Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 30 Machi 2020

ARUSHA YAZINDUA ZOAEZI LA KUPULIZA DAWA KUUWA VIJIDUDU NA KUWAKINGA ABIRIA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA CORONA

- Hakuna maoni
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro akipuliza dawa ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa corona katika moja ya mabasi kwenye uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika stendi ya mabasi makubwa jijini humo.


Na Jusline Marco;ArushaMkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.Gabriel Daqarro amezindua zoezi la upulizaji wa dawa ya kuuwa vijidudu kwa lengo la kuwakinga abiria na maambukizi ya virusi vya Corona pindi wanapotumia vyombo vya usafiri.

Zoezi hilo limezinduliwa leo rasmi kwa mabasi yanayotoka Jiji la Arusha kuelekea mikoa mingine , pamoja na vyombo vingine vya usafiri wa umma vinavyotumika katika safari za ndani ya Jiji la Arusha.

Mhe.Gabriel Daqaro amesema kuwa operesheni hiyo ya upulizaji wa dawa utakuwa endelevu na utashirikisha wadau ambao tayari wameanza kutoa michago yao kuwezesha zoezi hilo.

Aidha Daqarro amewataka wananchi kutokuwa na taharuki na hofu pamoja kuzusha maneno ya upotoshaji juu ya ugonjwa huo bali waachie mamlaka husika kutoa taarifa pamoja na elimu.

"Kuna watu wana dhana potofu wanasema Corona haiwezi kuwapata watu weusi hayo ni mawazo potofu kikubwa ni kuchukua tahadhari na kufata maagizo ya wataalamu wetu wa afya" amesema mkuu huyo wa wilaya.

Naye mganga mkuu wa jiji la Arusha Dr. kheri Kyaga amesema kuwa ni vyema wasafirishaji wote wakahakikisha abiria wanatumia vitakasa mikono au kusafisha mikono kwa maji tiririka kabla ya kupanda chombo cha usafiri ili wafike salama bila maambukizi ya ugonjwa huo.

Amesema kuwa maeneo ya stendi yanauwezekano mkubwa wa kuambukizana hivyo jukumu kuu ni kunawa mikono na kuepuka misongamano isiyo ya lazima kwani itasaidia kuepukana na janga hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha usafirishaji mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (AKIBOA) Locken Adolf Massawe amesema zoezi la upuliziaji dawa vyombo vya usafirishaji ni endelevu na litahusisha vyombo vya usafiri wa jumuia ambapo bodaboda, magari makubwa na madogo.

" AKIBOA tutaendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya ugonjwa huu"amesema.

Sambamba na mpango huo,Chama cha wasafirishaji abiria (AKIBOA) na wadau wa usafirishaji wametoa vifaa kinga vikiwemo vitakasa mikono pamoja na dawa za kupulizia vyombo vya usafiri vyenye gharama ya Shilingi milioni 7 ili kusaidia wananchi kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.

WAZIRI MKUU APOKEA MISAADA YA SH. BILIONI 1.185 KUKABILIANA NA COVID-19

- Hakuna maoni
Waziri Mkuu,   Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. milioni 230  ukiwa ni mchango wa Benki ya UBA wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Usman Isaka na wa nne kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Farhiya Warsama. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  wakikagua jenereta lilitolewa na familia ya Karimjee  Jivanji ya jijini Dar es salam lenye thamani ya sh. milioni 75 wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili  ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Azan Zungu.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipima joto la mwili wakati alipowasili ofisini kwake  Magogoni jijini Dar es salaam kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisafisha mikono wakati alipowasili ofisini kwake  Magogoni jijini Dar es salaam kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajil ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa fedha pamoja na vitu mbali mbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 1.185 kutoka kwa wadau.

Amewataka Watanzania wote waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae zaidi nchini. “Hii ni vita kubwa inahitaji tupigane kwa lengo la kuzuia janga hili lisisambae zaidi nchini, hivyo tuzingatie maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtaka kila Mtanzania ashiriki kwenye vita hii”

Amepokea msaada huo leo (Jumamosi, Machi 28, 2020) katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni, jijini Dar Es Salaam. Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao na kuwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.

Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni taasisi za kifedha ikiwemo benki ya UBA Tanzania  iliyotoa sh. milioni 230, CRDB sh milioni 150 na  NMB sh milioni 100. Wadau wengine ni  Karimjee Jivanjee Ltd na kampuni zake tanzu waliotoa sh. milioni 200 pamoja na kuhaidi kufanyia matengenezo kinga ya magari yote ya Toyota yanayotumika katika kukabiliana na COVID-19 kwa muda ya siku saba bure, Familia ya Karimjee imetoa jenereta la KVA 180 lenye thamani ya sh. milioni 75.

Wengine ni Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) ambao wametoa bidhaa mbalimbali zikiwemo magari ya matangazo yatakayotumika kutoa elimu kwa muda wa miezi minne kupitia kampuni ya Advent Construction, maji ya kunywa (Bakhressa Group), Billboard (Ashton Media) vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh. milioni 150.

Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) walitoa matanki 1,000 yenye thamani ya sh. milioni 25, huku kila moja likiwa na ujazo wa lita 250, matanki hayo yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kunawia mikono, pia Kampuni ya GS1 Tanzania Limited imetoa vitakasa mikono chupa 1,600 zenye thamani ya sh. milioni nne.

