Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 29 Juni 2020

MILIONI 780 KUJENGA KLINIKI YA HUDUMA ZA METHADONE MKOA WA TANGA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za methadone Mkoa wa Tanga
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akikata upete wakiati akifungua rasmi kliniki ya huduma za methadone katika Mkoa wa Tanga, kushoto ni Mkuu Wa Mkoa wa Tanga Mhe. MArtin Shigela na aliye upande wa kulia ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Bw. James Kaji


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya wakipongeza kwa furaha wakati Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akimpatia dawa ya methadone kwa mnufaika wa huduma hiyo iliyozinduliwa mkoani humo.
 
Kamishna Jeneral wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Jamesi Kaji akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kiliniki ya huduma za methadone Mkoani Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akisema jambo wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za methadone kwa Mkoa wa Tanga.

 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela (kushoto) wakipokea maelekezo toka kwa msimamizi wa ujenzi wa jengo la huduma za tiba ya madawa ya kulevya linaloendelea kujengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga.

Ujenzi wa jengo la kliniki ya huduma za tiba ya madawa ya kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo Tanga ukiendelea ambapo uje zi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 780 za kitanzania.



Na WAMJW - Tanga
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaendelea kuboresha huduma za afya nchini ambapo shilingi milioni 780 zimetolewa kwa ajili ya kujenga kliniki ya huduma za methadone kwa waathirika wa madawa ya kulevya mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoo Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kituo cha muda cha kutoa tiba ya methadone kwa warahibu wa madawa ya kulevya kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo.
“Kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo Mfuko wa Dunia (Global Fund) na Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya tumepata zaidi ya milioni 780 na tumezileta kwa ajili ya kujenga jengo la kutolea huduma ya methadone” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo waziri ummy mwalimu hakusita kuupongeza uongozi wa mkoa wa tanga kwa ubunifu walioufanya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo PEPFAR na Amref -Tanzania, kwa kujenga kituo cha muda kwa ajili ya kutoa tiba kwa warahibu wa madawa ya kulevya ambacho kimegharibu shilingi milioni 20 za Kitanzania.
“Tumeona tunaweza kufanya huduma hizi kwa gharama nafuu, nnafurahi kuona kwamba zimetumika takribani shilingi milioni 20 kwa ajili ya kutengeneza kituo cha muda kwa huduma za kliniki katika Mkoa wa Tanga” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa ilikuwepo haja ya kuwa na kliniki ya methadone kwa Mkoa wa Tanga kutokana na kuwa na waathirika wengi wanaotumia madawa ya kulevya huku mkoa huo ukishika nafasi ya pili ya kuwa nawarahibu wengi wa madawa ya kulevya.
“Mkoa wa Tanga unashika nafasi ya pili ya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa madawa ya kulevya, takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Mkoa wa Tanga una watumiaji taribani 5190 wa madawa ya kulevya” amefafanua Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy amesema kuwa hadi sasa kuna kiliniki 8 ambazo zinatoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa Mkoa Wa Dar Es Salaam kliniki hizo zimeanzia katika hospitali ngazi ya mikoa na kushuka chini kwenye hospitali za ngazi ya halmashauri na kutaja maeneo yatakayofuata kuwa na huduma hizo ni pamoja na Bagamoyo, Kigamboni, Mbagala, Tegeta pamoja na Magereza Segerea.
Amesema kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Afya, Tanzania ina waathirika 8071 waoapatiwa huduma ya dawa za methadone kwa ajili ya kupunguza madhara ya dwa za kulevya ambapo kati yao wagonjwa 480 ni wanawake na 7591 ni wanaume.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Bw. James Kaji amesema kuwa wiki hii Tanzania inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kupinga madawa ya kulevya ambayo kwa mwaka huu kauli mbinu ni tujenge uelewa sahihi kwa tatizo la dawa za kulevya ili kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.
“Uzinduzi wa kituo hiki ni muendelezo wa vituo vingine 8 vinavyotoa huduma nchini ambapo kwa Dar es Salaam vipo vitatu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na Temeke; Mbeya – Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini; Mwanza – Hospitlai ya Rufaa ya Sekou Toure; Bagamoyo na Dodoma – Itega” amefafanua Kamishna Jenerali James Kaji  
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela amesema kuwa MKoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya shughuli za usafirishaji wa madawa ya kulevya na kufanya kuwa na idadi kubwa ya watumiaji ambao hiingia kwenye urahibu wa madawa hayo.
Aidha Mhe. Shigela ameiasa jamii kuepukana na matumizi ya madawa ya kulevya huku akiwaomba kutoa taarifa kwa mamlaka kwa wale wanaojihusisha na usafirishaji na biashara ya madawa ya kulevya.
“Kwa wale ambao wameathirika na madawa ya kulevya katika jamii zetu tuwaone ni kama sehemu ya ndugu zetu, tusiwanyanyapae, tuwaelekeze na tuwalete kwenye matibabu na tunaamini watarudi kwenye hali ya kawaida” amesisitiza Mhe. Shigela
 Mwisho.


