Mwakilishi wa Benki ya
NMB Bw. Juma Kimoli akikabidhi rasmi vitanda hivyo kwa Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya wazazi walioleta watoto kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili kitengo cha watoto. |
Waziri Ummy Mwalimu
akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa wodi ya
watoto wenye kuhitaji uangalizi maalumu (PICU), pamoja na wawakilishi wa Benki
ya NMB.
|
Na Emmanuel Malegi-DSM
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
ameziomba sekta binafsi ikiwamo benki ya NMB kuendelea kushirikiana na Serikali
katika kuboresha huduma za Sekta ya Afya nchini.
Waziri
Ummy amesema hayo leo wakati akipokea msaada wa vitanda vitano kutoka Benki ya
NMB vyenye thamani ya shilingi Milioni 35 kwa ajili ya wodi ya watoto
wanaohitaji huduma ya uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) na vitanda 10 pamoja na magodoro 10 kwa Hospitali ya
Muhimbili-Mloganzila vyenye thamani ya shilingi milioni 10.
Amesema
sekta binafsi zina wajibu mkubwa katika kuchangia shughuli za maendeleo ikiwamo
huduma za afya kama ilivyofanya Benki ya NMB.
“Nawapongeza
NMB kwa jitihada zao kwani msaada wa vitanda vya ICU ni msaada mkubwa kwa
watoto na pia benki hii inafanya vizuri kurejesha fedha zake kwa jamii ikiwemo
na kutoa gawio Serikalini”. Amesema Waziri Ummy.
Pia,
Waziri Ummy amesema kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tano, Muhimbili
inaendelea kutoa huduma za kibingwa za hali ya juu zikiwemo huduma ya
kupandikiza figo pamoja na huduma ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto
wenye matatizo ya kusikia.
Naye
mwakilishi wa Benki ya NMB, Bw. Juma Kimoli ameipongeza Muhimbili na serikali
ya awamu ya tano kwa kuboresha huduma za afya huku akisisitiza kuwa NMB imeweka
utaratibu wa kuisaidia sekta ya afya kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutoa
misaada mbalimbali kwa jamii.
Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Muhimbili, Bi. Zuhura Mawona
ameishukuru NMB kwa msaada huo kwa kuwa umekuja wakati ambapo Hospitali hiyo
kwa kushirikiana na wahisani imejenga wodi za uangalizi maalumu kwa watoto wenye
umri kati ya siku 1 hadi siku 28 (NICU) na wenye umri wa siku 29 hadi miaka 14
(PICU), hivyo kuwa na uhitaji wa vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vitanda.
“Vitanda
hivi vya kisasa vinatumia umeme na vinaweza kutumika kwa kupandishwa juu na
kushushwa kulingana na uhitaji, hivyo vinasaidia mgonjwa kulazwa
katika mlalo unaofaa na pia kupunguza maumivu ya mgongo kwa wauguzi na
madaktari wakati wa kutoa huduma”. Amesema Bi. Zuhura.
Mkurugenzi
huyo amesema kuwa vitanda hivyo pia vimesaidia wauguzi kutoa huduma kwa urahisi
na ufanisi zaidi ikiwamo kumwezesha mgonjwa kupumua (Intubation) kwa urahisi.
Kwa
niaba ya Hospitali ya Muhimbili, Bi. Zuhura ameishukuru NMB kwa kutoa msaada
huu na pia ameiomba kuongeza vitanda vingine kwani mahitaji ya vitanda ni
makubwa kwa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.
0 on: "TAASISI BINAFSI ZAOMBWA KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA AFYA KATIKA KUBORESHA HUDUMA NCHINI"