Kadhalika, Tanzania Oxygen ltd imetoa msaada wa sh. milioni 158 ambapo wamehaidi kufanyia ukarabati kiwanda kikubwa cha kuzalisha oxygen, Mount Meru imetoa vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni mbili, Hospitali ya Aga Khan imetoa dawa, sabuni, vitakasa mikono na vifaa tiba vyenye thamani ya sh. milioni 10.220.

Pia, kampuni ya gesi ya Oryx imehaidi kutoa msaada wa kusambaza gesi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine katika hospitali kama kufulia na kwenye vituo vya kuwahifadhi watu wanaohisiwa kuwa pamoja wagonjwa wa COVID-19. Gesi hiyo ina thamani ya sh. milioni 25, Tredea Cosmetics Ltd wametoa vitakasa mikono vyenye thamani ya sh.  milioni 1.6.

Umoja wa Mama lishe-Ilala na Machinga  wa Kariakoo wametoa sabuni na vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni mbili. Wakati huohuo, Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) wametoa shuka 50, magodoro10, sabuni za maji chupa 170 na vitakasa mikono chupa 400 vyote vikiwa na thamani ya sh milioni tano.

Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hausambai zaidi nchini. Alitumia fursa hiyo kuwashukuru madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wengine kwa huduma wanazozitoa.

Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema Ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa wanalio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti  yenye Jina la: National Relief Fund Electronic  Akaunti Na: 9921159801

MAJALIWA : NIMERIDHISHWA NA MAANDALIZI YA KITUO

- Hakuna maoni

Waziri Mkuu, Kaasim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  (wa tatu kulia) wakati alipokagua hospitali ya wilaya ya kibaha iliyopo eneo la Lulanzi  ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahuduma kwa wagonjwa wa Coroma, Machi 28, 2020.  Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo  na wa pili kushoto ni  Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari.. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua wodi za hospitali ya wilaya ya Kibaha  iliyopo eneo la Lulanzi  ambayo imetengwa  kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Corona Mchi 28, 2020. Kushto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilio. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu 

Na Mwandishi Wetu - Pwani
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili kuwahudumia watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na amesema ameridhishwa na maandalizi.

Aliyasema hayo jana (Jumamosi, Machi 28, 2020) wakati akizungumza na wananchi wilayani Kibaha, Pwani baada ya kukagua hospitali ya wilaya ya Kibaha ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu watakaogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabilia na COVID-19, ambapo kwa sasa watu wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandari lazima wapimwe na wakigundulika wanamaambukizi wanawekwa kwenye maeneo maalumu kwa muda wa siku 14.

“Tunazingatia sana wale wanaotoka kwenye nchi ambazo zimeathirika sana wakiingia hapa Tanzania tunawazuia kwanza, tunawapima na tunafuatilia historia yake anatoka wapi na tunaangalia katika siku 14 amepita kwenye nchi zipi.”

Waziri Mkuu alisema wawaweka kwenye maeneo maalumu ili kuweza kuwapima kila siku na kujirishika kama hawana maambukizi kwani mtu anaweza kupimwa leo akaonekana yuko vizuri lakini ana maambukizi ambayo bado hayaonekani kwenye vipimo. Kama katika kipindi cha siku 14 mtu atabainika hana maambukizi anaruhusiwa kwenda kujiunga na familia.

Pia, alisisitiza wananchi waendelee kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko na kwa wale wanaosafiri kwenye usafiri wa umma wasibanane kila mtu akae kwenye kiti.

Waziri Mkuu alisema wananchi wanapokwenda kufuata huduma kwenye masoko wahakikishe wanapeana nafasi baina ya mtu mmoja na mwingine na kabla hawajaingia katika maduka wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya corona.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kuwachukulia hatua watu wote wanaopotosha kuhusu taarifa za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). “Aliyetangaza kuwa shule zinafunguliwa tumeshamkamata na atachukuliwa hatua.”

Hivyo aliwataka wananchi wajihadhari na taarifa zinazotolewa na watu ambao si wasemaji rasmi. Alisema taarifa kuhusu virusi vya corona itatolewa na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Msemaji wa Serikali.

Alhamisi, 26 Machi 2020

HADI SASA TUMEWEZA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA NDANI KWA NDANI YA CORONA-WAZIRI UMMY

- Hakuna maoni
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, akieleza jambo, wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, akiwa na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid na Naibu Katibu Mkuu wake wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakifuatilia neno kutoka kwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha, wakati akiongea na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (COVID-19) Jijini Dodoma.



HADI SASA TUMEWEZA KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA NDANI KWA NDANI YA CORONA-WAZIRI UMMY
Na WAMJW-DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazeena Watoto, Ummy Mwalimu, amebainisha kuwa, hadi sasa Tanzania imeweza kudhibiti maambukizi ya ndani kwa ndani ya ugonjwa (COVID-19) na kuwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga.
 
Amesema, wasafiri 245 walioingia Tanzania Bara na Zanzibar tangu Machi 23, mwaka huu, wametengwa kwenye hoteli na maeneo yaliyoandaliwa na Serikali kwa gharama zao.
 
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Corona nchini.
 
Amesema hadi sasa hakuna maambukizi ya ndani (Local transmission) na wagonjwa 13 waliothibitika kuwa na virusi vya ugonjwa huo wanaendelea vizuri.
 
“Hatua mbalimbali zimechukuliwa kwa lengo lakutimiza dhamira nzuri ya serikali ya kupunguza hatari ya kusambaa kwa haraka maradhi haya nchini, tunashukuru Mungu bado hatuna ‘Local transmission,”amesema.
 
