa kazi. 

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ziada Sellah, kwenye mkutano baina yake na wauguzi na wakunga wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida.

Mkurugenzi huyo licha ya kusisitiza umuhimu wa kujiendeleza kielimu, pia amewapongeza watumishi wa kada ya uuguzi mkoani Singida, kwa kutekeleza vema majukumu yao, licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wakiwa kazini.

"Niwapongeze wauguzi wote kwa jitihada zenu mnazofanya kila siku za kuwahudumia wananchi,mmekua  muda mwingi mko na wagonjwa na hamchoki kutoa huduma kwa rika zote"Alisema Bi. Sellah

Alisema Wizara ya Afya inatoa udhamini kwa masomo ya ngazi za juu kwa watumishi wa sekta ya afya kila mwaka,hivyo wanapaswa kuomba nafasi hizo bila kusita.

Naye Muuguzi mkuu wa mkoa wa SINGIDA Hyasinta Alute, amesema kuwa hospitali na vituo vingi vya afya mkoani humo havina magari ya kubebea wagonjwa, hali inayohatarisha maisha ya wajawazito wanaopata rufaa, huku muuguzi mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Theresia Ntui, akiwaasa wauguzi kufanya kazi kwa weledi ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaofika Hospitalini hapo kupata huduma.

Ijumaa, 18 Septemba 2020

HOSPITALI NA TAASISI ZAELEKEZWA KUSIMAMIA VYEMA WANATAALUMA WA AFYA WALIO KATIKA MAFUNZO KWA VITENDO (WATARAJALI-(INTERNS)

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi


Na.WAMJW-Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa taasisi, vyuo vya afya, na waganga wafawidhi kuhakikisha wanawafuatilia kwa karibu wanataaluma wa afya walio katika mafunzo kwa vitendo , yaani watarajali (interns) ili waweze kupata umahiri(competences), utalaamu(skills) na maadili yanayotegemewa. 

Prof. Makubi ameyabainisha hayo wakati akiongea na wasajili wa Mabaraza ya kitaaluma yaliyopo chini ya wizara afya katika ukumbi wa wizara jiji hapa.

Prof. Makubi alisema Serikali imeenza kupata changamoto za baadhi ya Hospitali kushindwa kuwapa mafunzo stahili  wataraji hao na kujikuta wanamaliza mafunzo yao bila umahiri unaotegemewa katika kutoa huduma kwa wananachi.

"Serikali imeanza kuchunguza hizo hospitali na kama hazitasimamia vyema hawa wanataaluma walio mafunzoni, tutazifutia kibali cha kuwapokea"Alisisitiza 

Aidha, Prof. Makubi aliwataka wanafunzi walio kwenye mafunzo kwa vitendo kujituma katika mafunzo yao, kuonyesha nia ya kujifunza na kuweka bidii katika mafunzo yao ya vitendo mahali walipo. 

"Hawa wanataaluma wanapaswa kuonyesha tabia njema wakati wa mafunzo, kuwa watiifu, kulinda viapo vyao kuzingatia maadili ya taaluma zao na kujiheshimu katika lugha zao na hata mavazi wanayovaa mbele ya wateja wao ambao wengi ni wagonjwa na ndugu zao"Aliongeza. 

Hata hivyo Prof. Makubi ameyaagiza mabaraza hayo kuhakikisha utaratibu wa watarajali 'interns' wote kufanya mitihani baada ya mafuzo, uharakishwe ndani ya   mwaka huu ili serikali iweze kupima umahiri wa wanataaluma wote wanaomaliza mafunzo kwa vitendo.

Prof. Makubi aliipongeza Baraza la  Famasi  kwa kuratibu mitihani kwa wafamasia wataraji  na kulitaka  Baraza la Madaktari nalo likamilishe utaratibu wa mitihani kwa madaktari watarajali wote ili kulinda hadhi ya taaluma ya tiba na viwango vya kutoa huduma kwa wananchi.

