Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatano, 20 Novemba 2019

BILIONI 127 ZATOLEWA KUCHANGIA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA NCHINI TANZANIA

 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza jambo na Wadau wa Maendeleo wanaochangia Mfuko wa Pamoja wa Afya-HBF (hawapo pichani) walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

Jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Hombolo lililojengwa kutoka fedha za Mfuko wa Pamoja wa Afya (HBF)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa tatu lutona kushoto) akimuonyesha Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi. Mette Spandet maboresho ya mioundombinu yaliyofanyika katika Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili upande wa kulia) akiongea jambo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Norgaard Dissing Spandet mapema leo walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo kujionea hali ya utoaji huduma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kulia) akizungumza na wananchi waliokwenda kupata huduma katika Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

"Ukiwa mkubwa unawake kuwa nani?; Nataka kuwa kama wewe" (Utani) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na mtoto Agatha Daniel alipotembelea Kituo cha Afya Hombolo leo Jijini Dodoma

Na Englibert Kayombo – WAMJW, Dodoma.

Wadau wa mfuko wa Afya wa pamoja (HBF) wanaofadhili upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya jamii wachangia Shilingi Bilioni 127 ili kuboresha huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipofaya ziara na wadau wa maendeleo wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja walipotembelea Kituo cha Afya Hombolo Jijini Dodoma.

“Tumekuja hapa na wenzetu hawa wanaochangia mfuko wa afya wa pamoja ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2019/20 wametupatia Bilioni 127 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa kiasi cha Shilingi BIlioni 104 zitapelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ngazi ya Jamii huku kiasi cha Shilingi Bilioni 23 kikitarajiwa kutumika kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa mfuko wa afya ngazi ya juu.

“Kwa hiyo tunaona hapa fedha nyingi zitakuja huku chini kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitli za Wilaya, nawashukuru sana wadau wetu wa maendeleo kwa kutupatia Bilioni 127 kwa ajili kuboresha huduma za Afya Tanzania” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bi Mette Norgaard Dissing Spandet amesema kuwa mfuko huo umekuwa ukisaidia uboreshaji wa huduma za afya ngaza ya jamii kwa miaka 20 sasa na wanajivunia kuwa na uhusiano wa karibu na kusaidia katika upatikanaji wa bora huduma za afya nchini.

“Tunafuraha kufikia miaka 20 ya kusaidia katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania na tutaendelea kufanya hivyo zaidi kwa miaka mingi inayokuja” amesema Balozi Mette Spandet.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi ambaye Jiji lake ni mnufaika wa mfuko huo wa pamoja wa afya amesema kuwa walipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 na walizitumia vizuri kwa kuboresha na kujenga miundombinu katika Kituo cha Afya hapa Hombolo.

“Kwa shilingi Milioni 500 tumeweza kujenga nyumba ya mganga, jengo la kuhifadhi maiti, jengo la upasuaji pamoja na jengo la wodi ya kina mama” anasema Mkurugenzi Kunambi.

Mkurugenzi Kunambi amesema kuwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma wamefanikiwa kujenga wodi ya wototo iliyogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 63.

Mfuko wa pamoja wa afya unaoratibiwa na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI  huku wadau wa maendeleo wakiwa ni Nchi ya Switzerland, Canada, Denmark na Korea ya Kusini, Shirika la UNFPA, UNICEF na Benki ya Dunia umekuwa ukichangia kuboresha huduma za afya nchini Tanzania kwa miaka 20 sasa toka mwaka 1999 ambapo huduma za afya ngazi ya jamii zimekuwa zikiimarika mwaka hadi mwaka.

Mwisho

Ijumaa, 15 Novemba 2019

WANAUME ZAIDI YA MILIONI 4 NCHINI WAFANYIWA TOHARA.

- Hakuna maoni
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula akifafanua jambo wakati wa semina hiyo
.


 
 Wabunge wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na kamati ya  Katiba na Sheria walioshiriki semina ya kujengewa uelewa wa masuala ya mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI.

Waheshimiwa wabunge wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati ya semina hiyo

NA Catherine Sungura -Dodoma

JUMLA ya wanaume milioni 4,456,511 wamefanyiwa tohara kinga ya kitabibu tangu 2009 ilipoanza kutolewa hadi kufikia Septemba, 2019.

Hayo yamesemwa na Afisa Mpango kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk. Sasan Mmbando wakati wa semina ya kuwajengea uelewa wabunge wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Kamati yabkudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na kamati ya  Katiba na Sheria kuhusu mpango huo.