Aidha, amesema mgonjwa wa kwanza wa Arusha, amepona Corona na taratibu za kumruhusu kurudi nyumbani zinaendelea.
 
“Mgonjwa wetu amepona COVID19 na amepimwa mara tatu hana, tumeanza utaratibu wa kumrudisha nyumbani, kazi ambayo nimemuelekeza Katibu Mkuu aifanye sasa hivi suala la kutoa elimu ili kuondoa unyanyapaa, kulaumiana na kunyoshewa vidole Isabela,” amesema.
 
Kadhalika, amesema wasafiri hao 245 wamewekwa karantini kwa siku 14 kwenye maeneo maalum ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt.John Pombe Magufuli.
 
“Tangu agizo la Rais wasafiri 111 kwa Tanzania barana 134 kwa Zanzibar wametengwa kwenye hayo maeneo, na tunasisitiza mikoa yote nchini kuendelea na zoezi la kubainisha sehemu zitakazo tumika kuweka wasafiri bila kuleta usumbufu usio wa lazima,”amesema. 
 
Pamoja na hayo, Waziri huyo amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar imeendelea kufanya ukaguzi kwa kupima joto lamwili kwa wasafiri wote wanaoingia nchini.
 
“Kuanzia Januari mosi mwaka huu hadi sasa wasafiri 1,890,532 wamefanyiwa ukaguzi wa kupimwa joto kwenye vituo 27 vya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandarini na kwa saa 24 zilizopita jumla yawasafiri 3,471 wamefanyiwa ‘screening’,”amesema.
 
Amefafanua kuwa watu 273 wamepimwa sampuli za kupima virusi vya Corona katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii hadi Machi 26,2020.
 
“Kati ya sampuli hizo zilizopimwa 260 hazikuonesha uwepo wa virusi hivyo na sampuli 13 zilithibitika kuwa na virusi, wagonjwa hawa ni kutoka Mkoa wa Arusha (2), Dar es salaam(8), Zanzibar (2) na Kagera (1),”amesema.
 
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameshukuru msaada wa vifaa mbali mbali ikiwemo vya kupima virusi haraka (Rapid test kits) kutoka kwa Taasisi zilizopo Jamhuri ya watu wa China za Jack Ma na Alibaba na vitasambazwa kwenye hospitali zilizotengwa maalum kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.
 
Waziri Ummy amesema maabara iliyopo haijazidiwa na utaratibu mzuri umeandaliwa wa upimaji wa sampuli kutoka mikoani.
 
Aidha, amesema serikali inatarajia kuongeza maabara sita na Zanzibar moja.
 
“Tumeona pia kuna haja ya kuongeza maabara, tayari maabara ya Chuo Kikuu Sokoine (Sua) inaweza kupima sampuli, pia maabara za NIMR Mbeya, Tanga, Mwanza na Arusha ile maabara ya St.Nelson Mandela, hili tumeliona lakini tumeona kuna haja ya kuwa na ‘rapid test’, tupo vizuri hatujazidiwa na sampuli zinafika kwa wakati kwenye maabara yetu,”amesema.
 
Waziri huyo amesema vipimo vya kupima virusi kwa haraka vitawekwa kwenye Hospitali za Mikoa, Kanda na kwenye mipaka.
 
“Jumuia ya ya Afrika Mashariki pia jana tumepata msaada wa maabara zinazotembea, na tuta pata mbili kwa Tanzania ambazo zitapelekwa Arusha na Zanzibar,”amesema.
 
Naye, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad RashidMohammed, amewataka Watanzania kujikinga na ugonjwa huo huku akisisitiza kuwa Serikali haina nia ya kumuweka mtu kambini kumtesa.
 
Mwisho.

Jumatano, 25 Machi 2020

SERIKALI YAPOKEA MSAADA WA VIFAA VYA KUKABILIANA NA CORONA (COVID-

- Hakuna maoni
Mganga Mkuu wa  Serikali, Prof. Muhammed Bakari Kambi
akipokea msaada wa vifaa kinga kutoka China kwaajili ya kusaidia kukabiliana na Corona.
 
SERIKALI imepokea msaada wa vifaa kinga kutoka China kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na mlipuko wa maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona (COVID-19) kutoka taasisi ya Jack Ma na Alibaba.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Mganga Mkuu wa  Serikali, Prof. Muhammed Bakari Kambi amesema msaada huo ambao umetolewa na Taasisi ya Jack Ma na Alibaba ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliobainika kuwa na ugonjwa huo ni pamoja na vitendanishi (Rapid Tests) 20,000 na Barakoa (Masks) 100,000.

Prof. Muhammed amesema msaada huo utawasaidia wataalamu wa afya nchini wakati wa kuwahudumia waliobainika na watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona. 

Vifaa kinga vya msaada kutoka China kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na mlipuko wa maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona (COVID-19).


“Tunashukuru kwa msaada huo kama serikali,tumekuja hapa kushuhudia sehemu ya shehena ya tani tatu ya vifaa-tiba vilivyotolewa na Taasisi ya Jack Ma na Alibaba ambavyo vimewasili usiku wa leo na ndege ya mizigo ya Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia Ethiopia,” amesema Prof. Muhammed.

