Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumamosi, 23 Mei 2020

WANAWAKE WENYE TATIZO LA FISTULA WATAKIWA KWENDA KUPATA MATIBABU MAPEMA

- Hakuna maoni

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu

Na WAMJW-Dodoma

Wanawake wenye matatizo ya Fistula nchini wametakiwa kuacha tabia ya kujifungia ndani na badala yake wametakiwa kwenda kupata matibabu katika Hospitali zilizoainishwa na Serikali bila gharama yeyote.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika kuadhimisha siku ya Fistula duniani inayoadhimishwa tarehe 23 Mwezi Mei kila Mwaka, yenye kauli mbiu mwaka huu inayosema “Tokomeza unyanyasaji wa kijinsia: Tokomeza huduma ya afya isiyo na usawa; Tokomeza Fistula sasa!”.

Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa kuna wanawake takribani millioni mbili (2,000,000) wanaoishi na Fistula Duniani kote. Inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya kati ya 50,000 na 100,000 hupatikana kila mwaka, wakati juhudi za kutibu Fistula ulimwenguni kote huishia kutibu wagonjwa 20,000 tu.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy amesema inakadiriwa kuwa na wanawake takribani 2500 ambao wanapata fistula kila mwaka, huku idadi ya wanaopatiwa matibabu ikiwa ni  takribani wanawake 1,000 na kuongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika matibabu haya.

“Katika kipindi cha miaka Mitano kuanzia 2015 hadi Disemba, 2019 wanawake zaidi ya 5,500 wametibiwa Fistula. Mafanikio haya yanatokana na kampeni iliyoendeshwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na Wadau ambayo imeweka Mabalozi wa Fistula zaidi ya 3,000 nchi nzima wanaosaidia kuratibu rufaa na usafiri kwa wagonjwa kwenda Hospitali zinazotoa huduma ya Fistula”.  Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametaja takwimu zinazoonyesha kuwa idadi ya Wanawake wanaojitokeza kutibiwa Fistula kwenye Hospitaii za CCBRT, Bugando, Nkinga na Kuvulini Maternity Center imepungua kwa zaidi ya 30% kuanzia mwaka 2015 mpaka 2019. Mwaka 2015, wanawake 1337 walipatiwa matibabu ya Fistula, Mwaka 2016 walikuwa 1356, mwaka 2017 idadi hiyo ikashuka na kufikia 1060, mwaka 2018 ikashuka tena na kufikia  idadi ya wanawake 900, na mwaka 2019 ikashuka zaidi na kufikia wanawake 852.  Hii imetokana na kuimarika kwa huduma za Afya ya mama wajawazito ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

Waziri Ummy amewataka akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki mara tu anapojihisi mjamzito ili kuweza kuchunguza afya yake pamoja na mtoto.

“Mama mjamzito endapo atawahi kliniki mapema kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na mtoto na kuhakikisha anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya atapunguza uwezekano wa kupata tatizo la Fistula. Nitumie fursa hii kuendelea kuhimiza akina mama wajawazito kuwahi kliniki mapema, kukamilisha mahudhurio yote manne na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya”. Ameongeza Waziri Ummy.

Huduma za Fistula nchini zinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, CCBRT, Bugando, Hospitali ya Kanda ya Rufaa-Mbeya, Hospitali ya Nkinga Tabora, KCMC na Kivulini Maternity Center iliyoko Arusha. Tuna wataalamu waliobobea kwenye tiba ya Fistula kwenye Hospitali hizi.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy amesema ili kutokomeza Fistula nchini kunahitajika juhudi za pamoja za wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa Afya kwenye ngazi zote, Wizara mbalimbali, wadau wa Maendeleo, Wanahabari na Mashirika ambayo yamekuwa yakijihusisha na uhamasishaji wa matibabu ya Fistula. 

