Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu
Na
WAMJW-Dodoma
Wanawake
wenye matatizo ya Fistula nchini wametakiwa kuacha tabia ya kujifungia ndani na
badala yake wametakiwa kwenda kupata matibabu katika Hospitali zilizoainishwa na
Serikali bila gharama yeyote.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika kuadhimisha
siku ya Fistula duniani inayoadhimishwa tarehe 23 Mwezi Mei kila Mwaka, yenye
kauli mbiu mwaka huu inayosema “Tokomeza unyanyasaji wa kijinsia: Tokomeza huduma
ya afya isiyo na usawa; Tokomeza Fistula sasa!”.
Waziri
Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa
kuna wanawake takribani millioni mbili (2,000,000) wanaoishi na Fistula Duniani
kote. Inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya kati ya 50,000 na 100,000 hupatikana kila
mwaka, wakati juhudi za kutibu Fistula ulimwenguni kote huishia kutibu wagonjwa
20,000 tu.
Kwa
upande wa Tanzania, Waziri Ummy amesema inakadiriwa kuwa na wanawake takribani
2500 ambao wanapata fistula kila mwaka, huku idadi ya wanaopatiwa matibabu
ikiwa ni takribani wanawake 1,000 na
kuongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika matibabu haya.
“Katika
kipindi cha miaka Mitano kuanzia 2015 hadi Disemba, 2019 wanawake zaidi ya
5,500 wametibiwa Fistula. Mafanikio haya yanatokana na kampeni iliyoendeshwa
kwa ushirikiano baina ya Serikali na Wadau ambayo imeweka Mabalozi wa Fistula
zaidi ya 3,000 nchi nzima wanaosaidia kuratibu rufaa na usafiri kwa wagonjwa
kwenda Hospitali zinazotoa huduma ya Fistula”.
Amesema Waziri Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy ametaja takwimu zinazoonyesha kuwa idadi ya Wanawake wanaojitokeza
kutibiwa Fistula kwenye Hospitaii za CCBRT, Bugando, Nkinga na Kuvulini Maternity
Center imepungua kwa zaidi ya 30% kuanzia mwaka 2015 mpaka 2019. Mwaka 2015,
wanawake 1337 walipatiwa matibabu ya Fistula, Mwaka 2016 walikuwa 1356, mwaka
2017 idadi hiyo ikashuka na kufikia 1060, mwaka 2018 ikashuka tena na
kufikia idadi ya wanawake 900, na mwaka
2019 ikashuka zaidi na kufikia wanawake 852.
Hii imetokana na kuimarika kwa huduma za Afya ya mama wajawazito ikiwa
ni pamoja na upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura chini ya Uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.
Waziri
Ummy amewataka akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki mara tu anapojihisi
mjamzito ili kuweza kuchunguza afya yake pamoja na mtoto.
“Mama
mjamzito endapo atawahi kliniki mapema kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya
afya yake na mtoto na kuhakikisha anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma
za afya atapunguza uwezekano wa kupata tatizo la Fistula. Nitumie fursa hii
kuendelea kuhimiza akina mama wajawazito kuwahi kliniki mapema, kukamilisha
mahudhurio yote manne na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya”.
Ameongeza Waziri Ummy.
Huduma
za Fistula nchini zinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, CCBRT,
Bugando, Hospitali ya Kanda ya Rufaa-Mbeya, Hospitali ya Nkinga Tabora, KCMC na
Kivulini Maternity Center iliyoko Arusha. Tuna wataalamu waliobobea kwenye tiba
ya Fistula kwenye Hospitali hizi.
Pamoja
na hayo, Waziri Ummy amesema ili kutokomeza Fistula nchini kunahitajika juhudi
za pamoja za wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa Afya kwenye ngazi zote,
Wizara mbalimbali, wadau wa Maendeleo, Wanahabari na Mashirika ambayo yamekuwa
yakijihusisha na uhamasishaji wa matibabu ya Fistula.
MWISHO
0 on: "WANAWAKE WENYE TATIZO LA FISTULA WATAKIWA KWENDA KUPATA MATIBABU MAPEMA"