Alhamisi, 17 Septemba 2020

WANATAALUMA WA SEKTA YA AFYA WAPEWA MIEZI SITA YA KUJISAJILI NA KUHUISHA LESENI ZAOMganga Mkuu wa Serikali wa Serikali Prof. Abel Makubi

Na. WAMJW-Dodoma

Wanataaluma wote wa sekta ya afya nchini wametakiwa wawe wamejisajili, na kuhuisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaalam ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Aidha kwa wale ambao wamejiendeleza zaidi kitalaamu wanatakiwa kuwasilisha(update) vyeti vyao vya viwango katika mabaraza ili kutambulika kisheria na kitaaluma. 

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akiongea na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalam ya Wizara ya Afya pamoja na wasajili wa bodi zilizo chini ya wizara hiyo.

“Kila mwanataaluma aliyemaliza mafunzo yake ni vizuri awe amesajiliwa katika mabaraza yao, agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika, na uzuri hivi sasa kuna tovuti hivyo mnaweza kupata kujisali , kulipia na baadae kutumiwa  vyeti vyenu bila kuchelewa.  Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita wawe wamesajiliwa”. Alisisitiza

Pia wanatataaluma wanaojiendelea kwa ngazi mbalimbali ya taalauma ya afya kama uzamili na uzamivu 'PhD’ wanatakiwa kusajili hivi viwango katika mabaraza yao ili watambulike. 

Prof. Makubi amesema utaratibu huo umewekwa na Serikali kupitia mabaraza hayo hivyo kila mwana taaluma anatakiwa kujisajili au kuhuisha leseni ambazo zimeisha muda ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.

Aidha,Prof. Makubi ameongeza kuwa wizara kupitia mabaraza hayo imeweka miundombinu ya mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa kila taaluma kwa kufanya mitihani kwa ngazi zote."Lakini mtu aliyefanya mtihani nje ya utaratibu huu basi anatakiwa kuleta  ili kufanya usajili ili kupata alama na uwekwe kwenye kiwango stahili na ndio utaonekana bado upo kwenye kiwango cha uelewa kwenye taaluma yako na kuwatumikia wananchi”.

Kwa upande wa baadhi ya watu wa sekta ya afya wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma, Prof. Makubi ametoa miezi mitatu kwa wale wanataaluma wenye vyeti vyao wajisajilii ili kutambulika wapo katika kiwango fulani cha taaluma. 

“Kuna baadhi ya wataaluma wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha kitaaluma wakati hawajasajili vyeti vyao  kwenye mabaraza, nitoe mfano kuna wanataaluma wanaojiita mabingwa wa kitu fulani (specialist, consultant …) na wanajitangaza kwa wananchi wakati hatuna ushahidi na kumbukumbu. Kwahiyo tumekubaliana na mabaraza suala hilo sasa lifikie mwisho na wote waliojiendeleza zaidi waje wajisajili haraka kwa kuwasilisha vyeti vyao.” Alisisitiza Prof. Makubi.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Serikali aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa Hsopitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kuzingatia kusimamia utekelezaji wa maagizo haya kwenye sekta zote za afya ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma husika. “Taaluma zote za afya lazima ziendelee kuheshimika na kusimamiwa vizuri ili kulinda afya za wananchi kwa viwango vya juu na bila kuruhusu wanataaluma bubu”, Alisema Prof Makubi.

Pia kwa Waganga wa tiba asili wametakiwa kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala kwani serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano kwa kuwasaidia malengo yao ya utoaji wa tiba asili yanafanikiwa.

-MWISHO-

Jumatatu, 7 Septemba 2020

TANZANIA YATOKOMEZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU MWAKA MMOJA SASA

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 
Dkt. Leonard Subi

Na Gerard Chami - WAMJW, Arusha. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kutokomeza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu (Cholera) hapa nchini.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi wakati akizindua kikao kazi cha kufanya tathmini, maboresho na kuandaa mpango kazi wa miaka mitano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini. 


