Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akisema jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani) wakati wa ziara katika Gereza Kuu la Arusha.
ACP Dkt. Richard Mwankina akisoma taarifa ya Jeshi la Magereza kwa niaba ya Kamishna Generali wa Magereza Suleiman Mzee (hayupo pichani) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya.
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akisema jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na viongozi waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini (hawapo pichani)
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakisalimiana na maafisa wa Gereza kuu la Arusha walipofanya ziara gerezani hapo kuzungumza na wafungwa na mahabusu.
Na
Englibert Kayombo WAMJW -Arusha
Juhudi
za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi zimeliwezesha Jeshi la Magereza kuboresha huduma za matibabu na
upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU) hivyo kufikia
malengo ya milenia (90-90-90)
Hayo yamesemwa
na Uongozi wa Jeshi la Magereza wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanahusika na masuala ya Ukimwi na
Madawa ya Kulevya.
Akisoma
taarifa ya hali ya maambukizi ya VVU na upatikanaji wa tiba kwa magonjwa
nyemelezi kwa niaba ya Kamishna Jenereali wa Magereza Bw. Suleiman Mzee, ACP.
Dkt. Richard Mwankina amesema “huduma za Afya gerezani zimeboreshwa kwa kiwango
cha juu na imetusaidia kuweza kuboresha matibabu na upatikanaji wa dawa za
kufubaza makali ya VVU kwa wagonjwa”
ACP.Dkt.
Mwankina amesema kuwa kutokana na juhudi za Serikali za kupambana na VVU
kumekuwa na ongezeko la wafungwa na mahabusu kujitokeza kwa hiari kupima afya
zao hivyo kufikia lengo la kwanza (1st 90) ambapo baada ya
kuwagundua wagonjwa wa VVU waliweza kuwaanzishia dozi na kuwa na ufuasi mzuri
wa dawa (2nd 90) Wagonjwa hao wamekuwa na matokeo mazuri ya ufubazi
wa VVU (3rd 90) hivyo kufikia malengo ya milenia (90-90-90)
ACP.
Mwankina amesema kuwa wamefanikiwa kufikia malengo hayo ya milenia kutokana na
mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanatoa na kusimamia huduma za afya kwa
wafungwa, mahabusu pamoja na wataalam na familia zao.
“Kabla
ya Mwaka 2007 watumishi wa Jeshi la Magereza na familia zao, wafungwa pamoja na
mahabusu walikuwa wanapata huduma za afya katika vituo vya nje” amesema ACP.
Dkt. Mwankina
ACP.
Dkt. Mwankina amesema kuwa kuanzia mwaka 2007 huduma za afya zilianza kutolewa
ndani ya Jeshi la Magereza na walianza kujenga vituo hivyo ambavyo mpaka
kufikia mwaka 2020 idadi ya vituo hivyo vimefika 30.
Amefafanua
kuwa kupitia vituo hivyo wameweza kufanya upimaji wa hiari kwa wafungwa na
mahabusu katika nyakati tofauti ambapo walifanikiwa kuwabaini wagonjwa wa VVU
na kuwaanzishia dozi ya kufubaza makali ya VVU.
“Katika
kipindi cha Januari hadi Desemba 2019, jumla ya wafungwa na mahabusu 1372
katika Gereza Kuu la Arusha walijitokeza kwa hiari kupima afya zao na
tuliwabaini wa 34 kuwa na VVU, kati yao 31 ni wanaume na watatu ni wanawake”
amesema ACP. Dkt. Mwankina
Amesema
kuwa wameweza kufikia mafanikio haya kutokana na elimu ambayo wafungwa na
mahabusu wamekuwa wakiipata ambapo walijitokeza na kupima afya zao pamoja na
kuimarisha ushirikiano mzuri baina yao na vituo vya kutolea huduma za afya nje
ya magereza ili kuweza kupata huduma za rufaa za matibabu pindi ambapo huduma
za vipimo na tiba zaidi zinapokosekana ndani ya gereza.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya. Dkt. Leonard
Subi amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya masuala ya magonjwa ya
kuambukiza ikiwemo Ukimwi na TB katika magereza ambapo kwa mwaka 2019 jumla ya
magereza 17 yalinufaika na mafunzo hayo.
“Mwaka jana tumeweza kutoa elimu ya magonjwa ya kuambukiza
kwa magereza 17 nchini, ambapo tulitoa mafunzo kwa maafisa magereza 209 na
watumishi wengine 1378” amesema Dkt. Subi na kuendelea kusema kuwa lengo la
mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalam, wafungwa na mahabusu kutambua dalili na
athari zitokanazo na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Ukimwi na Kifua Kikuu”
Dkt. Subi amesema kuwa pamoja na mafunzo hayo waliendeshazoezi
la upimaji wa hiari kwa wafungwa na mahabusu ambapo jumla ya wafungwa 5005 na
mahabusu 6795 walipimwa afya zao.
“Katika upimaji huo tulibaini uwepo wa waginjwa 42 wenye
ugonjwa wa kifua kikuu na tuliweza kuwaanzishia matibabu mara moja” amesema
Dkt. Subi
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini
Suleiman Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza ni moja ya wahanga wa ugonjwa wa
VVU na hawapo nyuma katika kupambana na ugonjwa huo kwa wafungwa, mahabusu,
watumishi na familia zao.
Kamishna Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza linatoa
huduma za uchunguzi wa afya, tiba, ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya
ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Jeshi la Magereza lina jukumu la kuhakikisha wafungwa na
mahabusu wanapata huduma bora za afya kama ilivyo kwenye jamii nyingine” amesema
Kamishna Suleiman Mzee.
0 on: "JESHI LA MAGEREZA WAJIVUNIA KUFIKIA MALENGO YA MILENIA 90-90-90 DHIDI YA VVU"