Waziri wa Afya, Dkt. Ndugulile akifafanua jambo baada ya kumalizika kwa mkutano kujadili jinsi ya kupambana na Covid-19 nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya. |
Dkt. Ndugulile akijadiliana jambo pamoja na watafiti wa taasisi hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya utafiti kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) kwa kuwa kuna tofauti kubwa ya dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa hapa nchini ukilinganisha na wagonjwa waliopo nje ya nchi.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipokutana na watafiti wa taasisi hiyo wakati wakijadili maambukizi ya ugonjwa wa Corona na aina ya matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa hasa baada ya kubainika kuwa dalili za ugonjwa huo zinatofautiana na dalili za wagonjwa wa mataifa mengine.
“Kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti wa kisanyansi, moja ni uelewa wa jamii, tunataka kujua wagonjwa wanaougua Corona ni wagonjwa wa namna gani, wana magonjwa ya aina gani, dalili zinazowapata wagonjwa ni za aina gani. Hapa tunataka tupate uwelewa,” amesema Dkt. Ndugulile.
Pia, amesema kupitia utafiti huo wanataka kujua aina za matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa ili kuhakikisha ugonjwa wa Covid-19 unadhibitiwa hapa nchini.
“Kutokana na muitikio mkubwa wa tiba asili na tiba mbadala, kupitia kikao hiki nawaelekeza wataalamu wetu wajipange kufanya utafiti na kutoa majibu ya tiba ya maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Dkt. Ndugulile.
Amesema wamekubaliana na watafiti hao kufanyia kazi maagizo hayo ndani ya muda mfupi na kutoa majibu sahihi ambayo yatasaidia katika mapambano ya ugonjwa wa Corona.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya amesema mapambano dhidi ya ugonjwa Covid-19 ni vita ambayo inapaswa kufanyiwa utafiti ambao utasaidia kupatikana kwa njia sahihi za kukabiliana na maambukizi ya ugponjwa huo.
“Tunafahamu kwamba jamii za kiafrika zina utaalamu katika miti shamba. Katika hili kuna tafiti mbalimbali zinaendelea ili kuchunguza uwezo wa miti shamba kwa lengo la kupunguza makali ya Covid-19.
Mwisho
0 on: "DKT. NDUGULILE AIAGIZA NIMR KUFANYA UTAFITI KUHUSU UGONJWA WA CORONA"