Jumanne, 23 Juni 2020

UGONJWA WA CORONA USIWE KIGEZO CHA WATOTO KUKOSA CHANJO

- Hakuna maoni
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk.Ahmad Makuwani akisema jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) wakati wa semina ya huduma za chanjo.
Afisa Programu ya Chanjo wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau akisema jambo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Singida na Dodoma wakati wa semina ya huduma za chanjo nchini
Afisa Programu ya Chanjo wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau (aliyesimama) akisema jambo wa waandishi wa habari wa mikoa ya Singida na Dodoma kwenye semina ya huduma za chanjo Tanzania.

Waandishi wa habari wa mikoa ya Singida na Dodoma wakisikiliza wasilisho la mada wakati wa semina ya huduma za chanjo nchini.

Picha ya pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk.Ahmad Makuwani  watalaam pamoja na wanahabari wa Mkoa wa Dodoma.


Picha ya pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk.Ahmad Makuwani  watalaam pamoja na wanahabari wa Mkoa wa Singida.



 Na WAMJW - Dodoma

Serikali imeitaka jamii kuhakikisha watoto wanapata chanjo kipindi hichi chenye maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19) ili wapate kinga ya magonjwa mengine.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk.Ahmad Makuwani kwenye semina ya waandishi wa habari wa Mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu huduma za chanjo nchini.

Amesema maambukizi ya Corona kwasasa yamepungua na kuwataka watanzania kutotumia ugonjwa huo kama sababu ya kutowapeleka watoto kupata chanjo.

“Tulikuwa tunaenda vizuri lakini hivi karibuni idadi ya watoto na wasichana wanaopaswa kupata chanjo ya mlango wa kizazi imepungua, hizi chanjo ni muhimu sana jamii ipeleke watoto kwenye vituo wapate chanjo” amesema Dkt. Makuwani.

Amebainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kwasasa katika utoaji wa huduma za chanjo huku akidai kuwa kuna vituo zaidi ya 600 vinavyofanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Tunaamini mtatumia weledi wenu kuelimisha jamii kuhusu huduma ya chanjo mbalimbali zinazotolewa, wahimizeni wananchi kule vijijini wapeleke watoto wao kwa kuwa chanjo inatolewa kwenye vituo vya kutolea huduma" amesema Dkt Makuwani.

Amesisitiza kuwa waandishi waendelea kuhamasisha wananchi kunawa mikono kwa kuwa imesaidia kupunguza kasi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Awali, akizungumzia hali ya huduma za chanjo nchini, Ofisa Programu ya Chanjo wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau, alisema pamoja na jitihada za kuhakikisha magonjwa yanayizuilika kwa chanjo yanapewa kipaumbele kwa kuwapatia watoto chanjo lakini bado kuna jamii hazichanji watoto.

“Baadhi ya chanjo kiwango kipo chini ya kiwango kinachotakiwa, chanjo ya Surau na Rubella kitaifa tuna asilimia 76% ambayo iko chini ya kiwango cha utoaji wa huduma za chanjo ambayo inatakiwa kuwa asilimia 90” alisema Bi. Gadau kupitia tathmini ambazo hufanywa na Wizara kuona hali ya huduma za chanjo.

“Kuwepo kwa ugonjwa wa Corona sio sababu ya kutopeleka watoto kupata chanjo kwasababu wakichanjwa inasaidia kuwakinga na magonjwa mengi zaidi” amesisitiza Bi. Gadau.

