Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 22 Desemba 2019

WANANCHI SASA KUJIPIMA VIRUSI VYA UKIMWI - WAZIRI UMMY

Nembo ya UKIMWI





Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akieleza jambo wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi

WANANCHI SASA KUJIPIMA VIRUSI VYA UKIMWI - WAZIRI UMMY

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- Katavi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo amesema kuwa bunge la Tanzania limerasimisha sheria ya Wananchi kuweza kujipima wenyewe maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Waziri Ummy amesema hayo leo Disemba 20 katika ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za Afya na ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ikiwa ni jitihada za Serikali za kuboresha huduma za Afya nchini.

"Napenda kuwapa Habari njema kuwa Bunge la Mwezi wa 11 limepitisha Sheria, kwahiyo sasa ni rasmi Tanzania mtu kujipima maambukizi ya VVU mwenyewe, kwahiyo hivi vitendanishi (vifaa) vitakuwa vinauzwa kwenye maduka, pia kugawa bure baadhi ya maeneo kwa sababu wakati mwingine watu wanaona unyanyapaa kwenda kupima wenyewe," Amesema Waziri Ummy.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali imeweka angalizo kuwa, kujipima mwenyewe sio majibu ya mwisho, hivyo kuwataka wananchi kuwa, baada ya kujipima wanatakiwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa ajili ya kuthibitisha na ushauri zaidi wa jinsi ya kuishi.

Aidha, Waziri Ummy ameagiza kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa wananchi, hususan watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kutumia dawa kwa usahihi kulingana na maelekezo ya Watoa huduma za Afya katika vituo vya kutolea huduma za Afya nchini.

"Tuendelee kuhakikisha watu wote waliobainika na ugonjwa wa Ukimwi, waendelee kutumia dawa kwa usahihi kama walivyoelekezwa na Wataalamu wetu katika vituo vya kutolea huduma za Afya nchini". amesema Waziri Ummy.

Mbali na hayo, amesema kuwa kuna changamoto ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24, huku akiweka wazi kuwa kitaifa hali ya maambukizi mapya kwa vijana hao ni asilimia 40%, huku vijana wa kike ikiwa ni asilimia 80 na wakiume ikiwa ni asilimia 20.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amewatia moyo wanaoishi na maambukizi ya VVU kwa kuwakumbusha kuwa, kuhudhuria katika vituo vya Afya na kufuata maelekezo kama walivyopewa na Watoa huduma, pia kuishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi sio mwisho wa maisha.

"Niendelee kuwatia moyo kuwa na maambukizi ya Ukimwi sio mwisho wa Dunia, sio sentensi ya kifo, sikuhizi watu Wanaishi vizuri, kwahiyo nawahimiza kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, kupima na kuanza kutumia dawa". Amesema Waziri Ummy.

Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Bi Lilian Matinga amesema kuwa, hali ya upatikanaji wa dawa ipo vizuri Mkoani hapo, huku akidai kuwa kwa mwaka 2017/2018 bajeti ya dawa na vitendanishi ilikuwa Bilioni 2.9 na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Mkoa umetengewa jumla ya shilingi Bilioni 3.97 ikiwa ni ongezeko la shilingi Milioni 460.07.

Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu ni zaidi ya asilimia 90% katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini. alisisitiza.

Mwisho.

0 on: " WANANCHI SASA KUJIPIMA VIRUSI VYA UKIMWI - WAZIRI UMMY"