Katika hatua nyingine, Prof. Muhammed amemshukuru Afisa Ubalozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia Ethiopia Ndg. Tewodros Girma ambaye amekabidhi msaada huo kwa niaba ya Balozi wa nchi hiyo, Mhe. Yonas Yosef. 

MWISHO.

TAASISI YA BENJAMIN MKAPA YAMWAGA AJIRA 307 ZA WATUMISHI WA AFYA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma.

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula akifafanua jambo wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Mkondya akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari, katika Mkutano ulioongozwa na Waziri wa Afya leo Jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma. katikati ni naibu waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula (wakwanza kushoto).

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na Waandishi wa habari.


TAASISI  YA BENJAMIN MKAPA YAMWAGA AJIRA 307 ZA WATUMISHI WA AFYA.

Na Rayson, Mwaisemba, WAMJW-DOM

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Taasisi ya Benjamini Mkapa inayotekeleza mradi wa Uimarishaji mifumo endelevu na stahimivu ya Afya kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu, imeajiri jumla ya watumishi 307 ikiwa ni muendelezo wa kuimarisha huduma za Afya nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao na Waandishi wa habari, kilichofanyika Jinjini Dodoma.

“Tunapenda kuwataarifu mwendelezo wa kazi nzuri inayotekelezwa kupitia mradi huu na kwamba taratibu za ajira kwa wataalam wa afya wengine 307 zimekamilika. Lengo kuu la zoezi hili ni kuongeza nguvu katika utoaji huduma katika sekta ya afya”, alisema Waziri Ummy.

Katika kikao hicho kilichohudhuliwa na Naibu Waziri wa Afya na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Waziri Ummy amesema kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Mkapa, kuanzia mwaka 2018 hadi February 2020, imeweza kuajiri jumla ya watumishi wa afya 461 ambao wanatoa huduma za afya sehemu mbalimbali nchini.

Aliendelea kusema kuwa, Watumishi hawa watahudumu kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika mikoa 12 ya Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara, Shinyanga, Kigoma, Tabora, Katavi, Dodoma, Songwe na Kilimanjaro.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, wataalamu hao 307 wameshapangiwa kufanya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 68 zilizopo katika Mikoa 11, huku akibainisha kuwa Mikoa iliyonufaika ni Mwanza (34), Shinyanga (33), Mara (43), Simiyu (51), Geita (30), Kagera (34), Katavi (41), Tabora (43), Dodoma (27), Arusha (10) na Kigoma (42).

Alisema kuwa, Kupitia mchakato huu wa ajira, Kada sita za wataalamu wa Afya zimenufaika na kibali hiki kwa mgawanyo ufuatao; Kada ya Wauguzi wenye cheti (59), Wauguzi wenye Diploma (30), Maafisa Tabibu (73), Maafisa Tabibu Wasaidizi (100), Wataalamu wa maabara ngazi ya cheti (25) na ngazi ya Diploma (20).

Mbali na hayo, Waziri Ummy ameendelea kuwahimiza wataalamu wote waliopangiwa maeneo ya kufanyia kazi kuripoti mara moja kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2020, na kuanza kutekeleza majukumu yao katika vituo watakavyopangiwa.

“Napenda kuwahimiza wataalamu wote waliopangiwa maeneo ya kufanyia kazi kuripoti mara moja kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2020, ili kuanza kutekeleza majukumu yao katika vituo watakavyopangiwa” alisema

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa upataji taarifa (mawasiliano), huku akiwataka waombaji kufanya maombi ndani ya muda ulioelekezwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Dkt. Ellen Mkondya amesema kuwa, taasisi ya Benjamin Mkapa kwa miaka 14 imetoa ajira za wataalam wa afya 2181 ambao wamekuwa wakitoa huduma katika Hospitali na Vituo vya tiba nchini kote, hususan vituo vya serikali na baadhi kwenye vituo vya kidini.

“Taasisi ya BMF kwa miaka 14 yote tokea mwaka 2006 hadi Desemba 2019, tumeshaweza kutoa ajira za wataalam wa afya 2181 ambao wamekuwa wakitoa huduma katika Hospitali na Vituo vya tiba nchini kote, hususan vituo vya serikali na baadhi kwenye vituo vya kidini” alisema.

Mwisho.

Jumatatu, 23 Machi 2020

WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAPENI ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA WANANCHI - DKT.CHAULA

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara kuu afya Dkt. Zainab Chaula akiongea na waganga wakuu wa mikoa(hawapo pichani) wakati wa mkutano wa kujadili utayari wa kukabiliana na tishio la mlipuko wa virus  vya corona kwenye ukumbi wa mkutano wa hospitali ya taifa muhimbili-mloganzila

 Mkuu wa huduma za afya jeshini-JWTZ Kanali Moses Mlula akiongea na waganga wakuu wa mikoa ambapo alisema kama wataalam wanatakiwa kutoa mchango kwa serikali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kuangalia nchi zingine wanafanya nini.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa idara ya maafa kutoka.ofisi ya Waziri Mkuu Harrison Chinyuka aliwasisitiza waganga wakuu wa mikoa kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko  kwa wataalam wengine hususan timu za maafa kwenye mikoa yao

Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akiwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi wakati wa mkutano huo
 

Waganga wakuu wa mikoa nchi wakifuatilia hotuba ya katibu mkuu(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo

Na. Catherine Sungura - Dar es Salaam

Wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoletwa na kirusi wa Corona (COVID-19) ili kuepusha usisambae endapo atatokea muhisiwa wa ugonjwa huo hapa nchini. 