Dk. Mmbando alisema kuwa lengo la kwanza la afua hiyo lilikuwa kuwafikia wanaume na vijana milioni 2.8 kufikia Septemba, 2017.

“Hadi kufikia Septemba, 2017 tumeweza kuwafikia milioni 3,303,940 na kuwatahiri,” alisema.

Aidha, alisema katika lengo la pili kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 wana mpango wa kuwafikia wanaume milioni 2.7.

Alisema hadi kufikia Septemba, 2019, tayari wameweza kuwatahiri jumla ya wanaume 1,681,070 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya lengo.

Alisema afua hiyo inatekelezwa katika mikoa 17 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya HIV na kiwango kidogo cha utahiri nchini.

“Hata hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili kuwa na huduma endelevu na kupunguza matatizo ya njia ya mkojo, mfano UTI, ilianza kutoa huduma ya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60, 2013, kama utafiti wa kujifunzia (pilot study), katika mkoa wa Iringa hadi sasa imefikia mikoa 15 nchini,” alibainisha.

Alisema hadi kufikia Septemba, 2019 jumla ya watoto wachanga 13,603 wametahiriwa.

“Tohara ya watoto wachanga inafanyika katika mikoa 15, Iringa Njombe, Morogoro, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya na Kigoma,” alisema.
MWISHO

Alhamisi, 14 Novemba 2019

WAZIRI MKUU AWAASA WANANCHI KUJENGA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI.


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewaasa Wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi kwa dakika 30 angalau mara tatu kwa wiki.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, wakati akizindua Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika viwanja vya Jamhuri, Jijini Dodoma.

"Tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa kila wiki, niweke msisitizo kwa sekretarieti ya Mkoa na mamlaka ya Serikali za mitaa, kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliowekwa na mama yetu Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ", amesema Waziri Mkuu. 


Mbali na hayo, Waziri Mkuu, amesisitiza juu ya kupunguza matumizi ya vilevi, kama vile Pombe na sigara pamoja na kinywaji vyenye sukari, ambavyo kwa kiasi kikubwa uchangia magonjwa kama vile kisukari na Kansa jambo linalopelekea mzigo wa matibabu kwa wananchi.

"Tujitahidi sana kupunguza matumizi ya vilevi, hususan Pombe na Sigara, pamoja na vinywaji vilivyo na sukari  kama vile soda, juisi na chokoreti, tunajua wengi tunakunywa, basi wewe kama ni mshiriki mzuri basi pata kwa kiasi". Amesema Mhe. Kassim Majaliwa.Ameendelea, kusisitiza kwa kuwaagiza viongozi wa maeneo mbali mbali kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kufanya mazoezi angalau kila Jumamosi, na kuwataka kupunguza matumizi ya magari kila mara.

Aidha, Mhe. Majaliwa ameagiza viongozi kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kufanya mazoezi, na kusisitiza kuvifufua vikundi vyote vya mazoezi vilivyo kufa, huku akieleza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi ili washiriki katika mazoezi.  Amesema Halmashauri zote zihakikishe zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Waziri Mkuu amesema  wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe wanakimbia mchakamchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza. 


Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.

Hata hivyo, Waziri Ummy ameyataja magonjwa hayo ni kama vile, pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua na koo, huku akidai kuwa magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha.

Picha ya Pamoja ikiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akiwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma.

#TunaboreshaAfya.

Jumatatu, 11 Novemba 2019

WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA WEKEZENI KWENYE TAFITI-DKT. NDUGULILE

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza Wataalamu wa Sekta ya Afya nchini kuwekeza katika kufanya tafiti ili kutatua changamoto za Magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa Kuhusu Udhibiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza, lililohudhuriwa na Wataalamu mbali mbali wa masuala ya Afya, katika ukumbi wa chou cha UDOM, Jijini Dodoma.

Dkt Ndugulile amesema kuwa, Licha ya kuwa na tafiti mbali mbali za Magonjwa yasiyoambukiza, bado kuna haja yakufanya tafiti zakutosha, ili kuendana na kasi ya matatizo ya magonjwa haya ambayo yanazidi kuwa tishio katika jamii yet una Dunia kwa ujumla.

“Tunapoanza mpango huu, mimi niwaombe sana Wanazuoni na Wanataaluma wengine tuwekeze kwenye tafiti, mpango huu hautakuwa na maana, kama hatukuwa na takwimu, zitazosaidia kujua kama tunapiga hatua au la”, amesema Dkt. Ndugulile.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Magembe amesema Alisema, awali Serikali ilijikita katika kukabili magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria, kifua kikuu, ukimwi na mengineyo lakini sasa hali inaonesha kasi ya magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa.