MWISHO

Alhamisi, 21 Mei 2020

SERIKALI INAHAKIKISHA WALENGWA WOTE WA CHANJO WANAFIKIWA KATIKA KIPINDI CHA CORONA

- Hakuna maoni


Na Mwandishi Maalum – Pwani
20/05/2020 Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imejipanga kuwafikia walengwa wote waliostahili kupata chanjo na kuhakikisha kiwango kinabaki vilevile kama ilivyotarajiwa.
Hayo yamesemwa leo na Ofisa Mradi kutoka Mpango huo Lotalis Gadau wakati wa usimamizi elekezi wa kukagua utoaji huduma za chanjo  katika Mkoa wa Pwani  kwa kushirikiana na Engender Health kupitia Merck Sharp& Dohme B.V (MSD).
Gadau alisema kuwa katika kipindi hiki cha nchi kukabiliana na Ugonjwa wa Corona, Wizara imejipanga kuhakikisha watoa huduma wa afya wanaendelea kutoa huduma za chanjo kwa watoto wadogo pamoja na wasichana ambao walikua wapate chanjo ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi(HPV).
“Kama Wizara tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha chanjo zote zinakuwepo kwa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha watoto wote waliokuwa wanatarajia kupata chanjo wanapata,na watoa huduma wanachukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu”,
Alisema walikuwa wakisikia wananchi wana wasiwasi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma,“tumepita kwenye vituo vya afya kwenye mkoa huu na tumeona hali ni zuri kwani wazazi na mabinti wengi wanakuja kwenye vituo na tumewasisitiza kila mmoja anayeenda awe balozi anaporudi nyumbani kuhakikisha wataambiana ili kila anayestahili kupata chanjo anaenda kwenye kituo cha afya chochote cha jirani aweze kupata chanjo”.
Vile vile alisema kuhusu mabinti ambao walikua wapate  chanjo ya kuzuia  saratani ya malango wa kizazi  tofauti na awali ambapo walikua wakifuatwa mashuleni ila kutokana na janga  la Corona inasisitizwa wafike kwenye  vituo cha kutolea huduma za afya  vya karibu waweze kupata chanjo hiyo.

 Upande wa watoto wadogo, Bi. Gadau amesema hivi sasa umewekwa utaratibu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili ambao wanastahili kupatiwa chanjo wao wanatakiwa kupata chanjo kama ilivyo kawaida”Kwa kipindi hiki watoto ambao wamekamilisha ratiba ya chanjo na wanafika kituoni kwa ajili ya uzito tu wao wanatakiwa waende kila baada ya miezi mitatu hii ni kuepuka misongamano na tunasisitiza elimu ya afya ambayo ilikua ikitolewa kwa muda mrefu au kusubiriana kwa sasa  itatolewa kwa muda mfupi usiopungua dakika tano lakini endapo mtoto atapata homa au tatizo lolote anatakiwa kupekekwa kwenye kituo cha afya kwa ajili ya matitabu.
Naye Mratibu Huduma za Chanjo kwa Mkoa wa Pwani Abbas Hincha amesema kuwa asilimia 90 ya walengwa wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka 14 ambao hapo awali walikuwa wakipatiwa wakiwa shuleni ila kutokana na janga hili wanashirikia na walimu wa shule zao kwani walikua wameandikishwa hivyo wanawapatia namba za simu na kuwapigia wazazi na walezi ili kuwapeleka kupatiwa chanjo hiyo.
Alisema katika mkoa wake wamepanga mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuwashirikisha  watoa huduma ngazi ya jamii kuwatafuta mabinti hao kwenye maeneo yao na kuwakumbusha kwenda kupata chanjo.
Alisema muamko kwa chanjo kwa upande wa watoto wadogo unaendelea vizuri na kuna muitikio mzuri hivyo wanaendela kutoa elimu jinsi ya kujikinga na Corona na kwenye vituo ambavyo havina nafasi kubwa wanatoa huduma hizo nje ya kituo ili kuzingatia umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu

WAHIMIZWA KUJIPANGA, KUENDELEA KUTOA HUDUMA ZA MKOBA ZA CHANJO

- Hakuna maoni
Bi. Ipyana Mwamwala Muuguzi Mkunga wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba akimpima uzito mtoto Niran Daudi (7) pembeni ni mama wa mtoto huyo, Bi. Joyce Mwantobe. Picha na Englibert Kayombo

Bi. Elinivoniia Mchomvu Muunguzi Mkunga akisoma kitabu cha afya ya mtoto kabla ya kutoa chanjo katika Zahanati ya Fulwe, Wilaya ya Morogoro VIjijini. Picha na Englibert Kayombo


Ofisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Lugata akitoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa Corona.kwa wananchi waliofika katika Kituo cha Afya Mtego wa Simba Wilaya ya Morogoro Vijijini kupata huduma za afya

Ofisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, unaosimamiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Furaha Kyesi (kushoto) akimzungumza jambo na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba, Luambano Ally

Wananchi wakiingia katika Kituo cha Afya Mtego wa Simba kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono kwa maji yanayoririka na sabuni na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine


 Mwandishi Maalum - Morogoro
Huduma ya chanjo za mkoba hasa katika maeneo ya pembezoni (vijijini) zinapaswa kuendelea kutolewa kwa watoto chini ya miaka mitano ili kuhakikisha wote wanafikiwa kwa wakati unaopaswa, licha ya kuwapo kwa janga la Corona.