Maelekezo hayo yametolewa leo na Katibu Mkuu - Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula, wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) wa kujadili utayari, changamoto na hatua za kukabiliana  na tishio la mlipuko wa COVID-19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila jijini hapa. 

“Katika mkoa wewe mganga mkuu wa mkoa ndio mtaalam namba moja wa afya kwenye mkoa wako ambalo ndilo eneo lako la kazi, hivyo mnatakiwa kushauri viongozi katika kukabiliana na ugonjwa huu”. Alisisitiza Dkt. Chaula 

Amesema upashanaji elimu juu ya kujikinga na maambukizi kwa wananchi ni jambo muhimu sana kwani jamii inapaswa kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya ugonjwa huo unavyoambukizwa pamoja na dalili zake ili kila rika iweze kuwa na ufahamu na hivyo itasaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini. 

“Kama nchi za Afrika hivi sasa hatupo kwenye hatua ya utayari bali kwenye hatua ya kukabiliana. Kwani utaona ugonjwa huu umezikumba nchi nyingine, hivyo kama nchi lazima wataalam wote tujiandae kukabiliana na virusi hivi vya Corona ili endapo tutapata mgonjwa basi vyanzo vyote vya maambukizi vinatakiwa kudhibitiwa ili usienee. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia afya Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa TAMISEMI wapo tayari kupokea maelekezo na mafunzo yote ya kisekta ili kutimiza lengo tarajiwa la Serikali la kudhibiti na kukabiliana ugonjwa huo. 

Dkt. Gwajiama amesema kuwa mkutano huu utasaidia waganga wakuu wa mikoa nchini kutoka na mkakati wa pamoja wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu hususan mikoa ya mipakani kama Kagera, Katavi, Songwe, Kigoma, pamoja na mikoa mingine ambayo ipo kwenye hatari ya kuingia kwa magonjwa ya mlipuko. 

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka waganga wakuu hao kutoa mafunzo kwa wataalam wengine wa chini yao na viongozi wa mikoa na halmashauri ili kwenda pamoja katika kukabiliana na magonjwa wakati wa dharura. 

-MWISHO-

Jumatatu, 16 Machi 2020

FEDHA ZA MWENGE WA UHURU ZITUMIKE KUKABILIANA NA UGONJWA WA CORONA - RAIS MAGUFULI

- Hakuna maoni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli 



FEDHA ZA MWENGE WA UHURU ZITUMIKE KUKABILIANA NA UGONJWA WA CORONA- RAIS MAGUFULI

Na Englibert Kayombo - WAMJW, Dar Es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesitisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka huu na kuagiza Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Mwenge zitumike kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo alipokuwa akikagua hatua za ujenzi wa daraja, Ubungo Jijini Dar Es Salaama ambapo ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi juu ya ugonjwa huo wa Corona.

“Tumesikia ugonjwa huu wa corona umeshafika nchi jirani, ugonjwa huu ni hatari na hakuna kinga iliyopatikana mpaka sasa” amesema Rais Magufuli.

“Mwenge wa Uhuru hatutouwasha wala kuukimbiza mpaka tutakapohakikisha tatizo la ugonjwa wa corona limeisha” Amesema Rais Magufuli na kuagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kukimbiza Mwenge kupelekwa Wizara ya Afya kuongeza nguvu ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Rais Magufuli amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ni ishara ya amani na hawezi kuweka maisha ya Watanzania hatarini na ugonjwa huo hasa kwenye mikusanyoko ya watu wengi katika kipindi cha kukimbiza Mwenge wa Taifa.

Ijumaa, 6 Machi 2020

TAFITI ZA HOSPITALI YA KIBONG’OTO ZASAIDIA DUNIA KATIKA MAPAMBANO YA UGONJWA WA KIFUA KIKUU

- Hakuna maoni

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong'oto Dkt. Riziki Kisongo akisema jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kuu.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akisema jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu (hawapo kwenye picha) mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong'oto)

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu     Mhe. Oscar Mukasa akisema jambo kwa wajumbe wa kamati na wataalam katika kikao mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibkng'oto. Aliye upande wa kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buselu.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu Dkt. Mwigulu Nchemba (MB) akichangia hoja katika kikao na wataalam mara baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong'oto.


Mkurugenzi,wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi (kushoto) akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya, na Kifua Kikuu wakizungumza na wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi - Kibong'oto.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu na wataalam wakiwa wamevalia barakoa (mask)  kujilinda na maambukizi ya Kifua Kikuu sugu kabla ya kuelekea kwenye wodi za wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ambukizi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong'oto) Dkt. Riziki Kisongo akiwaelekeza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu namna ya kuvaa barakoa (mask) kabla ya kuelekea kwenye wodi za wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu hospitalini hapo. Aliye upande wa kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buselu

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu Dkt. Jasmine Tisekwa (kulia) akizungumza na mtoto Kidawa Baraza mwenye umri wa miaka 10 (kushoto) anayepata matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu Sugu katika Hospitali ya Kibong'oto

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu (kushoto) akizungumza na watoto wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu wanaopata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong'oto, Kilimanjaro.

Na Englibert Kayombo WAMJW – Kilimanjaro.

Tafiti za magonjwa ambuzuki kutoka Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi (Kibong’oto) zimesaidia Shirika la Afya Duniani (W.H.O) kubadilisha miongozo ya kutibu na kugundua vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Riziki Kisongo wakati akiwasilisha taarifa ya Hospitali hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifuaa Kikuu.

