Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 23 Machi 2020

WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAPENI ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA WANANCHI - DKT.CHAULA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara kuu afya Dkt. Zainab Chaula akiongea na waganga wakuu wa mikoa(hawapo pichani) wakati wa mkutano wa kujadili utayari wa kukabiliana na tishio la mlipuko wa virus  vya corona kwenye ukumbi wa mkutano wa hospitali ya taifa muhimbili-mloganzila

 Mkuu wa huduma za afya jeshini-JWTZ Kanali Moses Mlula akiongea na waganga wakuu wa mikoa ambapo alisema kama wataalam wanatakiwa kutoa mchango kwa serikali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kuangalia nchi zingine wanafanya nini.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa idara ya maafa kutoka.ofisi ya Waziri Mkuu Harrison Chinyuka aliwasisitiza waganga wakuu wa mikoa kutoa elimu ya magonjwa ya mlipuko  kwa wataalam wengine hususan timu za maafa kwenye mikoa yao

Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akiwa na Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi wakati wa mkutano huo
 

Waganga wakuu wa mikoa nchi wakifuatilia hotuba ya katibu mkuu(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo

Na. Catherine Sungura - Dar es Salaam

Wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaoletwa na kirusi wa Corona (COVID-19) ili kuepusha usisambae endapo atatokea muhisiwa wa ugonjwa huo hapa nchini. 

Maelekezo hayo yametolewa leo na Katibu Mkuu - Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula, wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) wa kujadili utayari, changamoto na hatua za kukabiliana  na tishio la mlipuko wa COVID-19 uliofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila jijini hapa. 

“Katika mkoa wewe mganga mkuu wa mkoa ndio mtaalam namba moja wa afya kwenye mkoa wako ambalo ndilo eneo lako la kazi, hivyo mnatakiwa kushauri viongozi katika kukabiliana na ugonjwa huu”. Alisisitiza Dkt. Chaula 

Amesema upashanaji elimu juu ya kujikinga na maambukizi kwa wananchi ni jambo muhimu sana kwani jamii inapaswa kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya ugonjwa huo unavyoambukizwa pamoja na dalili zake ili kila rika iweze kuwa na ufahamu na hivyo itasaidia kuepusha magonjwa ya mlipuko yasiingie nchini. 

“Kama nchi za Afrika hivi sasa hatupo kwenye hatua ya utayari bali kwenye hatua ya kukabiliana. Kwani utaona ugonjwa huu umezikumba nchi nyingine, hivyo kama nchi lazima wataalam wote tujiandae kukabiliana na virusi hivi vya Corona ili endapo tutapata mgonjwa basi vyanzo vyote vya maambukizi vinatakiwa kudhibitiwa ili usienee. 

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayeshughulikia afya Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa TAMISEMI wapo tayari kupokea maelekezo na mafunzo yote ya kisekta ili kutimiza lengo tarajiwa la Serikali la kudhibiti na kukabiliana ugonjwa huo. 

Dkt. Gwajiama amesema kuwa mkutano huu utasaidia waganga wakuu wa mikoa nchini kutoka na mkakati wa pamoja wa namna ya kukabiliana na ugonjwa huu hususan mikoa ya mipakani kama Kagera, Katavi, Songwe, Kigoma, pamoja na mikoa mingine ambayo ipo kwenye hatari ya kuingia kwa magonjwa ya mlipuko. 

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka waganga wakuu hao kutoa mafunzo kwa wataalam wengine wa chini yao na viongozi wa mikoa na halmashauri ili kwenda pamoja katika kukabiliana na magonjwa wakati wa dharura. 

-MWISHO-

0 on: "WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAPENI ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA WANANCHI - DKT.CHAULA"