Amesema kuwa Wizara imekuwa ikifanya usimamizi elekezi wa huduma za chanjo katika kipindi ambacho mlipuko wa ugonjwa wa corona ulivyoanza na shule kufungwa kuona hali ya utoaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwenye jamii ambapo wananchi wengi wamekuwa wakiogopa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakiogopa maambukizi na kuihamasisha jamii kwenda kupeleka watoto wao kupata chanjo hizo muhimu huku wakizingatia tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona.

Mwisho


Ijumaa, 19 Juni 2020

WAZIRI UMMY AZINDUA MWONGOZO WA MATIBABU YA SIKOSELI

- Hakuna maoni
Waziri Ummy Mwalimu akiwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakikata utepe kuzindua muongozo wa tiba ya wagonjwa wa Sikoseli nchini

Waziri Ummy Mwalimu akimsikiliza mmoja wa watoto waliozaliwa na Sikoseli wakati wa maadhimisho ya siku ya sikoseli duniani.

Waziri Ummy Mwalimu akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof. Lawrence Museru muongozo wa matibabu ya sikoseli mara baada ya kuzindua.



Picha ya Pamoja na Madaktari wa Watoto

Picha ya pamoja na Watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli

WAMJW- Dar es Salaam



Serikali imezindua mwongozo wa Taifa wa matibabu kwa watu wenye ugonjwa wa sikoseli, huku ikiagiza kuanzishwa kwa kliniki maalumu za kuchunguza ugonjwa huo katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kuhakikisha watu wengi hasa watoto wanafikiwa.

Akizindua mwongozo huo leo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuanzishwa kwa kliniki katika ngazi za wilaya na mikoa itasaidia watu mbalimbali kupata huduma ya utambuzi ya ugonjwa wa sikoseli karibu na maeneo wanayoishi.

“Naagiza vipimo vya utambuzi kupelekwa kwenye ngazi ya wilaya na mikoa ili kila mtu aweze kuchunguzwa kama ana tatizo la sikoseli". Amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri ameshauri upatikanaji salama wa damu kwa ajili ya watu wenye tatizo la ugonjwa sikoseli ili kuondoa changamoto ya tiba kwa wagonjwa mbalimbali.

Waziri wa Ummy ameshauri wananchi kufanya uchunguzi wa afya zao mapema ili kubaini kama wana ugonjwa huo kwani endapo watabaini itawasaidia kuanza matibabu mapema.

 Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya amewataka wadau wa ugonjwa huo kupunguza gharama za dawa kwani wagonjwa wengi hawezi kuzinunua.

“Naagiza pia dawa ya sikoseli ziingizwe katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili iwe rahisi kupatika kwa wagonjwa wengi". Amesema Waziri Ummy.

Nae Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi amesema Serikali imefikia hatua kubwa ya kuanzishwa kwa mwongozo wa Taifa wa matibabu kwa wagonjwa wa sikoseli kwa kuwa utazuia vifo vingi.

Amesema vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa sikoseli, vinaweza kuzuilika endapo utagundulika mapema kwa watoto wachanga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema katika kliniki ya wagonjwa wa sikoseli, watoto 50 hadi 70 wamekuwa wakipatiwa matibabu ya ugonjwa huo wakati kwa mwezi ni wagonjwa 211 hadi 300.

“Katika kliniki ya watu wazima, kwa siku wanaonwa wagonjwa 30 hadi 40 na kwa mwezi wagonjwa 160 hadi 200 wanatibiwa hapa Muhimbili". Amesema Prof. Museru.

Prof. Museru amesema watoto wenye ugonjwa huo wamekuwa wakipata tatizo la kupumua, damu kuganda mwilini na kiharusi.

Kauli mbiu ya mwaka huu, “Huduma Bora kwa Kila Mhitaji; Chukua hatua, panua wigo.”