"Tuna machapisho ya kisayansi 50 ambayo tumeyayachapisha kwenye majarida ya kimataifa, kati ya machapisho hayo; mawili yamechangia kwenye kubadilisha miongozo ya kutibu na kugundua vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu” amesema Dkt. Riziki

“Mwaka 2009 ilikuwa inachukua siku 392 ili mtu kugundulika kuwa ana ugonjwa wa Kifua Kikuu toka aende hospitali’ anasema Dkt. Riziki na kusema kuwa kupitia watafiti waliweza kutengeneza miongozo ambayo ilitoa dira ya kuwa na haja ya kuwa na vipimo vipya ambavyo vingepunguza muda wa kugundua mgonjwa wa Kifua Kikuu.

“Miongozo imesaidia kuja kwa vipimo vya kisasa vya ugonjwa wa Kifua Kikuu “GeneXpert Mashines” ambazo zinachukua masaa mawili na nusu kepee kufanya vipimo vya ugonjwa wa Kifua Kikuu” Amesema Dkt. Riziki.

Andiko lingine lililobadili tiba ya ugonjwa wa Kifua Kikuu amesema kuwa kupitia machapisho hayo, tiba ya ugonjwa wa Kifua Kikuu imebadilika na sasa wagonjwa wanatibiwa kupitia dawa na sii sindano kama ilivyokuwa awali.

“Tiba ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ilikuwa ni kwa njia ya sindano kwa muda wa miezi nane, utafiti ulivyofanyika hapa ilionekana asilimia 47 ya wagonjwa walikuwa wanapata matatizo ya usikivu” anasema Dkt. Riziki na kuendelea kusema kuwa kwa kuchapisha maandiko hayo yalisaidia kubadili tiba ya ugonjwa huo ambapo hadi hivi sasa tiba inatolewa kwa vidonge.

Naye Mkurugenzi wa  Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi inayofanya vizuri kwenye matibabu ya TB ambapo hadi hivi sasa ina vituo 145 vya matibabu ya Kifua Kikuu sugu nchi nzima, tofauti na awali ambapo ilikuwa na Hospitali ya Kibong’oto pekee.

“Lengo la kuwa na Hospitali ya Kibong’oto sio kwa ajili ya kutoa tiba pekee bali wanatakiwa kubobea kwenye tafiti, tiba na matokeo chanya kwa Taifa na Dunia kwa ujumla” amesema Dkt. Subi na kuendelea kusema kuwa Wizara ya Afya imeongezewa uwezo Hospitali hiyo wa kushughulikia magonjwa yote ambukizi, tafiti na ufuatiliaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Madawa ya Kulevya na Kifua Kikuu Mhe. Oscar Mukasa amefurahi kusikia Hospitali hiyo inatoa mchango wa mabadiliko ya sera za matibabu ya magonjwa kutokea Tanzania na kuwasihi waongeze juhudi zaidi na kuja na tafiti nyingi zaidi zitakazo saidia katika kupata tiba ya ugonjwa huo ambao bado ni tatizo kubwa kwa Watanzania.

Mwisho

Alhamisi, 5 Machi 2020

JESHI LA MAGEREZA WAJIVUNIA KUFIKIA MALENGO YA MILENIA 90-90-90 DHIDI YA VVU

- Hakuna maoni


Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akisema jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani) wakati wa ziara katika Gereza Kuu la Arusha.

ACP Dkt. Richard Mwankina akisoma taarifa ya Jeshi la Magereza kwa niaba ya Kamishna Generali wa Magereza Suleiman Mzee (hayupo pichani) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akisema jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na viongozi waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini (hawapo pichani)

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakisalimiana na maafisa wa Gereza kuu la Arusha walipofanya ziara gerezani hapo kuzungumza na wafungwa na mahabusu.




Na Englibert Kayombo WAMJW -Arusha

Juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi zimeliwezesha Jeshi la Magereza kuboresha huduma za matibabu na upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hivyo kufikia malengo ya milenia (90-90-90)

Hayo yamesemwa na Uongozi wa Jeshi la Magereza wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanahusika na masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya.

Akisoma taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na upatikanaji wa tiba kwa magonjwa nyemelezi kwa niaba ya Kamishna Jenereali wa Magereza Bw. Suleiman Mzee, ACP. Dkt. Richard Mwankina amesema “huduma za Afya gerezani zimeboreshwa kwa kiwango cha juu na imetusaidia kuweza kuboresha matibabu na upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU kwa wagonjwa”

ACP.Dkt. Mwankina amesema kuwa kutokana na juhudi za Serikali za kupambana na VVU kumekuwa na ongezeko la wafungwa na mahabusu kujitokeza kwa hiari kupima afya zao hivyo kufikia lengo la kwanza (1st 90) ambapo baada ya kuwagundua wagonjwa wa VVU waliweza kuwaanzishia dozi na kuwa na ufuasi mzuri wa dawa (2nd 90) Wagonjwa hao wamekuwa na matokeo mazuri ya ufubazi wa VVU (3rd 90) hivyo kufikia malengo ya milenia (90-90-90)

ACP. Mwankina amesema kuwa wamefanikiwa kufikia malengo hayo ya milenia kutokana na mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanatoa na kusimamia huduma za afya kwa wafungwa, mahabusu pamoja na wataalam na familia zao.