Pamoja na kundi hilo, kundi jingine linalopaswa kufikiwa na kupatiwa chanjo ya ni wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao wanapaswa kupatiwa ile ya HPV inayokinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo vinavyosabisha ugonjwa wa saratani ya kizazi.

Rai hiyo imetolewa jana na Ofisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara hiyo, Dk. Furaha Kyesi alipozungumza na uongozi wa Kituo cha Afya Mtego wa Simba, kilichopo Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro wakati wa ziara ya ukaguzi wa huduma za chanjo zinazotolewa kwenye vituo vya afya kipindi hiki cha mapambano dhidi ya janga la Corona.

Timu ya ufuatiliaji huduma za chanjo kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD) wa Wizara hiyo, maofisa chanjo wa Mkoa wa Morogoro na wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Engeder Health kupitia Merck Sharp & Dohme B.V (MSD), wapo mkoani humo kukagua namna huduma za chanjo zinavyoendelea kutolewa katika kipindi hiki cha janga la Corona.

“Kundi hili la wasichana lazima tuhakikishe tunalifikia, kwa sababu hawa awali msisitizo ulikuwa kuwapa chanjo kwa kuwafikia shuleni, lakini sasa shule zimefungwa kutokana na janga la Corona, lakini tunahitaji kuwafikia.

“Watoto chini ya miaka mitano nao lazima tuwafikie ili kwamba wakati tunapambana na Corona tuhakikishe pia tunaendelea kuwapa chanjo dhidi ya magonjwa mengine kama vile surua, polio, kuharisha na mengineyo, ili tusije tukapata mlipuko wa magonjwa,” amesema.

Kyesi ameshauri kwamba watoa huduma za afya waendelee kuzingatia mwongozo wa kujikinga na kufikia maeneo ya pembezoni hasa huko vijijini kuwapa huduma.

Awali akizungumza, Muuguzi Mkunga wa Kituo hicho, Ipyana Mwamwala alisema kila mwezi hupokea watoto wapatao saba na kuwapa chanjo mbalimbali kulingana na umri wao.

Amesema kituo hicho kimezungukwa na vijiji vinne ambavyo ni Sangasanga, New Land, Mkono wa Mara, Mkambarani na Mtego wa Simba (chenyewe).

“Wakina mama bado wana mwamko wa kuleta watoto kituoni lakini tunahitaji kwenda outreach kwa ajili ya kuwafikia pia wale ambao hawaji kituoni, vijiji vipo mbali na hapa,” amesema.

Ameongeza “Tupo tayari kwenda, tunatambua, tumetangaziwa kuna ugonjwa wa COVID -19 nchini ambao unatokana na maambukizi ya virusi vya Corona, hata hapa kituoni tumechukua hatua na hata tukienda kule tutazingatia kanuni zote za kujikinga sisi wenyewe na wale tunaokwenda kuwahudumia wasipate maambukizi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Luambano Ally amesema kutokana na taarifa hiyo ya tahadhari iliyotolewa na Wizara ya Afya, walilazimika kuchukua hatua za kuimarisha kujikinga ikiwamo kuweka ndoo za maji katika maeneo ya kuingia ndani ya kituo hicho.

“Kwenye milango yote ya kuingia ndani ya kituo kuna ndoo ya maji safi tiririka na sabuni lazima mtu anawe ndipo aingie huku ndani, lakini kama amejisahau kunawa pale au anahitaji tena kunawa akiwa humu ndani, kuna ndoo nyingine tumeweka ataweza kunawa pia.

“Hapa kituoni tumewapa taarifa kwamba kila anayekuja kupata huduma lazima avae barakoa, utaona hilo wanakijiji wanalitii na wamekuwa na mwamko, wanakuja wakiwa wamevaa, wananawa mikono, wanapata huduma na kurudi zao nyumbani,” amesema Ally.

MWISHO