Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. milioni 230 ukiwa ni mchango wa Benki ya UBA wakati
alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya mapambano
dhidi ya ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. Kulia ni Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Usman Isaka na wa nne kushoto ni
Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Farhiya Warsama. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakikagua jenereta lilitolewa na familia
ya Karimjee Jivanji ya jijini Dar es salam lenye thamani ya sh. milioni
75 wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali kwa
ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. Kushoto
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,
Mussa Azan Zungu.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipima joto la mwili wakati
alipowasili ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam kupokea
michango kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya mapambano dhidi ya
ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisafisha mikono wakati
alipowasili ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam kupokea
michango kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajil ya mapambano dhidi ya
ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amepokea msaada wa fedha pamoja na vitu mbali mbali kwa
ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na
virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 1.185 kutoka
kwa wadau.
Amewataka
Watanzania wote waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili
kuzuia usisambae zaidi nchini. “Hii ni vita kubwa inahitaji tupigane kwa
lengo la kuzuia janga hili lisisambae zaidi nchini, hivyo tuzingatie
maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtaka kila
Mtanzania ashiriki kwenye vita hii”
Amepokea msaada
huo leo (Jumamosi, Machi 28, 2020) katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu
iliyoko Magogoni, jijini Dar Es Salaam. Waziri Mkuu amewashukuru wadau
hao na kuwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika
hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.
Miongoni mwa
wadau waliotoa msaada huo ni taasisi za kifedha ikiwemo benki ya UBA
Tanzania iliyotoa sh. milioni 230, CRDB sh milioni 150 na NMB sh
milioni 100. Wadau wengine ni Karimjee Jivanjee Ltd na kampuni zake
tanzu waliotoa sh. milioni 200 pamoja na kuhaidi kufanyia matengenezo
kinga ya magari yote ya Toyota yanayotumika katika kukabiliana na
COVID-19 kwa muda ya siku saba bure, Familia ya Karimjee imetoa jenereta
la KVA 180 lenye thamani ya sh. milioni 75.
Wengine ni Watoa
Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) ambao wametoa bidhaa
mbalimbali zikiwemo magari ya matangazo yatakayotumika kutoa elimu kwa
muda wa miezi minne kupitia kampuni ya Advent Construction, maji ya
kunywa (Bakhressa Group), Billboard (Ashton Media) vyote vikiwa na
thamani ya zaidi ya sh. milioni 150.
Shirikisho la
Wenye Viwanda Tanzania (CTI) walitoa matanki 1,000 yenye thamani ya sh.
milioni 25, huku kila moja likiwa na ujazo wa lita 250, matanki hayo
yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kunawia mikono, pia Kampuni ya GS1
Tanzania Limited imetoa vitakasa mikono chupa 1,600 zenye thamani ya sh.
milioni nne.
Kadhalika,
Tanzania Oxygen ltd imetoa msaada wa sh. milioni 158 ambapo wamehaidi
kufanyia ukarabati kiwanda kikubwa cha kuzalisha oxygen, Mount Meru
imetoa vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni mbili, Hospitali ya
Aga Khan imetoa dawa, sabuni, vitakasa mikono na vifaa tiba vyenye
thamani ya sh. milioni 10.220.
Pia, kampuni ya
gesi ya Oryx imehaidi kutoa msaada wa kusambaza gesi kwa ajili ya
kupikia na matumizi mengine katika hospitali kama kufulia na kwenye
vituo vya kuwahifadhi watu wanaohisiwa kuwa pamoja wagonjwa wa COVID-19.
Gesi hiyo ina thamani ya sh. milioni 25, Tredea Cosmetics Ltd wametoa
vitakasa mikono vyenye thamani ya sh. milioni 1.6.
Umoja wa Mama
lishe-Ilala na Machinga wa Kariakoo wametoa sabuni na vitakasa mikono
vyenye thamani ya sh. milioni mbili. Wakati huohuo, Chemba ya
Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) wametoa shuka 50,
magodoro10, sabuni za maji chupa 170 na vitakasa mikono chupa 400 vyote
vikiwa na thamani ya sh milioni tano.
Baada ya kupokea
misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru
wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na
COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali
katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali katika kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha hausambai zaidi nchini. Alitumia fursa hiyo kuwashukuru
madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wengine kwa huduma wanazozitoa.
Kuhusu wadau
wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema Ofisi yake iko
wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto na kwa wanalio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza
kutuma fedha kupitia akaunti yenye Jina la: National Relief Fund
Electronic Akaunti Na: 9921159801
0 on: "WAZIRI MKUU APOKEA MISAADA YA SH. BILIONI 1.185 KUKABILIANA NA COVID-19"