“Kabla ya Mwaka 2007 watumishi wa Jeshi la Magereza na familia zao, wafungwa pamoja na mahabusu walikuwa wanapata huduma za afya katika vituo vya nje” amesema ACP. Dkt. Mwankina

ACP. Dkt. Mwankina amesema kuwa kuanzia mwaka 2007 huduma za afya zilianza kutolewa ndani ya Jeshi la Magereza na walianza kujenga vituo hivyo ambavyo mpaka kufikia mwaka 2020 idadi ya vituo hivyo vimefika 30.

Amefafanua kuwa kupitia vituo hivyo wameweza kufanya upimaji wa hiari kwa wafungwa na mahabusu katika nyakati tofauti ambapo walifanikiwa kuwabaini wagonjwa wa VVU na kuwaanzishia dozi ya kufubaza makali ya VVU.

“Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2019, jumla ya wafungwa na mahabusu 1372 katika Gereza Kuu la Arusha walijitokeza kwa hiari kupima afya zao na tuliwabaini wa 34 kuwa na VVU, kati yao 31 ni wanaume na watatu ni wanawake” amesema ACP. Dkt. Mwankina

Amesema kuwa wameweza kufikia mafanikio haya kutokana na elimu ambayo wafungwa na mahabusu wamekuwa wakiipata ambapo walijitokeza na kupima afya zao pamoja na kuimarisha ushirikiano mzuri baina yao na vituo vya kutolea huduma za afya nje ya magereza ili kuweza kupata huduma za rufaa za matibabu pindi ambapo huduma za vipimo na tiba zaidi zinapokosekana ndani ya gereza.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya. Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya masuala ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi na TB katika magereza ambapo kwa mwaka 2019 jumla ya magereza 17 yalinufaika na mafunzo hayo.

“Mwaka jana tumeweza kutoa elimu ya magonjwa ya kuambukiza kwa magereza 17 nchini, ambapo tulitoa mafunzo kwa maafisa magereza 209 na watumishi wengine 1378” amesema Dkt. Subi na kuendelea kusema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalam, wafungwa na mahabusu kutambua dalili na athari zitokanazo na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi na Kifua Kikuu”

Dkt. Subi amesema kuwa pamoja na mafunzo hayo waliendeshazoezi la upimaji wa hiari kwa wafungwa na mahabusu ambapo jumla ya wafungwa 5005 na mahabusu 6795 walipimwa afya zao.

“Katika upimaji huo tulibaini uwepo wa waginjwa 42 wenye ugonjwa wa kifua kikuu na tuliweza kuwaanzishia matibabu mara moja” amesema Dkt. Subi

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Suleiman Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza ni moja ya wahanga wa ugonjwa wa VVU na hawapo nyuma katika kupambana na ugonjwa huo kwa wafungwa, mahabusu, watumishi na familia zao.

Kamishna Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza linatoa huduma za uchunguzi wa afya, tiba, ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Jeshi la Magereza lina jukumu la kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama ilivyo kwenye jamii nyingine” amesema Kamishna Suleiman Mzee.

TANZANIA HAINA UPUNGUFU WA DAWA ZA ARV

- Hakuna maoni
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akisema jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na viongozi waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini (hawapo pichani)

Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akisema jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani) wakati wa ziara katika Gereza Kuu la Arusha.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya pamoja na wataala kwenye kikao cha pamoja wakijadiliana masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya gerezani katika kikao kilichoongzowa na Mwenyekiti Mhe, Oscar Mukasa

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakisalimiana na maafisa wa Gereza kuu la Arusha walipofanya ziara gerezani hapo kuzungumza na wafungwa na mahabusu.


Na Englibert Kayombo WAMJW - Arusha

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Tanzania haina upungufu wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV)

Dkt. Subi amesema kauli hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya walipofanya ziara ya pamoja kutembelea Gereza la Arusha (Kisongo)

“Hatuna upungufu wa dawa za ARV Tanzania na hatujawahi kuwa na upungufu wa dawa hizo zaidi miaka kumi iliyopita” amesema Dkt. Subi

Amesema kuwa upatikanaji wa dawa za ARV umekuwa ni wa uhakika na wagonjwa wote wanapata dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi.

“Ni kweli kuna baadhi ya dawa hasa za magonjwa nyemelezi, kuna muda kulikuwa na upungufu lakini hivi sasa tuna dawa za kutosha” amesema Dkt. Subi

Dkt. Subi ametolea mfano katika Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD), dawa ya “Ceptrin” kwa nchi nzima viko vidonge zaidi ya Milioni 62, ambapo kwa kanda ya Kaskazini wakiwa na vidonge Milioni 8.6 huku dawa za watoto zikiwa ni 786,000.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Suleiman Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza ni moja ya wahanga wa ugonjwa wa VVU/Ukimwi, na hawapo nyuma katika kupambana na ugonjwa huo kwa wafungwa, mahabusu, watumishi na familia zao.

Kamishna Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza linatoa huduma za uchunguzi wa afya, tiba, ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Jeshi la Magereza lina jukumu la kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama ilivyo kwenye jamii nyingine” amesema Kamishna Suleiman Mzee.

Jumatano, 4 Machi 2020

WAZIRI UMMY ATOA MASAA KWA HALMASHAURI ZOTE KUTENGA SEHEMU ZA KUWEKA WASHUKIWA WA CORONA

- Hakuna maoni
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongea wakati akifungua mafunzo ya jinsi ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Corona kwa viongozi wa dini mbalimbali waliojitokeza katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.
Mkurugenzi wa Maafa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Elias Kwezi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa dini kuhusiana na jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Corona usiingie nchini.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tigest Katisela akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa dini kuhusiana na jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Corona usiingie nchini.



