Na Englibert Kayombo, WAMJW - MWANZA
Watumishi wa kada ya afya nchini wameaswa kuhakikisha wanadhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kuwajibika ipasavyo wakiwa kazini na kuepukana na tabia za uzembe.
Kauli hiyo imetolewa na na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapologwe alipokuwa akizungumza na timu ya afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa mkoa huo.
“Suala la vifo, pasipokuwepo na uwajibikaji na umoja ni vigumu sana kuweza kulifanikisha, kuchukua hatua imekuwa changamoto kwa timu nyingi hivyo kupelea kuongezeka kwa vifo” amesema Dkt. Ntuli.
Ameendelea kusema kuwa wataalam wa afya hawatakiwi kuoneana aibu endapo mjumbe wa timu hatofanya kazi yake ipasavyo kwa uzembe wake mwenyewe achukuliwe hatua za kinidhamu ili kuweza kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.
Amesema kuwa wataalam wa afya wanapaswa kuwa wamoja na kushirikiana kikamilifu wakiwa kazini na kuacha kusubiri wataalam kutoka ngazi ya juu kuja kutoa maamuzi ya vitu ambavyo vingewezwa kufanywa na viongozi katika eneo husika.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel Tutuba amesema vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vimekuwa viongezeka mkoani humo na kuwataka watumishi wa kada ya afya kuhakikisha wanapunguza kiwango cha vifo hivyo kwa mkoa huo ambao ni kinara wa huduma bora za afya katika Kanda ya Ziwa.
Akitaja takwimu za vifo hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Tutuba amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 vifo vilikuwa 145, mwaka 2016 vifo 151, mwaka 2017 vifo 193, mwaka 2018 vifo 151, mwaka 2019 vifo 171 na kwa mwaka huu mpaka kufikia mwezi Septemba vimetokea vifo 142.
“Lazima tukae tutafakari, licha ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya lakini vifo vinaongezeka, tunapokutana hivi tusiishie tuu kupashiana, ni lazima tutimize wajibu wetu” amesisitiza Bw. Tutuba.
Hata hivyo Bw. Tutuba amepongeza watumishi wa kada ya afya mkoani humo kwa juhudi zao wanazofanya kuhakikisha wanaokoa maisha ya watanzania pamoja na raia wa kigeni wanaokuja mkoani humo kwa ajili ya huduma za matibabu.
“Tumejitahidi kufanya mazuri mengi, lakini badi hatujatekeleza kwa asilimia 100, tumefanya vizuri lakini bado tungeweza kufanya vizuri zaidi endapo kila mmoja angetimiza wajibu wake” amesema Bw. Tutuba.
Mwisho
0 on: " WATUMISHI KADA YA AFYA WAASWA KUDHIBITI VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI NA WATOTO WACHANGA."