“Ndiyo maana sasa Serikali imeona kuna ulazima wa kuwa na mpango wa kuyashughulikia haya magonjwa kwa pamoja, utaangalia upande wa matibabu na kujikita zaidi katika kuzuia watu wasiugue,” alisisitiza.

Aidha Dkt. Maghembe amesema, gharama za matibabu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza unazidi kuielemea jamii na Serikali, huku akidai kuwa, Magonjwa yasiyoambukiza yanachukua zaidi ya asilimia 40 ya bajeti ya sekta ya afya.


“Mtu anayekabiliwa na magonjwa ya kuambukizwa anaweza kutibiwa na kuondoka zake, lakini kwa upande wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo figo, moyo, shinikizo la damu, kisukari, mtu huyo anatibiwa milele na milele,”.

Aliendelea kusema, “Bajeti yetu yote ya afya inaingia kwenye magonjwa haya, ni gharama kubwa kuyatibu, kuanzia ugunduzi, dawa, vifaa tiba ni ghali, kuyatibu ni tofauti na yale ya kuambukiza.

Picha ya Pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile.

Ijumaa, 8 Novemba 2019

TANZANIA YAPUNGUZA MAAMBUKIZI YA MALARIA KWA ASILIMIA 50

- Hakuna maoni
Serikili kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kupunguza maambukizi ya malaria kwa takribani asilimia 50% kutoka 14.8% mwaka 2015 mpaka kufikia 7.3% mwaka 2017.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wakiongozana na Mawaziri kutoka nchi za SADC ziarani Mkoa wa Pwani, Kibaha walipotembelea Kiwanda cha Viuadudu wa kibaiolojia cha TBPL.

 Waziri Ummy Mwalimu amesema, mafanikio haya ni kutokana na kuwekeza rasilimali fedha, utashi wa viongozi, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla katika kutekeleza mikakati ya udhibiti wa malaria.

Mojawapo ya afua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kudhibiti ugonjwa wa malaria ni kujenga kiwanda cha viuadudu vya kibailojia kwa ajili ya kuua mazalia, alibainisha Waziri Ummy.

 Aliendelea kusisitiza kuwa matumizi ya viuadudu hivyo vya kibailojia ni kwa ajili ya kuangamiza viluilui vya mbu wanavyoeneza magonjwa mbalimbali yakiwemo; malaria, homa ya dengue, zika, homa ya manjano, matende, giri-majihoma ya bonde la ufa na chikungunya.

Aidha, Waziri Ummy amesema  kuwa ili kuendeleza mafanikio na hatimae kutokomeza kabisa malaria katika nchi zote za SADC tunahitaji kuongeza wigo na kuhakikisha nchi wanachama wanaongeza rasilimali fedha ili kutekeleza afua  mbalimbali za udhibti wa malaria, alisema.Aidha, Waziri Ummy akiongozana na Mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi Kusini mwa Afrika (SADC) alifanya ziara katika Bohari ya Dawa MSD, huku kwa kiasi kikubwa kuonekana kuridhishwa na hali ya utendaji kazi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), kutokana na mfumo mzuri wa manunuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi.

Waziri Ummy ambae pia ni, Mwenyekiti wa baraza hilo la Mawaziri amesema wameridhishwa na utendaji kazi wa bohari hiyo na kwamba sasa wanasubiri hatua za mwisho zikamilike manunuzi yaanze.

“Wameshuhudia MSD wana uwezo, utaalamu, vifaa kwa hiyo mawaziri wameridhika na hali waliyoikuta hapa  na tunaamini kwa kununua dawa kwa pamoja kama nchi za Sadc bei pia itashuka,” amesema Ummy Mwalimu.

Mbali na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa, MSD ina uwezo na utaalamu unaokidhi viwango katika manunuzi na usambazaji wa dawa, hali iliyopelekea kushinda zabuni ya usambazaji wa dawa kwa nchi wanachama wa SADC.


#SADC
#TunaboreshaAfya


Alhamisi, 7 Novemba 2019

SAMIA AZITOA WASIWASI NCHI WANACHAMA WA SADC JUU YA UWEZO WA MSD.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluh Hassan amezitoa wasisi Nchi wanachama wa SADC kuwa Bohari kuu ya Dawa (MSD) imejipanga vizuri kuhakikisha jukumu la uratibu wa manunuzi ya pamoja linatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Afya na UKIMWI wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), katika ukumbi wa BOT, Jijini Dar es salaam.