MWISHO

Jumatano, 17 Juni 2020

JARIDA LA WIZARA YA AFYA - TOLEO LA 1

- Hakuna maoni







WAZIRI UMMY AITAKA BODI MPYA YA TMDA KUWEZESHA UKUAJI WA UCHUMI, USHAMIRI WA BIASHARA NA UWEKEZAJI TANZANIA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akigawa vitendea kazi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya ushauri ya Wizara kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) Bw. Erick Shitindi mara baada ya kuzindua bodi hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu  (aliyesimama kushoto) akizungumza jambo kwa wajumbe wapya wa bodi ya ushauri ya Wizara ya Afya kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba TMDA

Picha ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na wajumbe wapya wa Bodi ya ushauri ya Wizara kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA)


Na WAMJW-DODOMA

Bodi mpya ya ushauri ya Wizara ya Afya kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetakiwa kuisimamia mamlaka hiyo na kuacha kufanya kazi ya kipolisi kwa wenye viwanda vidogo na vya kati na bali kuwawezesha kushamiri kwa biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akizundua bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Bw. Eric Shitindi Jijini Dodoma.

“Nimekuwa nikieleza TMDA haipaswi kufanya kazi ya kipolisi hususani kwa wenye viwanda vidogo na vya kati, mnapochukua maamuzi haya mnatakiwa mjiulize je yanachangai kuwezesha uendelevu wa uwekezaji au biashara katika ukuaji wa uchumi wa viwanda?” amehoji Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema jukumu kubwa la TMDA ni kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na udhibiri wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kuwataka wasiongeze tozo kubwa ili kupata makusanyo makubwa.

Kuhusu tozo zilizofutwa Waziri Ummy amesema kuwa kupitia bodi iliyomaliza muda wake walifanikiwa kufuta tozo zaidi ya 20 ambazo zilikua zinawaumiza wazalishaji na wafanyabiashara za madawa, vipodozi na vyakula lengo likiwa ni kumpunguzia gharama mtumiaji wa mwisho.

Ameyataja mafanikio mengine makubwa ya TMDA kuwa ni kutambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni moja ya Taasisi bora ya udhibiti dawa ambapo imefikia hatua ya umahiri namba tatu pamoja na kuwa Mamlaka ya Udhibiti ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya tatu ya umahiri kwenye mifumo ya udhibiti wa dawa baada ya kuhakikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO Maturity Level 3 Regulatory Authority); Kuweka mifumo ya utendaji kazi ambayo imefikia kiwango cha ISO 9001:2015 toka mwaka 2009; Maabara yake kuweza kufikia viwango vya ISO/IEC 17025:2015 nakupa ta ithibati ya WHO (WHO Prequalified Laboratory); Kuanzisha Ofisi za Kanda kwenye mikoa 8 kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la Ofisi na Maabara, Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru bodi iliyomaliza muda wake ambayo ilikua chini ya Mwenyekiti Balozi Ben Moses na wajumbe wake kwa kufanikisha mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha cha utendaji wao.

MWISHO

Jumatatu, 15 Juni 2020

SERIKALI IMEENDELEA KUTEKELEZA MAKUBALIANO YA KIMATAIFA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA VVU.

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza  jambo, wakati wa kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel akifurahia jambo, wakati wa kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa akisikiliza kwa makini taarifa kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU iliyosomwa na Waziri wa Afya.

Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa kamati ya Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii.

Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi (wakwanza kulia), akiwa na Meneja Mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI Dkt. Beatrice Mutayoba (wakatikati), wakati wa kikao cha kamati ya Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii.

Mkuu wa Kitengo cha Kinga Mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Magreth Kagashe akijibu swali lililoulizwa mjumbe wakati wa kikao cha kamati ya kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii.



Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii wakisikiliza taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa Waziri wa Afya.


SERIKALI IMEENDELEA KUTEKELEZA MAKUBALIANO YA KIMATAIFA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA VVU.

Na WAMJW-DOM.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza makubaliano ya kitaifa na kimataifa juu ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini kwa kuweka mipango inayolenga kuzuia maambukizi mapya na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo Ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika kikao cha Kamati za Kudumu za Bunge za Masuala ya UKIMWI na Huduma za Maendeleo ya Jamii kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya afua za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU, Jijini Dodoma.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau tumekuwa na mwitikio wa pamoja katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini kwa kuweka Mipango ya Kitaifa ambayo imekuwa ikilenga katika kuzuia maambukizi mapya na kutoa huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU” alisema.

