Na Englibert Kayombo WAF – Singida
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wataalam wa afya nchini kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukoma ili ifikapo Mwaka 2030 ugonjwa huo uwe umetokomea nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo leo kwenye Siku ya Kitaifa ya kuadhimisha Siku ya Ukoma Duniani iliyofanyika katika eneo la Sukamahela katika Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida.
“Niwapongeze wataalam wamefanya kazi nzuri sana ya kuwatambua wenye Ukoma lakini bado tuna kazi kubwa mbele yetu kwasababu tunataka miaka 9 ijayo kabla ya mwaka 2030 Ukoma uwe historia ndani ya Tanzania. amesema Dkt. Mollel.
Amesema wataalam wa afya pamoja na wadau wakiunganisha nguvu za pamoja na kushirikishana mikakati na afua mbalimbali za mapambano, Ugonjwa huo unaweza kuwa umetokomea hata kabla ya kufikia mwaka 2030.
“Ni lazima tushikamane, tusiishie kwenye kutunza utu wa watu wenye Ukoma tuu lakini tuhakikishe hakuna mwingine anayekwenda kupata ukoma, na hata kama yupo basi tuhakikishe tunamtambua mapema ili tumsaidie asiweze kupata ulemavu” amesisitiza Dkt. Mollel.
“Ni lazima tuutokomeze Ukoma; dawa za kuponyesha Ukoma tunazo na zinatolewa bila malipo, kiwango cha maambukizi mapya kimeshuka na kufikia chini ya asilimia 5, na pia asilimia 90 ya wagonjwa wote wapya tunawaowaibua ni wagonjwa walioambukizwa miaka mingi iliyopita” amefafanua Dkt. Mollel
Dkt. Mollel ameagiza fedha zinazotengwa na Serikali pamoja na kutolewa na wadau wa maendeleo ziwe zinaenda kushughulikia mapambano ya kutokomeza Ukoma.
“Fedha nyingi sana zinaweza kuwa zinatumika kujadili kuhusu Ukoma, kufanya Semina za Ukoma na kumjadili mgonjwa wa Ukoma kuliko hata fedha zinazokwenda kumsaidia mgonjwa mwenyewe” ameendelea kusema Dkt. Mollel.
Amewataka wataalam wa afya kubadilisha mikakati ya mapambano dhidi ya Ukoma kwa kuwafikia wagonjwa walipo pamoja na kutoa elimu zaidi kwa wananchi dhidi ya Ugonjwa wa Ukoma.