“Tangu mwezi Julai mwaka 2019 hatuna kesi yoyote iliyotolewa taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa Cholera hapa nchini. Kwa miaka kadhaa tumekua na takribani asilimia 11 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanyika katika maeneo tofauti ikiwemo kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, kaya karibu zote nchini kuwa na vyoo safi na bora, kuimarishwa kwa usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama nchini kipindupindu kilipungua mpaka asilimia 1.7 na kwa kipindi cha mwaka jana hadi sasa hatuna mgonjwa aliyetolewa taarifa kabisa kuwa na maambukizi hayo.” Amesema Dkt.Subi 


Amesema, kazi iliyopo hivi sasa na inayopewa kipaumbele na Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuchambua kwa umakini mkubwa mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa ugonjwa huu, kufanya ufuatiliaji, tathmini na uperembaji wa afua mbalimbali za afya hapa nchini na kuja na mpango kazi wa utekelezaji kimkakati katika kudumisha hali hii hapa nchini kwani hivi sasa nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo ni vema kudumisha hali ya afya ya wananchi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo, kukuza kipato na kuboresha hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja. 


Aidha Dkt.Subi amesisitiza kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono muda wote kwa maji safi yanayotiririka na sabuni kwani unasaidia kukabiliana na maradhi mengine zaidi ya Corona ikiwa ni pamoja na kudumishwa kwa utoaji elimu ya afya kwa umma ili twende pamoja kama taifa linaloendelea kwa kasi. 


Akiongezea Dkt.Subi amesema ni vema kwa pamoja tukaendelea kuongeza nguvu na ushirikiano katika kulinda vyanzo na mikondo ya maji safi na salama kwani maji ni uhai na uhai ni afya hivyo itatusaidia kama Taifa kupambana na maradhi mbalimbali mijini na vijijini. 


Vilevile Dkt.Subi amesema suala la chanjo ya kuzuia kipindupindu kwasasa sio kipaumbele na badala yake nguvu kubwa inazidi kuwekwa katika kuimarisha miundombinu stahiki ya huduma za afya, usafi zaidi wa mazingira na upatikanaji zaidi wa maji safi kwa wananchi katika maeneo yote. 


Nae Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa eneo la Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa Dkt.Janeth Mghamba akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ameahidi kwa niaba ya timu za wataalamu wa afya kuendelea kuwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa katika jamii wanazotoka (kata, mitaa na vijiji), kusukuma uimarishaji wa maabara katika ngazi zote; mkoa, wilaya, zahanati na halmashauri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu. 


Pamoja nae, Dkt.Faraja Msemwa kwa niaba ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umoja na mshikamano uliopo kwa kuwaweka wadau wa maendeleo karibu katika kukabiliana na majanga ya maradhi mbalimbali hapa nchini na yale yanayoikumba dunia kwa ujumla wake kwani afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote. 


Mwisho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg.Gerard Chami, amewataka wanahabari kuendelea kutumia vyombo vyao ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuelimisha umma juu ya utunzaji wa mazingira, matumizi sahihi na utunzaji wa vyoo bora, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kudumisha utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka na sabuni. 

Mwisho

Jumatatu, 31 Agosti 2020

SIMAMIENI USAJILI WA DAWA ZA ASILI KWA KUTOA ELIMU YAKUTOSHA KWA WATENGENEZAJI - PROF. MCHEMBE.

- Hakuna maoni

KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe akisema jambo  kwa wadau (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Siku ya Tiba ya Asili kwa Mwafrika

Dkt. Grace Magembe Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya

Mzee Issa Mdoe Mwakilishi wa Wagaga wa Tiba asili kutoka Mkoa wa Dodoma


Na WAMJW- DOM 

KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewaagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili. 

Prof. Mchembe ameyasema hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu ya "Miongo miwili ya Tiba Asili Afrika 2001 mpaka 2020 Nchi zina mafanikio gani".