Aliweka wazi kuwa, baadhi ya malengo yaliyotolewa ni Pamoja na, kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2020 na kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, huku akisisitiza lengo kuu ni kuhakikisha uwepo wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora za kinga dhidi ya VVU.

Aliendelea kusema kuwa, makubaliano haya yalianzishwa mwaka 2017 na nchi wanachama wa umoja wa mataifa, wahisani, asasi za kiraia na wadau mbali yakihusisha nchi 25 zenye viwango vikubwa vya maambukizi ya VVU ikiwemo Tanzania.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, Utekelezaji wa makubaliano haya umekuwa ukipimwa kuanzia 2018 kupitia kadi maalumu ambayo inaonyesha taarifa muhimu za mwenendo wa utekelezaji wa malengo ya kitaifa yaliyowekwa na nchi kama vile huduma jumuishi za kinga kwa vijana rikabalehe na wanawake vijana (miaka 15-24) pamoja na wenzi wao.

MWISHO.

Jumapili, 14 Juni 2020

WAZIRI UMMY AZITAKA HOSPITALI ZOTE NCHINI KUACHA KUWADAI DAMU WAGONJWA KABLA YA HUDUMA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma mapema leo.
Meneja wa Mpango wa Damu Salama nchini Dkt. Magdalena Lyimo akifafanua jambo kwa Waziri Ummy Mwalimu wakati alipotembelea kituo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.





Picha mbalimbali zikionesha Waziri Ummy Mwalimu akiwajulia hali wananchi waliojitokeza kutoa damu katika Kituo cha Damu Salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.


NA WAJMW-DODOMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali zote nchini za Serikali na binafsi, Zahanati na Vituo vya Afya kuacha kuwadai damu wagonjwa kabla ya kuwapa huduma.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wachangia damu duniani yenye kauli mbiu “Damu Salama inaokoa maisha” ambayo kitaifa yamefanyika katika kituo cha kidogo cha damu salama kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

“Nazitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi kuacha tabia ya kuwadai damu wagonjwa na ndugu kabla ya kumpatia mgonjwa huduma, mnatakiwa kutoa huduma kwanza na masuala ya wanandugu kuambiwa walete watu wa kuchangia damu kabla ya huduma ni kinyume na taratibu na kanuni za utoaji wa huduma za afya”. Amesisitiza Waziri Ummy.

Waziri Ummy amezitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi na vituo vya Afya nchini kushirikiana na Mpango wa taifa wa damu salama katika kukusanya damu na wasibaki wao kuwa watumiaji wa damu bila kuweka fedha au jitihada zozote za ukusanyaji.

Waziri Ummy amesema  takwimu zinaonyesha kuwa, wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani mwaka 2015 jumla ya chupa za damu 104,632 zilikusanywa, kupimwa na kusambazwa. Idadi hii imeongezeka hadi kufikia chupa 309,376 ziizokusanywa mwaka 2019 ambayo ni ongezeko la chupa 204,744 ambayo ni sawa na asilimia 195 ikilinganishwa na chupa za damu zilizokusanywa mwaka 2015.

“Tumeboresha huduma kwenye Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa kuwapitia mashine za kisasa za kupimia damu ambapo uwekezaji huo umegharimu karibu Bilioni 13. Kwa kutumia mashine hizi Mpango una uwezo wa kufanya vipimo 4000 kwa masaa 6 kutoka vipimo 1404 kwa mashine zilizokuwepo awali kabla Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuchangia damu ni tendo la huruma, utu na upendo hivyo amewashukuru wachangia damu wote nchini hususani wale wanaochangia mara kwa mara. Pia amewahamasisha wananchi ambao hawajawahi kuchangia waweze kuchangia damu angalau mara moja kwa mwaka.

Waziri Ummy ametaka Mpango wa damu salama nchini kuweka utaratibu wa kufikia kaya zote nchini na kuhamasisha angalau awepo mtu mmoja kwa kila kaya ambae atakua anachangia damu mara kwa mara ili kuweza kukidhi mahitaji ya kitaifa ya damu salama.

Mwisho Waziri Ummy ameipongeza mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kuweka mikakati mizuri ya uchangiaji damu ambapo mgonjwa mwenye uhitaji wa damu anahudumiwa kwanza kabla ya kutafuta ndugu wa kuchangia damu.

MWISHO