Baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa kituo cha afya cha Buigiri waliojitokeza kushuhudia makabidhiano ya Hadubini mpya za kupima kifua kikuu zilizotolewa na Wizara ya Afya.
Na WAJMW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto
Mhe. Ummy Mwalimu amesema maambukizi ya Kifua Kikuu (TB) yamepungua nchini
kutoka wagonjwa 164,000 mwaka 2015 hadi kufikia
wagonjwa 142,000 mwaka 2018.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akikabidhi Hadubini 57
katika Mkoa wa Dodoma zitakazotumika kufanya vipimo vya ugonjwa wa Kifua Kikuu
ambazo zitasambazwa katika Hospitali na Vituo vya Afya mbalimbali mkoani humo.
“Leo nimeanza zoezi la kukabidhi Hadubini 941 zilizonunuliwa
na Serikali kwa ufadhili ya Global Fund zenye thamani ya Tsh. Bilioni 3.3
ambapo leo nitamkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binilith Mahenge Hadubini 7
za Wilaya ya Chamwino zitakazosambazwa katika vituo vya Afya mbalimbali”.
Amesema Waziri Ummy.
Pamoja na hayo Waziri Ummy ametumia muda huo kueleza
mafanikio yaliyofikiwa na Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma ikiwa ni
pamoja na kupungua maambukizi mapya kwa asilimia 18 lengo likiwa ni asilimia 20
na vifo vimepungua kwa asilimia 27 lengo likiwa ni asilimia 35.
Aidha, Waziri Ummy amesema ugunduzi wa Kifua Kikuu
unaendelea kuimarika ambapo idadi ya wagonjwa waliogundulika na kuwekwa kwenye
matibabu imeongezeka kutoka wagonjwa 62,180 mwaka 2015 hadi kufikia 82,,140
mwaka 2019.
Kwa upande wa vituo vya ugunduzi wa tiba, Waziri Ummy
amesema katika kipindi cha miaka mitatu vituo vimeongezeka kutoka 662 mwaka
2016 hadi kufikia vituo 1201 mwaka 2019.
Katika kipindi cha miaka idadi ya wagonjwa waliogundulika
kuwa na Kifua Kikuu imepungua kutoka wagonjwa 164,000 mwaka 2015 hadi 142,000
mwaka 2018.
Waziri Ummy amesema vifo vinavyotokana na TB vimepungua kutoka makadirio ya vifo 30,000 mwaka 2015
hadi vifo 22,000 mwaka 2018.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Hadubini hizo zitapelekwa katika
vituo vipya vya kutolea Huduma za afya 487 ambavyo vimejengwa, Hospitali za
Mikoa 3, Hospitali za Wilaya 69 pamoja na vituo vya afya vya zamani 315 pia
kubadilisha hadubini zilizoharibika katika vile vituo vyenye uhitaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge
ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutambua ulazima wa kuwepo Hadubini
hizo katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya lengo likiwa ni kuondoa
usumbufu kwa wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
MWISHO
|
0 on: "WAZIRI UMMY AMESEMA UGONJWA WA KIFUA KIKUU UNAENDELEA KUPUNGUA NCHINI"