“Nitumie fursa hii kuwahamasisha nchi wananchama wa SADC kuwa MSD imejipanga vizuri kuhakikisha jukumu hili la uratibu wa manunuzi ya pamoja unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa” Amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande mwingine, Mhe. Samia alisema katika kipindi cha miaka mine, vituo vipya vya afya 352 vimejengwa na maeneo mbalimbali, ngazi ya kata, hospitali 67 katika ngazi ya Wilaya na hospitali 6 za mikoa katika kurahisisha utoaji huduma za afya.

Mbali na hayo, Mhe. Samia alisema Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya dawa  kutoka vyanzo vya ndani kutoka Sh30 bilioni kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia Sh260 bilioni 2019/2020, ikiwa ni juhudi za Serikali katika kuwahudumia Wananchi wa hali zote katika jamii.

“Vilevile Serikali kupitia Taasisi yake ya MSD imetengeneza mfumo wa ugavi unaosimamia manunuzi ya pamoja ya dawa na vitendanishi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za manunuzi nchini na kwa nchi wanachama wa Sadc, hii yote ni katika kufikia afya kwa wote,” alisema.Aidha, Mhe. Samia alisema, tayari Tanzania iliashaanza kuandaa mazingira ya kuingia katika mchakato huo kwa kuwekeza katika sekta ya afya na kuweka mifumo madhubuti inayowawezesha wananchi kumudu gharama za matibabu.

“Ili kufikia lengo la afya bora kwa wote na kutatua changamoto ya ugharamiaji wa huduma za afya, Serikali inatarajia kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote, hali itayosaidia Wananchi kumudu gharama kubwa za matibabu”, alisema.


Mhe. Samia aliendelea kusema kuwa, Kwenye suala la kufikia lengo la afya kwa wote, Serikali ya Tanzania imeweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu na mifumo ya afya hususasn katika kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa kwa kuzingatia ubora.

Nae, Meneja wa kanda ya Afrika kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Rebeca Matshidiso Moeti  alisema kuwa, ni muhimu kila mwananchi kupata huduma za afya bila vikwazo kiuchumi, hii itaongeza thamani ya maisha.

“Mpango wa huduma ya afya kwa wote umeweza kusaidia kuokoa maisha pamoja na kuongeza thamani ya maisha kwa wananchi wengi, hasa katika nchi ambazo zimeshaanza utekelezaji,” alisema Dkt. Rebeca Matshidiso Moeti.

Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa, “Jumuiya ya SADC ilisaini itifaki ya afya (protocol health) mwaka 1999 ambayo ilizinduliwa mwaka 2004 kwa ajili ya kutoa muongozo wa masuala ya afya na UKIMWI, ,jumuiya ilianzisha mkakati wa maendeleo wa kanda kwa kipindi cha miaka mitano.

Aliendelea kusema kuwa, Mawaziri wa SADC wanaoshughulika na masuala ya UKIMWI wamekua wakikutana kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa program mbalimbali za afya na UKIMWI zilizoainishwa katika kipengele B cha mkakati huo.

“Mawaziri wenzangu leo tuna wajibu mkubwa wa kupitia, kujadili na kuridhia mapendekezo yatakayowasilishwa na wataalamu ambayo yanalenga kuhakikisha utekelezaji wa maazimio hayo pamoja na kulinda maslahi ya jumuiya yetu”, alisisitiza Waziri Ummy.

Jumatatu, 4 Novemba 2019

SERIKALI YANUIA KUTOKOMEZA TB – DKT. ZAINAB CHAULA.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Zainab Chaula akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wataalamu  wa Afya wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika  leo Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji TACAIDS Dkt. Leonard Maboko akiongea na Waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wataalamu  wa Afya wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jijini Dar es Salaam.

Makatibu Wakuu na Wataalamu  wa Afya wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wakiendelea na Mkutano  wa kuhusu masuala ya Afya, uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja ikiongozzwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainab Chaula baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Wataalamu  wa Afya wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jijini Dar es Salaam.SERIKALI YANUIA KUTOKOMEZA TB – DKT. ZAINAB CHAULA.

Na WAMJW-DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) nchini, ikiwa ni moja kazi ya malengo ya nchi za SADC ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula wakati akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu na wataalam wa afya wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wakijadili jumla ya ajenda 13 kuhusu masuala ya Afya, hususani HIV/AIDS, Malaria, TB na usambazaji wa dawa.

“Ajenda yetu kubwa ya kwanza, ni kujadili namna ya kuutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), tunataka inapofika Mwaka 2030 nchi zote zilizo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zinatokomeza ugonjwa wa KIfua KIkuu (TB)”, amesema Dkt. Chaula.

Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa, baadhi ya ajenda zingine zitazojadiliwa katika Mkutano huo, ni masuala ya kutokomeza HIV/AIDS na kutokomeza ugonjwa wa Malaria katika nchi wanachama wa SADC.

Aidha, Dkt. Chaula amesema kuwa, Nchi ya Tanzania, kupitia Bohari kuu ya dawa nchini (MSD) imepewa heshima kubwa katika jukumu la kusambaza dawa, vifaa na vifaa tiba katika nchi zilizo katika Jumuiya ya SADC.

“Nchi yetu ya Tanzania imepewa heshima kubwa ya kusambaza dawa, vifaa na vifaa tiba, kupitia Bohari kuu ya Dawa (MSD) katika nchi zilizo kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika kusini (SADC)”, alisema Dkt. Chaula.

Mbali na hayo, Dkt. Chaula amesema kuwa, masuala ya Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Chanjo ni baadhi ya ajenda zitazojadiliwa baina ya nchi wanachama wa Mkutano huo wa SADC, ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha Sekta ya Afya.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa, takribani watu 200 huambukizwa VVU kwa siku, watu 80 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, huku kati ya hao vijana wanaopata maambukizi, watu 60 ni vijana wa kike.

“Katika Siku moja watu 200 wanaambukizwa VVU, 80 ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, lakini changamoto zaidi ni kwa vijana wa kike, kwa sababu katika vijana 80 wanaopata maambukizi vijana wa kike ni 64, hivyo kama Serikali tunahakikisha kwamba tunawawezesha wasichana walio katika mazingira magumu kiuchumi kupata mahitaji yao ya muhimu na waweze kukaa shuleni”, alisema Dkt. Maboko.

Katika Mkutano huo, wenye wajumbe wa Nchi 16, nchi ya Tanzania imekuwa mwenyeji ikipokea uwenyekiti kutoka nchi  ya Namibia.

MWISHO

Ijumaa, 1 Novemba 2019

ELIMU YA TATHMINI YA UHAKIKI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA YAZIDI KUTOLEWA

- Hakuna maoni


Na WAMJW-DSM


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kutoa mafunzo kwa timu za Usimamizi wa uendeshaji wa huduma za afya katika Halmashauri (CHMTs) juu ya tathmini ya uhakiki wa ubora wa huduma za zinazotolewa katika eneo husika.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Yudas Ndugile siku ya Jumanne yameendelea kwa wiki moja lengo likiwa ni kuwaelimisha watoa huduma za afya kuzingatia misingi ya utoaji wa huduma bora za afya ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu.

Akiongelea mafunzo hayo Mratibu na mkufunzI kutoka Wizara ya Afya Dkt. Talhiya Yahya amesema  Lengo la kutoa nyota ni kuongeza chachu ya utoaji wa huduma za afya nchini ikiwa sambamba na uboreshaji wa miundombinu na watumishi wa afya kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa mahala pa kazi.

“Lengo la mafunzo haya ni kutoa elimu kwa CHMT kuhusu kutumia nyezo ya kielektroniki kufuatilia utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa vituo kutegemea na mapungufu yaliyopatikana katika vituo kipindi cha kufanya tathmini ya kutoa nyota kutokana na ubora wa kituo”. Amesema Dkt. Talhiya.

Dkt. amesema baada ya mafunzo  hayo anategemea kuona maboresho yakifanyika na tathmini ijayo ya kuhakiki ubora (Star Rating) vituo vingi vitakua na nyota tatu au zaidi.

Wakati huo huo, Wizara imetoa mafunzo kwa watumishi wa afya wa Hospitali mbalimbali za Jiji la Dar Es Salaam namna ya kufuata miongozo na taratibu za kukinga na kudhibiti maambukizi (IPC Standards).

Mafunzo hayo ya siku tano yamehitimishwa leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam tawi la Kijitonyama ambapo mratibu wa mafunzo hayo Dkt. Chrisogone German amesema lengo ni kuwajengea uwezo watumishi hao kufuata miongozo ya utoaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi.

Dkt. Chrisogone amesema muongozo wa mpya wa kukinga na kudhibiti maambukizi (IPC Guideline) wa mwaka 2018 ambao umefuata vigezo vya Shirika la afya Duniani (WHO) utaanza kutekelezwa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika mkoa wa Dar Es Salaam ikiwemo washiriki kujengewa uwezo wa utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mloganzila, Agha Khan, TMJ, Sali International, Hindu Mandal, BOCHI na Rabininsia.