Baadhi ya viongozi wa dini waliofika katika mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona unaoendelea kusambaa duniani. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya na kushirikisha viongozi wa dini mbalimbali nchini.
Picha ya pamoja ya Waziri Ummy Mwalimu akiwa na viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa maendeleo waliofika katika mafunzo ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona yanayofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.
Na Emmanuel Malegi-DSM

Waziri Ummy Mwalimu ametoa masaa 5 kwa kila Halmashauri kutenga sehemu maalum kwaajili ya kumuweka mshukiwa wa ugonjwa wa Corona na kufanya utaratibu wa uchunguzi na kutoa taarifa haraka Wizara ya Afya.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa dini nchini jinsi ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.

 "Ninatoa muda mpaka saa 10 jioni vituo vyote vya afya vya umma nchini viwe vimetenga sehemu maalum ya kuweka mshukiwa wa Virusi vya Corona na kuripoti haraka iwezekanavyo katika Wizara ya Afya kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki". Amesema Mhe. Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema mpaka sasa nchi yetu ni salama, hakuna mshukiwa wa COVID19 lakini Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali za dini.

"Tunawaomba viongozi wa dini muende mkatoe elimu kwa waumini wenu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi na pia kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua ambaye ana historia ya kusafiri nje ya nchi". Mhe. Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa taasisi za dini, taasisi za umma, maofisi na mashule ya Serikali na binafsi kuweka sehemu maalum ya kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria (hand sanitizers) ili kuepuka maambukizi yatokanayo na bakteria.

-MWISHO-

Jumanne, 3 Machi 2020

SERIKALI KUANZISHA KLINIKI SHIKIZI NNE ZA KUTOLEA HUDUMA ZA METHADONE KWA WAATHIRIKA WA MADAWA YA KULEVYA.

- Hakuna maoni

Dkt. Erasmus Mndeme Mkurugenze Mtendaji Hospitali ya Magonjwa ya Akili - Milembe akiwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani)

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya Mhe. Oscar Mukasa akisema jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) walipotembelea Kituo cha kutolea tiba ya madawa ya kulevya Itega, Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakiwasilikiza waraibu wa madawa ya kulevya katika kituo cha kutolea tiba ya madawa ya kulevya Itega, Jijini Dodoma.



Wajumbe wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakimsikiliza mtaalam katika kituo cha kutolea tiba ya madawa ya kulevya -Itega, Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na wataala walipofanya ziara kwenye kituo cha tiba ya madawa ya kulevya - Itega Jijini Dodoma


Na Englibert Kayombo WAMJW – Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iko mbioni kuanzisha huduma shikizi za tiba ya methadone kwa waathirika wa madawa ya kulevya ya Heroine.

Hayo yamesemwa na Dkt. Erasmus Mndeme Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Magonjwa ya Akili - Milembe alipokuwa akiwasilisha taarifa ya huduma za tiba kwa waathirika wa madawa ya kulevya kupitia dawa ya methadone na utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha kuhudumia waathirika wa madwa ya kulevya cha Itega Jijini Dodoma kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya walipofanya ziara ya ukaguzi wa huduma katika Kitui hicho.

“Kumekuwa na msongamano mkubwa katika maeneo yanayotoa huduma za methadone kwenye Jiji la Dar Es Salaam ambapo kwa sasa kwenye kliniki zote tatu idadi ya wagonja imeongezeka maradufu” anabainisha Dkt. Mndeme

Amesema kuwa hali hiyo imechagiza waratibu wa huduma hizo katika ngazi ya Taifa kufikiria mbinu mbadala ya kuboresha huduma hizo nchini.

“Mojawapo ya mbinu zilizokubalika katika kukabiliana na changamoto hii ni uanzishwaji wa satellite kliniki nne kwenye ngazi ya Halmashauri na kituo kimoja kwenye gereza la Seregea ifikapo 2020” amesema Dkt. Mndeme.

Dkt. Mndeme amesema kuwa mkakati wa uanzishwaji wa Satellite kliniki unalenga kupunguza msongamano kwenye kliniki na kutoa mwanya kwa watoa huduma kuwa na muda zaidi wa kuwaona wagonjwa na kuwapa huduma stahiki.

Amesema kuwa kupeleka huduma kwenye Halmashauri itasaida waathirika kupata huduma karibu na makazi yao.

Hata hivyo Dkt. Mndeme amesema kuwa Serikali imeandaa mkakati wa awamu ya pili ya upatikanaji wa huduma za kutoa dawa kwa waathirika “Methadone” kwa mwaka 2019-2020 huku huduma zikisogezwa kwenye mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma, Arusha na Kilimanjaro huku huduma zikiwa zimeanza kutolewa kwenye mikoa ya Dodoma na Pwani.

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya Mhe. Oscar Mukasa ameonyesha kufurahishwa na mkakati huo ambao utasaidia upatikanaji wa huduma kwa waraibu wa madawa ya kulevya na kuwataka wataalam kuongeza nguvu katika mapambano ya madwa ya kulevya na magonjwa ya kuambukiza baina ya waathirika wa madawa ya kulevya yakiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na ugonjwa wa kifua kikuuna na homa ya ini miongoni mwa waathirika wa madawa ya kulevya.