"Kwa maana hiyo basi nawaagiza Baraza la Tiba Asili na tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili" alisema Prof. Mabula Mchembe. 

Aliendelea kusisitiza kuwa, ni vyema Baraza la tiba asili na Mamlaka zote nchini, kushirikiana na taasisi zote zinazohusiana na tiba asili hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutokana na kuwepo kwa kitengo kinachohusiana na mimea. 

Prof. Mchembe amesema kuwa, katika kuadhimisha miaka 18 ya siku ya tiba asili ya Mwafrika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mambo mengi ikiwemo, kuitambua huduma ya tiba asili katika Sera ya Afya kuanzia, kutungwa kwa Sheria ya tiba asili na tiba mbadala Namba 23 ya mwaka, kutengenezwa kwa kanuni na miongozo mbalimbali ya Tiba Asili na Tiba Mbadala mwaka, kuanza kutoa mafunzo kwa Waratibu na watoa huduma wa tiba asili nchini.

Aidha Prof. Mchembe, ameliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili.

Mbali na hayo Prof. Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini kutumia fursa kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake. 

"Nitoe wito kwa Waganga na wadau wa Tiba Asili kutumia fursa iliyopo ya Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake" alisema Prof. Mchembe 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe amesema kuwa, kupitia maadhimisho ya tiba asili kama nchi tumepata mafanikio mengi sana ikiwemo kuongezeka idadi kubwa ya wananchi wanaotumia dawa za asili hususan katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona. 

"Kupitia maadhimisho ya tiba asili, tangu tumeanza kama nchi, Luna mafanikio mengi sana yameweza kupatikana, lakini kubwa naloweza kulisemea, ni kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaotumia dawa zetu za asili pamoja na tiba mbadala, na mfano mzuri ni katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, kama nchi tunaweza kusimama kifua mbele na kusema tiba zetu za asili zimetutoa kwa kiwango kikubwa, " alisema. 

Aliendelea kusema kuwa, pamoja na kuendelea na utafiti wa dawa mbali mbali za asili ambazo zilitumika katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, takribani zaidi ya watu 100,018 walitumia dawa za asili, ikiwemo njia ya kujifukiza (nyungu), na kuonesha mafanikio kwa kiasi kikubwa. 

Nae Kaimu Msajili Baraza la tiba asili na tiba mbadala Wizara ya Afya Ndg. Patrick Seme amesema kuwa, hadi sasa Baraza la tiba asili na tiba mbadala limeshasajili dawa 30, huku akiweka wazi kuwa kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa ni kidogo ukilinganisha na uhalisia, huku akiweka wazi kuwa Baraza linaendelea kuhakikisha linasajili dawa nyingi zaidi kwa kufuata kanuni na taratibu. 

"Kama mnavyofahamu kuwa mwaka 2017 tulianza kusajili dawa za asili kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kuwa hadi sasa dawa 30 zimesajiliwa. Kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa nichache sana ukilinganisha na uhalisia." Alisema. 

Akiwawawakilisha Waganga wa tiba asili Mkoa wa Dodoma Mzee Issa Mdoe amesema kuwa, Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kushirikiana na Waganga wa tiba asili limekuwa na mafanikio mengi yakiwemo kutoa elimu mara kwa mara kwa Waganga kujua dhana ya tiba asili ikiwemo kujiepusha na mauaji ya vikongwe na mauaji ya albono na mauaji ya watoto wadogo. 

Mbali na hayo Mzee Issa Mdoe ameweka wazi kuwa, baadhi ya changamoto zinazowakumba, zikiwemo gharama za usajili wa dawa kuwa juu, hivyo kuwafanya Waganga wengi kushindwa kisajili dawa zao, elimu ndogo ya malipo ya njia ya elektroniki inayopelekea baadhi ya Waganga katapeliwa na watu wasio waaminifu.

Mwisho.